Aliyehifadhiwa mochari kwa saa moja aeleza muujiza kuhusu ‘jinsi alivyofufuka’

Na VITALIS KIMUTAI

“NAFURAHI kuwa hai!”

Hayo ni maneno ya kwanza ya Peter Kiplangat Kigen, 32, kutoka Kaunti ya Kericho ambaye alipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Kipkatet baada ya kudhaniwa kimakosa kuwa alifariki.

“Ni muujiza kwamba napumua, naongea, kula na kutingisha miguu na mikono baada ya kutangazwa kuwa mfu. Hii ni kazi ya Mungu,” akasema katika mahojiano na Taifa Leo jana Alhamisi.

Alikuwa akiongea hospitalini anakoendelea kupokea matibabu, ambapo alielezea aliyoyapitia baada ya kujipata amelazwa katikati ya maiti katika mochari.

Baba huyo wa watoto wanne alipiga mayowe wahudumu wa hifadhi hiyo walipoanza kukata sehemu ya mguu wake ili watie dawa ya kuhifadhi maiti.

“Nilihisi uchungu mkali mguuni mwangu na nikalia kwa sauti ya juu. Ilikuwa ni kana kwamba nilikuwa nikichomwa kwa chuma ya moto uchungu ukienea hadi kwenye mifupa yangu,” akasema Bw Kigeni.

Jamaa, wanakijiji na watu wa kawaida walisongamana katika wadi ya wanaume ya hospitali hiyo ili angalau wamwone mwanamume huyo “aliyefufuka kutoka wafu” baada ya kutupwa katika sakafu baridi kwenye hifadhi ya maiti.

“Sifahamu kilichotendeka kilichotendeka kabla ya kujipata nimetupwa ndani ya mochari. Lakini baadaye nilihisi nikipelekwa kwa machela katika wadi mwili wangu ukiwa umewekwa paipu za plastiki. Hii, niligundua, ni baada ya kupiga kilele,” akasema Bw Kigen ambaye zamani alikuwa akihudumu kama kondakta wa matatu.

Ilisemekana kuwa jamaa huyo alizirai na kupelekwa katika wadi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi ambako madaktari walichukua muda wa saa moja kumsaidia kupata ufahamu.

Baadaye aliwalazwa katika wadi ya kawaida ya wanaume.

Alipozirai kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Keroncho, wadi ya Cheplanget, Jumanne asubuhi, Kigen alikimbizwa hospitalini na jamaa zake ambao hawakuamini kuwa angepona kwa sababu amekuwa akiugua kwa muda mrefu.

Jamaa zake walilalamika kuwa hakuhudumiwa katika wadi ya majeruhi alikokaa kwa saa kadhaa baada ya kuzirai.

“Sikuelewa ni jinsi gani wahudumu wa afya walivyoshawishika kuwa nilifariki na hivyo nikisafirishwa hadi katika mochari. Jambo hilo bado linanikera,” akasema Bw Kigen.

Jeraha katika mguu wake wa kushoto bado ulikuwa unampa maumivu.

Licha kwamba alikuwa mchovu huku akijikaza kuongea, Bw Kigeni bado anaweza kuwakumbuka jamaa na marafiki zake ambao walimtembelea. Aliweza kuwatambua kwa majina yao halisi.

Watu wa familia yake walisema Kigen amekuwa akiugua kwa muda mrefu.

Ubunge kuokoa vigogo kisiasa

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA ambao wanahudumu kwa muhula wa pili, na wa mwisho, watalazimika kuwania nyadhifa za ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2022 ili wawe katika nafasi bora ya kuteuliwa kwa nyadhifa za juu serikalini.

Hii ni baada ya mswada rasmi wa marekebisho ya Katiba kupitia Muafaka wa maridhiano (BBI) kutopendekeza kubuniwa kwa serikali za majimbo, ambazo baadhi ya magavana hao walipania kuongoza. Vilevile, BBI imedumisha vipengele vya katiba vinavyosema kuwa rais na magavana watahudumu kwa mihula miwili pekee.

Kulingana na mswada huo, uliozinduliwa Jumatano, Nairobi, Waziri Mkuu, manaibu wa waziri mkuu, sehemu ya mawaziri na manaibu waziri watakuwa wabunge, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo mawaziri hawapaswi kuwa wabunge.

Baadhi ya magavana 22 watakaostaafu 2022, walikuwa wameweka matumaini yao kwa marekebisho haya ya Katiba, kwamba wangepata mwanya wa kuwania nyadhifa za magavana wa majimbo.

Wengi wao waling’amua kuwa nafasi ya kuwania urais au kuwa mgombea-mwenza 2022 utakuwa finyu.

Mapema mwaka huu, magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Ali Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) walitetea kubuniwa kwa serikali za majimbo, kwa kile kilichofasiriwa kama nia ya kuendeleza kuwa na ushawishi wa kisiasa. Magavana hao, ambao awali walikuwa wametangaza nia ya kugombea urais, walitoa mapendekezo hayo wakati wa mikutano ya hamasisho kuhusu BBI katika uwanja wa Tononoka (Mombasa) na ule wa Bukhungu (Kakamega).

Wakili wa masuala ya kikatiba, Bw Bobby Mkangi anasema kuwa japo wadhifa wa ubunge unaonekana kuwa wenye hadhi ya chini kuliko ugavana, mswada wa BBI sasa umeufanya kuwa kivutio kwa magavana watakaokamilisha kipindi chao cha kuhudumu 2022.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba baadhi ya magavana, wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho, watalazimika kuwania nyadhifa za ubunge ili wazitumie kucheza karata zao za kuteuliwa katika nyadhifa za Waziri Mkuu, manaibu wa waziri mkuu, mawaziri na manaibu wa mawaziri. Hii ni kwa sababu wengine wao hawataki kusalia katika baridi ya siasa baada ya kuondoka afisini,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Alhamisi.

Kauli sawa na hii ilitolewa na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, aliyesema kuwa haitashangaza kuona baadhi ya magavana wanaotaka kuwania urais, wakiendea nyadhifa za ubunge kama ‘daraja’ la kukwea juu serikalini.

“Ukweli ni kwamba mswada wa BBI umewaacha magavana wanaohudumu kipindi cha pili katika hali ya kujikuna kichwa hasa baada ya wazo la kubuniwa kwa serikali za majimbo kutupiliwa mbali. Kwa hivyo, itawalazimu kuwania nyadhifa nyingine kuanzia ubunge, useneta na hata urais ili waendelee kuwa na usemi katika ulingo wa siasa,” akasema Bw Manyora, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alisema kuwa pendekezo la kubuniwa kwa maeneobunge mengine 70 zaidi litawafaa zaidi magavana hawa 22 kupata nafasi za kushindania nafasi hizo mpya.

Orodha ya kaunti 28 zilizogawiwa maeneobunge hayo mapya ina kaunti 15 zilizo na magavana wanaohudumu kwa awamu ya pili.

“Kwa mfano, Bw Oparanya anaweza kuwania kimojawapo cha viti viwili vya maeneobunge yatakayobuniwa katika Kaunti ya Kakamega. Naye Bw Joho anaweza kuwania katika mojawapo ya maeneo matatu mapya ambayo yatabuniwa katika Kaunti ya Mombasa endapo mswada wa BBI utapitishwa na Wakenya katika kura ya maamuzi,” akaeleza Bw Manyora.

Hata hivyo, wachanganuzi hao wanaonya kuwa magavana watakaowania nyadhifa za ubunge kwa lengo la kuteuliwa mawaziri watakuwa na kibarua kikubwa kujinadi kwa wapigakura.

Kulingana na Bw Mkangi, itabidi waweke matumaini yao kwa uwezekeno wa chama au muungano watakaotumia kisiasa kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu.

Hivi majuzi, Gavana Oparanya, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), alitangaza kuwa hatastaafu siasa baada ya kipindi chake kukamilika ila atapigania kiti cha kitaifa.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya Shiatsala, eneobunge la Butere, hakufichua wadhifa atakaopigania.

“Kipindi changu cha kuhudumu kama gavana kinakamilika 2022. Nimeamua kuwa sitaenda nyumbani lakini nitaendelea kupambana katika siasa za kitaifa. Sijui ni kiti kipi, lakini ninaamini kuwa nitakuwa katika meza ambako keki ya kitaifa inagawanywa,” akasema.

Magavana wengine wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho ni pamoja na Jackson Mandago (Uasin Gishu), Sospeter Ojaamong (Busia), Martin Wambora (Embu) na Paul Chepkwony (Kericho).

Wengine ni Josephat Nanok (Turkana), Mwangi wa Iria (Murang’a), Okoth Obado (Migori), Samuel Tunai (Narok), James Ongwae (Kisii), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) miongoni mwa wengine.

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Nguzo tano za Uislamu ni mfumo wa maisha ya kawaida kwa Muumini

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mungu Azzawajalla, swala na salamu zimwendee Mtume Mtukufu Swallallahu A’alayhi Wasallam.

Nguzo tano za Uislamu ni mfumo wa maisha ya Mwislamu. Ndizo ushahidi wa Imani, Swalah, utoaji wa Zakaah (kuwasaidia wenye dhiki), kufunga katika mwezi wa Ramadhan na kuhiji Makkah mara moja maishani kwa wale wenye uwezo.

1 Shahada ya Imani

Ushahidi wa Imani ni kusema kwa kusadikisha, “La ilaaha illAllaah, Muhammadur Rasulullah.” Maana ya matamshi haya ni, “Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na kwamba Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu.” Sehemu ya kwanza, “Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu,” inamaanisha kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake, na kwamba yeye hana mshirika wala mwana.

Ushahidi huu wa Imani unaitwa Shahada, ambayo ni kanuni nyepesi inayopaswa itamkwe pamoja na kusadiki ili mtu aweze kuingia katika Uislamu, kama ilivyoelezwa hapo juu. Ushahidi wa Imani ndiyo nguzo muhimu zaidi katika Uislamu.

2 Swalah

Waislamu huswali Swalah tano kila siku. Kila Swalah huchukuwa muda mfupi wa dakika chache tu. Swalah katika Uislamu ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mja na Mwenyezi Mungu. Hakuna kishenga baina ya Mwenyezi Mungu na mfanyaja ibada.

Ndani ya Swalah, mtu husikia ndani yake furaha, amani na faraja, na kwamba Allaah yu radhi naye. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Bilaal adhini, ili tufarijike nayo.)

Bilaal alikuwa mmojawapo wa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mwadhini. Swalah hufanyika wakati wa Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na ‘Ishaa. Mwislamu anaweza kuswali karibu pahala popote, kama vile mashambani, ofisini, viwandani au vyuoni.

3 Kutoa Zakaah

Kila kitu ni cha Mwenyezi Mungu, na hata mali zinazohifadhiwa na wanadamu kama dhamana. Maana halisi ya neno Zakaah ni zote mbili ‘kutwaharisha’ na ‘kukua.’ Maana ya kutoa Zakaah ni kutoa asilimia iliyotajwa bayana kutokana na mali fulani kwa kuwapatia makundi fulani ya watu wenye dhiki.

Asilimia inayopaswa kulipwa kutokana na dhahabu, fedha na pesa taslimu zenye kufikia kiasi kinacholingana na gramu 85 za dhahabu na kubaki katika miliki ya mtu kwa mwaka mmoja wa Kiislamu ni asilimia mbili na nusu. Tunavyovimiliki hutakasika kwa kutenga pembeni sehemu ndogo tu kwa ajili ya wenye dhiki, na kama vile kupogoa matawi ya mimea, huku kupunguza salio na kunatia moyo wa ukuaji mpya. Mtu anaweza kutoa zaidi kadri atakavyo kama Sadaka.

4 Kufunga katika Mwezi wa Ramadhan

Kila mwaka katika mwezi wa Ramadhan, Waislamu hufunga kuanzia alfajiri hadi kuchwa kwa jua, kwa kujizuia kula, kunywa na tendo la ndoa. Ingawa Swawm ni yenye faida za kiafya, huchukuliwa kimsingi kuwa ni namna ya kuisafisha nafsi kiroho.

