Kanisa la Glory OutReach Assembly lazingatia kuhubiri amani

Na LAWRENCE ONGARO

KANISA la Glory OutReach Assembly lililoko Kahawa Wendani limejitolea kuendeleza na kudumisha amani kote nchini kwa kuleta jamii zote pamoja.

Mchungaji wa kanisa hilo Bi Joyce Njeri alisema kanisa hilo kwa siku za hivi karibuni limezuru maeneo yaliyokosa amani ili kuhubiri amani na kuwapa wakazi chakula cha kiroho.

Baadhi ya maeneo ambayo wamezuru ili kuhubiri amani ni Turkana, Pokot na maeneo kavu yanayohitaji mahubiri thabiti.

Bi Njeri ambaye ni mtaalam wa kisaikolojia huku pia akihubiri alisema kipindi hiki cha corona walimekuwa na shughuli nyingi za kuhubiria watu na kuwapa matumaini.

“Tulipata ya kwamba kwa muda huo mrefu ambapo janga la corona lilivamia taifa, familia nyingi zilisambaratika na hata migogoro ilizidi nyumbani. Mimi kama mtaalam wa kiakili nimefaulu kuwapa matumaini makubwa watu wa familia nyingi,” alisema Bi Njeri.

Alisema licha ya waumini wengi kufika makanisani, kuna haja zaidi ya kuwapa ushauri wa jinsi ya kukabiliana na hali ya kimaisha.

Mwishoni mwa wiki kanisa hilo liliadhimisha miaka 30 kwa kuhubiri amani katika jamii huku wakitaka pia madhehebu mengine yawe na mwelekeo huo kote nchini.

Alisema wakati huu taifa linapokaribia uchaguzi mkuu 2022 wachungaji wana jukumu la kuhubiri amani katika maeneo ya ibada kote nchini.

“Iwapo Wakenya kwa jumla watazingatia amani bila kusukumwa na mawimbi ya siasa, bila shaka ifikapo mwaka wa 2022 watakuwa na uchaguzi wa amani usio na chuki na uhasama wa kikabila,” alisema Bi Njeri.

Muumini mmoja wa kanisa hilo Sebazungu Theophile aliye raia wa Rwanda alitoa mwito kwa Wakenya wawe makini na wazingatie amani zaidi.

“Mimi baada ya machafuko ya Rwanda mwaka wa 1994 nilipata shida kubwa wakati wazazi wangu wote waliuawa kinyama mbele yangu. Ilibidi nipate usaidizi kupitia shirika moja lisilo la kiserikali,” alifafanua Theophile.

Naye Bw Mwai Muchiri mkazi wa Githurai 45, ambaye ni mshiriki katika kanisa hilo alisema baada ya kupata ushauri kupitia mchungaji Njeri amerejea maisha yake ya kawaida baada ya kukumbwa na masaibu ya kimaisha chungu nzima.

NMS kuzindua mpango wa kusafisha jiji la Nairobi na viunga vyake mara moja kwa mwezi

COLLINS OMULO na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Kuimarisha na Kustawisha Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) litazindua mpango wa kusafisha jiji na viunga vyake kila mwezi.

Mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa mwezi ujao, Februari, hasa kusaidia kuondoa mrundiko wa taka ambazo zimeendelea kutapakaa katika baadhi ya sehemu jijini.

Vilevile NMS imetoa onyo kwa wakazi wenye mazoea kutupa taka kiholela kwamba watachukuliwa hatua kisheria.

Shughuli ya kuimarisha usafi jijini itatekelezwa katika kaunti zote ndogo, 17, Nairobi, Jumamosi ya kwanza kila mwezi.

Mpango huo unajiri wakati ambapo utupaji taka kiholela umeonekana kuongezeka, suala ambalo linazua hofu kwa wakazi na kusababisha maradhi yanayohusishwa na uchafu kama vile Kipindupindu.

Kaunti ya Nairobi inakadiriwa kuwa na watu milioni tano, idadi ambayo inakisiwa kwa siku ‘huachilia’ tani 3,000 ya taka, ongezeko kutoka tani 2, 500 hapo awali.

Kwa siku, NMS hukusanya tani 2, 500 za taka. Awali, serikali ya Kaunti ya Nairobi ilikuwa ikikusanya tani 1, 000 kwa siku.

“Hivi karibuni NMS itaanza usafishaji wa Nairobi, Jumamosi ya kwanza kila mwezi,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Meja Jenerali Mohammed Badi.

Wiki iliyopita, NMS ilizindua matrela manane yatakayokusanya taka eneo la Kamukunji na Eastleigh.

Jumla ya tani 15 za taka zilizotapakaa katika majengo ya watu maeneo hayo na pia kwenye majaa zilikusanywa.

Mwaka uliopita, 2020 Meja Badi alisema wakazi wa Nairobi watahitajika kufanya usafi wa mazingira wanayoishi kila mwezi, ambapo alipendekeza kila mkazi kutenga siku moja kwa minajili ya udumishaji wa usafi.

NMS inasubiri kupata mwelekeo wa bunge baada ya kuwasilisha hoja hiyo bungeni.

Mpango wa kushirikisha wakazi kusafisha jiji la Nairobi na viunga vyake si mgeni, ikikumbukwa kuwa aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko mwaka wa 2018 alikuwa amezindua mradi wa aina hiyo.

Chini ya mradi Ng’arisha Jiji, serikali ya Bw Sonko ilikuwa ikiendesha shughuli za kukusanya taka Jumamosi ya kwanza kila mwezi, ila baada ya kuandamwa na sakata za matumizi mabaya ya ofisi na mamlaka na ufujaji wa mali ya umma, Desemba 2019, mradi huo ulisambaratika.

Mpango wa NMS pia unajiri wakati ambapo serikali ya kitaifa inaendeleza mradi wa Kazi Mtaani, uliozinduliwa 2020 baada ya mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini.

Mradi huo unaotekeleza katika kila kaunti, unashirikisha kufanya usafi wa mazingira, ambapo vijana wanafyeka nyasi kandokando mwa barabara na njia mitaani, kuzoa taka, kuzibua mitaro ya majitaka, kati ya shughuli zinginezo za usafi.

Umeajiri zaidi ya vijana 250, 000 hasa walioathirika kwa kukosa kazi kipindi cha corona.

Mitaa mingi Nairobi, ikiwemo Kariobangi, Eastleigh, Dandora, Zimmerman, Githurai, Mathare, Kibra, kati ya mingineyo inaendelea kushuhudia utupaji wa taka kiholela.

Ni hatari katika usalama wa wakazi, hasa kutokana na mkurupuko wa magonjwa yanayohusishwa na uchafu.

Itakuwa busara ikiwa NMS pia itaangazia suala la majitaka, na ambayo yanazua hatari katika mingi ya mitaa Nairobi.

Hellen Obiri alenga kuonyesha wapinzani kivumbi kwenye Mbio za Nyika za Majeshi

Na AYUMBA AYODI

MALKIA wa Mbio za Nyika Duniani Hellen Obiri analenga kuonyesha wenzake kivumbi kwenye Mbio za Nyika za Majeshi (KDF) katika uwanja wa Moi Air Base jijini Nairobi hapo Ijumaa.

Bingwa huyo wa Riadha za Dunia mbio za mita 5,000 alipoteza taji la KDF mwaka 2020. Anatumai kurejesha taji hilo na kulitwaa kwa mara ya tano pia akilenga kuhifadhi ubingwa wa taifa.

Obiri alishinda taji la KDF kwa mara ya kwanza mwaka 2014 kabla ya kufagia mataji ya mwaka 2017 hadi 2019 akitwaa umalkia wa mbio hizo kitaifa pia miaka hiyo.

Aliingia katika mabuku ya kihistoria kwa kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda mataji ya dunia ya Mbio za Ukumbini (mita 3,000), Riadha za Dunia (mita 5,000) na Mbio za Nyika (kilomita 10).

“Natamani kushinda mataji ya KDF na kitaifa tena kabla nizamie msimu wa riadha za uwanjani,” alisema Obiri, ambaye alifungua msimu kwa kutwaa taji la Mbio za Nyika mjini Machakos mnamo Novemba 28.

“Sina cha kunitia hofu wakati huu ninapojitahidi kuwa katika hali nzuri,” alisema Obiri, ambaye ataamua kushiriki mbio za mita 10,000 na mita 5,000 ama moja ya vitengo hivyo kwenye Olimpiki mjini Tokyo baadaye mwaka 2021 baada ya duru mbili za kwanza za Riadha za Diamond League mjini Rabat, Morocco (Mei 23) na Doha, Qatar (Mei 28).

“Ndoto yangu kuu ni kushinda taji la Olimpiki mwaka huu,” alisema Obiri, ambaye aliridhika na medali ya fedha ya mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki 2016 nchini Brazil.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene

TAHARIRI: Mzozo mpakani na Somalia utatuliwe

KITENGO CHA UHARIRI

USALAMA wa nchi ni moja kati ya mambo makuu ya utawala wowote ulimwenguni.

Kenya kwa upande wetu, tunailinda nchi usiku na mchana kupitia vikozi mbalimbali vya jeshi la nchi (KDF).

Hata tunapokuwa tumelala, vijana wetu wa jeshi la angani, jeshi la majini na lile la nchi kavu, hukaa imara kuhakikisha kwamba hakuna adui yeyote anayeweza kutuvamia.

Kutokana na kujitolea kwa wanajeshi wetu na kiwango chao cha juu cha nidhamu, wamewahi kualikwa katika harakati nyingi za kurejesha amani katika mataifa kama Kosovo, Sierra Leone na katika eneo la Darfur, Sudan kati ya mengine.

Usalama wa nchi yetu ni muhimu zaidi, na haifai kuuhatarisha kwa kuruhusu mahasimu kutoka taifa jirani waendeleza uhasama wao katika ardhi yetu. Mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la Somalia na lile la Jubaland karibu na mji wa Mandera, yanaiingiza nchi katika hatari ya kugeuzwa uwanja wa mapigano.

Wanajeshi wa Somalia chini ya utawala wa Rais Mohammed Abdullahi Farmaajo na wale wa Jubbaland walio watiifu kwa Rais Ahmed Madobe, walikabiliana katika mji wa Bulahawa karibu na Mandera na kuvuruga shughuli mchana kutwa.

Inasemekana kuwa wanajeshi wa Somalia wanamsaka waziri wa Usalama wa Jubbaland, Abdirashid Hassan Abdinur maarufu kama Abdirashid Janan ambaye amekuwa mafichoni mjini Mandera.

Tangu wakati huo, Bw Janan amekuwa akijipanga ili kuteka mji huo wa Bulahawa.

Inasemekana amekuwa akipokea silaha kutoka Kismayu na kuimarisha kikosi chake cha jeshi kabla ya mashambulizi ya Jumatatu.

Kwa siku yote, biashara nyingi zilisalia kufungwa mjini Mandera kutokana na makabiliano kati ya wanajeshi hao huku akina mama na watoto wakitorokea usalama wao kwenye mji wa Sufti, ambao upo mpakani mwa Kenya na Ethiopia.

Mnamo Novemba 2020 Rais Farmaajo alimshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kuandaa mkutano na Rais Madobe, akishikila kwamba Kenya ilikuwa ikimsaidia kiongozi huyo kijeshi ili kuvuruga amani na utawala wake nchini Somalia.

Ingawa Kenya haikujibu madai hayo, suala hili si la kufumbiwa macho. Umoja wa Afrika (AU) wapaswa kuchukua hatua za haraka kuingilia mgogoro huo, unaoweza kuharibu sifa ya Kenya kama kisiwa cha amani.

WANGARI: KNUT ishirikiane na serikali kuboresha maslahi ya walimu

Na MARY WANGARI

MUUNGANO wa Kitaifa wa Walimu (KNUT) umekuwa ukikabiliwa na misukosuko tele inayotishia kuuzika katika kaburi la sahau.

KNUT ambayo kwa miaka mingi iliibua fahari miongoni mwa walimu waliokuwa wanachama wake, sasa imesalia kivuli tu cha hali yake ya awali huku ikigubikwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wake.

Kuanzia ukosefu wa pesa, misururu ya kesi zinazoiandama, siasa kuhusu usimamizi zinasababisha mivutano ya kila mara kuhusu uongozi, ni bayana kwamba hali si shwari kabisa katika muungano huo.

