• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
Al Shabaab walemaza biashara Lamu

Al Shabaab walemaza biashara Lamu

NA KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya manahodha 5000 wa boti na mashua za kusafirishia abiria kaunti ya Lamu wamekiri kukumbwa na ugumu wa kuiendeleza biashara hiyo kutokana na uhaba wa wateja katika siku za hivi karibuni.

Manahodha wanasema kukosekana kwa wageni hasa watalii wanaozuru eneo hilo tangu Kaunti ya Lamu ianze kushuhudia visa vya mashambulizi kutoka kwa magaidi wa Al-Shabaab mnamo 2014 ni mojawapo ya changizo kuu zinazopelekea biashara ya usafiri wa boti baharini kuendelea kudidimia kila kuchao.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatano, manahodha walikiri kukithiri kwa makosano na vita vya mara kwa mara baina yao kila wanaposhindania wateja ambao ni wachache mno.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki na Waendeshaji Boti Kaunti ya Lamu, Hassan Awadh, alisema biashara ya usafiri baharini imekuwa ndoto katika siku za hivi karibuni, jambo ambalo tayari limewasukuma baadhi yao kujitoa kwenye biashara hiyo.

Alisema kati ya boti na mashua zaidi ya 300 zinazohudumu kisiwani Lamu pekee, zaidi ya boti na mashua 50 hukaa bure bila kazi mchana kutwa kutokana na kukosekana kwa wateja.

Anasema aghalabu manahodha wengi kwa siku huishia kwenda nyumbani bila chochote kwa kukosa wateja wa kuwabeba.

Aliitaka serikali kuhakikisha usalama unadhibitiwa kote Lamu ili wageni waendelee kuzuru eneo hilo na vijana wapate ajira.

“Tunakumbwa na wakati mgumu msimu huu. Tangu shambulizi la Al-Shabaab litekelezwe Mpeketoni Juni 15, 2014, watalii na wageni wanaozuru Lamu wamepungua. Hali hii imechangia biashara ya usafiri baharini kusambaratika. Vijana hawana tegemeo lingine. Ikiwa hali itaendelea hivi, usalama hapa Lamu utakuwa kero kwani vijana wataanza kugeukia wizi,” akasema Bw Awadh.

Bw Abubakar Yusuf,45 ambaye ni baba wa watoto watatu na ambaye amedumu kwenye biashara ya usafiri wa boti kwa zaidi ya miaka 20 anasema sekta hiyo imebadilika pakubwa ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.

Bw Yusuf alisema angeweza kufanya safari zaidi ya kumi kutoka mjini Lamu hadi Mokowe kwa siku moja kutokana na idadi kubwa ya wasafiri iliyokuwepo.

Anasema tangu utovu wa usalama uanze kushuhudiwa Lamu, safari zake zimepungua hadi tatu au nne pekee kwa siku.

“Boti yenyewe ni ya tajiri ambaye afaa kulipwa kati ya Sh 1500 mpaka Sh 2000. Kwa siku waweza ng’ang’ana na kukosa hata hizo Sh 2000 za kumlipa mwenye boti. Hali hii inatufanya kuhatarisha hata ajira zetu kwani wenye boti huwa hawaelewi kwamba biashara ni mbaya,” akasema Bw Yusuf.

Bw Abdillahi Athman anayebeba abiria kutoka kisiwa cha Manda hadi kisiwa cha Lamu alisema wakati biashara  ilipokuwa nzuri alikuwa akipata hadi Sh 5000 kwa siku.

Anasema ukosefu wa abiria umemfanya kupata Sh 2000 hadi Sh 2500 pekee kwa siku.

Manahodha aidha waliitaka serikali ya kaunti ya Lamu kuanzisha maadhimisho ya sherehe za mara kwa mara kwani sehrehe hizo huvutia wageni wengi na kunogesha biashara yao ya usafiri wa baharini.

You can share this post!

Kesi ya Karua dhidi ya Waiguru kusikizwa na majaji wapya

ULIMBWENDE: Tumia mbinu hii ya vitunguu maji kutunza nywele

adminleo