Habari Mseto

Mzee afariki baada ya kujikata uume kwa makasi

July 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WANYORO

MWANAMUME wa miaka 55 amefariki katika Kaunti ya Embu baada ya kujikata sehemu zake za siri katika kijiji cha Ng’erwe, katika kile kinachoaminika kuwa matumizi ya bangi.

Mwanamume huyo, aliyetambuliwa kama Dominic Mugo, alifariki Jumatatu baada ya kuvunja damu nyingi.

Marehemu aliwashangaza wakazi baada ya kujikata nyeti kwa makasi .

Wanakijiji wenye mshangao walisema walisikia vilio kutoka nyumbani kwa marehemu, ambapo walimkuta akiwa amepoteza fahamu walipofika kwake. Walisema kuwa walimkuta akiwa ameshikilia makasi.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Embu Kaskazini, Bw Jeremiah Tumo alisema wanakijiji hao walitafuta gari na kumkimbiza katika Hospitali ya Embu Level Five lakini akafariki kabla ya kufikishwa.

Wanakijiji hao hata hivyo walisema wanashuku marehemu alifanya kitendo hicho kutokana na matatizo ya kiakili, kwani alikuwa mtumizi wa bangi.

Bw Tumo alisema eneo hilo huwa na watumizi wengi wa bangi, ikizingatiwa kwamba linapakana Mlima Kenya.

“Ni kweli kwamba mwanamume huyo alifanya kitendo hicho katika kile kinaonekana kuwa tatizo linalotokana na bangi. Wakazi walisema kuwa huwa wanamwogopa kwani alikuwa akizua ghasia. Ingawa tukio hili ni la kusikitisha, ni funzo kwetu kuhusu madhara ya mihadarati,” akasema.

Bw Tumo alisema kuwa tatizo hilo limekithiri eneo hilo kiasi kwamba muuzaji mmoja anachunguzwa baada ya kupatikana kuwa na uhusiano na mwanafunzi wa shule moja iliyokumbwa na ghasia mwezi uliopita.

Alisema kuwa wanashirikiana na wanachama wa Nyumba Kumi ili kuwanasa walanguzi hao.

“Mhudumu mmoja wa bodaboda anachunguzwa kwa madai kwamba huwa anawauzia wanafunzi mihadarati. Hatutalegeza kamba katika operesheni hiyo,” akasema Bw Tumo.

Alisema tayari polisi wameanza uchunguzi kuhusu kilichofanyika. Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Mochari ya Gakwegori.