Kidero kufikishwa mahakamani kwa ufisadi
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero, anatarajiwa kufikishwa mahakamani Alhamisi kushtakiwa kwa ufisadi.
Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Jumatano jioni walimkamata gavana huyo aliyeondoka na kusema atashtakiwa pamoja na watu wengine saba kwa ufujaji wa fedha za umma alipokuwa mamakani.
Kulingana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), wengine watakaoshtakiwa ni aliyekuwa Katibu wa Kaunti, Bi Lilian Wanjiru Ndegwa, na maafisa waliokuwa wakuu wa fedha Bw Jimmy Mutuku Kiamba, Bw Stephen Ogaga Osiro, Bw Luke Mugo Gatimu, Bw Maurice Ochieng Okere na Bw Gregory Mwakanongo.
Wengine waliohusishwa na sakata hiyo ni wafanyabiashara John Githua Njogu na Grace Njeri Githua wa Lodwar Wholesalers/Ngurumani Traders Ltd.
“DPP alikagua faili iliyowasilishwa kwake na EACC akaridhika kwamba watu waliotajwa wanastahili kushtakiwa,” ikasema taarifa ya afisi ya DPP inayosimamiwa na Bw Noordin Hajji.
Hivi majuzi, EACC ilifichua kwamba inachunguza magavana 30 wakiwemo wengine ambao walisalia mamlakani baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kufikia sasa, viongozi wengine wa kaunti waliokamatwa na EACC kwa madai ya ufisadi ni Gavana wa Busia, Bw Sospeter Ojaamong, na aliyekuwa Gavana wa Nyandarua, Bw Daniel Waithaka.