Mama Mtanzania mashakani kuingiza kiwete Kenya kumtumia kujitajirisha

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE raia wa Tanzania anayewashiriki katika ulanguzi wa binadamu ameshtakiwa kumwigiza humu nchini mtoto kiwete mwenye umri wa miaka saba kufanya kazi ya kuomba katika barabara za jiji la Nairobi.

Bi Kwandu Cheye mwenye umri wa miaka 43 alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani, Nairobi Bw Francis Andayi.

Mashtaka dhidi ya Bi Cheye yalikuwa kati ya Mei na Agosti 2018 alimsafirisha mtoto huyo kiwete kutoka nchini Tanzania hadi Nairobi nchini Kenya alipomtumia kujitajirisha kwa “kumpeleka kwenye barabara kuomba.”

Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi alimweleza Bw Andayi kuwa Bi Cheye alikuwa anampeleka mlalamishi katika moja ya barabara za mtaa wa Eastleigh, Nairobi kuomba.

“Pesa zote ambazo mlalamishi alikuwa anapewa na wahisani zilikuwa zinachukuliwa na Bi Cheye kujitajirisha,” Bw Andayi alifahamishwa, mshtakiwa aliposomewa mashtaka.

Mahakama iliambiwa kuwa wakazi wa mtaaa wa Eastleigh walimnusuru mtoto huyo, ambaye jina lake hatuwezi kuchapisha kwa sababu ya umri wake mdogo, na kumpeleka katika kituo cha polisi.

“Alipookolewa, mtoto huyo alikuwa na mkebe uliokuwa na Sh450 alizokuwa amepewa na wahisani,” hakimu alijulishwa.

Bi Cheye alikanusha mashtaka matatu dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

“Je, uko na uwezo wa kumwajiri wakili akutetee kwa vile kesi hii inayokukabili ni kali. Ukipatikana na hatia utasukumiwa kifungo cha miaka mingi gerezani,” Bw Andayi alimshauri.

“Sina uwezo kifedha kusaka  huduma za wakili. Naomba hii mahakama inisaidie,” Bi Cheye alijibu.

“Basi itabidi uandike barua kupitia kwa afisa mkuu wa hii mahakama upewe wakili atakayekutetea. Karani wa mahakama atakusaidia kujaza fomu ya kuomba huduma za wakili,” Bw Andayi alimweleza.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu. Kesi itasikizwa Agosti 23, 2018.