Kando na hayo, kuchipuka kwa makundi hasimu kama vile Muungano wa Walimu wa Shule za Msingi Nchini (KUPPET), Muungano wa Walimu Wanawake Nchini (KEWOTA) na mengineyo, kumevuruga hali hata zaidi na kutishia kuvunjilia mbali kundi hilo.

Kwa kuzingatia historia ya sekta ya walimu nchini, ni vigumu kuamini kwamba miaka michache tu iliyopita, KNUT ilikuwa muungano mkuu uliozungumza kwa sauti imara na kusikika huku ukiwaunganisha walimu kote nchini.

Mwaka wa 2019 hususan ulikuwa mbaya zaidi kwa KNUT huku idadi ya wanachama wake ikipungua pakubwa kutoka zaidi ya 187,000 hadi 106,000.

Katibu Mkuu wa KNUT Wilson Sossion huenda ndiye aliyeathirika pakubwa kutokana na misukosuko katika muungano huo aliouongoza kwa muda mrefu huku akijitahidi kwa vyovyote kuzuia usizame.

Si ajabu kumwona akiwa amejawa na uchungu mwingi kila mara anapojitokeza kuzungumzia na kutetea maslahi ya KNUT.

Huku KNUT ikionekana kudidimia, Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) inaonekana kuzidi kujiimarisha na kuchukua nafasi yake.

Hali hiyo ililazimu taasisi ya Elimu Kimataifa pamoja na Muungano wa Wafanyakazi Kimataifa (ITUC) kumwandikia barua Rais Uhuru Kenyatta ukimtaka aingilie kati kuhusu masaibu ya KNUT, ni picha halisi ya jinsi mambo yalivyo.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wanahoji kwamba masaibu ya KNUT ni ya kujitakia.

Baada ya kunawiri kwa miaka mingi huku ikionekana kuwa na nguvu hata kushinda serikali inayowakilishwa na TSC, huenda KNUT ilipofushwa na ushindi wake wa kila mara.

Mashaka ya KNUT hasa yalianza 2013 huku ikionekana kushindwa kufanya kazi na serikali mpya iliyochukua usukani ambapo matokeo yake yalikuwa migomo ya kila mara ya walimu iliyotatiza sekta ya elimu.

Ni kweli kuna masuala tata yanayostahili kutatuliwa, hata hivyo, si jambo la busara kuruhusu KNUT kusambaratika kabisa.

Ni sharti usimamizi wa KNUT utilie maanani nafasi yake kama muungano wa kitaaluma, ukubali na kushirikiana na serikali katika kuboresha maslahi ya walimu.

Huenda bado kuna matumaini endapo wadau husika kutoka pande zote mbili watalegeza misimamo yao mikali na kushirikiana kutafuta suluhu.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

Mtambue ‘Madam Vicky’ wa kipindi cha ‘Maria’

Na JOHN KIMWERE

NI mwanamitindo wa muda mrefu na miongoni mwa waigizaji wanaovumisha kipindi cha Maria ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV ambapo huandaliwa na Jiffy Pictures.

Anasema alianza kujituma kwenye masuala ya maigizo bila kutarajia lakini ni talanta anayopania kuikuza zaidi. Sheila Ndanu ambaye kwa jina la msimbo (usanii) anafahamika kama Madam Vicky ameibuka kati ya vivutio vya wengi katika kipindi hicho kilichoanzishwa mwaka uliyopita.

”Ingawa nilikuwa napenda kutazama kipindi cha Mali, binafsi sikuwahi fikiria kama ipo siku nitashiriki masuala ya burudani ya uigizaji. Lakini mwaka jana ndio nilisukumwa nianze kushiriki katika kipindi hicho kama mamake Vicky,” anasema na kuongeza kuwa alianza kama mzaha lakini uigizaji umeibuka ajira kwake.

Anasema anajihisi mwenye furaha tena sana maana amebahatika kuibuka kati ya wasanii wanaoshiriki kipindi cha Maria kinachojivunia kujizolea wafuasi wengi tu ndani ya mwaka mmoja.

LYNN WHITFIELD

Katika mpango mzima anasema anatamani sana apate kazi zingine za uigizaji huku akipania kupalilia talanta yake kufikia kiwango cha kimataifa.

Anadokeza kuwa ingawa ni mgeni kwenye gemu analenga kufikia hadhi ya mwigizaji wa kimataifa mzawa wa Marekani aitwaye Lynn Whitfield aliyeshiriki filamu kwa jina Greenleaf.

‘Madam Vicky’ alipohojiwa katika ofisi za Nation Media Group. PICHA/ JOHN KIMWERE

Anadokeza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo ana imani atakuwa anatosha mboga kushiriki filamu za kimataifa. ”Nimegundua kwamba wakati wa Mungu hakuna anayeweza kuuzuia maana sikutambua kama nina talanta ya uigizaji lakini hatimaye nimejipata katika jukwaa hilo,” akasema.

KAUNTI 47

Anatoa wito kwa serikali za Kaunti zote 47 kote nchini zianzishe vituo vya kutoa mafunzo kwa waigizaji wanaokuja ili kutambua vipaji vyao mapema. Pia anasema itakuwa vyema kama serikali inaweza kuwa inafadhili wasanii wanaoibukia ili kujiunga na vyuo husika kusomea masuala ya maigizo.

Kwa waigizaji wa humu nchini Madam Vicky anasema angependa sana kufanya kazi na wasanii kama Neomi Ng’ang’a na Mary Gacheri walioshiriki filamu kama Maempress na Mali mtawalia. Barani Afrika anawazia kupanda jukwaa moja na wanamaigizo wa filamu za Kinigeria (Nollywood) kama Rita Dominic na Patience Ozokwor.

CHANGAMOTO

Madam Vicky (55) anasema mwanzoni alipitia kipindi kigumu hasa kuelewa mistari yake kulingana na maandishi. ”Ingawa nilikuwa zimezoea masuala ya wanamitindo nilipoanza uigizaji nilikuwa muoga sana. Lakini licha ya hayo tayari ninaendelea kuimarika kila uchao, sina matatizo kama mwanzoni.”

Alifunguka kuwa mwanzoni alikuwa na uoga katika uigizaji. PICHA/ JOHN KIMWERE

Anadokeza kuwa anajivunia kugundua ana talanta ya uigizaji ambapo amebahatika kutumia sehemu ya mapato yake kusaidia watoto mayatima pia waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi.

Mwigizaji huyu anashukuru serikali kwa kuhidhinisha taifa hili kuwa na mfumo wa mashirika mengi ya habari kinyume na ilivyokuwa miaka iliyopita. Hata hivyo imechangia wengi wakiwamo wanamaigizo kupata ajira kwenye vyombo vya habari nchini.

”Mfumo huo umechangia kuwepo ushindani mkubwa hali inayolenga kupaisha tasnia ya filamu nchini,” alisema na kuongeza kuwa waigizaji wa Kenya wanapiga hatua wanakolenga kufikia wenzio wa filamu za Hollywood.

Chipukizi apania kufikia upeo wa Burna Boy

Na JOHN KIMWERE

BAADA ya kukaa kimya ndani ya miaka minne iliyopita msanii ya kizazi kipya, Vincent Olsatima Athienta amerejea tena raundi hii akipania kutimiza azimio lake katika jukwaa la muziki wa burudani.

Mwanamuziki huyu ambayo kwa jina la msimbo anajulikana kama Fitty Blackboy amepania kuzamia utunzi wa nyimbo zake anakolenga kufikia hadhi ya kimataifa.

”Bila kujipigia debe ninaamini Mungu amenibariki kwa kipaji cha utunzi wa nyimbo za kizazi kipya,” alisema na kuongeza kwamba licha ya kutopiga hatua kipindi kilichopita ana imani muda wake wa kutamba utakapotimia hakuna atakayezuia.

BEDROOM

Ingawa janga la corona limezuia wanamuziki wengi kutofanya shoo zozote, ndani ya kipindi hicho anajivunia kurekodi na kuachia fataki tano. Msanii huyu ambaye hughani teke zake kwa mtindo wa Hip Hop (Swahili rap) anajivunia kuachia nyimbo kama: ‘Wikendi’ aliyoshirikisha Chris Kanya, ‘Bedroom’ (Cover) ya Harmonize aliyomshirikisha Javic Shamba.

Akishiriana na Unknown ameachia nyimbo kwa jina ‘Leo,’ bila kuweka katika kaburi la sahau teke inayozidi kutamba kwenye mitandao ya kijamii ‘Fikra’ aliyomshirikisha Jubai. Nyimbo hizo zote zimerekodiwa Wavelab Records mjini Bungoma. Anadokeza kuwa fataki hiyo imepokelewa vizuri na wafuasi wake maana ndani ya miezi miwili sasa imepata watazamaji zaidi ya 2000.

NIONYESHE NJIA

Kando na nyimbo hiyo anajivunia teke zingine kama: ‘Ndani ya fani,’ na

‘Nionyeshe Njia’ iliyopata mpenyo na kupeperushwa kupitia Televisheni ya KBC. Anasema hatua hiyo ilimtia motisha zaidi katika sekta ya muziki wa burudani. Kwa wasanii wa humu nchini analenga kifikia kiwango cha Jones Khaligraph aliyetunga vibao nyingi tu ikiwamo ‘Leave me alone,’ na ‘Gwala,’ aliyoshirikisha Ycee. Afrika analenga kukaza buti ili kutinga upeo wa msanii maarufu kwa jina Burna Boy mzawa wa Nigeria.

Kwa muziki wa Bongo anasema hupangawishwa na fataki zake msanii Fid Q hasa teke zake ‘Propaganda,’ ‘Sihitaji marafiki,’ pia hupendezwa na teke ‘Najiona mimi,’ ‘Niaje ni vipi’ utunzi wake Joh Makini.

CHANGAMOTO

Je, pandashuka gani ambazo msanii huyu hukutana nazo? “Hakika kazi ya muziki si lele mama. Mambo sio mteremko, ni tofauti kabisa na jinsi watu hudhania, gharama za kurekodi pia kuzitafutia soko nyimbo za muziki wako ni ikwazo kikubwa kwa wasanii wengi hasa wale hawajapata miziki,” anasema. Aidha anaghadhabishwa na mtindo wa baadhi ya vituo vya redio na televisheni kucheza muziki wa kigeni zaidi katika vipindi vyao.

Katika mtazamo huo anatoa wito kwa MaDJ kuzipatia nyimbo za wasanii wa nyumbani kipau mbele. Pia anawataka wasanii wa kike ambao wanaonekana kuvamia jukwaa la burudani kwa fujo kutokufa moyo bali wakaze buti na kuamini wanaweza.

Katika mpango mzima anasema bado hakuna analojivunia katika muziki lakini amejifuza mengi kimuziki na kimaisha. Katika miaka mitano ijayo anasema anataka kuwa msanii wa kuigwa na wengi wanaume kwa wanawake.

NAOMI MABEYA: Mama Kayai amekuwa chocheo kwa uigizaji wangu

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI anatosha mboga kufanya vizuri katika tasnia ya maigizo na kitinga upeo wa kimataifa miaka ijayo. Anadai kuwa amepania kujituma mithili ya mchwa ili kutimiza ndoto yake wala hatokubali chochote kuzima ndoto yake.

Naomi Mabera Mabeya maarufu kama Kemunto aliye kati ya waigizaji wanaokuja hapa nchini ni mwanafunzi wa mwaka wa nne kwenye Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

Anasema alianza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka 2017 ambapo anadhamiria kuibuka miongoni mwa waigizaji mahiri duniani kama Taraji Penda Henson aliye kati ya walioigiza kwenye kipindi cha Empire. Kando na uigizaji Kemunto anamiliki brandi yake katika mtandao wa Youtube kwa jina ‘Gusii nation TV’ aliyoanzisha mwaka 2019.

VITIMBI

“Ingawa nikiwa mtoto nilitamani sana kuhitimu kuwa wakili kama taaluma yangu maishani bado nilikuwa nashiriki uigizaji tangia nikisoma Shule ya Msingi,” binti huyo alisema na kuongeza kuwa anatamani sana kuibuka staa na kushiriki filamu za hadhi ya Hollywood na Nollywood. Katika mpango mzima anasema alivutiwa na maigizo baada ya kutazama uigizaji wake, Mama Kayai aliyekuwa akishiriki kipindi cha ‘Vitimbi’ kilichokuwa kinapeperushwa kupitia runinga ya KBC.

Anasema ndani ya miaka mitatu iliyopita amebahatika kushiriki filamu nyingi tu ambazo zimepata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga kadhaa nchini ikiwamo moja ya mtandaoni iitwayo Ndizi TV. Kati ya filamu hizo zikiwa ‘Selina,’ ‘Njoro wa uba,’ na ‘Nganya,’ (Maisha Magic East), ‘Auntie Boss (NTV) kati ya zingine. Anatoa wito kwa serikali za kaunti zote 47 zifungue vituo vya kukuza talanta za wasanii wanaokuja nchini wavulana kwa wasichana maana wamefurika wengu tu katika kila pembe mwa Kenya.

Naomi Mabera Mabeya maarufu kama Kemunto. PICHA/ JOHN KIMWERE

TOTO DIKEH

Kisura huyu anasema barani Afrika angependa kufanya kazi na waigizaji wengi tu huku akitaja baadhi yao kama: Toto Dikeh na Mercy Johnson ambao wote huigiza filamu za Kinigeria (Nollywood). Kwa wenzie wa humu nchini angependa sana kushirikiana na mcheshi anayekuja Eunice Wanjiru Njoki (Mammito) pia mwigizaji Beatrice Dorea Chege (Maggie Maria).

”Bila kupepesa macho huku na kule nashukuru wafuasi wangu kwa sapoti yao kwa kazi zangu,” alisema na kuongeza kuwa kama haingekuwa wao angefikia kiwango alicho kwa sasa katika masuala ya maigizo.

CHANGAMOTO

Anasema kuwa katika sekta ya maigizo wanapitia changa moto nyingi tu ikiwamo kukosa fedha za kugharamia shughuli zao kikazi.

”Ningependa kushauri wanawake wenzangu kuwa ni muhimu tuwe wabunifu ili kujihepusha dhidi ya changamoto za kukosa ajira. Kiukweli taifa hili lina waigizaji wengi ambapo lakini nafasi sio nyingi,” akasema.

Serikali yaweka kafyu, operesheni Kapedo

Na CECIL ODONGO

HUKU hali ya usalama ikiendelea kudorora katika eneo la Kapedo kwenye mpaka wa Kaunti za Turkana na Baringo, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amesema serikali inalichukulia eneo hilo kama la vita na itaweka kafyu ya mapema.

Kwa sasa nchi nzima ina kafyu ya kuanzia saa nne usiku hadi saa 10 alfajiri. Hata hivyo, kafyu ya Kapedo itaanza saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi.

Zaidi ya watu 10 wamefariki kutokana na uvamizi wa majangili katika eneo la Kapedo kwa muda wa mwezi moja pekee na Waziri Matiang’i pia alifichua kuwa ataweka notisi kwenye gazeti la serikali ili operesheni ya kijeshi iendeshwe eneo hilo.

“Tunataka kumalizana na huu utovu wa usalama kabisa ili eneo hilo lisalie salama. Kutimiza hilo lazima tukabiliane na majangili na viongozi wa kisiasa ambao wanahusika na ukosefu huo wa usalama,” akasema Dkt Matiang’i mnamo Jumatatu baada ya mkutano na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace aliye ziarani hapa nchini.

Hii itakuwa mara ya pili ambapo Kapedo itachapishwa kwenye gazeti la serikali kama eneo hatari zaidi kiusalama baada ya Baraza Kuu la Usalama kufanya hivyo mnamo 2017. Operesheni inayopangwa italenga Rumuruti, Ol Moran, Kirimon, Marmanet, Mukogodo Mashariki, Segera, Mithiga na Matuiku.

Mnamo Alhamisi wiki jana, polisi wawili waliokuwa wakishika doria Kapedo waliuawa kutokana na mashambulizi ya kushtukiza yaliyotekelezwa na majangili hao. Afisa huyo wa cheo cha Inspekta na dereva wake walikuwa kwenye msafara wa magari matatu, waliposhambuliwa katika daraja linalopatikana kwenye mpaka wa kaunti za Turkana na Baringo.

Siku iliyotangulia, miili ya raia sita ilipatikana ikiwa na majeraha ya risasi ikikisiwa waliuawa na majangili hao ambao pia wamekuwa wakiiba mifugo.

Tyler Onyango afurahia kuchezeshwa na Ancelotti

Na GEOFFREY ANENE

MZAWA wa Uingereza mwenye asili ya Kenya, Tyler Onyango ameelezea furaha yake kuchezea timu ya watu wazima ya Everton kwa mara ya kwanza kabisa hapo Januari 24, 2021.

Onyango, ambaye alizaliwa mjini Luton mnamo Machi 4 mwaka 2003, alipewa nafasi hiyo na kocha Mwitaliano Carlo Ancelotti katika mechi ya Kombe la FA ambayo Everton ilichabanga Sheffield Wednesday 3-0 na kuingia raundi ya 16-bora.

Muingereza Dominic Calvert-Lewin, raia wa Brazil Richarlison na raia wa Colombia Yerry Mina walifunga mabao ya Everton katika mchuano huo ambao Ancelotti aliamua kuwapa matineja Onyango, 17, na Thierry Small, 16, nafasi katika dakika 85. Onyango alijaza nafasi ya kiungo mwenzake Andre Gomes, 27, kutoka Ureno naye beki Small akaingia katika nafasi ya kiungo kutoka Colombia James Rodriguez, 29.

Onyango, ambaye Kenya inatumai atakubali kuvalia jezi ya Harambee Stars, alisema baada ya mechi kuwa analenga kutumia fursa hiyo kupiga hatua zaidi katika uchezaji wake uwanjani Goodison Park.

Ameimarika sana katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kiasi cha kusukuma Ancelotti kumjumuisha katika timu ya kwanza.

Aliingia katika timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 msimu uliopita na kujitokeza kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo msimu huu katika timu hiyo inayonolewa na David Unsworth.

Onyango amekuwa akifanya mazoezi mara kwa mara na kikosi cha Ancelotti, pamoja na Small, na alikiri kuwa alipokuwa kwenye benchi ya timu ya kwanza alikuwa ameshika roho mkononi.

“Nilijua tukiongoza kwa mabao kadhaa huenda tukapata fursa ya kuonjeshwa mechi hiyo,” alieleza runinga ya evertontv.

“Nilikuwa na wasiwasi, lakini nilipoingia uwanjani nilihisi vizuri na kufurahia.

“Nimekuwa katika klabu hii tangu niwe na umri wa miaka minane, nikajitahidi kupanda katika timu za umri tofauti, na kupata fursa ya kuchezea timu ya kwanza ni kitu kikubwa sana kwangu.

“Ukiwa mtoto, unakuja hapa Goodison, kutazama mechi ama kama watoto wa kuokota mipira (ball boy) na kukaa hapa na kuota tu.

“Ni ndoto, kwa hivyo kuingia uwanjani na kusakata kabumbu ni kitu cha kufurahia sana.

“Kupewa nafasi pamoja na kinda mwingine ambaye pia amepitia katika akademia na kusoma naye, inafanya fursa hiyo kuwa spesheli zaidi.

“Kufanya mazoezi na wachezaji hawa ni kitu cha kujivunia. Katika muda mdogo, unahisi umeimarika sana, makali yako yako juu, kasi ya mchezo wako iko juu, una nguvu za kimwili.”

Onyango alitaja beki wa pembeni kushoto Seamus Coleman, 32, na kiungo wa kati Tom Davies, 22, kuwa wachezaji ambao wamekuwa mchango mkubwa kwake tangu aanze kufanya kazi na kikosi cha watu wazima.

Hakuwa tayari kutaja makocha waliomsaidia katika safari ya kufika aliko sasa akihofia huenda akaacha mmoja nje ya orodha yake.

“Wote wamenisaidia sana kwa njia moja ama nyngine na ninashukuru kila mmoja, kutoka niingie timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka minane hadi Under-23,” alisema Onyango.

Aliongeza, “Sikulala nilipofahamu kuwa nimetiwa katika kikosi cha mechi… Ninachostahili kufanya sasa ni kuongeza bidii maradufu ili niweze kupata fursa kama hizi, kuzinyakua na kuridhisha na kufanya niweze kuaminiwa.”

Everton inashikilia nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu kwa alama 32 kutokana na ushindi 10, sare mbili na vichapo vitano.

Kingi aungama mambo si shwari kwa ODM Pwani

Na MOHAMED AHMED

KAUNTI ya Kilifi ambayo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 ilichagua viongozi wote kwa chama cha ODM, imeanza kuyumba na kuchukua mwelekeo tofauti dhidi ya kinara wa chama hicho Raila Odinga.

Kilifi ndiyo kaunti pekee nchini ambayo Gavana, wabunge, Seneta, Mbunge Mwakilishi wa Kike na wawakilishi wadi (MCAs) walichaguliwa kupitia ODM.

Lakini sasa Gavana Amason Kingi ambaye ndiye mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Kilifi, ameingia kwenye kampeni dhidi ya chama hicho, hatua ambayo itakuwa ni pigo kuu kwa Bw Odinga.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Bw Kingi alisema kuwa kwa muda sasa Pwani imekosa uwakilishi mzuri katika meza ya kitaifa, kwa sababu ya kuwakilishwa kupitia vyama vingine kikiwemo ODM.

Bw Kingi alisema hayo huku akiweka wazi kuwa hatawania tiketi yaUrais kupitia chama cha ODM.

“Mimi sitawasilisha ombi langu la kuwania kiti hicho kupitia ODM. Hilo liwe wazi kabisa. Azma ya kuwania kiti hicho bado ipo, lakini haitatimia kupitia ODM. Kwa sasa mwelekeo wangu ni kuhakikisha kuwa tunapata chama chetu cha Pwani,” akasema Bw Kingi.

Alisema kuwa mpango wake ni kuhakikisha kuwa vyama vyote ambavyo vipo Pwani vinakuja pamoja na kuwa kitu kimoja, na kusisitiza kuwa ni katika muungano huo ndipo Pwani itaweza kusikika na sio kuendelea kutegemea watu wengine kama vile imetegemea ODM kuwakilisha matakwa yake kwa muda.

Taifa Leo imegundua kuwa kuna mpango wa magavana wa Pwani pamoja na viongozi wengine kutoka kanda hiyo kukutana wiki hii ili kujadiliana kuhusiana na umoja huo wa Pwani ambao umeonekana kubabaisha viongozi.

“Ni kweli kutakuwa na mkutano wa viongozi lakini mpango wetu ni kufanya mambo bila kupiga fujo maana kuna wale maadui zetu ambao wanatishiwa na kuungana kwa Pwani. Hivyo basi, tusubiri tu ndani ya siku hizi chache na watu wetu wataona mwelekeo,” akasema Bw Kingi kuhusiana na mkutano huo ambao unatazamiwa kuleta mwelekeo mpya.

Mwito wa umoja huo umepelekea Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kujiondoa katika kumuunga mkono Bw Odinga.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana ambaye pia alipata kiti chake kupitia ODM anavutia upande wa wabunge hao wawili.

Wabunge wengine wa Kilifi akiwemo Michael Kingi (Magarini), Teddy Mwambire (Ganze), William Kamoti (Rabai) na Ken Chonga (Kilifi Kusini) wanavutia upande wa Bw Kingi na wanaunga mkono mwito wa umoja wa Pwani.

Bw Kingi alisema mpango wake ni kuvileta pamoja vyama vya Kadu Asili, Shirikisho, Umoja Summit na Devolution Party of Kenya (DPK) miongoni mwa vyengine pamoja.

Mpango huu unatazamiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu kulingana na Bw Kingi.

“Tayari tupo kwenye mazungumzo na viongozi tofauti na washikadau. Maongezi hayo yanahusisha viongozi wa vyama hivyo ambavyo vipo tayari Pwani,” akasema.

Hatua hii inatazamiwa kukisambaratisha chama cha ODM ambacho siku za hivi majuzi kilipata pigo katika kaunti ya Kwale kwa kushindwa kunyakua kiti cha Msambweni katika uchaguzi mdogo.

Kushindwa kwenye uchaguzi huo na kuja kwa mwito unaoongozwa na Bw Kingi kunakiweka pabaya chama cha ODM wakati siasa za 2022 zinapopamba moto.

Chelsea wamtimua kocha Frank Lampard baada ya miezi 18

Na MASHIRIKA

CHELSEA wamemfuta kazi kocha Frank Lampard, 42, baada ya kudhibiti mikoba yao kwa kipindi cha miezi 18 pekee.

Nafasi ya Lampard sasa inatarajiwa kutwaliwa na aliyekuwa mkufunzi wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel, aliyetimuliwa na Paris Saint-Germain (PSG) mnamo Disemba 24, 2020.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun nchini Uingereza, Chelsea wamekuwa wakimtafuta kocha anayejivunia umilisi wa lugha ya Kijerumani ili achochee matokeo bora zaidi kutoka kwa Timo Werner na Kai Havertz waliojiunga nao mwanzoni mwa muhula huu kutoka Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Lampard ambaye ni kiungo wa zamani wa Chelsea anaondoka uwanjani Stamford Bridge akiwaacha miamba hao waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya tisa kwa alama 29 kwenye msimamo wa jedwali.

Hii ni baada ya Chelsea kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Leicester katika mchuano wao uliopita ligini. Awali, kikosi hicho kilikuwa kimesajili ushindi mmoja pekee kwenye jumla ya michuano mitano mfululizo ya EPL.

Mchuano wa mwisho kwa Lampard kusimamia kambini mwa Chelsea ni ule uliowashuhudia masogora wake wakiipepeta Luton Town ya Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) 3-1 kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Januari 24 ugani Stamford Brigde.

Ushindi huo wa Chelsea ambao walizidiwa maarifa na Arsenal kwa mabao 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo 2019-20, sasa utawakutanisha na Barnsley kwenye raundi ya tano ya kipute hicho muhula huu.

Lampard aliajiriwa na Chelsea kwa mkataba wa miaka mitatu mnamo Julai 2019 baada ya kuaminiwa kuwa mrithi wa kocha Maurizio Sarri aliyeyoyomea Juventus ambao baadaye walimtimua jijini Turin baada ya msimu mmoja na kumpa mikoba kiungo wao wa zamani, Andrea Pirlo.

Katika msimu wake wa kwanza akidhibiti chombo cha Chelsea, Lampard kikosi hicho kuambulia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la EPL mnamo 2019-20 na kutinga fainali ya Kombe la FA.

Hata hivyo, Chelsea almaarufu The Blues sasa wamepoteza jumla ya mechi tano kati ya nane zilizopita ligini, idadi hiyo ikiwiana na michuano waliyopoteza kutokana na 23 mnamo 2019-20.

Lampard hakusajili mchezaji yeyote katika msimu wake wa kwanza wa ukocha kambini mwa Chelsea kutokana na marufuku iliyochochewa na hatua yao ya kukiuka kanuni za matumizi ya fedha za Uefa.

Hata hivyo, alishawishi kikosi hicho kinachomilikiwa na bwanyenye Roman Abramovich kufungulia mifereji ya fedha katika msimu wake wa pili ambapo Chelsea walitumia zaidi ya Sh30 bilioni kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za muhula huu.

Chelsea walijinasia huduma za wanasoka saba wa haiba kubwa wakiwemo Ben Chilwell aliyeagana na Leicester City kwa kima cha Sh6.3 bilioni na Kai Havertz aliyebanduka kambini mwa Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa Sh9.9 bilioni.

Hicho ndicho kiasi kikubwa zaidi cha fedha kwa Chelsea kuwahi kutumia sokoni katika muhula mmoja wa uhamisho wa wachezaji tangu walipojisuka upya kwa juma ya Sh26 bilioni mwanzoni mwa msimu wa 2017-18.

Wanasoka wengine waliosajiliwa na Chelsea mwanzoni mwa msimu huu ni Hakim Ziyech, Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Thiago Silva na Edouard Mendy.

Lampard ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Chelsea, akijivunia mabao 211 kati ya 2001 na 2014. Aidha, anashikilia nafasi ya saba kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kuwajibishwa mara nyingi zaidi na timu ya taifa ya Uingereza ambayo aliisakatia mara 106 kwa kipindi cha miaka 15 tangu 1999.

Katika kipindi cha miaka 13 ya usogora uwanjani Stamford Bridge, Lampard alichezeshwa mara 648 na akasaidia Chelsea kutia kibindoni jumla ya mataji 11 yakiwemo manne ya EPL na taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012.

Kibarua chake cha kwanza cha ukocha kilikuwa kudhibiti mikoba ya Derby County ambao kwa sasa wananolewa na kiungo wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Wayne Rooney.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Derby, Lampard aliongoza kikosi hicho kutinga mchujo wa kupanda ngazi ya kushiriki kivumbi cha EPL ila kikazidiwa maarifa na Aston Villa.

Lampard ndiye kocha wa 10 kuajiriwa kwa mkataba wa kudumu na Abramovich kambini mwa Chelsea tangu mfanyabiashara huyo maarufu mzawa wa Urusi na raia wa Israel kutwaa umiliki wa kikosi hicho mnamo 2003.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Abramovich ametumia zaidi ya Sh15 bilioni kuwafidia makocha waliowahi kufutwa na Chelsea kabla ya Lampard kupigwa kalamu.

Baada ya kukamilisha kampeni za EPL katika msimu wa 2019-20 kwa alama 66 baada ya kusajili ushindi mara 20 na kupoteza mechi 12, Chelsea kwa sasa wamepoteza michuano sita kutokana na 19 ya ufunguzi wa msimu huu wa 2020-21.

UDAKU: Neymar hapoi! Sasa amejinasia kidege Emilia wa Argentina

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA wa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr, 28, amepata hifadhi mpya ya penzi lake kwa mwanamuziki maarufu raia wa Argentina, Emilia Mernes.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, wawili hao walianza kubadilishana arafa za kimahaba baada ya Emilia kuhudhuria hafla ya kufunga mwaka 2020, iliyoandaliwa na Neymar jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Dhifa hiyo ya siku tatu iliyopagazwa jina ‘Neymarpalooza’, ilihudhuriwa na watu 500 wakiwemo wanamitindo Kiki Passo, Michelle Nevius na Jessica Bartlett kutoka Amerika. Vile vile, makahaba Camila Remedy na Fernanda Brum kutoka Brazil walikuwepo.

Siku ya mwisho Neymar alionekana akisakata densi na Emilia, 24, huku wakiimba kwa pamoja kibao cha hivi punde cha mwanamuziki huyo: “Siendi tena msituni kuwinda wakati kuna mbalamwezi. Waambie vipusa wanaokufuata kwamba mimi ni chaguo lako.”

Akihojiwa na The Sun wiki jana, Lizardo Ponce, ambaye ni rafiki wa karibu wa Emilia, alikiri kwamba Neymar alimtembelea kidege huyo nchini Argentina majuma mawili yaliyopita.

“Emilia amekuwa akimsifia sana Neymar; jinsi alimridhisha chumbani, alivyo mkarimu na pia mcheshi. Ilivyo, kilele cha urafiki wao ni ndoa. Tuwape muda; yaliyopo kati yao yatajitokeza,” akaeleza Lizardo na kuongeza kwamba dalili zote zinaashiria wawili hao wanakula bata, na haitakuwa ajabu wakivishana pete za uchumba karibuni.

Baada ya mahojiano hayo, Neymar alipakia kwenye Instagram picha yake na Emilia.

Naye kidosho huyo akajibu kwa picha nyingine akitia ‘emoji’ za furaha na kuandika: “Nakupenda kwa moyo wangu wote, na mimi huamini katika miujiza ya mwanzo bora kwa kila jambo jipya.”

Tangu Neymar atemane na mwigizaji raia wa Brazil, Bruna Marquezine, sogora huyo wa zamani wa Barcelona ametoka kimapenzi na vidosho wa kila sampuli, akiwemo mwanamitindo raia wa Amerika, Natalia Barulich.

Hata hivyo, walitengana mwanzoni mwa Desemba 2020 baada ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Brazil kuanza kumtambalia kimapenzi mwanamitindo na mwanahabari wa Uhispania, Melodie Penalver.

Awali, gazeti la Proto Thema nchini Ugiriki lilisema kwamba Neymar alikuwa radhi kuliwania upya tunda la Bruna baada ya Melodie kuanza kumfungulia mzinga mwigizaji Cristian Jerez aliyewahi kushirikiana naye kuendesha kipindi cha ‘Temptation Island’ kwenye mojawapo ya runinga za Uhispania.

Neymar amekuwa singo tangu atengane rasmi na Bruna aliyemburudisha kimapenzi kwa miaka sita. Hadi kufichuka kwa uhusiano wake na Emilia, Neymar aliwahi pia kuchovya kwenye mizinga ya warembo Liza Brito, Danna Paola, Mari Tavares, Larissa de Macedo Machado almaarufu Anitta na Ellen Santana aliyetawazwa mshindi wa Miss BumBum nchini Brazil mnamo 2018.

Penzi la Neymar limewahi pia kuwaniwa na vipusa Giovanna Lancelotti, Sabine Jemeljanova, Selena Gomez, Soraja Vucelic, Chloe Grace Moretz, Noa Saez, Izabel Goulart na Alsessandra Ambrosio.

Neymar ana mtoto mmoja wa kiume – Davi Lucca da Silva Santos aliyezaliwa na mrembo raia wa Brazil Carolina Dantas, 27, mnamo Agosti 24, 2011.

Mmoja wa mashabiki wa Emilia kwenye Instagram aliandika: “Nashawishika kuiamini safari hii ya mapenzi. Tamanio langu sasa ni kuona Neymar na Emilia wakila yamini ya ndoa.”

Man-United wadengua Liverpool katika Kombe la FA na kufuzu kukutana na West Ham kwenye raundi ya tano

Na MASHIRIKA

BAO la Bruno Fernandes kupitia frikiki ya dakika ya 78 liliwasaidia Manchester United kuwapepeta Liverpool 3-2 kwenye mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Jumapili uwanjani Old Trafford.

Liverpool ndio waliopigiwa upatu wa kushinda mechi hiyo baada ya Mohamed Salah kufuta juhudi za awali za Mason Greenwood na Marcus Rashford waliowaweka Man-United katika dakika za 26 na 48.

Vikosi hivyo vilikuwa vikivaana kwa mara nyingine wiki moja baada ya kuambulia sare tasa kwenye gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Anfield.

Dalili zote zikiashiria kwamba timu hizo zingetoshana nguvu kwa mara nyingine, Fernandes alitokea benchi na kuzidisha kasi ya mashambulizi ya Man-United na presha kutoka kwa masogora hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer ilimfanya Fabinho kumkabili Edinson Cavani visivyo nje ya kijisanduku cha penalti.

Fernandes aliyesajiliwa na Man-United kutoka Sporting CP ya Ureno kwa kima cha Sh6.6 bilioni mnamo Januari 2020, alimwacha hoi kipa Alisson Becker dakika 12 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Ushindi wa Man-United unawapa tiketi ya kuchuana na West Ham United katika raundi ya tano ya Kombe la FA msimu huu. Ni mchuano utakaomkutanisha kocha David Moyes wa West Ham na waajiri wake wa zamani, Man-United, uwanjani Old Trafford.

Liverpool walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakipania kusajili ushindi wa kwanza kutokana na mechi saba zilizopita katika mashindano yote. Mara ya mwisho kwa Liverpool wanaofunzwa na kocha Jurgen Klopp kushinda mechi ni Disemba 19 ambapo waliwapepeta Crystal Palace 7-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Selhurst Park.

Chini ya Klopp, Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa EPL, sasa wamekosa kushinda mechi yoyote kati ya tano zilizopita ligini na wametandaza jumla ya michuano minne bila kufunga bao.

Kichapo cha 1-0 kutoka kwa Burnley mnamo Januari 21, 2021 kinamaanisha kwamba ushindi wa pekee ambao umesajiliwa na Liverpool mwaka huu wa 2021 ni ule wa 4-1 waliovuna dhidi ya makinda wa Aston Villa kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 8 ugani Villa Park.

Hadi walipoangushwa na Burnley, Liverpool walikuwa wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 68 za EPL kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Anfield.

Baada ya chombo chao kuzimwa na Man-United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, mechi tano kati ya sita zijazo ambazo Liverpool watasakata ligini zitakuwa dhidi ya vikosi vinavyoshikilia nafasi saba za kwanza kufikia sasa jedwalini.

Masogora hao wa Klopp watafunga mwezi huu wa Januari dhidi ya Tottenham Hotspur na West Ham United kabla ya kupepetana na Brighton, Manchester City na Leicester City kwa usanjari huo. Baada ya kuwaendea RB Leipzig ya Ujerumani kwenye mkondo wa kwanza wa raundi ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 16, Liverpool watawaalika Everton ugani Anfield kabla ya kuchuana na Sheffield United uwanjani Bramall Lane.

Kushindwa kwa Liverpool uwanjani Old Trafford mnamo Jumapili usiku kunamaanisha kwamba kikosi hicho cha Klopp kimefaulu kusonga mbele kwenye Kombe la FA baada ya raundi ya nne mara moja pekee mnamo 2019-20.

Kwa upande wao, Man-United hawajawahi kukosa kutinga hatua ya robo-fainali za Kombe la FA tangu 2013-14.

Rekodi mbovu ya Liverpool ilichangia motisha ya Man-United walioshuka dimbani wakijivunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Watford kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA msimu huu.

Katika mashindano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu, Man-United wamepoteza mechi moja pekee kati ya 13 zilizopita tangu wabanduliwe mapema kwenye gozi la UEFA.

Walijibwaga ugani dhidi ya Liverpool wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakitoka nyuma mnamo Januari 20 na kupokeza Fulham kichapo cha 2-1 katika EPL uwanjani Craven Cottage. Ushindi huo uliwawezesha kuwaruka tena Leicester na Man-City na kurejea kileleni mwa jedwali kadri wanavyopania kutia kibindoni taji la 21 la EPL muhula huu wa 2020-21.

Licha ya rekodi nzuri katika misimu ya hivi karibuni kwenye mapambano ya kuwania mataji mbalimbali isipokuwa UEFA, Man-United wametia kapuni Kombe la FA mara moja pekee katika kipindi cha miaka 16 iliyopita.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Sheffield United katika EPL mnamo Januari 27 ugani Old Trafford huku Liverpool wakiwaendea Tottenham siku moja baadaye.

Man-United kwa sasa wamewabandua Liverpool kwenye Kombe la FA mara 10. Aidha, Liverpool wameshinda mechi moja pekee kutokana na 15 zilizopita katika mashindano yote ugani Old Trafford. Kikosi hicho kimepoteza mechi 10 na kuambulia sare mara nne na hakijawahi kushinda mechi yoyote kutokana na nane zilizopita uwanjani Trafford.

Man-United wameshinda kila mojawapo ya mechi zao nane zilizopita za Kombe la FA nyumbani huku Liverpool wakiwa mabingwa watetezi wa kwanza wa taji la EPL kubanduliwa mapema katika raundi ya nne ya Kombe la FA baada ya Man-City mnamo 2014-15.

Wazee Lamu washauri wanaume waache kutumia kiholela dawa za ashiki

Na KALUME KAZUNGU

WAZEE chini ya Baraza la Wazee Lamu wamewashauri vijana na wakongwe watumie njia za asili katika jitihada zao za kutafuta kuongeza nguvu au kuamsha hamu ya kufanya mapenzi badala ya kumeza kiholela vidonge vya kuamsha ashiki ambavyo baadaye vinasababisha madhara.

Wazee hao wameeleza kutamaushwa kwao na jinsi wanaume wanavyofariki kiholela kisha baadaye ikidaiwa walikuwa wametumia dawa hizo za kuongeza hisia za mapenzi.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Sharif Salim, alisema wakati umewadia kwa wanaume, hasa vijana kutafuta ushauri kutoka kwa wazee ili kufahamishwa mbinu za jadi na salama za kufuata katika harakati zao za kupiga jeki burudani wawapo na wapenzi wao.

Bw Salim aliwashauri wanaume kunywa supu na hata kula nyama ya pweza, mafuta na nyama ya kasa wa baharini, akisisitiza kuwa vyakula kama hivyo husaidia kuleta msisimko wa mahaba kitandani.

Pia aliwashauri vijana kuzingatia lishe bora, ikiwemo kula samaki kwa wingi katika mlo wao iwapo wanahitaji nguvu za kufanya mapenzi.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wazee pia alitaja mitishamba kama vile kungumanga ya kusaga, unywaji wa kahawa tungu na vyakula vingine vya kiasili, ikiwemo mhogo na njugu kuwa miongoni mwa lishe ambayo vijana na wanaume wa umri mkubwa wanafaa kuzingatia ili waweze kuamsha hisia za kufanya mapenzi na kuwakidhi vilivyo wawapendao.

“Zamani na hata sasa sisi tumedhibiti nguvu zetu za kufanya mapenzi kwa kutumia njia za asili ambazo ni salama na za uhakika,” akasema Bw Salim.

Alisema ni vyema wazee kwa vijana kurejelea mbinu za jadi, ikiwemo kunywa supu ya pweza, kula mafuta na nyama ya kasa wa baharini, kutumia kungumanga ya kusaga, njugu na vyakula vinginevyo ambavyo ni salama kwa afya zao.

Naibu Katibu wa Baraza hilo, Abubakar Shelali alitaja utovu wa maadili na utandawazi kuwa miongoni mwa mambo yanayosukuma jamii kufanya mambo kinyume na jadi.

Alisema kinyume na awali ambapo watu walikuwa wakianza mapenzi wakiwa na umri mkubwa wa hadi miaka 30 na zaidi, ulimwengu wa sasa umewakengeusha watu kiasi kwamba mtoto wa umri wa miaka 12 au 13 tayari anashiriki mapenzi na mwenzake wa jinsia tofauti.

Alisema hali hiyo imesababisha wanaume wa sasa kukosa nguvu wakiwa bado wadogo kiumri kutokana na kwamba tendo hilo la mahaba wamelianza mapema, hivyo kuishia kulikinai.

“Vijana wa sasa wanasukumika kutumia vidonge vya kuamsha hisia za mahaba kwani hisia hizo wanazikosa kutokana na kwamba wamekuwa wakifanya kwa muda mrefu tangia wakiwa na umri mdogo,” akasema Bw Shelali.

Wazee hao pia walitaja tabia limbukeni ya mipango mingi ya kando miongoni mwa wanaume kuwa mojawapo ya misukumo inayowafanya kuchukua hatua ya kumeza vidonge vya kuwasisimua ili kuwakidhi wapenzi wao wengi kwa wakati mmoja.

Mohamed Omar alisema anaamini iwapo watu watakuwa waaminifu katika ndoa zao, suala la wanaume kupatikana wamefariki kwa kumeza Viagra litapungua nchini na ulimwenguni.

Naye Mzee Kassim Shee aliwashauri wanaume wa sasa kuacha kuiga mambo wanayoona mitandaoni, ikiwemo picha na video za ngono na vinginevyo.

“Misukumo yote ambayo wanaume, hasa vijana wa sasa wanaishia kuifanya bila shaka wanaipata kwenye mitandao. Utamezaje vidonge vya kuamsha hamu ilhali hujaelekezwa na daktari kufanya hivyo? Lazima watu waache upotovu wa mitandao na wabaki na uhalisia wao,” akasema Bw Shee.

Matamshi ya wazee hao yanajiri wakati ambapo wataalamu wa afya nchini tayari wameonya wanaume dhidi ya kutumia vibaya vidonge vya kuamsha mahaba, ikiwemo viagra bila ya kufuata ushauri ama uelekezi wa madaktari.

Hii ni kufuatia visa kadhaa vilivyoripotiwa hivi majuzi hapa nchini na taifa jirani Tanzania na ulimwenguni kote kuhusiana na wanaume ambao inadaiwa wamefariki baada ya wao kutumia vidonge vya kuamsha hamu ya mahaba.

Msihofu, tuko tayari kujaza nafasi za wakongwe Jelimo na Jepkosgei mita 800 – Moraa

Na AYUMBA AYODI

MALKIA wa mbio za kitaifa za mita 400, Mary Moraa amewataka makocha wasiwe na wasiwasi kuhusu uwezo wa Kenya kushindania medali za mbio za mita 800 baada ya magwiji Pamela Jelimo, Janeth Jepkosgei na Eunice Sum kuondoka.

Akizungumza baada ya kuweka kasi ya juu katika mbio za mita 800 kwenye msururu wa mbio za kupokezana vijiti za Shirikisho la Riadha Kenya (AK) wikendi, Moraa alisema kizazi kipya kikiongozwa naye kiko tayari kujaza mapengo hayo.

Moraa aliahidi Wakenya makubwa katika mbio za mita 800 mwaka 2021 akitupia jicho kufuzu kupeperusha bendera ya Kenya katika mbio hizo za mizunguko miwili kwenye Olimpiki jijini Tokyo, Japan mwezi Julai/Agosti.

“Ukweli ni kuwa naona niko na siku nzuri za usoni katika mbio za mita 800 kuliko za mita 400, lakini haimaanishi kuwa nitatupilia mbali kabisa mbio za mita 400. Nitashiriki mbio za mita 400 kujipima kasi,” alisema Moraa baada ya kukamilisha mbio za mita 800 katika nafasi ya kwanza kwa muda wa dakika 2:04.92 uwanjani Nyayo. Alifuatwa unyounyo na Josephine Chelangat (2:05.11) na Emily Cherotich (2:05.95).

Moraa, 20, ambaye aliwakilisha Kenya katika mbio za mita 400 kwenye Riadha za Dunia 2019 mjini Doha, Qatar, alisema kuwa analenga kutwaa tiketi ya kushiriki Riadha za Dunia za mbio za kupokezana vijiti mjini Silesia, Poland katika kitengo cha 4×400 ama 2x2x400 zitakazofanyika Mei 1-2.

Raundi ya tatu na mwisho ya mbio za kupokezana vijiti za AK itaandaliwa ugani Nyayo mnamo Februari 6 kabla ya mchujo wa kitaifa kufanyika Machi 26-27.

“Ninachotamani sana ni kuwa na maandalizi mazuri ya mbio za mita 800. Kile naweza kueleza Wakenya nitegeeni tu! Nitajituma vilivyo kupata muda unaohitajika kufuzu na nitafanya makubwa kwenye Olimpiki za Tokyo, Mungu akipenda,” alisema Moraa ambaye alizoa medali ya fedha ya mbio za mita 400 kwenye Riadha za Dunia za makinda wasiozidi umri wa miaka 18 mwaka 2017.

“Najua makocha wetu wamejawa na hofu kuhusu maisha ya baadaye ya Kenya katika mbio za mita 800, lakini tuko tayari kujaza mapengo yaliyoachwa na magwiji kama Pamela Jelimo, Janeth Jepkosgei na Eunice Sum,” alisema Moraa akiwa amejaa imani. Moraa anajivunia muda wake bora kwenye mbio za mita 800 wa dakika 2:03.27.

Jelimo aliandikisha historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kunyakua taji la mbio za mita 800 kwenye Olimpiki mjini Beijing, Uchina mwaka 2008 na pia anashikilia rekodi ya kitaifa ya dakika 1:54.01.

Jepkosgei alizoa taji la dunia la mbio za mita 800 mjini Osaka, Japan mwaka 2007 naye Sum akatawala Riadha za Dunia mwaka 2013 mjini Moscow, Urusi.

Hapo Januari 23, Jeremiah Mutai aliibuka mshindi wa mbio za mita 800 kwa dakika 1:47.40 akifuatiwa na bingwa wa Jumuiya ya Madola Wycliffe Kinyamal (1:47.77) ambaye amerejea kwa kishindo baada ya kuwa mkekani na jeraha la mguu na maumivu ya mgongo.

Cornelius Tuwei (1:47.80) na bingwa wa dunia wa makinda mwaka 2016 Kumari Taki (1:48.03) walikamilisha mduara wa nne-bora katika kitengo cha wanaume.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene

Seneta Mwaura aitaka serikali ijenge madarasa zaidi shule za umma

Na SAMMY WAWERU

SENETA Maalum Isaac Mwaura ameihimiza serikali kutengeneza madarasa zaidi katika shule za msingi za umma ili kusaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wanafunzi.

Bw Mwaura alitoa ombi hilo kutokana na hali aliyoshuhudia baada ya kuzuru Shule ya Msingi ya Mwiki, Githurai, iliyoko katika eneobunge la Ruiru, Kiambu.

Alisema shule zenye idadi ya juu ya wanafunzi ni vigumu watoto kuzingatia kigezo cha umbali wa zaidi ya mita moja kati yao.

“Utaeleza vipi shule yenye zaidi ya wanafunzi 3,500 kama hii ya Mwiki watoto wazingatie umbali kati yao?” Seneta Mwaura akahoji.

Shule ya Mwiki ndiyo yenye idadi ya juu zaidi nchini ya wanafunzi.

Akieleza kusikitishwa na taswira ya shule hiyo hasa kutokana na upungufu wa ardhi, Bw Mwaura alipendekeza serikali kujenga mara tatu au nne zaidi ya idadi ya madarasa yaliyoko kwa sasa katika shule za umma nchini.

Shule zilifunguliwa rasmi mnamo Januari 4, 2021, miezi tisa baada ya kufungwa kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini.

Kwa sababu ya upungufu wa madarasa, ili kutii mikakati na kanuni zilizowekwa kusaidia kuzuia msambao wa corona, baadhi ya shule zimekuwa zikiendesha shughuli za masomo chini ya miti.

Benzema afunga mabao mawili na kupaisha Real Madrid hadi nafasi ya pili kwenye La Liga

Na MASHIRIKA

KARIM Benzema alifunga mabao mawili na kusaidia Real Madrid kuweka kando maruerue ya kubanduliwa mapema kwenye Spanish Cup kwa kuwakomoa Alaves 4-1 katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Real waliduwazwa na Alcoyano ya Ligi ya Daraja la Tatu nchini Uhispania iliyowadengua kwenye gozi la kuwania taji la Copa del Rey msimu huu mnamo Januari 20, 2021.

Mabingwa hao watetezi wa La Liga walichukuwa uongozi kupitia Casemiro katika 15 kabla ya Benzema na Eden Hazard kufanya mambo kuwa 3-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Ingawa Joselu Luis Mato alipania kuwarejesha Alaves mchezoni katika dakika ya 59, chombo chao kilizamishwa na Benzema kunako dakika ya 70.

Ushindi huo wa Real uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 40, saba nyuma ya viongozi Atletico Madrid ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimesakatwa na washindano wao wakuu – Real, Barcelona na Sevilla.

Kocha Zinedine Zidane hakusimamia mchuano huo kati ya Real na Alaves kwa kuwa anaugua Covid-19.

DIMBA: ‘Big Mo’ Kean ametajwa kama kizazi kipya cha Azzuri

Na GEOFFREY ANENE

BIOTY Moise Kean ni mmoja wa wanasoka makinda wanaovuma kwenye Ligi Kuu nchini Ufaransa.

Mshambuliaji huyo wa kati mwenye nguvu na kasi anachezea klabu ya Paris Saint-Germain. Anaaminiwa kuwa mmoja wa wachezaji nchi ya Italia itategemea kuinua soka yake tena.

Italia imepitia changamoto kadhaa katika soka yake ikiwemo Azzuri kukosa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 60 mwaka 2018 kutokana na talanta kupungua.

Moise yuko katika kizazi kipya cha talanta kinachotarajiwa kurejeshea Italia sifa ya kuwa miamba wa soka ambayo walikuwa wamejizolea kwa miaka nyingi.

Mwanasoka huyo aliye na asili ya Ivory Coast, anachezea PSG kwa mkopo kutoka kwa Everton inayoshiriki Ligi Kuu Uingereza.

Mamaye Isabelle Dehe na babaye Biorou Jean Kean walihamia kaskazini mwa Italia katika mji wa mjini Vercelli kutoka nchini Ivory Coast kutafuta maisha mazuri.

Walimpata Moise mnamo Februari 28 mwaka 2000. Ripoti zinasema alizaliwa kimiujiza baada ya Isabelle kuambiwa na madaktari kuwa hawezi kupata watoto zaidi.

‘Big Mo’ anavyofahamika sasa kwa jina la utani, alilelewa na mzazi mmoja: Isabelle. Wazazi wake walitengana akiwa na umri wa miaka minne. Babake alirejea Ivory Coast na mamake kulazimika kuwa yaya ili kulea familia ya watoto wawili nchini Italia.

Moise alianza uchezaji wake katika soka ya mtaani baada ya familia hiyo kuhamia mjini Asti. Alipendezwa sana na soka ya mshambuliaji wa Nigeria Obafemi Martins ambaye alikuwa mali ya Inter Milan wakati huo.

Alipiga hatua kwa sababu ya kipa wa zamani wa Torino, Renato Biasi ambaye alitambua talanta yake na kumshika mkono katika safari yake. Biasi alimuingiza katika akademia ya Asti mwaka 2007 kabla ya kumwasilisha Torino mwaka uo huo.

Moise alikuwa na Torino hadi 2010 aliponyakuliwa na miamba Juventus. Alitumia mazingira mapya kuimarisha soka yake akijiunga na timu ya watu wazima ya Juve baada ya miaka sita, ikiwemo kuifungia mabao 24 katika mechi 25 msimu 2015-2016.

Alianza soka ya malipo katika timu ya Juve mnamo Novemba 19, 2016 akitumiwa dhidi ya Pescara kama mchezaji wa akiba katika nafasi ya gunge Mario Mandzukic katika ushindi wa mabao 3-0.

Alikuwa na umri wa miaka 16, miezi minane na siku 23 wakati wa mchuano huo wa Ligi Kuu ya Serie A; umri ambao ulimfanya kuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa miaka ya 2000 kushiriki mojawapo ya ligi nne kubwa barani Ulaya.

Aliandikisha rekodi nyingine kama hiyo aliposhiriki Klabu Bingwa Ulaya siku chache baadaye timu ya Juve ikichapa Sevilla 3-1 nchini Uhispania.

Katika mechi ya mwisho msimu huo, Moise pia aliweka rekodi ya kuwa mfungaji aliyezaliwa miaka ya 2000 kupachika bao katika mojawapo ya ligi tano kubwa barani Ulaya, timu yake ya Juve ikilaza Bologna 2-1 ugenini.

Licha ya kuendelea kuimarika, Moise alipelekwa Verona kwa mkopo msimu uliofuata kabla ya kurejea Juventus kwa msimu 2018-2019 na kisha kuuziwa Everton kwa Sh3.7 bilioni kwa kandarasi ya miaka mitano.

Katika msimu wake wa mwisho na Juve, Moise alibaguliwa kwa rangi na mashabiki wa Cagliari na kutetewa na nyota Raheem Sterling, Mario Balotelli na Paul Pogba baada ya Mwitaliano mwenzake Leonardo Bonucci kudai kinda huyo alichangia katika kubaguliwa kwake.

Hakufanya vizuri katika mechi 33 alizopewa uwanjani Goodison Park katika mashindano yote msimu 2019-2020 na kuelekea PSG kwa mkopo msimu huu.

Amejitokeza kuwa mojawapo wa wachezaji wazuri kwenye Ligue 1. Alianza msimu huu Everton kabla ya kuelekea PSG mnamo Oktoba 4, 2020.

Moise, ambaye aliwahi kumezewa mate na Manchester City na Arsenal, yuko katika vuta-nikuvute na PSG inayotaka aendelea kuwa naye huku Juve ikitaka kumnunua tena. Bei yake sokoni ni Sh4.7 bilioni.

Moise amelinganishwa kimchezo na Balotelli, ambaye pia wanatumia wakala mmoja Mino Raiola.

Kinda huyo anatoka katika familia ya wanasoka. Kakake mkubwa Giovanni Kean Dosse, 27, ni mshambuliaji wa kati wa US Termoli 1920. Pia ana binamu wawili wanaosakata soka ya kulipwa. Mshambuliaji wa kati Massimo Goh, 21, anayechezea Marignanese Calcio katika moja ya ligi ndogo za nchini Italia. Kisha beki Abdoulaye Bamba, 30, wa timu ya Angers inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

WARUI: Hatua ya dharura yahitajika kuzima utovu wa nidhamu shuleni

Na WANTO WARUI

TANGU kufunguliwa kwa shule mwezi huu wa Januari, visa kadha wa kadha vya utovu wa nidhamu vimetokea shuleni vikisababishwa na wanafunzi.

Kuna tetesi katika shule nyingi kuwa wanafunzi wamepoteza mwelekeo na hali yao ya nidhamu ni mbaya.

Kisa kilichotokea kule Kisii cha mwanafunzi wa kidato cha tatu kuwadunga visu walimu wake wawili ni cha kuatua moyo. Mwanafunzi huyu ambaye alikuwa amechelewa kufika gwarideni aliulizwa na mwalimu sababu ya kuchelewa. Alipoambiwa apige magoti, alienda kwenye bweni akachukua kisu ambacho alitumia kumdunga mwalimu huyo. Mwalimu wa pili naye alidungwa akijaribu kumsaidia mwenzake.

Juma lililopita, mwanafunzi wa miaka 17 wa shule ya Wavulana ya Wahundura, Mathioya katika kaunti ya Murang’a alifikishwa katika hospitali kuu ya Kenyatta kupata matibabu ya dharura baada ya kudungwa kisu na mwanafunzi mwenzake. Mwanafunzi huyo, Simon Muchunu, anasemekana kuwa alidungwa kisu kichwani na mwenzake wa kidato cha tatu baada ya kugombana kuhusu kufuli.

Kwingineko, mwanafunzi wa Gredi ya 4 katika shule ya msingi ya Kegati, Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii alijaribu kumuua baba yake kwa kumtilia sumu kwenye uji. Baba yake mwanafunzi huyo alikuwa amemwuliza kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na mwanafunzi mwingine wa Kidato cha Nne ambapo mtoto huyo alikasirika.

Visa hivi na vingine vingi ambavyo vinajitokeza, vinatuchorea taswira ya jinsi ambavyo utovu wa nidhamu umeshamiri miongoni mwa wanafunzi. Pana haja ya washika dau wa elimu ikiwemo Wizara ya Elimu, wazazi na walimu kuharakisha kutafuta mbinu mwafaka za kukabiliana na hali hii kabla mambo hayatumbukia nyongo.

Kipindi kirefu ambapo wanafunzi wamekaa nyumbani kutokana na athari ya mkurupuko wa gonjwa la Covid-19, kimesababisha hasara kubwa sana kwa wanafunzi. Wazazi wengi walishindwa kuwadhibiti watoto wao na kuwaacha wafanye watakavyo.

Wasichana wengi walijiingiza katika mapenzi ambayo yaliishia kwa mimba na maradhi ya zinaa. Wavulana nao waliingilia tabia za kihuni kama matumizi ya dawa za kulevya, wizi na ukora mwingine.

Ilivyo sasa shuleni, walimu wanakabiliwa na hali ngumu ya kudhibiti nidhamu. Wanafunzi walio shuleni sasa sio wale waliokuwamo miezi tisa iliyopita. Wamebadilika kabisa. Wengi wao wamepotoshwa, asilimia kubwa ikikosa maadili.

Pia ni muhimu walimu wawe macho sana ili kuzuia vifaa visivyotakikana shuleni kama vile visu kuingizwa ndani ya maeneo ya kusomea.

Wazazi, ambao inathibitika sasa kuwa wametelekeza wajibu wao wa malezi hawana budi kuinuka na kufanya jinsi wanavyotakiwa kufanya.

Mambo haya yote ambayo yanatokea yanaonyesha kuwa kunahitajika njia mpya na za haraka za kukabiliana na utovu wa nidhamu shuleni ikiwemo mashauriano miongoni mwa nyingine.

ONYANGO: Ushauri nasaha ndio dawa ya matatizo ya akili, mauaji

Na LEONARD ONYANGO

VISA vingi vya mauaji na watu kujitoa uhai ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika vyombo vya habari hivi karibuni havifai kupuuzwa.

Mauaji hayo yanaogofya na yanaweza kuwa kidokezo tu kuhusu madhara ya janga la virusi vya corona kwa afya ya akili.

Ndani ya mwezi mmoja uliopita, kumeripotiwa visa tele vya watoto kuua au kujaribu kuua wenzao, wazazi wao au walimu. Kadhalika, kumekuwa na ripoti nyingi za watu wazima kuua au kujaribu kutekeleza mauaji huku wengine wakijitoa uhai.

Kisa cha hivi karibuni ni cha afisa wa polisi wa kituo cha Nguruki, Kaunti ya Tharaka Nithi ambaye alhamisi mwili wake ulipatikana ukining’inia katika nyumba ya jirani.

Kwa mujibu wa polisi, afisa huyo wa polisi wa umri wa miaka 35, alijaribu kujikata shingo kabla ya kujinyonga.

Siku hiyo hiyo, wakazi wa mtaa wa Njiru, Kasarani, Kaunti ya Nairobi walipigwa na mshtuko baada ya Margaret Muchemi kuuawa na kisha mwili wake kuteketezwa na mwanaume anayeaminika kuwa mpenzi wake.

Maafisa wa polisi wiki iliyopita, walikamata mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Kaunti ya Bomet kwa madai ya kushambulia mwanafunzi mwenzake wa kike kwa panga.

Mauaji ambayo yamezua gumzo nchini ni yale yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi huu, ambapo Nicholas Njoroge, 55, mkewe, watoto wawili na mfanyakazi waliuawa kinyama katika eneo la Kagongo Karura, Kiambaa, Kaunti ya Kiambu.

Mwana wao Lawrence Simon Warunge ni miongoni mwa washukiwa wakuu wa mauaji hayo.

Jumatatu iliyopita, polisi walinasa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kwa madai ya kushambulia na kuua mlinzi wa shule yao katika Kaunti ya Vihiga.

Kulingana na polisi, mwanafunzi huyo alimuua mlinzi alipojaribu kuingilia kati alipokuwa akiwashambulia wanafunzi wenzake.

Wikendi iliyopita, polisi walikamata Christopher Mburu Wakahiu, 26, kwa madai ya kuua ndugu yake kwa kumdunga kisu katika eneo la Murang’a.

Pasta wa zamani Joel Mogaka, alinaswa wiki mbili zilizopita kwa madai ya kuua mkewe na kisha kupeleka mwili wake katika mochari.

Visa hivyo vyote na vingine vingi ni ishara kwamba kuna tatizo ambalo linafaa kushughulikiwa kwa haraka.

Tafiti ambazo zimefanywa katika mataifa mbalimbali zinaonyesha kuwa janga la virusi vya corona limechangia pakubwa katika kuongezeka kwa visa vya matatizo ya akili. Matatizo hayo yanachangiwa na msongo wa mawazo.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO), ilionyesha kuwa janga la virusi vya corona limeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wanaohitaji huduma za afya ya akili.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa mataifa mengi ya Afrika, ikiwemo Kenya, hayajachukulia kwa uzito suala la huduma za afya ya akili.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa watu wanne hujitoa uhai kila siku nchini Kenya kutokana na matatizo ya akili.

Visa vya watu kujitoa uhai na kuangamiza wengine huenda vikaongezeka mwaka huu iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kuhamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kutafuta huduma za ushauri nasaha. Serikali inafaa kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata huduma za ushauri nasaha kwa bei nafuu.

TAHARIRI: Dawa za nguvu za kiume zidhibitiwe

KITENGO CHA UHARIRI

SUALA la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kushiriki mapenzi, linahitaji mjadala wa kitaifa, ili kuepusha jamii kuangamizwa na utumzi mbaya wa dawa hizo.

Japokuwa lilianza kama uvumi, imebainika kuwa kweli kuna wanaume ambao wamefariki dunia baada ya kutumia vidonge vya kuwaongeza ashiki. Dawa hizo ambazo hupatikana kwa njia rahisi kwenye maduka ya dawa, sasa zimekuwa njia rahisi zaidi ya mauti, hata kushinda maradhi hatari.

Kinachosikitisha ni kwamba, hata baada ya watu kusikia habari za wenzao kufa kwenye magesti, uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umeonyesha kuna ongezeko kubwa la wanaume wanaozitafuta.

Wasichofahamu ni kwamba dawa hizo zinazofahamika kwa majina mengi likiwemo la Viagra, husaidia kusukuma damu kwa kasi. Msukumo huo ukiongezwa na nguvu zinazotumika, humfanya mtu kuwa kama aliyekimbia masafa ya mbio za Eliud Kipchoge. Katika maisha halisi, wanaume wengi huwa hawafanyi mazoezi ya kwenda kasi au urefu kama huo.

Wataalamu wa afya wanasema jambo hilo ni hatari, kwa kuwa damu huchemka kupita kiasi na kuna uwezekano mkubwa wa kupasuka mishipa muhimu, kama vile ya kwenye moyo au ubongo na kusababisha kifo.

Kinachohitajika sasa ni mazungumzo wazi kutoka kwa maafisa wa wizara ya Afya kuhusu madhara ya kutumia dawa hizi.

Serikali yapaswa kuanzisha kampeni sawa na ya kudhibiti maambukizi ya corona. Watu wahimizwe kufanya mazoezi, wale vyakula asili na wasijihusishe na vitendo vinavyoweza kuchangia kupungua kwa nguvu za kiume.

Viongozi wa kidini wahamasishe waumini kuhusu amri za kujiepusha na kushiriki mapenzi nje ya ndoa. Takwimu zote kufikia sasa zinaonyesha waliofariki kwenye tendo hilo hawakuwa katika nyumba zao. Ina maana kuwa walitumia dawa hizo kuonyesha ushujaa usiokuwa na maana kwa afya zao.

Bunge lina jukumu la kubuni kanuni za kudhibiti uuzaji na usambazaji wa dawa hizo. Hata kama kweli wanaume wanazihitaji, iwapo zitakuwa hazipatikani kwenye maduka ya dawa, basi hawatazinunua.

Mojawapo ya kanuni hizo iwe ni kuruhusu kuuzwa kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume kupitia barua ya daktari pekee. Daktari atakuwa amempima mgonjwa na kuelewa hali yake ya kiafya kama presha, sukari, kati ya maradhi mengine.

Suala la kukuza miwa bondeni laibua mzozo

Na BARNABAS BII

MGOGORO unatokota kati ya Wizara ya Kilimo na wakulima wa mahindi katika kaunti zinazokuza mahindi eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, ambalo ni kituo kikuu cha chakula nchini.

Hii ni kuhusu mipango ya kuanzisha sheria zitakazowazuia wakulima hao kuwekeza katika kilimo cha mazao ya kuuzwa kama vile miwa.

Serikali za kaunti katika maeneo yanayofahamika kwa ukuzaji wa nafaka tangu jadi ya Uasin Gishu, Nandi naTrans Nzoia zimeanzisha sera za kilimo zinazowazuia wakulima wa ngano na mahindi dhidi ya kupanua kilimo cha miwa.

Kaunti hizo zimewasilisha idhini kutoka makao makuu ya Wizara ya Kilimo zitakazohakikisha kwamba kilimo cha miwa hakitachukua nafasi ya kilimo cha mbegu za mahindi hivyo kutishia hali ya kuwepo chakula cha kutosha nchini.

Wakulima wengi wa nafaka katika Kaunti za Nandi, Uasin Gishu na Trans-Nzoia wanapanua mashamba yanayokuziwa miwa na kuibua wasiwasi kutoka Wizara ya Kilimo.

Serikali za kaunti zinataka kuanzishwe sheria kuhusu kilimo cha miwa katika maeneo yanayokuzwa mahindi.

Gavana wa Trans Nzoia Patrick Khaemba alisema licha ya juhudi kali za serikali za kuwataka wakulima kupanda aina nyingine ya mazao kando na mahindi, hatakubali kuanzishwa kwa kilimo cha miwa.

“Mwanzo wa kilimo ni katika kiwango cha mbegu na iwapo wakazi wataanza ukuzaji wa miwa, tutapoteza mwelekeo wetu kuhusu uzalishaji wa mbegu za mahindi zilizoidhinishwa,” alifafanua Bw Khaemba, huku akifichua mipango ya serikali ya kubadilisha sheria kuhusu kilimo cha zao hilo.

“Maajenti wa kilimo cha miwa ni maajenti wa ufukara vilevile. Mnaweza kuona waziwazi maisha ya taabu ya wakazi katika maeneo yanayokuza miwa,” alisema Bw Khaemba katika mahojiano ya awali.

Waziri wa Kilimo katika Kaunti hiyo Mary Nzomo alisema mazao ya miwa yamepandwa katika kinachokadiriwa kuwa ekari 5000 huku ekari nyingine 2000 zikiandaliwa kwa kilimo cha zao hilo, mkondo ambao ni wa kuhofisha.

“Tunachosema ni kwamba jambo hili litakuwa tishio dhidi ya kuwepo chakula cha kutosha nchini maadamu Trans Nzoia huzalisha asilimia 90 ya mbegu za mahindi nchini,”

“Kama kaunti, tumetoa ombi kwa wizara kulinda kaunti hii dhidi ya ukuzaji wa miwa kwa sababu ikiwa uzalishaji wa chakula utatatizwa, jambo hilo litaathiri kuwepo kwa chakula cha kutosha nchini,” alisema.

Waziri huyo alisema hakuna utafiti wowote uliofanywa na Idara ya Sukari Nchini unaounga mkono ukuzaji wa miwa eneo hilo.

Serikali yatakiwa kuwapa walimu ulinzi wa kutosha

EVANS KIPKURA na STEVE NJUGUNA

MUUNGANO wa walimu nchini umetoa wito kwa serikali kurejesha amani katika kaunti za Bonde la Ufa ambazo zinakumbwa na visa vya wizi wa mifugo na uharamia.

Walimu katika kaunti za Baringo, Samburu, Turkana na Elgeyo Marakwet wamesema maafisa wa muungano huo bado hawajarejea shuleni kwa sababu ya visa vya uharamia vinavyozidi kuongezeka katika sehemu hizo.

Msururu wa mashambulizi yaliyoshuhudiwa majuzi katika eneo la Tiaty na kaunti zinazopakana na Elgeyo Marakwet, Samburu na Pokot Magharibi, yametatiza shughuli za masomo.

Miungano hiyo sasa inaomba serikali kutilia maanani wajibu wake wa kuwapa raia wake ulinzi katika mazingira kama hayo.

“Hali inayoshuhudiwa Kapedo ni ya kuhuzunisha mno. Imeenea hadi katika kaunti jirani na kuzorotesha shughuli za masomo kote. Hii ni kwa sababu hakuna mwalimu yeyote aliye na ujasiri wa kufanya kazi mahali ambapo usalama wake unatishiwa,” alisema Bw Omboko Milemba, ambaye ni mwanachama wa Bunge la Kitaifa na mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha walimu cha KUPPET, wakati wa uchaguzi wa muungano huo tawi la Iten.

Bw Milemba alisema kwamba atawasilisha mswada bungeni kushinikiza walimu wapewe ulinzi na serikali kila mara mashambulizi yanapozuka.

Viongozi hao walisema iwapo serikali haitahakikisha kwamba kuna usalama katika maeneo yaliyoathirika, watawashauri walimu wasirejee kazini kabisa.

“Pasipo usalama haiwezekani kabisa kwa walimu kutekeleza majukumu yao. Serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa walimu unaimarishwa kote nchini.

“Tunahofia kwamba endapo mapigano yataendelea Baringo, Samburu na Marakwet, hakuna mwalimu atakayeenda darasani,” alisema Naibu Mwekahazina wa chama kingine cha walimu KNUT, Bw James Mugo Ndiku, alipoongoza chaguzi za muungano wa walimu tawi la Keiyo.

Wakati huo huo, KUPPET imehimiza Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuhamisha wale ambao wameshambuliwa na wanafunzi, katika siku za hivi majuzi.

Muungano huo ulilalamikia ongezeko la visa vya wanafunzi kushambulia walimu nchini, ukisema kwamba njia pekee ya walimu walioathirika kuepuka unyanyapaa ni kwa wao kuhamishwa kutoka shule husika.

“Mwalimu anaposhambuliwa na mwanafunzi hawezi tena kusimama mbele ya wanafunzi hao na kuwafunza vyema. Ndiposa tunahimiza TSC kutilia maanani ombi la kuhamisha walimu husika ili waepuke kudhalilishwa,” alisema Katibu Mkuu wa KUPPET tawi la Laikipia, Bw Robert Miano.

Alitaja kisa ambapo mwalimu alishambuliwa na mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Murichu, mjini Ndaragwa.

Bw Miano alisema iwapo TSC itakosa kumhamisha mwalimu huyo, basi atafanyiwa dhihaka na wanafunzi katika shule hiyo.

“Mwalimu alishambuliwa na mwanafunzi mbele ya wanafunzi wote. Ni rahisi kwake kugeuzwa dhihaka; wanafunzi watamkosea heshima. Njia pekee ya kuepuka hali hiyo ni kumhamisha,” akasisitiza.

Kiongozi huyo wa walimu alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuanzisha mpango masuala ya kijamii ili wanafunzi wapewe ushauri nasaha kuzima utundu miongoni mwao.

Watamjaribu Baba?

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM kimealika wanaomezea mate tikiti ya kuwania urais kwa chama hicho, na kuzua maswali iwapo yupo atakayethubutu kushindana na kiongozi wake, Raila Odinga.

Kinara huyo ambaye yuko kwenye ushirikiano wa handisheki, amekuwa mgombea urais wa ODM tangu chama hicho kilipoundwa 2007.

Baadhi ya wanachama waliowahi kuelezea nia ya kuwania mchujo wa urais ni magavana Hassan Joho (Mombasa), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Amason Kingi (Kilifi).

Magavana wote watatu wanahudumu muhula wao wa mwisho kikatiba na hawaruhusiwi kuwania tena ugavana. Kwa hivyo, wanaruhusiwa kuwania urais. Hata hivyo swali lililo vinywani mwa wengi ni iwapo watakuwa na ujasiri wa kuwasilisha maombi ya kumenyana na Bw Odinga katika kutafuta tiketi ya kupeperusha bendera ya ODM kwenye debe mwaka ujao.

Kupitia ilani iliyotolewa na Bodi ya Uchaguzi ya chama hicho, chama cha ODM kinataka walio na azima ya kugombea urais kutuma maombi yao kufikia Februari 26.

Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi, Bi Catherine Mumma, kwenye tangazo magazetini jana alisema, hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya ODM kuendeleza mipango ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Kufikia sasa, Naibu Rais Dkt William Ruto, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara (UNCTAD), Dkt Mukhisa Kituyi na Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana ni kati ya wale wameshatangaza hadharani nia ya kuwania urais.

Lakini Bw Odinga hajatangaza hadharani iwapo atawania au la, huku akisema kampeni ya kupigia debe marekebisho ya Katiba kupitia BBI haina uhusiano wowote na uchaguzi wa urais.

Bi Mumma kwenye wito wa maombi kutoka kwa wanachama alisema, wanaotaka kuwania urais kwa tiketi ya ODM ni lazima wawe watu wa maadili ya hali ya juu na tabia njema katika jamii.

“Wanaotuma maombi ni lazima watimize masharti yote ya sheria na kanuni za uchaguzi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC),” Bi Mumma alisema kwenye tangazo magazetini.

Alisema wawaniaji ni lazima wawe wanachama wa maisha ambao wamedhihirisha kujitolea kwa vitendo kutekeleza ajenda za chama cha ODM.

“Wanaotafuta urais kupitia ODM ni lazima wawe watu wa maadili mema na nidhamu ya hali ya juu,” alisema Bi Mumma.

Pia wanapaswa kuwa wapigakura waliosajiliwa nchini Kenya, walio na digrii kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa nchini Kenya na waliohitimu kugombea kiti cha ubunge.

Wanaotuma maombi ni lazima waambatishe hati ya kiapo wakithibitisha kwamba stakabadhi na habari kuwahusu ni za kweli.

Aidha, ni lazima walipe ada ya Sh1 milioni kwa chama kabla ya Februari 26, tarehe ya mwisho ya kupokea maombi.

“Wanaotuma maombi ni lazima waambatishe ushahidi kwamba wamelipa Sh1 milioni kwa akaunti ya benki ya chama cha ODM,” alieleza Bi Mumma.

Alisema ada hiyo haitarudishwa iwapo anayetuma ombi hatakabidhiwa tiketi ya chama hicho kugombea urais.

Ingawa Bw Odinga hajajitokeza peupe kutangaza nia yake ya kuwania kiti hicho kwa mara ya tano, kuna kila ishara, hasa kutokana na matamshi ya washirika wake wa karibu, kwamba atakuwa kwenye debe mwaka ujao.

Olunga aahidi kuvumisha Al Duhail katika mahojiano yake ya kwanza

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Michael ‘Engineer’ Olunga ameahidi makubwa katika mazungumzo yake ya kwanza tangu ajiunge na mabingwa wa Ligi Kuu ya Qatar (QSL) Al Duhail mnamo Januari 12, 2021 akitokea Kashiwa Reysol inayoshiriki Ligi Kuu ya Japan.

Katika kikao na wanahabari kabla ya mechi yake ya tatu, Olunga alitanguliza kuwa anafurahia familia yake mpya ya wachezaji.

Kisha, aliahidi kusaidia Al Duhail kubwaga Al Ahli Doha katika mechi ya raundi ya 16-bora ya Amir Cup itakayosakatwa leo Jumatatu pamoja na mashindano mengine yote.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema kuwa kila mtu kambini mwa Al Duhail yuko tayari kwa mtihani wa Al Ahli.

“Tunasubiri mechi hiyo muhimu ambayo pia ni ngumu, lakini tuko tayari na kila mtu anajitahidi kufanya vyema ili tuingie raundi ijayo ya mashindano hayo.”

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya aliongeza, “Niko tayari kwa majukumu nitakayopewa na kocha na nitakuwepo kusaidia timu yangu katika mashindano yote nitakayohitajika pamoja na mechi nyingine yoyote ili tupate ushindi.”

Olunga, ambaye aliibuka Mchezaji Bora wa Mwaka 2020 na pia Mfungaji Bora kwenye Ligi Kuu ya Japan mwaka 2020, alihitimisha kwa kusema anafurahia makao yake mapya.

“Nimechezea timu yangu mpya michuano miwili na unaofuata utakuwa wa tatu. Soka haina tofauti unaisakata Doha, Japan ama nchi nyingine yoyote. Kitu muhimu ni mchezaji kuwa mwepesi wa kukubali mabadiliko kufuatana na mazingira na ninafurahia kuwa na wachezaji wenza wapya.”

Mechi ya Amir Cup kati ya Al Duhail na Al Ahli itapigiwa ugani Grand Hamad. Al Duhail, ambao ni wenyeji, wamekanyaga Al Ahli mara tisa mfululizo kwa jumla ya mabao 31-7 kwa hivyo bado wanapigiwa upatu kuendeleza ukatili wao huo.

Katika klabu yake mpya, Olunga atakuwa na majukumu zaidi kuliko Kashiwa. Tofauti na Kashiwa ambako majukumu yalikuwa ya nyumbani tu, Al Duhail inashiriki Klabu Bingwa bara Asia na pia ni mwenyeji wa Klabu Bingwa Duniani mnamo Februari 4-1.

Al Duhail itafungua kampeni yake ya Klabu Bingwa Duniani dhidi ya miamba wa Afrika Al Ahly katika mechi ya raundi ya pili mnamo Februari 4. Mshindi kati ya Al Duhail ya kocha Sabri Lamouchi na wafalme hao wa Misri atatinga nusu-fainali kupepetana na mabingwa Klabu Bingwa Ulaya Bayern Munich kutoka Ujerumani.

Mechi nyingine ya raundi ya pili itakutanisha mabingwa Amerika ya Kati, Kaskazini na Caribbean (CONCACAF) Tigres UANL kutoka Mexico na wale wa Bara Asia Ulsan Hyundai kutoka Korea Kusini. Mshindi hapa atamenyana katika nusu-fainali na mshindi wa Amerika ya Kusini (CONMEBOL) ambaye atajulikana Januari 30 wakati klabu za Brazil Palmerais na Santos zitakabana koo katika fainali ya Libertadores. Makala ya 2020 ya Klabu Bingwa Duniani, ambayo yaliahirishwa kutoka Desemba mwaka jana kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona, atafahamika hapo Februari 11.

BI TAIFA JANUARI 25, 2021

DAMARIS Wangoi, 23, kutoka Nakuru ndiye anatupambia ukurasa leo. Yeye ni mjuzi wa masuala ya vipodozi. Uraibu wake ni kutazama filamu za Soap Opera na kusikiliza muziki wa kizazi kipya. Picha/ Richard Maosi

Dallas Allstars mabingwa wapya wa Koth Biro

Na JOHN KIMWERE

DALLAS Allstars imepambana mwanzo mwisho na kubahatika kutawazwa mabingwa wapya katika shindano la Koth Biro muhula wa 2020-21 ambayo ni makala ya 45.

Dallas Allstars iliyotokea eneo la Landmawe ilibeba taji hilo ilipolemea Ruaraka Allstars iliyokuwa ikipigiwa upatu kubeba taji hilo.

Ruaraka Allstars ilishindwa kufanya kweli licha ya kutegemea huduma zake Collins ‘Gattuso’ Okoth aliyekuwa akipigia Gor Mahia FC ambayo hushiriki Ligi Kuu Kenya.

Vijana wa Dallas wakiongozwa na nahodha, Clinton Olunga walitawazwa mabingwa wa kinyang’anyiro hicho walipofunga Ruaraka Allstars kwa mabao 8-7 kupitia mipigo ya matuta baada kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

Wachezaji wa Ruaraka kabla ya kuingia dimbani kucheza na Dallas Allstars katika fainali ya Koth Biro. Dallas ilipata ushindi baada ya kupiga Ruaraka mabao 8-7.  Picha/John Kimwere

Timu hiyo chini ya kocha, Stephen Mbogo huku ikishangaliwa na wafuasi wao waliofurika katika Uwanja wa Umeme Ziwani, Nairobi ilitandaza soka safi na kuonekana kuwalea wapinzani katika kipindi cha kwanza.

Ndani ya kipindi cha pili wachezaji wa timu zote walipata nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia vyema. David Onyango ndiye alipoteza kwa upande wa Ruaraka Allstars na kuchangia kukosa taji hilo.

Wafungaji wa Dallas walikuwa: Dryan Musa, Tyran Owino, Eliakim Muange, Griffins Maloba, Sammy Ben, Michael Amanda, Oscar Masika na Evans Irungu.

Wachezaji wa Dallas Allstars wakionyesha kombe baada ya kutuzwa mabingwa wa taji la Koth Biro mwaka huu wa 2021. Picha/John Kimwere

Nao waliofungia Ruaraka ya  Cyril Otieno walikuwa: Kevin Omondi, Collins Ochieng, Manami Lewis, Derrick Owino, Brian Juma, Tyson Otieno na Veron Nanjero.

”Bila shaka tunashukuru sana kuibuka mabingwa wa taji hilo la Koth Biro msimu huu baada ya kulisaka mara mbili bila mafanikio,” nahodha wa Dallas alisema na kuongeza kuwa muhula ujao watakuwa kazini kutetea ubingwa huo.

Mchezaji huyo anasema kwenye mechi za mwaka huu walijitahidi kwa udi na uvumba kukabili wapinzani wao. Dallas iliposhiriki kipute hicho mara ya kwanza ilibanduliwa kwenye mechi za makundi kabla ya kupigwa breki katika robo fainali.

Ruaraka ilishinda Terror Squad kwa mabao 3-1 nayo Dallas Allstars iliandikisha ufanisi wa mabao 5-4 dhidi ya kikosi cha Leads United kupitia mikwaju ya penalti.

Ruaraka Allstars ilijikatia tiketi ya kushiriki mchezo huo baada ya Tyson Otieno kusaidia kufunga Leads United bao 1-0 katika robo fainali. Nayo Githurai United iliumwa mabao 8-7 na Terror Squad kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Nao wachezaji wa Asec Huruma walizaba Biafra mabao 2-1 huku Dallas ikizoa matokeo sawa na hayo dhidi ya Kajiado Allstars.

Kikosi cha Dallas Allstars kilijumuisha: Clinton Olunga(nahodha), Felix Sambu, Hemstine Smith, Pius Odhiambo, Amos Okoth, Sammy Ben, Michael Amanda, Griffins Maloba, Eliakom Muange na Tyran Owino. Wengine walikuwa Dryan Musa, Eugene Wethuli, Cyrus Mwangi, Ryan Kariuki, Vincent Ajode, Protus Otieno, Kennedy Kimotho, Oscar Masika, Peter Wambua na Evans Irungu.