BI TAIFA FEBRUARI 20, 2018

JACQUILINE Saitabau, 21, anatupambia tovuti yetu leo. Anapenda kusafiri, kusoma vitabu na kupamba warembo. Picha/ Anthony Omuya

Miguna Miguna alikuwa hatari kwa usalama wa nchi, mahakama yaambiwa

Mawakili James Orengo (kulia) , Dkt John Khaminwa na Nelson Havi wanaomwakilisha Dkt Miguna Miguna na wakili wa Serikali Emmanuel Mbittah. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

KUTIMULIWA kwa mwanaharakati Dkt Miguna Miguna humu nchini kumeendelea kuibua masuala mbalimbali huku Serikali ikiambia Mahakama Kuu kwamba alikuwa tisho kwa usalama wa nchi.

“Kabla ya uamuzi wa kumfurusha Dkt Miguna kutoka humu nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Bw Gordon Kihalangwa alikuwa amepashwa habari na maafisa wa upelelezi kwamba alikuwa tisho kwa usalama wa kitaifa,” Jaji Enock Mwita aliambiwa na Wakili wa Serikali Emmanuel Mbittah.

Na wakati huo huo Jaji Mwita alifahamishwa mwaka wa 2003 , Dkt Miguna alipata uraia wa Canada na kurudishwa kwake kwao na hakuna makosa yoyote kutokana na ufichuzi kwamba alikuwa anajihusisha na vitendo ambavyo ni hatari kwa usalama wa kitaifa.

Bw Mbittah alimweleza Jaji Mwita kufurushwa kwa Dkt Miguna ni kwa manufaa ya kila mwananchi.

“Bw Kihalangwa alipokea habari kutoka kwa maafisa wa uchunguzi wa jinai kwamba Dkt Miguna alikuwa anajihusisha na visa vilivyo tisho kwa usalama wa kitaifa na ilifaa arudishwe nchini Canada,” Bw Mbittah alisema.

Wakili huyo wa Serikali aliambia mahakama taarifa hizo za wapelelezi zilizojulishwa Bw Kihalangwa, zilielezewa Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i ambaye mara moja Dkt Miguna alimtangaza kuwa “mtu asiyetakikana humu nchini.”

Bw Mbittah alisema hakuna sheria yoyote ambayo serikali ilivunja ama kukaidi haki za Dkt Miguna katika kufutilia mbali cheti cha kusafiria cha Dkt Miguna na kumtangaza mtu asiyetakikana.

“Uamuzi wa kumfurusha Dkt Miguna uliochukuliwa na Bw Kihalangwa na Dkt Matiang’i haupasi kukosolewa kwa vile ulikuwa kwa mujibu wa sheria,” Jaji Mwita alifahamishwa.

Mahakama itatoa uamuzi Feburuari 23, 2018.

Bei ghali ya mafuta kupandisha gharama ya maisha

Kituo cha mafuta cha National Oil. Bei ya mafuta imekuwa ikipanda kwa miezi sita mfululizo tangu Septemba 2017. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

BEI ya mafuta inazidi kupanda nchini, na wananchi wanafaa kutarajia ongezeko la gharama ya maisha.

Kwa miezi sita mfululizo tangu Septemba 2017, bei ya mafuta imeonekana kupanda ambapo katika jendwali jipya la bei ya petroli ilipanda kwa Sh1.62 na Sh2.14 kwa dizeli, ilhali bei hiyo kwa mafuta taa ilipanda kwa Sh1.97.

Kulingana na shirika la kutetea haki za wateja (Cofek) huenda kupanda kwa bei ya mafuta kukasababisha kupanda kwa nauli ya magari.

Cofek ilisema huenda kukawa na ongezeko la matumizi ya mafuta chafu, hali inayotarajiwa kuathiri zaidi afya na magari.

Makampuni mengi hutumia mafuta katika kutengeneza bidhaa, huenda hali hiyo ikaathiri gharama ya uzalishaji wa bidhaa, alisema Mkurugenzi wa Chama cha Watengenezaji Bidhaa (KAM) Bi Phyllis Wakiaga.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia, bei za mafuta zitazidi kuongezeka hadi Sh5, 796 kwa pipa, kutoka Sh5, 485.5.

Wauzaji wa mafuta katika soko la kimataifa wamekubaliana kupunguza kiwango cha uzalishaji wa mafuta ili kudhibiti bei katika soko la kimataifa.

Uamuzi huo unaathiri bei ya mafuta moja kwa moja, hali itakayowazidishia mzigo wa gharama ya maisha wananchi.

Familia 710,000 kunufaika na msaada wa serikali

Na BERNARDINE MUTANU

FAMILIA kufikia 710,000 kote nchini zitapokea msaada kutoka kwa serikali mwishoni mwa Februari.

Fedha hizo ambazo hutolewa mara moja kila baada ya miezi miwili zitanufaisha watu wasiojiweza katika jamii.

Mradi huo, ‘Inua Jamii’ unalenga kupunguza viwango vya umaskini katika jamii. Pesa hizo ni za Novemba na Desemba 2017.

Watu hao watanufaika kutokana na ufadhili wa Sh2.8 bilioni na zitatolewa kupitia kwa afisi za kaunti ndogo na afisi za kaunti.

Chini ya mpango huo, serikali ilitoa Sh1.4 bilioni kwa watoto mayatima na maskini, Sh188 milioni kwa walemavu na Sh1.24 bilioni kwa wazee walio na miaka 65 na zaidi.

Awamu ya utoaji wa fedha hizo itakamilika Februari 22, alisema Katibu Mkuu katika Idara ya Kusimamia Maslahi ya Kijamii, Susan Mochache.

Juhudi za Kenya kununua ndege za kijeshi zagonga mwamba

Na BERNARDINE MUTANU

MPANGO wa Kenya wa kupata ndege za kijeshi umekwama baada ya serikali kushindwa kuingia katika mkataba na wauzaji katika muda unaofaa.

Serikali ilikuwa na mpango wa kupata ndege hizo kwa gharama ya Sh43 bilioni kutoka Marekani.