Kwa kujizuia dhidi ya starehe za kidunia, japo kwa muda mfupi, mfungaji hupata huruma ya kweli kwa wanaopatwa na njaa, kadhalika na kuongezeka kwa maisha yake ya kiroho.

5 Kuhiji Makkah

Hija ya kila mwaka Makkah ni faradhi ya kufanywa mara moja tu maishani kwa wenye uwezo wa kimwili na mali katika kuitekeleza. Kadri ya watu milioni mbili huenda Makkah kila mwaka kutoka kila sehemu duniani. Ingawa mara zote Makkah huwa imesheheni wageni, Hija ya mwaka hufanywa katika mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya kiislamu. Mahaji wa kiume huvaa nguo maalumu na rahisi ambayo huondosha tofauti za kimatabaka na tamaduni kiasi kwamba wote huwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mahujaji wakiswali katika Msikiti wa Haram huko Makkah. Msikitini humu mna Ka’abah (jengo jeusi linaloonekana katika picha) ambalo Waislamu hulielekea wakati wakiwa katika Swalah. Ka’abah ni mahali pa ibada ambapo Mwenyezi Mungu Aliwaamuru Mitume Ibraahiym na mwanaye, Isma’iyl waijenge.

Ibada za hija ni pamoja na kuitufu Ka’abah mara saba na kwenda mchakamchaka baina ya kilima cha Swafa na Marwa mara saba, sawa na Hajar alivyofanya wakati akitafuta maji. Kisha, Mahujaji husimama pamoja katika uwanja wa ‘Arafah na kumwomba Mwenyezi Mungu wakipendacho na kwa ajili ya maghufira, katika kile ambacho mara nyingi hufikirika kuwa ni onyesho la awali la Siku ya Malipo.

Mwisho wa Hijjah huweza kujulikana kwa sikukuu ya ‘Iydul-Adhw-haa, ambayo husherehekewa kwa Swalah. Sikukuu hii na ‘Iydul-Fitwr, sherehe ya kuadhimisha mwisho wa Ramadhan ndiyo sikukuu mbili za kila mwaka katika kalenda ya Kiislamu.

Huenda Kenya ikose Jaji Mkuu kwa miezi 6

Na JOSEPH WANGUI

KENYA huenda itakaa bila Jaji Mkuu halisi hadi Juni 2021 baada ya jaribio la Tume ya Huduma za Majaji (JSC) kumshinikiza Jaji David Maraga kutoa idhini ya uteuzi wa mapema wa mrithi wake kugonga mwamba.

Jaji Maraga, anayetazamiwa kutoa hotuba yake ya mwisho hii leo (Ijumaa) kuhusu Hali ya Idara ya Mahakama mwakani, anatarajiwa kuanza likizo yake ndefu ya mwezi mmoja mnamo Desemba 14, kabla ya kustaafu kwake rasmi Januari 12, 2021.

Duru kutoka Tume hiyo zilizokataa kutajwa ziliashiria kuwa alikataa pendekezo la makamishna wanane lililomtaka kutia sahihi fomu ya kutangaza kuwepo kwa nafasi, ili Tume hiyo ianze mchakato wa kuteua mrithi wake.

Jaji Maraga imeelezwa alikataa ombi hilo kwa misingi kwamba haliambatani na kanuni na sheria kuhusu kustaafu kwa majaji.

Mchakato wa kustaafu kwa jaji huanza na barua kutoka kwa Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama inayomwagiza jaji anayeelekea kustaafu kwenda likizo ndefu kabla ya kustaafu.

Msajili Mkuu Anne Amadi alithibitisha Alhamisi kwa Taifa Leo kwamba Bw Maraga alipatiwa barua ya kwenda likizo ndefu mnamo Februari 2020.

“Barua hii (ya likizo ndefu) ilitolewa Februari. Huwa inatolewa mara moja tu,” alisema Bi Amadi.

Mwanzoni mwa mwaka, kulikuwa na ripoti kuhusu Bw Maraga kustaafu mapema kama mtangulizi wake Bw Willy Mutunga, ili kuzuia hali ambapo afisi hiyo kuu zaidi katika Idara ya Mahakama inasalia bila mtu.

Kutokana na muda unaohitajika kisheria kuhusiana na mchakato wa uteuzi wa jaji, huenda Kenya ikasalia bila Jaji Mkuu hadi Juni, 2021.

Endapo hakutakuwa na changamoto zozote na kuchukulia kuwa uteuzi wa mrithi wa Bw Maraga utafanyika pasipo vizingiti vyovyote, tarehe ya mapema zaidi ambayo JSC inaweza kukamilisha uteuzi wa Jaji Mkuu mpya ni Juni 2021.

Sheria haijasema lolote kuhusu iwapo mchakato wa uteuzi wa Jaji Mkuu unaweza kuanzishwa kabla ya wadhifa huo kusaliwa wazi.

Huenda hii ndiyo sababu kundi hilo la makamishna lilimtaka Bw Maraga kutia sahihi fomu ya kutangaza kuwepo kwa nafasi kutoka Tume hiyo ili kuanzisha mchakato huo.

Hii ni kwa sababu anayeshikilia afisi hana mamlaka baada ya kuondoka afisini.

Jaji Mkuu pia anashikilia wadhifa wa mwenyekiti wa JSC.

Kulingana na Sheria kuhusu JSC, mchakato wa uteuzi huanza baada ya Tume kubuni jopo linalojumuisha wanachama wasiopungua watano.

Refarenda: Ruto kujipima nguvu katika ngome yake

ERIC MATARA na TOM MATOKE

UZINDUZI wa ukusanyaji sahihi za kufanikisha marekebisho ya katiba sasa umefungua wazi uwanja kwa Naibu Rais William Ruto kudhihirisha ubabe wake wa kisiasa katika eneo la Rift Valley.

Eneo hilo ni miongoni mwa yale yanayotarajiwa kuwa na upinzani dhidi ya refarenda, kwa vile Dkt Ruto anaaminika kuwa na ufuasi mkubwa.

Wandani wa Dkt Ruto katika ngome hiyo yake ya kisiasa tayari wameanza upya kuwakabili viongozi wanaounga mkono mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Katika ukanda huo, Kiongozi wa Kanu, Bw Gideon Moi, mwenzake wa Chama Cha Mashinani, Bw Isaac Ruto na Gavan wa Elgeyo Marakwet, Bw Alex Tolgos, wana jukumu la kushawishi wapigakura kutia sahihi kwenye mswada wa mapendekezo ya kurekebisha katiba.

Mswada huo ulizinduliwa rasmi Jumatano na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, katika hafla ambayo Dkt Ruto hakuhudhuria.

Tayari, Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang, aliye mwandani wa Naibu Rais ameonya kwamba hataruhusu ukusanyaji wa saini za kuunga BBI katika kaunti yake.

“Katika Kaunti ya Nandi hatutakubali. Mtu asijaribu kuja kutafuta saini hapa, hakuna mtu atapeana saini katika kaunti yetu ya Nandi, kwenda tafuta mahali kwingine,” alisema Bw Sang.

Matamshi hayo tayari yamesababisha Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kusema itamuita Bw Sang kumhoji kufuatia kauli hiyo.

“Kaunti ya Nandi ni miongoni mwa maeneo saba ambayo NCIC imetambua kama yanayoweza kukumbwa na fujo kuhusu BBI na kwenye uchaguzi mkuu ujao. Tutamuita Gavana Sang kuandikisha taarifa,” alisema Kamishna wa NCIC, Bw Abdulaziz Farah.

Tolgos asema mswada una manufaa

Wakati huo huo, Bw Tolgos pia alipuuzilia mbali wafuasi wa ‘Tangatanga’ wanaopinga kura ya maamuzi na kuwataja kuwa wabinafsi kwani mswada uliopendekezwa una manufaa chungu nzima hasa kwa serikali za kaunti.

“Tunawaomba wasitutatize tunapohamasisha umma, nasi pia tutawapa muda kueleza misimamo yao wakitaka hivyo,” akasema.

Bw Sang alisisitiza kuna changamoto tele zinazohitaji kutatuliwa na viongozi wakati huu wala si kujihusisha kwa kura ya maamuzi.

Magavana wengine wanaounga BBI eneo la Rift Valley ni Lee Kinyanjui (Nakuru), Samuel Tunai(Narok), Joseph ole Lenku(Kajiado), Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Ndiritu Muriithi (Laikipia) na Prof John Lonyangapuo (Pokot Magharibi).

Kwa kuwa eneo la Rift Valley ni ngome yake ya kisiasa, Dkt Ruto huenda akaamua kudhihirisha ubabe wake kwa kuzima shughuli hiyo eneo hilo.

Mnamo Jumatano, Naibu Rais aliendelea kuelezea matumaini kwamba hata baada ya kuzinduliwa kwa ukusanyaji sahihi bado kuna nafasi ya kupatikana kwa muafaka ili kusiwe na kura ya maamuzi ya kuleta migawanyiko nchini.

“Hata baada ya kuzinduliwa kwa ukusanyaji sahihi, naamini bado kuna nafasi ya kupatikana kwa maelewano ili kufanyike refarenda itakayowapa Wakenya nafasi ya kujieleza bila ushindani. Umoja na nguvu ndio inahitajika katika vita dhidi ya Covid-19 na ukarabati wa uchumi,” akasema Dkt Ruto kupitia akaunti yake ya Twitter.

Hii ni ishara kwamba hakuridhishwa na mabadiliko ambayo yalifanywa katika ripoti ya BBI na mswada wa marekebisho wa Katiba, na ikizingatiwa kwamba meli ya refarenda tayari imeng’oa nanga, huenda asiwe na budi ila kuendeleza kampeni za kupinga marekebisho ya katiba.

Sonko aelekea ‘kichinjioni’ hoja ikipita

Na COLLINS OMULO

MADIWANI wa Kaunti ya Nairobi wameanza rasmi mchakato mpya wa kumng’oa Gavana Mike Sonko mamlakani.

Hii ni baada ya madiwani 86 kutia saini ilani ya kuwasilisha hoja ya kumtimua gavana huyo anayekumbwa na matatizo tele katika uongozi wake. Sahihi 42 pekee ndizo zilizohitajika.

Akitaja hoja hiyo, Kiongozi wa Wachache katika bunge la kaunti, Bw Michael Ogada, aliwasilisha sababu mbalimbali za dhamira ya kumng’oa Sonko mamlakani.

Miongoni mwa sababu hizo ni madai ya kukiuka katiba, utumizi mbaya wa mamlaka, utendaji wa uhalifu chini ya sheria ya kitaifa na kimataifa, na kukosa uwezo wa kimwili na kiakili kuendesha shughuli za serikali za kaunti inavyofaa.

Bw Ogada alisema wiki ijayo, atawasilisha ushahidi wa kutetea sababu alizotoa huku akisisitiza kuwa Gavana ameshindwa hata kutekeleza majukumu aliyobakishiwa baada ya kukabidhi mengine kwa Serikali Kuu.

“Hatutaendelea kukaa tukisubiri milele. Wakati sasa umefika na madiwani wa Nairobi tumeamua lazima tuchukue hatua na kuhakikisha hali ya kawaida inarudishwa jijini,” akasema diwani huyo wa Embakasi.

Aliongeza, “Hatua pekee tunayoweza kuchukua kama madiwani ni kumtimua aende nyumbani ili wananchi wachague gavana mwingine na tusonge mbele. Wakazi lazima wahudumiwe.”

Kwa upande wake, kiranja wa wachache katika bunge hilo, Bw Peter Imwatok alisema Spika Benson Mutura atamkabidhi gavana notisi hiyo inayoeleza sababu za madiwani kutaka aondolewe mamlakani.

Baadaye Sonko atapewa siku saba kuwasilisha utetezi wake kabla ya hoja rasmi ya kumtimua ipelekwe katika bunge hilo.

“Kufikia Alhamisi ijayo, madiwani watatoa uamuzi wao na sioni kama watakuwa na uamuzi mwingine ila kumtuma akajitetee mbele ya Seneti,” akasema Bw Imwatok.

Hii ni mara ya pili kwa madiwani kujaribu kumng’oa mamlakani gavana huyo.

Jaribio la kwanza mnamo Februari lilitibuka wakati Rais Uhuru Kenyatta alipoingilia kati.

Hoja ya kumtimua ikipitishwa na madiwani 82 kati ya 122 wa Nairobi, Spika Mutura atatakikana kumjulisha Spika wa Seneti kuhusu uamuzi wa madiwani kabla siku mbili zikamilike.

Katika siku za hivi majuzi, Sonko amekuwa akimshambulia wazi Rais Kenyatta katika mitandao ya kijamii, pamoja na Mkuu wa Idara ya Huduma za Nairobi (NMS) Jenerali Mohamed Badi.

Hisia mseto kuhusu BBI

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa kisiasa Alhamisi waliibua hisia mseto kuhusu ripoti ya BBI baada ya kuzinduliwa kwa shughuli ya ukusanyaji wa sahihi kuunga mkono marekebisho ya Katiba.

Huku baadhi yao wakiunga mkono mswada huo wa marekebisho ya Katiba wengine walishikilia kuwa taifa haliko tayari kwa kampeni za kisiasa haswa wakati huu wa janga la corona

Kiongozi wa Chama cha Amani National Congresss (ANC) Musalia Mudavadi Alhamisi alisema kuwa mengi ya masuala tata ambayo aliibua yameshughulikiwa.

“Nilihudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa ukusanyaji wa sahihi katika ukumbi wa KICC ambako mswada wa BBI ulizinduliwa. Tathmini yangu ya haraka ilionyesha kuwa masuala ambayo mimi na Wakenya wengine tuliibua yameshughulikiwa kwa kiwango kikubwa,” akawaambia wanahabari katika kituo cha Musalia Mudavadi Centre kilichoko Riverside, Nairobi.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior pia aliunga mkono kauli ya Bw Mudavadi akisema mengi ya mapendekezo yaliyoibua utata na pingamizi yaliondolewa kwenye ripoti ya mswada wa BBI wa awali.

“Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa 2020 umeboreshwa kuliko rasimu ya zamani. Mengi ya masuala tata kama vile kuongezwa kwa idadi ya maeneobunge, mamlaka ya Seneti, Uteuzi wa Afisi ya Afisa wa kupokea malalamishi kuhusu majaji, suala la ugavi wa fedha kati ya serikali kuu na zile za kaunti na kuhamishwa kwa majukumu ya Kaunti ya Nairobi hadi Serikali Kuu sasa yamewekwa bayana,” akasema Bw Kilonzo Junior ambaye pia ni kiranja wa wachache katika seneti.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga alisema rasimu ya mwisho ya ripoti ya BBI imeshughulikia suala ya uwakilishi wa jinsia bungeni.

“Tangu taifa hili lijinyakulie uhuru, tumepambana na suala hili la usawa wa jinsia bila mafanikio. Ni furaha yetu kama wanawake kwamba BBI sasa imelishughulikia kwa ukamilifu. Huu ni ushindi kwa wanawake wa Kenya,” akasema.

Lakini Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, Aaron Cheruiyot (Kericho) aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando na Wakili mashuhuri Ahmednasir Abdullahi walipinga ripoti hiyo wakisema haijashughulikia matakwa ya Wakenya.

“Chini ya BBI bunge litakuwa na angalau wabunge 520 ndani ya miaka 15 ijayo huku bunge la Kitaifa likiwa na kati ya wajumbe 420 na 430,” akasema Murkomen ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto.

Manchester City washinda Olympiakos 1-0

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amesisitiza kwamba mabao “yatajileta yenyewe” baada ya Manchester City kufunga goli moja pekee dhidi ya Olympiakos licha ya kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 25, 2020 nchini Ugiriki.

Ushindi wa Man-City katika mchuano huo uliwakatia tiketi ya hatua ya 16-bora ya UEFA huku wakisalia na mechi mbili zaidi za kutandaza katika Kundi C.

Masogora wa Guardiola walijibwaga ugani dhidi ya Olympiakos wakihitaji alama moja pekee ili kujipa uhakika wa kusonga mbele katika kampeni za UEFA.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Man-City waliowaelekezea Olympiakos jumla ya fataki 25, lilifungwa na chipukizi raia wa Uingereza, Phil Foden katika dakika ya 36.

Licha ya kuchezea katika uwanja wa nyumbani, Olympiakos walishindwa kuelekeza kombora lolote langoni mwa wageni wao hadi dakika ya 88. Hata hivyo, jaribio lao hilo lilidhibitiwa vilivyo na kiungo Ilkay Gundogan aliyeshirikiana vilivyo na Bernardo Silva.

Kiungo Kevin de Bruyne aliachwa nje ya kikosi cha Man-City kilichomkaribisha tena fowadi Sergio Aguero kwa dakika 13 za mwisho wa kipindi cha pili baada ya kupona jeraha la goti.

Ni matarajio ya Guardiola kwamba ushindi waliouvuna dhidi ya Olympiakos utawapa motisha zaidi kutamba katika jumla ya michuano 11 ijayo kabla ya kampeni za mwaka huu wa 2020 kukamilika rasmi.

Man-City walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Olympiakos wakipania kujinyanyua baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 na Tottenham Hotspur katika mchuano wa awali wa EPL mnamo Novemba 21, 2020.

Man-City ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwenye jedwali la EPL kwa alama nane zaidi nyuma ya viongoziu Tottenham, wanashuhudia mwanzo mbaya zaidi ligini tangu 2008.

Kikosi hicho kilichotwaa ufalme wa EPL mnamo 2017-18 na 2018-19, hakijafunga zaidi ya bao moja katika EPL tangu wapokezwe kichapo cha 5-2 na Leicester City mnamo Septemba 2020.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Burnley katika EPL mnamo Novemba 28 kabla ya kuwaendea FC Porto ya Ureno kwa gozi la UEFA mnamo Disemba 1, 2020.

Thika Shakers Academy yasaidia vijana kujiimarisha katika talanta na nidhamu

Na LAWRENCE ONGARO

NI kituo kimojawapo cha kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi kwa kuinua mchezo wao wakilenga kuafikia viwango vya kimataifa baadaye.

Thika Shakers Academy ni kituo kilichoko mtaani Makongeni, Thika na kwa muda sasa kimekuwa chini ya kocha Swaleh ‘Betto’ Harub tangu mwaka 2018.

“Tuliunda kituo hiki kwa lengo la kukuza talanta za chipukizi hawa ikiwemo kuwafunza maadili mema katika jamii. Pia tunawaepusha na maovu kupitia kucheza soka,” akasema kocha.

Kufikia sasa kituo hicho kimezalisha wachezaji kadha ambao huenda watapata nafasi katika klabu maarufu za humu nchini hivi punde.

Kocha Harub anasema kituo hicho kina wanasoka chipukizi wapatao 150 ambao miaka yao kiumri ni 10 hadi 20.

Thika Shakers Academy yasaidia vijana kujiimarisha katika talanta na nidhamu. Picha/ Hisani

Kocha huyo anawahimiza wazazi kuzingatia mambo mawili kwa wana wao. Mambo hayo ni kuzingatia masomo na michezo hasa soka.

“Mambo hayo mawili yanastahili kuambatana pamoja ili mwanasoka yeyote aweze kupiga hatua kimaisha,” akasema kocha huyo.

Pia anawapongeza Bethwel Onyango na Kenneth Ambaye ambao kwa uwezo wao wamekuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba chipukizi hao wanapiga hatua zaidi.

“Jambo muhimu ninalotilia mkazo ni nidhamu,” alisema kocha huyo.

Thika Shakers Academy kuna vitengo tofauti vya wachezaji. Kuna chipukizi wasiozidi umri wa miaka 10, 12, 15 na 20.

Kocha Harub ana ujuzi wa hali ya juu kwa sababu amenoa klabu kadha za humu nchini.

Kocha huyo amekuwa na West Kenya Sugar FC, Kericho Zoo FC, Timsales FC ma Pioneer High School FC ya Murang’a.

Licha ya pandashuka za hapa na pale kituo hicho kinajizatiti kufanya mema katika siku zijazo.

Thika Shakers wanategemea wanasoka Martin Kazungu, Arafat Harub, Jimmy Odera, Kelvin Kinoti, John Mutua na Joseph Shonko. Wengine ni Reuben Kyali, Joseph Ng’a ng’a, Eugene Rakwar na Austin Karanu.

Anasema yeye kama kocha anajitahidi kuhakikisha soka ya vijana hawa katika eneo la Thika inaleta mshikamano baina ya wakazi.

Kocha huyo anasema kikosi chake hufanya mazoezi mara tatu kwa wiki; Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi katika uwanja wa ICT, Makongeni mjini Thika.

Anasema nidhamu ya wachezaji wa kikosi hicho ndiyo siri ya ufanisi.

“Tuko na nidhamu ya kutosha na hii huvutia wengi kutaka kucheza nasi,” akasema kocha huyo.

Raila afafanua kuhusu mkanganyiko kwenye hotuba yake

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amepuuzilia mbali madai kuwa hakufahamu kuhusu mabadiliko ndani ya ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) na mswada wa marekebisho ya Katiba.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Odinga amesisitiza Alhamisi kuwa hotuba yake katika hafla ya uzinduzi wa sahihi za kuunga mkono mswada aliyoitoa katika ukumbi wa KICC iliangazia masuala ambayo yaliibua utata katika mswada wa BBI uliozinduliwa Oktoba 26.

“Hiyo haikumaanisha kuwa Bw Odinga hakuwa na habari kuhusu marekebisho yaliyofanyiwa ripoti ya BBI na mswada wa marekebisho ya Katiba,” ikasema taarifa iliyotumwa na msemaji wa Bw Odinga, Dennis Onyango.

Kulingana Bw Odinga, hotuba yake wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika jumba la KICC, ilinuiwa kufafanua kuwa “sio mapendekezo yote, hata yangu, yalijumuishwa katika mswada wa mwisho utakaowasilishwa kwa kura ya maamuzi.”

Mojawapo ya mapendekezo yaliyopingwa ni lile linalovipa vyama vya kisiasa nafasi ya kuteua makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Pendekezo hilo liliondolewa. Lakini katika hotuba yake Bw Odinga alitetea wazo la kuruhusiwa kwa vyama vya kisiasa kuteua makamishna wa IEBC ilivyofanyika mnamo 1997.

“Uchaguzi mkuu wa 2002 utakumbukwa kama ambao ulioendeshwa kwa njia huru na haki kwa sababu baadhi ya makamishna wake waliteuliwa na Rais Moi (Daniel) na wengine wakapendekezwa na vyama vikuu vya kisiasa. Hii ilibuni mazingira ambapo makundi yote mawili ya makamishna yalikuwa yakikosoana,” akasema Bw Odinga.

TZ yararua Somalia bila huruma Cecafa ikipamba moto

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Tanzania wamefuzu kushiriki nusu-fainali ya mashindano ya soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 baada ya kunyeshea Somalia 8-1 mjini Arusha, Alhamisi.

Ngorongoro Heroes, ambao walikung’uta 6-1 katika mechi ya Kundi A na ya kufungua mashindano haya mnamo Novemba 20, walizamisha Somalia kupitia mabao ya Abdul Hamisi Suleiman dakika ya tatu, Ben Sarrkie (14), nahodha Kelvin Pius John (25, 33, 60), Kassim Haruna (47), Frank George (65) na Anuar Jabir (86). Somalia ilikuwa imesawazisha 1-1 kupitia mchezaji Sahal Muhamed dakika ya sita kabla ya kusambaratishwa kabisa.

Ijumaa itakuwa zamu ya Rising Stars ya Kenya dhidi ya Sudan katika mechi ya Kundi C. Stars ya kocha Stanley Okumbi ilianza kampeni yake kwa kucharaza Ethiopia 3-0 Novemba 23. Sudan ilipigwa 3-2 na Ethiopia katika mechi yake ya kwanza hapo Novemba 25 kwa hivyo mechi ya Ijumaa inatarajiwa kuwa moto.

Mshindi wa kundi C pia ataungana na Tanzania ambayo imeonyesha mapemamapema kuwa haitakubali taji litoke nchini humo. Kenya na Sudan zilikutana mara mbili jijini Nairobi katika mechi za kirafiki majuma matatu yaliyopita ambapo Stars waliibuka washindi kwa jumla ya mabao 5-2.

Uganda Hippos iko pazuri kufuzu kushiriki nusu-fainali kutoka Kundi B baada ya kulipua Burundi 6-1 Novemba 25. Hippos ilitoka 0-0 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi yake ya ufunguzi. Mshindi wa mashindano haya atajikatia tiketi ya kuwa nchini Mauritania kwa Kombe la Afrika la Under-20 mwaka 2021.

RATIBA NA MATOKEO:

Kundi A

Tanzania 6-1 Djibouti (Novemba 22)

Djibouti 2-1 Somalia (Novemba 24)

Somalia 1-8 Tanzania (Novemba 26)

Kundi B

Sudan Kusini 0-0 Uganda (Novemba 23)

Uganda 6-1 Burundi (Novemba 25)

Burundi na Sudan Kusini (Novemba 27)

Kundi C

Ethiopia 0-3 Kenya (Novemba 23)

Sudan 2-3 Ethiopia (November 25)

Kenya na Sudan (Novemba 27)

Nusu-fainali

Mshindi Kundi B na Mshindi Kundi C (Novemba 30)

Mshindi kundi A na timu iliyomaliza mechi za makundi ya pili kwa alama nyingi (Novemba 30)

Mechi ya kupata nambari tatu na nne (Desemba 2)

Fainali (Desemba 2)

Faith Kipyegon kuacha mbio za mita 1,500 na kuhamia mbio za mita 5,000 baada ya Olimpiki za Tokyo

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500, Faith Chepng’etich Kipyegon amefichua azma ya kuanza sasa kunogesha mbio za mita 5,000 baada ya kukamilika kwa Michezo ya Olimpili ya 2021 jijini Tokyo, Japan.

“Maazimio yangu sasa yamebadilika na ninalenga kujitosa kikamilifu katika fani ya mbio za mita 5,000 baada ya kushiriki mita 1,500 kwa mara ya mwisho kwenye Olimpiki zijazo nchini Japan,” akasema Kipyegon.

Hata hivyo, bingwa huyo wa zamani wa dunia katika mbio za mita 1,500 amesema hana maazimio ya kushiriki fani mbili tofauti kwa sambamba jinsi alivyofanya mwanariadha Vivian Cheruiyot aliyetamalaki mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kabla ya kuhamia barabarani kwa riadha za masafa marefu.

“Nikiwa mdogo, nilikuwa nikimtazama sana Cheruiyot na nikavutiwa na jinsi alivyofaulu kutamba katika fani mbili tofauti za riadha. Kwa kuwa sasa nina fursa ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wangu katika ngazi nyingine, na ninatarajia makuu,” akasema Kipyegon.

Kipyegon, 26, amejivunia mafanikio tele katika mbio za mita 1,500 – fani ambayo imemzolea dhahabu ya Olimpiki, mataji mengi ya haiba duniani, medali nyingi katika duru za Diamond League, mbio za nyika na mbio za Jumuiya ya Madola mnamo 2014 jijini Glasgow, Scotland.

Kipyegon alijivunia mojawapo ya kampeni bora kwenye ulingo wa riadha mwaka huu wa 2020 baada ya kutoshindwa kwenye mashindano matano tofauti huku akisajili muda bora wa dunia wa dakika 1:57.68 kwenye mbio za mita 800 na dakika 2:29.15 katika mbio za mita 1,000 kwenye duru ya Doha Diamond League nchini Qatar.

Kampeni za Diamond League msimu ujao kuanzia Rabat, Morocco

Na CHRIS ADUNGO

WARATIBU wa mbio za Diamond League wamefichua kalenda ya mashindano hayo katika msimu ujao wa 2021.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kampeni hizo zitajumuisha duru 14 za riadha zitakazoanzia jijini Rabat, Morocco mnamo Mei na kumalizikia Zurich, Uswisi mnamo Septemba.

Jiji la Doha nchini Qatar litakuwa mwenyeji wa duru ya Mei 28 kabla ya Roma nchini Italia kuandaa duru ya Juni 4, kisha Oslo nchini Norway (Juni 11). Duru za Stockholm, Monaco na London zimeratibiwa kufanyika katika kipindi cha majuma mawili ya mwanzo wa Julai.

Baada ya likizo ya mwezi mmoja itakayopisha Olimpiki za Tokyo nchini Japan, mashindano ya Diamond League yatarejelewa kwa duru ya Shanghai mnamo Agosti 14 kabla ya Eugene (Agosti 21) kisha China iandae duru nyingine kwa mara ya pili mnamo Agosti 22.

Duru za mwisho zitafanyika barani Ulaya katika majiji ya Lausanne, Paris na Brussels kabla ya fainali ya msimu kufanyika Zurich kati ya Septemba 8-9.

Kwa mujibu wa waandalizi wa mbio za Diamond League, ratiba iliyotolewa kwa minajili ya kampeni za msimu wa 2021 si ya mwisho na huenda ikabadilika kutegemea hali ya maambukizi ya virusi vya corona duniani.

Kutoandaliwa kwa mbio zozote za nyika hadi kufikia sasa kulichangia matokeo mseto yaliyosajiliwa na Wakenya kwenye duru mbili za ufunguzi wa kivumbi cha Diamond League mnamo 2020.

Haya ni kwa mujibu wa kocha wa timu ya taifa ya riadha, Julius Kirwa ambaye ameshikilia kwamba mbio za nyika zimekuwa zikiwapa wanariadha wa humu nchini jukwaa mwafaka la kujiandalia kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa kila msimu.

“Kihistoria, mbio za nyika zimekuwa zikiwapa Wakenya stamina na uthabiti wa kutamba katika mashindano yote mengine yanayofuatia kila msimu. Kutokuwepo kwa mbio hizo muhula huu kulichangia mseto wa matokeo yaliyoandikishwa na Wakenya jijini Monaco nchini Ufaransa na Stockholm, Uswidi,” akatanguliza.

Kilele cha msimu wa mbio za nyika mwaka huu kingekuwa kuandaliwa kwa kivumbi cha Afrika nchini Togo mnamo Aprili. Hata hivyo, janga la corona lilichangia kuahirishwa kwa mbio hizo mnamo Machi.

Bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri alitawala fani hiyo kwenye kivumbi cha Diamond League jijini Monaco (14:22.12) kabla ya kuambulia nafasi ya 11 jijini Stockholm katika mbio za mita 1,500 kwa muda wa dakika 4:10.53.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chepkoech aliibuka wa sita jijini Stockholm katika mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 14:55.01 huku Ferguson Rotich akimaliza wa nne (1:45.11) katika mbio za mita 800.

Timothy Cheruiyot ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za 1,500 ndiye wa pekee aliyedumisha umahiri wake kwa kuibuka mshindi wa fani hiyo katika duru zote mbili za Diamond League.

Ingawa hivyo, Kirwa anaamini kwamba matokeo ya Wakenya yangeimarika zaidi katika duru za Brussels, Ubelgiji (Septemba 4), Naples, Italia (Septemba 17), Doha, Qatar (Septemba 25) na China (Oktoba 17).

“Ni matumaini yetu kwamba corona itadhibitiwa vilivyo hivi karibuni ndipo tuanze msimu wa mbio za nyika kabla ya msimu ujao wa Diamond League. Hilo litawapa wanariadha, hasa katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 jukwaa mwaridhawa zaidi la kujifua pia kwa Michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan,” akasema.

RATIBA YA DIAMOND LEAGUE 2021:

Rabat – Mei 23

Doha – Mei 28

Roma – Juni 4

Oslo – Juni 10

Stockholm – Julai 4

Monaco – Julai 9

London – Julai 13

Shanghai – Agosti 14

Eugene – Agosti 21

China – Agosti 22

Lausanne – Agosti 26

Paris – Agosti 28

Brussels – Septemba 3

Zurich – Septemba 8-9

Wahudumu wa tuktuk Githurai wakarabati barabara mbovu iliyopuuzwa na viongozi

Na SAMMY WAWERU

JUMA hili limekuwa lenye shughuli chungu nzima kwa wahudumu wa tuktuk eneo la Githurai ambao wanakarabati barabara mbovu.

Chini ya muungano wa Tuktuk na magari madogo ya usafiri na uchukuzi aina ya Maruti, ndio GTMA, wahudumu hao wameikarabati barabara inayounganisha mtaa wa Githurai na Mwihoko, Kaunti ya Kiambu.

Baadhi ya sehemu katika barabara hiyo zimekuwa katika hali mbovu.

“Misongamano ya mara kwa mara na isiyoisha eneo hili na ambayo pia huathiri Thika Road, husababishwa na ubovu wa barabara hii,” Paul Kagiri msimamizi wa nidhamu GTMA ameambia Taifa Leo.

Imekuwa ratiba ya kila saa hasa eneo la Chuma Mbili, Kwa Nyanya na Kassmatt Jumbo, Githurai kushuhudia misongamano kutokana na mashimo yaliyoko katika barabara hiyo ya lami.

Wahudumu hao wamechukua jukumu la kukarabati barabara hiyo, baada ya kilio chao kwa viongozi waliochaguliwa kuwawakilisha serikalini kuonekana kupuuzwa.

“Tunawaona wakijishughulisha na Ripoti ya Maridhiano (BBI) badala ya kututatulia changamoto zinazotukumba na ambazo zilifanya tuwachague. Si mara moja, mbili au tatu tumewasilisha malalamishi yetu bila mafanikio,” akalalamika Joseph Ndung’u, mhudumu.

Kuwepo kwa mashimo, pia wanasema kunachangia kuharibika kwa tuktuk na magari mengine yanayotumia barabara hiyo.

“Isitoshe, misongamano inatupotezea wakati ambao tungekuwa tumejiendeleza kimapato na kukuza uchumi,” akasema mhudumu mwingine, akisema wakati wa mvua hali huwa mbaya zaidi.

Katika ukarabati huo, wanatumia raslimali zao kununua mawe ya kujaza kwenye mashimo, vifaa na pia kutumia magari yao kuyasafirisha.

Wahudumu wa tuktuk Githurai wakikarabati baadhi ya sehemu mbovu za barabara inayounganisha Githurai na Mwihoko, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Marekebisho hayo ni ya muda tu, na endapo serikali ya kaunti ya Kiambu na pia serikali kuu haitawajibika, huenda barabara ya Githurai – Mwihoko ikaharibika kupindukia.

Ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kuwa barabara hiyo i machoni mwa viongozi waliochaguliwa eneo hilo, wakiongozwa na diwani, mbunge na pia gavana, ambao huitumia mara kwa mara.

KCB yalenga kutikisa msimu mpya kuingia mashindano ya CAF

Na GEOFFREY ANENE

WANABENKI wa KCB wanalenga kuwa katika orodha ya klabu zitakazopeperusha bendera ya Kenya kwenye mashindano ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) msimu 2021-2022.

Kutimiza azma hiyo, kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno amesema Alhamisi kuwa KCB itajituma vilivyo katika msimu mpya wa 2020-2021 ili ipate tiketi kwa kushinda Ligi Kuu ama kubeba Kombe la Shirikisho la Soka Kenya (FKF Cup).

Mshindi wa Ligi Kuu huingia Klabu Bingwa Afrika naye bingwa wa FKF Cup hufuzu kuwakilisha nchi katika Kombe la Mashirikisho Afrika (Confederation Cup).

“Tumekuwa tukifanya mazoezi tukifuata masharti yaliyowekwa na wizara za Afya na Michezo ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Lengo letu msimu huu ni kushinda Ligi Kuu. Tusiponyakua taji la ligi, basi tutajikakamua kuibuka mabingwa wa Kombe la FKF. Tunataka kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Afrika na hakuna njia nyingine ya kufanya hivyo isipokuwa kushinda mashindano hayo,” Otieno alisema Alhamisi baada ya kuongoza vijana wake kutitiga Kibera Black Stars 3-0 katika mechi ya kupimana nguvu uwanjani Ruaraka.

Kocha huyo aliongeza kuwa KCB iko tayari kwa msimu mpya.

Amejawa imani kuwa vijana wake wanaweza kufanya ndivyo baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Bandari katika mechi yao ya mwisho kabla ya ligi kusitishwa ghafla kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona mwezi Machi.

