Makala

BAO LA KETE: Mchezo unaoenziwa na wazee wa Lamu

August 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

BAO la kete ni mchezo ambao huchukuliwa na wengi kama njia mojawapo ya kupitisha muda hasa baada ya shughuli za siku.

Aghalabu mchezo huo pia hutumiwa kupitisha wakati hasa kwa waja ambao hawana kazi za kufanya na wazee wa umri mkubwa.

Aidha kwa wakazi wa Lamu, mchezo huo ambao umetwaa umaarufu mkubwa siku za hivi karibuni huchukuliwa tofauti kabisa.

Mbali na bao kupitisha muda kwa wale ambao hawana kazi za kufanya, mchezo huo umekuwa kivutio kwa vijana, wazee, wageni na hata watalii wanaozuru eneo hilo.

Kulingana na Bw Ali Chanzaa ambaye amekuwa akishiriki mchezo huo kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, bao la kete limeweza kukutanisha wale ambao wametengana kwa muda mrefu.

Bao limewakutanisha wakazi kutoka miji ya Faza, Kizingitini, Kiunga, Pate na sehemu zingine za Lamu ambao huja katika kisiwa cha Lamu ili kushiriki mchezo huo.

“Kupitia bao, wazee ambao wamekuwa sehemu mbalimbali za kaunti na nje ya Lamu kwa shughuli za kikazi hukutanika tena,” akasema Bw Chanzaa.

Bw Okeli Shauri anasema mchezo wa bao umepelekea kudumishwa na kuendelezwa kwa utamaduni wa Lamu.

Anasema mchezo huo huwa mojawapo ya viambata vinavyojumuishwa na kufanyiwa maonyesho maalum wakati wa hafla ya utamaduni wa Lamu inayoadhimishwa kila mwaka eneo hilo.

“Bao ni mojawapo ya michezo inayojumuishwa wakati wa maadhimisho ya tamasha za utamaduni wa Lamu. Bao lenyewe linatuwezesha kuhifadhi tamaduni zetu. Tumerithi mchezo huo kutoka kwa mababu zetu na tunauendeleza na kupokezana kizazi hadi kizazi,” akasema Bw Shauri.

Naye Bw Khalifa Adamu alisema bao la kete limesaidia kujenga urafiki na kudumisha amani na umoja miongoni mwa wakazi wa kabila zote za Lamu.

“Bao si mchezo wa kujifurahisha tu. Wakazi hapa wamedumisha upendo, uwiano na utangamano kupitia mchezo huu. Kila mnapocheza, wahusika hujihisi ni kuwa kitu kimoja, hivyo upendo kujengwa zaidi bila ya kuzingatia huyu ni wa kabila gani,” akasema Bw Adamu.

Kuna wale ambao hutumia mchezo wa bao kujipatia mapato.

Mmoja wa vijana wa Lamu, Bw Yusuf Omar, alisema wao wamekuwa wakichez bao kwa kutumia pesa.

“Tunatoa kati ya Sh 100 mpaka Sh 1000. Inategemea mtakavyokubaliana kiwango cha fedha mtakachotoa mchezoni. Anayeshinda mchezo huchukua fedha hizo. Unaweza enda na Sh 200 pekee na baada ya mchezo ukawa umekusanya zaidi ya Sh 1000. Mchezo wa bao nauchukulia kama kazi yangu,” akasema Bw Omar.

Waziri wa utalii na Biashara wa Kaunti ya Lamu, Bw Dismas Mwasambu anasema kumekuwa na watalii ambao hutoka  sehemu mbalimbali za nchi na ulimwengu kote ambao huzuru Lamu kujionea jinsi bao la kete linavyochezwa.

“Tunafurahia mchezo wa kete. Umekuwa kivutio kwa watalii hapa Lamu. Wanazuru eneo hili ili kujionea jinsi mchezo huo unavyofanyika,” akasema Bw Mwasambu.

Kadhalika mchezo huo una mafunzo ya kimsingi maishani.

Bw Yusuf Alale anaeleza kwamba kupitia mchezo wa bao, matajiri na maskini huishi kwa kujikubali wakijua fika kwamba leo au kesho huenda kila mmoja akaishi maisha tofauti na alivyo sasa.

“Bao la kete huchezwa kwa kutumia mbegu (kete) 64. Huchezwa baina ya watu wawili ambao kila mmoja huwa na kete zake 32. Wachezaji hujaribu sana ili wasipokonywe kete zao mchezoni.

Hata hivyo mshindi lazima abakie na kete nyingi kushinda mwenzake. Hii inamaanisha leo unaweza kuwa tajiri lakini kesho ukapokonywa au ukasambaratika kutoka kwa utajiri wako. Lazima ujikubali kama inavyohitajika kwa mchezaji anayeshindwa kwenye mchezo wa bao,” akasema Bw Alale.

Wachezaji wa bao aidha wanaitaka serikali ya kaunti ya Lamu kubuni kituo maalum kitakachoshughulikia maslahi ya mchezo huo ili kuuendeleza kote Lamu.