TAHARIRI: Kinaya ni kuwa hela za ushuru bado zitafujwa
NA MHARIRI
Hayawi hayawi hatimaye huwa na sasa baadhi ya ushuru mpya uliopendekezwa na serikali kwenye bajeti tayari umeanza kutekelezwa.
Ushuru katika bidhaa za kilimo tayari umeshaanza kutekelezwa; wakulima walioenda dukani jana kununua bidhaa kama mbolea na dawa za mimea wakilazimika kuongeza kati ya Sh100-300 kwa kutegemea bidhaa husika.
Ushuru kuhusu huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu ulishaanza Julai, na kinachosubiriwa mwezi ujao ni ule utakaopekelea mafuta ya petroli kuuzwa Sh130 kwa lita.
Lakini kinachoonekana kukera wananchi zaidi, haswa wale walioajiriwa ni ule ushuru wa asilimia 0.5 ya mshahara utakaotozwa kila mfanyakazi kwa ajili ya mradi wa Serikali wa kujenga nyumba za bei nafuu, almaarufu UHC.
Ki msingi, kile serikali inasema ni kuwa inataka kukata watu mishahara ili ijengee wale walio na pato la chini nyumba za bei nafuu. Katika nchi yoyote ile, pendekezo hili lingeshabikiwa sana na lingeleta mabadiliko ya aina yake.
Lakini hii ni Kenya. Hii ni nchi ambayo ufisadi umekiti mizizi katika kila idara na kila sekta ya kimaisha kiasi kwamba hivi sasa ni vigumu kufikiria nyanja yoyote ya kimaisha ambayo haijakolea na kutafunwa na ufisadi.
Kwa mfanyakazi anayefanya bidii na anayetozwa ushuru wa kupindukia tayari kwa misingi ya PAYE, VAT na huduma kadhaa kama NHIF, kumuongezea mzigo wa 0.5% kwenye mshahara wake ni kumjaribu imani na uvumilivu wake.
Kinachoongeza uchungu zaidi ni kuwa hakuna thibitisho lolote kwamba pesa hizo zitatumika kikamilifu kwenye mradi huo.
Na pili, hakuna hakikisho kwamba anayetozwa ushuru huo atafaidika kwa vyovyote na nyumba hizo au hata angalau wale wanaolengwa wanufaike.
Kinachotazamiwa kutokea ni kwamba bado wale mabwanyenye walio na majumba tele jijini ndio watakaonunua nyumba hizo za bei nafuu na kuuzia au kukodisha kwa walala hoi, kama ilivyoshuhudiwa kwenye mradi wa nyumba Kibera.
Kuna maamuzi mengi tatanishi ya kifedha yanayofanywa kwenye taifa hili na itawalazimu wananchi wawazie na kuona kwamba watastahimili kwa kiwango kipi.