Wakati wa kusimamishwa kwa ligi hiyo mwezi Machi, KCB ilikuwa katika nafasi ya tano baada ya kuzoa alama 41.

KCB imeratibiwa kufungua msimu mpya dhidi ya mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka uwanjani Kenyatta mjini Machakos mnamo Novemba 29. Itamenyana na Nairobi City Stars uwanjani Nyayo mnamo Desemba 4 kabla ya kufunga mwaka 2020 dhidi ya Kakamega Homeboyz mnamo Desemba 12.

Wanabenki wa KCB hawajawahi kushinda ligi. Baadhi ya wapinzani wao wakuu katika kampeni ya msimu mpya ni mabingwa wa mataji 19 Gor Mahia na washindi wa zamani AFC Leopards, Tusker, Sofapaka, Mathare United na Ulinzi Stars. Washiriki wengine kwenye ligi hiyo ni Homeboyz, Kariobangi Sharks, Zoo, Nzoia Sugar, City Stars, Bidco United, Vihiga United, Posta Rangers, Western Stima, Bandari na Wazito.

Lewandowski aongoza Bayern kupepeta Salzburg 3-1 na kufuzu kwa hatua ya 16-bora UEFA

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski alifunga bao lake la 71 katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kusaidia Bayern Munich kupiga RB Salzburg 3-1 na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya kampeni za msimu huu zikisalia mechi mbili zaidi za kupigwa kwenye hatua ya makundi.

Lewandoski ambaye ni raia wa Poland alifungua ukurasa wa mabao dhidi ya wageni wao Red Bull Salzburg kutoka Austria kunako dakika ya 42 kabla ya chipukizi raia wa Ufaransa, Kingsley Coman kuongeza goli la pili dakika 10 baadaye.

Nyota wa zamani wa Manchester City, Leroy Sane aliongeza bao la tatu kwa upande wa Bayern katika dakika ya 68, sekunde chache baada ya kiungo Marc Roca wa Bayern kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchuano wake wa kwanza wa UEFA.

Salzburg walifutiwa machozi na Mergim Berisha aliyemwacha hoi kipa Manuel Neuer katika dakika ya 73.

Chini ya kocha Hansi Flick, Bayern ambao ni mabingwa watetezi wa UEFA kwa sasa wanajivunia kushinda mechi zote nne za Kundi A ambalo pia linajumuisha Atletico Madrid na Lokomotiv Moscow.

Idadi ya mabao ambayo sasa yamefungwa na Lewandowski kwenye kipute cha UEFA inawiana na magoli yanayojivuniwa na nyota wa zamani wa Real Madrid, Raul Gonzalez.

Wawili hao wanashikilia nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika UEFA nyuma ya Lionel Messi wa Barcelona (mabao 118) na Cristiano Ronaldo wa Juventus (mabao 131)

Mbali na Lewandowski, Coman na Sane, mchezaji mwingine aliyeridhisha zaidi kwa upande wa Bayern ni kiungo wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry ambaye alichangia bao la Coman na Sane.

Licha ya kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha pili, Salzburg ambao ni miamba wa soka ya Austria, sasa hawana ushindi wowote katika kampeni za UEFA hadi kufikia sasa msimu huu na wanavuta mkia wa Kundi A.

Atletico ya kocha Diego Simeone iliambulia sare tasa katika mchuano mwingine wa Kundi A uliowakutabnisha na Lokomotiv Moscow nchini Uhispania. Bayern kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 12, saba mbele ya Atletico. Lokomotiv wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Salzburg.

Jinsi mafuriko yanavyoathiri shule zilizoko katika mitaa ya mabanda Nairobi

Na SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

SHULE nne katika mitaa ya mabanda ya Mukuru katika Kaunti ya Nairobi zitafungwa ikiwa serikali haitachukua hatua ya haraka kuzuia mafuriko yaliyosumbua kwa zaidi ya miaka mitano.

Shule hizo zinaathiriwa na mafuriko kila mwaka kutokana na unyakuzi wa ardhi katika kingo za mto Ngong.

Shule zilizoathirika ni pamoja na Shule ya Msingi St Bakhita, Shule ya Upili ya St Michael, Shule ya Upili ya Viwandani na shule ya msingi ya St Elizabeth.

Shule hizo nne ziko katika kaunti ndogo ya Makadara. Aidha, wanayakuzi wa ardhi ambao humwaga mchanga ndani ya mto na kulazimisha maji kupita kuelekea shuleni baada ya kujenga nyumba na vibanda katika kingo za mto.

“Mara tu wanapotupa tani za mchanga kwenye kingo za mto, maji husukumwa kuelekea shuleni. Hata baada ya shule hizo kulalamikia idara husika, hakuna hatua iliyochukuliwa, ’’ mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutajwa katika vyombo vya habari alisema. Jitihada kali za bodi ya usimamizi wa shule hazijazaa matunda baada ya kuripoti kwa serikali ya kaunti ya Nairobi na Mamlaka ya Kutunza Mazingira Nchini (NEMA).

Jumatano, Taifa Leo iliona ukuta wa shule katika Shule ya Msingi ya St Elizabeth baada ya ukuta wa awali kuanguka kwa sababu ya mafuriko.

Ukuta wa shule katika Shule ya Msingi ya St Elizabeth. Picha/ Sammy Kimatu

Mwaka 2019 mafuriko yalilazimisha zaidi ya wanafunzi 1,300 katika shule hiyo kukaa nyumbani. Kina cha kilikuwa takribani futi nne katika eneo yoye ya shule.

“Kila mwaka, tunalazimika kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa sababu maji hujaa kote shuleni huku nayo masomo yakivurugwa,” mwalimu mmoja wa Shule ya St Elizabeth akaeleza.

Kufuatia mafuriko, shule zinakabiliwa na gharama za ziada pia. Vivyo hivyo katika shule ya upili ya St Bakhita na St Michael, mambo sio tofauti.

Wafanyakazi walikuwa na shughuli nyingi wakijenga vizuizi vya maji nje ya ua la shule hizo ili kuzuia maji kuharibu ukuta baada ya wafanyabiashara kando ya Mto Ngong uliotamba kutoka barabara ya Likoni katika sehemu kati ya Daraja la Express kuelekea mtaa wa mabanda wa Mukuru-Maasai.

Mabwanyenye wamejenga nyumba za kukodisha na yadi za wafanyabiashara wa juakali zilizojengwa juu ya mchanga.

Mto umegeuzwa na kulazimisha maji kuelekea ukuta wa shule hizo mbili.

Uhuru aelezea matumaini ya BBI ‘kusuluhisha changamoto zote nchini’

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta amesema utaratibu wa kubadilisha katiba kupitia mpango wa BBI utasaidia kusuluhisha changamoto zilizojikita mno nchini kama vile msururu wa vurugu baada ya uchaguzi.

Rais alisema mchakato huo unanuiwa kuimarisha mfumo wa kikatiba wa Kenya kwa kurekebisha sehemu chache zilizoleta utata katika Katiba ya sasa

“Tunahitaji kuimarisha katiba ya 2010 iwapo tutaendelea na safari yetu ya miongo mingi ya kutafuta maslahi bora ya Wakenya,” akasema Rais Kenyatta alipohutubu katika jumba la KICC, Nairobi wakati wa uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji sahihi za marekebisho ya katiba kuambatana na mapendekezo ya BBI.

Alikuwa ameandamana na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Rais Kenyatta alisema hayo Jumatano katika Jumba la KICC katika Kaunti ya Nairobi ambako yeye na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walizindua mchakato wa kutia saini ili kuunga mkono marekebisho ya katiba kuambatana na mpango wa BBI.

“Tunapoanza shughuli za kutia saini, tunatambua kwamba juhudi hizi zinalenga kuhimiza mashauriano ya kidemokrasia kulingana na katiba,” akasema.

Alisema kwamba haja ya kurekebisha katiba ni dhahiri kutokana na tisho lisiloisha la vurugu baada ya uchaguzi na wasiwasi wa umma kuhusu ukosefu wa ushirikishwaji wa wote katika shughuli za serikali.

“Ukweli ni kwamba kimsingi, maisha huhitaji mabadiliko ya mara kwa mara iwapo tutatatua changamoto zetu na kutumia kikamilifu nafasi zilizoko,” akasema Rais Kenyatta akitahadharisha kwamba misimamo mikali ya katiba ni kichocheo cha vita.

Akiangazia baadhi ya mapendekezo bora katika mswada wa BBI, Rais Kenyatta alisema marekebisho hayo yatahakikisha kushiriki kikamilifu kwa wanawake katika ustawi wa kitaifa kwa kuongeza idadi yao katika taasisi za uwakilishi ikiwemo Seneti ambako watachukua asilimia 50 ya viti.

“Hii inamaanisha watasimamia jinsi tutakavyotumia asilimia 35 ya fedha ambazo zitagatuliwa katika maeneo ya kaunti,” akaeleza.

Aidha, Rais Kenyatta alisema kuna mpango mpya wa kuhakikisha uwakilishi zaidi na kamilifu wa wanawake katika Bunge la Kitaifa.

Rais Kenyatta alisema matakwa ya watu wanaoishi na ulemavu pamoja na vijana yameshughulikiwa pia kwenye marekebisho yaliyopendekezwa kwa kuhakikisha kwamba watawakilishwa kikamilifu katika bunge la kitaifa.

Makundi haya mawili yametengewa nafasi sita za uteuzi, nne za wanaoishi na ulemavu na viti viwili vya vijana.

Ili kuhakikisha kila Mkenya anafurahia demokrasia ambayo katiba ya mwaka 2010 iliahidi, Rais alisema mswada wa BBI utasuluhisha tatizo la uwakilishi usiotosha katika baadhi ya maeneo ya nchi.

“Hii itawezesha kuwepo kwa utaratibu wa haki na usawa katika ugavi wa rasilimali za kitaifa,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema mapendekezo ya BBI yatahakikisha kushirikishwa zaidi kwa umma katika viwango vyote uwakilishi kama, yaani, wadi, maeneo bunge, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa,”

Kiongozi wa Taifa pia alizungumza kuhusu manufaa ya yeye ‘kushirikiana’ na Bw Odinga, akisema hatua hiyo ilituliza taifa na kutoa nafasi ya kutambua marekebisho muhimu ambayo yataimarisha umoja, kushiriki kwa wote, usawa na maongozi bora.

Kwa upande wake, Bw Odinga aliwahimiza Wakenya kujitokeza kwa wingi na kutia saini mswada huo wa BBI kwa muda mfupi ili mchakato huo uingie katika hatua nyingine ya kuelekea kura ya maamuzi.

“Ni wakati muhimu kuwa nchini Kenya na kushiriki katika harakati za kuandika historia. Katika hatua hizi, tunashughulikia matumaini yetu wala sio hofu katika kutafuta umoja na maendeleo tunayoazimia.

“Kwa kutia saini zetu hii leo baada ya kusoma mswada huo, mwaweka alama ya kuidhinisha mchakato huo,” akasema Bw Odinga.

Miongoni mwa viongozi wa vyama waliotia saini stakabadhi hiyo ya BBI kwenye uzinduzi huo walikuwa Musalia Mudavadi (Amani National Congress-ANC), Isaac Rutto (Chama Cha Mashinani-CCM), Wafula Wamunyinyi wa Ford Kenya, Alfred Mutua wa Maendeleo Chap Chap-MCC, Gideon Moi (Kanu) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya.

Atalanta yaduwaza Liverpool kwenye UEFA ugani Anfield

Na MASHIRIKA

ATALANTA walifunga mabao mawili chini ya dakika nne za kipindi cha pili na kuwacharaza Liverpool 2-0 katika matokeo yaliyoacha wazi kampeni za Kundi D za kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kikosi cha Liverpool kilichojivunia mabadiliko mengi kilishindwa kuelekeza kombora lolote langoni pa Atalanta kwenye mchuano huo uliotandaziwa ugani Anfield mnamo Novemba 25, 2020.

Josip Ilicic aliwaweka Atalanta kifua mbele katika dakika ya 60 kabla ya Robin Gosens kufungia miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) goli la pili dakika nne baadaye.

