Fahamu muda sahihi unaopaswa kula matunda

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

WATU wengi hula matunda wakati wowote wanapojisikia wao bila ya kutambua kuwa inatupasa kula matunda kipindi maalumu na pia hilo tunda inabidi liwe na sifa maalumu, sio kula tunda tu mradi ni tunda.

Watu wengi hupenda kula tunda kwa muda wanaoutaka wao au wanayala kwa kujikuta tu wanayala matunda pasipo kupanga au wengi wamejenga mazoea kula matunda baada ya mlo.

Kwanza inabidi tuzitambue faida za matunda katika miili yetu. Matunda yana faida nyingi sana kwa afya ya binadamu, hivyo yatupasa kuyapa kipaumbele mkubwa katika milo yetu ya kila siku.

Matunda ni chanzo kikubwa cha vitamini mwilini, hulinda mwili kwa kuongeza kingamwili, hupunguza uzani wa mwili kwa watu wanene, hulainisha ngozi, huondoa sumu mwilini, hufanya mishipa ya damu kusafirisha damu vizuri, huongeza na kuimarisha nguvu ya mwili na kadhalika.

Kula tunda kipindi ukiwa na njaa

Ukila tunda wakati tumbo liko wazi au unahisi njaa, husagika kwa urahisi. Baada ya saa moja au zaidi unaweza kula sasa mlo wako mwingine wa kawaida.

Usile matunda baada ya mlo

Watu wengi wamezoea kula matunda baada ya mlo kamili.Inaelezwa kuwa ulaji wa matunda baada ya mlo sio sahihi kwa sababu matunda huyeyuka haraka kuliko chakula cha kawaida . Tunda linapokuwa tayari kutoka tumboni kuelekea kwenye utumbo mwembamba huzuiliwa na chakula. Baada ya muda tunda huchanganyikana na chakula na kuoza na hatimaye huzalisha asidi ambayo humfanya mtu kuumwa tumbo baada ya kula matunda, lakini pia virutubisho vyake hupotea.

Ili kuepukana na hali hiyo ya msongamano kwenye tumbo, kula matunda saa moja kabla ya mlo au angalau masaa mawili baada ya mlo. ukizingatia utaratibu huo utakuwa umetoa nafasi ya chakula kusagika na bila kuzuia uyeyukaji wa matunda

Zingatia kiwango cha sukari kwa baadhi ya matunda

Baadhi ya matunda kama vile papai na ndizi mbivu yana kiasi kingi cha sukari. Ingawa karibu kila tunda huwa na sukari lakini baadhi yana kiasi kingi zaidi. Hivyo inashauriwa kula matunda kwa kiwango cha wastani kila siku .Aidha unapokula tunda hakikisha unakula kwa ukamilifu wake ili kupata virutubisho vyake. Kwa mfano unapokula chungwa hakikisha unakula pamoja na nyama zake ili kupata virutubisho vyote muhimu vilivyomo. Pia ulapo tango jitahidi baada ya kuliosha ule pamoja na maganda yake.

Jiwekee tabia ya kula matunda ya aina mbalimbali kwa nyakati tofauti ili kupata Vitamini na Madini tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya mwili. Hii ni kwa kuwa matunda ndiyo yanayojenga na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya maradhi na kamwe hutasumbuliwa na magonjwa mara kwa mara.

Raila Odinga, Rais Kenyatta watoa mamilioni kusaidia matibabu ya Benjamin Ayimba

Na GEOFFREY ANENE

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga hajaachwa nyuma katika kuchangishia kocha wa zamani wa timu ya Kenya Shujaa Benjamin Otieno Ayimba ambaye ni mgonjwa.

Siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwa wa kwanza kujitokeza na mchango wa Sh1 milioni, Bwana Odinga ametoa kiasi sawa na hicho.

Michango hiyo miwili ilitangazwa na Seneta wa Kaunti ya Nairobi Johnson Arthur Sakaja kupitia mtandao wake wa Twitter mnamo Aprili 10 na Aprili 11.

Mnamo Aprili 9, familia ya Ayimba pamoja na Shirikisho la Raga Kenya (KRU) lilitangaza kuwa nahodha huyo wa zamani wa timu za taifa za raga ya wachezaji saba kila upande na ile ya wachezaji 15 kila upande anahitaji Sh2 milioni kufanikisha matibabu yake.

Iliitisha msaada kutoka kwa wahisani kupitia nambari ya Paybill ya 8021673 jina la akaunti likiwa ni Benjamin Otieno Medical.

“Benja amekuwa akifika hospitali mara kwa mara kupokea matibabu tangu mwisho wa mwaka 2020 baada ya kuchunguzwa kiafya na kupatikana anaugua malaria ya ubongo. Afya yake imezorota kwa haraka na anahitaji usaidizi wetu sana. Tunaomba wahisani kusaidia kutoa mchango wowote wa kifedha kufanikisha matibabu bora kuhakikisha anarejelea hali nzuri. Bili yake ya hospitali kwa sasa ni zaidi ya Sh2 milioni. Maombi yako na mchango wako utamfaa sana,” KRU ilisema.

Wanafunzi wa nchi za nje wapenda vyuo vikuu vya nchini Kenya

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimeorodheshwa cha tano kupendwa na wanafunzi kutoka bara la Afrika na nje ya bara hili.

Utafiti huo uliofanywa majuzi na shirika la utafiti la CPS Research International unatoa maelezo kuwa MKU inapendwa pia na wanafunzi hao kutokana na mpangilio mwafaka uliopo huko.

Shirika hilo liko nchini Kenya na limekuwa likifanya utafiti wa kutathmini jinsi vyuo tofauti vinavyoendesha mipango ya elimu.

Kwa vyuo vya kibinafsi, MKU imeorodheshwa ya tatu nchini kwa kupata wanafunzi kutoka nje ya nchi, halafu pia ilipata nafasi ya nne kwa ubora wa mpangilio wake kielimu ikizoa alama za asilimia 57.05.

MKU imekuwa mstari wa mbele kwa maswala ya kufanya utafiti na ubunifu katika maswala ya elimu.

Baadhi ya maswala muhimu yanayowapa ari wanafunzi kutoka nchi za nje kufika MKU, ni ubora wa elimu, sifa zake, ushirikiano uliopo na jinsi wanavyowakuza wanafunzi chuoni.

Jambo jingine linalovutia wanafunzi kufika kwa baadhi ya vyuo vya nchini Kenya ni elimu ya hali ya juu, kupata malazi kwa njia ifaayo, muda mwafaka wa masomo uliowekwa na masomo kukamilika wakati bora zaidi bila kuchelewa.

Pia wanafunzi wengi kufika nchini kutafuta elimu ya juu kwa sababu ya sheria za kusafiri zilizopo, hali ya usalama, utamaduni uliopo, na mazingira mema ya kuishi.

Kulingana na utafiti huo Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) kina wanafunzi wengi kutoka nchi za nje ambapo idadi yao inafika 1,300. Nafasi ya pili ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika – Kenya (USIU-Kenya) ambacho kina wanafunzi wapatao 1,100. Nafasi ya tatu inakamatwa na Chuo Kikuu cha Strathmore ambacho kinahifadhi wanafunzi 660.

Kiptanui na Tanui waibuka washindi wa Xiamen Siena Marathon

Na GEOFFREY ANENE

ERICK Kiptanui alitawazwa mfalme mpya wa mbio za kilomita 42 za Xiamen Siena Marathon zilizofanyika nchini Italia, Jumamosi.

Taji la wanawake pia lilinyakuliwa na Angela Tanui (2:20:08) aliyefuatwa na Mkenya mwenzake Purity Changwony (2:22:46) na Muethiopa Gedamu Gebiyaneshayele (2:23:23) mtawalia.

Kiptanui, ambaye atafikisha umri wa miaka 30 hapo Aprili 19, alizoa ushindi baada ya kukamilisha umbali huo kwa saa 2:05:48 Jumamosi. Rekodi ya Xiamen Marathon ya saa 2:06:19 imedumu tangu Mkenya mwenzake Moses Mosop aweke mwaka 2015 nchini Uchina.

Kiptanui ni Mkenya wa kwanza kunyakua taji la Xiamen tangu Mkenya mwenzake Vincent Kipruto mwaka 2016.

Alijiweka pazuri kuzawadiwa Sh3.2 milioni za kutwaa taji hilo. Hatapata tuzo ya kuweka rekodi mpya ya Xiamen Marathon ya Sh1.9 milioni kwa sababu moja ya sheria za mbio hizo waandalizi wanasema ni kuwa mtu mmoja haruhusiwi kutuzwa mara mbili. Unaruhusiwa kuchukua tuzo ya juu. Ikiwa angevunja rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 inayoshikiliwa na Mkenya Eliud Kipchoge angepokea bonasi pekee ya kufanya hivyo ambayo waandalizi walitangaza Januari kuwa Sh107.3 milioni.

Kiptanui alifuatwa na Muethiopa Abdi Nigassa (2:05:57), Mmoroko Othmane El Goumri (2:06:18), Yohane Ghebregeris kutoka Eritrea (2:06:28), Muethiopa Kebede Wami (2:06:32) na Mkenya Solomon Kirwa Yego (2:06:41) mtawalia.

Wakenya Lucas Rotich (2:07:23), Bethwell Rutto (2:07:41), Edwin Kimaru (2:07:51) na Bethwel Yegon (2:08:18) walinyakua nafasi ya 11 hadi 14 katika usanjari huo nao Michael Njenga (2:08:28) na Stanley Kiprotich Bett (2:08:57) wakaridhika na nambari 16 na 20, mtawalia.

Makala hayo ya 18 yalivutia wakimbiaji 12,000. Kiptanui na Tanui watapokea tuzo zao wakipatikana hawakutumia dawa za kusisimua misuli kupata mafanikio hayo.

ANC yadai ODM inamtisha Uhuru kwa kutisha kuungana na Dkt Ruto

Na CHARLES WASONGA

MIPANGO ya ODM kubuni muungano na Naibu Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ni njama ya chama hicho kumlazimisha Rais Uhuru Kenyatta kuunga mkono azma ya Raila Odinga ya kuwania urais, chama cha ANC sasa kinadai.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili, mwenyekiti wa chama hicho Kelvin Lunani alisema mazungumzo ambayo Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alikuwa nayo na Dkt Ruto katika mbuga ya Maasai Mara ni sehemu ya mpango wa kufanikisha ajenda hiyo.

“Pia hatua ya chama hicho kuonyesha undumakuwili kuhusu iwapo kingali kinaunga mkono handisheki au la ni sehemu ya njama. Hii inaonyesha kuwa ODM haikuwa na imani na mchakato wa BBI endapo haiendelezi masilahi yao finyu,” akaeleza Bw Lunani.

ODM imekuwa ikionyesha dalili za kwamba itafanya kazi na Dkt Ruto katika kila viongozi wake wanasema ni kulipiza kisasi kwa kile wanachodai ni “usaliti kutoka kwa Rais Kenyatta.”

Machi 2021 Seneta wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na mwenzake wa Rarieda Otiende Amollo walidai kuwa Katibu katika Afisi ya Rais Karanja Kibicho anapanga kutenga Bw Odinga katika mipango ya urithi wa Rais Kenyatta kwa kuhujumu mchakato wa BBI.

Kulingana na Bw Lunani, ODM inajaribu “kubuni maadui kutoka nje” kama hatua kuokoa meli yake inayozama huku ikitoa taarifa za kukanganya iwapo Bw Odinga atawania urais au la.

“Njama hii ya kuwakanganya wafuasi wao na Wakenya kwa ujumla kuhusu mgombeaji wa urais wa ODM inaonyesha kuwa hakuna demokrasia ndani ya chama hicho. Vile vile, hali hii inaonyesha kuwa umaarufu wa ODM unadidimia kwa kasi mno,” akaeleza.

Wiki jana, mkurugenzi wa uchaguzi katika ODM Junet Mohamed alisema kuna mipango ya chama hicho kuandaa Mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) ili itoa usemi wa mwisho kuhusu suala hilo ambalo limeendelea kuwakanganya wafuasi wake.

Mnamo Aprili 1, 2021, siku ya mwisho ambayo wanaotaka kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho walipaswa kuwasilisha maombi yao, Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEC) ilisema kuwa Bw Odinga, Oparanya na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ndio walikuwa wamewasilisha maombi yao.

Lakini siku moja baadaye Katibu Mkuu Edwin Sifuna alitoa kauli tofauti akisema Bw Odinga hakuwa amewasilisha maombi yake.

“Imekuwa msimamo wa Bw Odinga kwamba atazungumzia suala la uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kukamilishwa kwa mchakato wa BBI. Tangazo ambalo lilitolewa jana (Aprili 1, 2021) ilikuwa ni mzaha kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wajinga (April 1 Fool’s Day),” akasema.

