Wakili ataka ICC kuchunguza suala la waliofurushwa Mau
Na VITALIS KIMUTAI
WAKILI mmoja kutoka humu nchini amewasilisha ombi kwa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), kuanzisha uchunguzi dhidi ya serikali ya Kenya.
Wakili huyo ameishtaki serikali kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu kuhusiana na kufurushwa kwa waliohamia katika Msitu wa Mau.
Bw Leonard Sigey Bett alisema kufurushwa kwa zaidi ya familia 40,000 kutoka kwa jamii moja eneo hilo, uharibifu wa mali na kuchomwa kwa nyumba ni ukiukaji wa haki na anaitaka afisi ya mwendeshaji wa mashtaka(OTP) kufanya uchunguzi.
Kulingana na ombi hilo, wakili huyo alisema kufurushwa kwa walowezi hao ni kuondolewa kwa lazima kwa watu na ukiukaji wa haki za kibinadamu kinyume na kifungu cha 7(d,I na k) katika mkataba wa Roma, unaosimamia ICC.
Afisi ya Mwendeshaji Mashtaka(OTP) ilithibitisha kupokea ombi hilo kutoka kwa wakili huyo kwa niaba ya familia zilizofurushwa katika operesheni inayoendelea na inayoendeshwa na maafisa wa usalama kutoka vitengo tofauti.
Bw Mark P Dillon, mkuu wa kitengo cha mawasiliano na ushahidi OTP alithibitisha katika barua iliyotiwa sahihi Agosti 20 na iliyoandikiwa Bw Bett kwamba ombi lake lilikuwa limepokewa Hague, makao makuu ya ICC.
“Tutazingatia ombi hili, inavyofaa na kuambatana na mkataba wa Roma unaosimamia ICC,” alisema Bw Dillon katika barua hiyo.
“Inafaa kuelewa kuwa hii ni barua ya kuthibitisha kupokea ombi lako, na haimaanishi kuwa kuna uchunguzi ulioanzishwa au utaanzishwa na OTP,” aliongeza katika barua hiyo.
Bw Dillon hata hivyo alisema, “Uamuzi utakapoafikiwa, tutakujulisha kwa kukuandikia jibu na kukupa sababu za kufikia uamuzi huo.
Moja ya mambo ambayo ICC itazingatia ni ikiwa mahakama za humu nchini zimeshindwa kutatua mzozo huo, na kutekeleza haki kwa wahusika.
Suala hilo la watu waliofurushwa katika msitu huo limeibia hisia kali nchini , huku viongozi wa kisiasa pia wakirushiana cheche za maneno.
Hata hivyo, serikali imejitetea kuwa wanaotimuliwa ni wale walionyemelea msitu.