TAHARIRI: Wabunge waache kutumiwa visivyo

Bw Rashid Achesa aliyeidhinishwa na  wabunge kusimamia Wizara ya Michezo. Picha/Maktaba

Na MHARIRI

Kifupi:

 • Ni muhimu wabunge watathmini kwa kina uwezo wa baadhi ya walioteuliwa na kuzingatia masuala nyeti yaliyoibuliwa
 • Wabunge wa Jubilee waweke maslahi ya chama kando, na kuhakikisha wamewapa Wakenya mawaziri wanaofaa
 • Kuna Wakenya wengi wanaohitimu kuongoza wizara  kwa hivyo haifai kwa Rais kuteua wasiofaa kwa sababu za kisiasa
 • Dkt Matiang’i alifanya kazi mufti katika sekta ya elimu na ni vyema wabunge wapate sababu kwa nini alihamishwa

BAADA ya kuwapiga msasa watu waliopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kuhudumu katika Baraza la Mawaziri, wabunge jana walianza kuijadili ripoti kuhusu shughuli hiyo.

Tayari kuna utata kuhusu kiwango cha masomo cha baadhi ya walioteuliwa, na ni muhimu wabunge watathmini kwa kina uwezo wa baadhi ya walioteuliwa na kuzingatia masuala nyeti yaliyoibuliwa na umma kuwahusu.

Kwa mara nyingine, inasikitisha kuwa wabunge wa upinzani walisusia kikao cha kujadili ripoti hiyo Jumatano na kuachia wabunge wa chama tawala cha Jubilee nafasi ya wazi kuidhinisha majina hayo.

Ni muhimu wabunge husika wa Jubilee waweke maslahi ya chama chao kando, na kuhakikisha wamewapa Wakenya mawaziri wanaofaa kuwahudumia kikamilifu, bila kujiingiza katika masuala ya siasa.

Wito wetu ni kwa wabunge husika wasisite kutowaidhinisha baadhi ya walioteuliwa iwapo kuna ushahidi wa kutosha kuwa hawataweza kuchapa kazi ipasavyo.

Alipotangaza Baraza la Mawaziri, Rais Kenyatta alisema anaendelea kuunda serikali yake, na kwa hivyo kuna nafasi ya kufanya mabadiliko.

Kauli hiyo inatoa fursa kwa Wakenya kumpa Rais Kenyatta rai zao, kuhusiana na baadhi ya watu aliowapendekeza.

Mmoja wa walioteuliwa alieleza wabunge wazi kuwa elimu yake iliishia shule ya msingi na ni muhimu kudumisha hadhi ya afisi ya waziri wa serikali kwa kuhakikisha kuwa anafuzu kuongoza wataalamu wengine katika wizara yake.

Kando na utata wa kiwango cha masomo miongoni mwa baadhi ya walioteuliwa, kumeibuka tashwishi kuhusiana na kuhamishwa kwa Dkt Fred Matiang’i kutoka Wizara ya Elimu hadi ile ya Usalama.

 

Sababu ya Matiang’i kuhamishwa

Ni wazi Dkt Matiang’i alifanya kazi mufti katika sekta ya elimu na ni vyema wabunge wapate sababu nzuri kutoka kwa rais kwa nini waziri huyu ahamishwe hadi wizara ya usalama.

Sharti wabunge watathmini masuala kama haya kwa kina kabla ya kuwaidhinisha waliopendekezwa.

Kuna Wakenya wengi wanaohitimu kuongoza wizara na idara mbalimbali za serikali kwa hivyo haifai kwa Rais kushinikiza kuteua wasiofaa kwa sababu za kisiasa.

Itakuwa jambo la busara kwa rais kuhakikisha hatamu yake ya mwisho uongozi haijakumbwa na msukosuko kutokana na uzembe na ufisadi kwa kuwateua watu wenye maadili na waliohitimu.

Wakenya wafukuza donge nono Diamond League, wakwepa Jumuiya ya Madola

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI wengi nyota wa Kenya hawajasisimuliwa na mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika nchini Australia mnamo Aprili 4-15, 2018.

Badala yake wameamua kutafuta donge nono kwenye Riadha za Diamond League.

Baadhi ya watimkaji shupavu walioamua kulenga macho yao kwa Riadha za Diamond League zitakazofanyika kutoka Mei 4 hadi Agosti 31, 2018 ni bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 800, David Rudisha.

Mshikilizi huyu wa rekodi ya dunia ya mbio hizo za mizunguko miwili alishinda medali ya fedha miaka minne iliyopita Kenya ilipomaliza juu ya jedwali la riadha kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola kwa dhahabu 10, fedha 10 na shaba tatu.

Bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 1,500 mwaka 2008 Asbel Kiprop, mfalme wa Nusu-Marathon duniani Geoffrey Kamworor na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya mbio za kilomita 21 Peres Jepchirchir hawatashiriki mashindano hayo nchini Australia.

Kiprop ameamua kuelekeza nguvu zake katika maandalizi ya Riadha za Diamond League, ambazo mshindi hutunukiwa Sh5, 062,500.

Bingwa wa New York City Marathon Kamworor atatetea taji lake la Nusu-Marathon duniani mnamo Machi 24, siku chache tu kabla ya mashindano ya Jumuiya ya Madola kuanza.

Jepchirchir, ambaye alishinda Nusu-Marathon duniani mwaka 2016 jijini Cardiff, Wales, yuko katika likizo ya uzazi.  Kamworor na Jepchirchir walijishindia karibu Sh3, 039,060 kila mmoja jijini Cardiff.

Malkia wa mbio za mita 1,500, Chepng’etich, ambaye alinyakua mataji ya Jumuiya ya Madola (2014), Olimpiki (2016) na Dunia (2017), pia yuko katika likizo ya uzazi.

Bingwa wa mbio za mita 800 wa Jumuiya ya Madola mwaka 2006, Janeth Jepkosgei, 34, ni mmoja wa wakimbiaji 170 walioalikwa kushiriki mchujo wa kuunda timu ya kuenda Australia.

Mchujo huo utafanyika katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi hapo Februari 17, 2018. Wanariadha 60 watapata tiketi ya kupeperusha bendera ya Kenya mjini Gold Coast, Australia.

Chebii kutetea taji la Lake Biwa Mainichi Marathon, Japan

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Ezekiel Chebii amethibitisha atatetea taji la Lake Biwa Mainichi Marathon nchini Japan hapo Machi 4, 2018.

Chebii, 27, anajivunia muda bora kuliko wapinzani wake katika mbio hizi za kilomita 42 wa saa 2:06:07 aliotimka mjini Amsterdam nchini Uholanzi mwaka 2016.

Mahasimu wake wakuu ni Mswizi Tadesse Abraham, 35, na Muethiopia Abera Kuma, ambao walitimka muda wao bora wa saa 2:06:40 na 2:05:56 mwaka 2016 na 2014, mtawalia. Watatu hawa wanapigiwa upatu kutwaa taji la mwaka 2018.

Hata hivyo, kuna wakimbiaji wengine ambao hawawezi kupuuzwa. Wakimbiaji hao ni bingwa wa Gold Coast Marathon mwaka 2017 Takuya Noguchi, Satoru Sasaki, Takuya Fukatsu, Fumihiro Maruyama, Kenta Murayama, Asahi Kasei na Masato Imai (wote kutoka Japan).

Jake Robertson (New Zealand) na mkazi wa Japan, Macharia Ndirangu (Kenya) wanakamilisha orodha ya wakimbiaji wanaoweza kushinda makala haya ya 73.

Daniele Meucci (Italia), Cristhian Pacheco (Peru), Mohammed Zani (Morocco), Samson Gebreyohannes (Eritrea) na Mkenya Michael Githae (Kenya) pia wako katika orodha ya washiriki watajika.

UEFA Valentino Dei: KTN Home kuonyesha Liverpool ikivaana na Porto

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Liverpool na straika wa timu ya taifa ya Brazil, Roberto Firmino wamesema kwamba uthabiti unaojivuniwa na miamba hao wa soka ya Uingereza katika safu yao ya uvamizi ni moja kati ya mambo yatakayowachochea kuyazima makali ya FC Porto usiku wa Jumatano nchini Ureno.

Vikosi hivyo viwili vitashuka dimbani kuvaana katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Estadio do Dragao saa 22.45.

Kipute hicho kitapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya KTN Home kwa ushirikiano na kampuni ya Mediapro kutoka Uhispania.

Kwa mujibu wa kocha Jurgen Klopp, kikubwa zaidi kitakachowatambisha vijana wake ni kiu ya kuendeleza ubabe walioudhirisha katika mechi za makundi ambapo Liverpool waliibuka kidedea baada ya kuwapiga kumbo Sevilla, Maribor na Spartak Moscow.

 

Mabao 23

Katika kampeni hizo, masogora hao wa Klopp walitikisa nyavu za wapinzani mara 23 huku Firmino akipachika wavuni jumla ya mabao sita.

Nyota mzawa wa Misri, Mohamed Salah ambaye anatazamiwa Jumatano kuongoza idara ya ushambuliaji ya Liverpool alitia kapuni mabao matano sawa na kiungo Phillipe Coutinho aliyejiunga na Barcelona mnamo Janauri 2018.

Liverpool wanajibwaga katika mchuano huo wakitawaliwa na motisha ya kuwakomoa Southampton 2-0 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza wikendi iliyomshuhudia Salah akijizolea bao lake la 29 hadi kufikia sasa katika michuano yote aliyowapigia waajiri wake hao.

 

Virgil van Dijk

Mchuano huo utakuwa jukwaa mwafaka vilevile kwa beki ghali zaidi duniani, Virgil van Dijk kudhihirisha ukubwa wa uwezo alionao katika soka ya bara Ulaya huku Porto wakipania kuzitegemea pakubwa huduma za mafowadi Vincent Aboubakar na Moussa Marega.

Hadi kufikia sasa, Aboubakar amewafungia Porto jumla ya mabao 26 kutokana na michuano 32 iliyopita huku Marega akizititiga nyavu za wapinzani wao mara 16 katika mechi 20 zilizopita.

Marwa kusimamia Kombe la Dunia Urusi

 

Refa bora wa mwaka 2017 wa kunyanyua kibendera nchini Aden Range Marwa. Picha/ Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

REFA bora wa mwaka wa kunyanyua kibendera nchini Kenya mwaka 2017, Aden Range Marwa amejumuishwa katika orodha itakayokuwa katika Kombe la Dunia nchini Urusi mnamo Juni 14 hadi Julai 15, 2018.

Marwa, ambaye ni mwalimu wa somo la hisabati na kemia katika shule moja ya upili kutoka Kaunti ya Migori, ni Mkenya pekee katika orodha hiyo.

Marefa waliochaguliwa kutoka Afrika na Shirikisho la Soka duniani (FIFA) ni Grisha Ghead (Misri), Abid Charef Mehdi (Algeria), Sikazwe Janny (Zambia), Tessema Weyesa Bamlak (Ethiopia), Diedhiou Malang (Senegal) na refa bora Barani Afrika mwaka 2014, 2015 na 2016 Gassama Bakary Papa (Gambia).