Kulingana na Afisi ya Uwajibikaji ya Serikali ya Marekani(GAO) serikali ya Kenya ilishindwa kuhakikisha kuwa ilihitaji ndege hizo 12 za kijeshi pamoja na mashine za kurusha makombora, bunduki atomatiki na mabomu ya kuelekezwa.

Serikali iliagiza ndege hizo kwa mara ya kwanza Desemba 2015 na kufikia sasa imekiuka muda wa makataa ya kudhinisha mkataba huo mara mbili.

Mara ya kwanza ilikuwa Juni 2017, baada ya maafisa wa serikali kuelezea kuwa walikuwa na changamoto juu kwa sababu ya Uchaguzi Mkuu Agosti 8.

Vile vile, Kenya ilishindwa kutimiza makataa ya Septemba 16, baada ya muda huo kurefushwa.

Serikali ya Marekani imesema Kenya haijatoa maelezo zaidi kuhusiana na mkataba huo, hali inayosababisha shaka kuhusiana na ununuzi wa ndege hizo na zana zingine za kijeshi.

KenGen kuzalisha megawati 160 kutokana na mvuke

Kiwanda cha kuzalisha umeme kutokana na mvuke katika eneo la Olkaria. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

KAMPUNI ya uzalishaji wa umeme nchini (KenGen) imetangaza mpango wa kuongeza megawati 160 katika mfumo wa umeme humu nchini.

Kiasi hicho cha kawi kitatiwa katika mfumo wa usambazaji wa umeme wa kitaifa kabla ya Juni 2019.

Kulingana na Meneja Mkurugenzi wa KenGen Rebecca Miano, mradi huo wa Sh17 bilioni unaendelea vyema na kufikia 2020, KenGen itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 721.

Kufikia sasa, KenGen inazalisha megawati 533.8 kwa njia ya mvuke, eneo la Olkaria.

Mpango huo utaigharimu serikali Sh135 bilioni, alisema. Serikali ilizindua mpango wa kuzalisha umeme kwa njia ya mvuke katika juhudi ya kuimarisha uwepo wa kawi safi nchini.

Gharama ya umeme kupanda zaidi kusiponyesha

Kifaa cha kidijitali cha kuhesabu matumizi ya umeme. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

HALI ya maisha itakuwa ngumu zaidi siku chache zijazo ikiwa mvua haitanyesha, kutokana na ongezeko la gharama ya umeme.

Hii ni kutokana na kuwa maji katika bwawa la Masinga, ambalo ni kubwa zaidi katika uzalishaji wa umeme nchini kwa njia ya maji yamepungua kwa kiwango kikubwa.

Huenda serikali ikalazimika kutumia dizeli kuzalisha umeme, bidhaa iliyo ghali (mara sita zaidi ya stima inayotokana na maji), katika kuzalisha stima ikilinganishwa na maji.

Pia stima kutokana na mvuke ni ghali sana (mara tatu kuliko inayotokana na maji)na huenda gharama ya uzalishaji wa umeme ikahimiliwa na wananchi.

Bwawa la Masinga, na viwanda vingine vya uzalishaji wa stima kwa njia ya maji, limeathiriwa na ukame mkubwa unaoshuhudiwa nchini.

Bwawa la Sondu-Miriu kwa mfano linazalisha umeme nusu ya kiwango chake, kwa sababu ya upungufu mkubwa wa maji.

Kiwango cha maji kikishuka zaidi ya ilivyo kwa sasa katika Bwawa la Masinga, huenda serikali ikalazimika kufunga kiwanda hicho cha kuzalisha umeme, alisema Waziri wa Kawi Bw Charles Keter.

IEBC yasema inahitaji Sh8 bilioni kutathmini upya mipaka

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) Bw Wafula Chebukati. Utathmini wa mipaka utafanyika baada ya hesabu ya watu ya 2019. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) inahitaji Sh8 bilioni kutathmini mipaka ya maeneobunge na wadi kwa mara ya pili.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati, tathmini inafaa kufanyika kati ya Februari na Agosti 3, 2021.

Alisema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba inayosimamiwa na Bw Jeremiah Kioni, Mbunge wa Ndaragwa.

Kulingana na Bw Chebukati, watategemea data kutoka kwa ripoti kuhusu idadi ya watu nchini inayotarajiwa kutolewa mwaka  2019.

Kulingana na kifungu cha 89 cha Katiba, IEBC inafaa kutathmini mipaka kati ya miaka nane na miaka 12 na tathmini inafaa kukamilika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa ubunge kufanywa.

Itakuwa tathmini ya kwanza tangu Katiba mpya kuzinduliwa 2010. Mipaka ya maeneobunge na wadi iliundwa kwa kufuata katiba hiyo.

NYS yapewa ekari 100,000 kukuza pamba Galana-Kulalu

Wakulima wakivuna pamba katika eneo la Molo, Nakuru. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

HUDUMA ya Kitaifa ya Vijana (NYS) imepewa ekari 100,000 za mradi wa unyunyiziaji wa Galana-Kulalu.

Hii ni katika juhudi za serikali za kuzindua tena kilimo cha pamba. Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa alisema mradi wa Galana-Kulalu uliambatana na ajenda nne za Jubilee.

Alisema hayo eneo la Gilgil wakati wa kuhitimu kwa vijana wa NYS. Katika mpango huo kilimo cha pamba kinatarajiwa kubuni nafasi 50,000 za kazi na ukuzaji wa mapato kutokana na mauzo ya nguo katika soko la kimataifa hadi Sh20 bilioni.

“Kama sehemu ya kuzindua tena sekta ya pamba, NYS itapewa ekari 100,000 za Galana-Kulalu,”alisema rais Ijumaa.

Mradi wa unyunyiziaji wa Galana-Kulalu ulilenga kuimarisha chakula nchini wakati ukame na njaa unaangamiza wananchi wengi.

Mkaguzi mkuu sasa yuko huru kukagua hesabu za KDF

Na BERNARDINE MUTANU

MKAGUZI mkuu wa hesabu za serikali amepewa idhini ya kukagua matumizi ya mabilioni ya fedha zilizotolewa kwa jeshi na taasisi zingine za usalama nchini.

