• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Mudavadi awaonya vikali Malala na Osotsi

Mudavadi awaonya vikali Malala na Osotsi

NA CECIL ODONGO

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress Musalia  Mudavadi amewaonya vikali  Senata wa Kakamega Cleophas Malala na Mbunge Maalum Godfrey Osotsi  dhidi ya kuendelea kudunisha na kukaidi maamuzi ya chama.

Bw Mudavadi amesema kwamba mienendo ya  wabunge hao wawili inatazamwa na kufuatiliwa kwa makini na hivi karibuni wataangushiwa adhabu kali katika mkutano wa baraza kuu(NEC) la chama

“Ningependa kutoa onyo kali kwa Bw Malala na Bw Osotsi ambao hawajihusishi tena na maswala ya chama na hata kunikashifu hadharani. Tunawatazama na chama kinaandaa kuwaadhibu kali, ” akasema Bw Mudavadi.

Wabunge hao wawili katika siku za hivi karibuni wameonekana kuwa watetezi wakuu wa Kinara wa ODM Raila Odinga na wamekuwa wakimkashifu  kiongozi huyo hadharani tangu akose kuhudhuria kuapishwa kwa Bw Odinga Machi 9.

 Aidha Mudavadi alitangaza rasmi kwamba yeye ndiye kinara mpya wa upinzani nchini na kupuuza madai kwamba kuna mpango wa kumjumuisha katika baraza la mawaziri.

Vile vile makamu huyo wa rais wa zamani alisema kwamba serikali ya muungano ni njia inayotumiwa na viongozi wakuu nchini kuua demokrasia ya vyama vyingi na kuirudisha taifa nyuma katika enzi za chama kimoja.

“Habari kwamba nitauungana na serikali hazina msingi wala mashiko. Kama chama tunapinga mabadiliko ya baraza la mawaziri ili kuwatunuku watu binafsi nafasi ya uongozi. Hii ni njia ya kuua demokrasia,” akasema Bw Mudavadi Jumatano wakati wa uzinduzi wa mrengo wa kitaifa wa vijana wa chama hicho katika makao yao makuu mjini Nairobi.

Aidha kinara huyo wa ANC alipinga pendekezo la kubadilisha katiba akisema mchakato mzima lazima uhusishe Wakenya wote badala ya watu wachache wanaolenga kujitunuku vyeo.

Akigusia ajenda za mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila odinga, Bw Mudavadi alisema mazungumzo hayo hayajumuishi Wakenya wote kwa sababu hakujaandaliwa mazungumzo ya kitaifa yanayohusisha viongozi wote wakuu na wakilishi wa maeneo yanayohisi yametengwa na serikali.

You can share this post!

Wakazi wa mitaa ya mabanda waandamana kupinga ubomoaji

Ufaransa yaharamisha simu za tableti shuleni

adminleo