Marefa wasaidizi (wanyanyuaji vibendera) ni Etchiali Abdelhak (Algeria), Hmila Anouar (Tunisia), Camara Djibril (Senegal), Samba El Hadji Malick (Senegal), Birumushahu Jean Claude (Burundi), Aden Range Marwa (Kenya), Achik Redouane (Morocco), Ahmed Waleed (Sudan), Dos Santos Jerson Emiliano (Angola), Siwela Zakhele Thusi (Afrika Kusini), Safari Olivier (Ivory Coast) na Ssonko Mark (Uganda).

Timu za taifa za Misri, Tunisia, Morocco, Senegal na Nigeria zilifuzu kuwakilisha Bara Afrika nchini Urusi. Mataifa 32 yatashiriki Kombe la Dunia ambapo mechi 64 zitasakatwa katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.

Filamu ya kimataifa ‘Black Panther’ yazinduliwa jijini Kisumu

Mwigizaji maarufu kutoka humu nchini Lupita Nyong’o (kushoto) akiigiza katika filamu mpya ya kimataifa ‘Black Panther’. Picha/ Hisani

NA CECIL ODONGO

FILAMU ya aina yake ya muigizaji maarufu nchini Lupita Nyong’o ‘Black Panther’ ilizinduliwa Jumanne rasmi kwa mara ya kwanza humu nchini na Afrika nzima kwenye hafla ya haiba kubwa iliyoandaliwa jijini Kisumu.

Lupita mwenye umri wa miaka 34, anatazamwa kama muigizaji bora kutoka bara la Afrika kwenye jukwaa la sinema za Hollywood.

Kuandaliwa kwa onyesho hilo hapa nchini ni njia moja ya kumpa heshima na kumtunuku kwa juhudi zake zilizomfikisha kwenye anga za juu za uigizaji.

Japo mshindi huyo wa tuzo za Oscar hakuhudhuria sherehe hiyo, viongozi wa kaunti ya Kisumu wakiongozwa na Naibu Gavana wa Kisumu Mathews Owili, waziri wa Michezo na Utamaduni kwenye kaunti Bi Achi Ojany Alai miongoni mwa wageni wengine mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi walikUwepo kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Ratiba ya Lupita iliwa na shughuli nyingi kwa hivyo hangeweza kupata muda wa kufika nchini.

 

Ujasusi

Kwenye sinema ‘Black Panther’ Lupita huigiza kama mhusika Nakia ambaye ni jasusi kwenye ufalme unaoitwa Wakanda. Yeye ni moja wa wa wenye usemi mkubwa kwenye familia ya Wakanda.

Ilikuwa ni fahari kubwa kwa mji wa Kisumu kuteuliwa kuandaa uzinduzi huo wa kwanza Afrika japo kuna miji kadhaa ya hadhi barani. Kaunti ya Kisumu ndiko anakotoka mwigizaji Lupita na babake Prof Peter Anyang’  Nyong’o ambaye ndiye gavana.

Hoteli nyingi za mji huo zilizaa wageni huku tiketi za ndege kuelekea mji huo kutoka kwingineko zikichukuliwa zote na wasafiri walioenda kushuhudia uzinduzi huo.

Vyombo vya habari vya kimataifa na vya ndani ya nchi pia havikusazwa kwa kuwa vyote vilikuwepo kunasa matukio yote.

Kutakuwa na utazamaji wa sinema hiyo Jumatano Siku ya Wapendanao kule Anga Sky Cinema, Nairobi na shoo ya kwanza kwa umma itafanyika Alhamisi Anga IMAX.

Uzinduzi huo aidha umetuliza joto la kisiasa katikakaunti hiyo anakotoka kinara wa NASA Raila Odinga aliyeapishwa kuwa ‘rais wa wananchi.’

Wakazi wa kaunti hiyo walionekana kufurahia kumuona mmoja wao akiigiza katika filamu ya Hollywood, hali iliyoondoa fikra za kisiasa katika Siku ya Valentino.

FUNGUKA: ‘Amenigeuza ngoma ila nampenda kupindukia’

Na PAULINE ONGAJI

Kwa Muhtasari:

 • Huenda binti huyu akavunja rekodi kwa kuongoza orodha ya vipusa walioleweshwa na kupumbazwa na penzi
 • Japo binti huyu kabarikiwa na urembo na kiakili, hana bahati katika masuala ya mahaba
 • Nilipomhoji mume wangu, alinishambulia kwa mangumi na mateke, kitendo kilichoniacha na majeraha mabaya
 • Marafiki zangu wamefanya kila wawezalo kunitenganisha naye lakini kwangu penzi hili hatari ni sumaku

UNAPOPATA  fursa ya kusikia hadithi ya Miriam, 30, hauna shaka ila kuamini waliyosema wahenga kuwa kipendacho roho hula nyama mbichi.

Huenda binti huyu ambaye ni mhudumu wa kiafya katika mojawapo ya hospitali kuu eneo la Nakuru akavunja rekodi kwa kuongoza orodha ya vipusa walioleweshwa, kuduwazwa na hata kupumbazwa na penzi.

Kwanza kabisa hebu nikupe maelezo mafupi kumhusu. Alizaliwa mtoto wa nne katika familia yao eneo la bonde la ufa ambapo tangu utotoni alikuwa aking’aa kimasomo.

Kwa bahati mbaya hakufaulu kupata alama za kutosha kumwezesha kusomea udaktari, lakini kutokana na penzi lake la masuala ya matibabu akaamua kusomea uuguzi.

 

Donge nono

Baada ya kukamilisha kozi yake chuoni, binti huyu alibahatika kupata ajira katika mojawapo ya hospitali zinazotambulika ambapo huu ukiwa mwaka wake wa sita katika kazi hii, ni miongoni wa wahudumu wa kiafya wanaoheshimika na kupokea donge nono katika hospitali hiyo.

Isitoshe, uzuri wake kisura na kimaumbile umemfanya kuwa kivutio cha wanaume wengi hasa anakofanya kazi.

Lakini japo binti huyu kabarikiwa na urembo na akili, hana bahati katika masuala ya mahaba. Bibi huyu amenasa jicho la kaka fulani ambaye ni mwanajeshi ambapo wamekuwa wachumba kwa miaka mitano sasa.

Kinachofanya uhusiano wao usiwe wa kawaida ni kwamba miaka michache iliyopita binti huyu aligundua kuwa dume hili lilikuwa na mke na watoto ambao lilikuwa limewaficha eneo la mashambani.

 

Mangumi na mateke

“Niligundua kupitia simu niliyopokea kutoka kwa mwanamke aliyejitambulisha kama mkewe, akiniarifu kuwa kaka huyu ni mumewe na baba ya wanawe watatu.

Nilipomhoji mume wangu, alinishambulia kwa mangumi na mateke, kitendo kilichoniacha na majeraha mabaya kiasi cha kunifanya kulazwa hospitalini kwa mwezi mmoja.

Na pigo hili limekuwa kama ada kila ninapomuuliza kuhusu mkewe ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu nilipogundua.

Kwa mfano nakumbuka wakati mmoja alinipiga vibaya na kunivunja miguu, hatua iliyoaniacha nikitumia kiti cha magurudumu kwa mwezi mmoja. Kadhalika kuna wakati ambapo alinipiga na kunifanya nipoteze mimba ya miezi mitatu, vile vile kupoteza fahamu kwa wiki mbili.

 

Kichapo chageuka sumaku

Lakini la kushangaza ni kuwa muda unavyozidi kusonga ndivyo ninavyozidi kumpenda mwanamume huyu huku kichapo chake kikiwa sumaku kwake. Baada ya kupona majeraha ninayoyapata mikononi mwake, mimi mwenyewe ndiye humtafuta.

Kisa hicho cha mwisho ambapo nilipoteza mimba, mambo yalikuwa mabaya sana kiasi cha kuwa ndugu yangu alipiga ripoti polisi na kuhakikisha kwamba ametiwa nguvuni. Lakini ni mimi mwenyewe niliyemlipia dhamana na kumuondoa jela na kukataa kumshtaki mahakamani.

Jamaa na hata marafiki zangu wamefanya kila wawezalo kunitenganisha naye lakini kwangu penzi hili hatari ni sumaku ambapo sawa na ndimu inavyoongeza ladha kwenye uji, linazidi kunoga kila ninapopokea kichapo”.

WANGARI: NASA yafaa ielekeze nguvu zake katika siasa za ustawi

Vinara wa NASA Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wakihutubu. Picha/ Maktaba

Na MARY WANGARI

KATIKA mahojiano ya dakika tatu na BBC wiki iliyopita, kiongozi wa NASA Raila Odinga alitaka uchaguzi mpya ufanyike kufikia Agosti lakini akakana njama za kuongoza mapinduzi ya serikali.

Hamna shaka kwamba kiongozi huyo wa upinzani, na muungano wake wa kisiasa, ana masuala ambayo hayajatatuliwa na mara kwa mara wameeleza malalamishi yao kuhusu mchakato wa uchaguzi uliosababisha marudio ya uchaguzi mwaka jana.

Hata hivyo, inasikitisha kwamba Raila yamkini anaelekeza malalamishi yake kwa watu wasiofaa. Madai ya uchaguzi mpya yamekuwa mojawapo ya mbinu ambazo yeye na vinara wenzake wa NASA wamekuwa wakitumia kuihangaisha serikali ya Jubilee.

Lakini ni kana kwamba kinara mwenza wa NASA anachukua mkondo tofauti, ambapo katika mkutano wa hadhara hivi majuzi alihimiza kuwepo kwa mjadala kati ya upinzani na Rais Uhuru Kenyatta, ili “kupunguza joto la kisiasa”.

 

Walakini

Wakati muungano kama NASA unapojitwika jukumu la kushinikiza uchaguzi mpya miezi michache tu baada ya mapambano makali ya siasa ambapo watu walitoa uamuzi wao, inadhihirisha bayana kuwepo kwa walakini fulani.

Kwingineko, matamshi kama yale ya Moses Wetangula yanarejesha Wakenya katika mazingira ya uchaguzi, jambo ambalo halifai kabisa.

Matamshi hayo yalisababisha wawekezaji kurefusha muda wao wa ‘kungoja na kuona’, ulioathiri kiasi uchumi mwaka jana kufuatia kucheleweshwa kwa uwekezaji wenye thamani ya mabilioni.

Jinsi tunavyofahamu, mwaka 2017 Kenya ilipitia kipindi kigumu cha kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu Agosti, uchaguzi wa marudio uliofuatia Oktoba 25 pamoja na kesi kali za uchaguzi.

Ni dhahiri kwamba taifa linahitaji mno kuondokewa visanga vya kisiasa kama vile vinavyoonyeshwa na upinzani na kujishughulisha na maendeleo ya kitaifa.

