• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
KURUNZI YA PWANI:  Watu wengi hutoweka bila kupatikana Lamu

KURUNZI YA PWANI: Watu wengi hutoweka bila kupatikana Lamu

Na KALUME KAZUNGU

NI jambo la kawaida katika eneo la Pwani kusikia kuwa mtu ametoweka bila ya kupatikana tena. Wengi wanaopatikana, huwa wameuawa na miili yao huwa imeoza au hata kuliwa na wanyama mwitu.

Kati ya maeneo yote ya Pwani, Lamu imeorodheshwa ya kwanza kwa visa vya kupotezwa kwa au kuuawa kwa vijana katika hali tatanishi wakiwa mikononi mwa walinda usalama Ukanda wa Pwani.

Kulingana na ripoti ya hivi punde kutoka kwa Shirika la kutetea haki za binadamu la HAKI Africa, jumla ya vijana 46 waliripotiwa kupotezwa au kuuawa na polisi na jeshi (KDF) katika hali isiyoeleweka eneo la Pwani.

Kati ya 46, vijana 15 walipotezwa au kuuawa wakiwa kaunti ya Lamu ilhali waliobakia wakipotezwa au kuuawa wakiwa maeneo mbalimbali ya kaunti zote sita za Pwani.

Akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Huduma Centre mjini Lamu, Mkurugenzi Mkuu wa HAKI Africa, Hussein Khalid, alisema shirika hilo tayari limewasilisha malalamishi kortnini kuhusiana na hali hiyo aliyoitaja kuwa ya kutia hofu.

Bw Khalid alisema ni jambo la kusikitisha kwamba walinda usalama wamekuwa wakiendeleza dhuluma na ukandamizaji wa raia na hata kuendelea ukiukaji wa haki za binadamu katika harakati zao za kuweka usalama hapa nchini.

Alimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i na Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet kuingilia kati na kukomesha dhuluma hizo zinazoendelezwa na maafisa wao wakiwa kazini.

“Kama shirika, hatujaridhishwa kamwe na hali inayoendelea miongoni mwa vitengo vya usalama. Polisi na KDF wamekuwa mstari wa mbele kuwakamata vijana na kuwapoteza au kuwaua katika hali isiyoeleweka.

Tumepokea malalamishi chungu nzima kutoka kwa wanafamilia wakitaka idara ya usalama kueleza waliko watu wao.

Sisi hatutakubali kuvumilia ukiukaji wa haki za binadamu ukiendelezwa na maafisa wetu wanaofaa kutulinda. Ningewasihi Bw Matiang’i na Bw Boinnet kuchunguza hao maafisa wa usalama. Y

eyote atakayepatikana kwamba alihusika katika kuwapoteza vijana akamatwe na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria. Hakuna ambaye yuko juu ya sheria eti kwa sababu yeye ni polisi au jeshi,” akasema Bw Khalid.

Kauli ya afisa huyo inajiri wakati ambapo familia nyingi kaunti ya Lamu zimekuwa zikiililia serikali kueleza waliko watu wao wanaoaminika kukamatwa na maafisa wa polisi na jeshi.

Katika eneo la Witu, familia ya Bw Mohamed Abdala Ali,32 ambaye alitoweka tangu Juni 14 mwaka huu tayari imejitokeza kuiomba serikali kueleza aliko jamaa wao.

Dakake mwaathiriwa, Bi Amina Abdalla, anasema licha ya kupiga ripoti kwa polisi mara kadhaa ili kusaidia katika kumtafuta jamaa wao, polisi wamekuwa wakipuzilia suala hilo, jambo ambalo familia hiyo inashuku huenda walinda usalama wanahusika katika kupotea kwa jamaa huyo.

Mjini Lamu, familia ya mzee Said Makka bado imeachwa gizani kufuatia kutoweka kwa kijana wao, Imrana Said Makka miaka minne iliyopita.

Bw Imrana, 29, anadaiwa kukamatwa na maafisa wa polisi akiwa mjini Malindi mnamo Machi 31, 2015 na tangu hapo hajulikani alipo.

Mjini Manda, kaunti ndogo ya Lamu Magharibi, familia ya Bw Mohamed Avukame Haroun,43 imekuwa ikihangaika kumtafuta aliko baada ya kukamatwa nje ya Mahakama Kuu ya Mombasa mnamo Aghosti 23, 2017.

Familia inaamini kwamba waliomkamata jamaa wao ni maafisa wa polisi kutokana na kwamba walipomkamata walikuwa wamejihami kwa bunduki na pingu.

Kijijini Kwasasi tarafa ya Hindi, familia moja pia inahangaika kumtafuta jamaa wao, Ali Bunu, 42 ambaye anadaiwa kuchukuliwa na wanajeshi wa KDF kutoka shambani mwake mnamo usiku wa Aprili 8, 2016.

Walioshuhudia tukio hilo wanadai wavamizi walimlazimisha kuingia gari la jeshi kabla ya kusafirishwa kuelekea kambi ya KDF eneo la Bar’goni.

Mjini Mpeketoni, samilia nyingine inahangaika kumtafuta jama wao, Osman Abdi ambaye alitoweka muda mfupi baada ya shambulizi la kigaidi mnamo Juni 15, 2014.

Jamaa huyo ambaye alikuwa muuzaji maziwa anadaiwa kunaswa na maafisa wa polisi na kulazimishwa kuingia kwenye gari lao na kutoweka ghafla.

Hadi sasa hajulikani aliko.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Kampuni inayowafaa wanafunzi werevu...

TANA RIVER: Miundomsingi mibovu ndicho kiini cha wanafunzi...

adminleo