Habari Mseto

NMG yataka wanahabari wake waachiliwe na polisi

August 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) pamoja na shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa zimewataka polisi katika Kaunti ya Mombasa kuwaachilia huru wanahabari wawili waliokamatwa Alhamisi.

Wapigapicha hao wa NTV na Taifa Leo mtawalia Karim Rajan na Laban Wallonga walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi wa kituo cha Bamburi, baada ya kupiga picha za ujenzi wa hoteli ambayo inadaiwa kuwa katika shamba la bahari hindi.

Mhariri Mkuu wa NMG Bw Tom Mshindi (pichani) alikashifu hatua ya kuwakamata wanahabari hao, akisema ni mambo yaliyopitwa na wakati

“Ni makosa kwa polisi kuwakamata wanahabari ambao wanafanya kazi yao, kwa kuwa wanafuata amri kutoka watu wenye usemi,” Bw Mshindi akasema.

Walipokamatwa, wawili hao walikuwa kazini eneo la Shanzu, japo mwandishi wa Taifa Leo Winnie Atieno alifanikiwa kukwepa.

Hoteli hiyo inasemekana kumilikiwa na afisa mkuu katika serikali. Katika video iliyochapishwa na tovuti ya Nation.co.ke na ambayo ilirekodiwa na Bi Atieno, wafanyakazi wa hoteli hiyo wanaonekana wakiwanyanyasa wapiga picha hao.

Hata hivyo, kamanda wa polisi jijini Mombasa Johnstone Ipara alijiepusha na suala hilo akisema “sitaki kujihusisha.”

Vilevile, mkurugenzi mkuu wa Haki Africa Hussein Khalid, alikashifu hatua hiyo ya polisi, akiitaja kuwa ya kushtua, na kusisitiza kuwa hakuna ufuo wa mtu binafsi nchini.