Kanisa Katoliki laitaka Kenya kusitisha mpango wake wa kufunga kambi za wakimbizi

Na CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya mahakama kusimamisha, kwa muda, Kanisa Katoliki nchini limeshauri serikali ya Kenya kutofunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma zinazohifadhi zaidi ya wakimbizi 500,000.

Kwenye taarifa, Muungano wa Maaskofu wa Kanisa hilo (KCCB) umesema ni muhimu kwa serikali kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi hao kwa sababu hawatakuwa salama katika mataifa asilia. Wengi wa wakimbizi hao wanatoka mataifa ya Somalia na Sudan Kusini.

“Hawa ni watu ambao maisha yao yamevurugwa kwa namna mbalimbali, ikiwemo usimamizi mbaya wa rasilimali, ukosefu wa asasi za utawala na siasa isiyokomaa. Isitoshe, wakimbizi hawa hawatakuwa salama katika nchi zao ambazo wakati huu zinakumbwa na mapigano na aina nyingine za uhalifu,” ikasema taarifa iliyoandikwa mnamo Aprili 9, 2021, na kutiwa sahihi na mwenyekiti wa KCCB Askofu Mkuu Philip Anyolo.

Maaskofu hao wametoa wito kuwe na mazungumzo kuhusu suala hilo kati ya serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine husika “ili kupatikane mwelekeo kuhusu suala hili.”

Muungano huo vile vile, umeitaka serikali kuimarisha usalama na usaidizi kwa wakimbizi hao huku wakitaka jamii ya kimataifa iisaidie Kenya kubeba mzigo wa kuwahudumia katika kambi zao.

Wito wa maaskofu hao unajiri baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i mnamo Machi 23 kuitaka UNHCR iandaa utaratibu wa kufunga kambi hizo. Alisema uwepo wa wakimbizi hao katika kambi za Dadaab na Kakuma umechangia ungezeko la visa vya utovu wa usalama katika maeneo ya karibu “na taifa la Kenya kwa ujumla”.

“Uwepo wa wakimbizi hawa pia umechangia uharibifu wa mazingira katika maeneo karibu na kambi hizo,” akasema Dkt Matiang’i

Kwa upande wake shirika hilo la wakimbizi lilikubali kuwahamisha wakimbizi hao katika mataifa ya Amerika, Canada, Sudan Kusini na Ethiopia. Kenya imeitisha mkutano mwingine na UNHCR wiki ijayo kujadili suala hilo kwa kina.

Jumla ya wakimbizi 512,494 wako nchini. Wakimbizi 224,462 wanaishi katika kambi ya Dadaab, 206,458 katika kambi za Kakuma na Kalobeyei na 81,574 ambao wanaishi katika maeneo ya miji.

Waislamu walalamikia gharama ya juu ya maisha mwezi mtukufu wa Ramadhani ukiwadia

Na KALUME KAZUNGU

WAUMINI wa dini ya Kiislamu, Kaunti ya Lamu wamelalamikia hali ngumu ya kiuchumi, ikiwemo ongezeko la bei za vyakula wakati huu ambapo mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaanza juma hili.

Waumini hao wanasema licha ya serikali kutangaza awali kwamba imeondoa ushuru unaotozwa kwa tende, walisema hatua hiyo bado haitoshi kwani vyakula vingi, ikiwemo mchele bado vinauzwa bei ghali.

Wakiongozwa na Ustadh Said Seif, waliiomba serikali kupitia Rais Uhuru Kenyatta kuangazia suala la bei za vyakula nchini na kuhakikisha zimepunguzwa.

“Tunashukuru kwamba sassa bei ya tende ni nzuri msimu huu wa Ramadhani lakini hiyo haitoshi. Vyakula vingi muhimu vinavyotumika wakati wa Ramadhani bado viko bei ghali. Ombi letu ni kwamba serikali isikie kilio chetu na kusukuma bei za vyakula kushukishwa,” akasema Bw Seif.

Naye Bw Is’haq Khatib alisisitizia haja ya serikali na wahisani kujitokeza na kusaidia familia zisizojiweza msimu huu wa Ramadhani.

Bw Khatib alisema janga la Korona limeathiri familia nyingi, ikizingatiwa kuwa wakazi wengi wamepoteza ajira kutokana na janga hilo.

“Waliokuwa tegemeo kwa familia wamepoteza kazi na hawawezi kukimu mahitaji ya familia. Tunapoingia mwezi wa Ramadhani, ningeomba serikali na wahisani kuzingatia kuzipa familia zisizojiweza msaada wa chakula ili pia zifurahie Ramadhani,” akasema Bw Khatib.

Waumini hao wa dini ya kiislamu pia waliisukuma serikali kulegeza kamba katika utekelezaji wa sheria zinazodhibiti makali ya Covid-19 nchini kipindi chote cha Ramadhani.

Ustadh Mohamed Abdulkadir aliomba serikali kubadili majira ya kafyu kutoka saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri.

Ustadh Mohamed Abdulkadir. Picha/ Kalume Kazungu

Badala yake, Bw Abdulkadir alipendekeza saa hizo kusukumwa hadi saa tano za usiku ili kuwapa Waislamu muda wa kutosha kutekeleza sala mbalimbali msimu wa Ramadhani.

“Badala ya kafyu kuanza saa nne usiku, tunapendekeza ianze saa tano usiku hadi saa kumi alfajiri. Tunaamini wakifanya hivyo tutapata muda mwingi wa kutekeleza sala zetu,” akasema Bw Abdulkadir.

Rais aomboleza kifo cha mamake aliyekuwa Katibu wa Wizara El-Maawy

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki wa Mama Shariffa El-Maawy ambaye alifariki Jumapili nyumbani kwake Nairobi akiwa na umri wa miaka 89.

Mama Shariffa ni mamake aliyekuwa Katibu katika Wizara (PS) ya Ujenzi, marehemu Mariam El-Maawy.

Katika ujumbe wake wa faraja ambao nakala yake ilitumwa kwa vyombo vya habari, Rais Kenyatta alimtaja Mama Shariffa kama mzalendo aliyeitumikia taifa hili kwa miaka mingi na kwa kujitolea.

“Kama taifa tunamshukuru Mama Sharrifa kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi haswa katika nyanja za elimu na afya.

“Mama Sharrifa ni miongoni mwa kundi la kwanza la wakunga waliosajiliwa nchini na ametoa huduma zake kwa miaka mingi kote nchini, haswa katika kaunti za Lamu, Garissa, na Kwale ambako pia alifunza wahudumu wengi wa afya,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa taifa alisema Mama Shariffa alikumbatia elimu wakati ambapo ni wanawake wachache zaidi nchini walipata nafasi ya kunawiri kimasomo.

“Mama Sharifaa alikuwa ni kielelezo chema na mwanamke mkakamavu ambaye alifaulu kupata elimu ya kisasa wakati ambapo ni wanawake wachache waliweza kupata elimu ya kisasa,” Rais Kenyatta akaomboleza.

Kiongozi wa taifa aliomba Mungu aipe familia ya mwendazake nguvu ya kustahimili machungu ya kumpoteza.

Mariam El-Maawy alifariki mnamo Septemba 28, 2017 kutokana na majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa na wafuasi wa kundi la kigaidi la Al shabaab katika mji wa Mpeketoni, kaunti ya Lamu.

Shambulio hilo lilitokea katika eneo la Milihoi katika ya Koreni na Hindi, umbali wa kilomita 40 kutoka mji wa Mpeketoni.

Gari lake lilisimamishwa kabla ya kushambuliwa kwa gurunedi ambapo aliokolewa na maafisa wa jeshi la Kenya (KDF) na Polisi.

DINI: Dunia hii ina mitihani mingi, usitamauke, mtafute Mungu ndiye mtetezi wako

 

Na WYCLIFFE OTIENO

UMEWAHI kujipata katika hali ya mtihani mgumu?

Siku moja nilipata habari kumhusu mtu mmoja katika kijiji fulani nchini Congo. Bwana huyo alialikwa katika sherehe na alielekea kule kwa gari lake.

Akiwa njiani alifika pahali akashindwa kulidhibiti gari hilo likagonga mti uliokuwa kando ya barabara na kubingirika bondeni.

Lakini alibahatika kushika tawi la mti na akajipata amening’inia. Akamlilia Mungu sana amuokoe. Baada ya muda mrefu, akiwa hoi na amefikia mahali pa kukata tamaa, alisikia sauti ya Mungu.

Lakini alipuuza maana sauti ilimtaka afanye jambo la kipuuzi. Mara ya pili akasikia sauti ikisema, “Achilia!” Lakini akapuuza. Mara ya tatu akasikia sauti, “Kama waniamini achilia tawi hilo nikuokoe!” Alikemea sauti hiyo na akakataa kuachilia.

Huo ulikuwa mtihani mgumu sana. Lakini kuishi au kufa kwa huyu bwana kulitegemea kuiamini sauti ya Mungu na kutii. Wakati mwingi Mungu anatutarajia kufanya mambo ambayo ni magumu. Lakini huwa ameficha mafanikio yetu katika mambo hayo. Kama kweli tunamsadiki Bwana tutatii na kufanikiwa sana.

Maisha tunayoishi yamejaa mitihani migumu. Lakini Mungu ametupa uwezo wa kufanikiwa katika kila hali.

Wakati huu wa janga la corona, ni wakati mgumu. Hakika huu ni mtihani mgumu. Lakini Mungu ametupa uwezo wa kushinda. Mtihani huu pia utapita. Mungu hujitwalia utukufu katika mafanikio yetu. Tunachohitaji ni kumwamini na kumtumainia hata mtihani uwe mgumu kiasi gani.

Katika Mwanzo 22, Ibrahimu alijipata katika mtihani mgumu sana. Baada ya kupitia miaka mingi ya maudhi kwa kukosa mototo, Mungu akamkumbuka na kumbariki na Isaka. Alipokuwa anafikiria ni wakati wa kusherehekea, “Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

Lakini Ibrahimu akamtii Mungu na kuondoka ili aende kumtoa mwanawe kama sadaka ya kuteketeza. Ibrahimu alimsadiki Mungu. Ibrahimu alimtumainia Mungu. Ibrahimu alimwamini Mungu. Huu ulikuwa mtihani mgumu. Lakini hakuwa na shaka na Mungu. Alikumbuka alipokuwa miaka 75 Mungu alimtoa kwao na akaahidi kumbariki. Alipotimiza miaka 100 Mungu tayari alikuwa amedhihirisha uaminifu wake. Alijua kuwa aliyembariki mara ya kwanza, anaweza kumbariki mara ya pili

Ibrahimu alikuwa mtu wa imani. Ibrahimu alikuwa rafiki wa Mungu. Ukiwa na imani utakuwa rafiki wa Mungu. Mazingira yako yanaweza kuwa magumu, lakini imani yako inaweza kubadilisha matokeo.

Mchungaji John Maxwell alisema, “unaweza kukosa uwezo wa kubadilisha mazingira yako, lakini una uwezo wa kubadilisha mtazamo wako”.

Ibrahimu aliondoka akiwa na mtazamo chanya, licha ya mtihani mgumu. Mwanzo 22:4-5, “Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.”

Angalia Mtazamo wa Ibrahimu aliwaambia wajakazi wanaenda kuabudu halafu watarudi. Lakini kulingana na agizo la Mungu, Isaka hangerudi maana alienda kuteketezwa. Hata alipoulizwa na Isaka kuhusu sadaka, angalia alivyojibu. Mwanzo 22:6-8 “Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja.

Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.

Moyoni mwa Ibrahimu, alijua vyema kuwa anaenda kumtoa mwanawe kama sadaka ya kuteketeza. Lakini alimtumainia Mungu na alikuwa tayari kumtii katika kila hali. Hatimaye Mungu alijidhihirisha kwa kujitolea kondoo. Akapaita mahali pale Yehova-yire.

Usiogope unapojipata katika mtihani mgumu. Mungu atajitolea. Mungu atakutetea. Utafanikiwa katika mtihani huo. Hakuna jambo gumu kwa Mungu. Mtumainie, msadiki, mtegemee katika kila hali.

Vyote ulimwenguni na mbinguni ni mali yake. Palipohitajika damu ya mwanakondoo asiye na mawaa ili ulimwengu usamehewe, Mungu alimtoa mwanawe wa pekee Yesu Kristo. Tukimwamini tunapata uzima wa milele. Bwana atajitolea!

MALENGA WA WIKI: Walibora aendelea kukumbukwa kwa mchango wake muhimu kukuza Kiswahili

Na HASSAN MUCHAI

JUMAMOSI, ilikuwa siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha mwandishi nguli Ken Waliaula maarufu kama Ken Walibora kutokea.

Ripoti za awali kutoka kwa maafisa wa usalama zilionyesha kuwa Ken alifariki kutokana na ajali ya barabarani eneo la Landhies jijini Nairobi.

