• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:55 PM
Mwanamume aua mtoto kwa kunyimwa chakula na mkewe

Mwanamume aua mtoto kwa kunyimwa chakula na mkewe

NDUNGU GACHANE na GERALD BWISA 

MWANAMUME wa umri wa miaka 48 kutoka kijiji cha Gaichanjiru, Kaunti ya Murang’a alikamatwa Jumatano kwa kumuua mmoja wa pacha wake wa miezi 9 baada ya kukosana na mkewe kuhusu chakula.

Kulingana na Mkuu wa Polisi eneo la Kandara Peter Mugwika, mwanamume huyo alifika nyumbani akiwa mlevi na kumtaka mkewe ampakulie chakula.

Mkewe alimfahamisha kuwa hakukuwa na chakula nyumbani humo ndiposa akamchukua pacha huyo aliyekuwa akinyonya kisha akamrusha kwa ukuta na kuanguka kwa sakafu.

Bw Mugwika alisema mwanamume huyo amekamatwa na maafisa wa polisi wanaendelea kukamilisha uchunguzi ili wamfungulie mashtaka ya mauaji.

“Mtoto huyo pacha aliporushwa na kuanguka alianza kulia na mamake akamchukua na kumlalisha lakini baada ya saa mbili aligundua mtoto huyo kwa jina Vincent Kangethe alikuwa amekufa,”alielezea Bw Mugwika.

Baadaye, mama huyo alipiga ripoti katika kituo cha Kabati ambapo mshukiwa huyo, Francis Muiruri alikamatwa na mwili wa mtoto huyo ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Gaichanjiru.

Bw Mugwika aliwataka wakazi wa eneo hilo kujiepusha na ulevi na kusaka ushauri nasaha wakati wanakabiliwa na mizozo ya kifamilia.

Jirani wa familia hiyo, Elijah Kamau aliwataka maafisa wa polisi kuharakisha uchunguzi ili mshukiwa huyo afunguliwe mashtaka ya mauaji.

“Hatuwezi kuishi na mtu kama huyo katika kijiji chetu,”alisema Bw Kamau.

Kwingineko, mwanamume mwenye umri wa miaka 31 alihukumiwa kufungwa jela miaka 15 kwa kumuua mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka tisa akimuadhibu.

Fred Wekesa Wanyonyi anayefahamika kwa jina maarufu Makoti, alipatikana na hatia na Jaji wa Mahakama Kuu ya Kitale Hillary Chemitei.

Wekesa alikuwa akikabiliwa na shtaka la kumuua David Wafula, katika kijiji cha Chebarus Kaunti ya Tranzoia mnamo Januari 25, 2015. Akimhukumu, Jaji Chemitei alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi kikamilifu.

“Kifo cha marehemu kilisababishwa na ukatili wa mshtakiwa ambaye alikuwa baba yake,” Jaji Chemitei alisema.

“Mahakama pia imezingatia ripoti ya tabia ya mshtakiwa inayosema alikuwa na mwenendo mbaya. Kwa hivyo, anahukumiwa kufungwa jela miaka 15,” aliamua Jaji Chemitei.

Kwenye taarifa yake ya mwisho kwa mahakama, mshtakiwa alikiri kwamba alitenda kosa hilo akisema alikuwa akimfunza adabu mtoto huyo kama mzazi.

Alisema hakupanga wala hakujua mtoto huyo angekufa.

Aliomba mahakama imhurumie akisema atakuwa mwangalifu siku zijazo.

Hata hivyo, kulingana na ripoti ya probesheni iliyotayarishwa na Bw Lex Gimnyigei, mshtakiwa alisifika kwa tabia yake ya kuhangaisha watu kijijini na hata familia yake hadi mkewe akatoroka. Alisema Wekesa alionekana na jirani akitumia ngumi na mateke kumpiga mtoto huyo.

You can share this post!

RAILA: Kwa nini simpendi Ruto

Madiwani wa kike kuadhibiwa kwa kupigania dume

adminleo