Mohamed Salah aliyekuwa akirejea kambini mwa Liverpool kwa mara ya kwanza baada ya kukosa michuano mitatu iliyopita kwa sababu ya corona, alipoteza nafasi ya pekee aliyoipata katika dakika ya 71.

Pindi baada ya kufungwa bao la pili, kocha Jurgen Klopp wa Liverpool alifanya mabadiliko manne ya haraka kwa kuleta uwanjani Roberto Firmino, Diogo Jota, Andrew Robertson na Fabinho japo hatua yake hiyo haikuzaa matunda yoyote.

Kichapo ambacho Liverpool walipokezwa kilikuwa chao cha kwanza uwanjani Anfield tangu Septemba 2018.

Licha ya kipigwa, Liverpool bado wanasalia kileleni mwa Kundi D kwa alama tisa, mbili zaidi mbele ya Ajax na Atalanta. Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) sasa wanahitaji ushindi katika mchuano mmoja zaidi kati ya miwili ijayo dhidi ya Ajax na Midtjylland ili kufuzu kwa hatua ya mwondoano.

Klopp alilaumu waratibu wa michuano ya EPL kwa kichapo hicho walichopokezwa na Atalanta akishikilia kwamba mrundiko wa mechi katika ratiba ya kipute hicho ulichangia idadi kubwa ya majeraha na uchovu.

Kukosekana kwa wanasoka kadhaa wa haiba kubwa kambini mwa Liverpool pia kulichangia kusuasua kwa kikosi cha Klopp kilichosalia kutegemea maarifa ya chipukizi Curtis Jones, Rhys Williams na Neco Williams.

Kuchezeshwa kwa makinda hao kulifanya Liverpool kuwa kikosi cha kwanza baada ya miaka 10 kuwahi kuwajibisha matineja watatu raia wa Uingereza katika mchuano mmoja wa UEFA.

Liverpool ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Brighton katika mechi ya EPL mnamo Novemba 28, 2020, walifanyia kikosi chao kilichoshinda Leicester City 3-0 mnamo Jumapili mabadiliko matano muhimu. Miamba hao watakuwa baadaye wenyeji wa Ajax mnamo Disemba 1, 2020 ugani Anfield kwa gozi la UEFA.

Miongoni mwa wansoka wa haiba waliokosa kuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool dhidi ya Atalanta kwa sababu ya majeraha ni Trent Alexander-Arnold, Joe Gomez, Virgil van Dijk, Jordan Henderson, Xherdan Shaqiri, Naby Keita, Thiago Alcantara na Alex Oxlade-Chamberlain.

Real Madrid yadidimiza matumaini ya Inter Milan kusonga mbele kwenye gozi la UEFA

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Inter Milan kutinga hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu yalididimizwa na Real Madrid waliowapokeza kichapo cha 2-0 kwenye mchuano wa Kundi B mnamo Novemba 25, 2020, ugani San Siro, Italia.

Kiungo raia wa Chile, Arturo Vidal alionyeshwa kadi nyekundu na refa Anthony Taylor, hatua iliyoyumbisha kabisa uthabiti wa kikosi cha Inter Milan kinachonolewa na kocha Antonio Conte.

Real waliwekwa uongozini na Eden Hazard kupitia penalti ya dakika ya dakika ya saba kabla ya Achraf Hakimi kujifunga na kufanya mambo kuwa 2-0.

Matokeo hayo yalisaza Inter kwenye mkia wa Kundi B kwa alama mbili nyuma ya Shakhtar Donetsk wanaoshikilia nafasi ya tatu kwa pointi nne. Borussia Monchengladbach ya Ujerumani inashikilia nafasi ya kwanza kundini kwa alama nane, moja zaidi kuliko nambari mbili Real ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la UEFA.

Gladbach walifunga mabao matatu ya kipindi cha kwanza na kupaa hadi kileleni mwa Kundi B baada ya kuzamisha chombo cha Donetsk kwa mabao 4-0.

Real walikosa huduma za wanasoka Sergio Ramos na Karim Benzema katika mchuano huo.

Inter hawajasajili ushindi wowote katika kampeni za UEFA msimu huu na sasa wako katika hatari ya kutofuzu kwa hatua ya 16-bora ya kivumbi hicho kwa mara ya kwanza tangu 2011-12.

Ushindi wa pili mfululizo uliosajiliwa na Real dhidi ya Inter mwezi huu Novemba umewaweka karibu na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA kwa mara ya 25 katika historia.

AFYA: Ni muhimu kupumzika

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

KUTOKANA na mabadiliko ya mtindo wa maisha, watu wengi hawapati muda wa kutosha wa kupumzika.

Ni wazi kuwa wengi hawafahamu umuhimu wa kupumzika, ndiyo maana hawatengi muda wa kutosha wa kupumzika.

Ni ukweli kuwa kupumzika kuna manufaa makubwa sana kwenye miili na utendaji wetu wa kazi kila siku.

Huongeza uwezo wa kumbukumbu

Ubongo wa mwanadamu unahitaji kupumzika ili uweze kujijenga na kufanya kazi vyema. Ikiwa mtu hatapata muda wa kutosha wa kupumzika, uwezo wake wa kumbukumbu utapungua.

Huondoa hatari ya kupata kiharusi

Kiharusi ni ugonjwa unaosababishwa na kupasuka kwa mishipa midogo ya damu kwenye ubongo; hili husababisha damu kuvuja ndani ya ubongo.

Uchovu hasa ule unaoambatana na msongo wa mawazo unaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo na kisha kusababisha ugonjwa wa kiharusi.

Hulinda afya ya moyo

Kupumzika kuna manufaa makubwa kuimarisha afya ya moyo wako. Ni wazi kuwa kasi ya usukumaji wa damu wakati wa kufanya shughuli mbalimbali ni tofauti na wakati unapokuwa umepumzika.

Hivyo basi, unapopata muda wa kupumzika unaupa moyo wako nafasi ya kupunguziwa mzigo wa kusukuma damu kwa kasi, ambao umeubeba wakati ulipokuwa unafanya shughuli mbalimbali.

Hutoa muda wa mwili kujijenga

Miili yetu inahitaji kujijenga kila mara hasa baada ya shughuli nyingi. Kwa njia ya kupumzika utaweza kuupa mwili wako nafasi nzuri ya kujijenga na kurejesha tena nguvu iliyotumika wakati wa shughuli mbalimbali.

Huimarisha misuli

Tunapopumzika misuli yetu inajijenga na kurudisha ute wake uliopotea wakati wa shughuli mbalimbali. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kila baada ya kazi tunapata muda wa kutosha wa kupumzika ili tuboreshe afya za miili yetu.

Huondoa msongo wa mawazo

Chanzo kimojawapo cha msongo wa mawazo ni uchovu, na chanzo kimojawapo cha maradhi mbalimbali ni msongo wa mawazo.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha tunapumzika ili akili na fikra zetu zijisafishe na kutuepusha na tatizo la msongo wa mawazo.

Hutuwezesha kula vizuri

Ni ukweli kuwa tukiwa tumechoka hatuwezi kula vizuri. Hivyo kupata muda mzuri na wakutosha wa kupumzika kutakuwezesha kula chakula vyema.

AKILIMALI: Uuzaji samaki wawezesha mjane kujijengea ploti

Na PHYLLIS MUSASIA

BIASHARA ya kuuza samaki huonekana kawaida wa watu wengi lakini kwake Bi Consolata Achieng’ ni kazi yenye thamani.

Kwa zaidi ya miaka 15, Bi Achieng’ amekuwa akiuza aina mbalimbali ya samaki, kazi ambayo imemsaidia kuwalea wanawe baada ya kifo cha mumewe mapema 2011.

Kabla ya kuanza biashara yake mwenyewe, alikuwa ameajiriwa na mwanamke mmoja ambaye alimuuzia samaki na kupokea malipo kila siku, kulingana na kazi yake.

“Niliajiriwa kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya kuanza biashara yangu mwenyewe. Wakati huo, nilipata changamoto za mtaji na ikanibidi ninyenyekee huku nikijifunza maswala ya biashara,” akasema Bi Achieng’.

Kabla ya kuhamia Nakuru, Achieng’ aliishi Kisumu na wakati wa kazi hiyo, aliweza kutambua sehemu mbalimbali za kuagiza samaki kwa bei nafuu.

“Licha ya kwamba nilikuwa nimeajiriwa, sikuangalia mshahara tu, ila nilikuwa darasani pia kwani maono yangu ya kumiliki biashara yalisalia akilini mwangu,” akasema Bi Achieng’.

Alipogura kazi hiyo ya kibarua, Bi Achieng’ alisema alianza biashara yake kwa mtaji wa Sh1, 000 pekee, pesa ambazo alichangiwa na marafiki.

Pesa alizolipwa mbeleni likidhi mahitaji madogo ya nyumbani pekee. “Hata ingawa pesa hizo zilikuwa kidogo, wakati huo samaki wa kuagiza walikuwa bei ya chini na ilikuwa rahisi kupata faida. Nilijipa moyo na kukaza kamba,” akasema.

Baada ya mumewe kuaga dunia, Bi Achieng’ alisema hali iligeuka tofauti na maisha yakawa magumu zaidi. Majukumu yote ya nyumbani yalimlimbikizia na akalemewa kusawazisha biashara pamoja na kukimu mahitaji ya nyumbani.

Usaidizi aliopata kutoka kwa mumewe ulikuwa umeisha na ikambidi kujikakamua hata zaidi.

“Mume wangu alipoaga, watoto wetu walikuwa bado wadogo na nikachukua jukumu la kuwasomesha pamoja kukidhi mahitaji mengine kama kuwalisha kupitia biashara hii,” akasema.

Samaki wake, yeye huagiza kutoka maziwa Naivasha na Victoria, katika kaunti ya Kisumu, ambapo husafirishwa kupitia magari ya usafiri wa umma.

Bi Achieng’ huuza samaki kama vile Tilapia, Nile perch (mgogo wazi kwa njia ya mtaani), pamoja na Mad fish.

Samaki hao huletwa wakiwa bado mbichi ambapo huwakausha kwenye jua nyumbani kwake kijijini Asieko, Nakuru Magharibi.

Inapotimu mwendo wa saa kumi jioni, Bi Achieng’ hufika sokoni Soko Mjinga Takriban kilomita tano kutoka nyumbani kwake kwa ajili ya mauzo.

“Nauza samaki wakiwa wamekaangwa kwa mafuta au wakiwa freshi ukilingana na matakwa ya mteja,” akasema.

Samaki wadogo huuzwa kati ya Sh100 na Sh250 na wale wakubwa kati ya Sh300 na Sh450.

Kwa siku moja, Bi Achieng’ huuza kati ya samaki 40 na 50 au 60 wakati biashara ni nzuri.

“Faida yangu huwa tofauti kila siku kwani hutegemea nimeuza samaki wangapi. Huwa ninapata faida ya kati ya Sh5, 000 na Sh6, 000,” akasema.

Alifichua kuwa biashara hiyo imemwezesha kuweka akiba ambayo sasa hivi imejenga nyumba tano za kukodisha katika sehemu ya kando ya nyumba yake.

“Nilipojenga nyumba za kwanza mbili za kukodisha, sikutumia hela zingine ila zile zilizoweka akiba kwa muda. Nilipotaka kuongeza nyumba zaidi ndipo nilichukua mkopo katika benki na ninaendelea kulipa,” akasema.

Hata hivyo, Bi Achieng’ alisema amepitia changamoto nyingi kwenye biashara hiyo ikiwemo kupotea mzigo wa samaki wakati anapoagiza.

Mara si moja, amefika katika stendi ya magari kuchukua mzigo wake na kupata haupo licha kulipia maelfu ya pesa.

Aidha, wakati mwingine biashara huwa mbovu na kumsababishia hasara ya hali ya juu.

“Wakati fulani unapata kuwa wateja ni wachache na samaki ni wengi. Hapo huwa nakadiria hasara kubwa kwa kulazimika kutengeneza samaki hao kuwa kitoweo nyumbani,” akasema.

Changamoto nyingine Bi Achieng’ alisema ni kuchukua ni kuagiza mzigo kabla ya kufanya malipo na kisha mauzo yanakuwa ya kiwango cha chini. Wakati mwingi amelazimika kulipia mizigo kutumia pesa zake mwenyewe haswa kwa wafanyabiashara wa Kisumu ambapo samaki huwa bei ghali.

