Hata mruke angani, marufuku ya makaa itadumu, aapa Gavana Ngilu

Gavana Charity Ngilu akihutubia wanahabari nje ya mahakama kuu ya Milimani Machi 5, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Kitui Bi Charity Ngilu, Ijumaa alisisitiza kwamba hakuna kurudi nyuma katika kutekeleza amri ya kutochoma makaa.

“Hata wapande juu ya miti , ama waende baharini ama waruke angani, hata kufanyike nini, amri ya marufuku ya kukata miti na kuchoma makaa katika kaunti ya Kitui itadumu,” Bi Ngilu alisema punde tu mahakama ilipotupilia mbali kesi ya kupinga uchaguzi wake.

Wafuasi waliofuruka katika mahakama ya Milimani walimhakikishia Gavana huyo kwamba “watapambana na wachomaji makaa kwa kila hali.”

Bi Ngilu alisema marufuku hiyo ya makaa na usombaji changarawe itadumu.

“Kaunti ya Kitui imegeuzwa kuwa jangwa. Miti ya asili yote imekatwa na kuchomwa makaa na wafanyabiashara kutoka kaunti nyingine. Marufuku hii itadumu,” alisema Bi Ngilu huku akishangiliwa.

Bi Ngilu aliwashauri wakazi wote wa Kitui na jimbo lote la Ukambani walinde misitu , kupanda miti na kutochoma makaa.

Mshukiwa wa ugaidi kusalia ndani hadi kesi iamuliwe

Ahmed Yusuf Okoth katika mahakama ya Nairobi aliponyimwa dhamana kwa kosa la ugaidi. Picha/Richard Munguti

RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa ugaidi, Ahmed Yusuf Jumatatu aliamriwa akae rumande kwa kosa la ugaidi hadi kesi inayomkabili isikizwe na kuamuliwa.

Hakimu mkuu Francis Andayi  alikataa ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana akisema, “atachana mbuga akiachiliwa huru kwa sasa.”

Bw Andayi alisema adhabu ya kosa linalomkabili mshtakiwa ni kali  kwa vile ni kifungu cha miaka 30 kwa kosa la kushiriki katika ugaidi.

Anakabiliwa na mashtaka matano miongoni mwao kutoa mafunzo ya ugaidi kwa wanafunzi wa shule eneo la Trans-Nzoia.

Akisoma uamuzi alisema , “Upande wa mashtaka umethibitisha kwamba utatoroka ukipewa dhamana.”

Mshtakiwa atakaa rumande hadi kesi iamuliwe. Ushahidi utaanza kutolewa Machi 16.

Hakimu aamuru anayedaiwa kuiba kioo apelekwe hospitalini kutibiwa nyeti zilizoumizwa akikamatwa

Joseph Odero Olanjo akiwa kortini Jumatatu aliposhtakiwa wizi wa kioo cha gari la makavazi ya kitaifa- Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU Mkuu katika Mahakama ya Milimani Nairobi Francis Andayi ,  Jumatatu alimwamuru afisa mkuu wa polisi katika mahakama hiyo ampeleke mshukiwa hospitali kutibiwa nyeti zake baada ya kuungama alivutwa yeti zake na walinzi waliomshika akiwa na kioo cha gari la makavazi ya kitaifa.

“Mheshimiwa naumia sana. Naumwa na dhakari yangu. Sehemu yote ya eneo la nyeti zangu inauma. Nilivutwa mboo yangu na mabawabu walionishika, naomba uamuru nipelekwe hospitali,” aliomba Joseph Odero Olanjo.

Olanjo aliendelea, “Mbali na yeti zangu, natokwa na damu pua la kushoto. Niliumizwa vibaya. Naomba nipelekwe hospitali.”

Mshtakiwa huyo pia alimsihi hakimu aamuru atibiwe kidole cha kati cha mkono wake wa kulia kilichokeketwa kwa wembe na askari waliomtia nguvuni.

Akasema , “Unavyoniona nimesimama mbele yako mimi naumwa na kila kiungo mwilini mwangu. Naomba uamuru nitibiwe.”

Bw Andayi aliamuru afisa msimamizi wa idara ya polisi mahakamani ampeleke hospitali.

Olanjo alishtakiwa kwa wizi wa kioo chenye thamani ya Sh40,000 cha gari la Makavazi ya Kitaifa mnamo Machi 1, 2018.

Taabani kwa kukosa kulipia ngozi ushuru

Godfrey Bosire akiwa kizimbani aliposhtakiwa kwa uuzaji ng’ambo zaidi ya kilo milioni 3 za ngozi za ng’ombe na kukwepa kulipa mamlaka ya ushuru nchini (KRA) Sh204 milioni. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumatatu kwa kuuza ngozi za ng’ombe kilo 3,862,264  ng’ambo na kukwepa kulipa serikali ada ya forodha iliyopelekea serikali kupoteza ushuru wa Sh204 milioni.

