Habari Mseto

Wavuvi watatu wahofiwa kuzama baharini

August 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

WAVUVI watatu hawajulikani waliko ilhali mwingine mmoja akiokolewa baada ya boti waliyokuwa wakivulia samaki kuzama baharini katika eneo la Kiwayu, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Wavuvi hao walikuwa wametoka kijiji cha Kizingitini kuelekea kisiwa cha Kiwayu na Ndau ili kutekeleza uvuvi kabla ya boti yao kusombwa na mawimbi makali na kuzama kwenye bahari ya kina kirefu eneo hilo la Kiwayu.

Mmoja wa wavuvi hao Omar Shali Sharif alifaulu kuogelea hadi nchi kavu eneo la Kiwayu ambapo alimpasha habari chifu wa eneo hilo kuhusiana na yaliyokuwa yametokea baharini.

Wale ambao hadi sasa hawajulikani waliko ni Athman Ali Gogo, Lali Shali na Huri Kale Shebwana.

Akithibitisha ajali hiyo Ijumaa, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri alisema msako mkali unaonuiwa kuwatafuta na kuwaokoa au hata kupata miili ya watatu hao tayari unaendelea eneo hilo la tukio.

Bw Kanyiri alisema juhudi za maafisa wa polisi wanaoshughulikia masuala ya baharini wakishirikiana na wapiga mbizi wa kujitolea zinaendelea na zimekuwa zikitatizwa na upepo mkali unaovuma baharini eneo hilo la Kiwayu.

“Ni kweli. Kuna boti imezama eneo la Kiwayu. Mvuvi mmoja ameweza kuokolewa ilhali wengine watatu bado hawajulikani walipo. Msako umekuwa ukitatizwa na mawimbi makali na upepo unaoshuhudiwa kwa sasa baharini hasa eneo hilo la Kiwayu,” akasema Bw Kanyiri.

Mizigo na wasafiri wakiwa wamejazana kwenye boti kutoka kisiwa cha Lamu kuelekea Kizingitini. Wavuvi watatu hawajulikani waliko baada ya mashua yao kuzama baharini eneo la Kiwayu, Kaunti ya Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Aliwataka wavuvi na mabaharia wengine kuwa waangalifu na kuepuka kuendeleza shughuli zao kwenye bahari ya kina kirefu hasa msimu huu ambapo Lamu na Pwani kwa jumla imekuwa ikishuhudia upepo na mawimbi makali baharini.

Pia aliwashauri wavuvi kuhakikisha wanajiandikisha kwenye vikundi vyao vya uvuvi (BMU) hasa kila mara wanapoondoka kwenda baharini.

Tukio hilo pia limethibitishwa na Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, David Lusava aliyesema juhudi zinaendelezwa ili kuwapata waliotoweka baharini.

Ajali za boti zinazosababisha watu kupotea baharini na hata maafa si ngeni kaunti ya Lamu.

Mnamo Juni 1 mwaka huu, wavuvi wawili walifariki ilhali wengine watatu wakiokolewa pale mashua waliyokuwa wakitumia kuvulia iliposombwa na mawimbi makali na kuzama baharini eneo la Manda-Maweni, Kuanti ya Lamu.

Mnamo Agosti 13 mwaka jana, watu 12 wakiwemo watoto, bibi na shangazi wa mwanasiasa wa ODM, Bw Shekuwe Kahale, walifariki pale boti walimokuwa wakisafiria kutoka Kizingitini kuelekea kisiwa cha Lamu kuzidiwa na mawimbi makali na kuzama baharini katika eneo la Manda Bruno.

Juni 20 mwaka jana, watu 10 walifariki papo hapo pale mashua walimokuwa wakisafiria kutoka kisiwa cha Lamu kuelekea Ndau ilipozama baharini katika eneo la kivuko cha Mkanda.