Idhini hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu baada ya Jaji Chacha Mwita kusema kuwa Sehemu 40 ya Ukaguzi wa Matumizi ya Fedha za Umma (2015) na sehemu zingine za sheria hiyo haikuambatana na Katiba.

Kulingana na sehemu hiyo, wahusika wa ufisadi katika taasisi hizo wanaweza kukingwa. Lakini baada ya uamuzi huo wa Jaji Chacha, inamaanisha kuwa yuko huru kukagua matumizi ya kifedha katika Shirika la Upelelezi (NIS), jeshi (KDF) na Huduma ya Kitaifa ya Polisi.

Kulingana na jaji huyo, sheria hiyo na zingine nane, ziliingilia uhuru wa Kikatiba wa Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali.

Sehemu hizo ni 4(2), 8, 12, 17(1), 18, 27, 40, 42 na 70, ambazo zaidi alisema zilikuwa kinyume cha kanuni na mwongozo uliotolewa na Katiba.

KCB, Equity na Co-operative zashushwa na Moody’s

Na BERNARDINE MUTANU

BENKI tatu za Kenya zimeshushwa hadhi na shirika la wawekezaji la Moody’s.

Benki hizo ni KCB, Equity na Co-operative. Benki hizo zilishushwa hadhi kutokana na kushuka kwa viwango vya serikali za upataji mikopo.

Katika taarifa, shirika hilo lilisema benki hizo zilikuwa zimeshukishwa kutoka kiwango cha B1 hadi B2.

Benki hizo zilishukishwa kutokana na kushukishwa kwa kiwango cha serikali ya Kenya kuhusiana na mikopo mapema

Ndege nne za Jambojet kuimarisha safari Afrika

Na BERNARDINE MUTANU

KAMPUNI ya Jambojet imepanga kununua ndege nne katika muda wa miezi 18 ijayo kwa lengo la kuimarisha operesheni zake nchini na katika eneo la Afrika.

Mkurugenzi Mku wa Jambojet Willem Hondiusa alitangaza mpango huo Alhamisi, Entebbe, Uganda, wakati wa kuzindua safari ya kwanza ya ndege ya kampuni hiyo kimataifa.

Jambojet ni tawi la Kenya Airways na inatarajia kununua ndege mbili zilizotumiwa aina ya Bombadier Q400 kufikia Juni 2018 na zingine mbili mpya mapema 2019.

Bw Hondius alisema serikali kwa niaba ya Jambojet imetuma ombi kwa ndege hiyo kuidhinishwa kuanza ziara zake Rwanda, Ethiopia, Sudan, Congo, Tanzania na Burundi.

“Maombi yalitumwa Oktoba 2017 na tunatumainia kuwa kufikia mwisho wa mwaka, tutakuwa tumeanza safari zetu katika mataifa mawili,” alisema wakati wa mahojiano na wanahabari Entebbe, Uganda.

Kampuni hiyo ikinunua ndege nne, itakuwa na jumla ya ndege nane, alisema mkurugenzi hiyo.

Miguna Miguna arudishwe nchini, mahakama yaamuru

Mawakili Nelson Havi (kulia) na Cliff Ombeta wateta kuhusu ukaidi wa maafisa wakuu serikali kutotii maagizo ya korti. Picha/RICHARD MUNGUTI

RICHARD MUNGUTI

KIZAAZAA cha kumfurusha mwanaharakati na kiongozi wa vuguvugu la National Resistany Movement (NRM) la muungano wa Nasa, Dkt Miguna Miguna, kiliendelea kutifuka Alhamisi baada ya Mahakama Kuu kuamuru arudishwe Kenya kutoka Canada.

Jaji Luka Kimaru aliamuru Dkt Miguna arudishwe Kenya kwa vile Serikali ilikaidi agizo la korti mwanasheria huyo mbishi na mwenye matata afikishwe kortini.

Jaji Kimaru alisema hatua ya serikali kumfurusha Miguna ni kinyume cha katiba na sheria za kimataifa zinazosema kuwa mmoja hawezi kupokonywa uraia wake.

Miguna ni mzaliwa wa eneobunge la Nyando, kaunti ya Kisumu lakini alipata uraia wa Canada alipoenda kupokea masomo ya juu.

Mawakili Cliff Ombeta na Nelson Havi waliomba agizo hilo la Serikali lifutiliwe mbali na Miguna arudishwe nchini.

Jaji Kimaru alisitisha kuwachukulia hatua kali wakuu wa Polisi Joseph Boinnet na George Kinoti ndipo wamrudishe Miguna nchini kuendelea na kesi aliyoshtakiwa na aliuyoshtaki.

Yatima asukumwa rumande kuhusu wizi wa Sh2.5 milioni

Mshukiwa wa wizi Adeshara Krishan Bhailal almaarufu Anilkumar Jakharia akiwa kizimbani kwa wizi wa Sh2.5milioni. Picha/ RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

YATIMA anayekesha kwenye barabara za Nairobi alishtakiwa kwa wizi wa Sh2.5milioni kutoka kwa benki.

Adeshara Krishan Bhailal alishtakiwa kwa kuibia benki ya  Guaranty Trust Bank (GT Bank) pesa hizo.

Kiongozi wa mashtaka Bi Sega hakupinga akiachiliwa kwa dhamana lakini wakili wake Bw David Ayuo alishangaza korti kwa sababu ya ufichuzi wake.

“Mteja wangu huyu hana makazi rasmi jijini Nairobi. Alitupwa na familia yake,” Ayuo alimweleza hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani.

Bi Onkwani aliambiwa Bhailal “hana wazazi, na jamaa aliokuwa akiishi nao walimfukuza akaanza kuishi kwa barabara za jijini Nairobi.”

“Unamaanisha mshtakiwa hana familia anayoishi nayo baada ya wazazi wake kuaga?” Onkwani alishangaa.

“ Ndio mshtakiwa hana familia. Anategemea wasamaria wema,”  Ayuo akajibu.

