MIGUNA MIGUNA: Ajipiga kifua kisha kukunja mkia na kusalia Canada

Na WYCLIFFE MUIA

MWANASIASA na wakili mbishi aliyefurushwa nchini, Dkt Miguna Miguna alikunja mkia kuhusu kurejea Kenya Jumatano licha ya kusisitiza awali kuwa angerejea nchini, ije mvua au jua.

Bw Miguna, ambaye amejitangaza kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) hakutoa sababu maalum ya kukatiza safari licha ya msimamo wake awali kuwa alikuwa amepanga safari yake kikamilifu na angewasili uwanja wa JKIA mwendo wa saa kumi alasiri Jumatano.

Kwenye ujumbe alioweka kwenye mitandao akitangaza kuahirisha safari yake, Bw Miguna alisema muungano wa NASA umekufa na ODM sio chama cha upinzani tena kwani kimejiunga na Jubilee, na kuwa sasa NRM ndicho chama kipya cha upinzani.

Pia aliwahimiza wafuasi wake kuendeleza uwazi hadi atakaporuhusiwa kurudi nchini.

Alisema Idara ya Uhamiaji imekataa kutii agizo la mahakama la kumpa uraia wa Kenya na kuwa mawakili wake walimshauri asubiri.

Mnamo Machi, wakili huyo ambaye pia ana uraia wa Canada alizua vionja uwanjani JKIA aliporudi Kenya lakini akakatazwa kuondoka uwanjani humo.

 

Sindano ya kumlemaza

Alizima juhudi za kumwondoa kwa kuzua sarakasi za kila aina lakini hatimaye alirudishwa Dubai kabla ya kuelekea Canada. Alidai alidungwa sindano ya kumlemaza aliporudishwa Canada.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwake kufukuzwa nchini mwaka huu, mara ya kwanza ikiwa ni alipofurushwa muda mfupi baada ya kumwapisha Raila Odiniga kama “rais wa wananchi” mnamo Februari 28.

Kwa hatua yake ya jana, Bw Miguna aliwavunja moyo baadhi ya wafuasi wake ambao walikuwa wamesisimka kumpokea tena nchini.

Kabla ya kutangaza kusitisha kurejea kwake jana, alikuwa ameapa kurudi nchini liwe liwalo, na kudai hatua ya Kenya kumnyima pasipoti ili atumie ya Canada ni mtego.

Mapema mwezi huu, wakili huyo aliapa kurejea nchini: “Narudi Kenya Mei 16. Mimi ni Mkenya kwa kuzaliwa. Sharti serikali itekeleze maagizo ya mahakama ya kunipatia pasipoti yangu bila masharti.”

 

Aombe uraia upya

Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji imesisitiza sharti wakili huyo ajaze fomu za kuomba uraia wa Kenya kabla ya kuomba pasipoti.

Mawakili wake pamoja na Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR), wamekuwa wakishinikiza serikali impe pasipoti ili arejee nchini.

“Kwa sababu Idara ya Uhamiaji imekataa kunipa pasipoti na kunirejesha nchini bila masharti kama ilivyoagizwa na korti, nimeagiza mawakili wangu waripoti kwa mahakama kuwa serikali imekaidi maamuzi yake,” alisema katika ujumbe wake Jumatano akiwa Canada.

Naibu mwenyekiti wa KNCHR George Morara alisema korti inasubiriwa kutoa mwelekeo kufikia Ijumaa hii.

Wiki iliyopita, Katibu wa Idara ya Uhamiaji, Gordon Kihalangwa alisema bado Bw Miguna si Mkenya hadi atume maombi ya uraia.

“Idara haitampa pasipoti Miguna kwa sababu hajatuma maombi. Lazima kwanza apate uraia wa Kenya kabla ya kupata pasipoti,” alisema Kihalangwa.

Masaibu ya Dkt Miguna yalianza baada ya kuongoza kuapishwa kwa kinara wa upinzani Raila Odinga kama ‘rais wa wananchi’ mnamo Januari 30.
Siku chache baada ya kiapo hicho, Miguna alikamatwa na kupelekwa Canada.

 

Sarakasi JKIA

Mnamo Aprili 29, wakili huyo alifurushwa hadi Dubai baada ya siku tatu za sarakasi katika uwanja wa ndege wa JKIA, Nairobi.

Baadaye alisafiri kutoka Dubai hadi Canada ambapo amekuwa akiishi.

Dkt Miguna amekuwa akimshtumu Bw Odinga kwa kumtelekeza baada ya kumuapisha.

“Muafaka wao wa kisiasa unapasha kurejesha uongozi wa kisheria na wala si kelele za refaranda,”alisema Miguna

Wakili huyo alikana madai kuwa anapanga kutumia ‘vichochoro’ kuingia nchini adai ni njia ya kutaka kumuua.

“Wale wanapendekeza nipitie katika mipaka ya Tanzania au Ugandan kisiri wametumwa na Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Wanataka kutumia maafisa wa usalama wa Uganda, Tanzania na Kenyan kuniteka nyara, waniue na wanizike katika makaburi fiche au wanitupe Ziwa Victoria.”

Kasisi akanusha kughushi hati kumiliki hospitali

Na RICHARD MUNGUTI

KASISI  kutoka Amerika anayezozania umiliki na usimamizi wa hospitali ya kimisheni ya St Marys Lang’ata  alishtakiwa Jumanne kwa ufisadi.

Kasisi William Charles Fryda wa kitengo cha Maryknoll Fathers & Brothers cha Marekani alikanusha mashtaka matatu ya ughushi, kujitengenezea hati na kufanya njama za kutekeleza ufisadi.

Kasisi Fryda alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

Kasisi huyo alishtakiwa kwa kughushi barua ya maafiisa waliokuwa wanaruhusiwa kutia saini katika akaunti ya hospitali hiyo ya St Marys kwenye benki ya  Prime (PB) miaka mitano iliyopita.

Alishtakiwa kutekeleza uhalifu huo mnamo Septemba 17, 2103 mahala pasipojulikana humu nchini.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000.

Maafisa wakuu wa Chase Bank washtakiwa kuiba mamilioni

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wakuu wa benki ya Chase Bank  (CB) iliyofilisika walishtakiwa Jumatano kwa kufanya njama za kuibia benki hiyo Sh577 milioni.

Aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Benki hiyo Mohammed Zafrulla na maafisa wengine wa CB  Mabw Duncan Kabui Gichu, James Mwaura Mwenja na Makarios Omondi Agumbi walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku.

Washukiwa hao walikabiliwa na shtaka lingine la usafishaji wa pesa.

Washtakiwa pia walidaiwa walikuwa wanajipa mikopo bila dhamana.

Yadaiwa walitekeleza uhalifu huo kati ya Septemba 2014 na Machi 31, 2015.

Zafrulla Khan , mkurugenzi wa benki hiyo alishtakiwa kuipa kampuni ya Emmar Properties mkopo wa $ 5,475,801.92 kutoka kwa benki ya CB bila idhini.

Waliotajwa kwa sakata ya NYS wajiuzulu wasitatize uchunguzi – Mbadi

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano ametakiwa kuwauliza maafisa waliotajwa katika kashfa ambapo Sh9 bilioni zilipotea katika Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS) wajiondoe kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi vile vile amewataka maafisa hao kujiuzulu kwa hiari kwa sababu huenda wakatatiza uchunguzi unaoendelea.

Waliotajwa katika sakata hiyo ni Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Lilian Mbogo, Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai na Waziri wa Afya Sicily Kariuki, ambaye aliongoza wizara hiyo mnamo 2016. Ni wakati huo ambapo pesa hizo zilidaiwa kupotea.

“Wito wangu wa kutaka maafisa hawa wakae kando kwa muda haumaanishi kuwa ni wenye hatia. Hofu yangu ni kwamba huenda wakatatiza uchunguzi unaendeshwa na asasi mbalimbali wakati huu,” Bw Mbadi akawaambia wanahabari afisini mwake katika majengo ya bunge.

“Maafisa hao wajiuzulu kwa hiari yao ama Rais Uhuru Kenyatta awalazimishe kukaa kando kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi,” akaongeza Bw Mbadi ambaye pia ni Mbunge wa Suba Kusini.