 

Waepuke ubinafsi

Iwapo kweli NASA ina nia njema kwa taifa, viongozi wake sharti waepukane na mwelekeo wa kibinafsi wa siasa unaojisawiri kuwa kisingizio cha kujali maslahi ya wananchi.

Wakati umewadia kwa siasa kali na wanaoziendeleza kusalia nyuma ili kuwezesha taifa kusonga mbele.

Ni muhimu kukumbuka kwamba, huku upinzani ukiwa na nafasi ya kuchangia katika demokrasia, shughuli hiyo ifanywe kwa kujali maslahi ya wananchi ambao ndio wakuu.

Ikiwezekana, kuifanya serikali iliyopo kuwajibika pasipo kugeukia visanga visivyo na manufaa na kulalamika kila uchao.

Ni muhimu kwa upinzani kukomesha msimamo wake wa kundi la wapiganaji na badala yake kugeukia siasa zenye mwelekeo unaojali maslahi ya wananchi ili kuwezesha manufaa ya kila mwananchi kwa jumla.

NGILA: Jubilee ikabiliane na visiki hivi ili kutimiza Ajenda Nne Kuu

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wahutubia taifa katika Ikulu ya Nairobi. Picha/ Maktaba

Na FAUSTINE NGILA

Kwa Muhtasari:

 • Katika mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, serikali inalenga kuimarisha sekta za viwanda, afya, ujenzi na kilimo 
 • Mwelekeo ambao taifa hili linafuata ni wa hasara kwa wananchi wote
 • Utawala wa serikali unafaa kutambua kuwa amani hutokana na haki na si kinyume chake
 • Wakenya wanakumbana na gharama ya juu ya maisha, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa na utovu wa usalama

SERIKALI ya Jubilee imekariri kuwa itaunda zaidi ya nafasi 1.29 milioni za ajira kutokana na viwanda kufikia mwaka 2022.

Hii ina maana kuwa kwa wastani, serikali itaunda nafasi 706 kila siku ili kutimiza ahadi hiyo. Katika mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, serikali inalenga kuimarisha sekta za viwanda, afya, ujenzi na kilimo (chakula).

Kufikia mwishoni mwa 2018, utawala wa Jubilee unalenga kuongeza idadi ya wananchi wenye bima ya afya kutoka milioni 16.53 hadi milioni 25.74.

Serikali pia inapanga kujenga nyumba 500,000 itakazokodisha kwa bei nafuu katika miji mikuu kufiki 2022, mpango ambao inasema utaunda nafasi 350,000 za kazi.

Katika sekta ya ngozi, Rais Uhuru Kenyatta anadhamiria kufanikisha utengenezaji wa viatu milioni 20 nchini kufikia 2022, na kuongeza mapato kutokana na mauzo ya kigeni hadi Sh50 bilioni.

 

Mwelekeo wa hasara

Lakini tukirejelea matukio ya kisiasa humu nchini – kuanzia hatua ya kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga kulishwa kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’, hadi mbinu za utawala wa Jubilee za kuzima wazo la marais wawili, Mkenya ataelewa kuwa mwelekeo ambao taifa hili linafuata ni wa hasara kwa wananchi wote.

Katika hali ya sasa ya kisiasa, huenda tukawa na chaguzi mbili sambamba iwapo matatizo yaliyopo hayatasuluhishwa kufikia mwaka 2020.

Hii ndiyo taswira ambayo haifurahishi wengi, lakini ni ithibati kuwa tulicho nacho kwa sasa hapa Kenya, ni changamoto kuu za uongozi katika pande zote za kisiasa, ambazo ni mwiba katika ndoto ya Ajenda Nne Kuu.

Changamoto hizi zinaonekana wazi katika upande wa Rais Uhuru Kenyatta – ikilinganishwa na Bw Raila Odinga – kwa kuwa Rais ndiye nahodha halisi wa chombo hiki kuhusu usimamizi wa ujenzi wa taifa.

Lakini lazima kama Wakenya tutoe maoni yetu kuhusu suluhu ambazo zitaturejesha katika njia bora ya ukuaji wa demokrasia na uchumi.
Mwanzo, sote twafaa kukubali kuwa tuko chini ya katiba, na wala si juu yake.

Tukirejelea kipengee cha 10 cha katiba na mambo yanayoshikilia taifa letu la kidemokrasia, tutapa kuwa tunafaa kuwa na uzalendo, umoja, ugatuzi wa mamlaka, sheria, demokrasia na kuwashirikisha wananchi.

 

Ubinadamu wa taifa

Kuna yale mambo ambayo yanashikilia ubinadamu wa taifa kama heshima, usawa, haki za kijamii, ushirikishi, haki za kibinadamu, kutotenga wengine na kulinda matabaka ya chini.

Mengine kama maadili, uwazi na uwajibikaji yanaashiria utawala bora.

Utawala wa serikali unafaa kutambua kuwa amani hutokana na haki na si kinyume chake, na kwamba haki inahitaji usalama kwa mkono mmoja na haki zetu kwa mkono wa pili.

Pili, ni kuhusu kuimarisha uchumi wa nchi. Fikiria kuhusu utawala ambao unaangazia kupanua uchumi, maliasili, maarifa na utangamano baina ya jamii mbalimbali.

Kwa sasa, tunashuhudia watu wengi wenye ujuzi na maarifa lakini wamegawanyika katika misingi ya kisiasa. Hii haiwezi kusaidia katika utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu.

 

Ukosefu wa usawa

Tatu, kuna ukosefu wa usawa – matajiri dhidi ya walalahoi – ambao hutokana na kukiukwa kwa mambo manne – usawa wa jinsia, usawa wa maeneo, umri na kushirikishwa kwa jamii zote.

Fikiria kuhusu matatizo ya kila siku yanayowakumba Wakenya – gharama ya juu ya maisha, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa, utovu wa usalama.

Hizi ndizo changamoto ambazo Ajenda Nne Kuu za utawala wa Jubilee unafaa kuangazia kwa kina na kuleta sera mwafaka na mipango tekelezi kuzipunguza.

Kenya ikifuata haya hadi 2022, kwa yakini, haitapoteza dira na itapiga hatua kadha katika kuunda nafasi za ajira zipatao milioni 1.29.

 

TAHARIRI: Serikali ikome kuwabagua wanawake katika usajili KDF

Usajili wa vijana kwenye jeshi waendelea mjini Lamu Februari 12, 2018. Kati ya wanajeshi 2,000 watakaosajiliwa kote nchini, kutakuwa na wanawake kati ya 140 na 160. Wenzao wa kiume watakuwa kati ya 1,840 na 1,860. Picha/ Kalume Kazungu

Na MHARIRI

Kifupi:

 • Kati ya wanajeshi 2,000 , kutakuwa na wanawake kati ya 140 na 160. Wenzao wa kiume watakuwa kati ya 1,840 na 1,860
 • KDF yapaswa kueleza vigezo ilivyotumia kuwapatia wanawake asilimia nane pekee
 • Kuwasajili asilimia nane pekee, kutaendeleza dhana kuwa nafasi ya wanawake ni jikoni pekee

USALAMA wa nchi ni jambo ambalo halifai kufanyiwa mzaha. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiambiwa kwamba masuala ya usalama hayafai kuzungumzwa na wananchi, kwa kuwa hizo ni siri kuu ambazo maadui zetu hawafai kuzijua.

Lakini hakuna siri katika jambo hili tunalotaka kulizungumzia. Usajili wa makurutu watakaojiunga na vikosi vya jeshi letu (KDF) umefanywa kwa njia ambayo inaonekaa kukiuka mwongozo wa katiba kuhusu jinsia.

Alipokuwa akizindua usajili huo Jumatatu, Naibu Mkuu wa Majeshi Jenerali Joseph Kasaon alitangaza kwamba wanawake watakuwa kati ya asilimia saba na nane.

Kati ya wanajeshi 2,000 watakaosajiliwa kote nchini, kutakuwa na wanawake kati ya 140 na 160. Wenzao wa kiume watakuwa kati ya 1,840 na 1,860.

 

Masikitiko

Kinachohuzunisha zaidi ni kwamba KDF haikutangaza na mapema ni maeneo yapi ambako hawatarajii kusajili wanawake kujiunga na jeshi.

Kutokana na hilo, wanawake wamekuwa wakijitokeza katika viwanja mbalimbali kutaka kazi hiyo. Lakini kwa masikitiko makubwa, wamekuwa wakiambiwa kuwa hawahitajiwi.

Jambo hili linavunja mioyo Wakenya ambao wamejaaliwa kuwa na mabinti pekee. Wanaona kama walifanya makosa kuzaa watoto wa kike, ambao hawawezi kuitumikia nchi yao kwa kuilinda dhidi ya adui kutoka nje.

Jenerali Kasaon ana wajibu wa kuwaeleza Wakenya kuanzia leo, ni maeneo gani yaliyosalia ambako wanawake hawatasajiliwa. Kauli hiyo ikitangazwa hadharani, itasaidia watu kuokoa muda, nauli na nguvu zao kurauka asubuhi na mapema na kwenda katika viwanja vya usajili.

 

Thuluthi mbili

Pia tunajua kwamba kwa vile Katiba inasisitiza kusiwe na zaidi ya thuluthi mbili za jinsia moja, KDF yapaswa kueleza vigezo ilivyotumia kuwapatia wanawake asilimia nane pekee.

Jambo hili lafaa kuangaliwa kwa makini na haraka. Ikiwezekana, Mkuu wa Majeshi Jenerali Samson Mwathethe anapaswa kuingilia kati, ili idadi ya wawake katika jeshi letu angalau ifikie asilimia 15.

Tunajua kuna wanaoamini kuwa wanawake wengi wana mioyo ya huruma na hawawezi kwenda vitani. Lakini kuwasajili asilimia nane pekee, kutaendeleza dhana kuwa nafasi ya wanawake ni jikoni pekee.

Dhana hii ikiendelezwa, itarejesha nyuma hatua tulizopiga katika kuhamasisha wanawake kufanya kazi za jinsia ya kiume.

 

BI TAIFA VALENTINO DEI 2018

KAREN Kappuch anatupambia ukurasa wetu Valentino Dei ya mwaka huu. Yeye ni mwanamitindo jijini Nairobi na anaenzi kuimba, kusikiliza muziki, kusafiri na kutazama filamu. Picha/ Anthony Omuya

Wakerwa na mhubiri kuwataka waoe kanisani

Na DENNIS SINYO

MAGEMO, WEBUYE MASHARIKI

WAUMINI wa kanisa moja la eneo hili walitishia kugura kanisa hilo wakidai pasta wao alikataa watu kuoa kwa njia za mkato na kuwataka wafanye harusi.

Kwenye ibada Jumapili, pasta huyo aliwakashifu baadhi ya waumini aliodai walikuwa wakioa kwa njia za mkato. Mhubiri huyo alidai alikuwa amechoka kuitwa kuombea watoto kwenye familia ambazo hakujua wenyewe walivyooana.