Maiti ya Ken ilitambuliwa siku tano baadaye katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali Kuu ya Kenyatta. Kabla ya maiti kupatikana, Ken alikuwa ametangazwa kupotea.

Kifo chake kiliwapata Wakenya na ulimwengu kwa jumla kwa simanzi kuu na hali ya kutoamini. Viongozi mashuhuri nchini akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake na viongozi wengine wa ngazi za juu walituma risala zao wakielezea kusikitishwa sana na mauti hayo.

Kabla ya kufariki, Ken alikua amejizolea sifa kedekede kutokana na kazi zake za uandishi wa vitabu, uanahabari na spoti. Alikuwa msomi wa kujitegemea aliyeipigania nafsi yake kuendeleza masomo yake hadi mataifa ya kigeni ili kukivumisha Kiswahili.

Sherehe za Jumamosi zilitarajiwa kuwa za kipekee na sawia na siku ya mazishi yake, taifa halikuweza kuadhimisha kumbukumbu za kifo chake kwa njia za watu kukutana na kufanya sherehe kutokana na hofu ya msambao wa virusi vya corona ambavyo vimeendelea kuhangaisha mataifa mengi ulimwenguni.

Badala yake, wakereketwa wa lugha ya Kiswahili na wapenzi wake Ken waliandaa makongamano ya mitandaoni. Wengine hata waliungana kupitia makundi ya WhatsApp kutunga mashairi ya kuliwaza na kumsifu Ken kutokana na kazi nzuri aliyoiacha duniani kabla ya mauti yake kutokea.

Mmoja wa waandalizi wa makongamano haya ni Bi Phibian Muthama ambaye kupitia kikundi chake cha The Writers Guild alikuwa ameandaa kikao maalum kuanzia saa kumi jioni hadi saa moja usiku au kuelekea saa mbili. Kikao chake kilichowashirikisha wasomi wa juu katika nyanja ya lugha ya Kiswahili kiliwahusisha Dkt Mosol Kandagor, Bi Aida Mutenyo, Prof F.E.M.K Senkoro na Abdilatif Abdallah.

Waratibu wake walikuwa Bi Muthama, Prof Leonard Muaka na Bi Kawthar Iss-hack. Kipindi kiliwapa fursa wapenzi wa lugha ya Kiswahili kutunga, kughani au kukariri mashairi yao moja kwa moja kwa njia wanayoifahamu na kuienzi wao wenyewe.

Lau si janga la corona, kijiji cha Bonde kilichoko eneo la Makutano ya Ngozi , Cherangany katika Kaunti ya Trans Nzoia, kingefurika mashabiki wa Ken kutoka pembe zote za Afrika Mashariki.

Kabla ya Rais Kenyatta kutoa masharti mapya ya kufungwa kwa kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru, mipango ya kufika Cherangany ilikuwa ikiendelea. Aidha kusitishwa kwa shughuli zozote zinazohusiana na watu wengi kukutana pamoja kwa shughuli za ibada, mazishi , sherehe au mikutano ya aina yoyote ikiwemo siasa, kuliharibu kabisa mipango ya wapenzi wa Ken.

Kwa mujibu wa Kaka yake, Bw Patrick Lumumba, familia ilitaka sana kuwaalika wageni nyumbani lakini ikalazimika kukatiza sherehe yoyote ambayo ingeenda kinyume na agizo la Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Lumumba alisema wako tayari kuwakaribisha wageni pindi serikali itakapolegeza masharti yake na wakati ugonjwa huu utakuwa umethibitiwa jinsi ipasavyo.

“Mahali alipozikwa Ken pamekuwa kama makavazi, ni kama mnara. Wageni wamekuwa wakija hapa kuona alikozikwa Ken, wengine kupigwa picha kufanya utafiti wao. Wengine ni wanahabari wanaotaka kuandika habari zao. Natumai tutakuwa na shughuli chungu nzima siku za usoni kwani tumekuwa tukipokea maombi mengi kutoka kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili kuzuru hapa,”’ Bw Lumumba alieleza.

Kwa sasa, Ken hayuko nasi lakini mbegu aliyoipanda imechipuka na kuzaa mavuno. Kaunti ya Trans Nzoia na Bungoma alikotoka Ken zimekuwa chimbuko la waandishi mashuhuri wa habari na fani nyinginezo za usanii.

Mungu azidi kuilaza roho yake mahali pema penye waja wema. Amen.

Raila awindwa na Uhuru, Ruto

JUSTUS WANGA na WANDERI KAMAU

UKURUBA wa kisiasa unaoendelea kudhihirika kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, umeibua wasiwasi miongoni mwa washirika wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hali hiyo imewachochea kuandaa msururu wa mikutano, baadhi yao iliyohudhuriwa na Rais Kenyatta.

Jumamosi, Rais Kenyatta alitarajiwa kukutana na Bw Odinga kufuatia mkutano uliofanyika Jumatano kati ya Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega na Dkt Ruto katika eneo la Maasai Mara, Kaunti ya Narok.

Mkutano huo ulipangwa “kujadili kuhusu hali ya handisheki kutokana na mwelekeo mpya wa kisiasa nchini.”

“Nilisikia kuhusu mkutano huo ingawa sijui kama ulifanyika,” akasema Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe, kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Mbunge ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga alisema mkutano huo ulipangiwa kufanyika ama jana Jumamosi au leo Jumapili.

“Huenda wasitoe picha kwa umma kama mlivyoona wengine wakifanya. Ni kweli kuna mkutano uliopangiwa kufanyika wikendi hii,” akasema, akiongeza kuna haja kuzihakikishia kambi za kisiasa za viongozi hao wawili kwamba kila kitu ki shwari.

Wandani wa karibu wa Rais Kenyatta wanasema kwa kubuni ushirikiano na Dkt Ruto, Bw Odinga atakuwa amempotezea Rais miaka mitatu, hasa kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), hatua ambayo pia ilimfanya kukosana kisiasa na Dkt Ruto.

“Bw Oparanya anatuambia ulikuwa tu mkutano wa kawaida. Kwingineko anasema Bw Odinga alifahamu kuhusu uwepo wake. Tutangoja kusikia moja kwa moja kutoka kwa Bw Odinga,” akasema Bw Murathe, ambaye ni mshirika wa Rais Kanyatta.

Ilibainika mwelekeo huo umezua wasiwasi katika kambi ya kisiasa ya Rais Kenyatta, washauri wake wakihofu kwamba itawalazimu kuanza mikakati mipya kisiasa ikiwa watawapoteza Bw Odinga na Dkt Ruto kwa wakati mmoja.

Kufuatia hayo, wadadisi wa siasa wanasema nia ya Bw Odinga ni kudhihirisha kuwa bado ni mwanasiasa mwenye maono, na hawezi kukosa kufanya maamuzi mbadala ikiwa atasalitiwa.

Tangu 2018, Bw Odinga amekuwa kwenye ushirikiano wa kisiasa na Rais Kenyatta, maarufu kama handisheki.

Hata hivyo, ushirikiano huo umeonyesha dalili za kuyumba, baada ya ripoti kuibuka kwamba Rais Kenyatta anaupendelea muungano wa kisiasa wa One Kenya Alliance.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na mwenzake Gideon Moi (Baringo).

“Lengo la Bw Odinga ni kuonyesha kuwa bado ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kisiasa nchini. Analenga kuwaonyesha washindani wake kuwa ana njia mbadala za kujijenga ikiwa wataendesha njama zozote kujaribu kumzima kisiasa,” akasema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Vile vile, wadadisi wanasema kuwa lengo lingine ni kuwadhihirishia Wakenya, Rais Kenyattta na washindani wake kisiasa kwamba, hata yeye anaweza kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuutikisa ulingo wa kisiasa nchini.

“Baada ya Rais Kenyatta kudaiwa kuunga mkono muungano wa One Kenya Alliance, ilimdhihirikia Bw Odinga na ODM kuwa si lazima rais amuunge mkono moja kwa moja kuwania urais 2022. Hivyo, imembidi Bw Odinga kudhihirisha pia yeye ni mwanasiasa anayeweza kuvuruga na kusambaratisha njama za kisiasa anazopanga Rais Kenyatta na waandani wake,” akasema mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo.

Wadadisi wanasema huenda isiwe vigumu kwa wawili hao kushirikiana, kwani wote watafaidika kwa kufanikiwa kuvuruga mikakati ya kisiasa ya Rais Kenyatta na muungano wa One Kenya Alliance.

Mnamo 2007, wawili hao walihudumu katika baraza la ‘Pentagon’ wakati Bw Odinga aliwania urais kwa tiketi ya ODM.

Hata hivyo, walikuwa kwenye kambi tofauti kisiasa kwenye kura ya maamuzi 2010 kuhusu Katiba ya sasa.

ICC yadai Gicheru alihonga mashahidi wajiondoe kwa kesi

Na WALTER MENYA

KESI inayomkabili wakili Paul Gicheru katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), imezingirwa na madai ya mashahidi kushawishiwa kuondoa ushahidi wao baada ya kupokea hongo.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Fatou Bensouda, unadai kwamba Bw Gicheru alitumia afisi yake katika jumba la Veecam, mjini Eldoret kukutana na mashahidi kisha kuwalipa ili wakatae kutoa ushahidi na pia kuondoa ule walikuwa wameuwasilisha kortini.

Stakabadhi kutoka ICC zilionyesha kwamba mashahidi hao walilipwa pesa taslimu ili kufuta ushahidi huo na wengi wao waliweka pesa zao kwenye benki. Baadhi walilipwa ili kuwashawishi wenzao waondoe ushahidi waliokuwa wamewasilisha ICC.

Kwa mujibu wa stakabadhi iliyochapishwa mnamo Ijumaa kutoka kortini, upande wa mashtaka ulieleza kwamba Bw Gicheru alikutana na mashahidi katika miji ya Eldoret, Nakuru, Nairobi na mingine kuwashawishi waondoe ushahidi wao.

Kwenye hati ya kukamatwa kwa mwanaharakati Walter Barasa ambaye alikuwa akidaiwa alihitilafiana na mashahidi, upande wa mashtaka unadai kwamba alisafiri hadi nchi jirani kuwahonga mashahidi ambao walikuwa wamepewa ulinzi.

“Gicheru alihusika pakubwa katika kuvuruga ushahidi na pia kuwashawishi mashahidi ambao walikuwa wakipewa ulinzi kwa kuwahonga. Hii ndiyo maana mashahidi wengi walijiondoa baada ya kupewa pesa hizo baadhi hata wakitishiwa maisha iwapo wangeghairi nia,” akasema Bi Bensouda katika kesi dhidi ya Bw Gicheru.

Mawakili wa Bw Gicheru tayari walisema kortini kwamba hawatawasilisha orodha ya ushahidi kwa kuwa Bi Bensouda ana kibarua kigumu cha kuthibitisha madai yote.

“Hatutawasilisha ushahidi wowote ila tunatarajia upande wa mashtaka uwasilishe ushahidi wake kisha wauthibitishe. Sheria za ICC zinakubali hili na tunasubiri pia kutetea mteja wetu,” akasema wakili wa Bw Gicheru, Bw Michael G Kamavaz wakati wa kikao kortini Aprili 8.

Hata hivyo, upande wa mashtaka unataka upande wa utetezi uwasilishe orodha ya ushahidi wake badala ya kutegemea wao.

“Ingawa kutoa ushahidi si lazima kwa mujibu wa sheria, kuwasilisha orodha ya ushahidi ni lazima,” akasema Bi Bensouda.

Wakati huo huo, mashahidi wanane ambao walikiri kuhongwa na Bw Gicheru walifichua mahakamani kuwa walilipwa mamilioni ya fedha ili waondoe ushahidi wao. Hata hivyo, walirejea kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo ili kutafuta ulinzi baada ya kutishiwa maisha.

Upande wa mashtaka pia ulifichua kwamba ingawa mashahidi hao waliahidiwa mamilioni ya fedha, baadhi yao hawakulipwa pesa hizo zote na walipolalamika walitishiwa maisha.

Kwa mfano shahidi aliyesajiliwa kama P-0397 aliahidiwa Sh5 milioni iwapo angejiondoa kwenye kesi hiyo lakini akapokea Sh1 milioni pekee. Ingawa alikimbilia usalama wake na kupewa hifadhi na upande wa mashtaka, alitekwa nyara na akakosa kutoa ushahidi katika kesi dhidi ya Naibu Rais Dkt William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang.

Shahidi mwengine aliyesajiliwa P-800 alidai kuwa aliahidiwa Sh2 milioni lakini akapokea Sh500,000 pekee kutoka kwa Bw Gicheru ili amshawishi shahidi mwengine ajiondoe katika kesi hiyo.

Wahudumu 4,000 kupoteza kazi hoteli Pwani

Na WACHIRA MWANGI

ZAIDI ya wafanyakazi 4,000 katika sekta ya hoteli watapoteza kazi kwani hoteli za Pwani zinapanga kusitisha shughuli kwa miezi mitatu.