Kashfa hiyo imekuwa ikichunguzwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na wale wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Licha ya madai kuwa ni Sh9 bilioni zilipotea, Bi Mbogo alisema Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imekuwa ikipeleleza kupotea kwa Sh900 milioni wala sio Sh9 bilioni jinsi ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari, sakata hiyo ilipofichuliwa juma lililopita.

Alitoa madai hayo kwenye barua aliyomwandikia mkubwa wake Prof Kobia, siku mbili baada Rais Uhuru Kenyatta kumwita ili atoe ufafanuzi kuhusu sakata hiyo ambayo imeipaka tope wizara hiyo kwa mara nyingine.

Katika sakata hii, inadaiwa kuwa maafisa wa NYS walibuni kampuni bandia, na kughushi stakabadhi za zabuni na kutumia udhaifu wa Mfumo wa Ulipaji Fedha Kielektroniki, almaarufu IFMIS, kupora mabilioni ya pesa za umma.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) imewaita Bi Mbogo, Bw Ndubai na maafisa wengine wa wizara hiyo kuelezea jinsi pesa hizo zilivyopotea.

Maraga awataka majaji na mahakimu wazingatie maadili ili kukuza imani

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga Jumatano aliwataka majaji na mahakimu wote wawe na maadili mema ndipo wananchi wawe na imani katika idara ya korti.

Jaji Maraga aliyekuwa anaongoza sherehe ya kumteua Jaji Lydia Achode kuwa Jaji msimamizi wa Mahakama Kuu alisema jukumu kuu la “ maafisa wa idara ya mahakama ni kutekeleza haki pasi kusita.”

“Kile unatakiwa kufanya sasa ni kuimarisha utekelezaji wa huduma ndipo wananchi wa kawaida almaarufu ‘Wanjiku’ wafaidi na huduma za idara ya mahakama,” Jaji Maraga alimshauri Jaji Achode.

Jaji Achode alikuwa anatwaa usimamizi wa mahakama kuu kutoka kwa Jaji Richard Mwongo ambaye alihamishwa kutoka Nairobi.

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga awahutubia majaji na mahakimu jijini Nairobi Mei 16, 2018. Picha/ Richard Munguti

Jaji  Achode aliteuliwa mnamo Aprili 23, 2018 katika hafla iliyosimamiwa na maafisa kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Alizoa kura 43 kati ya kura 80 zilizopigwa.

Jaji Achode aliwashinda  wenzake Majaji Mary Kasango na Jaji Asenath Ongeri.

Jaji Achode ambaye ni jaji mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa msimamizi wa majaji wa mahakama kuu aliajiriwa katika idara ya mahakama kama hakimu.

Alihudumu akiwa hakimu mkazi wa kiwango cha pili (DM2) katika Mahakama ya Kericho mwaka wa 1986.

Jaji Achode ahutubu baada la kulishw akiapo Mei 16, 2018. Picha/ Richard Munguti

Alipandishwa vyeo hadi alipoteuliwa Jaji mwaka wa 2011 na kupelekwa Mombasa.

Kabla ya kuteuliwa Jaji alikuwa anahudumu kwa wadhifa wa Msajili  mkuu wa idara ya mahakama na katibu wa tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama.

Mbali na kusimamia majaji wengine na kuhakikisha kuna uangavu katika idara hiyo pia atakuwa mwanachama wa kamati ya kumsahuru Jaji Mkuu (CJ) David Maraga (JLAC).

“Nitahakikisha kuwa sijawakandamiza majaji wenzangu kwa kuwataka mfanye kile mimi siwezi kufanya. Hata mimi ni jaji kama ninyi,” alisema Jaji Achode katika hotuba yake.

Pasta akana kuvamia shamba Kariobangi

Pasta John Karanja Wanjengu akiwa kizimbani Mei 15, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MUHUBIRI wa kanisa la  Kenya Assemblies of God (KAG) alishtakiwa Jumanne kwa kuvamia shamba la wenyewe.

Pasta John Karanja Wanjengu mwenye umri wa miaka 56 alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Alikanusha shtaka dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Pasta Wanjengu alishtakiwa kwa kuvamia ploti nambari 150 mnamo Julai 31, 2006.

Mshtakiwa alikana alivamia shamba hilo akiwa na nia ya kuvuruga amani ya Bw Simon Kuria Wanyoike.

Upande wa mashtaka ulidai Pasta Wanjengu alipania kutwaa umiliki wa ploti hiyo.

Hakimu alimwachilia kwa dhamana ya Sh100,000.

Kesi itasikizwa Juni 18, 2018.

Jaji Ouko awataka wenzake kujiepusha na ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI

Rais wa Mahakama ya Rufaa Jaji William Ouko Jumanne aliwahimiza majaji watumie uhuru waliopewa katiba kwa manufaa ya umma.

Jaji Ouko aliwataka majaji wote wawe wakizingatia haki za umma wanapotekeleza majukumu yao.

Jaji Lydia Achode alipoapishwa kuwa Jaji msimamizi wa Mahakama Kuu Mei 15, 2018. Picha/ Richard Munguti

Akizugumza wakati wa kuteuliwa kwa Jaji Lydia Achode kuwa Jaji msimamizi wa Mahakama kuu, Jaji Ouko alisema Rais Uhuru Kenyatta aliitaka idara ya mahakama ishiriki katika utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Serikali ambazo ni Afya, Uzalishaji wa vyakula vya kutosha , utengenezaji bidhaa viwandani na makao bora.

Jaji huyo aliwahimiza majaji na mahakimu wachukulie kazi zao kwa uzito na kujiepusha na visa vya ufisadi.

“Kama vile Rais Kenyatta alisema  nawahimiza majaji na mahakimu msikilize na kuamua kesi za ufisadi kwa wakati unaofaa ndipo matajiri na mabwanyenye wasichukulie maagizo ya korti kwa mzaha,” alisema Jaji Ouko.

Washukiwa wengine 3 wakodolea macho kifo

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA saba wanaoshtakiwa kwa kumtwanga na kumpora kimabavu mfanyabiashara Timothy Muriuki  Sh100,000 wanakondolea macho adhabu ya kifo wakipatikana na hatia.

Wanashtakiwa chini ya kifungu cha sheria nambari 296 (2) za uhalifu na adhabu yake huwa ni  kifo ama hakimu akiwaonea huruma awafunge kifungo cha maisha.

Kufikishwa mahakamani kwa Mabw Benjamin Peter Mulinge, Bernard Onyango Otieno na Michael Banya Wathigo kumefikisha saba idadi ya washukiwa walioshtakiwa kwa shambulizi hilo miongoni mwao Bw Muriuki akiwamo Mbunge anayewakilisha Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Simon Mbugua.

Watatu hao walikanusha mbele ya hakimu mkuu Bw Francis Andayi kuwa walimnyang’anya Bw Muriuki Sh100,000 na kumwumiza wakati wa kisa hicho.

Mnamo Jumanne mshukiwa wa nne Bw Brian Shem Owino alishtakiwa kwa kumnyany’anya mfanyabiashara huyo.

Kutoka kushoto: Michael Mbanya Wathigo, Ronald Onyango Otieno na Dishon Peter Mulinge wakiwa kortini Milimani Mei 16, 2018 kwa kumshambulia mfanyabiashara Timothy Muriuki. Picha/ Richard Munguti

Wote walioshtakiwa ni Mabw Mbugua, Mulinge, Otieno, Wathigo, Owino, Antony Otieno Ombok  almaarufu Jamal na Benjamim Odiambo Onyango almaarufu Odhis.

Mshukiwa mwingine wa nane Bw Sangira Stephen Ochola anaendelea kuchunguzwa na polisi ibainike ikiwa alihusika na kisa hicho.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kuwa “ hapingi Mabw Mulinge,Otieno na Wathigo wakiachiliwa kwa dhamana.”

Alimsihi hakimu awaachilie washukiwa hao kwa masharti ya dhamana kama ya washukiwa walioshtakiwa awali.

“Washukiwa waliofikishwa kortini awali waliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000. Naomba korti iwaachilie washukiwa hawa kwa masharti sawa na hayo,” Bw Naulikha alisema.

Wakili Danstan Omari anayewakilisha washtakiwa hao watatu aliomba korti aamuru akabidhiwe nakala za mashahidi.