Inasemekana aliwaonya waumini ambao hawajaoa kuhakikisha kwamba wanamfahamisha kabla ya kuoa. “Kuanzia leo hakuna mtu hapa atakubaliwa kuoa bila mhubiri kujulishwa. Tunataka tuwe na mpangilio maalum na sio watu kuiba wake za watu, kuwatesa wake na shida ikitokea pasta anaitwa kuingilia kati,” alionya mhubiri huyo.

Maneno hayo hayakuwafurahisha wengi wakisema kuoa ni mapenzi ya mtu na si lazima atangaze.

Jamaa mmoja alisikika akisema kwamba hakuwa na uwezo wa kufanya harusi na atafanya ndoa ya kitamaduni. Alimlaumu pasta kwa kuingilia maisha ya kibinafsi ya watu.

“Kama mtu hana hizo pesa za kufanya harusi, utamlazimisha na hawezi?’ ’aliuliza mama mmoja.

Pasta alisema kanisa lilikuwa likipata aibu kubwa washiriki wake wakioa na kufukuza wake zao jinsi wanavyotaka ilhali kanisa linawashauri waishi kwa amani.

“Sitakubali watu kuoana usiku na mchana wanaachana, ninataka mambo ya wazi watu waishi kwa amani,” alisema pasta huyo.

Inasemekana waumini waliamua kususia hafla za kanisa wakisema tayari pasta alikuwa amewadunisha.
Hata hivyo, waliokuwa wamepanga harusi walifurahia ushauri wa pasta wakisema mambo ya giza hayafai kuruhusiwa kanisani.

 

Kalonzo ajipata kwa njiapanda: Je, niapishwe? Niondoke NASA? Vipi 2022? Wakamba watanifuata?

Kinara wa NASA na kiongozi wa chama cha Wiper Bw Stephen Kalonzo Musyoka. Maswali manne kuhusu siasa yanamkosesha usingizi. Picha/ Maktaba

Na WYCLIFFE MUIA

Kwa Muhtasari:

 • Bw Musyoka amejipata kona mbaya ya kisiasa kutokana na shinikizo za kuapishwa
 • Wiper inaangazia zaidi kinyang’anyiro cha urais 2022, kitapuuza chochote kinachoweza kuzuia Bw Musyoka kuwania urais
 • Bw Musyoka atishia kujiondoa NASA iwapo baadhi ya viongozi wa NASA wataendelea kumtusi
 • Anakabiliwa na hatari ya kutengwa na baadhi ya wafuasi wa upinzani kwa ‘kuwasaliti’ kuhusu suala la kiapo
 • Huenda Mudavadi, Kalonzo na Wetang’ula wakaungana na kuanza kutafuta kura za Mlima Kenya

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka Jumanne alikiri kuwa suala la kula kiapo kama ‘naibu rais wa wananchi’ linamnyima usingizi huku akikiri kuwa hatua hiyo itakuwa kinyume cha sheria.

Makamu huyo wa zamani wa Rais amejipata kona mbaya ya kisiasa kutokana na shinikizo za kuapishwa kama ‘naibu rais wa wananchi’ huku washauri wake wakuu wakimuonya kuwa huenda hatua hiyo ikaathiri azma yake ya urais ifikapo 2022.

Wakili Kioko Kilukumi anasema iwapo Bw Musyoka atashtakiwa kwa kula kiapo na apatikane na hatia, huenda akazuiliwa kisheria kuwania urais, suala ambalo Wiper ingetaka kuzuia.

Akiongea na wanahabari Jumanne, Bw Musyoka alikanusha ripoti kuwa ataapishwa Februari 28 na kusisitiza kuwa anaendelea kushauriana kwa kina na vinara wenza wa upinzani kabla ya kutangaza msimamo wake kamili.

 

Anaangazia 2022

Mwenyekiti wa chama cha Wiper ambaye pia ni Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana alisema chama hicho kinaangazia zaidi kinyang’anyiro cha urais 2022, na kuwa kitapuuza chochote kinachoweza kuzuia Bw Musyoka kuwania urais wakati huo ukifika.

Tangu kinara wa NASA Raila Odinga aapishwe Januari 30, Bw Musyoka amekuwa akikejeliwa na baadhi ya viongozi na wafuasi wa upinzani kwa madai kuwa ni “mwoga” huku wengine wakitaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho achukue nafasi yake katika NASA.

Jumanne, Bw Musyoka alitishia kujiondoa NASA iwapo baadhi ya viongozi wa NASA wataendelea kumtusi kuhusiana na hatua yake ya kususia kiapo.

 

Kutumiwa na Jubilee

“Mimi na Raila ni kama pacha na sielewi kwa nini viongozi wachache ndani ya NASA wanatumiwa na Jubilee kuleta mgawanyiko. Nawaonya viongozi hao kuwa tuna uwezo wa kujiondoa katika muungano tuone watafanya nini,” alisema Bw Musyoka.

Alisema kuwa atakutana na vinara wenzake wa NASA: Bw Odinga (ODM), Musalia Mudavadi (Amani National Congress) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) ili kujadili kwa kina suala la kiapo chake.

“Raila mwenyewe na mimi Kalonzo tunajua vyema kuwa kiapo hiki ni kinyume cha Katiba. Huo ndio ukweli wa mambo. Iwapo tutakubaliana kuwa tutakula kiapo kinyume cha Katiba na tuelewane jinsi ya kukabiliana na athari zake ni sawa.

Mimi niko tayari wakati wowote kuapishwa,” alisema Bw Musyoka jana baada ya kufanya kikao na kundi la viongozi wanawake wa chama cha Wiper mjini Athi River.

 

Hatari ya kutengwa

Kwa upande mwingine, Bw Musyoka anakabiliwa na hatari ya kutengwa na baadhi ya wafuasi wa upinzani na kutemwa kwa ‘kuwasaliti’ kuhusu suala hilo la kiapo. Pia kuna suala la iwapo ngome yake ya Ukambani itamfuata akiamua kujiondoa NASA.

Jumamosi iliyopita, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama alitishia kumgonga Bw Musyoka na Biblia kichwani iwapo atasita kuapishwa.

Naye naibu kinara wa Wiper Farah Maalim aliweka wazi kuwa hakuna uwezekano wa Bw Musyoka kula kiapo kama ‘naibu rais wa wananchi’. “Sidhani kuwa Kalonzo ataapishwa. Ningefurahia sana iwapo Kalonzo angechukua msimamo imara na kusema, ‘samahani mimi ni wakili sitaki kufanya haya’,” alinukuliwa Bw Maalim.

Naibu Spika huyo wa zamani alidai kuwa Bw Odinga ndiye alishinikiza ulaji wa kiapo, uamuzi ambao ulipingwa na vinara wenzake watatu.

 

Mpasuko ndani ya NASA

“Tangu mwanzo Kalonzo, Wetang’ula na Mudavadai walipinga vikali kuapishwa. Sioni NASA ikidumu baada ya kiapo cha Raila. Natabiri kuwa Mudavadi, Kalonzo na Wetang’ula wataungana na kuanza kutafuta kura za Mlima Kenya. Siasa ndio zimeanza,” aliongeza Bw Maalim.

Madai ya Bw Maalim hata hivyo yalikanushwa na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr, akisema hayo ni maoni yake kibinafsi na wala sio ya chama cha Wiper.

Viongozi wa Wiper wamekuwa wakisisitiza kuwa wanajiandaa kuzindua mikakati ya kumtawaza Bw Musyoka kuwa mwaniaji wa urais 2022.

Prof Kibwana alisisitiza kuwa mkataba wa maelewano baina ya vigogo wa NASA ni sharti ufuatwe na Bw Odinga hafai kuwania tena urais 2022.

Gavana Kibwana alisema wakati umewadia kwa Bw Odinga kurudisha shukrani kwa kuunga mkono Bw Kalonzo katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

 

Githu Muigai ainua mikono, Kihara na Ogeto ndani

Mwanasheria Mkuu Profesa Githu Muigai aliyejiuzulu Februari 13, 2018 asalimiana na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi. Picha/ Maktaba

Na LUCY KILALO

Kwa Muhtasari:

 • Yasemekana amejiuzulu kutokana na ukinzani kati ya anachoamini na aliyotakiwa kufanya kisiasa
 • Huenda Prof Githu alishauriwa ajiuzulu ili ajiandae kuchukua nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP)
 • Akiwa ofisini kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria

JOTO kali katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu limeonekana kuwa sababu kuu ya Profesa Githu Muigai kuamua kujiondoa kwenye wadhifa huo Jumanne.

Wachanganuzi wanaona kuwa Prof Muigai, ambaye amekuwa mshauri mkuu wa serikali katika masuala ya kisheria chini ya Rais Uhuru Kenyatta, amefunganya virago vyake kutokana na ukinzani kati ya anachoamini kama mtaalamu anayeheshimika sana katika taaluma ya sheria na aliyotakiwa kufanya kisiasa.

Mara kadha amekuwa akitoa ushauri, ambao ulipingwa na Wakili Mkuu wa Serikali Bw Njee Muturi, aliyeteuliwa jana kuwa Naibu Mkuu wa Utumishi katika Ikulu chini ya Nzioka Waita.

“Nimepokea kwa masikitiko kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai. Ninamshukuru kwa huduma yake katika kipindi cha miaka sita na nusu iliyopita. Nimemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa Paul Kihara Kariuki, kuchukua nafasi yake,” Rais alitangaza kwenye Twitter.

 

Nafasi ya DPP

Wachanganuzi wengine wanasema huenda Prof Githu alishauriwa ajiuzulu ili ajiandae kuchukua nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), iliyoachwa wazi na Bw Keriako Tobiko ambaye aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mazingira.

Wanaomfahamu Prof Githu wanasema kama msomi wa masuala ya sheria amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza wanafunzi wake wafuate sheria kikamilifu.

Katika siku za majuzi akiwa ofisini kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria, ikiwemo kukamatwa kwa viongozi wa upinzani na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani katika muda unaotakiwa.

Vile vile, serikali imeonekana kudharau maagizo ya mahakama, la punde zaidi likiwa ni kuhusu mwanasiasa wa upinzani, Dkt Miguna Miguna.

 

Mabadiliko mengine

Kwenye mabadiliko mengine aliyotangaza Rais Kenyatta Jumanne, Bw Abdikadir Mohammed, ambaye amekuwa mshauri wake wa masuala ya sheria na kikatiba ametumwa kuwa balozi nchini Korea Kusini.

Wakili aliyemtetea Rais kwenye kesi ya uchaguzi, Kennedy Ogeto naye aliteuliwa Wakili Mkuu wa Serikali kuchukua nafasi ya Bw Muturi.

Rais pia aliwateua aliyekuwa Makamu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Prof Olive Mugenda, aliyekuwa Karani wa Bunge Patrick Gichohi na aliyekuwa waziri wa Kilimo Felix Koskei kuhudumu kama makamishna wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Watatu hao sasa watapigwa msasa na Bunge kabla ya kuchuka vyeo hivyo. Umma umepewa siku saba kutuma maoni au pingamizi kuhusiana na watatu hao.

Mnamo Jumatatu jioni, rais aliwateua Bw Charles Hinga Mwaura kuwa katibu wa Nyumba, Bw Kevit Desai (mafunzo ya kiufundi) na Bw Joseph Irungu (Maji na Usafi).

 

Taharuki yatanda kijijini mwanamume kuvamiwa na kuuawa kanisani

Na MAGDALENE WANJA

HOFU ilitanda katika kijiji cha Kimangu eneo la Rongai, kaunti ya Nakuru baada ya manamume mwenye umri wa miaka 75 kufariki baada ya kuvamiwa kanisani.

Bw Francis Imili alitoka nyumbani kwake na kuelekea kanisa la Sacred Heart Catholic Church Kimangu ambako amehudumu kama mwelekezi kwa zaidi ya miaka 20.

Ibada ilipokuwa ikiendelea, mwamume mwenye umri wa makamu aliingia kanisani huku akibeba fimbo na kumshambulia Bw Imili na kumgonga kichwani. Bi Peninah Wanjiru alisema kuwa alipogongwa kichwani na fimbo hiyo aliangukia kiti ambapo aliumiazaidi baada ya kugongwa usoni.

“Kabla ya kumkimbiza hospitalini, tulitumia vitambaa kufunga sehemu ya kichwa chake iliyokuwa ikivuja damu sana,” alisema Bi Wanjiru.

Hali ya Bw Imili iliendelea kuwa mbaya zaidi, alisema Bi Wanjiru, na wakalazimika kumpeleka katika hospitali ya Nakuru Level Five ambako alifariki akipokea matibabu.

Mkewe marehemu, Bi Tabitha Haluba, alisema kuwa mumewe alimuacha nyumbani kuelekea kanisani ila hakuandamana naye sababu alikuwa ametembelewa na wajukuu wake.

Bi Haluba alisema kuwa mumewe amemuacha na watoto 10 huku akiongeza kuwa baadhi yao bado wako katika shule ya upili.
Washirika wa kanisa hiyo, waliitaka serikali kuwapa ulinzi wanapohudhuria ibada

Uzani mdogo wafanya vijana kukataliwa jeshi

Shughuli ya vijana kusajiliwa kwenye kikosi cha jeshi la Kenya (KDF) kaunti ya Lamu ikiendelea Februari 12, 2018. Vijana wengi walitemwa kwa kukosa kufikisha uzani unaohitajika. Picha/ Kalume Kazungu

KALUME KAZUNGU na FADHILI  FREDRICK

MAKURUTU wengi waliojitokeza kutafuta nafasi ya kusajiliwa kwenye kikosi cha jeshi la Kenya (KDF) kaunti ya Lamu Jumanne walitemwa kutokana na kupungukiwa na uzani wa mwili uliohitajika.

Zaidi ya makurutu 30 hawakuweza kufikisha kilo 54.5 kwa upande wa wanaume na kilo 50.0 kwa upande wa wanawake kama ilivyohitajika.

Wengi wa makurutu waliojitokeza kwa shughuli hiyo iliyofanyika katika bustani ya Kibaki mjini Lamu walikuwa na uzani wa kati ya kilo 49 kwenda chini.

Afisa Msimamizi wa shughuli ya usajili wa makurutu kuingia jeshini katika kaunti ya Lamu, Luteni Kanali Zacharia Burudi, aliambia wanahabari kuwa idadi kubwa ya makurutu pia walitemwa nje kutokana na meno yaliyobadilishwa rangi kufuatia ulaji mwingi wa miraa.

Bw Burudi kadhalika alisema kiwango duni cha masomo hasa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne (KCSE) pia ni kizingiti kilichopelekea vijana wengi wa Lamu kukosa nafasi ya kusajiliwa kujiunga na KDF.

Aliwasihi wazazi na utawala wa kaunti ya Lamu kutoa hamasa kwa vijana wajiepusha na ulaji mwingi wa miraa unaoharibu meno yao.

Pia aliwahimiza wakazi wa Lamu kujikaza zaidi kimasomo ili wafaulu kuajiriwa serikalini, ikiwemo kupata nafasi za ajira jeshini.

 

Kilo 49

“Wanaume wanahitajika kuwa na kilo 54.5 ilhali wanawake wanastahili kuwa na kilo 50.0. Wengi wao tuliwatoa mapema kwani walikuwa na uzani wa kilo 49 kwenda chini” akasema Bw Burudi.

Katika kaunti ya Kwale, zaidi ya wanawake 30 walijitokeza eneobunge la Msambweni, lakini wakafahamishwa kuwa KDF ilitaka wanaume pekee.

Wanawake waliokuwa wamejitokeza kushiriki zoezi hilo lililofanyika katika Shule ya Msingi ya Jomo Kenyatta walikasirishwa na hatua hiyo na kusema kuwa sio mara ya kwanza kuondolewa kwa sababu ya jinsia.

“Mwaka 2017 walitoa udhuru kama huo. Je, inamaanisha hakuna nafasi zaidi kwa wanawake katika jeshi?” mwanamke mmoja aliuliza, akiongeza kuwa hii ni mara ya pili wanawake kuondolewa katika zoezi hilo.

 

Wakazi Kisii waandamana kukejeli matamshi ya Babu Owino dhidi ya Matiang’i

Wakazi waandamana mjini Kisii kukashifu matamshi yasiyo na heshima ya mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino dhidi ya waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i hapo Februari 13, 2018. Picha/ Benson Momanyi

Na JADSON GICHANA

WAKAZI wa Kisii, Jumanne waliandamana kulalamikia matamshi ya mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, dhidi ya Waziri wa Usalama Fred Matiang’i.

Walizunguka mitaa ya mji wa Kisii, huku wakiimba nyimbo za kumsifu waziri Matiang’i wakimshutumu kiongozi wa NASA na viongozi wengine katika muungano huo kwa kumkosoa na kumtusi waziri kwa kazi ambayo anafanya.

Walisema kuwa sio vyema kwa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga  kwa kumlaumu waziri huyo kwa kufanya kazi yake.

Walizungumza baada ya kukamilisha maandamano hayo wakiongozwa na Enock Mogeni ambaye aliambia upinzani wakome kufanya siasa kwa kila jambo waziri Matiangi anafanya.

Alieleza kuwa wakati huu ni wa serikali kufanya kazi ya kuleta maendeleo kwa wakenya wote.

“Tuko hapa leo kusimama kidete na waziri wetu Dkt Matiang’i kama ndugu yetu. Tumeamua kumuunga mkono afanye kazi yake kwa mujibu wa sheria bila kutishwa na yeyote,” akasema.

“Nimekasirishwa sana na baadhi ya viongozi na wafuasi wao kumtukana na kumkejeli Dkt Matiang’i kwa chochote anapofanya.

Ninawaomba mmpe wakati mwafaka afanyie wakenya kazi,” alisema Bw Mogeni.

 

Waislamu watakiwa kutumia kondomu

Mipira ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa na Ukimwi almaarufu kondomu. Picha/ Maktaba

Na WINNIE ATIENO

WAISLAMU nchini wametakiwa kutumia kinga aina ya kondomu ili kukabiliana na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, hata hivyo baadhi ya waumini hao wamepinga hatua hiyo.

Kwenye maadhimisho ya siku ya kondomu duniani Jumanne, katika eneo la Pwani, mamia ya vijana walipewa kondomu ili wajikinge dhidi ya maambukizi ya ukimwi hatua ambayo ilipingwa vikali na viongozi wa kidini mbalimbali.

Shirika la kimataifa la kukabiliana na Ukimwi maarufu kama Aids Healthcare Foundation (AHF), lilisambaza takriban kondomu 300,000 kuwafaa wakazi wa Mombasa na kuwapima watu 600 ili wajue hali zao.

Mwaka 2017, shirika hilo lilisambaza takriban kondomu 4, 800, 000 kando na kupima watu 526, 618 waliojua hali zao.

“Mombasa pekee shirika letu liliwapima watu 108, 026 na kusambaza kondomu 1, 377, 544. Kondomu inatumika kama kinga ya magonjwa ya zinaa,” akasema mkurugenzi wa  kuhamasisha umma katika shirika hilo Faith Ndungu.

Afisa mkuu wa uhamasisho na mauzo wa shirika hilo duniani Terri Ford alisema ufadhili wa kondomu unakumbwa na changamoto dhidi ya ufadhili.

 

Maadhimisho ya Siku ya Valentino yanoga

Na WAANDISHI WETU

Kwa Muhtasari:

 • Mwaka huu imeambatana na Jumatano ya majivu, na huenda waliozingatia dini wakakosa kuitilia mkazo
 • Wale wasiokuwa na wa kuandamana ama kusherekehea pamoja siku hii, wanaweza kujipa raha wenyewe!
 • Maeneo yanayovutia watu wengi ni ziwa la Nakuru, makavazi ya Lord Egerton Castle pamoja na hoteli mashuhuri
 • Wakenya wengi wana mpango wa kuwapeleka wapenzi katika hoteli moja mashuhuri

SHAMRASHAMRA za maadhimiso ya Siku ya Valentino inayotambuliwa kuwa ya wapendanao zimeonekana kunoga katika baadhi ya maeneo nchini.

Hata hivyo, siku hii mwaka huu imeambatana na Jumatano ya majivu, na huenda waliozingatia dini wakakosa kuitilia mkazo.

Japo huwafaa wenye kutarajia wapenzi, wake ama waume wao kuwakumbuka, kwa zawadi na njia nyingine, wasiokuwa na wa kuwatunza kwa njia hiyo huenda wakagubikwa na hofu na majonzi.

 

Jipe raha mwenyewe

Hata hivyo, utafiti wa Kisayansi uliotolewa majuzi, unaonyesha kuwa hata wale wasiokuwa na wa kuandamana ama kusherekehea pamoja siku hii, wanaweza kujipa raha wenyewe! Utafiti huo unaeleza kuwa kuna manufaa ya kuwa pekee yako tu.

Unasema kuwa watu hao wana uhusiano thabiti wa kijamii, wako salama kimwili na wanajikuza zaidi wakiwa pekee yao.

Katika kaunti ya Nakuru, sehemu za burudani zimejitayarisha kuwapokea wateja wanaofika kwa maadhimisho ya siku hiyo.

Baadhi ya maeneo yanayotarajiwa kuvutia watu wengi ni ziwa la Nakuru, makavazi ya Lord Egerton Castle pamoja na hoteli mashuhuri.
Makavazi ya ‘Lord Egerton Castle’ yaliyoko eneo la Ngata, Nakuru yana historia pevu katika somo la mapenzi, japo kwa kinaya.

 

Harusi

“Tumekuwa tukipokea wageni wengi haswa wanaofanya harusi, makundi ya vijana wanaokuja kujiburudisha na wapenzi wanaokuja kupunga unyunyu humu. Siku ya Valentino tunatarajia zaidi ya wageni 300,” akasema Emanuel Oduor, mfanyakazi katika makavazi hayo.