Sekta ya utalii inakabiliwa na changamoto na wakati mgumu kutokana na makali ya janga la Covid-19.

Msambao wa homa hiyo umechangia hoteli kadha kukosa biashara wakati wa msimu wa Pasaka na hali inatarajiwa kuendelea kuwa mbaya.

Rais Uhuru Kenyatta aliweka masharti makali ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo baada ya wimbi la tatu kuanza kushuhudiwa nchini Machi.

Kutangazwa kwa marufuku ya kuingi na kuondoka Nairobi na kaunti za Nakuru, Kajiado, Kiambu na Machakos, kumeathiri biashara ya utalii katika ukanda wa Pwani. Hii ni kwa sababu wateja wengi wa hoteli hizo hutoka kaunti hizo nne ambazo zilifungwa kwa kuandikisha idadi kubwa ya maambukizi ya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Waendeshaji Biashara za Hoteli (KAHC), tawi la Pwani Sam Ikwaye alisema sekta hiyo itaporomoka ikiwa Rais Kenyatta hatafungua nchi wiki chache zijazo.

“Tunafunga hoteli. Imekuwa kawaida yetu kufunga hoteli, kwa muda, msimu wa watalii wachache ili kutoa nafasi kwa ukarabati kufanywa. Wafanyakazi hupewa likizo ambapo wanaendelea kulipwa mishahara lakini hiyo haitafanyika wakati huu,” Bw Ikwaye akasema.

Alisema kuwa katika mwaka wa 2020 wafanyakazi walikamilisha likizo zao za kulipwa na kwamba wakati huu wamelazimisha kuwapa likizo zisizolipiwa.

Ikwaye alisema hali hiyo imesababishwa na kufungwa kwa kaunti tano ambazo huchangia idadi kubwa ya wageni katika hoteli za Pwani.

“Baadhi ya hoteli zenye vitanda 300 vimepata wageni 10 pekee, idadi ambayo haiwezi kuleta faida yoyote,” akaeleza.

Alisema hoteli zilizoathiriwa zaidi ni pamoja na zile zilikoko; Mombasa, Diani, Watamu na Malindi.

“Hoteli za Mombasa hawa hazifungwa kwa sababu ya wageni wanaotaka kufanya mikutano. Lakini wakati huu hali ni tofauti kwa sababu Nairobi ambako wengi wa wageni hao hutoka imefungwa hadi wakati usiojulikana, alivyotangaza Rais Kenyatta,” Bw Ikwaye akasema.

Licha ya kwamba ni idadi ndogo ya Wakenya wamepewa chanjo kufikia sasa, wadau katika sekta ya utalii wanaitaka serikali kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa hoteli pia wanachanjwa.

“Ikiwa wafanyakazi katika sekta hiyo watapewa chanjo, hali hiyo itavutia wageni wengi kutoka nchini na mataifa ya ng’ambo,” Bw Ikwaye akaongeza.

Alisema katika bara Uropa, serikali zimeweka masharti ya kuzuia msambao wa corona huku zikiendeleza shughuli za utoaji chanjo lakini nchini Kenya hatua kama hiyo haijachukuliwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Utalii Nchini (KTF) Mohamed Hersi alisikitika kuwa sekta ya utalii imeporomoka.

TAHARIRI: Kudungwa chanjo hakutozuia corona

KITENGO CHA UHARIRI

WAKATI huu ambapo baadhi ya kaunti zimefungwa kama njia ya kudhibiti maambukizi ya maradhi ya corona, Wakenya wengi wanaendelea kuathiriwa na uamuzi huo.

Ingawa kaunti zilizofungwa kwa sababu ya viwango vya juu vya ugonjwa huo ni; Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru, karibu kaunti nyingine 42 zimeathiriwa.

Nairobi ndiyo inayounganisha reli ya kisasa (SGR) kutoka Mombasa. Safari za magari kati ya miji hiyo miwili zilisimamishwa.

Kufungwa huko kumesababisha kuathirika kwa sekta ya utalii. Zaidi ya wafanyakazi 4,000 katika hoteli za kitalii watapoteza kazi kufuatia uamuzi wa hoteli nyingi za Pwani kupanga kusitisha shughuli kwa miezi mitatu. Msambao wa homa hiyo umechangia hoteli kadha kukosa biashara wakati wa msimu wa Pasaka na hali inatarajiwa kuendelea kuwa mbaya.

Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Waendeshaji Biashara za Hoteli (KAHC), tawi la Pwani Sam Ikwaye alisema sekta hiyo itaporomoka ikiwa Rais Kenyatta hatafungua nchi wiki chache zijazo.

Kulingana na afisa huyo, mwaka 2020, wafanyakazi walikamilisha likizo zao za kulipwa na kwamba wakati huu wamelazimika kuwapa likizo zisizolipiwa. Baadhi ya hoteli zenye vitanda 300 zimepata wageni 10 pekee, idadi ambayo haiwezi kuleta faida yoyote. Zilizoathiriwa zaidi ziko maeneo ya Mombasa, Diani, Watamu na Malindi.

Changamoto hii na nyingine zinapoendelea, imebainika kuwa baadhi ya watu waliopata chanjo wameamua kutozingatia kanuni za kuzuia ugonjwa huo.

Kuna watu wanaowalipa polisi kitu kidogo na kufumbiwa macho wanapoingia au kutoka maeneo yaliyofungwa. Unapofika kwenye vituo vingi vya safari za mbali jijini Nairobi, utawasikia watu wakinadi safari za kwenda Mombasa au Kisumu, huku maafisa wa polisi wakipita. Ujasiri wa aina hii unaonyesha kuna jambo wanalofahamu watu hao.

Vitendo hivi ni hatari kwa afya ya wahusika na watu wengine, hata wanaojichunga.

Majuzi, Gavana Kiraitu Murungi (Meru) na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero, waliambukizwa corona hata baada ya kupata chanjo.

Wataalamu wanasema kwamba jambo hili halifai kuwashangaza watu. Kwamba huchukua muda wa wiki kadhaa kabla ya chanjo anayodungwa mtu kuanza kuupa mwili kinga inayohitajika. Kwa hivyo inawezekana mtu akachanjwa leo Jumapili na akapata corona Jumapili ijayo.

Isitoshe, wataalamu hao wanasema lengo la kupewa chanjo si kuzuia mtu kupata corona, bali kupunguza makali ya ugonjwa huo iwapo ataupata. Kwa mfano kama mtu angepata corona ya kulazimu alazwe ICU, akiupata baada ya chanjo atalazwa chumba cha wagonjwa wasiohitaji kuwekewa mitungi ya gesi.

Sakaja amshukuru Rais Kenyatta kwa kutoa Sh1 milioni kumfaa Ayimba

Na GEOFFREY ANENE

RAIS Uhuru Kenyatta amekuwa mstari wa mbele kuitikia wito wa kuchangishia kocha wa zamani wa Timu ya Shujaa, Benjamin Ayimba ambaye ni mgonjwa.

Mchango wa Rais Kenyatta wa Sh1 milioni ulitangazwa na Seneta wa Kaunti ya Nairobi Johnson Arthur Sakaja kupitia mtandao wake wa Twitter mnamo Aprili 10.

Mnamo Aprili 9, familia ya Ayimba pamoja na Shirikisho la Raga Kenya (KRU) lilitangaza kuwa nahodha huyo wa zamani wa timu za taifa za raga ya wachezaji saba kila upande na ile ya wachezaji 15 kila upande anahitaji Sh2 milioni kufanikisha matibabu yake.

Iliitisha msaada kutoka kwa wahisani kupitia nambari ya Paybill ya 8021673 jina la akaunti likiwa ni Benjamin Otieno Medical.

“Benja amekuwa akifika hospitali mara kwa mara kupokea matibabu tangu mwisho wa mwaka 2020 baada ya kuchunguzwa kiafya na kupatikana anaugua malaria ya ubongo. Afya yake imezorota kwa haraka na anahitaji usaidizi wetu sana. Tunaomba wahisani kusaidia kutoa mchango wowote wa kifedha kufanikisha matibabu bora kuhakikisha anarejelea hali nzuri. Bili yake ya hospitali kwa sasa ni zaidi ya Sh2 milioni. Maombi yako na mchango wako utamfaa sana,” KRU ilisema.

JAMVI: Kilio IEBC ikiendelea na chaguzi ndogo bila ya kampeni

Na MWANGI MUIRURI

KANUNI zilizopitishwa hivi majuzi na serikali kuzuia ueneaji wa virusi vya corona, zimeanza kutoa taswira ya jinsi hali itakavyokuwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 endapo taifa litaendelea kulemewa na janga la corona.

Ijapokuwa kumekuwepo chaguzi ndogo nyingi tangu janga hilo lilipoingia nchini Machi mwaka uliopita, kampeni za hadharani kuhusu chaguzi zilizopangiwa kufanyika Mei 18, zimekwama.

Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapania kuandaa chaguzi tatu ndogo katika mazingara mageni kabisa ambapo kampeni zimezimwa kufuatia masharti ya kupambana na janga la Covid-19.

Ingawa IEBC ilitoa mwanya wa kati ya Machi 29 hadi Mei 15 kwa wawaniaji kuvumisha kampeni zao, kwa sasa hali si hali kwa kuwa ubunifu ndio unahitajika ili kujipigia debe.

Chaguzi hizo zitaandaliwa katika maeneobunge ya Juja na Bonchari na katika wadi ya Rurii iliyoko kaunti ya Nyandarua. Uchaguzi mdogo wa Useneta Kaunti ya Garissa umefutiliwa mbali baada ya kuibuka mwaniaji mmoja tu ambaye ni Abdul Haji na ikabidi atawazwe mshindi wa kumrithi babake Yusuf Haji aliyeaga.

Tayari, baadhi ya wawaniaji wameanza kulia wakisema kwamba chaguzi hizo zinafaa ziahirishwe hadi wakati kutakuwa na mwanya wa kufanya kampeni za kukutanisha watu moja kwa moja wachumbiwe.

Hali haswa ni ngumu zaidi kwa wawaniaji 12 wa Juja—eneobunge ambalo liko katika Kaunti ya Kiambu—ambako hata baa na hoteli zimeagizwa kufungwa hivyo basi kuzima mianya yote ya kuwafikia wapigakura moja kwa moja.

Ni katika hali hiyo ambapo Bw Joseph Njoroge Mburu ametoa ilani ya hadi Jumanne wiki ijayo kwa IEBC akiitaka iahirishe chaguzi hizo hadi wakati hali ya kawaida itakaporejea.

La sivyo, amesema kuwa ataandaa kesi ya kuomba mahakama ishinikize IEBC kutangaza kuahirishwa kwa chaguzi hizo.

Bw Mburu ambaye anawania Juja kwa tiketi ya People Party of Kenya (PPK) analia kuwa “hatuwezi tukazimwa kufanya kampeni kisha tutarajiwe kushindana katika uwanja ulio na usawa na uwazi.

Baadhi ya wagombeaji wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na SMS kuvumisha ajenda zao.

Hata hivyo, kuna changamoto kwa vile tofauti na mikutano ya hadhara, wameshindwa kujua jinsi jumbe hizo zinapokewa na wapigakura.

Akahoji: “Mpigakura ambaye hata kujinunulia barakoa ya Sh5 ni shida, aliye na mahangaiko ya kufungiwa riziki kufuatia matangazo hasi ya kupambana na Covid-19 ambayo hayaambatanishwi na mikakati ya kutoa afueni kwao, aliye na mahangaiko ya gharama kubwa ya maisha…utamwambia namna gani atenge bajeti ya kugharamia intaneti ndio afuatilie kampeni za uchaguzi mdogo? Hata hiyo, raha na saa za kuketi chini azame mitandaoni eti anafuatilia kampeni atatoa wapi?”

Bw Mburu alisema kuwa sheria za uchaguzi hutoa mwanya wa kampeni za moja kwa moja kati ya wawaniaji na wapigakura “lakini kwa sasa hata mkutano wa watu wawili kwa msingi wa kisiasa umezimwa.”

Alisema kuwa kuendelea mbele na kuandaa uchaguzi huo ni sawa na kuwavizia wawaniaji hasa wale ambao hawana rasilimali za kulipia matangazo ya runinga na redio.”

Alisema kuwa chaguzi hizo zikiandaliwa kama ilivyoratibiwa, kutakuwa na mwanya mkubwa wa kutotoa taswira kamili ya umaarufu wa wawaniaji na ufaafu wao.

Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro anasema kuwa “ni wakati mgumu wa kuchapa kampeni kwa kuwa ni lazima pia uzingatie usalama wa kiafya kwa wapigakura na ukionekana kama unakaidi masharti yaliyowekwa, unagongwa na propaganda na wapinzani kuwa wewe ni sawa na muuaji ambaye analenga kuwamaliza wapigakura kwa kuwaambukiza corona.