BBI: Uhuru, Raila wapuuza vilio

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga jana Jumatano walipuuza wito wa makundi mbalimbali kuwa pawepo mashauriano kuhusu ripoti ya Muafaka wa Maridhiano (BBI) kwanza kabla ya kuzindua mchakato wa ukusanyaji saini za kuidhinisha kura ya maamuzi.

Wawili hao walizindua ukusanyaji saini za wapigakura wanaounga mkono mswada wa marekebisho ya katiba, licha ya wito wa wengi kuwa pawepo fursa ya ziada ya kushauriana kuhusu vipengee kadhaa kwenye ripoti hiyo.

Vilevile, uzinduzi huo ulipuuza wito wa wananchi wengine wanaosema kuwa wakati huu kuna matatizo mengi kama vile janga la corona lililoathiri uchumi sana, ambayo yanafaa kutatuliwa badala ya kuelekeza mawazo kwa marekebisho ya katiba.

Mswada unaopendekeza marekebisho ya katiba kupitia kwa BBI, umebainisha kuwa raia huenda wakabebeshwa mzigo mzito licha ya hali ngumu ambayo tayari inawakumba.

Katika muda wote tangu ripoti ya kwanza ya BBI ilipotolewa, kulikuwa na wito kutoka kwa viongozi mbalimbali, mashirika na raia wa kawaida waliotaka baadhi ya masuala yarekebishwe kwa manufaa ya umma.

Hata hivyo, mswada uliozinduliwa jana umeonyesha kuwa marekebisho yaliyofanyiwa ripoti hiyo yanalenga zaidi kutuliza nafsi za wanasiasa ambao watategemewa kufanikisha refarenda.

Mbali na nyadhifa mpya za uongozi kama vile waziri mkuu, manaibu wake wawili na cheo cha kiongozi rasmi wa upinzani, mswada huo umeongeza idadi ya maeneobunge kutoka 290 hadi 360.

Hii ina maana kuwa Bunge la Kitaifa litakuwa na jumla ya wabunge 366, pamoja na wabunge sita ambao watateuliwa kuwakilisha makundi ya watu wenye mapungufu ya kimwili na vijana.

Katika bunge la Seneti, mswada huo unapendekeza kwamba kila kaunti iwakilishwe na maseneta wawili, mwanamume na mwanamke. Hiyo ina maana kuwa idadi ya maseneta itapanda kutoka 67 hadi 94.

Aidha, hii ina maana kuwa Wakenya watahitajika kugharimia mishahara na marupurupu ya wawakilishi hawa wakati huu ambapo uchumi wa Kenya umeathirika pakubwa na janga la Covid-19.

Japo mswada huo unapendekeza kuwa nusu ya mawaziri watatoka bungeni, umependekeza kubuniwa kwa nyadhifa za manaibu wa mawaziri. Vyeo hivyo vipya sasa vitatambuliwa kikatiba endapo Wakenya wataidhinisha marekebisho hayo ya Katiba katika kura ya maamuzi.

Kilio kingine ambacho baadhi ya wananchi walikuwa wametoa, ni kuhusu pendekezo la kubuniwa kwa Baraza la Polisi Nchini (KPC).

Baraza hilo lingesimamiwa na waziri wa Masuala ya Ndani, hatua ambayo wadau wengi waliona kuwa sawa na kuingilia uhuru wa Idara ya Polisi hasa majukumu yanayosimamiwa na Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC).

Ingawa mswada uliozinduliwa Jumatano uliondoa sehemu ya kubuni baraza hilo, kuna pendekezo kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi awe na mamlaka zaidi katika NPSC ambayo ni tume huru.

“NPSC ibadilishwe ili itambue mamlaka ya Inspekta Mkuu kama mwamrishaji mkuu wa idara ya polisi,” inasema sehemu ya mswada.

Vilevile, pendekezo tata kuhusu uteuzi wa afisi ya kupokea malalamishi kuhusu maafisa wa mahakama umepigwa msasa, ingawa bado unampa rais mamlaka ya kuteua atakayesimamia afisi hiyo.

Kulingana na mswada huu mshikilizi wa wadhifa huo sasa atateuliwa na rais kisha kuidhinishwa na Seneti.

Suala hilo liliibua pingamizi kali kutoka kwa baadhi ya viongozi wakiwemo wabunge na mawakili wakidai kuwa uteuzi wa mshikilizi wa afisi hiyo na rais utaingilia uhuru wa Idara ya Mahakama.

Mbali na hayo, sekta ya afya inayokumbwa na misukosuko mingi imeonekana kusahaulika katika mpango wa kurekebisha katiba.

Wadau katika sekta hiyo wamekuwa wakitaka kubuniwa kwa Tume ya Kitaifa ya Afya kusimamia masuala ya wahudumu wa afya, lakini hilo halijatajwa kwenye mswada wa BBI.

Miongoni mwa watakaovuna zaidi endapo mapendekezo hayo yatapitishwa ni madiwani ambao watatengewa hazina ya fedha za maendeleo. Madiwani pia wataruhusiwa kuwa mawaziri wa kaunti.

Vilevile, maseneta watapewa mamlaka ya kufanya maamuzi kadhaa ya kisheria bila kupitia Bunge la Taifa.

Kwa upande mwingine, magavana watapata afueni kuhusu bajeti kwani imependekezwa iwe kikatiba kwamba wapewe asilimia 50 ya bajeti endapo madiwani watakataa kupitisha mswada wa bajeti katika kaunti.

Kaunti 28 zimependekezwa kuongezwa maeneobunge ambapo Nairobi itapata 12, Nakuru (5), Kiambu (6), Kilifi (4), Mombasa (3) na zilizosalia kupata kati ya eneobunge moja hadi matatu.

NGILA: Blockchain kwa lugha ya Kiswahili! Heko TZ

Na FAUSTINE NGILA

JE, mbali na kung’amua kuwa nchi jirani ya Tanzania inatawaliwa na Rais John Magufuli, ni lipi lingine unalotambua kuhusu nchi hiyo?

Naam, katika ulingo wa teknolojia, Tanzania ni mojawapo ya mataifa yanayopiga hatua kubwa katika kupigia debe uvumbuzi wa kisasa.

Taifa hilo la zaidi ya watu milioni 56 limekuwa katika mstari wa mbele katika kupunguza ada ya matumizi ya intaneti Afrika. Ndilo taifa linaloongoza hapa Afrika Mashariki kwa mauzo ya intaneti ya bei nafuu kwa wananchi.

Tofauti na Kenya ambapo bei ya intaneti ni Sh112 kwa kila GB moja ya data, Tanzania watakulipisha Sh78 pekee kwa wastani, kulingana na utafiti.

Na sasa wiki iliyopita, nchi hiyo imeandika au kufasiri kitabu cha kwanza kabisa kinachoelezea teknolojia ya kisasa ya Blockchain na manufaa yake.

‘Jielimishe Kuhusu Blockchain’ ni kitabu kilichozinduliwa kwa wasomaji mnamo Novemba 20 kupitia mtandao wa kuuza bidhaa mtandaoni nchini Tanzania wa Posta Shop, kinanuia kuelezea kuhusu teknolojia hiyo kwa lugha rahisi kwa Waafrika.

Mwandishi wake, Sandra Chogo, ambaye ni mhadhiri wa masuala ya teknolojia ibuka (4IR) ameiletea Tanzania fahari tele katika ulimwengu wa teknolojia, ikizingatiwa Kiswahili huzungumzwa katika mataifa 15 barani Afrika, huku pia kikiwa na wafuasi nchini Amerika, Ujerumani, Ufaransa, Australia na mataifa ya Uarabuni.

Ingawa Kenya ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuandika kitabu kuhusu Blockchain, ilifanya hivyo kwa lugha ya Kiingereza ambayo wananchi wa mashinani hawawezi kuielewa kwa urahisi.

Ilichofanya Kenya ni majaribio ya kuunda mfumo wa lugha ya kuunda programu za kompyuta na kuchanganua data almaarufu Python kwa kutumia Kiswahili.

Lakini ikalemewa kuandika kitabu cha Kiswahili cha kuelezea wanafunzi kuhusu teknolojia hiyo.

Nimekuwa kwenye safu hii kwa miaka kadhaa sasa, na ninaweza kusema kwa imani kuwa matumizi ya blockchain ni mengi mno, na yana uwezo mkubwa zaidi ya teknolojia zote kutatua matatizo tunayoshuhudua hapa barani.

Kwa mfano, ufisadi, wizi wa kura, uuzaji wa bidhaa ghushi, wizi wa mitandaoni, leseni na vyeti feki na hila zozote zile ni visiki ambavyo vinaweza kuondolewa kwa suluhu za blockchain.

Kwa kuandika kitabu hicho kwa lugha ya Kiswahili, wananchi katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini wataweza kuona manufaa ya teknolojia katika kusuluhisha vizingiti katika maisha yao.

Changamoto kuu katika teknolojia za kisasa imekuwa jinsi zinavyoelezwa kwa Waafrika.

Waandishi wengi ni wa mabara ya Ulaya, Amerika na Asia na wamekuwa wakitumia lugha yenye maneno mazito ya Kiingereza yanayoeleweka kwa wasomaji wao.

Lakini sasa Afrika imeanza safari ya kuelezea kuhusu teknolojia nyingine kama Uchanganuzi wa Data, 5G, Uchapisho wa 3D, Teknolojia za Kiotomatiki (AI) ambazo zitapata matumizi yake hapa barani kwa upana.

Ruto amhepa Uhuru tena

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto jana Jumatano alikosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji wa sahihi za mageuzi ya katiba kupitia mchakato wa BBI katika jumba la KICC, Nairobi.

Hii ilikuwa mara yake ya pili mwaka 2020 kutohudhuria hafla iliyoongozwa na Rais licha ya waandalizi kusema alialikwa.

Mapema mwaka 2020, hakuhudhuria kongamano kuhusu janga la corona, kiti chake kikabaki wazi ukumbini.

Kiranja wa Wachache bungeni, Bw Junet Mohammed aliambaia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto alialikwa lakini “hakuthibitisha kuwa angefika.”

“Ni baada ya hapo ambapo makarani wetu waliondoa jina lake kwenye ratiba rasmi ya wanenaji,” akasema Bw Mohammed aliye mwenyekiti-mwenza wa kamati simamizi ya mchakato wa BBI.

Kiti kimoja kilichoonekana wazi baina ya Rais Kenyatta na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ilidaiwa kuwa ndicho alichotengewa Dkt Ruto.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Spika wa Seneti Kenneth Lusaka, mawaziri, magavana na wabunge wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Pia walikuwapo viongozi wa vyama vingine vya kisiasa kama vile Musalia Mudavadi (ANC), Moses Weteng’ula (Ford Kenya), Gideon Moi (Kanu), Dkt Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap) na kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyeripotiwa kusafiri ng’ambo, aliwakilishwa na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Farah Maalim.

Dkt Ruto ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa mapendekezo yaliyomo kwenye BBI alihudhuria hafla ya uzinduzi wa ripoti ya pili ya BBI Bomas mnamo Oktoba 20,2020.

Alitumia fursa hiyo kudondoa mapungufu kadha katika ripoti hiyo.

AWINO: Nani atawanusuru Wakenya dhidi ‘viriba’ vya wabunge?

Na AG AWINO

WASWAHILI husema kujaliwa leo kesho kuna Mungu.

Yaani wewe binadamu, jishughulishe tu na ya leo, ye kesho ni Mungu tu anayejua.

Waswahili hawakunena haya kwa sababu hivi ndivyo binadamu anavyostahili kuishi, ila walitaka kuangazia hatari iliyopo iwapo hujiangalii wala kujiandaa kwa maisha ya kesho ipasavyo.

Mwishoni mwa wiki, ripoti iliibuka kwamba Wabunge sasa wanataka bidhaa zote ambazo zimekubaliwa kuingia humu nchini kutoka nje zipigwe msasa ili kubaini viwango vya kemikali zilizopo kwenye bidhaa hizo.