Bw Godfrey Bosire alikanusha shtaka hilo mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya miliamni Bw Francis Andayi.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha aliomba kesi hiyo dhidi ya Bw Bosire itajwe Jumanne kwa lengo la kuiunganisha na  nyingine ambapo Bi Clare Marisiana Odimwa alishtakiwa kwa kosa kilo hilo.

Bw Naulikha alisema nakala za mashahidi katika kesi hiyo ziko tayari na kuwa Bw Bosire anaweza kuzipokea aandae tetezi zake.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa katika kesi dhidi ya Odimwa mahakama ilimwachilia kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Pia alisema mshtakiwa huyo  alipewa dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000.

Wakati huo huo Bi Margret Awino Magero alishtakiwa kwa kupokea sabuni na mafuta ya kupikia za thamani ya Sh 17 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Mabw Jeremiah Kiplangat Kendagor na Bw  Lukas  Oketch Mandagi Desemba 2016.

Alikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu.

Waliovuta bangi ili wakanengue viuno kwa shoo ya Freddie McGregor wajikanganya mahakamani

Kevin Munene (kushoto) na Nicholas Kamau Wambui wakiwa katika mahakama ya Milimani waliposhtakiwa kupatikana na misokoto mitano ya bangi. Picha/Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

WANASARAKASI wawili walijikanganya mahakamani waliposhauriwa na hakimu wakiri mashtaka ya kupatikana na bangi misokoto mitano kisha waombe msamaha wasamehewe ili waachiliwe waende nyumbani.

“Najua kwamba mlikuwa mnaivuta hii bhangi ndipo mkacheze densi katika tafrija iliyoandaliwa na mchezaji regge wa kimataifa Bw Freddie McGregor aliyekuwa ameandaa shoo katika ukumbi wa Jomo Kenyatta International Conference (KICC),” hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani  Bw Francis Andayi aliwaambia wawili hao.

“Si ni kweli mlikuwa mnavuta ili mkacheze densi?” Bw Andayi aliwauliza wawili hao waliOkuwa na mtindo wa nywele wa Rasta.

“Ni kweli . Tulikuwa tumewasha msokoto wa kwanza polisi walipotufumania,” alijibu Munene

“Milikuwa mmepatikana na misokoto hii ni kweli au sio kweli?” hakimu aliwahoji zaidi.

“Hapana huyu mwenzangu ndiye alinipa msokoto wa kwanza kuvuta. Sikuwa na bangi hii mimi,” alijibu Kamau.

Hakimu akasema, “Badala ya kuenda jela zaidi ya miaka saba nawashauri ombeni msamaha mkisema kwamba ni upumbavu mko nao wa ujana na kwamba hamtarudia tena kupatikana na bangi ndipo niwaachilie mkashiriki katika ujenzi wa taifa.”

 

‘Siwezi kujiita mpumbavu’

“Mimi siwezi kusema ni mpumbavu hata!,” akasema Kamau.

“Wacha nikushauri usijaribu kuwa mwerevu. Mtaumia bure tu na kukaa rumande kabla ya kesi inayowasubiri kusikizwa na kuamuliwa,” hakimu aliwashauri .

Hakimu aliwashauri adhabu ya msokoto mmoja na tani za mhadharati huu uliopigwa marufuku ni moja tu.

Kamau aling’ang’ana kujinasua na kutopatikana na bangi hiyo ndipo hakimu akawaambia, “kwa vile mmekataa kusikiza ushauri sasa mtaenda rumande na kila mmoja wenu ataachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 ama dhamana ya pesa taslimu Sh50,000.”

Munene, kusikia mambo yamewaendea mrama alirudi tena kizimbani na kumsihi hakimu amsamehe lakini akaambiwa , “ mmepewa fursa mjiokoe lakini mkakataa.”

“Naomba niachiliwe nikalipe nyumba kwa vile itafungwa na Landilodi,” alimweleza hakimu huku akiambiwa , “Tuma pesa kwa njia ya mtandao wa Mpesa kwa landlilodi wako.”

“Haki ya Mungu niko na Sh500 tu kwa mfuko,” Munene alimweleza hakimu huku akiomba msaada lakini akajibiwa ,  Mngikubali ushauri mngekuwa nje sasa lakini sasa lipeni dhamana mtoke.”

Shtaka dhidi yao lilisema walikutwa na misokoto mitano ya bhangi Machi 4 katika uwanja wa KICC.

Mng’oa meno aamriwa asikizane na shemeji zake

Kutoka kushoto: Ashman Sapra, Dkt Nisha Sapra na Bi Kuldip Sapra wakiwa katika Mahakama ya Milimani Machi 5, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

DAKTARI wa kung’oa meno na shemeji zake wawili Jumatatu walipewa muda wa wiki moja waafikiane kuhusu ugavi wa mali ya Sh700 milioni wanayong’ang’ania.