“Siku hiyo nina mpango wa kumpeleka mpenzi wangu katika hoteli moja mashuhuri kisha eneo la kujitazamia mazingira mwanana. Nimemnunulia zawadi kemkem,” Kennedy Kimani akaeleza.

Jijini Mombasa, shughuli ziliendelea kunoga huku wauzaji wa maua wakijiweka katika maeneo maalum ambako wanatarajia kupata wateja.

Katika barabara ya Nyerere, tulikutana na Mgeni Juma mwenye umri wa miaka 18 akiuza maua nje ya ukumbi huo.

 

Ripoti za LUCY KILALO, PETER MBURU na KAZUNGU SAMUEL

 

MAWAIDHA YA VALENTINE DEI: Uchu wa ngono si mapenzi kamwe!

Na BENSON MATHEKA

Kwa Muhtasari:

 • Kulingana na Kate, Rich alikuwa gwiji chumbani. Lakini tangu akutane na Deno mambo yamebadilika
 • Sio watu wengi wanaoweza kutofautisha mapenzi ya dhati, tamaa na uchu wa ngono japo wanadai kuwa katika mapenzi
 • Watu wengi hawajipatii muda kuwawezesha kuwa na hakika ikiwa hisia zao kwa wenzao ni za mapenzi ya dhati au uchu wa ngono
 • Mtu akiwa kwenye mapenzi ya dhati mwili hutoa homoni kama vile Oxytocin inayofahamika kuwa homoni ya mapenzi

FEBRUARI 14, 2018 ikiwa Siku ya Wapendanao Kate anafurahi kwamba ametambua maana ya mapenzi ya dhati. Kwa miaka minne kabla ya kukutana na Deno, Kate alikuwa kwenye uhusiano na Rich.

Wakati huo alidhani alikuwa akimpenda Rich sana. Walikuwa wakifanya mapenzi na kulingana naye, Rich alikuwa gwiji chumbani. Hata hivyo, tangu akutane na Deno mambo yamebadilika.

Kate anahisi tofauti sana. Anamfikiria Deno kila wakati na hawezi kumtoa katika mawazo yake. “Nafikiri ninampenda kwa dhati. Napenda kila kitu kumhusu japo hana mapato kama Rich,” asema Kate.

Kulingana na watalaam wa masuala ya mapenzi, sio watu wengi wanaoweza kutofautisha mapenzi ya dhati, tamaa na uchu japo wanadai kuwa katika mapenzi.

 

Ni uroda tu

Wanaonya watu kutoamini kwamba wanaowashehenezea sifa za mapenzi Siku ya Wapendanao wanawapenda kwa dhati wakisema wanachotaka wengi ni kula uroda tu.

“Kuna mambo matatu ambayo huwa vigumu kutofautisha. Kuna mapenzi ya dhati, kumtamani mtu kwa sababu ya kitu fulani unachotaka kutoka kwake na uchu ambao watu hudhani ni mapenzi ya dhati,” asema Darius Mnyala wa Shirika la Big Hearts jijini Nairobi.

Anasema mapenzi ni hisia zenye nguvu kutoka moyo wa mtu. Hisia zinazoteka mtu hadi anashindwa kujielewa. “Sawa na hisia zingine, hisia za mapenzi huwa tofauti kwa watu kwa kutegemea umri na aina ya uhusiano wao na pia mtu binafsi,” asema Bw Mnyala.

Anasema kuna tofauti ya kumpenda mtu na kufanya mapenzi na mtu. “Kupenda mtu ni tofauti na kufanya mapenzi na mtu. Kuwa na mapenzi na mtu ni hisia kali ya ndani kwa ndani ambayo haiwezi kuepukika mwanzo wa uhusiano.

Ukiwa kwenye mapenzi na mtu, unaona uzuri wake kila wakati. Hisia kama hizi huwa kali na nzito kiasi cha kusababisha maumivu hasa ikiwa mtu unayempenda hana hisia kama zako,” asema Bw Mnyala.

 

Mapenzi ya dhati 

Joyce Wariara, mshauri wa kituo cha Love Paradise anasema hisia za mapenzi ya dhati huwa zinajijenga kwa wakati na kisha kukita mizizi ndani ya mtu na kuanza kuchanua na kunawiri.

“Watu wengi hawajipatii muda kuwawezesha kuwa na hakika ikiwa hisia zao kwa wenzao ni za mapenzi ya dhati au uchu wa ngono. Wanapeana mili yao kwa kila mtu anayewashawishi kufanya mapenzi wakidhani wako katika mapenzi ya dhati. Uchu wa kufanya mapenzi si mapenzi ya dhati kamwe. Haya ni mambo tofauti,” aeleza Bi Wariara.

Kulingana na wataalamu, mapenzi ya dhati hujijenga kwa hatua japo si lazima hatua hizo ziwe kwa mpangilio maalumu.

“Kwa kawaida, mapenzi huanza kwa kuhisi mvuto, kisha ndoto na kulemewa na hisia za mapenzi kuhusu mtu fulani na hatimaye kushindwa kumtoa mtu huyo katika moyo wako. Hali kama hii inaweza kuwaunganisha watu wawili katika maisha yao yote,” asema Bw Mnyala.

 

Huoni ubaya

Ukiwa katika mapenzi ya dhati huwa unamfikiria mtu wako siku yote na kufurahia kila kitu anachofanya. Aidha unahisi kuwa na furaha na hauoni ubaya wa mtu wako.

Unamvumilia na kumsaidia katika kila hali tofauti na uchu ambao ni wa muda tu. “Ukitaka kujua umetekwa kimapenzi, huwa unapata hisia za ajabu ukimuona, hisia ambazo huwezi kuzieleza. Unatabasamu kila wakati ukimuona au kusikia sauti yake. Unataka kufanya kila kitu ili kumfurahisha,” asema Bi Wariara.

Hata hivyo, mtaalamu huyu asema kwa baadhi ya watu, ni vigumu kutofautisha mapenzi ya dhati na tamaa ya kimwili. “Unaweza kuongozwa na tamaa na hata kushiriki tendo la ndoa na kulifurahia lakini uwe haumpendi kamwe,” aeleza Bi Wariara.

 

Homoni ya Oxytocin

Wataalamu wanasema mtu akiwa kwenye mapenzi ya dhati mwili hutoa homoni kama vile Oxytocin inayofahamika kama homoni ya mapenzi.

“Ni homoni hii inayofanya mtu kuhisi tofauti akimuona, kumsikia, kumkosa au kuwa na mtu anayependa kwa dhati,” aeleza Bw Mnyala.

Anasema kuna tofauti ya kupenda mtu na kufanya mapenzi. “ Kushiriki tendo la ndoa kunafahamika kama kufanya mapenzi kwa sababu ni sehemu ya uhusiano wa kimapenzi.

Lakini mapenzi na tendo la ndoa ni tofauti sana, unaweza kuwa na moja bila nyingine. Watu wengi hushiriki tendo la ndoa na mtu wanayempenda lakini pia unaweza kula uroda kwa sababu ya uchu.

Hata hivyo wanaofurahia tendo la ndoa kwa dhati ni wanaoburudishana na mtu wanayempenda,” asema Bw Mnyala.

 

FATAKI: Si lazima kuzaa au kuolewa ndipo ukamilike kama mwanamke, usiishi kuridhisha waja

Na PAULINE ONGAJI

Kwa Muhtasari:

 • Maishani mwake hajawahi kuolewa ila alibahatika kukutana na dume la miaka 65 mtandaoni
 • Jamii imeweka viwango fulani kuhusu umri muafaka kwa mwanamke kuolewa
 • Ikiwa ndoto yako ni kusafiri duniani kote, basi usijinyime ili kuridhisha maoni ya watu

SIKU kadha zilizopita nilikuwa nikisafiri kuelekea nyumbani kutoka shughuli za kawaida katikati ya jiji la Nairobi.

Katika basi ambalo nilikuwa nimeabiri kulikuwa na mjadala uliokuwa unaendelea redioni ambapo watangazaji hao walikuwa wanazungumzia kuhusu binti ambaye alikuwa amepiga kueleza yanayomsibu.

“Nina miaka 52 na sijawahi olewa lakini nafurahi kutangaza kuwa nimebahatika kumpata mchumba ambaye napanga kufunga naye ndoa mwezi Julai,” alisema kwa furaha.

Kipusa huyo ambaye kulingana na sauti yake alionekana kuwa mrembo, maishani mwake hajawahi kuolewa ila alibahatika kukutana na kaka huyu mwenye umri wa miaka 65 kupitia mtandao wa kuunganisha wapenzi. Kwa mujibu wa binti huyu, mwanamume huyu alikuwa amejaribu ndoa mbili bila mafanikio.

“Miaka ilikuwa imepita kiasi cha kwamba watu walikuwa wananiambia kuwa hakuna matumaini ya kuolewa tena, lakini kwangu nilifahamu kuwa mwishowe ningepata mume,” alisema.

Ni hali ambayo utakubaliana nami kuwa imekuwa ikikumba mabinti wengi hasa wanapotimu umri fulani.

 

Umri wa kuolewa

Hii ni kwa sababu jamii imeweka viwango fulani kuhusu umri muafaka kwa mwanamke kuolewa. Kuna umri fulani maishani ambapo kama mwanamke unaanza kufanya watu kuingiwa na wasiwasi huku maswali ya lini utakapoolewa yakianza kuchipuka.

Wiki kadha zilizopita nilizungumzia taarifa fulani alizochapisha mtangazaji mmoja kuhusu jamii ilivyomkandamiza mwanamke huku ikiendelea kushusha thamani yake anavyozidi kuongeza umri tofauti na jinsi mwanamume husifiwa kwa uzuri wake anavyozidi kuzeeka.

Nakumbuka pia nikisisitiza kuwa huo ni upuuzi mtupu na ni uwongo ambao umeenezwa kwa muda mrefu kiasi cha kufanya wengi kuanza kuuamini.

Kuna binti fulani ambaye ni rafiki yangu kwenye mtandao wa Facebook ambaye siku kadha zilizopita alizungumza kuhusu jinsi amekuwa akipokea shinikizo kutoka kwa baadhi ya marafiki zake kupata mtoto huku wengi wakionekana kuhofia kwamba huenda akatalikiwa kabla ya kuafikia haya.

 

Ni lazima uzae?

Swali langu ni nani aliyesema kwamba ni lazima uzae ndio ukamilike kama mwanamke?

Nikidhani tuna muda mfupi sana ulimwenguni ambapo itakuwa muhimu kutumia wakati huo mchache kufanya jambo linalokufurahisha.

Ikiwa ndoto yako ni kuimarika katika taaluma na kusafiri duniani kote, basi usijinyime ili kuridhisha maoni ya watu. Na iwapo ndoto yako iko katika masuala ya mahusiano usiache kizingiti chochote hata iwe umri kikufungie njia.

Nakumbuka hadithi ya mwanamke wa miaka 92 kutoka Uganda ambaye hatimaye aliolewa baada ya kusubiri kwa miaka.

