Akanusha mashtaka ya kuiba mamilioni

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Ijumaa kwa kuibia benki iliyotiwa chini ya msimamizi ya Dubai (DBK) Sh159 milioni.

Bw Zein Abubakar Said alikanusha mashtaka mawili alipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Bw Said aliyewakiishwa na wakili Kirathe Wandugi alifikishwa kortini baada ya kutiwa nguvuni mjini Mombasa.

Mahakama ilielezwa kuwa kesi dhidi ya Bw Said itaunganishwa na nyingie iliyoorodheshwa kusikizwa Novemba 28, 2018.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Avedi alimweleza hakimu kuwa hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

“Sipingi mshtakiwa akipewa dhamana. Kesi hii itaunganishwa na nyingine ambapo washukiwa wanne wameshtakiwa. Kesi hiyo nyingine itasikizwa Novemba 28 na itatajwa Septemba 5, 2018,” Bi Mutuku alifahamishwa.

Wakili Wandugi hakupinga kesi hiyo ikiunganishwa na hiyo ya awali.

Mahakama ilielezwa katika kesi hiyo ya kwanza washukiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni au walipe dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000.

Bi Mutuku aliamuru Bw Said alipe dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu ndipo aachiliwe.

Aliagizwa afike kortini Septemba 5 kesi dhidi yake iunganishwe na hiyo nyingine dhidi ya washukiwa wanne.

Habari zinazohusiana na hii