Mahakama haikumwonea huruma ila iliamuru azuiliwe katika gereza la viwandani hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Wawili wakana kuiba Sh50 milioni hospitali ya Mater

Solomon Odeny (kulia) na Paul Oming’o katika mahakama ya Milimani waliposhtakiwa kwa kuibia hospitali ya Mater zaidi ya Sh50 milioni. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MHASIBU na mfanyakazi katika kampuni ya mawasiliano ya Wananchi Telecom walikanusha mashtaka mawili ya kuibia pesa hospitali ya Mater miaka 11 iliyopita.

Solomon Odeny na Paul Oming’o walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Walikana kati ya Aprili 3, 2006 na Januari 31, 2017 jijini Nairobi wakishirikiana na watu wengine ambao hawajashtakiwa waliiba kitita cha Sh50,143,948 mali ya hospitali ya Mater Misericordiae.

Shtaka la pili dhidi ya Bw Oming’o lilisema kuwa kati ya Julai 22, 2012 na September 2, 2016 aliiba Sh29,997,514 alipokuwa ameajiriwa kama mhasibu na hospitali hiyo ya Mater.

Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu hadi Juni 6, 2018 kesi itakaposikizwa.

Omtatah amletea matata wakili Ogeto

Wakili Kennedy Ogeto aliyeteuliwa kuwa wakili mkuu wa Serikali na Rais Uhuru Kenyatta. Picha/ RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah Jumatatu aliwasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga uteuzi wa wakili Kennedy Ogeto kuwa wakili mkuu wa Serikali.

Katika kesi aliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Milimani Nairobi Bw Omtatah alisema Rais Uhuru Kenyatta alikaidi katiba alipomteua Bw Ogeto katika wadhifa huo wa umma.

Mwanaharakati huyo amesema Rais Kenyatta alikaidi katiba kwa kumteua Bw Ogeto kuwa wakili mkuu wa Serikali kabla ya kutangaza nafasi katika afisi hiyo.

Bw Ogeto aliteuliwa kutwaa wadhifa huo baada ya aliyekuwa wakili mkuu wa Serikali Bw Njee Muturi kupelekwa kuwa naibu wa mkuu wa wafanyakazi katika Ikulu.

Bw Omtatah amesema hakuna mahojiano yaliyofanywa kuona iwapo Bw Ogeto amehitimu.

Kabla ya kuteuliwa Bw Ogeto alikuwa mmoja wa mawakili waliomwakilisha Rais Kenyatta katika kesi ya kupinga uchaguzi wake Agosti 8 na Oktoba 26 2017.

Tena alikuwa anamwakilisha Rais Kenyatta katika kesi mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) aliposhtakiwa kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008 ambapo watu zaidi ya 1,000 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kufurushwa makwao.

Mbali na kesi hii dhidi ya Bw Ogeto , Bw Omtatah amemshtaki pia Rais Kenyatta kwa uteuzi wa mawaziri.

Rais hafai kukosolewa akiteua mawaziri – Mahakama

Wakili Dunstan Omari aliyewatetea wakuu wa Idara ya Magereza Isaya Osugo na Omar Tawane Gudai. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

KATIKA uamuzi wa kihistoria, Mahakama ya Kuamua Mizozo ya Wafanyakazi (ELRC) imesema Rais Uhuru Kenyatta hapasi kukosolewa au  kuhojiwa mahakamani kwa uteuzi wa mawaziri na watumishi wengine wakuu serikalini.

Mahakama ilisema katiba imewapa wananchi mamlaka ya kumchagua wanayempenda kuwa akitekeleza majukumu fulani kwa niaba yao.

Jaji Nelson Abuodha alisema Rais Kenyatta hutekeleza majukumu yake miongoni mwao kuwateua watumishi wa umma “ kutokana na mamlaka aliyopewa na wananchi waliomchagua.”

Jaji Abuodha alisema katiba inasema nguvu na mamlaka ni ya wananchi na inaweza kutekelezwa na yule aliyechaguliwa na wananchi kama vile Rais Kenyatta.

Hata hivyo Jaji Abuodha alitahadharisha uteuzi wowote unaofanywa na Rais haupasi kuwa wa kuwatunuku au kuwalipa wale walio na maoni sawa ya kisiasa ama wale waliotekeleza jukumu fulani ya kisiasa.

Jaji Abuodha aliyekataa kuwatimua kazi maafisa wawili wakuu katika idara ya Magereza ambao waliteuliwa na Rais Kenyatta kuhudumu kwa muda wa miaka miwili  zaidi baada ya kuhitimu umri wa wa kustaafu wa miaka 60, alisema sheria za kuajiri watumishi wa umma zinamruhusu kuongezea muda walio na ujuzi maalum.

Jaji Abuodha aliamuru Mabw Isaya Osugo na Omar Tawane Gudai waendelee kuhudumu hadi kipindi chao kikamilike.

Wawili hawa waliongezewa muda wa kuhudumu mnamo Juni 29, 2016.

Bwanyenye akana mashtaka mapya

Bwanyenye Mohan Galot (kulia) na mkewe walipofika katika mahakama ya Milimani JumatatU. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

BWANYENYE Mohan Galot na mkewe walifikishwa katika mahakama ya Milimani wakikabiliwa na mashtaka ya kughushi cheti cha kuandikisha kampuni ya Galot Industries akidai ni halali.

Shtaka lasema Mohan  Galot alighushi cheti hicho mnamo Agosti 5 2016 akidai kilitolewa na Msajili wa Kampuni katika afisi ya mwanasheria mkuu Bw Nicholas Oduor.

Mawakili Kirathe Wandugi na Prof Tom Ojienda walipinga Bw Galot akisomewa mashtaka na kuyajibu waLisema, “upande wa mashtaka unatumia kitengo cha mahakama kwa njia mbaya.”

Mawakili hao walimshambulia kiongozi wa mashtaka Daniel Karori na maafisa wa polisi wanaochunguza kesi dhidi ya Bw Galot wakisema “afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ilikuwa inafanya mchezo wa paka na panya.”

Bw Wandungi alisema wamejulishwa na wanahabari kuhusu mashtaka mapya dhidi ya Bw Galot.