Kwa ufupi hakuna umri mkubwa zaidi unaomfungia mwanamke kuolewa. Ikiwa unahisi kuwa haujampata anayekufaa zaidi, zidi kutafuta bila haraka. Usiharakishe, kama wasemavyo wakati wa Mungu ndio mwafaka!

 

Utafiti: Wasiotafuna mlo vyema hatarini kunenepa kupindukia

Na MASHIRIKA

WATU wanaofakamia chakula bila kutafuna wako katika hatari ya kuwa wanene kupindukia, kulingana na matokeo ya utafiti uliotolewa Jumanne.

Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Kyushu na kuhusisha watu 60,000 nchini Japan, ulibaini kuwa watu wanaokula polepole na kutafuna chakula kwa muda mrefu wana nafasi finyu ya kuwa wanene kupindukia ikilinganishwa na wale wanaokula harakahara.

Watafiti walichunguza na kufuatilia kwa karibu tabia za watu walioshiriki utafiti huo kati ya 2008 na 2013

Idadi kubwa ya watu 4,192 wanaokula polepole na kutafuna chakula kwa muda mrefu, walipatikana na uzito wa chini.

Idadi kubwa ya watu walikula kwa kasi bila kutafuna walipatikana wakiwa na uzito kupindukia.

Watafiti walibaini kuwa watu wanene waliobadili tabia na kuanza kutafuna chakula kwa muda mrefu, ndani ya kipindi cha miaka sita, walipunguza uzito kwa kiasi kikubwa.

Watafiti pia waligundua kuwa watu wanaokula kila mara wako katika hatari ya kuwa wanene kupindukia.

 

Msemaji wa Machar kunyongwa kwa kujaribu kupindua serikali ya Sudan Kusini

MSEMAJI wa kiongozi wa waasi Riek Machar, Bw James Gatdet Dak azogwa na mawazo baada ya kuhukumiwa kunyongwa kwa kutekeleza uchochezi na kujaribu kupindua serikali ya Sudan Kusini. Picha/ Maktaba

Na MASHIRIKA

JUBA, SUDAN KUSINI

MSEMAJI wa kiongozi wa waasi Riek Machar, amehukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kutekeleza uchochezi na kujaribu kupindua serikali.

James Gatdet Dak alisafirishwa kwa nguvu na Kenya kwenda Sudan mnamo Novemba 2016, hatua iliyokosolewa na Umoja wa Mataifa (UN) na makundi ya kutetea haki za kibinadamu kuwa ilikiuka sheria za kimataifa.

Mahakama Kuu jijini Juba ilimhukumu Gatdet adhabu ya kifo pamoja na kifungo cha miaka 21 gerezani, Jumatatu, kwa kujaribu kupindua serikali ya Rais Salva Kiir.

Wakili wa Gatdet, Monyluak Alor Kuol alipinga hukumu hiyo huku akisema kuwa ilikiuka mkataba wa amani uliotiwa saini Desemba uliotaka wafungwa wote wanaozuiliwa kwa sababu za kisiasa kuachiliwa huru.

“Nimesikitika sana. Kesi za kisasa hazifai kufanyika kwa sasa,” akasema Kuol.

Gatdet alishtakiwa pamoja na William John Endley, raia wa Afrika Kusini, ambaye alikuwa mshauri wa Machar.

Kesi dhidi ya Endley inaendelea na mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi mwishoni mwa mwezi huu.

 

Kituo cha redio cha Kikristo chafungwa kudunisha wake

Na AFP

KIGALI, RWANDA

SERIKALI Jumatatu ilifunga kituo cha redio cha Kikristo kwa kupeperusha mahubiri ya kuwadunisha wanawake.

Kituo cha Amazing Grace FM, kinachomilikiwa na Amerika, kilifungwa kwa miezi mitatu baada ya mhubiri wake Nicolas Niyibikora kuwataja wanawake kama hatari, waovu na wavunjaji wa mipango ya Mungu mnamo Januari 29.

Mahubiri hayo yalishutumiwa na makundi mbalimbali ya wanaharakati. Chama cha Wanahabari Wanawake nchini Rwanda kiliripoti kituo hicho kwa Tume ya Kusimamia Vyombo vya habari.

Tume pia imemtaka mhubiri huyo kuomba msamaha kwa kutoa matamshi ya kuwadunisha wanawake katika mahubiri yake.

 

ANC sasa yamkabidhi Rais Zuma barua rasmi ya kumtaka ang’atuke mamlakani

Na AFP

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

Kwa Muhtasari:

 • Ikiwa Zuma, atapuuza wito wa kung’atuka mamlakani, atang’olewa kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni
 • Zuma ameomba muda wa miezi mitatu kung’atuka mamlakani
 • Ripoti tofauti zilidai Rais Zuma alimjibu Ramaphosa: “Nifanyie unachotaka lakini sibanduki”
 • Uchumi wa Afrika Kusini umedorora wakati wa utawala wake

CHAMA tawala cha African National Congress (ANC), sasa kimemkabidhi rasmi Rais Jacob Zuma barua ya kumtaka ajiuzulu. Uongozi wa ANC ulimtaka kung’atuka baada ya viongozi wa ngazi za juu kukutana Jumanne asubuhi.

Ikiwa Rais Zuma, 75, atapuuza wito wa chama cha ANC kung’atuka mamlakani, atang’olewa kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.

Viongozi na wabunge wa ANC wanatarajiwa kukutana leo katika majengo ya bunge ili kujadili hatua itakayochukuliwa dhidi ya Rais Zuma baada ya kukaidi agizo la kumtaka kung’atuka.

Rais Zuma ambaye amekuwa akiongoza Afrika Kusini tangu 2009 anakabiliwa na sakata mbalimbali za ufisadi.

Tangu naibu wake Cyril Ramaphosa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa ANC Desemba, mwaka jana, Rais Zuma amekuwa akishinikizwa kujiuzulu.

 

Barua

Katibu Mkuu wa ANC Ace Magashule Jumanne alimpelekea Rais Zuma barua ya kumtaka kujiuzulu katika Ikulu ya Rais jijini Pretoria.

Hata hivyo, jibu la Rais Zuma kwa Bw Magashule halikujilikana mara moja. Viongozi wa ANC Jumatatu walikutana kwa zaidi ya saa 13 ambapo waliafikiana Rais Zuma ang’atuke.

Katika mkutano huo wa Jumatatu, Rais Zuma na makamu wake Ramaphosa walijibizana kwa hasira hadharani.

Shirika la habari la serikali, SABC, liliripoti kuwa Bw Ramaphosa alimpa Rais Zuma muda wa saa 48 kujiuzulu.

Lakini wanachama wa ANC wanaounga mkono Rais Zuma wanasema kuwa kiongozi huyo hatajiuzulu kabla ya muhula wake kukamilika mwaka ujao.

Baadhi ya vyombo vya habari pia viliripoti kuwa Rais Zuma ameomba muda wa miezi mitatu kung’atuka mamlakani.

 

‘Sibanduki’

Ripoti tofauti zilidai Rais Zuma alimjibu Ramaphosa: “Nifanyie unachotaka lakini sibanduki”.

Msemaji wa Zuma jana alikataa kuzungumza na wanahabari huku mwanawe, Edward, akisema kuwa atazungumza baada ya chama cha ANC kutoa uamuzi wake wa mwisho.

Ijumaa, mmoja wa wake wa Zuma, Tobeka Madiba-Zuma, aliandika katika mtandao wa Instagram kuwa mumewe yuko tayari kupigana hadi mwisho badala ya kujiuzulu.

Bi Tobeka Madiba-Zuma hata alishutumu mataifa ya Magharibi kuwa kuunda njama ya kutaka kumng’oa mamlakani Rais Zuma.

“Atakamilisha miradi aliyoanzisha na hatakubali maagizo kutoka kwa mataifa ya kigeni,” akasema.

Uchumi wa Afrika Kusini umedorora wakati wa utawala wa Rais Zuma huku serikali yake ikikumbwa na sakata za ufisadi kila uchao.

Maandalizi ya Stars U-20 yakosa kung’oa nanga tena

Kiongozi wa makocha wanaohusika katika utafutaji wa vijana wanaojivunia utajiri wa vipaji kwa minajili ya kikosi hicho cha Rising Stars, Stanley Okumbi. Picha/Maktaba

Na CHRIS ADUNGO

Kwa Muhtasari:

 • Chipukizi hao walitarajiwa kuingia kambini katika uwanja wa kimataifa wa MISC Kasarani mnamo Februari 5, 2018
 • Okumbi amekuwa akitumia mashindano ya Chapa Dimba Na Safaricom kutambua makinda wenye uwezo 
 • Ziara ya kutafuta tiketi ya kuelekea nchini Niger mnamo 2019 kwa Kombe la AFCON inatarajiwa kuanza mapema Aprili 2018
 • Okumbi amesalia katika benchi la kiufundi la Harambee Stars licha ya kuvuliwa wadhifa wa kocha mkuu

TIMU ya taifa ya soka ya wanaume kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 (Under-20) ilikosa kuanza Jumanne , maandalizi yake kwa minajili ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kama ilivyopangwa awali.

Ni mara ya pili kwa maandalizi ya kikosi hicho kuchelewa kuanza licha ya ugumu na uzito wa kibarua kilichopo mbele ya vijana hao almaarufu Harambee Rising Stars.

Chipukizi hao walitarajiwa kuingia kambini katika uwanja wa kimataifa wa MISC Kasarani mnamo Februari 5, 2018 lakini shughuli za kuwasaka wachezaji wa kuunga na kukamilisha kikosi chenyewe hazikuwa zimekamilika.

Kiongozi wa makocha wanaohusika katika utafutaji wa vijana wanaojivunia utajiri wa vipaji kwa minajili ya kikosi hicho cha Rising Stars, Stanley Okumbi alisema Jumanne kwamba wako katika hatua za mwisho za kukamilisha kuunga orodha ya mwisho ya wachezaji watakaopeperusha bendera ya Kenya katika michuano hiyo.

 

Mkutano

Hata hivyo, Okumbi alisisitiza kwamba majina ya wachezaji na tarehe ya kuanza rasmi kwa mazoezi itatolewa na wadau husika baada ya kuandaliwa kwa mkutano muhimu mnamo Alhamisi.

Okumbi ambaye sasa ni kocha msaidizi wa Harambee Stars baada ya Mbelgiji Paul Put kurithi mikoba yake, amekuwa akitumia mashindano ya Chapa Dimba Na Safaricom kutambua makinda wenye uwezo wa kukitambisha kikosi cha Rising Stars katika kampeni hizo za kimataifa.

Isitoshe, alidokeza uwezekano wa kuzihemea pia huduma za chipukizi walio chini ya umri wa miaka 20 katika klabu mbalimbali za humu nchini.