Hata hivyo Dkt Nisha Sapra  alielezea waziwazi kwamba shemeji wake wawili Kuldip Sapra na Ashman Madan Sapra “ hawatamsikiza kwa vile wanasema alimuua ndugu yao Yogesh Sapra  miaka 13 iliyopita.”

Pia Dkt Sapra alimweleza hakimu mkuu  Bw Francis Andayi kwamba hajui kama haki itatendeka kabla ya kuamuliwa kwa kesi inayomkabili ya kumuua mumewe Yogesh Agosti 2005.

Lakini Bw Andayi aliwaeleza watatu hao Kuldip , Ashman na Dkt Sapra kwamba “kesi zote zilizo katika Mahakama za Kenya kuhusu mali ya Yogesh zitafikia tamati siku moja hata kama zitachukua miaka mingapi.”

Bw Andayi aliyekuwa anatarajiwa kusoma uamuzi iwapo Kuldip na Ashman wataagizwa wajibu mashtaka manne ya ugushi wa stakabadhi kuhusu ugavi wa mali aliyoacha Yogesh alipoaga ilichukua mkondo mpya na kuwauliza, “kwa nini hamwezi kusikizana na kufikia suluhu katika mzozo huu ambao kwa maoni yangu utachukua miaka mingi kuamuliwa?”

Ndugu hao- Kuldip na Ashman wamepinga uamuzi wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kuwashtaki kwa kughushi stakabadhi ya umiliki wa mali ya Yogesh.

 

Wafikirie tena

Bw Andayi aliwashauri  watatu hao wafikirie tena na tena kuhusu kufikia suluhu ya mzozo huo wa umiliki wa mali.

Kuldip na Ashman wanasisitiza kwamba “hawajagushi hati yoyote kuhusu mali ya ndugu yao mbali ni Dkt Sapra aliyetia sahihi cheti akisema hataki kuwa msimamizi wa mali ya mumewe (ndugu yao) kwa vile anakabiliwa na kesi ya kumuua mumewe.”

Kabla ya kusoma uamuzi uamuzi Bw Andayi aliuliza , “J,  mlalamishi katika kesi hii yuko kortini?”

Dkt Sapra alisimama na kusema, “ Ndiyo mheshimiwa, niko mahakamani.”

“Kuja mbele,” Bw Andayi alimwamuru.

Alipoenda mbele na kusimama kizimbani, hakimu aliwauliza watatu hao , “Je, kuna uwezekano wa kufikia suluhu nje ya mahakama ya  mzozo huu ambao umesikizwa na mahakama karibu zote isipokuwa Mahakama ya Juu?”

 

Siku 40

Alisema amesoma faili zote za kesi hiyo akiandaa uamuzi wake na ameona wakati mmoja wakili Harun Ndubi na Kwame Nkuruma wanaowatetea Kuldip na Ashman pamoja na wakili wa Dkt Sapra walikuwa wameitisha siku 40 watafute suluhu ya mzozo huo wa umiliki wa mali ya Yogesh.

“Je, nyote mnaelewa Kiingereza?” Bw Andayi aliwauliza Kuldip, Ashman na Dkt Sapra.

“Ndio tunaelewa,” walijibu.

Bw Andayi aliwataka mawakili wafanye kikao cha pamoja na kutafuta suluhu ya mzozo huo.

“Kesi hizi za mizozo ya umiliki wa mali huzua uhasama mkali katika jamii. Naamini katika Jamii ya Wahindi kuna Wazee wanaoweza kusuluhisha mzozo huu ikitiliwa maanani Yogesh alifariki na hata kesi hii ikifanywa miaka na mikaka hatafufuka. Hata watoto wake huenda wakachukua mwelekeo mwingine na kuwakatalia mbali wajomba wao na hata kumchukia mama yake (Nisha Sapra),” alisema Bw Andayi.

Marehemu alikuwa amejaliwa watoto watatu  Rishi Sapra (mvulana) , Rakhee na Priya ( wasichana) wanaosoma nchini Canada.

Katika barua waliyoandikia Mahakama Kuu ya Kenya mnamo Juni 22, 2015, wana hao waliambia korti kwamba wangependa wajomba wao Kuldip na Ashman kusimamia mali ya baba yao na wala sio mama yao Dkt Sapra.

Jaji Aggrey Muchelule anayesikiza kesi hiyo ya umiliki wa mali ya Yogesh aliwateua Kuldip na Ashman kusimamia mali aliyoacha mwenda zake.

Kesi itatajwa Machi 13, 2018.

Kimetto kushiriki Boston Marathon baada ya miaka minne

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya wanaume, Dennis Kimetto, ametangaza atashiriki Boston Marathon nchini Marekani mnamo Aprili 16, 2018.

Kimetto, ambaye anajivunia kasi ya juu kuwahi kutambuliwa na Shirikisho la Riadha duniani (IAAF) katika mbio hizi ya saa 2:02:57, hajakuwa akionekana tangu aweke rekodi hiyo katika Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2014.

Mwaka 2015, aliwakilisha Kenya katika Riadha za Dunia jijini Beijing nchini Uchina, lakini hakukamilisha mbio.

Alijiondoa kushiriki Chicago Marathon nchini Marekani mwaka 2016 kwa sababu ya kujeruhiwa mguu wake wa kushoto.

Kimetto aliapa kuvunja rekodi hiyo ya dunia katika Chicago Marathon mwaka 2017, lakini hakufanikiwa kumaliza makala hayo. Alijiondoa kabla ya kukamilisha kilomita 25.

“Nahisi niko na nguvu sasa kutokana na mazoezi nimekuwa nayo tangu mwaka jana (2017). Natumai nitarejea kwa kishindo mjini Boston,” Kimetto, ambaye alianza kushiriki mbio za kilomita 42 mwaka 2012, aliambia gazeti la Daily Sport.

Esperance ya Tunisia yatua nchini kuchuana na Gor Machakos

Na GEOFFREY ANENE

MIAMBA wa soka wa Tunisia, Esperance, wamewasili nchini Kenya kwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika.

Mabingwa hawa wa Tunisia mara 27 wametua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Jumatatu usiku.

Esperance, ambao walishinda mataji ya Afrika mwaka 1992 na 2017 na kumaliza nambari mbili mwaka 1999, 2000, 2010 na 2012, watalimana na wenyeji Gor Mahia hapo Machi 7 saa kumi jioni uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor, hawajawahi kushinda mashindano haya ya kifahari katika historia yao.

Gor ya kocha Dylan Kerr iliwahi kukutana na Esperance katika ulingo wa kimataifa kwenye shindano la Cup Winners’ Cup mwaka 1987. Ilinyakua taji kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya 2-2 jijini Tunis nchini Tunisia na 1-1 jijini Nairobi. 

Gor ilinyakua tiketi ya kushiriki raundi ya kwanza ilipobandua nje Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-1 nayo Esperance ikang’oa ASAC Concorde ya Mauritania mashindanoni kwa jumla ya mabao 6-1.

Kazi rahisi kwa Prisons na Pipeline baada ya droo ya voliboli

Na GEOFFREY ANENE

DROO ya mashindano ya voliboli ya Klabu Bingwa Afrika ya wanawake imefanywa, huku wawakilishi wa Kenya, Pipeline na Prisons, wakiwekwa katika makundi yanayoonekana rahisi.

Mabingwa mara saba Pipeline wamo Kundi C ambalo pia linajumuisha washindi wa medali ya fedha mwaka 2017 El Shams (Misri), FAP (Cameroon), DGSP (Congo Brazzaville) na Vision (Uganda). Tishio kubwa hapa kwa Pipeline ya kocha Japheth Munala ni Shams na FAP.

Prisons ya kocha David Lung’aho, ambayo inajivunia mataji matano ya Afrika, italimana na INJS (Cameroon), Customs (Nigeria), Douanes (Burkina Faso) na Asec Mimosas (Ivory Coast) katika Kundi D. Katika kundi hili, Prisons na INJS zina uzoefu wa miaka mingi.

Mabingwa mara nane Al Ahly (Misri) wako kundi A pamoja na Nkumba (Uganda), Nyong (Cameroon) na Rwanda Revenue Authority (Rwanda). Mkenya Dorcas Ndasaba ndiye kocha mkuu wa wawakilishi hawa wa Rwanda.

Mabingwa watetezi Carthage (Tunisia) watalimana na Harare (Zimbabwe), Chlef (Algeria), Bafia (Cameroon) na Botswana Defence Force katika Kundi B.

Timu mbili za kwanza kutoka makundi haya manne zitaingia robo-fainali.

 

Vikosi vya timu za Kenya:

Pipeline – Trizah Atuka (nahodha), Noel Murambi, Leonida Kasaya, Celestine Nafula, Monica Biama, Naomi Too, Rose Jepkosgei, Yvonne Sinaida, Janet Wanja, Agrippina Kundu, Rael Tebla, Esther Wangeci, Lucy Akinyi na Christine Ngugi. Benchi la kiufundi – Japheth Munala (kocha mkuu), Margaret Indakala (kocha msaidizi)

Prisons – Mercy Moim (nahodha), Joy Luseneka, Herma Jepyegon, Loise Jepkosgei, Edith Wisa, Emmaculate Chemtai, Shyrine Jepkemboi, Diana Khisa, Lorine Chebet, Everlyne Makuto, Sharon Chepchumba, Yvonne Wavinya, Elizabeth Wanyama na Judith Tarus. Benchi la kiufundi – David Lung’aho (kocha mkuu), Josp Barasa (kocha msaidizi).

Marwa ashtakiwa kwa kumdhalilisha Spika

Na LEONARD ONYANGO

MAHAKAMA ya Rufaa imeagiza Katibu Wizara ya Ugatuzi Nelson Marwa ashtakiwe kutokana na madai ya  kumdhalilisha Spika wa Bunge la Kaunti la Mombasa Harub Ebrahim Kharti.

Bw Kharti alimshtaki Bw Marwa mnamo Januari 2017 kwa kumhusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya na kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Kukamatwa kwa Bw Kharti kulizua uhasama baina ya Bw Marwa aliyekuwa Mshirikishi wa Ukanda wa Pwani, na Gavana wa Mombasa Hassan Joho. Gavana Joho alivamia afisi za mkoa wa Pwani na kutaka Bw Kharti aachiliwe huru.

Mnamo Machi 14, mwaka 2017, Jaji wa Mahakama Kuu Njoki Mwangi aliamua kuwa Bw Marwa hakufaa kushtakiwa kwa sababu alitoa matamshi hayo kwa niaba ya serikali kama Mshirikishi wa Ukanda wa Pwani.

Mahakama Kuu ilitoa uamuzi huo baada ya aliyekuwa Mkuu wa Sheria Githu Muigai kusema kuwa Bw Marwa hawezi kushtakiwa yeye binafsi kwa kuwa alitamka maneno hayo kama mwakilishi wa serikali.

Mahakama ya Rufaa Jumanne iliamua kuwa matamshi yaliyotolewa yatathibitishwa kuwa yaliambatana na sera za serikali ikiwa kesi dhidi yake itasikilizwa hadi mwisho.

Polo aponea kifo alipofumaniwa ‘akitafuna mbuzi’ katika zizi la jirani

Na TOBBIE WEKESA

KWAMWENJAS, NYERI

KALAMENI mmoja aliponea kwenye tundu la sindano alipofumaniwa na mzee wa boma akiwa katika chumba cha binti yake.

Kulingana na mdokezi, baba ya mrembo alikuwa akitoka kwa boma la jirani. Alipofika kwa boma lake, aliamua kupitia karibu na chumba cha binti yake ambapo alishtuka kusikia sauti nzito kutoka ndani.

Mzee aliamua kusimama ili kubaini sauti ilikuwa ya nani na nini kilichokuwa kikiendelea ndani. “Hii sauti haikosi ni ya mwanaume. Leo atanijua,” mzee aliapa.

Inadaiwa polo alikuwa amemtembelea mrembo na kisha akaalikwa chumbani kisiri. Duru zinaarifu kwamba chumbani, polo alikuwa tayari juu ya mzinga akirina asali. Kilichomuuza ni sauti yake nzito.

Habari zilizotufikia zinasema mzee aliamua kuugonga mlango kwa mkongojo aliokuwa ameshika. “Hiyo sauti ni ya nani?” mzee alimuuliza binti yake.

Binti hakumjibu mzee. “Nauliza ni nani huyo yuko humu ndani? Nataka kumjua,” mzee alizidi kuteta.

Inadaiwa kuwa mzee alianza kuusukuma mlango akitaka kuingia ndani kwa nguvu. “Mnafanya nini humu ndani?” mzee aliwakaripia. Kwa kugundua kuwa chuma chake ki motoni, polo alianza kutafuta namna ya kuhepa.

“Hauna aibu kuja kwangu bila idhini. Leo mtu lazima mguu ubakie hapa,” mzee aliapa huku akiwaita majirani.

Penyenye zinasema polo alijipenyeza kwenye dirisha na kutimua mbio kabla ya majirani kufika.

“Kijana wewe una bahati. Hiyo sauti yako peleka mbali kabisa. Huwezi kuja na kula katika zizi langu. Nikikupata tena utajua mimi ndiye mwenye hii boma,” mzee alimkemea polo huku akimfuata nyuma.

 

SHANGAZI AKUJIBU: Mapenzi yake ni ya mdomo tu, hakuna vitendo

Shikamoo shangazi. Kuna msichana ambaye nampenda kwa dhati lakini nina shaka iwapo yeye pia ananipenda. Sababu ni kuwa ananipenda kwa maneno tu si kwa vitendo. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi huanzia kwa ahadi za maneno wala si vitendo. Kama mwenzako anakuhakikishia kwa maneno kuwa anakupenda, kuwa na subira hadi atakapokuwa tayari kugeuza maneno yake kuwa vitendo.

Mumewe amerudi, nifanye nini?
Shangazi hujambo? Nimekuwa na uhusiano wa miaka mitatu na mwanamke aliyeachana na mumewe na ana watoto watatu. Sasa baba ya watoto wake amerudi. Nishauri.
Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, mwanamke huyo na mume wake wameamua kurudiana. Kama ndivyo, huna budi kujiondoa kwani wenu umekuwa uhusiano tu wala hujamuoa. Sasa amekuwa tena mke wa mwenyewe na itakuwa haramu kuendelea na uhusiano huo.

