Habari Mseto

Kushuka kwa ada ya umeme kuchukua muda

August 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Huenda bei ya umeme ikashuka baada ya Wizara ya Kawi kumaliza mikataba ya ununuzi wa kawi (PPA).

Waziri wa Kawi Charles Keter Jumatano alisema hilo liliafikiwa baada ya jopo lililoundwa kutathmini wazalizaji wa kibinafsi wa umeme na PPA.

Kulingana na wizara huyo, kumalizwa kwa kandarasi hizo kutashusha bei ya umeme nchini.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Kenya Power, kuna wazalishaji 12 wa kibinafsi wa umeme kote nchini, mmoja wa hali dharura na watatu wa kuagiza stima nje ya nchi kwa uwezo wa 3,029 MW kufikia Juni 2017, zaidi ya kiwango cha kampuni ya kuzalisha umeme nchini (KenGen) ambayo ilizalisha 1,610 MW katika kipindi hicho.

Kampuni hizo ni Iberafrica Power, Tsavo Power, Thika Power, BioJuole Kenya Limited, Mumias-Cogeneration na OrPower 4.

Zingine ni Rabai Power, Imenti Tea Factory Hydro, Gikira Hydro, Triumph Power, Gulf Power, and Regen-Terem Hydro.

Kulingana na jopo hilo, mikataba mingi ya PPA hufadhiliwa na mashirika ya kimataifa ambayo hutumia dola, hali ambayo hufanya gharama ya umeme kwenda juu.

Bw Keter alisema mapendekezo ya jopo hilo yatatekelezwa baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri.