Nahodha wa Changamwe Ladies aomba wadhamini wazisaidie klabu kufika Ligi Kuu

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MCHEZO wa mpira wa miguu wa wanawake unaweza kuwa maarufu na kuimarika zaidi Pwani ikiwa wahisani watajitolea kuzidhamini klabu ambazo zina nia ya kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Kenya (KWPL).

Nahodha wa Changamwe Ladies FC, Fidu Namayi ameeleza kuwa kuwa Pwani ina wasichana wengi wenye vipaji vya kucheza kandanda ya hali ya juu lakini wengi wao wanabakia kucheza mechi za kirafiki na za mashindano kwa kuwa hawapati kuonekana qwakicheza ligi kuu.

“Ni jambo la kuhuzunisha kuwa wakati huu hatuna klabu yoyote ya wanawake kutoka Pwani inayoshiriki Ligi Kuu sababu timu zetu zote ziliteremshwa ngazi kutokana na kushindwa kukamilisha kucheza mechi zao za ugenini kwa ukosefu wa udhamini,” akasema Fidu.

Anasema ni jambo la kutia moyo kwa baadhi ya wadhamini kutayarisha mashindano ya mara kwa mara baina ya klabu za Pwani kwani kufanya hivyo kutavutia wasichana wengi kujiunga na mchezo huo ambapo wataweza kuinua vipaji vyao.

“Tunaomba wadhamini wajitokeze kuzisaidia klabu zetu zinazoshiriki ligi mbalimbali zipate kupanda ngazi hadi ligi kuu kwani ndipo tutapata kuonekana na wengi wataweza kuchaguliwa katika timu ya taifa ya Harambee Starlets,” akasema nahodha huyo.

Mwaka uliopita, serikali ya kaunti ya Tana River ilidhamini mashindano ya Coast Ladies Football Tournament mjini Hola ambapo klabu tisa zilishiriki na Mombasa Olympic, inayoshiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza iliibuka washindi.

Mashindano mengine yaliyodhaminiwa na wakili George Kithi yalifanyika mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi kabla ya kusimamishwa kwa michezo ambapo Kilifi Ladies iliishinda Changamwe Ladies kwa bao 1-0.

Mwanajeshi aliyeshtakiwa kwa kosa la kudhulumu mtu aachiliwa huru

Na BRIAN OCHARO

MWANAJESHI wa zamani, Swabir Abdulrazaq Mohamed, Ijumaa alipata afueni baada ya kupewa dhamana ya Sh50,000 kutokana na shtaka la kumpiga mtu na kumsababishia majeraha ya mwili.

Bw Mohamed, ambaye hadi Jumatatu alikuwa akifanya kazi Mombasa, alikanusha shtaka la kumshambulia Evans Odhiambo alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Vincent Adet.

Upande wa mashtaka unadai mtuhumiwa pamoja na watu wengine ambao hawakuwa mahakamani, walifanya kosa hilo mnamo Septemba 14, 2020, katika eneo la Shimanzi, Mombasa.

Bw Mohamed alipewa dhamana licha ya pingamizi kutoka kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ambayo ilitaka azuiliwe hadi mwathiriwa awekwe chini ya Mpango wa Kulinda Mashahidi.

“Mhasiriwa hana makazi na tunaogopa kwamba mshukiwa anaweza kumshawishi kabla ya kutoa ushahidi,” akasema kiongozi wa Mashtaka Ogega Bosibori. Pia Bi Bosibori aliambia korti kuwa umma bado una machungu na mshukiwa na kwamba kuzuiliwa kwake kutamhakikisha usalama wake.

“Hii pia ni kwa usalama wake mwenyewe kwa sababu tunahisi umma umemtambua vyema, na kwa hivyo itakuwa hatari kwake kuwa huru kuanzia sasa,” akaongeza.

Aidha Bi Bosibori alisema jambo hilo limevutia umma na kwa hivyo linapaswa kushughulikiwa kwa uangalifu mwingi. Bi Bosibori pia alidai kwamba wachunguzi bado hawajapata ushahidi katika eneo ambako mwanajeshi huyo alidaiwa kutenda kosa hilo.

Mawakili wa mshukiwa, Said Ali na Nabil Mohamed walipuuza madai ya upande wa mashtaka kuwa hayana msingi na kuhimiza korti impe dhamana. “Mshukiwa nii afisa wa zamani, ni raia anayetii sheria. Tunasihi korti isitilie maanani uvumi unaenzwa na upande wa mashtaka,” akasema Bw Ali.

Kwenye uamuzi wake, hakimu alikubaliana na mawakili hao na kusema kuwa upande wa mashtaka ulipaswa kutoa sababu zaidi zenye mashiko kuishawishi mahakama imzuilie mshukiwa.

Ombi kama hilo la kutaka mshukiwa azuiliwe kwa siku 14 zaidi lilikataliwa Jumatano huku mahakama ikiwapa wachunguzi siku tatu ya kukamilisha upelelezi wao. Upande wa mashtaka ulitaka wiki mbili ili kuwezesha maafisa wake kukagua kanda ya video kumtafuta mwathiriwa na pia kupata rekodi zake za matibabu.

Pia, ilitaka siku zaidi kuthibitisha ikiwa mwaathiriwa aliiba chochote, na ikiwa wizi huo ulirekodiwa katika kituo chochote cha polisi.

Raila apewa ujumbe wa Ruto

Na JUSTUS WANGA

GAVANA wa Kakamega, Wycliffe Oparanya, jana alikutana na Kinara wa ODM Raila Odinga na kumpasha ujumbe wa kikao chake na Naibu Rais William Ruto katika Mbuga ya Masai Mara, Kaunti ya Narok mnamo Jumatano na Alhamisi wiki hii.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa Bw Oparanya alikutana na Bw Odinga nyumbani kwake Karen kwa zaidi ya saa tano, ambapo alimpasha ujumbe kutoka kwa Dkt Ruto.

Baada ya mkutano huo, Bw Oparanya alikiri kwamba Bw Odinga alikuwa na habari kuhusu mkutano wake na Dkt Ruto.

Duru zilisema kuwa Bw Oparanya alimweleza bosi wake kuhusu hamu ya Dkt Ruto kushirikiana na ODM kuunda muungano kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Pia ilidokezwa kuwa baada ya mkutano wa Ijumaa, Bw Odinga alimpatia Bw Oparanya baraka za kuendelea kushauriana na naibu rais kuhusu watakavyofanya iwapo jahazi ya handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta itazama.

Mkutano kati ya Bw Oparanya na Dkt Ruto katika Masai Mara unaripotiwa kushangaza wandani wa Rais Kenyatta, hasa baada ya Bw Odinga kukosa kujitokeza hadharani kukanusha kuwa ndiye aliyemtuma gavana wa Kakamega.

Bw Odinga na washirika wake wameingiwa na kiwewe cha uaminifu wa Rais Kenyatta kwa handisheki baada yake kuanza kujihusisha zaidi na muungano mpya wa One Kenya Alliance unaojumuisha Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Gideon Moi na Moses Wetang’ula.

Alipoulizwa kama kweli mkutano wa Masai Mara ulikuwa umepangwa, Bw Oparanya alikanusha akisema walipatana kila mmoja akiwa kwenye shughuli zake.

“Nilikuwa kwenye shughuli zangu za kibiashara nilipompata naibu rais huko. Nilimpigia simu Bw Odinga na kumjulisha na akaniambia ni sawa nikifanya mazungumzo naye,” akasema Bw Oparanya.

“Nilijua nikionekana na Dkt Ruto itakuwa habari kubwa ndiposa nikampigia simu mkubwa wangu. Raila aliniambua hakuna maadui wa kudumu katika siasa na ni sawa tukikutana,” akaongeza Bw Oparanya.

Mwezi jana naibu rais alisema anaweza kushirikiana kisiasa na Bw Odinga. Hii ni licha ya wawili hao kuwa na uhusiano wenye uhasama kwa miaka mingi hasa baada ya handisheki mnamo 2018.

Ripoti zilieleza kuwa katika mkutano wa Masai Mara, Dkt Ruto alimuuliza gavana wa Kakamega kuhusu iwapo ODM ilikuwa ikipanga muungano wowote kwa ajili ya 2022.

“Nilimwambia Ruto kuwa kufikia sasa hatujachukua hatua yoyote ya kubuni muungano. Pia tulijadili masuala ya kitaifa,” akaeleza gavana huyo.

Wachanganuzi wa siasa wamepuzilia mbali kuwa mkutano kati ya Dkt Ruto na Bw Oparanya ulikuwa wa kubahatisha.

Mwezi jana gavana huyo alionekana kukubaliana na Dkt Ruto kuhusu masuala ya kitaifa aliposema kuwa mchakato wa BBI sio suala muhimu kwa ODM kwa sasa kwani kuna mambo mengine ya dharura kama vile Covid-19 na madeni ya taifa.

Matamshi hayo pamoja na ya vigogo wengine wa ODM kuhusu kuhisi Rais Kenyatta anamsaliti Bw Odinga yalimfanya rais kumtafuta ili kumtuliza.

Baadhi ya washirika wa wanasiasa wakuu wanashuku kuwa rais anawachezea kwa kumpa kila mmoja wao matumaini ya kumuunga mkono kuwania urais 2022

Hii ni kutokana na Rais Kenyatta kuwaweka wote katika hali ya mshikemshike kwa kukosa kujitokeza wazi kuonyesha mahali roho yake imo kikamilifu.

Baadhi ya wafuasi wa Bw Odinga wana wasiwasi kuwa Rais Kenyatta anajaribu kumchezesha dhidi ya waliokuwa washirika wake kwenye muungano wa National Super Alliance (Nasa)

Mbunge wa ODM aliyezungumza na Taifa Leo alisema kuwa kuwa hawamwelewi tena Rais Kenyatta, kwani vitendo vyake vinaonyesha kuwa anamhujumu Bw Odinga.

“Vitendo vya rais vinaonyesha nia mbaya na anatukanganya,” akasema mbunge huyo aliyeomba tusitaje jina lake.

Suluhu akutana na ujumbe wa Uhuru, kukutana na Museveni

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta amemwalika kiongozi wa Tanzania Rais Samia Suluhu kuzuru Kenya ili kuimarisha na kukuza uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rais Kenyatta, kupitia ujumbe wake uliokutana na Rais Suluhu katika Ikulu ya Dar es Salaam, Jumamosi, alisema kuwa Kenya iko tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali.

Ujumbe wa Rais Kenyatta uliongozwa na waziri wa Michezo Amina Mohamed na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu.

Kwa upande wake, Rais Suluhu alisema kuwa serikali yake itaendeleza uhusiano mwema uliokuwepo baina ya Kenya na Tanzania wakati wa uongozi wa mtangulizi wake John Pombe Magufuli aliyeaga dunia mnamo Machi 17, mwaka huu.

Rais Suluhu aliitaka Kamati ya Ushirikiano wa Pamoja (JPC) iliyobuniwa kuimarisha ushirikiano baina ya Kenya na Tanzania kuanza vikao mara moja. Kamati ya JPC ilikutana kwa mara ya mwisho mnamo 2016.

Janga la corona lilisababisha uhusiano baina ya Kenya na Tanzania kudorora baada ya Kenya kuwataka wasafiri kutoka katika taifa hilo jirani kuwekwa karantini kwa siku 14 mwaka jana.

Tanzania ililipiza kisasi kwa kupiga marufuku ndege za Kenya kuingia nchini humo, hali iliyosababisha Kenya kuruhusu Watanzania kuingia humu nchini bila kuwekwa karantini.

Hatua ya Kenya kupiga marufuku mahindi kutoka Tanzania kwa madai ya kuwa na sumu pia ilisababisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili kuyumba.

Kenya, hata hivyo, iliondoa marufuku hiyo na kutoa masharti makali yanayofaa kutimizwa kabla ya mahindi ya Tanzania kuingizwa humu nchini.

Rais Suluhu, kesho Jumapili anatarajiwa kuelekea nchini Uganda ambapo atakutana na Rais Yoweri Museveni.

“Rais Suluhu ataimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda na kushiriki makubaliano ya mwisho kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi,” ikasema taarifa ya Ikulu ya Tanzania.

Mradi huo wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta wa Afrika Mashariki (EACOP) utagharimu Sh350 bilioni. Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445 litasafirisha mafuta ghafi kutoka katika eneo la Hoima, Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Usinduzi wa mradi huo ulifaa kufanyika Machi, mwaka huu, lakini shughuli hiyo iliahirishwa hadi mwezi huu kufuatia kifo cha Magufuli.

Mnamo Septemba 2020, Rais Museveni alikutana na Magufuli katika eneo la Chato, Tanzania ambapo viongozi wawili hao waliafikiana kuharakisha mradi huo.

Rais Suluhu ameahidi kuhakikisha kuwa miradi yote iliyoanzishwa na Magufuli inakamilishwa.

Kiongozi huyo wa Tanzania, wiki iliyopita, alisema kuwa serikali yake italaaniwa na Magufuli endapo haitakamilisha miradi aliyoianzisha.

Wabunge wa ODM wakosoa ubomoaji wa Njiru

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu wa ODM wameisuta serikali kuhusiana na ubomoaji ambao ulitekelezwa wa makazi ya watu uliotekelezwa katika eneo la Njiru, Nairobi

Matingatinga yaliyodaiwa kuwa ya Idara ya Utoaji Huduma Jijini Nairobi (NMS) yalibomoa makazi ya watu katika kipande kimoja cha ardhi katika eneo hilo, ambacho inadaiwa kimejengwa katika ardhi ya serikali.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge Ijumaa, wabunge T. J Kajwang’ (Ruaraka), Anthony Oluoch (Mathare) na Zuleikha Hassan (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kwale) walitaja kitendo hicho kama cha kikatili na kinachoonyesha kuwa serikali haijali maslahi ya watu wanyonge.

Bila kutaja majina, wabunge hao watatu walidai kuwa familia ya afisa mmoja mmoja serikali ndio inayopania kutwaa ardhi hiyo ambako zaidi ya familia 5,000 zimeishi kwa miaka mingi. Ubomoaji huo ulitekelezwa mnamo Machi 27.

“Iweje kwamba wewe mtu mwenye mamlaka na tayari una ardhi kubwa unawashambulia watu wadogo na kubomoa nyumba zao kwa njia ya kikatili? Hii ni kinyume cha sheria ikizingatiwa kuwa watu hawa wameishi katika kipande hicho cha ardhi kwa zaidi ya miaka 20,” akasema Bw Kajwang’.

Mbunge huyo ambaye ni wakili alidai kuwa nia ya ubomoaji huo ni kujitajirisha watu fulani wala sio kukomboa ardhi ya serikali.

Kwa upande wake, Bw Oluoch alisema kwa ODM kuamua kufanya kazi na serikali ya Jubilee, haimaanishi kuwa “sisi kama wabunge wa upinzani hatujaacha wajibu wetu wa kukosoa maovu yanayotekelezwa na serikali.”

“Ikiwa unadhani kwamba kwa sababu tunashirikiana kisiasa unaweza kutunyamazisha umejidanganya. Ijulikane kwamba tungali sauti ya wananchi. Tutapinga kile ambacho ni kibaya tukiwa katika viti vya nyuma bungeni,” akasema mbunge huyo wa Mathare.

Wabunge hao walisema wakazi hao walifurushwa bila kupewa ilani inavyohitajika kisheria.

Bi Zuleikha aliitika maelezo kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Ndani akisema “tunasikia kuwa agizo hilo la ubomoaji lilitoka huko.”

Karakara ni matunda ya thamani na rahisi kuyastawisha

Na SAMMY WAWERU

MATUNDA ya karakara ni kati ya yanayompa mapato ya kuridhisha kijana Robert Kirinyet, ambaye ni mkulima wa mimeamseto Kaunti ya Bomet.

Aliingilia ukuzaji wa matunda hayo mwanzoni mwa 2019, baada ya kushawishiwa na rafiki yake kazini kukumbatia mimea ya thamani.

Akiwa alianza na miche 140 ya mikarakara, kufikia sasa Kirinyet ana jumla ya 600 inayozalisha.

Anasema anaendelea kuandaa robo ekari zaidi ili kuyaongeza, kutokana na mapato ya kuridhisha anayotia kibindoni kupitia karakara.

Kwa sasa anayalima katika kipande cha shamba chenye ukubwa wa robo tatu.

Kinachomvutia zaidi katika ukuzaji wa matunda hayo, ni wepesi wake kuyapanda na kuyatunza.

Mosi, anasema ukishaandaa shamba, chimba mashimo yenye kina cha urefu wa futi moja, kuenda chini.

“Upana, mimi huyapa kipenyo (diameter) cha sentimita 15,” aelezea Kirinyet.

Kulingana na ufafanuzi wake, nafasi kati ya mashimo huipa umbali wa mita moja, na laini za mashimo mita moja na nusu.

Mkulima huyo anasema mikarakara haina ugumu kupanda, akielezea kwamba huchanganya udongo na mbolea ya mifugo; ng’ombe, mbuzi na kuku, ikizingatiwa kuwa pia ni mfugaji.

“Baada ya upanzi, shughuli muhimu ni kuitunza kwa njia ya fatalaiza, mbolea na maji ya kutosha,” anasema.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasisitiza ufanisi katika kilimo cha matunda hauna siri, ila kuwa na chanzo cha maji ya kutosha.

“Kabla kuingilia kilimo cha matunda, hakikisha una chanzo cha maji ya kutosha. Isitoshe, kumbatia mfumo wa mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji,” anashauri Daniel Mwenda, mtaalamu.

Kulingana na mdau huyo, mataifa kama vile Israili na Misri, yameboresha kilimo cha matunda ilhali ni jangwa kwa sababu ya kukumbatia uvunaji maji.

Kando na matunzo kwa njia ya maji na mbolea, mikarakara inahitaji kusitiriwa kwa fito.

“Katika kilele cha fito, ziunganishe kwa nyaya. Mikarakara hutambaa na maumbile hayo huiwezesha kuzalisha kwa wingi na mazao bora,” asema mkulima Kirinyet.

Robert Kirinyet, mkulima wa matunda aina ya karakara Kaunti ya Bomet. Picha/ Sammy Waweru

Vile vile, ni muhimu kupogoa matawi (pruning), ili kupunguza ushindani wa lishe na kuruhusu miale ya jua kupenyeza.

Kulingana na Kirinyet, ekari moja inahitaji jumla ya fito 1, 400.

Mbali na hayo, muhimu pia ni palizi kuzuia kero ya kwekwe ambayo huchangia maenezi ya magonjwa na wadudu.

“Inapoanza kuchana maua na kutunda, wadudu aina ya vidukari ni waharibifu sana. Wasipodhibitiwa kwa dawa za wadudu, mkulima hatapata mavuno. Hula maua na matunda yanayojitokeza,” anaonya, akihimiza mkulima kuhusisha mtaalamu wa kilimo ili kushauriwa dawa bora na ambazo hazina athari kwa binadamu.

Magonjwa ya matunda pia hushuhudiwa.

Mwaka mmoja baada ya upanzi, mkulima huanza kuvuna matunda ya kwanza.

Kerinyet anaiambia Taifa Leo kwamba kwa sasa anavuna kati ya kilo 50 na 100 kila wiki, katika kipande cha shamba chenye ukubwa wa robo tatu.

“Mavuno huendelea kuongezeka kila juma,” anasema.

Ukiitunza vyema mikarakara utaivuna kati ya miaka mitano hadi minane. Soko la mazao yake ni mithili ya mahamri moto.

Shujaa, Lionesses kurejea nyumbani leo Jumamosi kutoka raga ya Dubai

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za taifa za raga ya wachezaji saba kila upande za Kenya maarufu kama Shujaa (wanaume) na Lionesses (wanawake) zinatarajiwa kurejea nyumbani Aprili 10 baada ya kukamilisha raga ya Emirates Invitational 7s mjini Dubai, Ijumaa.

Shujaa ya kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu ilipepeta majirani Uganda 36-5 na kukamata nafasi ya tano kutoka orodha ya mataifa manane yaliwania taji la wanaume.

Lionesses ya kocha Felix Oloo ilimaliza ya mwisho baada ya kuoshwa 43-0 na Japan katika mechi ya kuamua nambari tano na sita (mwisho).

Mashindano haya yalitanguliwa na mazoezi ya siku nne. Shujaa ilikamilisha mashindano ya kwanza ya Dubai yaliyoandaliwa Aprili 2-3 katika nafasi ya tatu nayo Lionesses ilivuta mkia.

Vijana wa Simiyu walianza mashindano ya pili ya Dubai kwa kuzaba Uganda 28-10, Canada 21-10 na Uhispania 17-14 katika mechi za Kundi Buluu mnamo Aprili 8.

Mambo yaliwaendea vibaya katika mchuano wao wa kwanza wa siku ya pili walipolimwa 15-12 na Chile katika robo-fainali.

“Inasikitisha jinsi tulivyocheza dhidi ya Chile kwa kufanya makosa madogomadogo na mengine yasiyofaa ambayo mwishowe tuliishia kujuta kwa sababu tuliteremka hadi shindano la Sahani,” alisema Simiyu.

Vijana wake walijinyanyua katika nusu-fainali ya Sahani dhidi ya Uhispania.

“Tuliweza kufanya vitu kadhaa sawa ilivyotakikana dhidi ya Uhispania vilivyotusaidia kuwakanyaga 27-15. Tutaendelea kujiimarisha kwa sababu tunatumia mashindano haya kujipima kwa ajili ya Raga za Dunia na Michezo ya Olimpiki baadaye mwaka huu,” nahodha Andrew Amonde aliongeza.

Katika fainali ya Sahani, Jacob Ojee, Alvin Otieno na Vincent Onyala walipachika mguso mmoja kila mmoja naye Johnstone Olindi akafunga miguso miwili. Tatu kati ya miguso hiyo sita iliandamana na mikwaju. Uganda, ambayo inanolewa na Mkenya Tolbert Onyango, ilipata mguso mmoja kupitia kwa Aaron Ofoywroth.

Lionesses ilipata mafunzo kadhaa ya kutia moyo. Oloo na nahodha Philadelphia Olando walipongeza wachezaji kwa kuimarika.

Mabingwa hao wa Afrika mwaka 2018 walionyesha kuimarika dhidi ya wazoefu wa Raga za Dunia Canada na Amerika walipopoteza 22-5 na 22-10, mtawalia.

“Tulisumbua miamba hao. Unapolinganisha ukubwa wa vichapo tulipokea mwezi Februari mjini Madrid na hivi vya Dubai utaona tumepiga hatua. Bado kuna kazi kubwa ya kufanywa, hasa tunavyoanzisha mipira. Tuko asilimia 60 na tunahitaji kuwa juu zaidi ya hapo kabla tuende shindano la Los Angeles mwezi June,” alisema Oloo.

Nahodha msaidizi Sheila Chajira aliumia Alhamisi na kushauriwa apumzike siku kadhaa kabla ya kurejea uwanjani. Matokeo yote ya Lionesses ya Dubai: Aprili 8 – Canada 22 Lionesses 5, Ufaransa 31 Lionesses 5, Japan 10 Lionesses 10; Aprili 9 – Lionesses 12 Brazil 15, Amerika 22 Lionesses 10, Japan 43 Lionesses 0.

CHOCHEO: Kukataa mchezo wa huba ni kuhatarisha ndoa – Washauri

Na BENSON MATHEKA

CIDY anajuta kumkaushia mumewe Zack kwa uroda alipokataa kumnunulia zawadi siku yake ya kuzaliwa.

Zack alivumilia kwa miezi miwili akitumia kila mbinu kumshawishi Cidy lakini akakataa kumtimizia haki yake ya tendo la ndoa kisha akaamua kutafuta huduma kwingine na kumpata Rose ambaye baada ya kuchepuka naye mara tatu, alimweleza alikuwa na mimba yake.

“Uhusiano wangu na Zack umeingia doa na sasa anataka kumuoa Rose. Makosa yalikuwa yangu. Kama singemnyima haki yake ya tendo la ndoa singekuwa katika hali hii,” asema Cidy.

Ndoa yao ni ya kitamaduni na kisheria, Zack anaruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja. Katika kisa sawa na cha Cidy, Kimani anasema kwamba mkewe alichepuka na mpenzi wake wa zamani baada ya kukosa kumchangamkia kitandani kwa miezi minne.

“Tulikosana nilipogundua kwamba alikuwa amechukua mkopo na kununua nyumba bila kunifahamisha. Japo sio vibaya kufanya hivyo, tuligombana na nikahama chumba cha kulala licha yake kutumia kila mbinu nirudi ikiwa ni pamoja na kuniomba msamaha na kunikabidhi stakabadhi zote za nyumba aliyonunua. Baadaye niligundua alikuwa akimchangamkia mpenzi wake wa zamani na nikajuta kwa tabia yangu,” asema Kimani.

Ingawa mkewe aliungama kwamba hakuwa amezini na jamaa huyo, Kimani alihisi kwamba tabia yake ilihatarisha ndoa yake na akatafuta ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu ambao waliwapatanisha.

Kulingana na Dick Ipetu, mshauri mwandamizi katika shirika la Abundant Love jijini Nairobi, wachumba huwa wanaweka uhusiano wao kwenye hatari wanapokaushiana uroda baada ya kutofautiana na kugombana.

“Ni kweli ugomvi huwa unavuruga uhusiano kati ya wanandoa lakini wanaponyimana haki ya tendo huwa wanaangamiza ndoa yao. Ni kawaida ya tofauti kuzuka na kufanya mtu kukosa hisia za mapenzi kwa mwenzake lakini ili kuokoa ndoa, suluhu inafaa kupatikana haraka kabla ya jahazi kuzama,” aeleza Ipetu. Hivi ndivyo Cidy alikosa kufanya na ndoa yake sasa iko mashakani.

Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema kwamba haki ya tendo la ndoa ni gundi inayounganisha wachumba na mtu hafai kumnyima mwenzake kumwadhibu wanapotofautiana.

“Inasukuma mtu kuwa na mipango ya kando na huu ndio ukweli na ikifikia hapo huwa kuna uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa na kusababisha majuto,” asema Ipetu.

Kulingana na Pasta Winnie Kibui wa shirika la First Love Restoration Center jijini Nairobi, kunyima mchumba wako haki ya tendo la ndoa bila sababu maalumu ni sawa na kujiondoa katika ndoa.

“Wakati ambao wanandoa hawafai kushiriki tendo la ndoa ni mmoja wao akiwa mgonjwa. Kuna wanandoa wanaoishi miji tofauti na kwa sababu wanajua siri hii wanasafiri muda mrefu kuhakikisha kuwa wanapeana haki yao ya ndoa. Ajabu ni kwamba unapata wanaoishi nyumba moja wananyimana kwa sababu ya mambo madogo wanayoweza kuepuka au kusuhuhisha,” asema Kibui.

Kulingana na wataalamu, wachumba wanaponyimana tendo la ndoa huwa wanatumbukiza wenzao kwa majaribu.

“Kwanza, unamtumbukiza mtu kwenye mateso ya kisaikolojia na kumweka katika majaribio. Akipata mtu wa kumchangamkia atapita naye na utakuwa umevuruga uhusiano wako,” asema.

Kulingana na Pasta Kibui, watu wakioana huwa ni kitu kimoja na kinachowaunganisha ni tendo la ndoa.

“Kama hakuna sababu ya kimazingira au maradhi, sioni sababu ya mtu kumnyima mpenzi wake haki ya ndoa. Ni sawa na kunyima mwili wako kwa kuwa mtu na mkewe ni kitu kimoja,” asema.

Hata hivyo, asema ili kufurahia tendo lazima kuwe na uhusiano mwema kati ya wachumba.

“Epukeni mizozo, eleweni kuwa ni kawaida kuwa na tofauti za kimaoni ambazo kamwe, narudia, kamwe, hazifai kufanya mtu amnyime mwenzake haki yake ya ndoa na ikizuka hali ambayo hamchangamkiani, tafuteni ushauri kutoka kwa wataalamu na viongozi wa kiroho,” asema.

Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, moja ya sababu za kuvunjika kwa ndoa ni kunyimana haki ya ndoa.

Mipango kuandaa Muturi kuwania urais 2022 yaiva

Na ALEX NJERU

YAMKINI juhudi zinaendelea za kuandaa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kuwa kigogo wa siasa za eneo la Mlima Kenya na hata kuwania Urais baadaye mwaka 2022.

Kutawazwa kwa Bw Muturi kama msemaji wa jamii za Mlima Kenya na wazee wa Kiama Kiama (Kikuyu), Nyangi Ndiririri (Embu), Ngome (Mbeere) na Njuri Ncheke (Meru na Tharaka) sasa kunamweka kama mwanasiasa mwenye mamlaka zaidi eneo la Mlima Kenya baada ya Rais Uhuru Kenyatta.

Ingawa mwanzoni kutawazwa kwake kuliibua nyufa za kisiasa mlimani, baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakimpinga awali sasa wamerejea katika kambi yake huku mikakati ya kisiasa ikiendelea kupangwa kuhakikisha anadhibiti eneo hilo kisiasa.

Japo Rais Kenyatta hajawahi kuzungumzia hadharani kutawazwa kwa Bw Muturi, wandani wake sasa wanamuunga mkono mbunge huyo wa zamani wa Siakago na hata kudai kwamba yeye ndiye kiongozi ambaye anapendelewa na Rais.

Baadhi ya wanasiasa nao wamekuwa wakimtembelea nyumbani kwake Kanyambora kimya kimya huku madiwani wa Tharaka Nithi wakawa kati ya wanasiasa ambao wameonyesha uaminifu wao kwa Spika Muturi.

Mnamo Alhamisi, madiwani hao wakiongozwa na Spika David Mbaya na Kiongozi wa wengi Peterson Mwirigi walimtembelea Bw Muturi nyumbani kwake na kumpa mbuzi wawili wakubwa ishara kuwa wanakubali uongozi wake.

Bw Mwirigi alisema kiongozi wa hadhi eneo hilo baada ya Rais Kenyatta eneo la Mlima Kenya, Bw Muturi anafaa kwa wadhifa wa urais kwa kuwa alihudumu kama mbunge kwa mihula miwili na pia spika kwa muda huo.

Kiongozi wa wachache Wilson Nyaga naye alisema ni wakati wa kiongozi kutoka Mlima Kenya Mashariki kutoa kiongozi mpya wa eneo hilo. Kaunti za Tharaka-Nithi, Embu na Meru ndizo zinapatikana Mlima Kenya Mashariki.

“Kwa zaidi ya miaka 60 uongozi wa eneo hili umetokea Magharibi mwa mlima huu na sasa ni wakati wa kiongozi kutokea Mlima Kenya Mashariki,” akasema Bw Nyaga.

Diwani maalum Millicent Mugana naye amewataka wakazi wote wa kaunti za Mlima Kenya wamuunge mkono Bw Muturi ili ashinde kiti cha Urais 2022.

Baadhi ya madiwani wa kaunti ya Tharaka-Nithi ambao walikuwa wakimuunga mkono Naibu Rais Dkt William Ruto nao wamevuka na sasa wapo mrengo wa Bw Muturi.

Katika kaunti nzima ya Tharaka Nithi, ni Seneta Kithure Kindiki amesalia kambi ya Dkt Ruto.

Taifa Leo imebaini kwamba, madiwani kutoka Kaunti ya Meru wanapanga kumtembelea Bw Muturi nyumbani kwake kueleza uaminifu wao na kumpigia upato 2022.

Bw Muturi mwenyewe amewashukuru madiwani hao kwa kuonyesha imani katika uongozi wake na akawataka wahakikishe wanawahudumia raia vyema na waungane pamoja ili kuzungumze kwa sauti moja katika siasa za kitaifa.

“Tumakinikie umoja wetu na kuwahudumia vyema waliotuchagua,” akasema Bw Muturi.

Kando na wanasiasa, Bw Muturi amekuwa akishauriana na viongozi wa kijamii, wale wa dini na wafanyabiashara ili kujitafutia umaarufu.

Mikopo: Wakenya wamchangia mwanaharakati

Na HILLARY KIMUYU

WAKENYA Ijumaa walimchangia mwanaharakati Mutemi wa Kiama dhamana ya Sh500,000.

Mwanaharakati huyo alikuwa ameachiliwa kwa dhamana na mahakama ya Nairobi baada ya hakimu kukataa ombi la upande wa mashtaka la kumzuilia kwa muda wa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi.

Alishtakiwa kwa makosa ya kukaidi sheria za mtandao kuhusiana na kampeni ya Wakenya kwa IMF wakiitaka isikopeshe Kenya tena.

Kundi linalojiita Muungano wa Watetezi mtandaoni ndilo lilitoa wito kwa Wakenya waungane kumchangia Bw Kiama dhamana hiyo.

“Nawashukuru sana Wakenya. Muungano wa watetezi umehakikisha kuwa mwanaharakati huyo anaachiliwa huru. Lazima kama Wakenya tusimame imara na kuhakikisha tunapata haki na kulinda uhuru wa kujieleza,” akasema Bw Kiama.

Mwanaharakati huyo alishtakiwa kwa kuwa na mabango mawili yaliyoonya IMF dhidi ya kutoa mkopo kwa Wakenya hasa kwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Korti pia ilimuonya Bw Mutemi dhidi ya kutumia akaunti zake za mitandaoni na awe akipiga ripoti kwa afisa wa uchunguzi kila siku hadi wakati kesi hiyo itakapotajwa Aprili 20, 2021.

“Hii notisi inaonya ulimwengu kwamba mtu ambaye picha yake na majina yake yapo kwenye bango hili haruhusiwi kushiriki biashara zozote kwa niaba ya raia wa Jamhuri ya Kenya.

“Taifa na vizazi vijavyo havitawajibikia kutokana na athari mbaya ya mikopo aliyochukua yeye,” ikasema notisi hiyo iliyomtia Bw Kiama matatani.

UMBEA: Hakuna mpenzi mzuri au mbaya inategemea tu ikiwa mnafaana

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA kawaida dunia sio mbaya, isipokuwa wanadamu ndio wabaya.

Na kwa dhana hii wapo akina dada ambao daima huamini kwamba hakuna mwanaume mzuri. Kwamba wanaume wote ni wabaya, tabia zao hazifai na tena mienendo na dhamira zao hufanana.

Kwa upande mmoja nitakubaliana nao, lakini pia kwa upande mwingine sitakubaliana nao.

Hakuna mtu anayezaliwa na ubaya, bali mazingira na maisha tunayokulia huchangia kwa kiasi kikubwa kutathmini maisha yetu ya baadaye tunapoingia katika uhusiano na hatimaye ndoa.

Wengi wetu tunapokua huwa tunakutana na mambo mengi. Yapo mazuri na mabaya pia. Na kawaida ya binadamu ni kukumbuka yale ambayo sio mazuri kwa urahisi zaidi kuliko yale ambayo ni mazuri.

Miongoni mwa hoja ambazo zinawakosesha raha baadhi ya wanawake, furaha na amani mioyoni mwao, hasa katika upande wa mapenzi ni kuamini kuwa, kuna mwanamke mzuri na mbaya.

Wapo baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakijishuku kuwa inawezekana dhana hiyo ndiyo chanzo cha wao kuachwa na wanaume wanaokuwa nao.

Inawezekana pia kuna mwanamke amewahi kusikia kwa mtu au amekuwa akisimangwa na mpenzi wake kuwa yeye ni mbaya wa sura na maumbile hivyo kumkosesha amani maishani mwake. Na wapo wale ambao wamekuwa wakisimangwa kwamba wana roho mbaya zilizotawaliwa na kutu.

Vivyo hivyo, kwa wanaume, wapo wanaohangaika huku na kule kutaka apate mwanamke mzuri wa maumbile huku akiamini labda aliye naye ni wa kawaida au si mzuri.

Hii ni dhana ambayo imeziteka fikra za wengi, kwa kuamini kuwa inawezekana aliyenaye si mwanaume au mwanamke mzuri.

Labda msomaji hujui hii, kuwa, hakuna mwanaume au mwanamke mzuri au mbaya. Isipokuwa mwanaume au mwanamke mzuri ni yule ambaye mnaendana, mnaelewana, mnaridhiana na mnaridhishana mnapokuwa faragha.

Ninasema hivyo kwa sababu uzuri ambao unasemwa na kufikiriwa na walio wengi ni uzuri usioweza kusikika, kuhisika, kushikika au kuhadithika.

Mapenzi ni hisia ambayo moyo huitaka kutoka kwa mwanamke au mwanaume husika. Ndiyo maana unaweza kuwa na mpenzi, ukaachana naye kwa mbwembwe nyingi kwa kuamini kuwa si mwanamke au mwanaume anayestahili kuishi na wewe wala mpenzi mwingine yeyote kwa sababu hana uzuri ambao uliufikiria, lakini mwisho wa siku wewe ukaangukia kisogo na mwenzako akafanikiwa kuwa na maisha mazuri ya mapenzi kuliko wewe.

Kuna wakati mwingine unaweza kumuona mpenzi uliyenaye ni mbaya, lakini wakati huohuo kuna mwenzako pale ndiyo kwenye pumziko la moyo wake. Yuko tayari kufanya jambo lolote ilimradi asimuache aende au awe naye.

Wakati mwingine unaweza kuwa unagombana na mpenzi wako kwa sababu tu, hamshabihiani kwa baadhi ya mambo ikiwemo kutokuridhishana.

Inawezekana wewe ni mwanamke ambaye unamuona mwanaume wako kama siyo mzuri kwa sababu hakuridhishi, vivyo hivyo mwanaume unaweza kuona mke uliyenaye siyo sahihi kwa sababu hujaridhika na jinsi alivyo.

Ukubali au ukatae, lakini ukweli ni kwamba, hakuna mwanamke mbaya, wanawake wote wako sawa isipokuwa inategemea na nini ambacho mwanaume amekipenda na kukielewa zaidi kutoka kwa mwanamke.

Ukitaka kuamini hilo, kuna mwanaume mwingine anaonekana ni mtanashati, lakini mpenzi au mke wake ni mwenye muonekano wa kawaida tu. Lakini ukweli ni kwamba mwanaume huyo inawezekana ameridhika na hali aliyonayo mwenza wake.

Ninachotaka kusisitiza ni kwamba kabla hujamhukumu mwenzako kwamba ni mbaya, ujiangalie pia mtazamo wako kwa huyo mwenzako. Huenda tatizo liko kwako pia na wala sio huyo unayedhani ana tatizo.

sizarinah@gmail.com 

MWANAMUME KAMILI: Usijitie zuzu, tia bidii kujua yanayomhusu mke wako

Na DKT CHARLES OBENE

MNAOJITUMA kufa kupona wenzenu kuwapa nafsi na moyo vilevile, sikateni tamaa wala kushika tama na kusononeka kwa tabia za wafidhuli wanaume wa leo.

Baadhi ya wanaume wa leo wanafanya dharau kwa kutojua tu. Ipo siku wanaume majefule watakuja tambua utamu wa mapera msimu wa maembe ujapo kwisha. Hakuna haja ya michirizi ya chozi wala kamba shingoni kufia mahabani!

Kutojua jambo sio ujinga; ujinga ni kukataa kujifunza! Kuna baadhi ya wanaume wenye akili za nanga hata kujifunza ni kazi. Uzito huu wa akili unatokana na tabia za wanaume wa leo kutopenda kujuzwa ya hekima. Wanajifanya kujua kila kitu. Hawaambiliki hawasemezeki!

Hakuna azaliwaye mjuvi wa mambo na vijimambo duniani. Hakuna msomi kwa mambo ya nyumbani ama chumbani. Sote ni wanafunzi tunaopata funzo moja baadha ya nyingine kila kukicha. Wanaume kwa wanawake wamejanjarukia mengi kuyajulia ukubwani. Aidha kutokana na kuelimishwa, kujuzwa, kunong’onezewa ama kuuliza tu hasa akina sisi tusiojua kuficha fundo moyoni. Hivyo basi sina shaka kwamba mwanamume kutojua jambo ni mwenyewe kupenda. Isitoshe, mwanamume kukataa kuelimika ni kwa raha zake.

Kuna mengi ambayo wanaume wa leo wameyafumbia macho na kujifanya hawajui! Kweli sijaelewa jinsi mwanamume anavyoweza kupachika mimba na mwishowe kukataa kuwajibikia malezi ya mwanawe akitilia shaka asili na fasili ya mtoto yule. Vipi mtu kutilia shaka uzao wa mtoto katika dunia hii ya teknohama?

Huwa wapi hawa wanaume wanaoibuka na kuwakana watoto wakijua wazi walifanya mambo ya wakubwa? Ama ndio nyie mnaojua kupanda ila kuvuna. Ndio wao hao wanaopanda kitandani na madaftari ama majadala kuyasoma wakati watu wazima wanakuwa shughulini.

Ndio wao hao wanaopokea simu na kujadili biashara kwa lisali moja tena usiku wa manane wakiwa juu ya mnara. Ndio wao hao wanaokesha mitandaoni ya kijamii ilhali wanawajibikia shughuli za watu wazima.

Jamani zindukeni nyie wenye kuwafanyia wenzenu dhihaka kama hizo!

Inachukiza mwisho wa chuki mtu kukufanyia dharau sampuli ile. Mwenzio kajisabilia kwako mwili na nafsi, fikra na akili, pumzi na uhai wala huoni haja kumpa hata tone la heshima? Madaftari na majalada ya kusomwa usiku wa manane ndio heshima? Ndio heshima anayostahili mke kwa kukuchagua wewe na kukufanya mtu mbele ya watu? Nyie wanaume wa leo mna nini? Afadhali mwenye kukupa talaka kuliko mwanamume apandaye kitandani na rununu na kujadili biashara wakati mkewe anasubiri kupanda wanakopanda waliojazibika kimahaba! Afadhali mtu kusalia peke yake maishani kama mwezi kuliko kudunishwa namna ile.

Heri kuzama baharini na kuliwa na samaki kuliko dharau sampuli ile. Komeni nyie wanaume wenye maudhi na dharau hizi! Nani kawaambia wanawake hawana biashara ama hamu ya kusoma majalada na madaftari kitandani? Hebu kivalie kiatu cha mwenzio kabla kumdunisha namna ile. Tabia hizi hazina nafasi katika meza ya watu wanaothamini wenzao.

Tulivyo wachapa kazi, baadhi yetu tunasingizia shughuli aina ainati kama sababu ya kupitwa na mengi ya chumbani na vilevile nyumbani. Ukweli ni kwamba baadhi yetu ni wanaume limbukeni tusiopenda kujituma kimaisha na kujua mambo yanayohusu mke. Ndio maana wanaume wa leo hawachelei kukana watoto kama kwamba hawakuhusika walivyohimilika mama yao.

La ajabu ni kwamba hata kuuliza siku za hedhi tunaona kama kazi ya sulubu. Ndio maana wanawake wanalalama mno kwenye nyumba na vyumba vya watu wazima! Afadhali hata beberu maana anazo akili za kutoa ishara za kamba kukatikia malishoni! Mambo ya kuelimishana polepole kitandani ndio hayo tunayatolea macho.

Ukali wa baadhi ya wanaume wa leo unatokana hasa na akili zao butu. Kuna mambo ya chumbani wasiojua kaka zetu ila hawataki kuuliza! Mwanamume kamili ni akili. Misuli tuipeleke shambani au ukulini! Tatizo ni kwamba ni kwamba mwanamume wa leo anaona haya hata kumweleza mpenzi au mkewe kwamba hana pesa! Wachache mno wanaweza kukiri kwamba hali si hali mfukoni.

Atwoli apewa miaka mingine mitano kutetea wafanyakazi

Na VICTOR RABALLA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, jana alichaguliwa tena bila kupingwa kuongoza chama hicho kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Bw Atwoli aliibuka mshindi baada ya mpinzani wake mkuu, Bw Seth Panyako, kuzuiwa kushiriki kwa kutokuwa mwanachama wa Cotu.

Bw Panyako anahudumu kama Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi Kenya (KNUN).

Bw Atwoli amekuwa kwenye nafasi hiyo tangu mwaka 2001 na hajawahi kushindwa kwenye uchaguzi wowote.

Wanachama wote 34 wa kamati kuu simamizi vile vile walichaguliwa bila kupingwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Masuala ya Wafanyakazi ya Tom Mboya, jijini Kisumu.

Kwenye hotuba yake, Bw Atwoli aliwashukuru wajumbe 250 walioshiriki kwa kuonyesha imani kwenye uongozi wake.

“Kufuatia ushindi huo, nitaendelea kujitolea kupigania haki za wafanyakazi bila kuogopa vitisho vyovyote,” akasema.

Aliwaambia washiriki hao daima kutoogopa kusimama na ukweli.

Aliwashauri kukataa aina yoyote ya dhuluma ambayo huenda wakakumbana nayo.

“Naahidi kuwatumikia kwa nguvu zangu zote. Sitawasaliti kutokana na imani ambayo mmenionyesha,” akasema kwenye ujumbe alioandika katika Twitter.

Maafisa 12 wa kamati kuu ya chama hicho ni Mabw Rajab Mwodi (Mwenyekiti), Joel Chebii (Naibu Mwenyekiti wa Kwanza), Francis Murage (Naibu Mwenyekiti wa Pili), Benson Okwaro (Naibu Katibu Mkuu), Earnest Nadome (Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza) na Bi Carolyn Rutto (Naibu Katibu Mkuu wa Pili).

Wengine ni Bi Rebecca Nyathogora (Mwekahazina Mkuu), Bw Washington Adongo (Naibu Mwekahazina), Bw Francis Wangara (Mdhamini wa kwanza) na Bw Joseph Onchonga (Mdhamini wa pili).

Wanachama 22 wa bodi kuu ya chama pia walichaguliwa kwenye shughuli hiyo ambayo iliendeshwa kwa njia ya kawaida na ile ya mtandao.

FATAKI: Ajabu jamii kutilia shaka werevu wa binti kwa kuangalia maumbile

Na PAULINE ONGAJI

MAJUMA kadhaa yaliyopita kulikuwa na binti fulani aliyetuzwa tuzo ya uanahabari wa sayansi ambapo hadithi yake iliangaziwa na kuchapishwa kwenye jukwaa la mtandao wa gazeti analofanyia kazi.

Makala hayo yaliandamana na picha moja mufti ya binti huyo ambapo ilionyesha uzuri wake sio tu kisura, bali kimaumbo.

Picha hiyo ilionyesha sehemu yote ya mwili wake kutoka utosini hadi miguuni, ikimulika umbo lake la chupa.

Lakini cha kushangaza ni kwamba pindi makala hayo yalipochapishwa, badala ya watu kumpongeza kwa kuafikia hayo, cheche za matusi ndizo zilizotawala kwenye sehemu ya maoni, chini ya chapisho hilo.

Kulingana na asilimia kubwa ya waliotoa maoni hayo, maafikio ya binti huyo hayakutokana na bidii yake, ila yalichochewa na mwonekano wake.

Aidha, kauli ya wengi ilikuwa kwamba hakuna jinsi binti mrembo anavyoweza kupokea tuzo za haiba ya juu hivyo, ila tu kwa kuteremshia mtu au watu fulani bendera.

Ni sawa na makala ya binti fulani wa chuo kikuu kimoja aliyetambuliwa kama mwanafunzi wa kipekee kupata alama za juu zaidi katika taasisi hiyo. Katika habari hizo, picha iliyotumika ilimuonyesha binti huyo akiwa amevalia mavazi ya kupendeza na kujipodoa kweli kweli.

Cha kushangaza ni kwamba maoni ya wengi hapo yalikuwa kuhusu mwonekano wake na wala sio maafikio yake kimasomo.

Ni jambo la kustaajabisha na kuhuzunisha, lakini huo ndio uhalisi wa jamii yetu. Tunaishi katika jamii ambapo uerevu wa mwanamke unapimwa kuambatana na mwonekao wake wa nje, yaani ikiwa una kichwa kizuri juu ya mabega yako basi haupaswi kupendeza, na ikiwa wapendeza, basi sharti kichwa chako kiwe tupu.

Nakumbuka wakati mmoja nikizungumzia kuhusu mjadala wa wanawake wanaojipodoa na wasiotumia vipodozi, ambapo nilisema kwamba hayo ni mpambo ya nje na kamwe hayaathiri kilichoko kichwani mwako. Kujipodoa au kutojipodoa hakubadilishi hali ya ubongo wako.

Cha msingi ni kwamba suala la kuwahukumu hasa mabinti kupitia mavazi au mwonekano wa nje, inathibitisha tabia ya jamii yetu ya kutosoma. Yaani, inadhihirisha uvivu wetu wa kuwa na mazoea ya kuhukumu kitabu kwa jalada lake, badala ya kupitia yaliyomo.

TAHARIRI: Chanjo inatolewa sasa michezo irudi

KITENGO CHA UHARIRI

HATIMAYE, zoezi la kuchanja wanasoka nchini dhidi ya virusi vya corona linang’oa nanga rasmi hii leo katika uwanja wa Kasarani, kukiwa na matumaini tele kwamba mechi za kandanda zitarejelewa tena hivi karibuni.

Takriban dozi 700 zitatolewa kwa wachezaji na maafisa wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwanza, kabla baadaye kupewa wanasoka wa timu za wanawake, Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) na ligi za chini.

Zoezi la leo linafuatia lile la kuwachanja wanamichezo wa timu za taifa zitakazowakilisha Kenya katika michezo ya Olimpiki na mingine ya kimataifa mwaka huu, lililoanza Alhamisi.

Katika shughuli hii wizara za Michezo na Afya zinalenga watu 3,500 katika timu hizo; kuanzia wanamichezo, makocha, maafisa wa michezo na mtu yeyote yule anayehusika moja kwa moja na wanamichezo kote nchini.

Zoezi hili la utoaji chanjo pia limeshuhudia maafisa wa mbio za magari za Safari Rally wakipokea dozi hiyo muhimu, wanapojiandaa kwa mashindano ya kimataifa baadaye mwezi Juni.

Rais Uhuru Kenyatta alipositisha tena michezo kufuatia wimbi la tatu la corona, aliweka kipaumbele utoaji chanjo kama kigezo muhimu katika kuondoa marufuku hiyo. Hii ikitekelezwa sambamba na masharti yale mengine ya kuvaa maski wakati wote ukiwa nje katika maeneo ya umma, kunawa mikono kwa maji na sabuni au kutumia sanitaiza, na kuepuka mikusanyiko.

Pilkapilka hizi zote za utoaji chanjo ni habari njema, na dhihirisho la jinsi wizara na mashirikisho ya michezo zinajitahidi kuhakikisha uhondo wa mechi na mashindano unarejelea tena viwanjani.

Fani ya michezo ni sekta muhimu sana nchini. Kando na uhondo huo kwa maelfu ya mashabiki, kunao watu wengi tu wanaoenda viwanjani kwa madhumuni ya kufanya mazoezi ya mwili.

Kubwa zaidi, sekta hii ni kitega uchumi kwa maelfu ya watu walioajiriwa humo moja kwa moja au wanahusika kwa njia nyingine. Ujira huu wote umekwama kwa sasa sababu ya corona huku maelfu ya wanamichezo wakikosa la kufanya nyumbani.

Hivyo, tunasihi wizara za michezo na afya pamoja na mashirikisho yote ya michezo kuvalia njuga suala hili la chanjo ili kuhakikisha wanamichezo, maafisa na kila mhusika anapokea kinga hii muhimu.

MUTUA: Napongeza na kushabikia Tanzania chini ya Suluhu

Na DOUGLAS MUTUA

MMOJA kati ya Wakenya waliomshabikia sana marehemu rais wa Tanzania, John Magufuli, ni mwanahabari mwenzangu aliyedai Rais Samia Suluhu Hassan, atafuata nyayo za mtangulizi wake.