Bw Osoro ambaye anashirikisha kampeni za United Democrativc Alliance (UDA) katika uchaguzi huo aliambia Taifa Jumapili kuwa “kwa sasa tunatumia mabango, mitandao ya kijamii na matangazo kwa vyombo vya habari ambavyo vinatangaza kwa lugha za mashinani ya kwetu kuwafikia watu.”

JAMVI: Mjane atakuwa mbunge wa kike wa kwanza Kisii?

Na WYCLIFFE NYABERI

MEI 18, wakazi wa eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii watakwenda debeni kumchagua mbunge wao mpya baada ya kifo cha Oroo Oyioka aliyeaga dunia mwezi Februari kutokana na maradhi ya kisukari.

Kwenye uchaguzi huo mdogo, wanawake watatu watajimwaya debeni kumenyana na wanaume kumi katika kinyang’anyiro ambacho wengi wametabiri kitakuwa kivumbi kikuu.

Wawaniaji hao wanawake ni Bi Teresa Bitutu ambaye ni mjane wa marehemu Oroo Oyioka, atakayepeperusha bendera ya chama kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA), mwakilishi wa kike wa zamani wa kaunti ya Kisii Bi Mary Sally Otara (United Green Movement) na Bi Margaret Nyabuto wa chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC).

Katika jamii ya Abagusii, kama ilivyo katika jamii nyingi nchini, wanawake hawapati nafasi nzuri kuchaguliwa kwenye nyadhifa za uongozi ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Hivyo basi uchaguzi wa Bonchari kwa mara nyingine utaiweka jamii hiyo kwenye mizani ikiwa itakwenda kinyume na mila na itikadi zilizopitwa na wakati na kumpa nafasi mwanamke fursa ya kuongoza au la.

Tangu taifa la Kenya lijinyakulie uhuru na viongozi kuanza kuchaguliwa kwenye nyadhifa mbali mbali za kisiasa, hakuna hata mwanamke mmoja kutoka jamii hiyo amewahi kuchaguliwa kwenye kiti kikubwa cha kisiasa. Wanawake wamekuwa wakijiliwaza tu kwenye viti walivyotengewa na katiba ya 2010.

Ikiwa wanawake watabahatika, basi viti watakavyochaguliwa ni vile vya chini vya uwakilishi Wadi. Kwa mfano, ni wanawake wawili tu waliopata nafasi ya kuchaguliwa kama madiwani katika mabunge ya sasa ya kaunti za Kisii na Nyamira. Wao ni Bi Rosa Kemunto wa Majoge Bassi na Bi Callen Atuya wa Bokeira.

Japo wawaniaji hao wanawake wameonyesha imani kuwa watazivunja taasubi za kiume na hulka za wanawake kutochaguliwa na kuandikisha historia ya mmoja wao kuibuka mshindi kwa mara ya kwanza, bado kibarua ni kigumu ikizingatiwa wanawake hao watalazimika kuwakabili wawaniaji wengine waliopewa tikiti na vyama vikuu nchini kama vile Jubilee na ODM.

Jamvi lilitafuta maoni ya wachanganuzi wa siasa na wazee kutoka jamii ya Abagusii ili kutathmini ni kwa nini wanawake hupata wakati mgumu kuuza sera zao kwa wapigakura wanapotafuta kuchaguliwa.

Kulingana na katibu wa Baraza la wazee wa jamii ya Abagusii Bw Samuel Bosire, wanawake wachache jasiri wanaojitokeza kuwania viti vya kisiasa hukumbana na mazingira ya kisiasa ambayo yamejaa uhasama, kejeli na matusi kutoka kwa wapigakura ambao huwadharau wanawake na kuwaona kuwa hawafai kuwania uongozi.

Badala yake, Mzee Bosire anadokeza kuwa wapiga kura hasa wanaume huwaona kina mama kama walioharibika wanaposimama kupingana na wanaume kisiasa.

Hata hivyo, katibu huyo alisema kuwa kina mama huibuka kuwa viongozi wazuri na hivyo basi jamii inafaa kuwajaribu kwenye kazi hizo.

Alitolea mfano Rais wa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania Bi Suluhu Hassan na kusema huu ni wakati wa jamii za Kenya kuwaamini wanawake katika nyadhifa za uongozi kwani wengi wameonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza vyema.

Bi Rachael Otundo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa machache ya Afrika ambayo yameweka mikakati ya kuimarisha uongozi kwa kubuni vitengo mbali mbali vya utawala lakini bado mengi yanafaa kufanywa ili kuziba mwanya wa kijinsia unaoshuhudiwa kwenye siasa. Hivyo basi, Bi Otundo anashikilia kuwa uamuzi wa vyama vya UDA, UGM na MCC kuwapa wanawake tikiti ya kujaribu bahati zao Bonchari kumrithi marehemu Oyioka ni nzuri na inayofaa kuungwa mkono.

Bi Bitutu katika kampeni zake amekuwa akiwarai wakazi wampe nafasi akamilishe kipindi cha mumewe na anashikilia kuwa ni yeye anayeifahamu vyema kazi aliyokuwa ameanzisha mumewe.

Naye Bi otara anasema kuwa alipokuwa mwakilishi wa kike, kuna mengi aliyoyafanikisha na angependa kuendeleza miradi aliyoachia njiani ikiwemo ya kuwapa sauti watu wasiojiweza na walemavu. Bi Nyabuto naye amejinadi kuwa msomi na anayejua shida za watu waishio vijijini. Amedokeza kuwa akipewa nafasi, ataimarisha viwango vya elimu Bonchari lakini uamuzi wa mwisho ni wa mpiga kura.

Wanawake hao watakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Bw Zebedeo Opore (Jubilee), Mhandisi Pavel Oimeke (ODM), Jonah Onkendi (The New Democrats) Kelvin Mosomi (Party of Democracy Unity), Mokaya Charles (Progressive Party of Kenya), Atancha Jeremiah (Agano Party), Matagaro Paul (Mwangaza Tu), Victor Omanwa (Party of Economic Democracy), David Ogega (Kenya Social Congress) na Eric Oigo (National Reconstruction Alliance).

JAMVI: Kukwama kwa refarenda Juni kutakavyomjenga Ruto

Na BENSON MATHEKA

IWAPO kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) haitafanyika jinsi ilivyopangwa, Naibu Rais William Ruto atakuwa ameshinda pakubwa na kupata nguvu zaidi kisiasa dhidi ya viongozi wengine wanaounga mchakato huo.

Dkt Ruto hajawahi kuuchangamkia mchakato huo akisema handisheki iliyozaa BBI kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ililenga kumzuia asigombee urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na kubuni nyadhifa za uongozi kwa watu wachache badala ya kujali maslahi ya wananchi wa kawaida.

Kulingana naye, iwapo ni lazima kura hiyo ifanyike, inafaa kuwa pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022. Amekuwa akisema hakuna dharura ya kubadilisha katiba wakati ambao kuna masuala muhimu ya kushughulikia nchini likiwemo janga na corona na Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee.

Kwa sababu ya kupinga mchakato huo, Dkt Ruto alitengwa serikalini na katika chama tawala cha Jubilee na mapema Februari mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alimtaka ajiuzulu badala ya kupinga mipango ya serikali.

Bw Odinga amekuwa msitari wa mbele kumshambulia Dkt Ruto kwa kupinga BBI na kura ya maamuzi.

Mipango ya Bw Odinga, ilikuwa ni kura ya maamuzi kufanyika Juni mwaka huu. Mswada wa kura ya maamuzi uliopitishwa na mabunge zaidi ya 40 pia uliweka muda wa mwaka mmoja kutekeleza mabadiliko ya kikatiba na kiusimamizi kupitia BBI.

Wadadisi wanasema kuna kila dalili kwamba huenda kura ya maamuzi isifanyike Juni mwaka huu ilivyopangwa baada ya bunge kusitisha vikao vyake hadi Mei 4, kufuatia maambukizi ya corona.

Kufikia wakati wa kuandika makala haya, hakukuwa na dalili kwamba bunge litaitwa kwa kikao maalumu kushughulikia mswada huo.

Mnamo Alhamisi Spika wa bunge Justin Muturi alisema hakuwa amepokea mawasiliano yoyote yanayoweza kumfanya kuita kikao spesheli cha bunge kujadili mswada wa kura ya maamuzi wa BBI.

“Kamati ( ya pamoja ya bunge na seneti) hazijawasilishwa ripoti yake na bila ripoti hiyo kikao spesheli cha bunge hakiwezi kuitwa kwa kuwa hakutakuwa na cha kujadili,” akasema Muturi.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kutofanyika au kukwama kwa refarenda kutakuwa ushindi mkubwa kwa Dkt Ruto, sio kwa sababu amekuwa akipinga mchakato huo, bali kuwa amekuwa akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 wakati wanasiasa wengine wanaomezea mate urais walikuwa wakiuunga mkono.

Kutoaminiana

“Japo alionekana pekee akipinga mchakato huo huku wanasiasa wengine wakuu wakiuunga mkono, kutofanyika kwa kura ya maamuzi kutamfaa zaidi. Kumbuka amekuwa akisema kuna masuala muhimu yanayofaa kushughulikiwa badala ya kura ya maamuzi,” asema mchanganuzi wa siasa David Wafula.

Anaeleza kuwa kumetokea dalili za kutoaminiana kati ya kambi za Rais Kenyatta na Bw Odinga kunakoweza kusambaratisha mpango mzima wa kubadilisha katiba kwa manufaa ya Dkt Ruto ambaye atatumia kufeli kwa kura ya maamuzi kujipigia debe kwenye kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Wadadisi wanasema kura ya maamuzi inaweza kufanyika tu kabla ya Agosti mwaka huu au pamoja na uchaguzi mkuu ujao.

“Ikiwa itafanyika pamoja na uchaguzi mkuu ujao, Dkt Ruto pia atakuwa ameshinda kwa kuwa amekuwa akipendekeza hilo. Kwa vyovyote vile, kutofanyika kwa kura ya maamuzi, au ikifanyika pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022, iwapo hilo linawezekana,

itakuwa baraka kwa Dkt Ruto na pigo kubwa kwa waasisi, wanamikakati, wanaounga na wanaotegemea mchakato huo kuondoka katika baridi ya kisiasa,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Katana Kalume.

“Je, waasisi na watetezi wataambia nini Wakenya kura ya maamuzi ikikosa kufanyika ilhali Dkt Ruto aliipinga na wakampuuza wakimuita kila aina ya majina hadi akatengwa serikalini?” asema Katana.

“Wakisingizia janga la corona, itakuwa ni kukubaliana na Dkt Ruto ambaye amekuwa akisisitiza kwamba BBI haifai kupatiwa kipaumbele wakati wa janga hilo. Watakuwa wamemjenga huku wakiaibika,” asema.

Wadadisi pia wanasema kusambaratika kwa mchakato huo kutamfaidi Dkt Ruto huku dalili zikionyesha huenda akaungana na Bw Odinga baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kuhisi kwamba Rais Kenyatta hana nia ya kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wachanganuzi wanasema iwapo Dkt Ruto na Bw Odinga wataungana, ni naibu rais atakayenufaika pakubwa ikizingatiwa amekuwa akipigwa vita na mkubwa wake Rais Kenyatta ambaye duru zinasema anampendelea Seneta wa Baringo Gideon Moi, hasimu mkuu wa Dkt Ruto katika eneo la Rift Valley.

Bw Moi ni kiongozi wa chama cha Kanu ambacho kimeungana na Wiper cha Kalonzo Musyoka, Amani National Congress cha Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetangula kuunda muungano wa One Kenya Alliance unaosemekana kuwa na baraka za Rais Kenyatta.

Wadadisi wanazidi kuhoji kwamba wanne hao wanategemea nyadhifa zilizopendekezwa kwenye mswada wa kubadilisha katiba wa BBI.

Ni muungano huu ambao wachanganuzi wanasema umechangia uhusiano baridi kati ya waasisi wa mchakato wa kubadilisha katiba huku chama cha ODM kikihisi kwamba Bw Odinga anachezwa na hivyo kumfanya kutafuta Dkt Ruto waungane kisiasa.

JAMVI: Ni mwanzo mpya katika dunia ya Suluhu, Biden

Na WANDERI KAMAU

DUNIA inapitia mapambazuko mapya kisiasa katika ngazi ya kimataifa, kufuatia mageuzi makubwa ya kisera ambayo yameanzishwa na marais wapya Samia Suluhu wa Tanzania na Joe Biden wa Amerika.

Ni mwelekeo mpya wa kisera katika dunia ambayo ilikuwa imezoea mbwembwe, semi kali na misimamo tata ya marais John Magufuli (Tanzania) na mwenzake, Donald Trump (Amerika) hali iliyoathiri sana mahusiano ya nchi hizo na jamii ya kimataifa.

