Raia wa Uganda na DRC wasakwa kwa ulaghai wa dhahabu
Na RICHARD MUNGUTI
RAIA wawili wa kigeni wameamriwa watiwe nguvuni kwa kuwalaghai wafanyabiashara wa kimataifa zaidi ya Sh85 milioni katika kashfa ya dhahabu.
Mahakama ya Milimani Nairobi iliamuru raia wa Congo Bw Kelvin Essoa Nkoy na raia wa Uganda Bw Kayombya Gormon almaarufu Timothy Mureithi watiwe nguvuni kwa kuwalaghai Mabw Prakash Robert Deepal Baichan na raia wa Brazil Bw Samir Entoro jumla ya Sh85 milioni wakiwadanganya watawapelekea kwa njia ya ndege kilo 568 za dhahabu.
Bw Nkoy aliamriwa atiwe nguvuni na hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku ilhali Bw Gormon aliagizwa akamatwe na hakimu mkuu Bw Francis Andayi.
Wawili hawa wameshtakiwa pamoja na Wakenya Mabw Philip Nashon Aroko, Roy Shirekuli, wakili Munzala Javier Rumili, Sikanda Ismail Abdallah Saleh, Benson Muhanji na Jared Otieno.
Washtakiwa hawa wanakabiliwa mashtaka ya kuwalaghai wafanyabiashara hawa wa kimataifa pesa zao jijini Nairobi.
Mabw Aroko, Shirekuli , Rumili, Saleh na Otieno wanakabiliwa na shtaka la kumlaghai Bw Entoro dola za kimarekani $232,000 (Sh23,200,000) wakidai wangelimpelekea kilo nane za dhahabu mjini Dubai.
Shtaka lasema kuwa sita hao walimlaghai Bw Entoro kati ya Mei 15 na Juni 9, 2018.
Washtakiwa walikana shtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana isipokuwa Kayombya ambaye korti
Iliamuru atiwe nguvuni na polisi wa kimataifa na kurudishwa Nairobi kuendelea na kesi.
Wakili Stanley Kang’ahi aliomba mahakama iamuru maafisa wa polisi waachilie gari la Bw Aroko inayozuiliwa katika kituo cha Parklands.
Bw Kang’ahi aliamriwa awasilishe ombi rasmi akiomba gari hilo liachiliwa ikiwa haishikiwe kutumika kama ushahidi.
Afisa anayechunguza kesi hiyo alimweleza hakimu kuwa ugari hilo la Bw Aroko ndilo lilikuwa lasafirisha dhahabu hiyo na “ni mojawapo ya ushahidi.”
Bw Andayi aliombwa atengee kesi hiyo muda wa miezi miwili kumwezesha Bw Entoro asafiri ng’ambo kwa matibabu.
Washtakiwa hao walikanusha shtaka dhidi yao na Bw Andayi akaaamuru Bw Kayombya ambaye ni raia wa Uganda atiwe nguvuni.
Mbali na kuamuru Bw Nkoy atiwe nguvuni, Bi Mutukua aliamuru dhamana iliyopewa raia huyo wa Congo Nkoy itwaliwe na Serikali baada ya kutoroka.
Bi Mutuku alitoa agizo hilo baada ya kufahamishwa Bw Nkoy alitoroka na hajulikani aliko.
Bw Nkoy amewashtakiwa pamoja na Mabw Saleh na Muhanji kwa kumlaghai mfanya biashara wa kimataifa Bw Prakash Robert Deepal Baichan dola za kimarekani 621,100 (Sh62,110,000) wakijifanya walikuwa na uwezo wa kumpelekea kilo560 za dhahabu.
Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Pamellah Avedi kwamba Bw Baichan yuko ng’ambo na polisi wanajaribu kuwasiliana naye arudi nchini kutoa ushahidi.
Watatu hao wamekana walimndanganya Bw Baichan kuwa watampelekea kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta dhahabu hiyo.
Walikuwa wapeleke dhahabu hiyo uwanja wa ndege wa Dubai ulioko katika milki za uarabuni.
Kesi hiyo iliahirishwa kwa muda wa miezi miwili hadi Oktoba 12 2018