Alitumia uteuzi wa Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango, kama ushahidi kwamba genge la Magufuli lingali linashika usukani wa nchi.

Si kweli! Mambo yamebadilika tayari. Vyombo vya habari vilivyokandamizwa na kufungiwa na Magufuli viko huru sasa, sikwambii hata Corona inashughulikiwa kisayansi!

Tanzania ya Magufuli ilionekana kufuata nyayo za Ethiopia, enzi ya marehemu waziri mkuu Meles Zenawi, aliyevinyanyasa vyombo vya habari.

Labda Rais Hassan amesikia kilio cha kiongozi wa upinzani, Bw Tundu Lissu, aliyewahi kunukuliwa akieleza jinsi uchumi wa Tanzania ulivyokua enzi ya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na uhuru wa kujieleza na kuchangamana.

Mswahili husema mtenda kazi asishe ni sawa na asiyetenda; Bi Hassan anapaswa kuwaachia huru kikamilifu wanahabari na Watanzania kwa ujumla.

Hili ni muhimu hasa ikizingatiwa Rais mwenyewe aliviagiza vyombo vilivyofungiwa vifuate sheria za nchi.

Je, vitazifuataje sheria vilizodaiwa kuvunja kabla ya kufungiwa bila kujibana kiusemi au kujiachia na kuhatarisha kufungiwa tena?

Pa kuanzia ni Rais kuagiza vipengee kandamizi viondolewe kabisa kwenye sheria za nchi ili asije nduli mwingine kama Magufuli asizuke kavitumia kuirejesha nchi Misri.

Watanzania wana jukumu la kutekeleza katika upatikanaji wa uhuru wa wanahabari na wa kujieleza.

Wanapaswa kuishinikiza serikali ifanye mabadiliko ili matamanio yao yawekwe kwenye sheria za nchi, wasiketi kitako na kuamini serikali itawafanyia hisani.

Wanafaa kujua serikali hiyo tu iliyowapa uhuru inaweza kuutwaa kwani hakuna sheria zinazoizuia kufanya hivyo.

Uhusiano kati ya watawala wa nchi na vyombo vya habari tangu hapo ni wa kimapambano, mmoja asipepese jicho kwani serikali haina hulka ya kutenda hisani.

Kila wakati serikali inapotaka kufanya mambo yasiyofaa, wahanga wa kwanza ni wanahabari kwa kuwa wako chonjo daima na hawasiti kufichua maovu yakitokea.

Hata Bi Hassan mwenyewe akitaka kufanya kitu, mfano kutunga sera zisizo maarufu, watu wa kwanza kunyamazisha watakuwa wanahabari. Hisani yake ni ya muda.

Kwamba Rais huyo ana ukakamavu wa kukubali ushauri wa kisayansi kuhusu jinsi ya kukabiliana na Corona ni ithibati ya kujitenga na u-Magufuli.

Kuwaongoza Watanzania kuachana na gangaganga za mitishamba alizosifia si haba marehemu Magufuli ni hatua ya kijasiri inayoweza tu kuchukuliwa na anayejiamini.

Dunia inatazama na inapendezwa na uamuzi huo; hivi karibuni utasikia mataifa tajiri yakitua Tanzania na misaada ya chanjo na dawa. Hili litawezekana kwa urahisi kwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bi Liberata Mulamula, ameagizwa airejeshee Tanzania mahusiano mema.

Kama Mkenya, natarajia Bi Mulamula aimarishe uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ili nikienda zangu Dar es Salaam na Zanzibar nisihisi kama nalazimisha undugu.

mutua_muema@yahoo.com

KAMAU: Wajibu wa serikali kuhakikishia wanahabari usalama

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Aprili 10, 2020, dunia nzima iliamkia habari za kusikitisha kuhusu kifo cha msomi na mwanahabari maarufu, Prof Ken Walibora.

Prof Walibora alikuwa ametoweka kwa siku kadhaa, ndipo shughuli za kumtafuta alikokuwa zikaanza.

Juhudi za kubaini kitendawili hicho ziliishia katika mochari ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), ambako mwili wake ulipatikana.

Licha ya kuenziwa na wengi kwa mchango mkubwa aliotoa katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili na mawanda mengine ya kiusomi, kifo cha Prof Walibora kimebaki fumbo hadi sasa.

Hakuna aliyekamatwa wala kufunguliwa mashtaka, licha ya ahadi ya serikali kusaka na kuadhibu waliohusika kwenye mauaji hayo ya kikatili.

Inasikitisha kuwa wakati maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha Prof Walibora yanaendelea, tasnia ya uanahabari nchini inaomboleza tena mauaji ya kikatili ya mwanahabari mwingine.

Bi Betty Barasa, aliyehudumu kama mhariri wa video katika shirika la habari la KBC, aliuawa kikatili na watu wasiojulikana nyumbani kwake katika eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado, Jumatano usiku wakati akirejea nyumbani kutoka kazini.

Kulingana na taarifa za polisi, marehemu aliuawa na watu hao baada yao kukosa pesa walizokuwa wakitafuta nyumbani kwake.

Kama kawaida, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) imeahidi kufanya kila iwezalo kuhakikisha waliohusika kwenye ukatili huo wamebainika na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mauaji ya Bi Barasa yanatokea wiki mbili tu baada ya mauaji ya mwanahabari mwenzake, Bi Jennifer Wambua, aliyehudumu kama afisa wa mawasiliano katika makao makuu ya Wizara ya Ardhi, jijini Nairobi.

Bi Wambua alipatikana ameuawa kikatili katika msitu wa Ngong, Kajiado, baada ya kutoweka kwa siku kadhaa.

Bila shaka, hivi ni visa vinavyoonyesha kuwa maisha ya wanahabari si salama hata kidogo nchini.

Maisha yao yamegeuka kuwa ya roho mkononi. Wanaishi kwa hofu na mashaka kwamba, huenda wakaandamwa na mahasimu wao kutokana na majukumu wanayotekeleza katika jamii.

Maswali yanaibuka: Ni lini serikali itawahakikishia usalama wanahabari?

Tangu 2013, serikali ya Jubilee imekuwa ikiingilia uhuru wa wanahabari kiasi cha kufananisha majukumu yao na “uenezaji porojo tu.”

Katika nchi zilizostawi kidemokrasia, vyombo vya habari ni miongoni mwa taasisi zinazoheshimika sana na jamii. Katiba ya Kenya i wazi pia kuhusu haki za wanahabari.

Wanahabari si maadui wa raia. Si maadui wa nchi. Ni wazalendo wanaopaswa kulindwa kwa kila hali.

akamau@ke.nationmedia.com

Mumewe Malkia wa Uingereza aaga dunia

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MUME wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza , Prince Philip, babake Prince Charles, na kiongozi wa familia ya ufalme ya Uingereza, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 99.

Ikulu ya Buckingham ilitangaza kwamba, alifariki majira ya alfajiri. Philip alikuwa amelazwa hospitali mara kadhaa akiugua maradhi tofauti ya hivi punde ikiwa Februari.

Alifariki huku Ikulu ya Buckingham ikikumbwa na mzozo kuhusu mahojiano ambayo mjukuu wake Prince Harry na mkewe, Meghan, walifanya na Opray Winfrey mnamo Machi 7 na kufichua ukatili na ubaguzi wa rangi katika wanachama wa familia ya kifalme. Wadhifa wa Philip katika familia ya kifalme ulikuwa umegubikwa na Malkia ambaye ana nguvu zaidi.

Alikuwa akiandamana na Malkia katika ziara zake ulimwenguni na hafla za kitaifa. Mnamo 2017, akiwa na umri wa miaka 95, alitangaza kustaafu kwake kutoka majukumu ya umma.

Hata hivyo, hakutoweka kabisa katika macho ya umma. Mnamo Mei 2018, alihudhuria harusi ya Prince Harry na Meghan Markle akipungia watu mikono akiwa kwenye gari la kifalme pamoja na Malkia Elizabeth.

Katika maisha yake ya umma, Philip alikuwa akivalia magwanda ya kijeshi. Alikuwa mpwa wa kiongozi wa vita vya pili vya dunia Lord Mountbatten.

Kwenye taarifa, Ikulu ya Buckingham ilisema kwamba alifariki akiwa katika kasiri na kwamba itatoa matangazo zaidi.

“Familia ya kifalme inaungana na watu wote ulimwenguni kuomboleza kwa msiba huu,” alisema Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson. Akizungumza akiwa ofisi yake ya Downing Street, Waziri Mkuu alisema: “Alisaidia kuongoza familia ya kifalme kubaki asasi muhimu na furaha ya maisha ya kitaifa.”

Bw Johnson alisema alipokea habari za kifo cha Philip kwa huzuni kubwa.

“Philip alipendwa na vizazi hapa Uingereza kote katika Jumuiya ya Madola na kote ulimwenguni,” alisema.

Habari za kifo chake zilishtua watu wakaanza kutiririka hadi kasri la Windsor Castle.

Wakazi, wazee kwa vijana, waliacha maua katika lango la kasiri. Waziri wa kwanza wa Scotland, Nicola Sturgeon alisema alihuzunishwa na kifo cha Prince Philip.

Aliandika kwenye Twitter: “Ninatuma rambirambi zangu binafsi na za serikali ya Scotland kwa Malkia na familia yake.”

Kiongozi wa chama cha Labour Sir Keir Starmer alisema kwamba Uingereza imepoteza mtumishi wa kutajika wa umma na kwamba atakumbukwa kwa kujitolea kwake kwa Malkia.

Ubakaji: Mahakama yanyima 2 dhamana

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu aliyeshtakiwa pamoja na mwanamume anayedaiwa huwabaka wasichana wa vyuo vikuu, wamenyimwa dhamana na mahakama ya Kibera, Nairobi.

Hakimu Mwandamizi, Bi Esther Boke alisema Faith Washiali Bwibo na Abdirizak Adan Abdullahi ni hatari kwa usalama wa walalamishi, na itabidi wazuiliwe gerezani hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Bi Boke alikubaliana na kiongozi wa mashtaka Bw Allan Mogere kuwa Abdirizak, anayemiliki bastola atavuruga haki kwa kutoa vitisho kwa mashahidi wanaotazamiwa kufika kortini kuelezea kufafanua madai yao.

Hakimu alisema washtakiwa hao wawili watapewa fursa siku za usoni kuwasilisha upya ombi lao la kuachiliwa kwa dhamana “baada ya mashahidi wakuu kufika kortini kuelezea kilichojiri.”