Hakimu mkuu Francis Andayi aliamuru mashtaka hayo mapya dhidi ya Bw Galot yasisomwe hadi wakati mwingine.

Na wakati huo huo Bw Andayi akawaruhusu Mabw Wandugi na Prof Ojienda kuendelea kuwatetea wanaohusika na kesi hiyo.

KRA yapoteza mabilioni kutokana na bidhaa ghushi

Na BERNARDINE MUTANU

BIDHAA ghushi zilishusha kiwango cha mapato kutokana na ushuru kushuka kwa Sh7.35 bilioni.

Bidhaa hizo ni pamoja na stempu feki na kwa muda wa miezi sita hadi Desemba 31, zilisababisha hasara kubwa.

Kutoka Julai hadi Desemba 2017, ushuru unaotokana na uuzaji wa bidhaa ulishuka kwa asilimia tisa.

Kulingana na Shirika la Kutoza Ushuru nchini (KRA) Jumatatu, ikilinganishwa na kipindi hicho 2016 ambapo mapato kutokana na mauzo ya bidhaa yalikuwa Sh81.644, mwaka huu kiwango hicho kilishuka sana.

Katika muda wa miaka mitatu, kiwango cha mapato hayo kilikua kwa asilimia 16, alisema Kamishna Mkuu wa KRA John Njiraini.

KRA ilisema kuwa ushuru unaotakana na pombe na sigara ulishuka kwa asilimia 16.3 na asilimia 11.2 kwa mfuatano huo mwaka wa 2016.

Atwoli anagawanya jamii ya Abaluhya, aonya Wetang’ula

Kinara wa muungano wa NASA na kiongozi wa chama cha Ford Kenya Bw Moses Wetang’ula. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

KINARA mwenza wa muungano wa NASA Moses Wetang’ula ameitaka jamii ya watu wa Magharibi kupuuzilia mbali Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli huku akisema kuwa analenga kugawanya jamii ya Waluhya.

Bw Wetang’ula alimshambulia Bw Atwoli saa chache baada ya kiongozi huyo wa Cotu kutangaza Jumapili kwamba kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) ambaye pia ni kinara mwenza wa NASA Musalia Mudavadi ataendelea kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya.

Bw Atwoli alisema kwamba amemsamehe Bw Mudavadi, kwa kuhepa hafla ya kumuapisha kiongozi wa muungano huo Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018.

Bw Mudavadi, Bw Wetang’ula na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka walisusia hafla ya kuapishwa Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’.

Bw Atwoli aliyesema hayo baada ya mkutano wa faragha nyumbani kwa  Bw Mudavadi alisema: “Tumekubaliana kwamba Bw Mudavadi ataendelea kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya bila kutatizwa na yeyote.”

Lakini matamshi hayo yalimkera Seneta wa Bungoma Wetang’ula huku akiyataja kuwa ‘sarakasi’.

“Sarakasi za Atwoli hazitasaidia kwa lolote kuunganisha jamii ya Waluhya na badala yake anatugawanya,” akasema Bw Wetang’ula kupitia Twitter.

“Mbona Bw Atwoli anaangazia Mudavadi kwani hakuna Waluhya waliochaguliwa katika maeneo Bungoma, Trans Nzoia naNairobi?” akauliza Bw Wetang’ula.

Onyo Nzoia Sugar yaweza kushushwa daraja

Na CECIL ODONGO

HUKU ligi kuu hapa nchini ikiingia mechi za raundi ya nne wikendi hii kikosi cha soka cha timu ya Nzoia Sugar bado kinasuasua baada ya kupoteza mechi zao zote.

Vijana hao wa Kocha Bernard Mwalala wamepoteza mechi zote tatu licha ya kuhimili mawimbi makali msimu uliopita na kumaliza wa tisa kwenye msimamo wa jedwali la KPL.

Walichapwa 1-0 na klabu ya Kariobangi Sharks mechi ya kwanza, 2-1 na Mathare United kisha 1-0 na Nakumatt FC wikendi iliyopita.

Timu ya Nzoia pamoja na wenzao Homeboys ndizo timu za pekee kutoka uliokuwa mkoa wa Magharibi wanaoshiriki ligi kuu ya KPL. Klabu ya Western Stima iliyokuwa ikishiriki ligi hiyo ilishushwa daraja mwisho wa msimu jana walipomaliza kwenye nafasi ya 17.

Kulingana na Kocha Benard Mwalala ubutu wa washambulizi wake mbele ya lango la wapinzani ndio umewafanya kutopata matokeo mazuri.

Mastraika wake wamefanikiwa kuwafungia mabao manne pekee nao wapinzani wao kwenye mechi zote tatu wakiwafunga mabao tisa.

Msimu uliopita baada ya kutesa mara tatu ligi ikianza Nzoia sugar walikuwa na alama nne.Mwanzo huo wa wastani kwenye ligi hiyo uliwapa motisha na wakaepuka kushushwa daraja.

Kwenye dirisha ndogo ya usajili timu hiyo iliamua kudumisha wengi wa wachezaji wake lakini wakawasajli wachezaji wanane miongoni mwao difenda Edwin Wafula kutoka klabu ya western stima, chipukizi Harrison Osotsi kutoka shule ya upili ya Chavakali na Michael Osundwa kutoka Nakuru All stars.

Nzoia wanakabiliwa na kibarua kigumu huku mechi zao mbili zijazo zikiwashuhudia wakitesa dhidi ya klabu ya Tusker ugenini kisha wacheze na majirani wao Kakamega Homeboyz nyumbani.

Timu hiyo inacheza msimu wake wa pili ligini baada ya kupandishwa ngazi mwaka 2016 kushiriki ligi kuu. Mwaka huo walimaliza wa kwanza kwenye super league mbele ya Kariobangi Sharks na Nakumatt FC.

Watu 10 wanaswa kwenye msako dhidi ya karatasi za plastiki

Serikali ilipiga marufuku utumizi wa karatasi za plastiki mwaka 2017 na kutoa mifuko mbadala ya kubebea bidhaa. Picha/ Maktaba

Na CECIL ODONGO

SHIRIKA linalosimamia mazingira hapa nchini NEMA Jumatatu liliandaa msako wa ghafla kwenye soko maarufu la kuuza nyama la Burma jijini Nairobi ili kuwanasa watumizi wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.