 

Natafuta mume
Vipi shangazi? Nilimaliza shule 2014 na natafuta mume mwenye sifa zifuatazo: mwokovu, msomi, mwenye maono, mwenye bidi, mkarimu na mwaminifu. Mchezo kando. Tafadhali nisaidie.
Kupitia SMS

Ninaamini wapo wanaume walio na sifa zote hizo. Hata hivyo, siwezi kukusaidia kwani wajibu wangu hapa kutoa ushauri tu wala si kutafutia watu wachumba. Kuwa na subira na uendelee kutafuta, hatimaye uapata. Nakutakia kila la heri.

 

Mchumba amesema siwezi kumuoa
Mwanamke ambaye nilidhani nitamuoa amegeuka akaniambia haiwezekani kwa sababu binamu yake ameolewa na ndugu yangu. Nahofia akiniacha sitaweza kupata mwingine kama yeye. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Ingawa hakuna ubaya wowote kwake kuolewa katika familia moja na binamu yake hilo si jambo la kawaida katika jamii na labda limepingwa na jamaa zake. Kwa sababu hiyo, itabidi ukubali tu na uweke matumaini kwamba utapata mwingine anayekufaa.

 

Nilimsaidia sasa anataka nimuoe, tayari nina wake 3
Kuna msichana niliyemsaidia baada ya kupata ajali barabarani nikamsaidia kutibiwa hospitalini na pia kulipwa fidia. Sasa anataka nimuoe na tayari nina bibi watatu. Mimi nilitenda wema tu, sikutaka malipo. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Ulifanya vizuri kumsaidia msichana huyo lakini usikubali atumie ukarimu wako kwa njia isiyofaa. Mwambie wazi kuwa hutaki mke mwingine na kama unahisi amekuwa mzigo kwako ukatize kabisa mawasiliano kati yenu.

Napenda mzee lakini naogopa kusemwa
Nina umri wa miaka 30 na niliachana na mume wangu miaka kadhaa iliyopita. Kuna mzee wa rika ya baba yangu tunayependana sana na yuko tayari kunioa. Nataka sana lakini naogopa kwamba walimwengu watanisema. Nishauri.
Kupitia SMS

Wewe ni mtu mzima na una haki ya kujiamulia mambo yote kuhusu maisha yako. Ukikosa kufanya maamuzi kulingana na moyo wako kwa kuogopa kusemwa utakosa mengi mazuri. Isitoshe, hata ufanye nini, binadamu watakusema tu. Fuata moyo wako na uishi maisha yako.

 

Aliyenibaka anataka kuoa dada yangu
Kwako shangazi. Kuna mwanamume fulani ambaye alinibaka na sasa anataka kumuoa dada yangu. Je, niwatenganishe ama niachane nao? Tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Kama kweli mwanamume huyo alikubaka na ukaweka jambo hilo kuwa siri, huenda dada yako akose kukuamini na badala yake kudhani kuwa unamsingizia mchumba wake kusudi tu kuvunja uhusiano wao. Ni heri uachane nao.

 

Ameninyamazia
Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miezi miwili sasa. Siku za hivi majuzi amenishangaza kwani nikimpigia simu ama kumtumia SMS ananyamaza tu. Nishauri.
Kupitia SMS

Si lazima mtu akwambie ndipo ujue hakutaki. Hizo ni ishara kamili za mtu ambaye anataka kumuacha mwenzake bila kumwambia hivyo. Mbona uendelee kupoteza wakati wako?

 

NYOTA YAKO: MACHI 6, 2018

KONDOO
Machi 21 – Aprili 20: Uko katika hali ngumu kwa sababu una wapenzi wawili na huna hakika unayempenda. Hii sio hali nzuri na itakupatia tumbo joto. Ukweli ni kwamba nyota yako inakuonya dhidi ya kushughulika na mapezi wakati huu.

 

NG’OMBE
Aprili 21 – Mei 20: Una tabia ya kupapia mambo jambo ambalo limepelekea ufanye maamuzi yasiyoifaa. Epuka anasa kwa sababu itakuletea hasara tele. Kumbuka mwenda pole hajikwai na akijikwaa huamka tena.

 

MAPACHA
Mei 21 – Juni 21: Dalili zaonyesha hali gumu iliyokulemea imeisha. Hata hivyo utahitajika kuweka bidii katika kazi yako. Huu sio wakati bora wa kununua shamba, subiri hadi baadaye. Tumia fursa hii kujenga imani yako.

 

KAA
Juni 22 – Julai 22: Naona roho yako ya chuma wakati huu haitakufaa chochote. Itakubidi unyenyekee ili upate utakacho. Sifa ya huruma itakufaa zaidi wakati huu. Peleleza moyo wako.

 

SIMBA
Julai 23 – Agosti 22: Unatamani sana kuiga wafanyavyo watu wengine, hii imefanya mambo yako kukwama. Unashauriwa kuvumilia hali yako, ikibidi uibadilishe, weka juhudi za ziada lakini usiige ya watu wengine. Baadhi wanapitia mambo magumu kuliko yako.

