• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Wakenya na Wachina taabani kwa kusajili laini 30,000 za Airtel kulaghai watu

Wakenya na Wachina taabani kwa kusajili laini 30,000 za Airtel kulaghai watu

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wawili wa Uchina na Wakenya sita akiwamo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walishtakiwa kwa kushiriki katika uhalifu wa kimitandao Alhamisi.

Washtakiwa walikanusha kuandikisha laini 30,000 za simu za Kampuni ya Airtel wakitumia nambari za vitambulisho vya Wakenya bila kuwajulisha.

Walioshtakiwa ni  Zhou Danni, Xiao Bi , Maureen Wambui Chege,Wilfed Kimutai Ruttop,Joash Manyura Nyamanya , mwanafunzi wa chuo kikuu Alphonse Kibet Langat na Patrick Mwangi Wanjohi.

Washtakiwa walifikishwa mbele ya hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani ambaye aliombwa awaachilie kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi hilo ila aliisihi mahakama iamuru Mabw Danni na Bi wawe wakipiga ripoti kwa afisi ya Mkurugenzi wa idara ya upelelezi DCI mara moja kwa wiki hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Pia korti iliombwa iamuru wawasilishe pasipoti zao kortini.

Mawakili waliowatetea washtakiwa waliomba korti iamuru afisa anayechunguza kesi hiyo awarudishie washtakiwa simu zao za kiunga mbali , gari, vipakatalishi na hati nyingine zilizotwaliwa waliposhikwa.

Mahakama ilielezwa kuwa vifaa hivyo pamoja na gari itatumika kama ushahidi.

Lakini Bi Onkwani alimwamuru afisa anayechunguza kesi afike kortini Agosti 20 , 2018 kueleza msimamo wake kuhusu vifaa hivyo vilivyotwaliwa kutoka kwa washtakiwa.

Washtakiwa hao walizuiliwa katika gereza la kamiti hadi Agosti 20 mahakama itakapoamua kuhusu ombi lao la dhamana.

Shtaka la kwanza dhidi ya washtakiwa wote lilisema kuwa mnamo Januari 10 na Julai 16 washtakiwa walishirikiana kutekeleza uhalifu wa kimitandao kwa kuandikisha nambari za simu 30,000 za kampuni ya Airtel  wakitumia nambari za vitambulisho vya wakenya bila idhini yao.

Shtaka la pili lilisema kuwa waliandikisha nambari ya simu  ya Bw Mutuku Mutisya wakitumia nambari ya kitambulisho kwa njia ya undanganyifu.

Pia walishtakiwa kutumia nambari ya kitambulisho cha Serah John kuandikisha nambari ya simu ya Airtel.

Mahakama ilijulishwa kuwa waliandikisha nambari nyingine ya simu wakitumia kitambulisho cha Jackquiline Magdaline.

Pia waliandikisha nambari nyingine wakitumia vitambulisho vya Eric Onyango na Daniel Wairimu.

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walitiwa nguvuni Julai 26 mwaka huu na wamekuwa korokoroni kwa muda wa mwezi mmoja.

You can share this post!

Waititu awanasua mkewe, mwekezaji na vibarua mahakamani

Atwoli aanikwa na mkewe jinsi ameshindwa na majukumu ya...

adminleo