• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Babu Owino mbioni kuwasilisha mswada kurejesha wanafunzi watundu darasani

Babu Owino mbioni kuwasilisha mswada kurejesha wanafunzi watundu darasani

Na PETER MBURU

Huenda wanafunzi wengi wa taasisi za masomo na vyuo vikuu ambao wako nyumbani baada ya kutimuliwa kwa sababu tofauti wakapata afueni ya kurudi darasani, endapo mswada anaopanga kuwasilisha bungeni mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino utafaulu.

Bw Owino mnamo Jumatano aliliandikia bunge pamoja na mwenyekiti wake wa kamati ya elimu, utafiti na teknolojia Bw Julius Melly, akitaka wanafunzi ambao wametimuliwa vyuoni warejee, kwani wengi hawakutimuliwa kwa haki.

Kulingana na mbunge huyo, viongozi wa vyuo wamekuwa wakiwanyanyasa wanafunzi haswa walio na usemi wa kisiasa na huwa wanatumia mbinu ya kuwatimua vyuoni kuwanyamazisha.

“Wanafunzi wote waliotimuliwa kabisa ama kwa muda na vyuo vikuu/vyuo watarejea darasani hivi karibuni. Nimeliandikia bunge kuheshimu haki za wanafunzi za elimu kwani ni imani yangu kuwa sote tunafaa kupewa nafasi ya pili kufanya vyema ama vibaya,” akachapisha Bw Owino kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Kwenye barua aliyoliandikia bunge, mbunge huyo anasema kuwa ana ushahidi kuwa wengi wa wanafunzi waliotimuliwa walijaribu kujitetea lakini wakuu wa vyuo wakawanyima nafasi hiyo, hata walipoenda kortini na vyuo kuamrishwa viwarejeshe darasani.

Anasema adhabu ambayo vyuo vinatoa kwa wanafunzi ni kali mno, na kuwa wakuu wengi wa vyuo wanaadhibu wanafunzi kutokana na sababu za kisiasa.

Hivyo, Bw Owino analitaka bunge kuwaalika wakuu wa vyuo vilivyoadhiriwa kuelezea utaratibu uliotumiwa kuwatimua wanafunzi, na kuamrisha wizara ya elimu kutupilia mbali utimuaji wa wanafunzi hao.

Aidha, mbunge huyo anataka bunge kuidhinisha sheria ambayo itawazuia wakuu wa vyuo kuwatimua wanafunzi wanaopatikana na makossa yasiyohusiana na elimu moja kwa moja kwa zaidi ya miaka miwili.

You can share this post!

UBOMIAJI: Sonko na Waititu warukiana mitandaoni

Mali ya East Africa Cement kupigwa mnada kulipa wafanyakazi

adminleo