Msako huo ulihusisha maafisa wa shirika hilo na polisi wa Kituo cha Polisi cha Shauri Moyo wakiongozwa na OCS Bw Mark Odenyo.

Akizungumza na wanahabari baada ya operesheni hiyo, mkurugenzi mkuu anayesimamia mazingira kwenye shirika hilo kaunti ya Nairobi Bi Njoki Muriuki alilalamikia ongezeko la matumizi ya mifuko hiyo jijini.

Mwana mazingira huyo alisema kuwa japo marufuku hiyo iliasisiwa miezi mitano iliyopita, wafanyibiashara wadogo wadogo bado wameikaidi na kuendeleza matumizi yake kinyume cha sheria.

“Tumewanasa zaidi ya wafanyabiashara 200 kote nchini na tukiwafikisha mahakamani wengi wao hushindwa kulipa faini kati ya sh150,000 hadi sh300,000,” akasema. “Wakati huu hatutalegea na kutoka hapa tutaenda Gikomba na Muthurwa,” akaongeza.

 

Onyo

Bi Njoki alitisha kufunga soko hilo iwapo hali haitabadilika na kuongeza kwamba mifuko ya plastiki huingia humu nchini kiharamu kutoka Uganda, Tanzania na Somalia.

Wanabodaboda ndio hutumika sana na wanabiashara kufikisha mifuko hiyo bila kugunduliwa na maafisa wa usalama.

Wafanyibiashara kumi walinaswa kwenye msako huo na Jumanne walifikishwa kwenye Mahakama ya Kibera ili kujibu mashtaka ya kupatikana na bidhaa haramu.

Hali iligeuka tete wenzao walipowakabili wanahabari waliokuwa wakinasa tukio hilo na ikabidi maafisa waliokuwepo kukaa macho zaidi ili kuwalinda.

Habari za operesheni hiyo ilienea haraka mno sokoni na mara moja shughuli za kibiashara zikasimama wengi wakiyafunga maduka yao kutokana na hofu ya kukamatwa.

Waziri wa Mazingira na Maliasili Keriako Tobiko alitoa onyo kali kwa maduka ya jumla na wafanyibiashara kwamba sheria itawakabili vilivyo wasipotii marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki.

Hali ya hatari nchini Ethiopia kudumu kwa miezi sita ijayo

Waziri wa Ulinzi nchini Ethiopia, Bw Siraj Fegessa. Picha/ Hisani

Na MASHIRIKA

HALI ya tahadhari iliyotangazwa nchini Ethiopia baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo itadumu kwa miezi sita, amesema waziri wa ulinzi nchini humo.

Aidha, hilo linalenga kuzima maandamano ya kisiasa na shinikizo za uhuru wa kujieleza kutoka kwa vyama vya kutetea haki za binadamu.

Tangazo hilo lilitolewa kwa mara ya kwanza na shirika la habari la serikali, baada ya mkutano wa baraza la mawaziri mnamo Ijumaa.

Kulingana na serikali, hilo linajumuisha marufuku dhidi ya magazeti ama majarida yoyoye “yanayoweza kuwachochea raia ama kuzua migawanyiko ya kisiasa.”

“Lengo kuu la serikali ni kukabili uwezekano wowote wa kuzuka kwa mapigano. Hatutaki hali ambapo watu wanapoteza maisha yao bila sababu zozote,” akasema Waziri wa Ulinzi, Siraj Fegessa.

Aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Hailemariam Desalegm alijiuzulu mapema wiki iliyopita “ili kutoa nafasi kwa mwafaka wa kisiasa kupatikana.” Bw Desalegm pia alijiuzulu kama kiongozi wa chama tawala cha Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF).

Agizo hilo linatarajiwa kupitishwa na Bunge kwa muda wa siku 15 zijazo.

 

Tobiko aanza kazi kwa kuonya wafanyabiashara haramu wakatao miti

Waziri mpya wa Mazingira na Misitu, Keriako Tobiko. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

WAZIRI wa Mazingira na Misitu Keriako Tobiko ameapa kukabiliana na wafanyabiashara laghai wanaokata miti ovyo bila kibali.

Bw Tobiko, aliyekuwa akizungumza mara baada ya kutwaa rasmi wizara kutoka kwa Bi Judi Wakhungu, alionya kuwa maafisa wa wizara wanaoshirikiana na wafanyabiashara hao laghai watatimuliwa na kushtakiwa.

Waziri Tobiko alisema lengo lake kuu ni kuhakikisha kuwa asilimia 10 ya ardhi ya Kenya inakuwa na miti, kulingana na katiba.

“Nimekuwa nikisoma katika vyombo vya habari kwamba maafisa wa serikali wanashirikiana na wafanyabiashara laghai kukata miti ovyo kinyume cha sheria. Ninawaonya kuwa wahusika wote watakamatwa na kushtakiwa bila kujali urafiki wao na viongozi wa juu serikalini,” akasema Bw Tobiko.

Alionya kuwa wafanyabiashara waliopewa kibali cha kukata miti watapokonywa leseni hizo iwapo watapatikana wakikiuka sheria.
Waziri alitoa onyo hilo huku idadi ya malori yanayosafirisha mbao kutoka Mlima Kenya na misitu ya Aberdare na mistu mingineyo yakizidi kuongezeka.

Hali hiyo imewatia hofu wanaharakati wa kutunza mazingira hasa kutoka maeneo ya Mlima Kenya kuhofia kwamba wakataji miti haramu wamepenyeza katika misitu hiyo ambayo ni vyanzo vya maji.

“Sheria inahitaji kuwa unapokata mti unapanda mwingine, lakini wao wanakata bila kupanda. Wafanyabiashara wa aina hiyo watapokonywa leseni na kukabiliwa kisheria,” akasema.

Bw Tobiko alisema kuwa marufuku dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki itaendelea.