Nchini Tanzania, Rais Suluhu tayari ameanza kuondoa baadhi ya sera tata alizoendeleza Dkt Magufuli, hali inayotajwa kuanza kugeuza mwelekeo wa taifa hilo katika ulingo wa kimataifa.

Kwa muda wa wiki mbili tu, kiongozi huyo ameagiza kutathminiwa upya kwa msimamo wa Tanzania kuhusu janga la virusi vya corona, kuondolewa kwa marufuku iliyokuwa imewekewa baadhi ya vyombo vya habari na kuwaagiza maafisa wa serikali yake kutotumia nguvu wanapowatoza kodi wawekezaji kutoka nje.

Akilihutubia taifa hilo Jumanne baada ya kuwaapisha makatibu wapya wa kudumu wa wizara na wakuu wa idara mbalimbali za serikali, Bi Suluhu alisema Tanzania inahitaji kuwa na msimamo unaobainika kuhusu janga la corona.

“Hatuwezi kujitenga kama sisi ni kisiwa. Hatuwezi kukubali chochote tutakacholetewa, lakini hatuwezi kuendelea kusoma takwimu kuhusu maambukizi ya corona duniani ilhali hali yetu haijulikani,” akasema Bi Suluhu.

Tanzania ilitoa maelezo yake ya mwisho kuhusu corona Aprili 2020 na haijawahi kutoa maelezo mengine baada ya Dkt Magufuli kutangaza kwamba “imelishinda janga hilo.”

Kutokana na mwelekeo huo mpya, wadadisi wanasema kuwa huenda uongozi wa Rais Suluhu ukaashiria mwanzo mpya kwa sura ya Tanzania katika ulingo wa kimataifa, baada ya uongozi wa Rais Magufuli kuonekana kuitenga, hasa na majirani wake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama Kenya, Uganda, Burundi, Sudan Kusini na Rwanda.

“Mwelekeo ambao Rais Suluhu ameanza kuonyesha unaashiria kama mwanzo wa safari ya kuondoa makosa ambayo Dkt Magufuli alifanya. Ingawa bado ni mapema, huenda lengo lake kuu ni kurejesha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi zingine,” asema Dkt Godfrey Musila, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.

Katika kujaribu kurejesha uhuru wa vyombo vya habari, wadadisi wanasema Bi Suluhu analenga kurejesha urafiki wa Tanzania na nchi kama Amerika na Uingereza, ambazo zilikuwa zikimkosoa sana Dkt Magufuli kwa sera zake kali dhidi ya vyombo hivyo.

Chini ya utawala wa Magufuli, serikali ya Tanzania ilifunga magazeti mengi yaliyochapishwa kwa njia ya mtandao, na yaliyoandika habari ama makala ya kukosoa serikali yake.

Baadhi ya magazeti yaliyofungwa ama kupigwa faini kwa kumkosoa kiongozi huyo ni The Citizen, Mwananchi, Mawio, Mwanahalisi kati ya mengine.

Wanahabari pia walijipata pabaya, baadhi yao wakitoweka katika hali tatanishi. Miongoni mwa wanahabari hao ni Azory Gwanda, ambaye alitoweka katika hali tatanishi mnamo 2017, huku mwenzake, Erick Kabendera akikamatwa na kuzuiliwa korokoroni kwa tuhuma za kuandika habari za “kichochezi.” Katika ulingo wa kisiasa, uhusiano wa Tanzania na majirani wake uliathirika sana, kiasi kwamba marais wa nchi za EAC walikwepa kuhudhuria mazishi ya Dkt Magufuli, kando na Rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za kimataifa, uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa vigezo ambavyo nchi nyingi za Magharibi huangalia katika kuendeleza urafiki wake na mataifa ya Afrika.

“Nchi kama Uingereza na Amerika hutilia maanani sana uzingatiaji wa masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu. Hiyo ndiyo sababu ambapo Rais Suluhu ameanza kutathmini upya baadhi ya misimamo iliyoendeshwa Dkt Magufuli ili kurejesha urafiki kati ya Tanzania na mataifa hayo,” akasema Bw Muga.

Rais Suluhu pia ameagiza idara za serikali kutowahangaisha wawekezaji kutoka nchi za nje, akiwataja kama mhimili mkuu katika ukuzaji wa uchumi wa taifa hilo. Chini ya mwamko huo mpya, wadadisi wanaeleza dunia itashuhudia mwelekeo mpya katika masuala ya kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi, kwani hata Rais Biden wa Amerika ameanza kuondoa baadhi ya sera tata zilizoendeshwa Trump.

Miongoni mwa sera hizo ni kurejesha uhusiano na baadhi ya mataifa ambayo Trump alikuwa amepiga marufuku raia wake kwenda Amerika kwa kisingizio cha kuendesha ugaidi.

Hatua hiyo iliathiri sana urafiki wa Amerika na Afrika, hasa baada ya nchi kama Sudan na Somalia kujipata kwenye orodha hiyo tata.

Kijumla, wadadisi wanaeleza kuwa kuondoka kwa marais Trump na Magufuli kutaathiri sana mahusiano na sera za kimataifa za nchi hizo, kwani wawili hao waliziongoza kama kwamba “haziwezi kuyategemea mataifa yale mengine.”

“Misimamo mikali ya viongozi hao haikuathiri tu nchi zao katika ngazi ya kimataifa, bali mahusiano kati ya raia katika mataifa jirani. Kuondoka kwao ni funzo kubwa kwamba kwa taifa kustawi katika nyanja zote, linahitaji kushirikiana na nchi zingine,” asema Dkt Amukowa Anangwe, ambaye ni msomi na mchanganuzi wa masuala ya kimataifa.

Kulingana naye, kuna uwezekano mkubwa mikakati ya kufufua upya EAC kuanza kushika kasi, kwani Rais Suluhu ameonyesha nia ya kuziba pengo lililokuwepo kwenye mahusiano ya taifa lake na wanachama wa EAC.

JAMVI: Kizungumkuti cha kuteua ‘Rais’ One Kenya Alliance

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa One Kenya Alliance (OKA) unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuteua mgombeaji wake wa urais huku ukiendelea kujinadi kote nchini.

Hii ni kwa sababu vigogo wote wanne wanaunda muungano wao wanapania kurithi kiti cha urais, Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Agosti 2022.

Wao ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi.

Muungano huu ulipata nguvu mwezi jana baada ya wagombeaji wake kuvuna ushindi katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Matungu (Kakamega), Kabuchai (Bungoma) zilizofanyika Machi 4, na uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos uliofanyika mnamo Machi 18.

Vigogo hao walidai kuwa ushindi wa Bw Oscar Nabulindo wa ANC (Matungu), Bw Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya (Kabuchai) na Agnes Kavindu Muthama, wa Wiper katika kaunti ya Machakos, ni ishara ya wao kufaulu kutwaa uongozi wa nchi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Tunajivunia ushindi wetu katika chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na Machakos. Hii ni dalili kwamba muungano wa One Kenya Alliance utashinda katika uchaguzi mkuu ujao kwani lengo letu ni kuleta mwanzo mpya na kuondoa uvundo katika siasa za nchi,” akasema Bw Musyoka kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini wiki jana.

Lakini alipoulizwa nani kati yao wanne atapeperusha bendera ya urais katika muungano huo, kiongozi huyo wa Wiper alidinda kutoa jibu la moja kwa moja.

Akasema hivi: “Ni mapema zaidi kujibu swali hilo wakati huu kwani kibarua kilichoko mbele yetu sasa ni kuuza sera za One Kenya Alliance katika pembe zote nchini. Hata hivyo, nina uhakika kila mmoja wetu yuko tayari kuweka kando masilahi yake kwa ajili ya kufanikisha azma ya kuhakikisha kwamba tunatwaa mamlaka mwaka 2022.”

Naye Bw Mudavadi ambaye mwaka jana alisema kuwa jina lake sharti liwe kwenye karatasi za uchaguzi wa urais, anasema itakuwa rahisi kwa wao kuelewana kuhusu nani kati yao atawania urais kwani “maoni, sera na itikadi yetu ni moja.”

“Ikiwa tulielewana na tukaungana nyuma ya mgombeaji mmoja katika chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na Machakos, mbona tushindwe kuelewana kuhusu kiti cha urais 2022,?” akauliza kiongozi huyo wa ANC.

Lakini wandani wa vigogo hao wanne tuliozungumza nao kwa ajili ya kuandaa makala hii walitoa mseto wa hisia kuhusu suala hilo la ni nani anafaa kupeperusha bendera ya muungano wa OKA katika uchaguzi mkuu ujao.

Japo anakiri kwamba muungano huo unakabiliwa na kibarua kigumu katika mpango mzima wa uteuzi wa mgombeaji urais, mbunge wa Tiaty William Kamketi (Kanu) anasema kuwa seneta Moi ndiye anafaa kupewa nafasi hiyo.

“Kazi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu vigogo wetu wote wanne wanatosha. Lakini miongoni mwa wote hao ni Gideon pekee ambaye hajawahi kuwania urais na hivyo anafaa kujaribiwa kwa sababu ndiye hajawahi kugombea kiti hicho katika chaguzi zilizopita,” anasema.

Bw Musyoka aliwania urais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo aliibuka wa tatu nyuma ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais mstaafu Mwai Kibaki. Alipata jumla ya kura 867,045, nyingi za kura hizo zikitoka katika ngome yake ya Ukambani.

Naye Bw Mudavadi aliwania urais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo alipata kura 568,456 kwa tiketi ya chama cha United Democratic Front (UDF). Rais Kenyatta ndiye aliibuka mshindi katika uchaguzi huo akifuatwa na Bw Odinga.

Kwa upande wake, Bw Wetang’ula alijiondoa katika kinyang’anyiro cha urais mnamo 2017 na kuunga mkono Bw Odinga aliyepeperusha bendera ya muungano wa Nasa. Aliahidiwa cheo cha Waziri wa kusimamia watumishi wa umma Nasa ingeshinda na kuunda serikali.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala pia anaungama kuwa muungano wa One Kenya Alliace una kibarua kigumu kuteua mgombeaji wake huku akipendekeza kubuniwa kwa jopo maalum la kuendesha shughuli ya uteuzi wa mpeperushaji bendera ya urais.

“Nakubali ni changamoto kuu wakati huu ikizingatiwa mmoja wa wapinzani wetu kama vile Naibu Rais tayari ameanza kuchapa kampeni za urais. Lakini japo napendekeza kiongozi wangu Bw Mudavadi ndiye apewe tiketi hiyo, ingekuwa bora kama shughuli ya uteuzi ingeendeshwa na jopo maalum lenye wawakilishi kutoka vyama tanzu katika One Kenya Alliance,” akasema Bw Malala.

Seneta huyo wa Kakamega anaongeza kuwa wakati huu ANC iko mbioni kujiimarisha kote nchini kupitia usajili wa wanachama wapya kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wapya kuanzia ndani ya mashinani hadi kitaifa.

“Naamini kwamba baada ya kukamilishwa kwa shughuli hii, ANC kitakuwa thabiti na kupata sura ya kitaifa, hali ambayo itaboresha nafasi ya kiongozi wetu Mudavadi kuteuliwa kuwa mgombeaji urais wa One Kenya Alliance,” akaeleza seneta Malala.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua anasema kuwa kigezo kikubwa ambacho kitatumiwa kuamua ni nani miongoni mwa vinara hao wanne wa One Kenya Alliance ni idadi ya kura ambazo kila mmoja wao anaweza kuleta.

“Kwa mfano Mudavadi na Wetang’ula watalazimika kuwashawishi wenzao kwamba moja wao akiteuliwa ataweza kuleta jumla ya kura zaidi ya 3 milioni za uliokuwa mkoa wa magharibi. Eneo hilo linajumuisha kaunti za Kakamega, Bungoma, Vihiga, Busia na sehemu kubwa ya kaunti ya Trans Nzoia. Hii ni kando na kura za watu kutoka jamii ya Waluhya wanaoishi maeneo mengine ya nchi,” anasema.

“Naye Bw Musyoka atahitaji kutoa hakikisho kwamba atavuna jumla ya kura 1.7 milioni za eneo la Ukambani na zingine za kutoka nje ya eneo hili. Lakini Seneta Moi atakuwa na kibarua kigumu kwa sababu sehemu kubwa ya zaidi ya kura 3.5 milioni kutoka Rift Valley ziko mfukoni mwa Dkt Ruto,” anaongeza Bw Mokua.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba katika mkutano waliofanya Jumapili wiki jana nyumbani kwa Bw Wetang’ula, mtaani Karen, vinara hao wa One Kenya Alliance walipendekeza kubuniwa kwa sekritariati itakayoongoza shughuli zake.

Asasi hiyo pia inatarajiwa kuweka mikakati ya kubuniwa kwa kitengo kitakachosimamia masuala ya teuzi za wagombeaji wa muungano kutoka ngazi ya udiwani hadi urais.