Bw Andayi aliwaachilia kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu kila mmoja na kuamuru kesi zote zitajwe Mei 23 ndipo ziunganishwe ziwe kesi moja,

Katika kesi dhidi ya Bw Ochola hakimu alimtaka mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji awasilishe ushahidi kuhusu madai yanayotolewa kortini badala ya kuacha korti “ itegemee uvumi.”

Korti iliorodhesha kesi kusikizwa Julai 17.

Deya aachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA  Kuu jumanne ilimwachilia Askofu Gilbert Deya kwa dhamana ya Sh10 milioni.

Jaji Luka Kimaru alisema ijapokuwa kuna tashwishi Deya atachana mbuga, ameona heri amwachilie kwa vile upande wa mashtaka ulishindwa kukamilisha kesi katika muda wa siku 90.

“Mshtakiwa huyu anashukiwa atatoroka lakini upande wa mashtaka haukukamilisha kesi dhidi yake katika muda wa siku 90 kama ilivyoamriwa na mahakama kuu miezi mitano iliyopita,” alisema  Jaji Kimaru.

Jaji alisema atamwekea masharti makali Askofu Deya anayekabiliwa na mashtaka ya kuiba watoto.

Mahakama ilisema Askofu Deya yuko na tabia ya kuikejeli mahakama na  pia kujaribu kutoroka.

Mnamo Desemba 2017 hakimu mkuu Francis Andayi alikuwa ameamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh1 milioni.

Askofu ameshtakiwa kwa wizi wa watoto wadogo.

Mhasibu akana kuiba mamilioni ya mwajiri

Na RICHARD MUNGUTI

MHASIBU mmoja alishtakiwa Jumanne kwa wizi wa Sh8.6milioni.

Bw Stanley Mwangangi Mukinya alishtakiwea kwa kosa la kuiba pesa hizo kutoka kwa mwajiri wake Xylon Motors.

Bw Mukinya alikana aliiba pesa hizo kati ya Novemba 2, 2016 na Septemba 14, 2017.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha kuwa kesi dhidi ya Mukinya itaunganishwa na nyingine dhidi ya Nancy Waithera Mwangi itakayotajwa Mei 23.

“Naomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana sawa na ile ya Bi Mwangi ya Sh300,000 pesa taslimu,” alisema Bw Naulikha.

Hakimu mkuu Francis Andayi alimwachilia mhasibu huyo.

Idara ya magereza yaagizwa imtengee nafasi mshukiwa mwenye kilo 150

Na RICHARD MUNGUTI

IDARA ya Magereza ilitakiwa Jumanne iweke mipango ya malazi kwa mshukiwa mmoja wa ufisadi kutokana na uzani wake mkubwa wa kilo zaidi ya 150.

“Natahadharisha idara ya magereza ihakikishe kuwa James Mutua Nzuni amepewa makao mema kutokana na uzani wake,” hakimu mkuu Francis Andayi alisema Jumanne.

Bw Nzuni (pichani) alisindikizwa hadi mahakamani kwa mwendo wa kinyonga na afisa wa polisi .

“Hebu keti hapa,” Bw Nzuni alionyeshwa kiti na afisa wa polisi.

“Asante,” alisema huku akichukua muda mrefu kufikia kiti na kuketi.

Bw Nzuni mmwenye umri wa miaka 53 alikabiliwa na shtaka kupokea pesa Sh945,000  kwa njia ya udanganyifu akidai ataangalia kesi zilizokuwa zimekwama katika mahakama kuu,.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka kisha akaomba aachiliwe kwa dhamana. Upande wa mashtaka haukupinga.

Alikana alipokea pesa hizo akijifanya angelichunguzia kampuni ya Ashut Engineering kesi zake katika mahakama kuu.

Alichiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh300,000 hadi Mei 23 kesi itakapotajwa.

Mwanafunzi ashtuka kuambiwa adhabu ya kuiba simu ni kifo

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa shule ya upili mwenye umri wa miaka 18 alishtakiwa Jumanne kwa wizi wa mabavu ambao adhabu yake ni kifo akipatikana na hatia ama kifungo cha maisha gerezani.

Punde tu alipofahamishwa adhabu ya kesi inayomsubiri alishtuka na kuomba mahakama imsaidie.

Grophat Wanjala Muruli (pichani) aliyemsihi hakimu amsaidie kusaka wakili wa kumtetea kwa vile adhabu inayomkondolea macho ni kali alisema “sikujua nitafunguliwa mashtaka makali jinsi hii. Ikiwa nitanyongwa basi nahitaji kusaidiwa.”

Awali hakimu mkuu Francis Andayi alimwuliza mwanafunzi huyo “mbona unajiingiza kwa uhalifu wa kiwango cha juu jinsi hii. Unajua kwamba adhabu ya mashtaka yanayokubali ni kunyongwa ama kutumikia kifungo cha maisha?”

“Hebu nikuulize ni kitu gani kiliendelea kabla ya wewe kushikwa,” Bw Andari alimwuliza mshtakiwa.

“Nilikuwa naendesha kibao chenye magurudumu nilipovamiwa na washambulizi walionipiga na kuninyang’anya simu pamoja na ile nilikuwa nimechukua,” alijibu Wanjala.

“Mbona walikupiga? Ulipigwa kwa sababu ulimnyang’anya kwa nguvu Josiah Mwangi Wango simu yenye thamani ya Sh18,000. Kumbe wakati mnafanya skating na wenzako huwa mnachunguza mtakaowapora.

Basi siku zako 40 amhazo mwizi huiba kabla ya kukamatwa zilitimia ulipokamatwa,” alisema Andayi akiongeza , “Si huu ni ule ujinga tu vijana mnajiingiza katika uhalifu pasi kufungua macho?”

Hata hivyo Bw Andayi alimweleza bodi ya masuala ya sheria la mahakama itamsaidia kupata wakili wa kumtetea kwa “vile adhabu yake ni kifo akipatikana na hatia.”

Hata hivyo mshtakiwa alikubaliwa kuwasilisha ombi la dhamana baada ya afisa wa urekebishaji tabia kumhoji yeye pamoja na familia yao.

Kesi itatajwa Mei 23. Alikana  alimnyang’anya kimabavu Bw Wangu simu ya rununu mnamo Mei 13, 2018. Itasikizwa Julai 3, 2017.

Polisi wageukia Safaricom kupata taarifa kumshtaki mwanahabari

Na RICJARD MUNGUTI

POLISI hawajakamilisha kuchunguza kesi dhidi ya mwanahabari anayeshukiwa alihusika na shambulizi la mfanyabiashara Bw Timothy Muriuki katika hoteli moja jijini Nairobi mwezi uliopita, hakimu mkazi katika mahakama ya Nairobi Bi Miriam Mugure aliambiwa Jumanne.

Kiongozi wa mashtaka Bi Anne Pertet alisema polisi hawakukamilisha uchunguzi wa kesi dhidi ya Bw Sangira Stephen Ochola kwa vile hawakuwa na nambari yake ya simu.

“Polisi walitaka kuitisha orodha ya simu ambazo Bw Ochola alipiga kabla na baada ya kisa hicho. Hawakufanya chochote lakini sasa wameipata watapeleka ombi kwa Safaricom wapewe sajili ya simu alizopiga mshukiwa huyu,” alisema Bi Pertet.

Aliomba kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili ndipo ripoti iwasilishwe ikiwa mshukiwa huyo atafunguliwa shtaka la wizi wa mabavu.

Bi Mugure aliamuru kesi dhidi Bw Ochola litajwe mnamo Juni 4, 2018.

Alipofikishwa kortini wiki iliyopita wakili Cliff Ombeta alipinga mwanahabari huyu akizuiliwa kwa muda wa siku saba kuwezesha polisi kumhoji na kutambuliwa na mlalamishi ambaye aliporwa Sh100,000 na waliomshambulia.

Akiwasilisha ombi la kumzuilia Bw Ochola ,  Koplo Francis Mwita alisema polisi wanachunguza kosa la wizi wa mabavu.

Lakini Mawakili  Ombeta, Nelson Havi , Michael Osundwa , Rodger Sagana  na Harun Ndubi walimweleza hakimu polisi wanataka kumtesa mshukiwa kwa vile walikuwa wamemshtaki Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Simon Mbugua na washukiwa wengine wawili kwa wizi wa mabavu.