“Juhudi za watu wanaopinga marufuku ya mifuko ya plastiki kutaka marufuku kuondolewa haitafua dafu,” akasema Bw Tobiko.

 

Chanzo cha uskwota Pwani ni unyakuzi wa ardhi – Ripoti

Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi Dkt Muhammad Swazuri. Picha/ Maktaba

Na KAZUNGU SAMUEL

KISA cha majuzi katika Kaunti ya Kwale ambapo watu kutoka Nairobi walivamia ranchi moja na kudai kuimiliki, ni mojawapo ya visa vinavyoonyesha kusambaa kwa shida za mashamba katika ukanda wa Pwani.

Kulingana na mshirikishi wa masuala ya ardhi katika ukanda wa Pwani, Bw Nagib Shamsan, tatizo la uskwota na mashamba Pwani linaendelea kwa kuwa hakuna serikali ambayo iko tayari kulishughulikia.

“Mwaka wa 2009 kulikuwa na ripoti ya Jopo la Njonjo ambalo ilibuniwa kuchunguza kwa kina shida za mashamba katika ukanda wa Pwani.

Nilihusika pakubwa katika kutayarisha ripoti hiyo na ilikuwa na mapendekezo makubwa ambayo yangetatua shida za mashamba Pwani,” akasema Bw Shamsan kwenye mahojiano na Taifa Leo jijini Mombasa.

Afisa huyo alisema kuwa ripoti hiyo ililenga sana eneo la Maili Kumi katika ukanda wa Pwani ambako visa vya watu kuvamia mashamba na kudai ni ya mababu zao vimezagaa.

Katika ripoti hiyo, iligundulika kuwa ni familia chache ambazo zinamiliki ardhi katika ukanda wote wa Pwani huku wakazi wengi wakiwa maskwota. Visa hivyo vingi vinapatikana katika kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale.

“Katika ripoti hiyo tuligundua kwamba kuna familia 128,900 ambazo ni maskwota katika eneo la Pwani. Wenye mashamba wasiokuwepo wanamiliki ekari 77,753 za mshamba katika eneo la Pwani.

Ni mashamba haya ambayo yamekuwa kiini cha mizozo kati ya wakazi na maajenti wa wamiliki hao. Wengi wa wamiliki wanaishi katika mataifa ya Kiarabu,” akasema Bw Shamsan kwenye mahojiano yetu.

 

Lawama

Hata hivyo, alilaumu serikali kwa kushindwa kumaliza shida ya mashamba katika eneo la Pwani licha ya kuwa na uwezo wa kuweza kutimiza hilo.

Naye afisa mkuu wa shirika la Kenya Land Alliance,  Bw Odenda Lumumba alisema kwenye mahojiano yetu kwamba serikali imeamua kupuulizia mbali suala la ardhi katika eneo la Pwani.

Alisema serikali inafahamu  fika jinsi inavyoweza kumaliza shida hiyo lakini kutokana na ulegevu, imeamua suala hilo libakie kama donda ndugu kwa Wakenya.

“Hivi majuzi, Tume ya Ardhi nchini (NLC) kupitia kwa mwenyekiti wake Prof Muhhamad Swazuri ilitangaza kwamba itaanza kuchukua ardhi za mabwenyenye na kuwagawanyia wananchi.

Lakini lazima tufahamu kuwa Prof  Swazuri na wengine waliowahi kushughulikia suala la ardhi walisema na bado hakuna kitu ambacho wametekeleza.

Serikali haina nia ya kumaliza shida za mashamba katika Pwani,” akasema Bw Lumumba.

 

Jeshi latoa ahadi ya kusajili wanawake zaidi siku zijazo

Zoezi la kuwasajili makurutu katika jeshi la Kenya eneo la Lamu Februari 2018. Picha/ Maktaba

Na WAIKWA MAINA na NICHOLAS KOMU

WANAWAKE zaidi watajiunga na Jeshi la Kenya (KDF) katika shughuli zijazo za kuwatafuta makurutu, amesema afisa mmoja mkuu wa jeshi.

Luteni Kanali Edward Onyango alisema kwamba maafisa wakuu katika jeshi hilo wanafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba limezingatia usawa wa kijinsia katika utaratibu wake wa uajiri.

Akizungumza Jumatatu katika uwanja wa Ol Kalou, kaunti ya Nyandarua wakati wa kusajili makurutu, Bw Onyango alisema kwamba jeshi limejitolea kuhakikisha kuwa vigezo vyote vya usawa wa kijinsia vimezingatiwa.

“Tunafanya mashauriano kuhakikisha kwamba wanawake zaidi wamejiunga na jeshi katika awamu zijazo za kutafuta makurutu. Tumejitolea kuhakikisha kwamba wao pia wamepata nafasi ya kuhudumia nchi yao.

Licha ya hayo, siwezi kutaja kwa undani wa mikakati hiyo, ila kila mmoja anapaswa kufahamu kwamba kuna mikakati inayoendelea kukabili hali hiyo,” akasema.

Kwenye zoezi hilo, changamoto kuu waliyokumbana nayo katika eneo hilo ni viwango vya chini vya elimu.

 

Elimu na umri

“Tumewakataa watu wengi kwa kukosa stakabadhi zifaazo za elimu. Pia, tumeshangazwa na idadi kubwa ya watu waliopitisha umri unaotakikana. Ilitulazimu kuwakataza kushiriki katika zoezi hilo. Hata hivyo, tumeridhishwa na idadi ambayo ilijitokeza,” akasema.

Kwa majuma kadhaa yaliyopita, kumekuwa na malalamishi kutokana na idadi kubwa ya wanawake ambao walizuiwa kushiriki katika zoezi hilo.

Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na hali hiyo ni Samburu, Kwale na Laikipia .

Awali, msemaji wa Jeshi, Kanali David Obonyo alikuwa amesisitiza kwamba jeshi limejitolea kuhakikisha linawaajiri wanawake wa kutosha, kulingana na katiba.

 

Shujaa Kimathi

Kwingineko, familia ya aliyekuwa mpiganiaji uhuru, Dedan Kimathi imeanza upya rai za kuitaka serikali ya Uingereza kufichua alikozikwa shujaa huyo.

