• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
SAKATA YA NYS: Kesi kuanza kusikizwa Januari 2019

SAKATA YA NYS: Kesi kuanza kusikizwa Januari 2019

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya sakata ya Sh469 milioni katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lilian Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu NYS Dkt Richard Ndubai na washukiwa wengine 41 itaanza kusikizwa Januari 7, 2019.

Kesi hiyo itaanza kusikizwa na hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko.

Kiongozi wa mashtaka Bw Gitonga Riungu alieleza Bw Ooko kuwa atatayarisha cheti kingine cha mashtaka kitakachowashirikisha washukiwa wote 47.

Faili tatu zimeunganishwa kuwa kesi moja baada ya hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti kumwamuru Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji agawanye kesi 10 zinazowakabili washukiwa hao wanaojumuisha wafanyabiashara wa Naivasha wa Familia ya Ngirita kuwa tatu.

“Kufuatia maagizo ya Bw Ogoti nimeunganisha kesi tatu kusikizwa kwa pamoja kwa vile mashahidi ni sawa,” alisema Bw Riungu.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa kuna washukiwa watatu ambao hawajajibu mashtaka.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa wakiongozwa na wakili Migosi Ogamba walisema wamepokea nakala za mashahidi kutoka kwa afisa anayechunguza kesi hiyo.

Mahakama ilifahamishwa kuwa nakala za usahidi ambazo hazijapokewa zitachukuliwa katika afisi ya mkurugenzi wa jinai (DCI).

Bw Ooko aliamuru kuwa kesi hiyo itaendelea kila siku kuanzia Januari 7, 2019 bila kuahirishwa.

Naye Bw Ogoti ataanza kusikiza kesi tano ambazo zimeunganishwa kusikizwa pamoja kuanzia Oktoba 29 mwaka huu.

Bw Ogoti alimwamuru Bw Haji Jumanne atenganishe kesi dhidi ya washukiwa hao wote ndipo sisikizwe na kuamuliwa kwa haraka.

“Kesi hizi zitasikizwa kila siku pasi kuahirishwa,” aliagiza Bw Ogoti.

Aliagiza washtakiwa wanaotaka kusuluhisha kesi dhidi yao na DPP wafanye hivyo na kuwasilisha makubaliano mahakamani.

Pia aliwaonya mawakili dhidi ya kuzembea katika kazi zao za kuwatetea washtakiwa akisema , “kesi hizi hazitacheleweshwa na kutokuwako kwa mawakili.”

Mahakama iliwatahadharisha mawakili na washtakiwa dhidi ya kufanya njama za kuahirisha kesi.

Katika kesi hiyo, washtakiwa watano kutoka kwa familia moja (Ngirita) wamefunguliwa mashtaka.

You can share this post!

Kizimbani kwa kufanya kazi kwa jengo lisilo na leseni

Pigo kuu kwa Ruto Pwani Kingi kuungana na Joho

adminleo