Mshukiwa wa nne wa wizi wa mabavu afikishwa kizimbani

Na RICHARD MUNGUTI

SIKU arobaini zilitimia pale mshukiwa  wa nne aliposhtakiwa Jumanne  kwa kumshambulia na kumnyang’anya kimabavu mfanyabiashara Sh100,000 katika hoteli moja jijini Nairobi Aprili 30, 2018.

Bw Brian Shem Owino alifikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi. Alikanusha alimnyang’anya kimabavu Timothy Muriuki Sh100,000 katika hoteli ya Boulevard.

Shtaka lilisema wakati wa wizi huo mlalamishi alijeruhiwa.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kuwa kesi dhidi ya Bw Owino iunganishwa na nyingine dhidi ya Mbunge anayewakilisha Kenya katika bunge Afrika Mashariki (EALA) Simon Mbugua aliye na Mabw Antony Otieno  Ombok almaarufu Jamal na Benjamim Odhiambo Onyango almaarufu Odhis walifikishwa kortini baada ya patashika kadhaa kati ya polisi na washikadau wa haki waliotaka haki ifanywe na waliomshambulia Bw Timothy Muriuki wachukuliwe hatua kali.

Polisi waliwatia nguvuni watatu hao Mei 8 na kuwafungulia mashtaka.

Brian Shem Owino akiwa katika Mahakama ya Milimani. Picha/ Richard Munguti

Kisa hiki  cha kushambuliwa kwa Bw Muriuki kilipeperushwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Washtakiwa waliomba waachiliwe kwa dhamana kupitia kwa mawakili Cliff Ombeta, Harun Ndubi,  Nelson Havi na Michael Osundwa.

Ijapokuwa ombi hilo lao halikupingwa na kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha , hakimu mwandamizi Martha Mutuku aliombwa awaachulie kwa masharti makali ikitiliwa maanani Bw Mbugua yuko na ushawishi mkubwa na atavuruga mashahidi.

Lakini Bi Mutuku aliwaachilia kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu akisema “hakuna ushahidi uliowasilishwa kuonyesha kwamba washtakiwa wako na uhusiano na mashahidi.”

Korti ilisema mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji anatakiwa kuwasilisha ushahidi kuhusu madai yanayotolewa kortini badala ya kuacha korti “ itegemee uvumi.”

Korti iliorodhesha kesi hiyo kusikizwa Julai 17.

Hakimu aliamuru kila mmoja wa washukiwa hao apewe nakala za mashahidi aandae utetezi wake.

Maafisa 4 ndani miaka 3 kwa wizi na kutumia afisi kujinufaisha

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Serikali za Wilaya, Sammy Kirui pamoja na maafisa wengine watatu wakuu wa baraza la jiji NCC Jumanne walisukumwa jela miaka mitatu na kupigwa faini ya Sh86 milioni.

Bw Kirui, aliyekuwa katibu mkuu wa NCC John Gakuo, katibu wa masuala ya sheria Mary Ng’ethe na mwanakamati wa kamati ya zabuni Alexander Musee wanajiunga na orodha ya waliokuwa maafisa wakuu wa serikali kusukumwa jela makatibu Sylvester Mwalikho na Rebecca Nabutola waliofungwa kwa ufisadi.

Wanne hao walipatikana na hatia ya kujihusisha na utowekaji wa Sh283milioni katika kashfa ya kununua ardhi ya kuwazika wafu katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos miaka 10 iliyopita.

Mbali na kifungo hicho cha jela wanne waliofungwa walitozwa faini kati ya Sh1milioni hadi Sh52milioni.

Hakimu Douglas Ogoti aliyewapata na hatia Mabw Kirui, Bw Gakuo, Bi Mary Ng’ethe na mwanakamati Bw Alexander Museee alisema “upande wa mashtaka umethibitisha wanne hao walitumia vibaya mamlaka ya afisi zao na kupelekea Serikali kupoteza zaidi Sh283milioni.”

Bw Ogoti aliwatoza Mabw Kirui na Gakuo faini ya Sh1milioni kila mmoja pamoja na kifungo cha miaka mitatu.

Naye Bi Ng’ethe alitozwa faini ya Sh52milioni ilhali Bw Musee alitozwa faini ya Sh32milioni.

Akipitisha hukumu aliyosoma zaidi ya masaa mawili , Bw Ogoti alisema washtakiwa walikaidi mwongozo wa ununuzi wa mali ya umma na kuidhinisha ardhi hiyo inunuliwe katika eneo ambalo halikufaa kwa makaburi.

Ardhi hiyo ilinunuliwa kati ya Desemba 2008 na Aprili 2009.

“Mabw Kirui na Gakuo walikaidi ushauri wa wataalamu wa masuala ya ununuzi wa ardhi waliosema ardhi hiyo haikufaa kwa kuwazika wafu lakini wakaamuru ununuzi uendelee,” alisema Bw Ogoti.

Mahakama ilisema washtakiwa wanne hao walipuuza sheria na mwongozo uliowekwa na kuruhusu mamilioni ya pesa za umma zitumiwe kwa njia isiyofaa.

Bw Kirui alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Serikali za Wilaya ilhali Bw Gakuo alikuwa Katibu mkuu wa baraza la jiji la Nairobi wakati wizi huo ulitekelezwa.

“Maafisa hawa walikuwa na uwezo wa kuzuia pesa hizi kutotoweka lakini walitumia vibaya mamlaka yao,” alisema Bw Ogoti.

Mahakama ilisema kuwa mashahidi waliofika kortini walieleza jinsi walikuwa wanakopeshwa pesa hadi kiwango Sh18milioni na baadhi ya washtakiwa.

“Pesa hizi zilipopelekwa City Hall ziligawanwa na maafisa wakuu waliokaidi ushauri kuwa ardhi hiyo haikufaa kwa kuwazika wafu kwa vile ilikuwa na mawe mengi,” alisema Bw Ogoti.

Ardhi hiyo ilikuwa itumike na baraza la jiji la Nairobi kuwapeleka maiti kuwazika katika kaunti ya Machakos.

Wanne hawa walikuwa miongoni mwa washtakiwa 15 walioshtakiwa kwa kashfa hiyo ya makaburi.

Wengine waliofikishwa kortini ni pamoja na aliyekuwa Meya Geoffrey Majiwa (aliyeachiliwa kwa kukosekana ushahidi) , Mabw Maina Chege, Naen Rech Limited, Newton Osiemo, Wakili Alphonce Mutinda, Nelson Otido, Joseph Kojwando, Alexander Musee, Daniel Nguku, Herman Chavera, William Mayaka na mawakili Paul Chapia Onduso na Davies Odero.

 

Maafisa wengine wa serikali waliofungwa awali kwa ufisadi ni waliokuwa makatibu Sylvester Mwaliko miaka mitatu kwa kashfa ya Anglo-Leasing na Bi Rebecca Nabutola.

Sikuiba moyo wa mfu, mpasuaji ajitetea

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mpasuaji mkuu wa maiti wa Serikali Dkt Moses Njue alifikishwa kortini Jumanne kwa kuiba moyo wa maiti katika Mochari ya Lee , Nairobi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Hali aliwasilisha mashtaka matatu dhidi ya Dkt Njue ya kuiba moyo wa mfu kwa lengo la kulemaza kesi iliyonuiwa kushtakiwa.

Daktari huyo wa kupasua maiti alifunguliwa mashtaka pamoja na mwanawe Dkt Lemuel Anasha Mureithi Njue ambaye hakufika kortini Jumanne alasiri.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka matatu ya kuiba moyo, kuharibu ushahidi na kuondoa kiungo katika maiti na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu.

Alishtakiwa kuiba moyo kutoka kwa maiti ya Timothy Mwandi Muumba iliyokuwa imehifadhiwa katika chumba cha Lee.

Na wakati huo huo hakimu mkuu Mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi alitoa kibali cha kumwagiza Dkt Lemuel Anasha Mureithi Njue afike kortini kabla ya siku kusikizwa kwa kesi hiyo mnamo Julai 3, 2018 kujibu mashtaka hayo matatu.

“Namwamuru mshtakiwa wa pili (Lemuel) afike kortini aitha Mei 28 ama kabla ya Julai 3, 2018 kujibu mashtaka,” aliamuru Bw Andayi.

Juhudi za Dkt Njue kupitia kwa mawakili wake kupinga asishtakiwe ziligonga mwamba baada ya Bw Andayi  kutupilia mbali ombi la kutaka kesi hiyo iahirishwe hadi Mahakama kuu itakaposikiza na kuamua ombi  lililowasilishwa na jamaa wa marehemu.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili wa Serikali Bi Cathertine Mwaniki aliyesema kuwa kesi iliyowasilishwa mwaka wa 2016  ilipania kushinikiza afisi ya DPP ichunguze kisa hicho.

“Uchunguzi ulifanywa na kitengo kinachotokana na mizozo ya kinyumbani katika afisi ya Mkurugenzi wa Jinai (DCI). Ilibainika baada ya uchunguzi kwamba moyo wa  Timothy Mwandi Muumbo kama inavyosemekana katika cheti cha mashtaka,” alisema Bi Mwaniki.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mshtakiwa alitiwa nguvuni baada ya polisi kufahamishwa maiti ya Timothy haikuwa na moyo.

Katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama kuu walalamishi waliwashtaki Dkt Njue, Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na mwanasheria mkuu  Jaji Paul Kihara ndio wanaoshtakiwa.

“Mashahidi wakiongozwa na Bw Billy Mbuvi wameandika taarifa kutoka kwa mashahidi wote itakayotegemewa na DPP,” alisema Bi Mwaniki.

Kiongozi huyo wa mashtaka alipinga ombi la mshtakiwa akisema walioorodheshwa kutoa ushahidi dhidi yake wameandikisha taarifa kwa polisi.

“Naomba hii korti ikatalie mbali ombi la mshtakiwa na kuamuru ajibu mashtaka,” alisema  Bi Mwaniki.

Hakimu alikubaliana na Bi Mwaniki kwamba hakuna sababu zozote za kuwezesha mahakama kusitisha kushtakiwa kwa Dkt Njue.

Gor itapigana kufa kupona dhidi ya USM Alger – Shakava

Na JOHN ASHIHUNDU

Nahodha wa Gor Mahia, Harun Shakava amesema kuwa anatarajia mechi ngumu dhidi ya USM Alger, Jumatano.

Gor watakabiliana na klabu hiyo ya Algeria ugani Kasarani katika pambano la marudiano la CAF Confederations Cup katika Kundi D.

Kulingana na nyota huyo wa zamani wa klabu ya Kakamega Homeboyz alisema wenyeji wako katika hali nzuri baada ya kucheza mechi kadhaa mfululizo.

“Tumecheza mechi kadhaa ambazo zimetupa ujuzi wa kutosha kukabiliana na upinzani wowote ule…tutakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wetu, na tutapigania ushindi kwa vyovyote vile,” Shakava aliongeza.

Mabingwa hao wa ligi kuu nchini walionyesha kiwango cha juu katika mechi ya kupimana nguvu dhidi ya Hull City, Jumapili kabla ya kushindwa 4-3 kupitia kwa mikwaju ya penalti, zilizoagana 0-0.

Migne aita wengine wanne kuimarisha kikosi cha Stars

Na JOHN ASHIHUNDU

Kocha wa Harambee Stars, Sebastian Migne amewaita kikosini wachezaji wanne wapya.

Nyota hao waliotwa kujiunga na timu hiyo ya Harambee Stars ni Whyvonne Isuza, Jafari Odenyi na Robinson Kamura wote kutoka AFC Leopards na Robert Arot wa Nakuru All Stars.

Kulingana na orodha hiyo, AFC Leopards na Kariobangi Sharks ndizo zilizo na idadi kubwa katika timu hiyo.

Wachezaji walioitwa ni Makipa: John Oyemba (Kariobangi Sharks), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars), Patrick Matasi (Posta Rangers).

Walinzi: Yusuf Mainge (AFC Leopards), Bolton Omwenga (Kariobangi Sharks), David Owino (Mathare United), Dennis Shikhayi (AFC Leopards), Michael Kibwage (AFC Leopards), Jockins Atudo (Posta Rangers), Johnstone Omurwa (Mathare United), Geoffrey Shiveka (Kariobangi Sharks), Moses Mudavadi (St Anthony Kitale), Robinson Kamura (AFC Leopards), Musa Mohamed (asiye na klabu), Eric Ouma (KF Tirana, Albania).

Viungo: Chrispin Oduor (Mathare United), Vincent Wasambo (Kariobangi Sharks), Cliff Nyakeya (Mathare United), Robert Arot (Nakuru All-Stars), Patillah Omotto (Kariobangi Sharks), Duncan Otieno (AFC Leopards), Marvin Omondi (AFC Leopards), Whyvonne Isuza (AFC Leopards) na Jafari Odenyi (AFC Leopards).

Washambuliaji: Elvis Rupia (Nzoia Sugar), Pistone Mutamba (Wazito FC) na Ovella Ochieng (Kariobangi Sharks).

Ingwe yawinda mshambuliaji wa Nzoia Sugar

Na JOHN ASHIHUNDU

KLABU ya AFC Leopards inapanga kuvamia ngome ya Nzoia Sugar kumnasa mshambuliaji matata, Elvis Rupia. Ripoti zimesema shughuli hiyo itafanyika mwezi ujao.

Nyota huyo maarufu kama Machapo, amekuwa muhimu katika kikosi hicho cha kocha Bernard Mwalala ambapo kufikia sasa amefunga mabao 11.

Mbali na Leopards, straika huyo vile vile amevutia timu nyingi zikiwemo za ligi kuu nchini Zambia.

Ingwe vile vile imevutiwa na kiwango cha Pistone Mutamba wa Wazito FC.

Rupia alikuwa mshambuliaji wa Nakuru All Stars kabla ya kuagana nayo iliposhuka ngazi miaka miwili iliyopita.

Madaktari wa Cuba kutua nchini Mei 28 kuhudumia wagonjwa mashinani

Na CECIL ODONGO

WIZARA ya Afya Jumatatu ilitia saini makubaliano kati yake na Baraza la Magavana kuhusu ushirikiano wa kiafya na kuweka mpango mahususi kuhusu jinsi madaktari 100 wataalam kutoka nchi ya Cuba watakavyohudumu hapa nchini.

Waziri wa Afya Sicily Kariuki alisema Madaktari hao ambao watahudumu kwa kandarasi ya miaka miwili, wanatarajiwa kutua hapa nchini tarehe 28 mwezi huu na kupelekwa kaunti mbalimbali ili waanze kutoa huduma katika hospitali mbalimbali.

Bi Kariuki alisisitiza kwamba kwa kuwa sekta ya afya iligatuliwa hawakuwa na jingine ila kuwashirikisha baraza la magavana katika mpango huo na kuongeza kwamba serikali kuu imehakikisha madaktari wote 100 wanaumilisi wa lugha ya Kiingereza ili kurahisisha mawasiliano kati yao na wenzao nchini.

Kulingana na waziri huyo madaktari 50 kutoka hapa nchini pia wanatarajiwa kusafiri hadi Taifa la Cuba kwa mafunzo spesheli ya kitaaluma katika mpango maalum wa kubadilishana ujuzi kati ya Kenya na Cuba mwezi Septemba mwaka huu.

“Bodi yetu imewakagua madaktari wote 100 kutoka Cuba na tumethibitisha wanauelewaji mpana wa lugha ya Kiingereza. Pia madaktari wetu 50 watasafiri hadi India kwa mafunzo ya kipekee ya ubadilishanaji wa ujuzi wa kitaaluma baadaye Septemba,” akasema Bi Kariuki.

Madaktari hao wanatarajiwa kutoa huduma spesheli na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafiri kutoka mbali kupata huduma spesheli za kiafya katika hospitali ya Kenyatta na ile ya rufaa ya Moi.

Hata hivyo hatua ya madaktari hao kuajiriwa kwa kandarasi hapa nchini imezua pingamizi kubwa kutoka kwa viongozi wa Chama cha cha Madaktari nchini(KMPDU) ambao wamesisitiza kwamba serikali kwanza ingewapa ajira madaktari 1200 wa hapa kabla haijawaleta wengine kutoka Cuba.

Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt Ouma Oluga amekuwa katika mstari wa mbele kupinga hatua hiyo ya serikali akisema Kenya ina madaktari wataalam wa kutosha ila tu serikali haiwathamini na haitaki kuwapa kazi.

Majuzi Dkt Oluga alilalamika kwamba serikali imeonyesha kutowajali madaktari nchini kwa kujishughulisha na kuwaleta wa nje na kufumbia macho mgomo unaoendelea wa wahadhiri ambao madaktari wanachama wa KMPDU wanashiriki.

Sina tamaa ya hela, asema bondia Benson Gicharu baada ya kustaaafu

Na GEOFFREY ANENE

HATIMAYE bondia Benson Gicharu ameangika glavu zake.

Afisa huyu wa polisi aliongeza kwamba hana mipango ya kujitosa katika ndondi za malipo jinsi wanamasumbwi wengi hufanya baada ya kuwakilisha mataifa yao.

“Nahisi wakati wangu wa kustaafu umewadia. Ni wakati mzuri mimi kupisha mabondia chipukizi ili pia waweze kuendeleza taaluma zao na kuwakilisha nchi,” alieleza Mei 14, 2018.

Gicharu, ambaye alizaliwa Mei 3 mwaka 1985, amekuwa katika taaluma hii kwa karibu miaka 20.

Katika kipindi hicho, amepeperusha bendera ya Kenya katika mashindano mbalimbali ya Bara Afrika, Jumuiya ya Madola na Olimpiki, miongoni mwa mengine.

Nyota yake ilianza kung’aa mwaka 2010 alipojishindia medali ya fedha katika michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Delhi nchini India. Alimlima Dexter Jordon kwa alama 8-0 katika robo-fainali ya uzani wa kilo 51 na kumlemea Oteng Oteng kutoka Botswana kwa alama 5-4 katika nusu-fainali kabla ya kupoteza dhidi ya Suranjoy Mayengbam kutoka India katika fainali.

Alivuna medali ya shaba katika uzani wa kilo 56 kwenye michezo ya Jumuiya Madola mjini Glasgow, Scotland mwaka 2014. Aliwazidi maarifa Sikiru Ojo (Nigeria) na Tafari Ebanks (Cayman) kwa alama 3-0 katika raundi ya 16-bora na robo-fainali, mtawalia, kabla ya kunyamazishwa na Muingereza Qais Ashfaq 3-0 katika nusu-fainali.

Gicharu alishiriki Olimpiki mwaka 2012 jijini London nchini Uingereza na 2016 jijini Rio de Janeiro nchini Brazil. Alibanduliwa nje katika hatua ya raundi ya 32-bora katika makala hayo mawili.

Afrika Kusini wajiondoa kwa kipute cha raga ya wanawake Botswana

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kuaibishwa mara mbili na Lionesses ya Kenya, miamba Afrika Kusini sasa wamejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Afrika cha raga ya wachezaji saba kila upande ya wanawake itakayoandaliwa nchini Botswana hapo Mei 26-27, 2018.

Lionesses, ambayo ilizaba Afrika Kusini 24-12 Aprili 5 katika mechi za Kundi X za kufuzu kushiriki Raga ya Dunia msimu 2018-2019 mjini Hong Kong na kuishinda tena 19-10 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia mnamo Aprili 14, sasa imeorodheshwa nambari moja katika orodha ya washiriki wataokuwa jijini Gaborone.

Kujiondoa kwa Afrika Kusini, ambayo ilipepeta Lionesses katika fainali za Kombe la Afrika mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017, kunawapa warembo wa kocha Kevin Wambua nafasi nzuri ya kushinda taji.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kuwazia kushinda taji, Lionesses lazima ipate matokeo mazuri katika Kundi A dhidi ya wapinzani wake Madagascar na Senegal. Kenya ilibwaga Madagascar 27-5 na Senegal 38-0 zilipokutana mara ya mwisho katika Kombe la Afrika nchini Tunisia mwezi Septemba mwaka 2017.

Kundi B linaleta pamoja mabingwa wa mwaka 2012 Tunisia pamoja na Uganda na Zimbabwe nao Morocco, Botswana, Mauritius na Zambia wako katika Kundi C.

Hatua kwa hatua, Simbas wajinyanyua viwango vya raga

Na GEOFFREY ANENE

KWA wiki ya pili mfululizo, Kenya imeimarika katika viwango bora vya raga ya wachezaji 15 kila upande duniani bila kuteremka uwanjani.

Katika viwango vipya ambavyo Shirikisho la Raga duniani (World Rugby) imetangaza Jumatatu, Simbas, timu ya Kenya inavyofahamika kwa jina la utani, imeruka juu nafasi moja hadi nambari 29.

Vijana wa kocha Ian Snook waliimarika kutoka nafasi ya 31 hadi 30 hapo Mei 7 baada ya Chile kulazwa 28-12 na Brazil katika Kombe la Amerika Kusini mnamo Mei 5. Wameimarika tena kutokana na Korea Kusini kupepetwa 30-21 na Hong Kong katika Kombe la Bara Asia hapo Mei 12.

Simbas haijacheza mechi ya kimataifa tangu ziara yake ya Hong Kong mwezi Novemba mwaka 2017. Itafungua mwaka 2018 dhidi ya majirani na mahasimu wa jadi Uganda katika Kombe la Elgon hapo Mei 26 jijini Kampala. Vijana wa Snook wanatarajiwa kuingia kambini Mei 18 katika eneo la Nanyuki.

New Zealand, Jamhuri ya Ireland, Uingereza, Australia, Scotland, Afrika Kusini, Wales, Ufaransa, Argentina na Fiji zinashikilia katika nafasi 10 za kwanza duniani, mtawalia. Zimesalia katika nafasi hizo.

Mabingwa wa Afrika, Namibia wamesalia katika nafasi ya 24 duniani. Namibia inashikilia nafasi ya kwanza Afrika baada ya Afrika Kusini, ambayo haishiriki Kombe la Dhahabu la Afrika (Gold Cup).

Kenya inafuata Namibia katika viwango bora vya Afrika, huku Uganda ikisalia katika nafasi ya 34 duniani na nambari tatu Afrika. Morocco imetupwa chini nafasi moja hadi nambari 40 duniani baada ya Paraguay kuzima Colombia 28-26 katika Kombe la Amerika Kusini.

Tunisia imenufaika na Colombia kupoteza. Imepaa nafasi moja hadi nambari 42 duniani. Zimbabwe inasalia katika nafasi ya 44 duniani. Namibia, Kenya, Uganda, Morocco, Tunisia na Zimbabwe zitawania ubingwa wa Kombe la Dhahabu la Afrika mwaka 2018 ambalo litatumika kuchagua mwakilishi wa Afrika katika Kombe la Dunia mwaka 2019.

Ratiba ya Simbas mwaka 2018:

Mei 26 – Uganda vs. Kenya (Elgon Cup, Kampala)

Juni 23 – Morocco vs. Kenya (Africa Gold Cup, Casablanca)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (Africa Gold Cup, Nairobi)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (Africa Gold Cup, Nairobi)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (Africa Gold Cup, Nairobi)

Agosti 18 – Namibia vs. Kenya (Africa Gold Cup, Windhoek)

Kikosi cha Simbas: Patrick Ouko (Homeboyz), Oscar Simiyu (KCB), Moses Amusala (KCB), Joseph Odero (Kabras), Nelson Nyandat (KCB), Curtis Lilako (KCB), Peter Karia, (KCB), Phillip Ikambilli, (Homeboyz), Coleman Were (Kabras), Oliver Mangeni (KCB),Malcolm Onsando (Quins),Eric Kerre (Impala),Wilson Kopondo, (Quins),Andrew Chogo (Kabras),George Nyambua (Kabras), Dalmus Chituyi (Homeboyz), Peter Misango (Quins), Elkeans Musonye (Strathmore), Martin Owila (KCB), Davis Chenge (KCB),  Samson Onsomu (Impala), Xavier Kipng’etich (Impala), Mohammed Omollo (Homeboyz),Isaac Adimo (Quins), Biko Adema (Nondies), Leo Seje (Impala), Maxwell Kangeri (Homeboyz), Peter Kilonzo (KCB), Zedden Marrow (Homeboyz), Tony Onyango (Homeboyz),Felix Ayange (Kabras), Jacob Ojee (KCB), Darwin Mukidza (KCB), Edmund Anya (Strathmore),Vincent Mose (Impala).