Bunge halitachelewesha BBI – Muturi

ALEX NJERU na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi ameelezea matumaini kwamba, mabunge ya Seneti na lile la Kitaifa yatakamilisha kushughulikia Mswada wa Marekebisho ya Katiba 2020 ndani ya muda uliowekwa licha ya changamoto zilizotokana na Covid-19.

Akiongea na wanahabari nyumbani kwake eneo la Mbeere, Kaunti ya Embu, Jumamosi, Bw Muturi hata hivyo, alisema kesi nyingi zilizowasilishwa kupinga mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa huenda yakachelewesha kufanyika kwa kura ya maamuzi.

Bw Muturi alisema kamati ya pamoja ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria inayoongozwa na Muturi Kigano (Mbunge wa Kangema) na Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni, itakamilisha kazi yake kufikia wakati mabunge hayo yatarejelea vikao baada ya mapumziko ya muda yaliyochangiwa na Covid-19.

Alwataka wanachama wa kamati hiyo kuendesha vikao vyao kwa njia ya mtandaoni na wakitaka kufanya mikutano ya ana kwa ana anaweza kuwaruhusu kufanyia mikutano ya kawaida katika ukumbi wa mijadala inayoweza kupokea watu 102.

“Mnamo Mei 4, Bunge la Kitaifa litakaporejelea vikao, sharti ripoti hiyo iwasilishwe ili iweze kujadiliwa na kupigiwa kura,” akasema Bw Muturi.

Aidha, Bw Muturi aliwataka wanachama wa kamati hiyo kutopiga msasa maoni yote waliokusanya kwa sababu hawawezi kuifanyia mabadiliko mswada huo maarufu kama Mswada wa BBI.

Mnamo Alhamisi, Bw Kigano alisema wakati huu kamati hiyo inachunguza maoni kadhaa yaliyotolewa na makundi mbalimbali wakati wa vikao vya kushirikishwa kwa umma.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pia ilitoa maoni na mapendekezo yake kuhusu pendekezo la kuundwa kwa maeneobunge mapya 70.

Wakati huo huo, madiwani wote 15 kutoka kaunti ya Tharaka Nithi wameunga mkono kutawazwa kwa Bw Muturi kuwa Msemaji wa eneo Mlima Kenya.

Kwenye taarifa madiwani hao, wakiongozwa na spika wa bunge la Tharaka Nithi, David Mbaya walisema Bw Muturi ndiye anatosha kurithi Rais Uhuru Kenyatta kama kigogo wa kisiasa wa eneo hilo, atakapostaafu 2022.

FUNGUKA: ‘Usinihukumu; napenda kuvalia mavazi ya kike’

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA ulimwengu huu uliojaa vituko kila kuchao, hata katika masuala ya mahaba, maajabu hayakosi.

Na hakuna anayewakilisha taswira hiyo vyema kama Phillip. Kwanza kabisa Phillip ni mwanamume wa mika wa 37 mkazi wa eneo la Nairobi.

Kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa amekuwa akifanya kazi kama msimamizi wa mojawapo ya mashirika makubwa ya kimataifa hapa nchini.

Bwana huyu ameweza kujiundia himaya ya mali katika sehemu mbali mbali nchini. Kutoka kwa majumba ya kifahari, hadi kwa magari ya uchukuzi, na fleti za nyumba za kukodesha, ni dhahiri kwamba kaka huyu kifedha amejihami vilivyo.

Tukija katika masuala ya kimaumbile, ni madume wachache ambao wanaweza jisimamisha kwenye orodha sawa na kaka huyu.

Utanashati wake ni wa kustaajabisha. Dume limeumbwa likaumbika. Vituguta vyake ni thabiti kana kwamba Maulana alipomuumba alitumia patasi yenye ncha kali kuchonga sehemu hii kwa ukamilifu.

Kwenye mashavu yake kamilifu kuna vibonyo vinavyobonyea ndani kila anaposema au kucheka, na kuonyesha meno yake yaliyojipanga kinywaani kwa laini nyoofu.

Umbo lake pia ni la kipekee. Mbali na kimo chake cha kati, kifua chake kipana na thabiti, kinahitimisha baadhi ya sifa zinazomfanya kuwa kivutio cha mabinti wengi.

Lakini licha ya sifa hizi zote, kaka huyu amekuwa na changamoto ya kupata mpenzi, mchumba au mke wa kudumu, kutokana na sababu anazofahamu mwenyewe:

“Napenda kuvalia suruali na mavazi mengine ya ndani ya wanawake ninapolala. Kwa hivyo ninapolala lazima nivalie chupi, sidiria na kamisi.

Na sio kwamba navalia mavazi mapya, la! Lazima yawe yale ambayo mpenzi au mchumbangu amevalia na hayajasafishwa. Namaanisha kwamba ikiwa umevalia mavazi haya mchana kutwa, ukija na kuyatoa nyumbani, usiyasafishe, bali unipe nami niyavalie usiku kucha.

Kuna wale wanaoshindwa kuelewa naridhika vipi tu kwa kufanya hivyo? Jibu ni sahili, kuyavalia tu, kunashibisha njaa yangu ya mahaba.

Kumbuka kwamba kwangu hayo ni mahaba tosha. Nikiyavalia tu sina haja ya kumgusa au kushiriki mahaba na binti yeyote.

Kwa hivyo ukitaka kuwa mchumba wangu basi ujiandae kunihudumia kwa kunipa mavazi yako ya ndani tu! Ngoma sina haja nayo, kwa maana kuwa hata watoto sitaki.

Lakini mimi sio mchoyo. Ukiwa mpenzi au mchumba wangu na kukubali masharti yangu, niko tayari kukuruhusu kuwa na uhusiano wa pembeni mradi tu ukirejea nyumbani, nami utanihudumia kwa njia hiyo.

Ni jambo ambalo limeninyima fursa ya kuwa na mchumba au mke wa kudumu. Wengi ninaokutana nao wanavutiwa na uzuri vile vile utajiri wangu, lakini inapowadia wakati wa kushibisha kiu yangu ya mahaba kuambatana na mbinu yangu, wengi hutoweka.

Kuna wale ambao mwanzoni hujaribu kuvumilia, lakini muda unavyozidi kusonga wanashika njia na kutoweka.

Lakini licha ya haya, sina nia ya kulegeza msimamo wangu na kamwe sitamlazimisha yeyote kukaa nami. Ikiwa unataka kuwa nami njoo, lakini sahau mahaba na mapenzi mengine ya kawaida. Mahitaji yako ya kifedha yatakidhiwa vilivyo lakini upande huo mwingine, sahau.”

Viongozi wamuomboleza mume wa Malkia Elizabeth

Na AFP

LONDON, Uingereza

VIONGOZI mbalimbali duniani wanaendelea kuomboleza kifo cha mumewe Malkia wa Uingereza Elizabeth II, Mwanamflame Philip, ambaye ni kiongozi wa ufalme wa Uingereza.

Marehemu mwanamflame Philip aliaga dunia mnamo Ijumaa akiwa na miaka 99 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama alikuwa kati ya viongozi wa kwanza waliomwomboleza Philip, akimtaja kama mtu mpole ambaye alitangamana na viongozi wote kwa usawa bila kujali hadhi kubwa aliyokuwa nayo katika jamii.

Mnamo 2011, Rais Obama aliishi katika Kasri la Buckingham kwa siku mbili na kushiriki chajio na familia hiyo ya ufalme. Aidha alikumbuka jinsi alivyokutana na Philip na mazungumzo yao katika ikulu hiyo wakati wa kongamano la mataifa yenye uchumi mkubwa, G20 mnamo Aprili 2009.

“Alikuwa mkarimu kama walivyokuwa wanasiasa wenye sifa kubwa kihistoria kama Winston Churchil, Kennedy, Nelson Mandela na Gorbachev. Ziara yetu katika Kasri la Buckingham ilikuwa ya heri kwa kuwa Philip alitangamana na wote vizuri licha ya kuwa kati ya watu wenye ushawishi na heshima kuu duniani,” akasema Rais Obama.

Marais wa Afrika hawakuachwa nyuma, wengi wakituma rambirambi zao kwa malkia Elizabeth 11 na kumsifia Philip.

“Zambia inaungana na nchi nyingine kutuma rambirambi kwa familia ya Ufalme wa Uingereza kufuatia kifo cha Philip. Alikuwa mtu mwenye utu na kiongozi mwenye hekima ambaye aliishi miaka mingi na kuwasaidia watu wengi duniani,” akasema Rais wa Zambia Edgar Lungu.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari pia alimwomboleza Philip akimtaja kama kiongozi wa ulimwengu ambaye aliishi maisha tulivu ndani ya ufalme na alikuwa mkarimu aliyewasaidia watu wasiojiweza.

“Alihusika katika kufadhili miradi ya vijana na kutunza wanyamapori. Ukarimu wake umehakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata ufadhili wa miradi mbalimbali kutoka Uingereza,” akasema Rais Buhari.

Ufalme wa Eswatini pia ulituma rambirambi zao kupitia wizara ya kigeni, wakisema maisha ya Philip katika ufalme wa Uingereza ulifungua milango ya misaada kwa nchi nyingi za kiafrika.

“Alisifiwa na vizazi vyote Marekani, mataifa ya Jumuiya ya Madola na Duniani. Hasa ukarimu wake utakumbukwa daima dawamu,” ikasema taarifa kutoka Ufalme wa Eswatini.

Aliyekuwa Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf na mwenzake wa Botswana Ian Khama walimiminia sifa marehemu, wakisema kifo chake ni pigo kuu kwa mataifa yaliyoko chini ya Jumuiya ya Madola.

Walibora akumbukwa kwa kongamano

ELVIS ONDIEKI na OSBORNE MANYENGO

ZAIDI ya wapenzi 1,000 wa lugha ya Kiswahili leo saa 10 jioni wanaandaa kongamano kupitia mtandao, kumuenzi na kumkumbuka msomi na mwandishi maarufu, Prof Ken Walibora aliyeaga dunia mwaka 2020.

Kongamano hilo linafanyika kupitia teknolojia ya Zoom likijumuisha wasomi wa Kiswahili pamoja na wengine na litatamatika saa mbili usiku.

Kulingana na aliyekuwa rafiki wa karibu wa Prof Walibora, Hezekiel Gikambi, kongamano hilo lina mada “Unamkumbuka Hayati Prof Ken Walibora kwa Lipi? na linaendelea kwa muda wa saa nne.

Prof F.E.M.K. Senkoro wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Abdilatif Abdalla wa Chuo Kikuu cha Hamburg nchini Ujerumani na Dkt Aidah Mutenyo ambaye ni mwalimu wa Kiswahili nchini Uganda, ni kati ya wanaotarajiwa kuhutubu katika kongamano hilo.

Kutoka hapa nchini, Maprofesa Mosol Kandagor, Simon Sossion, Tom Olali na waandishi wa vitabu Wallah Bin Wallah pamoja Pauline Keya pia watahutubu.

Kandagor ameeleza jinsi wanataaluma wanavyojizatiti hasa katika uandishi.

“Prof Ken Walibora alikuwa mnyenyekevu na hivyo ndivyo mtu aliyeelimika anafaa kuwa,” amesema Kandagor.

Najma ambaye ni bintiye mwandishi Said Ahmed Mohamed ametoa ujumbe wa baba yake na mama yake Rahma kuhusu ukuruba wao na Prof Ken Walibora.

“Walibora alifanya kazi pamoja na wazazi wangu na alikuwa mwaminifu,” amesema Najma.

Familia yake nayo imeitaka serikali kuisaidia kupata mali ambayo ilikuwa ikimilikiwa na mwanahabari huyo kwa kuwa hakuweka wazi mali yake wakati alipokuwa hai.

Nduguye Prof Walibora, Patrick Wafula ambaye ni mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Kipseon, alieleza Taifa Leo kwamba wanapata ugumu wa kupata mali ambayo ilikuwa ikimilikiwa na marehemu.

“Hakutuambia mali aliyokuwa akimiliki wakati alipokuwa hai,” akasema Bw Wafula.

Prof Walibora alizaliwa eneo la Cherang’any, Kaunti ya Trans Nzoia. Mke wake na watoto wake wanaishi Marekani na Bw Wafula anasema kuwa wamekuwa wakiwasiliana nao mara kwa mara.

Pia wanadai kwamba uchunguzi kuhusu kifo cha Prof Walibora umekwama na wamekuwa wakitathmini njia tofauti ili kufahamu ukweli kuhusu kiini cha kifo chake.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakitushauri tuajiri mchunguzi wa kibinafsi ili kufahamu kilichomuua. Tunataka kujua hasa nini kilisababisha kifo chake,” akaongeza Bw Wafula.

Nahodha wa Changamwe Ladies aomba wadhamini wazisaidie klabu kufika Ligi Kuu

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MCHEZO wa mpira wa miguu wa wanawake unaweza kuwa maarufu na kuimarika zaidi Pwani ikiwa wahisani watajitolea kuzidhamini klabu ambazo zina nia ya kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Kenya (KWPL).

