• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Waliobomolewa majengo Nairobi walete vibali – Polisi

Waliobomolewa majengo Nairobi walete vibali – Polisi

Na CHARLES WASONGA

POLISI sasa wanawataka wamiliki wa majengo ambayo yaliathirika katika ubomoaji unaoendelea kuwasilisha stakabadhi zinazoonyesha kuwa walipata kibali cha kujenga karibu na mito.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa msemaji wa polisi Charles Owino alisema stakabadhi hizo zitaisaidia serikali kuwapata maafisa wa serikali waliidhinisha ujenzi wa majengo hayo kinyume cha sheria.

Ubomoaji huo, Owino alifichua, unaendeshwa na Kamati ya Maalum iliyobuniwa na serikali kukomboa maeneo ya mito, almaarufu, Nairobi Regeneration Committee, iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Sharti tuwapate wale watu ambao waliidhinisha ujengo wa majengo haya wakati huo ili wawajibikie makosa waliyofanya,” akasema Bw Owino.

Kauli ya Idara ya Polisi inajiri baada ya Rais Kenyatta kuamuru kwamba maafisa wote wa serikali walioidhinisha ujenzi wa majengo hayo kando ya mito wachukuliwe hatua za kisheria

Tayari Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji amemwamuru Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuanzisha uchunguzi kuhusiana na uidhinishwaji wa majengo hayo kisha awalishe ripoti baada ya siku 21.

“Kwa kushauriana na Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko, nimeamuru DCI kuanza uchunguzi mara moja kubaini hali, taratibu na watu ambao walitoa idhini kwa ujenzi wa majengo hayo kando ya mito kinyume cha sheria,” Haji akasema.

Mnamo Ijumaa, maafisa wa serikali walibomoa jumba la kibiashara la Ukay Centre katika mtaa wa Westlands, siku mbili baada ya kubomolewa kwa jumba la Southend Mall liliko katika makutano ya barabara za Langata na Mbagathi.

Mnamo Jumanne majengo ya Java Restaurant na Kituo cha Petroli cha Shell katika mtaa wa Kileleshwa yalibomolewa.

Majengo mengine ambayo yamepangiwa kubomolea na Oshwal Centre lililoko karibu na Ukay Centre inayomilikiwa na mfanyabiashara tajiri Bimal Shah.

Zaidi ya majengo 340 ambayo yalijengwa kando ya mito katika kaunti ya Nairobi inatarajiwa kubomolewa katika operesheni hii ambayo imepangiwa kuendelea kwa muda wa wiki tatu zijazo.

You can share this post!

Swazuri atiwa nguvuni kuhusiana na sakata ya mamilioni SGR

Haji aje bungeni awakamate wabunge waliomeza hongo ya...

adminleo