Rising Stars imeratibiwa kuvaana na Tanzania katika mechi ya kirafiki mnamo Machi 3, 2018 jijini Dar es Salaam. Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) pia lilianika majuzi maazimio ya kuwajumuisha Rising Stars katika mashindano ya mataifa manne yatakayoandaliwa nchini Misri mapema mwezi Machi.

 

Aprili

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) bado halijafanya droo wala kutangaza tarehe rasmi za kupigwa kwa mechi za mchujo, lakini ziara ya kutafuta tiketi ya kuelekea nchini Niger mnamo 2019 kwa minajili ya Kombe la AFCON inatarajiwa kuanza mapema Aprili 2018.

“Tunanuia kutumia mchuano wa kupimana nguvu utakaotukutanisha na Tanzania ili kuwapa vijana uzoefu wa kutandaza soka hiyo katika kiwango cha kimataifa wakati wanapojiandaa kwa msururu wa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika,” akasema Afisa Mkuu wa FKF, Robert Muthomi kwa kukiri kwamba kipute cha Chapa Dimba Na Safaricom kiliwapa jukwaa mwafaka la kutambua vijana wenye uwezo mkubwa katika ulingo wa soka.

Kenya haijawahi kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 tangu 1981.

Katika juhudi za kuwania tiketi ya kushiriki mapambano hayo mnamo 2007, vijana wa nyumbani waliwakomoa Djibouti 1-0 katika awamu ya mchujo kabla ya kubanduliwa na Rwanda kwenye raundi ya kwanza baada ya kuzidiwa maarifa katika mechi za mikondo miwili iliyotandazwa jijini Nairobi na Kigali.

 

Kubanduliwa na Sudan, Lesotho na Misri 

Katika jaribio jingine mnamo 2009, Kenya walilambishwa sakafu na Sudan katika raundi ya kwanza licha ya kuwapepeta Somalia katika michuano ya michujo.

Miaka miwili baadaye, chipukizi hao waling’olewa na Lesotho waliowapokeza kichapo cha 1-0 katika mechi ya marudiano baada ya kusajili sare tasa katika kivumbi cha mkondo wa kwanza.

Awali mwaka huo, Stars walikuwa wamedumisha uhai wao wa kufuzu kwa fainali za 2011 baada ya wapinzani wao, Eritrea kujiondoa kisha kufanikiwa kuwatandika Sudan kwa jumla ya mabao 3-0 katika raundi ya kwanza.

Mnamo 2013, Kenya walidhalilishwa 3-0 na Misri ambao waliwabandua kwenye raundi ya kwanza ya michuano ya kufuzu kwa fainali za kipute hicho ambacho huandaliwa kila baada ya miaka miwili.

Okumbi alisalia katika benchi la kiufundi la Harambee Stars licha ya kuvuliwa wadhifa wa kocha mkuu na Mbelgiji Paul Put ambaye kwa sasa anahemewa na Guinea kupokezwa mikoba ya kikosi hicho cha taifa mwishoni mwa 2017.

Mabadiliko hayo katika kikosi cha Stars yalichochewa na matokeo duni yaliyosajiliwa na vijana wa taifa katika michuano miwili ya kirafiki dhidi ya Iraq na Thailand mwanzoni mwa Oktoba 2017 chini ya Okumbi ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Mathare United waliotawazwa wafalme wa KPL mnamo 2008 chini ya kocha wao wa sasa, Francis Kimanzi.

 

Droo ya KPL Top 8 sasa ni hadi Machi

Kocha Robert Matano baada ya kushinda kombe la KPL Top 8 mnamo 2013. Picha/ Maktaba

Na CHRIS ADUNGO

DROO ya kipute cha kuwania ubingwa wa taji la KPL Top8 mwaka imeahirishwa hadi mwezi Machi 2018. Kivumbi hicho kilikuwa kimepangiwa kuanza rasmi Februari baada ya waratibu kuthibitisha kurejea kwa mapambano hayo yanayokutanisha vikosi vilivyokamilisha kampeni za Ligi Kuu katika msimu uliopita ndani ya mduara wa nane-bora.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na KPL, michuano ya Top 8 kwa sasa imesogezwa kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kuwapa waratibu wakati maridhawa wa kukamilisha maandalizi muhimu.

Muhoroni Youth ambao waliteremshwa daraja kushiriki kampeni za Ligi ya Daraja la Kwanza msimu huu baada ya kukokota nanga mkiani mwa jedwali la KPL mwaka jana ndio mabingwa washikilizi wa taji la Top 8. Kikosi hicho kiliwabamiza Gor Mahia 1-0 kwenye fainali ya KPL Top 8 mnamo 2016.

Mnamo 2017, KPL ilifutilia mbali kivumbi hicho cha Top 8 katika kalenda yao ya mwaka huo. Kwa mujibu wa Jack Oguda ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL, kiini cha kutosakatwa kwa kivumbi hicho msimu huo ni hatua ya kujiondoa kwa waliokuwa wadhamini wakuu wa michuano hiyo, SuperSport .

 

Uhaba wa fedha

Kufutiliwa mbali kwa kipute hicho kwa pamoja na mashindano ya KPL kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 na 16 (KPL U-20 na U-16) kutokana na uchechefu wa fedha kulikuwa pigo kubwa kwa maendeleo ya soka ya humu nchini.

Licha ya kusisitizia kwamba vinara wa klabu za zitakazoshiriki kipute cha Top 8 msimu huu wameshauriwa kupunguza gharama za matumizi kwa minajili ya kivumbi hicho, waratibu wa mapambano hayo wameshikilia kuwa wamepania kutafuta wadhamini wa ziada watakaofadhili nyingi za shughuli zao.

Kipute cha KPL Top8 mwaka huu kitawashirikisha Gor Mahia, Sofapaka, Kariobangi Sharks na Posta Rangers, Kakamega Homeboyz, Tusker, Ulinzi Stars na AFC Leopards.

 

Runinga ya KTN kupeperusha gozi la Gor dhidi ya Zoo

Na CHRIS ADUNGO

Kwa Muhtasari:

 • Mechi hiyo itakayotandazwa uwanjani Kericho Green itakuwa ya kwanza ya Gor Mahia kuonyeshwa runingani
 • Gor watapania kutumia mchuano huo dhidi ya Zoo Kericho kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya KPL
 • Zoo Kericho ambao walidhalilishwa 4-2 na Ulinzi Stars ugani Afraha, Nakuru wanalenga kujinyanyua dhidi ya Gor Mahia

MCHUANO wa Ligi Kuu ya KPL unaotarajiwa kuwakutanisha kesho Zoo Kericho na Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo, utapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya KTN kwa ushirikiano na kampuni ya Mediapro kutoka Uhispania.

Mechi hiyo itakayotandazwa uwanjani Kericho Green kuanzia saa kumi alasiri Alhamisi itakuwa ya kwanza ya Gor Mahia kuonyeshwa runingani tangu kupulizwa kwa kipenga cha kwanza cha kuashiria mwanzo wa kampeni za Ligi Kuu msimu huu.

Awali, kipute hicho kilikuwa kimeratibiwa kusakatwa kuanzia saa tisa alasiri.

Gor Mahia ambao waliwakomoa Zoo Kericho 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa KPL msimu jana walilazimishiwa sare ya 1-1 na kikosi hicho katika mechi ya mwisho iliyowakutanisha uwanjani Kericho Green mwaka uliopita.

Chini ya kocha Dylan Kerr, Gor Mahia wanaingia katika mchuano wa Alhamisi wakijivunia hamasa ya kuwabamiza Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa mabao 2-0 katika kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) kilichowakutanisha mjini Machakos mwishoni mwa wiki iliyopita.

Aidha, wapambe hao wa soka ya humu nchini watapania kutumia mchuano huo dhidi ya Zoo Kericho kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya KPL baada ya kuanza vyema kampeni za msimu huu kwa kuwalaza Nakumatt 4-0 katika mechi yao ya kwanza iliyotandazwa mjini Machakos mnamo Februari 3, 2018.

      Pia waweza kupendezwa na habari hizi:

 

Nafasi ya 5

Alama tatu zilizovunwa na Gor Mahia katika mchuano huo kwa sasa zinawaweka katika nafasi ya tano kwenye jedwali linaloongozwa na mabingwa wa KPL 2008, Mathare United ambao waliwabamiza limbukeni Vihiga United 2-1 mnamo Februari 4 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Nzoia Sugar mwishoni mwa wiki jana uwanjani Kenyatta, Machakos.

Bandari, Chemelil Sugar na Kariobangi Sharks wanakamilisha orodha ya vikosi vinavyounga mduara wa nne-bora baada ya kujizolea jumla ya alama nne kila mmoja kutokana na michuano miwili ya ufunguzi wa kampeni za msimu huu.

Kwa upande wao, Zoo Kericho ambao walidhalilishwa 4-2 na mabingwa mara nne wa KPL, Ulinzi Stars katika mchuano uliowakutanisha ugani Afraha, Nakuru mnamo Februari 3 wanalenga kujinyanyua dhidi ya Gor Mahia ambao walijishughulisha vilivyo katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji kwa maazimio ya kutia fora katika kampeni za soka ya humu nchini na mechi za kimataifa za CAF.

Hadi kufikia sasa, Zoo Kericho wananing’inia padogo kwenye mkia wa jedwali la KPL na kwa pamoja na Nzoia Sugar ambao wamepoteza michuano yote miwili ya ufunguzi, ndivyo vikosi vya pekee ambavyo havina alama yoyote kapuni mwao hadi kufikia sasa.

 

Kileleni

Ushindi kwa Gor Mahia utawarejesha kileleni mwa jedwali kwa alama sita sawa na Mathare ila watawapiga kumbo vijana hao wa kocha Francis Kimanzi kutokana na wingi wa mabao.

Zoo Kericho nao watachupa hadi nafasi ya 10 jedwalini iwapo watawachapa Gor Mahia kwa zaidi ya mabao mawili bila jibu.

Bandari ambao walinyanyua ubingwa wa Ngao ya GOtv mnamo 2015 wanashikilia nafasi ya pili baada ya kuambulia pointi moja kutokana na sare tasa dhidi ya Chemelil Sugar.

Bandari wamezoa alama nne, mbili nyuma ya Mathare United. Chemelil na Kariobangi Sharks, ambao wameruka juu nafasi moja na tatu mtawalia, pia wamejizolea alama nne kila mmoja ila wanatofautiana kwa ubora wa magoli.

Sharks walidondosha alama mbili muhimu katika sare ya 2-2 dhidi ya Vihiga United mwishoni mwa wiki jana. Gor Mahia hawakupiga mechi yao ya pili ligini kutokana na majukumu ya kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Afrika.

Migongo ya masogora hao wa Kerr inasomwa kwa karibu na Ulinzi Stars ambao walishuka nafasi tatu baada ya kuchapwa 1-0 na SoNy Sugar waliotawazwa mabingwa wa KPL kwa mara ya mwisho mnamo 2006.

Ulinzi wanasalia na alama tatu walizozivuna kutokana na ushindi wao wa 4-2 dhidi ya Zoo Kericho.