• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Ufaransa yaharamisha simu za tableti shuleni

Ufaransa yaharamisha simu za tableti shuleni

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

SERIKALI imepiga marufuku simu za rununu na vidubwasha vingine vya tableti katika shule zote baada ya bunge kupitisha sheria mpya.

Sheria hiyo ilipitishwa kufuatia ahadi ya Rais Emmanuel Macron aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi, lakini wabunge wa upinzani walisusia kikao hicho cha bunge.

Ingawa viongozi serikalini wanasema uamuzi huo umenuiwa kulinda athari mbaya za simu kwa watoto, wale wa upinzani wanasema serikali inajitafutia sifa kwa kupitisha sheria zisizo na maana.

Wapinzani wengine wanasema hiyo ni hatua itakayorudisha Ufaransa nyuma wakati ambapo mataifa mengi ulimwenguni yanakumbatia teknolojia kwa elimu.

Marufuku itaekwa kwa wanafunzi wote wenye umri wa hadi miaka 15 wakati muhula mpya utakapoanza Septemba.

Wanafunzi hawataruhusiwa kuingia na simu zao shuleni na ikiwa ni lazima wazibebe, itakuwa ni marufuku kuziwasha wakati wowote wanapokuwa shuleni.

Tafiti mbalimbali zimeonyesha idadi kubwa ya matineja wanashikwa na uraibu wa kutumia au kuchezea simu za rununu kwa kiasi cha kuathiri uwezo wao wa kuwasiliana au kujumuika na wenzao kwa shughuli za kijamii.

Awali kulikuwa na sheria ambayo ilipiga marufuku utumizi wa simu hizo darasani, ambayo ilikuwa imepitishwa katika mwaka wa 2010.

-Imekusanywa na Valentine Obara

You can share this post!

Mudavadi awaonya vikali Malala na Osotsi

Watalii wanene walaumiwa kuvunja viungo vya punda

adminleo