Wasomi wa Kiswahili wakutana chuoni Moi kwa kongamano kuu
Na TITUS OMINDE
WASOMI na wataalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Afrika Mashariki wanashiriki katika kongamano la Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi, bewa kuu la Keses mjini Eldoret.
Kongamano hilo la siku tatu ambalo linaanza Jumatano limefadhiliwa na chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) na Idara ya Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Moi.
Washiriki katika kongamano hilo watajadili umuhimu wa Lugha ya Kiswahili katika mshikamano wa kitaifa na uwiano barani Afrika.
Mmoja wa waandalizi wa kongamano hilo, Dkt Allan Opijah alifichua kuwa mbali na kujadili mbinu bora za kuboresha lugha ya Kiswahili, kongamano hilo linalenga kutoa changamoto kwa serikali kukumbatia lugha hiyo katika juhudi za kuimarisha uwiano miongoni mwa Wakenya wa matabaka mbalimbali.
Kongamano hilo la kila mwaka ambalo ni la awamu ya 20 linatarajiwa kufunguliwa na mwenyekiti wa Tume ya Elimu ya Juu (CUE) Prof Chacha Nyaigoti Chacha.
Waandalizi wa kongamano hilo walitoa changamoto kwa bunge kubuni njia za kuboresha lugha ya Kiswahili nchini kupitia kwa katiba.
Wakihutubu mjini Eldoret, walitaka serikali kuwa na bajeti maalum ya kuboresha lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Kongamano la mwaka 2017 lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Kibabii katika Kaunti ya Bungoma.