“Hii mahakama haiwezi kufunga macho na masikio isisikie kilio cha walalamishi ambao wameelezea hofu kwamba wametishwa na kupata kichapo cha nguruwe walipokataa kuitikia matakwa ya mshtakiwa (Abdirizak),” alisema hakimu.

Bi Boke pia alisema alimsikiza baba ya mmoja wa walalamishi ambaye ni wakili mwenye tajriba ya juu aliposema “naumwa sana na kitendo hiki cha mshtakiwa wa kwanza kumbaka binti yangu na kumtupa jangwani aliwe na fisi. Mshtakiwa huyu hana utu hata!”

Hakimu alisema upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa kutosha kwamba washtakiwa watavuruga haki na “hata kuwatishia maisha walalamishi.”

Akasema, “Ili haki ionekane ikitendeka basi washtakiwa hawa watasalia gerezani hadi upande wa mashtaka uwasilishe ushahidi.”

Hakimu aliamuru kesi itajwe tena Aprili 20, 2021.

Hakimu alielezwa kuwa Abdirizak anaishi katika mtaa wa maafisa wakuu wa Jeshi (KDF).

Korti ilielezwa ni vigumu walalamishi na polisi kuingia mtaani humo kwa vile uko chini ya ulinzi mkali masaa 24.

Mahakama ilielezwa Abdrizak, “yuko na ashiki ya hali ya juu na hamu iliyopitiliza na kuthubutu kuwapepeta wasichana huku amewashikia bastola vichwani.”

Bw Mogere alipinga vikali mshukiwa huyo kuachiliwa kwa dhamana akisema “ni hatari kwa usalama wa kitaifa na pia kwa wasichana wa vyuo vikuu na wale walio balehe.”

Korti pia iliombwa imzuilie mshtakiwa huyo kwa hofu ya kuwachafua wasichana wenghine waliopo likizoni baada ya shule kufungwa.

Wakati huo huo, Bw Mogere alisema ingawa mshtakiwa anamiliki bastola polisi bado hawajafanikiwa kuipata.

“Abdullahi huyu hana utu. Alimbaka mteja wangu katika mtaa wa Mugoya ulioko eneo la South C kaunti ya Nairobi. Pia akimtumia Faith Washiali Bwibo, alimsaliti na kumpeleka mlalamishi tena eneo duni kaunti ndogo ya Naivasha, ambapo alimtupa kwenye jangwa usiku aliwe na wanyama mwitu baada ya kukataa dhuluma zake za kimapenzi.” wakili anayemwakilisha mwathiriwa, Bi Amazon Koech alieleza mahakama.

TANZIA: Mume wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza afariki

MASHIRIKA na SAMMY WAWERU

MUME wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince Philip ameaga dunia Ijumaa akiwa na umri wa miaka 99.

Tangazo hilo limetolewa na Kasri la Buckingham.

“Ni kwa masikitiko makubwa Malkia ametangaza kifo cha mume wake, Prince Philip,” inaeleza taarifa hiyo iliyochapishwa katika akaunti ya Twitter ya Kasri hilo.

Ikaongeza taarifa: “Alifariki kwa amani asubuhi ya leo (Ijumaa), Windsor Castle. Matangazo zaidi yatatolewa baadaye,” Kasri la Buckingham limesema.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ametuma salamu zake za pole kwa familia ya Malkia Elizabeth II, akisema amepokea habari hizo kwa mshangao na huzuni.

“Alikuwa mshirika wa kifalme aliyehudumu kwa muda mrefu. Ni mmoja wa walioshiriki Vita vya Pili vya Dunia na alitajwa kuwa Shujaa. Prince Philip alisaidia kuongoza familia ya Kifalme na Ufalme ili iweze kuwa taasisi muhimu,” akasema Waziri Mkuu Boris.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika risala zake za rambirambi amemfariji Malkia Elizabeth II, Familia ya Kifalme, Waziri Mkuu Boris Johnson na raia wa Uingereza.

Rais Kenyatta amesema Philip amekuwa nguzo ya umoja ulimwenguni.

“Mstahiki Prince Philip amekuwa ishara kuu ya maadili ya familia na umoja wa raia wa Uingereza na vile vile jamii ya kimataifa. Hakika, tunamwomboleza mtu mashuhuri aliyependa utangamano wa amani miongoni mwa wanadamu,” amesema Rais Kenyatta.

Akiwa mume wa Malkia Elizabeth II, alimsaidia kuongoza kwa kipindi cha muda wa miaka 65 mfululizo, hadi kustaafu kwake 2017.

Amekuwa nguzo kuu kwa Malkia kwa zaidi ya miaka 70. Cheo chake kimekuwa ni ‘Duke wa Edinburgh’.

Mwendazake ametajwa kusaidia kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo Uingereza.

Aidha, alikuwa mtoto wa kipekee wa kiume wa Mwanamfalme Andrew wa Ugiriki na Mwanamalkia Alice wa Battenberg.

Pamoja na Malkia Elizabeth II, walikuwa wamejaliwa kupata watoto wanne, wajukuu wanane na vitukuu 10.

Mhubiri Nyeri achoma karatasi za kutangaza huduma za waganga

Na SAMMY WAWERU

MHUBIRI mmoja eneo la Nyeri amewashangaza wenyeji kwa kuchoma karatasi zenye notisi za huduma za waganga zilizobandikwa katika maeneo ya umma, mabango na kwenye miti.

Mtumishi huyo wa Mungu na ambaye Taifa Leo imebaini anafahamaika kama Peter Gitahi, ameapa kuteketeza notisi zote Nyeri zinazotangaza huduma za uganga.

Pasta Gitahi ameendelea na hatua hiyo licha ya tetesi kuwa “ameonywa na baraza la waganga Nairobi”.

Juma hili, amekita kambi eneo la Chaka, picha zake akichoma notisi hizo zinazosambaa mitandaoni zikionekana kunaswa usiku.

“Anasaidia halmashauri ya jiji kusafisha mazingira. Matangazo yasiyolipiwa ada hayaruhusiwi,” #Fanuel Njiru akachangia kwenye Twitter, kufuatia chapisho analoonekana akichoma karatasi.

“Aache biashara za wenyewe zinawiri. Baadhi ya wahubiri pia wamegeuza nyumba ya Mungu kuwa biashara,” Monicah Peter akaandika, akizua ucheshi.

Duru zinaarifu Bw Gitahi ameapa kuendeleza oparesheni hiyo katika maeneo mengine ya nchi kama vile Mombasa.

“Sasa hapo pa Mombasa ajue hao si wachawi wa kawaida. Atakuwa anaona karatasi akienda kuitoa inageuka kuwa nyoka,” #Soni Sonee akazua ucheshi Facebook.

“Akija hapa Mombasa asahau Nyeri, kwa sababu hawa wa Mombasa ni moto wa kuotea mbali,” Jane Gicharu akatahadharisha.

Gor na Leopards mashakani

Na JOHN ASHIHUNDU

MABINGWA wa ligi kuu nchini, Gor Mahia na mahasimu wao wakuu, AFC Leopards huenda wakajipata mashakani kutokana na madeni wanayodaiwa na wachezaji wao wa zamani.

Tayari timu hizo kongwe zimepigwa marufuku kusajili kwa misimu miwili ijayo kwa kushindwa kulipa Dickson Ambundo na Vincent Habamahahoro mtawaliwa.

Akitoa habari hizo, Wakili Evans Majani alidai kwamba huenda klabu hizo zikateremshwa ngazi kwa kushindwa kulipa madeni hayo ya Sh3 milioni kwa jumla.

Ambundo anaidai Gor Mahia Sh1.2 milioni wakati Habamahahoro akiidai Leopards Sh1.8 milioni.

Majani alisema Fifa iliafikia uamuzi huo mwezi uliopita baada ya klabu hizo kupuuza agizo la Mahakama ya Kutatua Mizozo Michezoni (DRC).

“Iwapo wataendelea kupuuza agizo hili, tutalazimika kuandikia DRC kutafuta usaidizi wao na vikwazo zaidi ambavyo ni pamoja na kushusha timu hizo hadi daraja la chini,” aliongeza.

Majani alisema Wazito FC wamemlipa Issofou Bourhana na Augustine Otu na Piscas Kirenge, lakini wanadaiwa na Paul Acquah na Mansoor Safi Agu.

“Iwapo Gor Mahia na Leopards zitaendelea kutuzungusha, tutarejea kwa Fifa kwa hatua zaidi dhidi yao. Lazima walipe kwa sababu waliwatimua wachezaji hao ghafla,” alisema Majani.

Habari hizo zimetokea siku chache tu baada ya mlinzi Moussa Omar raia wa Burundi kusisitiza kwamba anataka Sofapaka imelipe Sh1 milioni kwa kumuachisha kazi ghafla mnamo 2019.

Akizungmza kuhusu tukio hilo, Maneja Mtendaji wa Sofapaka, Jimmy Ambajo alisema tayari wamezungmza na Omar kumtaka atulie hadi pesa zitakapopatikana. Alisema huenda wakamlipa kufikia Agoisti 2021.

Ombi la kuchangishia shujaa Ayimba ambaye ni mgonjwa Sh2 milioni

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya, Benjamin Ayimba anahitaji msaada wa Sh2 milioni kufanikisha matibabu yake.

Ayimba maarufu kama Benja amekuwa akizuru hospitali mara kwa mara tangu mwaka 2020 baada ya kupatikana na ugonjwa wa malaria ya ubongo.

“Hali yake imezorota kwa haraka na anahitaji msaada wetu wakati huu kuliko wakati mwingine katika maisha yake,” Shirikisho la Raga Kenya (KRU) limesema Aprili 9, likimtaja kama shujaa wa kweli aliye hai na wa kitaifa.

“Tunaomba wahisani kuchangia katika kumsaidia apate matibabu mazuri ya kumrejesha katika hali nzuri ya kiafya. Mchango wa kiasi chochote utasaidia,” KRU ilisema na kutangaza nambari ya Paybill kuwa 8021673 akaunti Benjamin Otieno Medical.

Kabla ya kuwa kocha mkuu wa Shujaa zaidi ya miaka 10 iliyopita, Ayimba alikuwa nahodha wa timu hiyo kati ya mwaka 2000 na 2005 ikishiriki pia Kombe la Dunia mwaka 2001 nchini Argentina na 2005 Hong Kong.

Yeye ndiye kocha wa Shujaa ambaye amewahi kuongoza timu hiyo kutwaa taji kwenye mashindano ya kifahari ya Raga za Dunia. Alikuwa usukani akisaidiwa na Paul Murunga wakati Shujaa iliduwaza miamba Fiji 30-7 katika fainali ya Singapore Sevens mwaka 2016.

