OBARA: Kutunza mazingira ni bora kuliko ajenda zote
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI ya Rais Uhuru Kenyatta huenda ina makosa mengi mno iliyotenda na kuathiri vibaya hali ya mwananchi wa kawaida tangu 2013, lakini jambo moja litakalonifanya kushukuru serikali hii daima ni ikiwa itafanikiwa kutatua janga la uharibifu wa mazingira.
Nina imani kuwa mtetezi mkuu wa mazingira nchini humu, marehemu Wangari Maathai, angekuwa mwingi wa furaha hivi leo iwapo angeshuhudia yale ambayo yanafanywa na serikali yetu.
Kuanzia kwa juhudi za kuondoa watu walioishi ndani ya Msitu wa Mau kiharamu, hadi ubomoaji wa majengo yaliyo karibu na mito na chemchemi zingine za maji, serikali haijaonyesha huruma kwa wanyakuzi ila kujitolea kurudishia mazingira yetu hadhi yake.
Kwa miaka mingi, suala la kuhifadhi mazingira halikuwa likichukuliwa kwa uzito katika masuala ya utawala wa nchi hii.
Tumekuwa tukijihusisha zaidi na changamoto nyingine zinazotukumba kama vile ufisadi, njaa, ukosefu wa rasilimali bora miongoni mwa mengine huku mazingira ikiachiwa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo hayawezi kufanikiwa bila mchango wa serikali.
Mashirika hayo yanaweza tu kutoa mchango wa kuhamasisha jamii na pengine kuendeleza miradi midogo ya kuhifadhi mazingira.
Inapofikia masuala ya uundaji wa sera na utekelezaji wa sheria kuhusu mazingira, ni sharti serikali ndiyo ijitolee kikamilifu.
Wakati huu ninafahamu kuwa Rais Kenyatta ana mambo mengi ambayo angependa kutimiza kabla akamilishe hatamu yake ya pili ambayo pia ni ya mwisho ya uongozi katika mwaka wa 2022.
Kwa mfano kuna ajenda zake nne kuu za maendeleo, kisha kuna janga la ufisadi analopambana nalo.
Kuhusu ajenda kuu za maendeleo, kwa mtazamo wangu haitakuwa rahisi kuzitekeleza kikamilifu kwani taifa hilo tayari lina madeni makubwa mno ilhali ajenda hizo zinahitaji ufadhili wa mabilioni ya pesa.
Kwa upande mwingine, kesi za ufisadi huwa ni nzito, zinahusu mambo mengi ambayo upelelezi wao na uendeshaji wa kesi huhitaji muda mrefu kabla kesi itamatike.
Hivyo basi, hata kama mahakama na idara nyingine husika katika vita dhidi ya ufisadi zitakaza kamba kujaribu kuharakisha kesi hizo, nadhani ni chache mno zinazoweza kutamatishwa kwa njia inayofaa kabla tufike mwaka wa 2022.
Kwa msingi huu, rais ana nafasi bora ya kutekeleza jambo moja muhimu ambalo litampa sifa sasa na katika viazi vyote vijavyo: utunzaji wa mazingira.
Mbali na hayo, sheria zetu ingawa zina nguvu, ni muhimu utathmini ufanywe ili kuziba mapengo yoyote ambayo yanaweza kutumiwa na mabwenyenye kutuharibia mazingira.
La mno ni kwamba uharibifu wa mazingira ni suala linaloenda sambamba na ufisadi na athari zake ni kusababishia taifa majanga ikiwemo mafuriko na kiangazi ambazo huathiri uwezo wetu wa kuzalisha lishe ya kutosheleza mahitaji ya wananchi.