USM Alger yatua nchini kukabiliana na Gor Confederations Cup

Na GEOFFREY ANENE

VIONGOZI wa Kundi D, USM Alger wametua jijini Nairobi tayari kupambana na Gor Mahia katika mechi ya Kombe la Mashirikisho (Confederations Cup).

Alger, ambayo ilifungua mechi za makundi kwa kupepeta Young Africans (Yanga) kutoka Tanzania 4-0 Mei 6, ilitoka nchini Algeria saa tisa alasiri Jumapili na kupumzika jijini Doha nchini Qatar kwa saa mbili na nusu kabla ya kuendelea na safari hadi Nairobi.

Mabingwa hawa mara saba wa Algeria watavaana na mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor, Jumatano saa moja usiku katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Klabu hizi hazijawahi kukutana katika historia yao. Alger, ambayo ilifika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2017 na fainali ya kombe hilo mwaka 2015, inatarajiwa kuwa na vipindi viwili vya mazoeziuwanjani Kasarani kabla ya kumenyana na Gor.

Timu hizi zilijiandaa kwa mchuano huu kwa kupoteza mechi zao. Alger ilizabwa 3-2 na JS Kabylie hapo Mei 11 katika mechi ya Ligi Kuu ya Algeria nayo Gor ikalemewa na Hull City kutoka Uingereza 4-3 kwa njia ya penalti katika mechi ya kirafiki uwanjani Kasarani mnamo Mei 13.

Alger inaongoza Kundi D kwa alama tatu ikifuatiwa kwa karibu na Gor na Rayon Sport ya Rwanda (alama moja kila mmoja) nayo Yanga inavuta mkia bila alama.

Kaunti yaanza kuchunguza ardhi zilizotolewa kwa umma kiharamu

Na VALENTINE OBARA 

SERIKALI ya Kaunti ya Kisumu imeanzisha uchunguzi kuhusu ardhi za umma zilizotolewa kwa wawekezaji kupitia njia haramu.

Jopokazi lililobuniwa na Gavana wa kaunti hiyo, Prof Anyang’ Nyong’o, litahitajika kuchunguza jinsi ardhi za umma zilivyonyakuliwa na watu binafsi tangu enzi za utawala wa mabaraza ya miji yaliyosimamiwa na mameya na kutoa mapendekezo kuhusu hatua inayostahili kuchukuliwa.

“Watahitajika kutoa ripoti ambayo itaongoza Serikali ya Kaunti ya Kisumu kwa ushirikiano na Tume ya Kitaifa ya Ardhi kutwaa ardhi za umma ambazo zilitolewa kinyume na sheria, nyumba za serikali, vyeti vya kukodisha ardhi za umma na mitaa iliyo Kaunti ya Kisumu,” ikasema taarifa ya kaunti iliyochapishwa katika baadhi ya magazeti jana.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza jopokazi kama hilo kubuniwa kwani kumewahi kuwepo mengine katika miaka iliyotangulia, ingawa hakujapatikana mafanikio kutatua unyakuzi wa ardhi uliotendeka kufikia sasa.

Kutokana na hali hii, serikali ya kaunti ilisema jopokazi lililochaguliwa litahitajika pia kutathmini ripoti zilizotolewa awali kuhusu unyakuzi wa ardhi na kutoa mapendekezo kuzihusu.

Serikali hiyo ilitoa agizo kuzuia uuzaji wa ardhi zinazolengwa kufanyiwa uchunguzi kuanzia sasa hadi wakati uchunguzi utakapokamilika. Agizo hili linahusu pia ardhi zilizopeanwa kwa watu binafsi na baraza la mji wa Kisumu lililokuwepo katika mwaka wa 2010.

Baadhi ya ardhi ambazo zilinyakuliwa kutoka kwa umma ziko mjini Maseno, mitaa ya Kanyakwar, Kibos, Migosi, Mamboleo na Dunga.

Wananchi walitakiwa kuwasilisha maoni au malalamishi kuhusu ardhi za umma zilizonyakuliwa kwa jopokazi hilo kuanzia Mei 14 hadi Juni 8, mwaka huu kibinafsi au kupitia kwa makundi.

Malalamishi yote yatahitajika kuambatishwa na stakabadhi husika.

Onyo kwa waundaji wa filamu bila leseni

Na LEONARD ONYANGO

BODI ya Kutathmini Ubora wa Filamu nchini (KFCB) imetishia kuwashtaki watengenezaji wa filamu wanaohudumu bila vibali, huku ikitoa makataa ya siku 14 kwao kujitokeza kuchukua leseni.

Mkurugenzi Mkuu wa KFCB Ezekiel Mutua Jumatatu alisema bodi hiyo itaanzisha msako wa kuwanasa watengenezaji wa flamu wanaohudumu kinyume cha sheria baada ya kukamilika kwa makataa hayo.

Kulingana na Kifungu cha 4 (1) cha Sheria kuhusu Utengenezaji wa Filamu, watengenezaji wa filamu zinazonuiwa kuonyeshwa kwa umma ni sharti waidhinishwe na bodi ya KFCB.

Sheria hiyo pia inapendekeza faini ya fedha zisizozidi Sh100,000 au kifungo kisichozidi miaka mitano gerezani au adhabu zote mbili kwa watengenezaji wa filamu wanaopatikana na hatia ya kuhudumu bila idhini.

Kifungu cha 34 cha sheria hiyo pia kinasema kuwa ikiwa shirika, kampuni au chama kitakiuka sheria hiyo maafisa wasimamizi wake watawajibika.

“Bodi imebaini kuwa baadhi ya watengenezaji wa filamu wa humu nchini na kimataifa wamekuwa wamekuwa wakihudumu bila leseni. Kwa hiyo bodi ingependa kuwafahamisha kuwa kutengeneza filamu za kutazamwa na umma bila kibali kutoka kwa KFCB ni haramu,” akasema Dkyt Mutua.

Bodi ya KFCB ndiyo imetwikwa jukumu la kutathmini ubora wa filamu kabla ya kupeperushwa au kusambazwa kwa lengo la kuwalinda watoto dhidi ya kuonyeshwa filamu hatari na zinazokiuka maadili ya kijamii.

“Kwa hiyo bodi imetoa makataa ya siku 14 kwa watengenezaji wa filamu ambao hawajaidhinishwa kujitokeza na kuchukua leseni la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria baada ya kukamilika kwa makataa hayo,” akasema Dkt Mutua.

Mwaka 2017, KFCB iliwataka watengenezaji wa filamu walioidhinishwa na bodi hiyo kutolipa ada zozote kwa serikali za kaunti.

Dkt Mutua alisema shughuli ya usimamizi wa filamu haikugatuliwa hivyo ni jukumu la serikali ya kitaifa.

“Mtengenezaji wa filamu anapopata leseni kutoka kwa KFCB hafai kwenda kutafuta kingine kutoka kwa serikali ya kaunti. Bodi ya KFCB iko tayari kuingilia kati kuhakikisha kuwa kaunti zinazohangaisha watengenezaji walioidhinishwa zinafikishwa mahakamani,” akasema Mkurugenzi Mkuu.

Uchafu kwenye mazingira ulivyozidisha athari za mafuriko mitaani

Na SAMMY KIMATU

MVUA ni baraka na Wakenya wamekuwa wakiiomba inyeshe baada ya kushuhudiwa mahangaiko yaliyosababishwa na ukame na kiangazi kwa muda mrefu.

Wakati huo wa kiangazi, mito ilikauka, maua yakanyauka, mifugo wakafa na waliosalia wakakonda kama ng’onda.

Watu walilaumiwa, tetesi zikiwa ufisadi na wafisadi kuongezeka katika biashara ya kuuza makaa, sambamba na ya mbao.

Kuna viongozi wa kisiasa, kwa mfano aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga aliyesema watu wamevamia na kukata miti katika Mlima Mau eneo la Rift Valley.

Alitoa kauli yake kwamba wanaoishi maeneo hayo ya msitu huo ambao ni moja katika ile kubwa nchini kwa kuvuta mvua wahamishwe.

