Kimataifa

#FreeBobiWine: Maandamano jijini Kampala yachacha

August 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

POLISI na wanajeshi jijini Kampala Jumatatu walikuwa na wakati mgumu kupambana na waandamanaji waliotatiza shughuli za jiji hilo, wakitaka mbunge wa upinzani Bobi Wine awachiliwe.

Wakiimba nyimbo za kuitisha uhuru wa mbunge huyo, waandamanaji hao walichoma vifaa na kufunga barabara, ikiwalazimu walinda usalama kupiga risasi hewani kuwatawanya.

Zaidi ya watu kumi walikamatwa wakati huo, katika oparesheni iliyoongozwa na naibu kamishna wa polisi Dennis Namuwooza.

Waandamanaji hao waliwalaumu polisi kuwa wamewakamata na kuwatesa wabunge Bobi Wine, Francis Zaake na wengine ambao walikamatwa Jumatatu wiki iliyopita, baada ya mzozo kuibuka baina ya wafuasi wa mbunge mteule Kassiano Wadri na wale wa mgombezi wa chama cha NRM Nusura Tiperu.

Vurugu hizo zilisababisha kifo cha dereva wa Bw Wine, Yasin Kawuma huku wengine wakibaki na majeraha ya risasi.

Zaidi ya watu 30, wakihusisha wabunge waandishi wa habari na raia walitiwa mbaroni.

Jumapili, mtu mmoja aliuawa huku wengine watano wakijeruhiwa wakati polisi walipokuwa wakikabiliana na waandamanaji eneo la Mityana, baada ya madai kuibuka kuwa hali ya afya ya mbunge wa eneo hilo Francis Zaake ilikuwa imedhoofika.

Kulingana na walioshuhudia, walioadhiriwa walikuwa baadhi ya mashabiki wa soka kutoka kaunti ya Singo ambao walikuwa wanaelekeaeneo la Kyaggwe kwa kushuhudia mchezo.

Walisema polisi walipiga risasi gari walilokuwa wakisafiria baada ya dereva wake kukataa kusimama walipomwamuru hivyo.