HabariSiasa

Tumbojoto bungeni kuhusu ombi la Ouda kutaka Ruto asiwanie 2022

August 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kisumu ya Kati Fred Ouda Odhiambo (pichani), Alhamisi amewasilisha ombi akipendekeza katiba ifanyiwe marekebisho ili kumzuia Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Pia anataka manaibu gavana ambao wamehudumu mihula miwili kuzuiwa kuwania ugavana. Anasema Naibu Rais na manaibu gavana huchaguliwa kwa tiketi moja na rais na magavana mtawalia.

Lakini Kiongozi wa Wengi bungeni Aden Duale amepuuzilia mbali ombi la Ouda akisema linakiuka kipengee 137 (1) cha Katiba..

Naye Mwenyekiti wa chama cha ODM aliye pia Kiongozi wa Wachache bungeni John Mbadi amesema ombi la Bw Ouda ni la kikatiba na lina mashiko ya kisheria.

Hata hivyo, Bw Mbadi anasema Bw Ouda angewasilisha marekebisho hayo moja kwa moja kwani kamati ya sheria inaweza kulihujumu.

Lakini mbunge wa Rarieda Bw Otiende Amollo amesema ombi hilo linakwenda kinyume cha katiba na linapasa kuuawa bungeni hata kabla ya kuwasilishwa kwa kamati ya bunge kuhusu sheria.

Spika Justin Muturi amesema, “Bunge hili linaweza kukataa ombi hili kwa sababu linalenga kufasiri vifungu vya katiba, 137 na 142. Hili ni jukumu la mahakama chini ya kifungu cha 165, wala sio la bunge.”

Chris Wamalwa, mbunge wa Kiminini, amesema ni haki ya Bw Ouda kuwasilisha ombi hilo kulingana na kipengee cha 119 cha Katiba.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro naye akasema ombi hilo halina maana na limewasilishwa kwa nia mbaya.

“Hatutaruhusu watu fulani waliodhaminiwa na wagombea fulani wa urais kutumia muda wa bunge kuwachafulia jina wenzao.” akasema.

Mbunge Olago Aluoch (Kisumu Magharibi) amesema ombi hilo linaipotezea bunge wakati na linapasa kukataliwa mara moja.

“Mheshimiwa Spika mbona afisi yako ilipitisha ombi kama hili?” Olago ambaye ni wakili mtajika akauliza.

Baadaye Spika Muturi alitupilia mbali ombi la Bw Ouda na kuamuru iwe shughuli ya Kamati ya Sheria inayoongozwa na mbunge William Cheptumo ( Baringo Kaskazini).