Habari Mseto

Wafungwa 8,000 wa kunyongwa waliosukumwa jela maisha wahukumiwe upya – Jopo

July 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WAFUNGWA 8,000 waliohukumiwa kunyongwa nchini wakiwemo wale ambao hukumu zao zilibadilishwa kuwa za kufungwa jela maisha, wanafaa kuhukumiwa upya, jopo la kuchunguza hukumu ya kifo linapendekeza.

Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kuamua kwamba hukumu hiyo sio lazima itolewe kwa wanaopatikana na makosa ya mauaji, wizi wa mabavu au kujaribu kutekeleza wizi wa mabavu.

“Tunapata kwamba wafungwa wanaosubiri kunyongwa wana haki ya kuhukumiwa upya ilivyoagiza Mahakama ya Juu katika uamuzi wa kesi ya Muruatetu.

Hii ni pamoja na wafungwa wote wakati uamuzi ulitolewa, wafungwa wote ambao hukumu ya kifo ilibadilishwa kuwa ya kufungwa jela maisha, wote waliofungwa jela baada ya uamuzi wa kesi ya Muruatetu kutolewa ambao hawana kesi ya rufaa,” inasema ripoti ya jopo hilo.

Francis Karioko Muruatetu na mshtakiwa mwenzake waliwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu kwamba wanyongwe.

Majajiwa Mahakama ya Juu kwenye uamuzi waliotoa Desemba 14, 2017 walikubaliana nao na kuagiza Mwanasheria Mkuu na idara husika kuchunguza hukumu hiyo upya.

Mnamo Januari mwaka huu, Mwanasheria Mkuu aliunda jopo hilo ambalo linapendekeza mabadiliko makubwa ya sheria kufuatia hukumu hiyo.

Ripoti ya jopo inaonyesha kuwa kufikia Machi 1 2018, kulikuwa na wafungwa 838 katika magereza ya Kenya waliokuwa wakisubiri kunyongwa na 6938 ambao hukumu yao ilibadilishwa kuwa kufungwa jela maisha.

Watu hao, walinusurika baada ya Mahakama ya Juu kuamua kwamba hukumu ya kifo haifai kuwa ya lazima kwa makosa waliyotekeleza.

Ripoti ya jopo hilo inaonyesha kuwa kufikia Desemba 2017, kulikuwa na kesi 3,998 za mauaji katika Mahakama Kuu nchini na kesi 3,430 za wizi wa mabavu katika mahakama za mahakimu nchini.

Kuna makosa matano ambayo adhabu yake ni kifo katika sheria ya kesi za uhalifu na tisa chini ya sheria ya jeshi ya Kenya. Kulingana na ripoti ya jopo hilo, wanaume 45 na wanawake 27 walipatikana na hatia ya mauaji. Wanaume 93 na wanawake watano walihukumiwa kunyongwa kwa kutekeleza wizi wa mabavu.

Inaonyesha kuwa wanawake wengi waliohukumiwa kunyongwa kwa makosa hayo walikuwa na umri wa kati ya miaka 26 na 35 wakati wa kuhukumiwa huku wanaume wakiwa na kati ya umri wa miaka 18 na 25 walipopatikana na hatia. Hakuna mfungwa aliyehukumiwa kunyongwa akiwa na umri wa zaidi ya miaka 55, kulingana na ripoti hiyo.