Huo ndio ulikuwa mwito mkuu kwenye maadhimisho ya miaka 61 tangu kukamatwa kwa shujaa huyo. Mjane wake, Bi Mukami Kimathi, hakuhudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa uwanja wa Dedan Kimathi mjini Nyeri mnamo Jumapili kutokana na matatizo ya kiafya.

Jamaa na viongozi waliohudhuria walimtaka Malkia Elizabeth wa Uingereza kukubali rai ya kumwandalia marehemu mazishi ya kishujaa.

Waliozungumza walisema Shujaa Kimathi anafaa kupewa mazishi yanayoafiki mtu wa hadhi aliyokuwa nayo alipokamatwa na kisha kunyongwa na wakoloni.

 

Polo asukumiwa makonde mazito kwa kunyima mama hela za saluni

Na CORNELIUS MUTISYA

KAVIANI, MACHAKOS

KIOJA kilishuhudiwa eneo hili mama wa umri wa makamo alipomsukumia mumewe makonde mazitomazito alipomnyima hela za kwenda saluni kusukwa.

Kulingana na mdaku wetu, polo aliuza parachichi kwa mawakala na alipotia kibindoni hela, akili ilimruka na akafululiza moja kwa moja kwa mama pima kujienjoi.

“Hakika, maskini akipata, matako hulia mbwata. Polo alipouza avakado, alijitoma baa kujienjoi na kusahamu majukumu yake mengine,’’ alisema mdokezi.

Twaarifiwa kwamba, polo alikuwa ameuza matunda hayo baada ya kuafikiana na mama watoto kuwa angemkabidhi hela zote ili aende saluni kusukwa, kugharimia vipodozi vyake na kununua chakula. Hata hivyo alighairi nia alipopata hela hizo.

Na alipokuwa akibugia mvinyo, mama watoto alijitoma ndani ya baa akiwa amepandwa na hasira za mkizi na akamparamia. Alimwaga pombe yote iliyokuwa mezani na akaanza kumfokea kwa hamaki.

“Umeuza avakado ili uje kulewa? Nipe hela za saluni haraka!’’ mama alimfokea mumewe.

Inasemekana kwamba, rabsha ilizuka ndani ya baa na mama watoto akamtwanga mumewe makonde mazitomazito nusura aone vimulimuli. “ Jamaa alikuwa amelewa kiasi cha kutojikinga dhidi ya kipigo cha mkewe,” alieleza mdokezi.

Hata hivyo, walevi waliingilia kati na kuwatenganisha wawili hao. Walimhimiza polo ampe mama watoto hela zilizobaki ili aende saluni kama walivyokuwa wamekubaliana wakiwa kwao nyumbani.

“Polo alimkabidhi mkewe pesa zilizobaki na hali ikawa shwari,” alisema mdaku wetu.
Mama alimuonya mumewe akome kumchezea kisha akaenda zake saluni na akaawacha walevi wakiendelea kupiga mtindi.

 

TAHARIRI: Umma usitwikwe mzigo wa madeni

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Patrick Njoroge. Deni la Kenya kwa sasa linakaribia Sh4 trilioni, hilo likimaanisha kwamba kiwastani, kila Mkenya ana wastani wa deni la Sh100,000 Picha/ Maktaba

Na MHARIRI

SERIKALI inapaswa kuzingatia ushauri wa mashirika ya kifedha kubuni mikakati ambayo itaipunguzia nchi deni la kitaifa.

Ushauri huo umetolewa na shirika la kifedha la Cytonn, ambalo limeonya kwamba Wakenya wanapaswa kuwa na hofu kutokana na kiwango kikubwa cha deni hilo, ambalo linaendelea kuongezeka kila kuchao.

Kulingana na ripoti kadhaa ambazo zimetolewa na mashirika mbalimbali ya kifedha, deni la Kenya kwa sasa linakaribia Sh4 trilioni, hilo likimaanisha kwamba kiwastani, kila Mkenya ana wastani wa deni la Sh100,000.

Kimsingi, huu ni mwelekeo wa kutia hofu, ikizingatiwa kwamba Kenya ingali taifa changa ambalo uchumi wake ni wa kiwango cha wastani.

Uchumi wetu ni mdogo sana, ikilinganishwa na nchi kama Amerika, Uingereza, Uchina, Japan, Ujerumani kati ya zingine.
Utathmini wa kina wa sababu kuu za ustawi wa chumi hizo unabainisha kwamba mojawapo ya nguzo kuu huwa ni kudhibiti deni la kitaifa la nchi.

Aidha, hilo huziwezesha sana nchi hizo kuendeleza mipango yake ya kimaendeleo bila changamoto za kifedha kwani huwa hazina matatizo kupata usaidizi kutoka kwa mashirika kama Benki Kuu ya Dunia ama Shirika la Kimataifa la Kifedha (IMF).

Hata hivyo, makosa mengi ya nchi zinazostawi ni kuwa, huwa zinachukua mikopo mikubwa kuwekeza katika miundomsingi, ila fedha nyingi hupotelea katika sakata za ufisadi.

 

Kisiki

Na ikiwa dhahiri kwamba Kenya imekuwa ikichukua mikopo mingi kuwekeza katika miundomsingi ya kuistawisha kiuchumi, pana haja kubwa kwa serikali kutathmini njia za kuhakikisha kuwa deni hilo haligeuki kuwa kisiki wa wananchi.

Njia ya kwanza ya kuhakikisha hayo ni kuwianisha Ajenda Nne za Maendeleo za Serikali na mikakati ambayo itachangia pakubwa katika uzalishaji wa fedha, ambazo zitaisaidia nchi kulipa madeni hayo kwa mapato yake yenyewe.

Pia, lazima ihakikishe kwamba wanaopatikana wakishiriki katika ufisadi wanakabiliwa vikali ili kuhimiza hali ya uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.

Hayo ndiyo yatahakikisha kwamba hatujipati katika mgogoro wa kifedha, kama ilivyojipata Ugiriki kwa kukosa kudhibiti deni lake la kitaifa.