• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Hatuwezi kumeza hongo ya Sh10,000, wabunge wajitetea

Hatuwezi kumeza hongo ya Sh10,000, wabunge wajitetea

Peter Mburu, Oscar Kakai na Hamisi Ngowa

WABUNGE wawili Jumatatu walijitokeza kupinga madai kwamba kulikuwa na hongo bungeni Alhamisi iliyopita kabla ya ripoti kuhusu sukari ghushi kutupwa.

Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing na mwakilishi wa wanawake kaunti ya Wajir Fatuma Gedi jana walipuuzilia mbali madai kuwa wabunge walipokea rushwa ili kuitupa ripoti ya kamati za biashara na kilimo, wakisema ni propaganda zisizo na msingi.

Bw Pkosing alisema sababu ya wabunge kuitupa ripoti hiyo ni kwa kuwa ilikosa uzito na ukweli, na aka akawatetea mawaziri wa fedha Henry Rotich, wa jamii ya Africa mashariki Adan Mohammed na aliyekuwa waziri wa kilimo Willy Bett, ambao ripoti hiyo ilipendekeza wachunguzwe kuhusiana na kuingizwa kwa sukari ghushi nchini.

“Hakuna kitu kwenye hiyo ripoti ambayo inawalaumu, tuwache siasa. Tulifanya kulingana na sheria ya bunge na si vyema kupiga kelele sababu upande wako haukushinda,” akasema Bw Pkosing .

Vilevile Bi Gedi alipinga madai kuwa alihusika kuwapa hongo wabunge Alhamisi ili waitupe ripoti hiyo, akilaumu wabunge wanaolalamika kuwa wametumwa kuwachafulia wabunge majina na watu wa kutoka nje.

“Wanafanyia kazi watu wengine kutoka sehemu zingine ambao lengo lao tu ni kuwachafulia majina wabunge. Nawezaje kumhonga kiongozi wa wengi bungeni kwa Sh10,000?” akahoji Bi Gedi, akisisitiza kuwa atakuwa tayari kuitupa ripoti nyingine itakayowasilishwa bungeni ikiwa na upungufu kama huo.

Lakini mbunge wa Likoni Mishi Mboko alikosoa  hatua ya wabunge walioitupilia mbali ripoti hiyo, akisema kuwa badala yao kuitupilia mbali, wangefaa kuichambua na kuondoa vipengee walivyohisi  kuwa vilikuwa na utata.

Bi Mboko aidha alisema kuna uwezekano wabunge hawakuzingatia mapendekezo mengine mazuri  yaliyokuwa katika ripoti hiyo ikiwemo utoaji wa muongozo ambao ungeweza kuzuia sakata kama hiyo kutokea  tena katika siku za usoni.

“Japo sikuwa bungeni wakati ripoti hiyo ilipowasilishwa, wabunge wangefaa kuichambua na kuondoa yale waliyohisi kuwa hayafai badala ya kutupilia mbali ripoti yote,’’akasema mbunge huyo.

You can share this post!

Kongamano kuandaliwa kuzima utovu wa usalama

Gor yaadhibu Homeboyz na kukaribia taji la 17 KPL

adminleo