Nahodha wa Changamwe Ladies FC, Fidu Namayi ameeleza kuwa kuwa Pwani ina wasichana wengi wenye vipaji vya kucheza kandanda ya hali ya juu lakini wengi wao wanabakia kucheza mechi za kirafiki na za mashindano kwa kuwa hawapati kuonekana qwakicheza ligi kuu.

“Ni jambo la kuhuzunisha kuwa wakati huu hatuna klabu yoyote ya wanawake kutoka Pwani inayoshiriki Ligi Kuu sababu timu zetu zote ziliteremshwa ngazi kutokana na kushindwa kukamilisha kucheza mechi zao za ugenini kwa ukosefu wa udhamini,” akasema Fidu.

Anasema ni jambo la kutia moyo kwa baadhi ya wadhamini kutayarisha mashindano ya mara kwa mara baina ya klabu za Pwani kwani kufanya hivyo kutavutia wasichana wengi kujiunga na mchezo huo ambapo wataweza kuinua vipaji vyao.

“Tunaomba wadhamini wajitokeze kuzisaidia klabu zetu zinazoshiriki ligi mbalimbali zipate kupanda ngazi hadi ligi kuu kwani ndipo tutapata kuonekana na wengi wataweza kuchaguliwa katika timu ya taifa ya Harambee Starlets,” akasema nahodha huyo.

Mwaka uliopita, serikali ya kaunti ya Tana River ilidhamini mashindano ya Coast Ladies Football Tournament mjini Hola ambapo klabu tisa zilishiriki na Mombasa Olympic, inayoshiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza iliibuka washindi.

Mashindano mengine yaliyodhaminiwa na wakili George Kithi yalifanyika mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi kabla ya kusimamishwa kwa michezo ambapo Kilifi Ladies iliishinda Changamwe Ladies kwa bao 1-0.

Mwanajeshi aliyeshtakiwa kwa kosa la kudhulumu mtu aachiliwa huru

Na BRIAN OCHARO

MWANAJESHI wa zamani, Swabir Abdulrazaq Mohamed, Ijumaa alipata afueni baada ya kupewa dhamana ya Sh50,000 kutokana na shtaka la kumpiga mtu na kumsababishia majeraha ya mwili.

Bw Mohamed, ambaye hadi Jumatatu alikuwa akifanya kazi Mombasa, alikanusha shtaka la kumshambulia Evans Odhiambo alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Vincent Adet.

Upande wa mashtaka unadai mtuhumiwa pamoja na watu wengine ambao hawakuwa mahakamani, walifanya kosa hilo mnamo Septemba 14, 2020, katika eneo la Shimanzi, Mombasa.

Bw Mohamed alipewa dhamana licha ya pingamizi kutoka kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ambayo ilitaka azuiliwe hadi mwathiriwa awekwe chini ya Mpango wa Kulinda Mashahidi.

“Mhasiriwa hana makazi na tunaogopa kwamba mshukiwa anaweza kumshawishi kabla ya kutoa ushahidi,” akasema kiongozi wa Mashtaka Ogega Bosibori. Pia Bi Bosibori aliambia korti kuwa umma bado una machungu na mshukiwa na kwamba kuzuiliwa kwake kutamhakikisha usalama wake.

“Hii pia ni kwa usalama wake mwenyewe kwa sababu tunahisi umma umemtambua vyema, na kwa hivyo itakuwa hatari kwake kuwa huru kuanzia sasa,” akaongeza.

Aidha Bi Bosibori alisema jambo hilo limevutia umma na kwa hivyo linapaswa kushughulikiwa kwa uangalifu mwingi. Bi Bosibori pia alidai kwamba wachunguzi bado hawajapata ushahidi katika eneo ambako mwanajeshi huyo alidaiwa kutenda kosa hilo.

Mawakili wa mshukiwa, Said Ali na Nabil Mohamed walipuuza madai ya upande wa mashtaka kuwa hayana msingi na kuhimiza korti impe dhamana. “Mshukiwa nii afisa wa zamani, ni raia anayetii sheria. Tunasihi korti isitilie maanani uvumi unaenzwa na upande wa mashtaka,” akasema Bw Ali.

Kwenye uamuzi wake, hakimu alikubaliana na mawakili hao na kusema kuwa upande wa mashtaka ulipaswa kutoa sababu zaidi zenye mashiko kuishawishi mahakama imzuilie mshukiwa.

Ombi kama hilo la kutaka mshukiwa azuiliwe kwa siku 14 zaidi lilikataliwa Jumatano huku mahakama ikiwapa wachunguzi siku tatu ya kukamilisha upelelezi wao. Upande wa mashtaka ulitaka wiki mbili ili kuwezesha maafisa wake kukagua kanda ya video kumtafuta mwathiriwa na pia kupata rekodi zake za matibabu.

Pia, ilitaka siku zaidi kuthibitisha ikiwa mwaathiriwa aliiba chochote, na ikiwa wizi huo ulirekodiwa katika kituo chochote cha polisi.

Raila apewa ujumbe wa Ruto

Na JUSTUS WANGA

GAVANA wa Kakamega, Wycliffe Oparanya, jana alikutana na Kinara wa ODM Raila Odinga na kumpasha ujumbe wa kikao chake na Naibu Rais William Ruto katika Mbuga ya Masai Mara, Kaunti ya Narok mnamo Jumatano na Alhamisi wiki hii.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa Bw Oparanya alikutana na Bw Odinga nyumbani kwake Karen kwa zaidi ya saa tano, ambapo alimpasha ujumbe kutoka kwa Dkt Ruto.

Baada ya mkutano huo, Bw Oparanya alikiri kwamba Bw Odinga alikuwa na habari kuhusu mkutano wake na Dkt Ruto.

Duru zilisema kuwa Bw Oparanya alimweleza bosi wake kuhusu hamu ya Dkt Ruto kushirikiana na ODM kuunda muungano kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Pia ilidokezwa kuwa baada ya mkutano wa Ijumaa, Bw Odinga alimpatia Bw Oparanya baraka za kuendelea kushauriana na naibu rais kuhusu watakavyofanya iwapo jahazi ya handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta itazama.

Mkutano kati ya Bw Oparanya na Dkt Ruto katika Masai Mara unaripotiwa kushangaza wandani wa Rais Kenyatta, hasa baada ya Bw Odinga kukosa kujitokeza hadharani kukanusha kuwa ndiye aliyemtuma gavana wa Kakamega.

Bw Odinga na washirika wake wameingiwa na kiwewe cha uaminifu wa Rais Kenyatta kwa handisheki baada yake kuanza kujihusisha zaidi na muungano mpya wa One Kenya Alliance unaojumuisha Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Gideon Moi na Moses Wetang’ula.

Alipoulizwa kama kweli mkutano wa Masai Mara ulikuwa umepangwa, Bw Oparanya alikanusha akisema walipatana kila mmoja akiwa kwenye shughuli zake.

“Nilikuwa kwenye shughuli zangu za kibiashara nilipompata naibu rais huko. Nilimpigia simu Bw Odinga na kumjulisha na akaniambia ni sawa nikifanya mazungumzo naye,” akasema Bw Oparanya.

“Nilijua nikionekana na Dkt Ruto itakuwa habari kubwa ndiposa nikampigia simu mkubwa wangu. Raila aliniambua hakuna maadui wa kudumu katika siasa na ni sawa tukikutana,” akaongeza Bw Oparanya.

Mwezi jana naibu rais alisema anaweza kushirikiana kisiasa na Bw Odinga. Hii ni licha ya wawili hao kuwa na uhusiano wenye uhasama kwa miaka mingi hasa baada ya handisheki mnamo 2018.

Ripoti zilieleza kuwa katika mkutano wa Masai Mara, Dkt Ruto alimuuliza gavana wa Kakamega kuhusu iwapo ODM ilikuwa ikipanga muungano wowote kwa ajili ya 2022.

“Nilimwambia Ruto kuwa kufikia sasa hatujachukua hatua yoyote ya kubuni muungano. Pia tulijadili masuala ya kitaifa,” akaeleza gavana huyo.

Wachanganuzi wa siasa wamepuzilia mbali kuwa mkutano kati ya Dkt Ruto na Bw Oparanya ulikuwa wa kubahatisha.

Mwezi jana gavana huyo alionekana kukubaliana na Dkt Ruto kuhusu masuala ya kitaifa aliposema kuwa mchakato wa BBI sio suala muhimu kwa ODM kwa sasa kwani kuna mambo mengine ya dharura kama vile Covid-19 na madeni ya taifa.

Matamshi hayo pamoja na ya vigogo wengine wa ODM kuhusu kuhisi Rais Kenyatta anamsaliti Bw Odinga yalimfanya rais kumtafuta ili kumtuliza.

Baadhi ya washirika wa wanasiasa wakuu wanashuku kuwa rais anawachezea kwa kumpa kila mmoja wao matumaini ya kumuunga mkono kuwania urais 2022

Hii ni kutokana na Rais Kenyatta kuwaweka wote katika hali ya mshikemshike kwa kukosa kujitokeza wazi kuonyesha mahali roho yake imo kikamilifu.

Baadhi ya wafuasi wa Bw Odinga wana wasiwasi kuwa Rais Kenyatta anajaribu kumchezesha dhidi ya waliokuwa washirika wake kwenye muungano wa National Super Alliance (Nasa)

Mbunge wa ODM aliyezungumza na Taifa Leo alisema kuwa kuwa hawamwelewi tena Rais Kenyatta, kwani vitendo vyake vinaonyesha kuwa anamhujumu Bw Odinga.

“Vitendo vya rais vinaonyesha nia mbaya na anatukanganya,” akasema mbunge huyo aliyeomba tusitaje jina lake.

Suluhu akutana na ujumbe wa Uhuru, kukutana na Museveni

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta amemwalika kiongozi wa Tanzania Rais Samia Suluhu kuzuru Kenya ili kuimarisha na kukuza uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rais Kenyatta, kupitia ujumbe wake uliokutana na Rais Suluhu katika Ikulu ya Dar es Salaam, Jumamosi, alisema kuwa Kenya iko tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali.

Ujumbe wa Rais Kenyatta uliongozwa na waziri wa Michezo Amina Mohamed na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu.

Kwa upande wake, Rais Suluhu alisema kuwa serikali yake itaendeleza uhusiano mwema uliokuwepo baina ya Kenya na Tanzania wakati wa uongozi wa mtangulizi wake John Pombe Magufuli aliyeaga dunia mnamo Machi 17, mwaka huu.

Rais Suluhu aliitaka Kamati ya Ushirikiano wa Pamoja (JPC) iliyobuniwa kuimarisha ushirikiano baina ya Kenya na Tanzania kuanza vikao mara moja. Kamati ya JPC ilikutana kwa mara ya mwisho mnamo 2016.

Janga la corona lilisababisha uhusiano baina ya Kenya na Tanzania kudorora baada ya Kenya kuwataka wasafiri kutoka katika taifa hilo jirani kuwekwa karantini kwa siku 14 mwaka jana.

Tanzania ililipiza kisasi kwa kupiga marufuku ndege za Kenya kuingia nchini humo, hali iliyosababisha Kenya kuruhusu Watanzania kuingia humu nchini bila kuwekwa karantini.

Hatua ya Kenya kupiga marufuku mahindi kutoka Tanzania kwa madai ya kuwa na sumu pia ilisababisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili kuyumba.

Kenya, hata hivyo, iliondoa marufuku hiyo na kutoa masharti makali yanayofaa kutimizwa kabla ya mahindi ya Tanzania kuingizwa humu nchini.

Rais Suluhu, kesho Jumapili anatarajiwa kuelekea nchini Uganda ambapo atakutana na Rais Yoweri Museveni.

“Rais Suluhu ataimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda na kushiriki makubaliano ya mwisho kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi,” ikasema taarifa ya Ikulu ya Tanzania.

Mradi huo wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta wa Afrika Mashariki (EACOP) utagharimu Sh350 bilioni. Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445 litasafirisha mafuta ghafi kutoka katika eneo la Hoima, Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Usinduzi wa mradi huo ulifaa kufanyika Machi, mwaka huu, lakini shughuli hiyo iliahirishwa hadi mwezi huu kufuatia kifo cha Magufuli.

Mnamo Septemba 2020, Rais Museveni alikutana na Magufuli katika eneo la Chato, Tanzania ambapo viongozi wawili hao waliafikiana kuharakisha mradi huo.

Rais Suluhu ameahidi kuhakikisha kuwa miradi yote iliyoanzishwa na Magufuli inakamilishwa.

Kiongozi huyo wa Tanzania, wiki iliyopita, alisema kuwa serikali yake italaaniwa na Magufuli endapo haitakamilisha miradi aliyoianzisha.