Bunge la Kifaifa liliagiza Kamati ya Bunge inayoshughulikia Kilimo, Bodi ya Dawa za Wadudu (PCPB) na Halmashauri ya Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) kuchunguza upya kiwango cha kemikali kinachopatikana kwenye dawa za kuzuia wadudu na pembejeo.

Wanataka ripoti hii kuletwa chini ya siku 90. Lengo lao likiwa hasa kutambua bidhaa zisizohitajika katika soko la humu nchini kutokana na hatari zinazosababishwa nazo.

Habari kuhusu kemikali zinazohatarisha maisha ya Wakenya zimekuwako tangu jadi.

Mwaka 2019, ripoti ya Shirika moja la Kigeni likishirikiana na Hospitali kuu Moi ilionyesha kwamba wanawake wengi walio katika maeneo ya ukuzaji mahindi – Trans-Nzoia na Bungoma- walikuwa wakiugua saratani ya Uzazi.

Mojawapo ya sababu iliyotolewa ni kwamba mahindi waliyoyala yana kiwango cha juu cha kemikali aina ya aflatoxin ambayo imehusishwa sana na kansa ya uzazi.

Mashirika mbalimbali, aidha yamejaribu kurai wananchi dhidi ya matumizi ya kemikali za kuzuia magugu na hata pembejeo kwani zina kiwango kikubwa cha kemikali hatari.

Madai haya sasa yamethibitishwa baada ya vuta nikuvute baina ya wafanyibiashara wenye njeje nzito na wabunge kubaini kuwa wamekuwa wakichezea maisha ya Wakenya kwa sababu ya pupa wa faida.

Ripoti kwamba baada ya KEBS kutahadharisha kwamba kampuni nyingi za kimataifa zilikuwa zikileta pembejeo za viwango vya chini na zilizokuwa na kemikali hatari aina ya Cadmium, wabunge waliwekewa shinikizo na wafanyibiashara hawa mnamo 2018.

Shinikizo zilikuwa nzito sana hivi kwamba walilazimika kupiga kura kuwakubalia kuendelea kuleta pembejeo hatari yenye bei nafuu nchini.

Ingawa kiwango cha kemikali ni asilimia 15 tu, walishinikizwa kukubali pembejeo yenye asilimia 60 ya kemikali.

Nyongeza ya asilimia 45.

Kwa kuwa pembejeo na dawa za kuzuia wadudu zenye viwango vya chini vya kemikali ni ghali, waagizaji wanapenda bidhaa zenye viwango vya juu kutokana na faida kubwa wanazopata.

Wakenye wajue hawana wa kuwajali. Tangu lini ukweli wa kisayansi ukawekwa katika kura ya maamuzi? Iwapo wanasayansi wameshashema kwamba kuna hatari fulani, sharti wasikilizwe.

Hata hivyo, kutokana na ‘bahasha’ nono, kwa miaka mitatu, Wakenya wamekuwa wakitumia pembejeo ambazo zinahatarisha maisha yao.

Bado tunajiuliza ni kwa nini tuna visa vingi vya watu wanaougua saratani na wengi wao kuaga dunia?

Kwa maoni yangu, agizo hilo la Bunge ni drama na sinema ambayo kila mara huwekwa wakati bahasha ‘hazijatembea’. Aidha, ni juhudi kiduchu baada ya muda mwingi kupita. Ni sawa na kilio cha chura kisichomzuia ng’ombe kunywa maji.

Kisa hiki kinanikumbusha madhara ya bomu la kiatomiki ambalo liliangushwa Hiroshima na Nagasaki, Japan mnamo 1945. Hadi wa leo, miaka 75 baadaye, madhara ya bomu hili bado yanashuhudiwa nchini humo.

Ni nani atakayewasaidia Wakenya dhidi ya viriba vya Wabunge na waagizaji ambao wamejitajirisha sana huku mamilioni wakisafirishwa ahera?

Bw Awino ni mwanamawasiliano anayeandika kuhusu masuala ya kilimo,

gawino@kmm.co.ke

Corona yasukuma milioni 2 kwa dhiki

Na PAUL WAFULA

JANGA la corona limesukuma Wakenya milioni mbili kwa orodha ya walio maskini kwa kiasi kwamba hawawezi kumudu mahitaji ya kimsingi, ripoti ya Benki ya Dunia imefichua.

Hatua hii ni pigo kwa juhudi za kumaliza umaskini ambazo Kenya ilikuwa imepiga kwa miaka mitano huku idadi ya watu wasio na ajira ikiendelea kuongezeka.

Ripoti hiyo, ambayo sasa inathibitisha kwamba uchumi wa Kenya umeathirika vibaya, inakadiria kuwa utadorora zaidi kwa asilimia moja mwaka huu.

Tayari, uchumi umedorora kwa asilimia 5.7 katika robo ya pili ya mwaka huu na utahitaji kustawi kwa kiwango kikubwa katika muda uliosalia kubadilisha hali jambo ambalo halitawezekana katika mazingira ya sasa.

“Kote ulimwenguni, uchumi unatarajiwa kudorora 2020, na athari hizi mbaya zinaweza kuenea hadi Kenya,” inasema ripoti ya hali ya uchumi nchini Kenya ya Novemba 2020.

Ripoti inaongeza kuwa janga hili limefuta na kufifisha mafanikio ambayo Kenya ilikuwa imepiga kuangamiza umaskini kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Janga hili limeongeza umaskini kwa asilimia nne (watu milioni mbili zaidi) kwa kuathiri vibaya maisha yao, kupungua kwa mapato yao na kukosa ajira,” inaeleza ripoti iliyotolewa Jumatano.

Inasema kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimeongezeka maradufu hadi asilimia 10.4 katika robo ya pili ya mwaka huu kwa kuzingatia vipimo vya ajira vya shirka la taifa la takwimu (KNBS).

Hata wale ambao wangali kazini wamepunguziwa saa za kazi kutoka saa 50 hadi 38 kwa wiki.

Kulingana na ripoti hiyo, moja kati ya biashara za kifamilia zimekwama kwa wakati huu na mbaya zaidi ni kuwa kati ya Februari na Juni, mapato ya biashara za kifamilia yalipungua kwa takriban asilimia 50.

“Hali hii ilizidishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha ambao uliongezea watu uchungu na mateso,” inaeleza ripoti hiyo.

Karibu kampuni zote zilishuhudia mauzo yakipungua kwa asilimia 50. Ripoti inasema kwamba asilimia 93 ya kampuni zote ziliripoti kupungua kwa mauzo katika muda wa siku 30 zilizopita ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka wa 2019.

Ni asilimia mbili ya kampuni zilizoripoti kuimarika kwa mauzo na kwamba moja katika kampuni tano nchini Kenya ilipunguza idadi ya wafanyakazi.

Kufuatia hali hii, benki ya dunia imechunguza matarajio ya uchumi wa Kenya na kusema utadorora kwa asilimia moja 2020 au asilimia 1.5 hali ikiwa mbaya zaidi.

“Hatua hii imechukuliwa kwa kuzingatia hali mbaya iliyoshuhudiwa Aprili 2020, kuzingatia kwamba athari za janga hili zimekuwa mbaya zaidi kufikia sasa kuliko ilivyotarajiwa ukiwemo mchango wa sekta ya elimu kufuatia kufungwa kwa shule Machi,” ripoti inaeleza.

Hali hii ya kusikitisha inafichua kwa nini serikali ya Kenya ina presha kujadili upya milima ya madeni yake na inaomba muda zaidi wa kulipa madeni ya kimataifa ili iweze kukabiliana na athari za janga la corona.

Wanasoka wanne wa Liverpool kuwania tuzo ya FIFA ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2020

Na MASHIRIKA

WANASOKA Virgil van Dijk, Mohamed Salah, Sadio Mane na Thiago Alcantara wa Liverpool wameteuliwa kuwania taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka 2020 katika tuzo za Best Fifa Football zitakazotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Disemba 17, 2020.

Kiungo wa Manchester City, Kevin de Bruyne pia yuko katika orodha ya wachezaji 11 ambao wameteuliwa kuwania ubingwa wa taji hilo kwa upande wa wanaume.

Beki Lucy Bronze wa Man-City na timu ya soka ya wanawake nchini Uingereza pia amejumuishwa katika orodha ya wachezaji 11 wa kike watakaopigania tuzo hiyo.

Jurgen Klopp wa Liverpool na Marcelo Bielsa wa Leeds United wanakamilisha orodha ya wakufunzi watano watakaowania taji la Kocha Bora wa Mwaka. Orodha hiyo inajumuisha pia Hans-Dieter Flick (Bayern Munich ya Ujerumani), Julen Lopetegui (Sevilla ya Uhispania) na Zinedine Zidane (Real Madrid ya Uhispania).

Kocha Emma Hayes wa kikosi cha wanasoka wa kike kambini mwa Chelsea atatoana jasho na kocha Sarina Wiegman wa timu ya taifa ya Uholanzi. Wiegman anatazamiwa kutwaa mikoba ya timu ya soka ya wanawake nchini Uingereza kuanzia Septemba 2021.

Kwa mujibu wa FIFA, walioteuliwa kuwania tuzo hizo watapigiwa kura na wawakilishi 200 wa vyombo vya habari na makocha wote wa timu za taifa kote duniani kupitia mtandaoni.

Shughuli ya kupiga kura itaanza rasmi mnamo Novemba 25, 2020 na kukamilisja Disemba 9, 2020.

Bao lililofungwa na fowadi wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min dhidi ya Burnley katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 26, 2020 limeteuliwa kuwania tuzo ya Goli Bora zaidi la mwaka almaarufu ‘Puskas Award’.

Goli lililofungwa na nahodha wa timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Wales, Sophie Ingle akichezea Chelsea dhidi ya Arsenal katika Women’s Super League limeteuliwa pia kuwania taji la Puskas Award. Bao lake litashindana na lile lilifumwawavuni na fowadi wa Scotland, Caroline Weir alipokuwa akichezea Man-City dhidi ya Manchester United. Bao jingine linalopigania tuzo hiyo ni ni lile lilifumwa wavuni na Jordan Flores wa Dundalk dhidi ya Shamrock Rovers.

MCHEZAJI BORA – WANAUME:

Thiago Alcantara (Uhispania, Liverpool)

Cristiano Ronaldo (Ureno, Juventus)

Kevin de Bruyne (Ubelgiji, Manchester City)

Robert Lewandowski (Poland, Bayern Munich)

Sadio Mane (Senegal, Liverpool)

Kylian Mbappe (Ufaransa, Paris St-Germain)

Lionel Messi (Argentina, Barcelona)

Neymar (Brazil, Paris St-Germain)

Sergio Ramos (Uhispania, Real Madrid)

Mohamed Salah (Misri, Liverpool)

Virgil van Dijk (Uholanzi, Liverpool)

MCHEZAJI BORA – WANAWAKE:

Lucy Bronze (Uingereza, Manchester City)

Delphine Cascarino (Ufaransa, Lyon)

Caroline Graham Hansen (Norway, Barcelona)

Pernille Harder (Denmark, Chelsea)

Jennifer Hermoso (Uhispania, Barcelona)

Ji So-yun (Korea Kusini, Chelsea)

Sam Kerr (Australia, Chelsea)

Saki Kumagai (Japan, Lyon)

Dzsenifer Marozsan (Ujerumani, Lyon)

Vivianne Miedema (Uholanzi, Arsenal)

Wendie Renard (Ufaransa, Lyon)

KOCHA BORA – WANAUME:

Marcelo Bielsa (Argentina, Leeds United)

Hans-Dieter Flick (Ujerumani, Bayern Munich)

Jurgen Klopp (Ujerumani, Liverpool)

Julen Lopetegui (Uhispania, Sevilla)

Zinedine Zidane (Ufaransa, Real Madrid)

KOCHA BORA – WANAWAKE:

Lluis Cortes (Uhispania, Barcelona)

Rita Guarino (Italia, Juventus)

Emma Hayes (Uingereza, Chelsea)

Stephan Lerch (Ujerumani, Wolfsburg)

Hege Riise (Norway, LSK Kvinner)

Jean-Luc Vasseur (Ufaransa, Lyon)

Sarina Wiegman (Timu ya taifa ya Uholanzi)