 

MASHUKE
Agosti 23 – Septemba 23: Badala ya kumsemasema rafiki yako akikukosea, tuma mtu akamuonye. Urafiki una thamani kuu na tabia hii itakufanya ukosane na marafiki wengi.
Kumbuka urafiki ni zaidi ya fedha na almasi.

 

MIZANI
Septemba 24 – Oktoba 23: Chukua muda ukae peke yako utafakari kuhusu maisha yako. Naona umelemewa na jambo fulani lakini ni kwa muda tu. Epuka marafiki wanaokuelekeza usikotaka. Hatima ya maisha yako iko moyoni mwako.

 

NGE
Oktoba 24 – Novemba 22: Hofu uliyo nayo ni ya kweli. Watu wamepanga njama kukulaghai. Habari njema ni kwamba kuna mngeni atakayekuibia njama zao. Fanya kila jambo kwa uangalifu zaidi, na watu wa nia mbaya watatoroka.

MSHALE
Novemba 23 – Desemba 21: Naona muujiza wa pesa ukikujia hivi karibuni. Huu utakuwa mwanzo wa kipindi kipya maishani. Lipa madeni yako ili wanaokudai wakuheshimu. Usiwadai walio na deni lako wakati huu.

 

MBUZI
Desemba 22 – Januari 20: atu hawakufuati kwa sababu wana haja nawe mbali wanapenda kukutumia tu. Hawataki muwe na uhusiano wa kudumu, wamegundua udhaifu wako. Chunga kwa sababu hatimaye wakichoka nawe watakudharau.

 

NDOO
Januari 21 – Februari 19: Unachokimezea mate si chako japo kinapendeza, chako ni kile unachodharau. Usipobadili nia mambo yatakwendea kombo. Usiache kibaya chako kwa kizuri cha wengine.

 

SAMAKI
Februari 20 – Machi 20: Ili kuepuka mambo mengi sana ya kukuudhi, kuwa na marafiki wachache. Na ili mambo yako yaende utakavyo kuwa na miradi michache. Unashauriwa ukome kupuuza ushauri wa wataalamu.

 

TAHARIRI: Dosari katika vitabu zirekebishwe haraka

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika shule ya Moi Girls, Eldoret wakionyesha vitabu walivyopewa chini ya mpango wa Serikali mapema mwaka huu. Walimu wamelalamika kuwa baadhi ya vitabu hivyo vina makosa yanayopotosha wanafunzi.
Picha/Jared Nyataya

Na MHARIRI

KUIBUKA kwa habari kwamba kuna kasoro nyingi kwenye vitabu vinavyotumiwa na wanafunzi ni jambo la kvunja moyo.

Walimu wanasema walianza kugundua makosa mengi mara walipopewa vitabu hivyo, na sasa wamelazimika kuviweka kando na badala yake wanatumia vingine ili wasipotoshe wanafunzi wao.

Vitabu hivyo vilivyogharimu Sh7.5 bilioni vilipeanwa kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza chini ya mpango wa Elimu Bila Malipo. Usambazaji wa vitabu hivyo ulizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Januari 5 mwaka huu na kufikia sasa vimesambazwa kwa wanafunzi wa shule za umma.

Malalamishi mengi zaidi yametoka kwa walimu wa Kiswahili, ambao wanasema mojawapo ya vitabu walivyopewa, kilichapishwa kwa haraka na kampuni moja mashuhuri ya uchapishaji nchini.

Makosa yaliyopatikana katika baadhi ya vitabu vya Kiswahili ni kama vile mifano potovu ya vivumishi, nomino, vitenzi na utumizi wa vipengele ambavyo havitambuliki katika lugha. Pia walimu wanasema mpangilio wa mada unakanganya.

Kulingana na walimu, kazoro hizo pia zimo kwenye vitabu vya masomo ya Kiingereza, Hesabu, Fizikia, Kemia na Biolojia.

Matatizo mengine yaliyopo yanahusu ufinyu wa mada. Hakuna maelezo ya kina. Wachapishaji waliharakisha bila kupitia ile kazi waliyokuwa wakichapisha.

Hii inaathiri wanafunzi kwa sababu wanasoma mambo ambayo hayawafai ama yanawapotosha

Afisa anayesimamia utafiti katika Taasisi ya Kenya ya Uundaji wa Mtaala (KICD), Bw Cyril Oyuga, amekiri kwamba taasisi hiyo imefahamu kuna dosari katika baadhi ya vitabu na tayari kuna mikakati iliyowekwa kusahihisha makosa.

Maadamu maafisa wa KICD wamekiri kuwepo kwa kasoro hizo, ipo haja kwa wao kuamuru vitabu hivyo vikusanywekuharibiwa, ili viandikwe tena kwa utaratibu.