Huduma za ukaguzi magari kutekelezwa kila Ijumaa mjini Murang’a

Na MWANGI MUIRURI

KAMISHNA wa Kaunti ya Murang’a Bw Mohamned Barre ametangaza Ijumaa kuwa huduma za ukaguzi wa magari zitaanza kutolewa na Mamlaka ya Usalama Barabarani Nchini (NTSA) kila Ijumaa mjini Murang’a.

Bw Barre ametangaza kuwa hatua hiyo imeafikiwa kufuatia ugumu wa wamiliki wa magari katika kaunti hiyo kuzimwa kupata huduma hizo katika miji ya Nairobi na Thika kufuatia ‘lockdown’ iliyowekwa kupambana na janga la Covid-19 Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza Machi 26.

Kamishna amesema marufuku hayo yamesababishia wengi kutatizika kwa kuwa ni kinyume na sheria za trafiki kuendesha gari ambalo halina cheti cha ukaguzi.

Bw Barre ametangaza kuwa maafisa wa NTSA sasa watakuwa wakikita kambi kila Ijumaa katika karakana ya Wizara ya Uchukuzi iliyoko katika barabara ya Kutoka Murang’a hadi Sagana.

“Serikali imetambua kuwa kuna shida kubwa kwa wamiliki wa magari wakisaka huduma hizi za ukaguzi. Mikakati hii ni ya kutatua shida hiyo na tutakuwa tukitekeleza wajibu huo kila Ijumaa,” akasema.

Aidha Bw Barre ametangaza kuwa leseni za kisasa zinazotolewa kidijitali zitaendea kupeanwa kwa waliojisali kila ijumaa ya wiki katika kituo cha Huduma Kilichoko Mjini Murang’a.

Visa vya wizi wa ng’ombe vyazidi Gatundu Kaskazini

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa vijiji vya Ngorongo na Kairi, Gatundu Kaskazini, wameachwa na hofu baada ya mifugo yao kuibwa.

Wakazi hao walieleza ya kwamba mnamo Jumatano ng’ombe wapatao wanane waliibwa majira ya usiku.

Bi Hellen Nyambura alisema ng’ombe wake wawili waliibwa mnamo Jumatano usiku.

Alieleza kuwa wezi hao, anashuku, ni watu hutoka mbali ambao walikuwa wamejihami kwa silaha hatari.

“Hata ng’ombe wangu mmoja alikuwa na ndama wake lakini pia aliibwa kutoka zizini,” alisema Bi Nyambura.

Naye Peter Ngige mkazi wa kijiji cha Kairi alisema wanashuku wengi wa wafanyakazi wa vibarua wa kazi za shamba katika maeneo hayo ndio pengine wanashirikiana na watu fulani ili kutekeleza wizi huo.

Alieleza kuwa wezi hao hupuliza dawa nyumbani kwa wenye ng’ombe zao halafu wanatekeleza wizi huo.

“Tunaitaka serikali kuingilia kati na kufanya uchunguzi mkali ili kubainisha kiini cha wizi huo kuenea bila mtu yeyote kutiwa nguvuni,” alifafanua Bw Ngige.

Wakazi hao wanaitaka serikali kuingilia kati kuona ya kwamba wezi hao wanakabiliwa vilivyo na kutiwa nguvuni.

Wanadai kuwa wizi huo unatekelezwa usiku wakati wa kafyu na kwa hivyo wanataka maafisa wa usalama wapige doria katika vijiji hivyo.

Tukio hilo limewaacha wakazi hao na hofu tele huku wengi wao wakiwaweka ng’ombe wao ndani katika nyumba zao.

Naye Gabriel Kimani wa kijiji cha Ngorongo alisema wezi hao wanaingia kwa boma kwa ujasiri majira ya usiku.

“Sisi kama wakazi wa eneo hilo tunashindwa kuelewa jinsi hasa wezi wanavyotembea usiku na ni wakati wa kafyu. Serikali ichukue hatua haraka kabla hawajatumalizia mifugo yetu,” alisema Bw Kimani.

Alieleza kuwa hata mbwa wanaofugwa vijijini huwa hawabweki ambapo wanashuku wezi hao hutumia dawa za kupuliza.

Supamaketi zina kibarua kudhibiti msongamano wa watu kipindi hiki cha janga la Covid-19

Na SAMMY WAWERU

LICHA ya serikali kuhimiza maeneo yanayotoa huduma za umma yadhibiti kiwango cha watu wanaoingia mara moja, maduka ya kijumla yangali na kibarua kigumu.

Kufuatia uchunguzi wa Taifa Leo katika supamaketi kadhaa mitaa mbalimbali Nairobi na Kiambu, misongamano ya wateja inaendelea kushuhudiwa kwenye foleni ya kashia.

Mfano, katika maduka ya kijumla ya Kassmatt Jumbo na Naivas eneo la Githurai, msongamano wa watu umekuwa si hoja kwa wahudumu na wasimamizi.

Taswira hiyo si tofauti na ya duka la jumla la PowerStar mtaa wa Zimmerman, kati ya mengine, hali hiyo ikiweka wafanyakazi na wateja wenyewe katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Ndio tunaelewa ni hatari, ila wateja nao hawatilii maanani maelekezo tunayowapa. Ni Mungu tu anatulinda,” akasema mhudumu mmoja wa duka la Naivas.

Msongamano huo wa wanunuzi unaibua maswali chungu nzima, kuhusu usalama wa taifa, maduka tuliyozuru yakiashiria taswira ya mengine.

Maji yanazidi unga kuanzia mwendo wa adhuhuri, kizungumkuti ambacho kinazua wasiwasi, ikizingatiwa kuwa hakuna anayejua hali ya mwenzake iwapo ameambukizwa virusi au la.

Licha ya maelekezo na ilani kuwekwa katika maduka hayo, wateja wameendelea kupuuza, na ni jukumu la wahudumu kuwakumbusha.

Kiambu na Nairobi ni miongoni mwa kaunti ambazo zimetajwa kuwa hatari katika maambukizi ya corona.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Machi 26, 2021, kukaza kamba kanuni na mikakati zilizowekwa kusaidia kuzuia corona, katika kaunti hizo mbili pamoja na Kajiado, Machakos na Nakuru.

Kenya inaendelea kuandikisha ongezeko la maambukizi, ikiwa ni pamoja idadi ya wanaoangamizwa na Covid-19.

Ni muhimu maduka ya jumla nchini yachukue tahadhari ya hatari inayowakodolea macho.

Hatua ya Rais Kenyatta kutangaza kusimamisha kwa muda mikutano ya umma, na inayoandiliwa kudhibitiwa idadi ya watu, maduka ya kijumla yanapaswa kuiga mkondo huo.

Hazina ya Kitaifa yalaumiwa kwa uzorotaji wa huduma vituo vya afya Kakamega

SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

HATUA ya Hazina ya Kitaifa kuchelewesha utoaji wa fedha kwa kaunti imechangia kuzorota kwa hali ya utoaji huduma katika vituo vya kiafya katika Kaunti ya Kakamega.

Waziri wa Afya katika kaunti hiyo Dkt Collins Matemba Alhamisi alisema uhaba wa fedha umechangia kaunti hiyo kulemewa kuendesha shughuli zake.

“Tumepokea fedha mara tano pekee tangu Mwaka wa Kifedha wa 2020/2021 ulipoanza. Hali hii imeathiri pakubwa shughuli zetu na hivyo kukwama kwa huduma katika vituo mbalimbali,” akasema Dkt Matemba.

Waziri huyo alikuwa akimjibu Mbunge wa Matungu Peter Nabulindo ambaye amependekeza kufungwa hospitali ya kaunti ndogo ya Matungu kutokana na hali mbaya katika hospitali hiyo.

Mbunge huyo alisema baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wadi za hospitali hiyo hawana chakula.

Wananchi katika eneo hilo wamelalamikia hali mbaya ya hospitali na kuitaka serikali ya Kaunti ya Kakamega kutoa suluhu kwa changamoto kadha zinazoikabili.

Kenya yaomba mkopo mwingine wa Sh86 bilioni kutoka Benki ya Dunia

Na CHARLES WASONGA

LICHA ya pingamizi kutoka kwa Wakenya, serikali inaendelea na mtindo wake wa kuomba mikopo kutoka kwa taasisi za kimataifa kufadhili mahitaji yake wakati huu wa janga la corona.

Hazina ya Kitaifa inasema inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) kwa nia ya kupata mkopo mwingine wa Sh86 bilioni, siku mbili baada ya Wakenya kulalamikia mkopo wa Sh255 bilioni kutoka kwa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).

Kwenye taarifa, Waziri wa Fedha Ukur Yatani alisema mkopo huo ambao utatolewa chini ya kitengo cha maendeleo katika benki hiyo, yaani Word Bank Development Policy Operations (DPO).

“Mazungumzo yanaendelea baada ya Kenya kuwasilisha ombi lake katika bodi ya wakurugenzi wa Benki ya Dunia ndani ya majuma kadha yajayo. Ikiwa mazungumzo hayo yatafaulu, tutapokea mkopo huo Mei au Juni 2021,” Yatani akasema Jumatano baada ya kufanya mazungumzo na Taufila Nyamadzabo, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, kanda ya Afrika.

Mnamo Mei 2020 Kenya ilipokea mkopo wa Sh106 bilioni kutoka Benki ya Dunia kuisaidia kufadhili bajeti yake na kukinga uchumi kutokana na athari zilizosababishwa na janga la Covid-19.

Mkopo huo utalipwa kwa kipindi cha miaka 30.

Kenya imeomba mkopo mwingine kutoka Benki ya Dunia siku chache baada ya IMF kuidhinisha mkopo wa Sh255 bilioni hatua ambayo ilichochea pingamizi nyingi kutoka kwa Wakenya katika mitandao ya kijamii.

Wakenya hao waliilaumu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwawekea mzigo mkubwa wa madeni ambao sasa imefika Sh8 trilioni kuanzia mwezi wa Januari.

Hata hivyo, waziri Yatani amepuuzilia mbali pingamizi hizo akishikilia kuwa Kenya ina uwezo wa kumudu mikopo yake na itatumia pesa hizo kwa njia nzuri.

Aliahidi kutoa maelezo ya kina kuhusu mikopo hiyo hivi karibuni ili kuzuia “Wakenya kupotoshwa na watu fulani ambao lengo lao kuu ni kuichafulia serikali jina.”