Lakini alipingwa sana na wapinzani wake wa kisiasa waliodai watu wao wanalengwa na kuonewa.

Lisilobidi hubidi. Hali hii ya kiangazi ilisukuma idara husika kuchukua hatua ya dharura kuokoa misitu ndipo waziri wa mazingira na misitu Bw Keraiko Tobiko akapiga marufuku ukataji miti kwa muda wa miezi mitatu.

Baada ya maombi makanisani, masokoni na misikitini Maulana alete mvua, hatimaye mvua imenyesha katika kaunti zote 47 tangu Machi.

Ajabu ni kwamba mvua hii ya masika iliyongojewa kwa hamu na ghamu imekuja na athari zake- mafuriko.

Katika vyombo vya habari tumesoma magazetini, kusikiza redioni na kutazama runingani watu na wanyama wakifariki pia baada ya kuporomokewa na nyumba. Mifano michache ni kama vile:- mkasa wa Solai (Nakuru) ambapo watu zaidi ya 40 walikufa baada ya bwawa la Solai kupasuka.

Kaunti za Murang’a na Makueni kuliripotiwa maporomoko yaliyowaacha wengi bila Makao.

Kaunti zingine ambazo wakazi waliathikika ni Tana River, Homa Bay, Nakuru, Isiolo, Moyale, Taita Taveta, Kilifi, Lodwar na Garissa.

Katika Kaunti ya Nairobi, kila kukinyesha, wanaoathirika zaidi ni wakazi kwenye mitaa ya mabanda iliyoko South B (Eneo bunge la Starehe), Mukuru-Kwa Reuben (Embakasi South) Kingstone na Lunga Lunga (Makadara)

Machi mwaka huu, shule nane zilifungwa kufuatia mafuriko yaliyokatiza masomo. Miongoni mwao ni Shule ya Msingi ya Brightstar, ya upili ya Brightstar, SDA Little Kids, New Dawn, Community Initiative and Bridge International – shule ya Upili ya Viwandani na ya msingi ya St Elizabeth miongoni mwa zingine.

Wakazi mitaani ya mabanda ya Mukuru- Fuata Nyayo, Mukuru-Kaiyaba, Mukuru-Hazina na Mukuru-Maasai hawakusazwa na janga hilo.

Nyumba zilisombwa na maji, vibanda na vyoo vikabomoka, vioski vikaingiwa na maji huku mali ya thamani isiyojulikana ikiharibika.

Mitaa yote hii imo kando ya mto Ngong. Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kwamba maji katika Mto Ngong hukosa mkondo baada ya wanyakuzi kujenga nyumba na kuta jambo linaloubana mto hivyo kunyima mto njia ya kupitisha maji.

 

Daraja limezibwa na taka

Kijijini Kaiyaba, hasa katika daraja la Kaiyaba/Hazina hapa utakuta rundo la taka kutoka kwa wenyeji na mlima wa taka zinazotupwa kutoka kwa kampuni kadhaa na kuziba daraja hilo.

Kukinyesha, taka hiyo huziba maji ndiposa nyumba hufurika licha ya mvua kuwa sio nyingi katika mtaa wa Kaiyaba na Hazina.

Takriban mita 500 kutoka katika daraja hili utakutana na bomba la kupitisha maji machafu linaloziba takataka upande wa chini na kulazimisha maji kufurika katika kijiji cha Maasai.

Taswira wakati huu ni kwamba nyumba zilizojengwa karibu na mto zilibomolewa na maji kutoka upande wa nyuma na mabati yakabebwa na maji.

Zingine huwa zoimejengwa juu ya magunia yaliyotiwa mchanga jambo linalolazimisha mto kubanika na maji kubadilisha mkondo.

Ilibidi mkuu wa tarafa ya South B, Bw Barre Ahmed na maafisa kutoka kwa Halmashauri ya Kusimamia Masuala ya Mazingira (NEMA) kuingilia suala la unyakuzi wa mto.

“Takataka iliyokuwa imeziba mto imezolewa na kwa wakati huu maji hupita vizuri na hatujapokea ripoti ya mafuriko katika vijiji vyetu tena licha ya mvua nyingi kunyesha mwezi Machi na Aprili,” Bw Barre akasema.

 

Onyo

Bw Barre ametoa wito kwa yeyote atakayepatikana akitupa taka ndani ya mto Ngong atakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Awali, mwakilishi wa wodi ya LandMawe, Bw Herman Azangu alikuwa akileta tinga tinga kuzoa taka punde ikiziba mto kabla ya mvua kunyesha ili aokoe watu kutokana na mafuriko.

Mtaani Kingstone, wanyakuzi wa ardhi wamebadilisha mkondo wa maji baada ya kumwanga milima ya mchanga na kujenga nyumba huku maji ya mto yakilazimika kupitia katiika uga wa shule ya Msingi St Elizabeth.

Utawala wa shule kupitia Mkurugenzi Mkuu, Mtawa Mary Killeen wameomba serikali kuchukulia wanyakuzi hao hatua kali kwani kunyeshapo hulazimika kufunga shule hadi maji yatakapoisha.

“Ni shule ya kisasa iliyogharimu wahisani kutoka serikali ya ujerumani mamilioni ya pesa,” Mtawa Mary akasema.

Baba mkwe wa mwanamke aliyegongwa na Pasta Ng’anga asema anahofia maisha yake

Na ERIC WAINAINA

BABA MKWEWE Bi Mercy Njeri, ambaye alifariki baada ya kugongwa na gari la mhubiri James Ng’ang’a amedai kwamba maisha yake yamo hatarini.

Marehemu alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kugongwa na gari hilo katika katika Barabara Kuu ya Nairobi-Nakuru.

Jumatatu, Peter Ndung’u aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Tigoni.

Aidha, anadai kwamba kwamba watu kadhaa walivunja na kuingia nyumbani kwake katika kijiji cha Murengeti Jumapili mchana, ambapo waliingia katika vyumba vyote ila hawakuchukua chochote.

Kesi ya mauaji dhidi ya Bw Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism Centre ilitupwa wiki iliyopita na mahakama moja ya Limuru kwa msingi wa ukosefu wa ushahidi wa kutosha dhidi yake.

Kulingana na Bw Mburu, watu hao waliingia kwake kwa kuvuka ua uliopo, ambapo walivunja milango yote na kuingia sebuleni.

Alisema kuwa walikaa ndani kati ya saa nne asubuhi hadi saa nane alasiri wakati yeye na familia yake walikuwa kanisani.

“Ni kama kwamba walikuwa wakitafuta kitu fulani, kwani waliingia katika kila chumba, ila hawakuchukua chochote. Hili linanaamisha kwamba hao si wezi wa kawaida,” akasema Bw Ndung’u.

Aidha, alisema kwamba aliripoti kisa hicho kwa polisi, ambapo walifika na kuandikisha taarifa kutoka kwa familia yake.

Bw Ndung’u alisema kwamba kabla ya uvamizi huo, alikuwa amegundua kwamba kuna watu kadhaa ambao walikuwa wakimfuata, hali iliyomfanya kuhofia usalama wake.

“Mapema Jumapili, nilikuwa nimefikiria kuripoti kwa polisi, kwani niliona hali hiyo kutokuwa ya kawaida. Watu wapya walikuwa wakinifuata na kunisalimia kila wakati.

Wengine wamekuwa wakiendesha pikipiki karibu na makazi yangu, hasa wakati wa usiku, jambo ambalo si la kawaida kwani nyumba yangu iko katika eneo limejificha sana,” akasema.

Na ijapokuwa alisema hana ushahidi kuhusisha matukio hayo na maamuzi ya kesi hiyo, alieleza kuwa hayo yalianza kujitokeza baada ya mahakama kutoa uamuzi huo.

Alisema kuwa hilo linapaswa kuchunguzwa mara moja.

“Hakuna hatua nyingine ningechukua, ila kuwaarifu polisi. Ningetaka wachunguze ili kubaini ikiwa hayo yana uhusiano wowote na maamuzi ya kesi hiyo,” akasema.

Kabla ya uamuzi wa kesi hiyo, familia ilikuwa imekataa juhudi za upatanisho kutoka kwa watu waliodai kutumwa na mhujbiri huyo.