• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
BLOCKCHAIN: Suluhu tosha kuzima ufisadi na wizi wa kura

BLOCKCHAIN: Suluhu tosha kuzima ufisadi na wizi wa kura

NA FAUSTINE NGILA

KWA Wakenya wengi, neno ‘blockchain’ ni geni, lakini kwa wawekezaji wa sarafu za dijitali na hata Hazina Kuu, ni neno ambalo wamelizoea kwa miaka mitatu sasa.

Hii ni teknolojia ya kihisabati ambayo imekuza uwepo wa sarafu za dijitali kama Bitcoin, ambayo inaweza kutumiwa na yeyote popote alipo, kama tu intaneti.

Ni teknolojia ya kipekee ambayo badala ya kutumia mabilioni ya fedha za umma tukiwaajiri makachero na wachunguzi katika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na ofisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI), inaweza kutusaidia kunasa wezi wa mali ya umma bila gharama kubwa.

Pia badala ya machafuko kutokea kila baada ya uchaguzi mkuu nchini kutokana na wizi wa kura na ukosefu wa imani na jinsi uchaguzi huendeshwa, teknolojia hii inaweza kutuokoa.

Blockchain ni teknolojia iliyokomaa na kutambulika kimataifa kutokana na uwezo wake wa kunasa historia yote ya data, uhamishaji wa pesa, ununuzi na uuzaji huku ikitoa taarifa zote kuhusu mmiliki wa kila aina ya mali.

Hakuna cha kuficha katika teknolojia hii, kwa kuwa kila tukio limewekwa wazi kwa umma kutazama, ila hauwezi kubadilisha chochote.

Kiini kikuu cha ufisadi kulemea asasi husika kuung’oa ni kuwa wahasibu na wakali wa teknohama kwenye mashirika ya serikali na hata kampuni za kibinafsi hubadilisha baadhi ya rekodi ili kuficha ukweli wa mambo na kupelekea wizi wa pesa za walipa ushuru.

Wafisadi wanajua jinsi ya kutumia teknolojia kuficha maovu yao na hivyo wanapofunguliwa mashtaka, wao huishia kuachiliwa au kesi kufutwa kwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Ikiwa teknolojia hii itatumiwa, itakuwa ni habari zitakazowavunja moyo wadukuzi wa mitandao yenye kifauroro cha kuendesha shughuli za kifedha za serikali kuu na zile za kaunti (IFMIS), wanaojitajirisha kila uchao kwa kufuta historia ya wizi.

Ni uvumbuzi ambao utamrahisishia kazi Mhasibu Mkuu wa serikali kwani atapata kila taarifa katika hali yake ya kiasili, huku kazi ya wahasibu wengi wanaoshirikiana kugeuza rekodi ikiyeyuka.

Hii ndiyo teknolojia ambayo itasaidia kuleta uwazi katika uchaguzi wowote ule hapa nchini kwani inawafungia nje maafisa wote wa IEBC ambao watajaribu kugeuza matokeo ya baadhi ya wawaniaji.

Hii ndiyo teknolojia ambayo itasaidia kuleta uwazi katika uchaguzi wowote ule hapa nchini kwani inawafungia nje maafisa wote wa IEBC ambao watajaribu kugeuza matokeo ya baadhi ya wawaniaji.

Itawatambua wanyakuzi wa ardhi wenye hatimiliki feki, wafanyakazi hewa serikalini na walanguzi wa dawa za kulevya huku ikitoa kila taarifa kuwahusu. Huu utakuwa ushahidi usioweza kupingika katika mahakama yoyote.

Blockchain itawang’oa mabroka wote kwenye ununuzi na uuzaji na kuchangia kushuka kwa bei za bidhaa sokoni.

You can share this post!

Mitandao ya kijamii itasaidia wanyonge kupata haki lakini...

DIGIFARM: Ithibati tosha teknolojia ndiyo suluhu ya baa la...

adminleo