Wakazi kutoka kaunti jirani wamechangia huduma mbovu Kiambu – Waititu
Na WANDERI KAMAU
GAVANA wa Kiambu, Ferdinand Waititu amedai kuwa idadi kubwa ya watu kutoka kaunti jirani ndiyo inayosababisha kudorora kwa huduma za afya katika hospitali nyingi za kaunti hiyo.
Bw Waititu alisema watu kutoka kaunti majirani kama Nairobi, Kajiado, Narok, Murang’a, Kitui, Nakuru kati ya zingine wamekuwa wakitafuta huduma za matibabu katika kaunti hiyo, hivyo kuongeza mzigo wa wahudmu wa afya katika hospitali za Kiambu.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Amerika Jumatatu, Bw Waititu alisema kuwa serikali yake imejitolea kikamilifu, ila hilo ndilo limekuwa changamoto kuu kwake.
Kauli yake inajiri baada ya kuibuka kwa hali za misongamano ya wagonjwa katika hospitali kadhaa, hasa Kiambu Level Five.
Hospitali zingine zinazokabiliwa na hali hiyo ni Tigoni na Thika Level Five.
Lakini akijitetea, Bw Waititu alisema kuwa ukosefu wa mwongozo ufaao umewafanya hata wakazi wenyewe kukosa nafasi ya kuhudumiwa ifaavyo.
“Ongezeko la watu kutoka kaunti jirani katika hospitali zetu ndicho kiini kikuu cha hali hii. Tunatafuta njia ambapo tutazipanua zaidi ili kuhakikisha misongamano hiyo inapungua,” akasema Bw Waititu.
Hali mbaya ya hospitali ya Kiambu Level Five imemfanya gavana huyo kukosolewa vikali, baadhi ya watu wakidai kuwa ameshindwa kudhibiti sekta ya afya.
Hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa wakati wa uongozi wa mtangulizi wake William Kabogo, ambapo Kaunti ya Kiambu ilikuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma za afya.
Misongamano katika Kiambu Level Five ni mikubwa kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wanasema wanalazimika kulala wawili katika kitanda kimoja, huku wengine wakilala sakafuni.
Pia kumeripotiwa katika baadhi ya hospitali kuwa wagonjwa hawapewi chakula na wanategemea kile wancholetewa na jamaa zao.
Wauzaji bidhaa pia wamekataa kutoa huduma kwa hospitali hizo kwa kukosa kulipwa.
Wiki iliyopita, Katibu katika Wizara ya Afya Peter Tum aliizuru hospitali hiyo baada ya malalamishi, na kutoa agizo kwa serikali za kaunti kuongeza kiwango cha fedha zinazotengea hospitali.
Katibu huyo alisema kuwa mojawapo ya sababu kuu zinazoandama hospitali hizo ni ukosefu wa fedha za kutosha, hivyo kutumia vifaa vichache zilizo nazo kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa.
Bw Waititu alisema kuwa lazima serikali za kaunti zibuni miongozo kuwashinikiza wakazi kutafuta baadhi ya huduma muhimu za matibabu katika hospitali za kaunti zao.
“Lazima pawe na mwongozo ufaao, kwani hali hii inawaathiri hata wakazi wa Kiambu wenyewe, licha ya kulipa kodi,” akasema.