Inaeleweka kuwa huenda kampuni za uchapishaji ziliharakishwa na zikawaharakisha waandishi, lakini maadamu kosa limeshajulikana, kilicho muhimu sasa ni kutolirudia.

Elimu ni jambo muhimu na msingi wa maisha kwa kila binadamu. Kile anachofunzwa mwanafunzi shuleni, humpa mwelekeo wa kufuata anapomaliza masomo.

Itakuwa busara ikiwa wanaohusika na masuala ya vitabu watachukua muda kupitia kila neno ndani ya vitabu vitakavyorekebishwa, ili wanafunzi wasipotoshwe.

 

 

Wafisadi katika Wizara ya Ugatuzi hawana pa kujificha – Marwa

Bw Marwa amesema magavana watafuatiliwa kuhusiana na namna wanavyotumia rasilimali za wananchi wanazopata ndani ya ugatuzi. Picha/ Maktaba

Na MOHAMED AHMED na WINNIE ATIENO

KATIBU wa Wizara ya Ugatuzi, Nelson Marwa ameapa kupambana na ufisadi katika wizara hiyo. Bw Marwa alisema kuwa kikosi maalum kimeundwa ili kupambana na ufisadi.

“Mambo ya ufisadi hamtasikia tena. Kile mutaona ni huduma kwa wananchi wote,” akasema Bw Marwa.

Visa vya madai ya ufisadi viliwahi kukumba wizara hiyo wakati wa muhula wa kwanza wa uongozi wa Jubilee.Kesi hizo za ufisadi zilipelekea kujiuzulu kwa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kama waziri.

Bw Marwa alisema kuwa kikosi hicho kitafuatilia kwa makini namna utendaji kazi utakavyoendeshwa chini ya ugatuzi.

Akizungumza katika hoteli ya Travellers wakati wa warsha ya majadiliano kuhusu ugomvi kati ya serikali kuu na zile za kaunti, Bw Marwa alisema magavana watafuatiliwa kuhusiana na namna wanavyotumia rasilimali za wananchi wanazopata ndani ya ugatuzi.

“Kila Mkenya ni muhimu kwetu. Tuko na magavana wanaoelewa namna mambo yanatakiwa kufanywa. Kwa hivyo lazima wapeane huduma bora kwa wananchi,” akasema Bw Marwa.

Alisema kuwa kuna haja ya kuwa na mpangilio ambao utahusisha kila Mkenya na sio mpango wa kufaidisha wachache.

“Ugatuzi ni lazima upeane heshima kwa wananchi. Kuhudumia Wakenya kwa njia sawa ndio lengo la kila wizara hivyo basi mwananchi lazima ahusishwe,” akasema.

Kwingineko, Kamati ya Seneti inayohusika na matumizi ya fedha za umma itaanza kutathmini miradi yote inayotekelezwa na magavana katika kaunti 47.

Pia, inataka kuhakikisha magavana wanatekeleza wajibu wao na hawafuji mali ya umma.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Moses Kajwang alisema mjini Mombasa kwamba shughuli hiyo itaanza Aprili.

 

Kugatua mikutano

Akiongea kwenye mkutano wa kamati hiyo katika hoteli ya Sarova Whitesands, Bw Kajwang alisema kamati hiyo imeamua kugatua mikutano yao ili Wakenya wawe na imani na ugatuzi.

“Mara kwa mara huwa tunapata ripoti kuhusiana na miradi iliyotekelezwa na magavana bila ya kutathmini ukweli kuhusiana na miradi hiyo ya maendeleo.

Lakini sasa tumebadilisha mtindo kwani tutaenda mashinani kudadisi miradi hiyo kabla ya kupitisha ripoti hizo,” akasema Bw Kajwang ambaye pia ni seneta wa Homabay.

Hata hivyo baraza la magavana limeitaka kamati hiyo ihakikishe magavana hawadhalilishwi kama hapo awali, walipokuwa wakihojiwa na kamati hiyo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Josphat Nanok alisema magavana wataitikia mwito ili kueleza kuhusu miradi na maswala yoyote tata yatakayoibuka.

“Sioni tatizo lolote kwa magavana kuitwa ili kuweka wazi swala lolote ibuka katika serikali za ugatuzi sababu ni wajibu wetu. Lakini kuwe na maelewano ili tushirikiane si kama hapo awali ambapo kulikuwa na utata mkubwa baina ya magavana na kamati,” Bw Nanok ambaye alihudhuria kikao kingine huko Mombasa akajibu.

Bw Nanok ambaye pia ni gavana wa Turkana aliitaka kamati hiyo kuwalenga wahusika badala ya kuwakandamiza magavana.

 

Makasisi waliotimuliwa kuhusu ushoga wataka korti iadhibu kanisa

Na JOSEPH WANGUI

KANISA Anglikana la Kenya limepuuzilia mbali ombi lililowasilishwa mahakamani na makasisi watatu ambao wanataka ibainishwe lilikiuka agizo la mahakama.

Watatu hao walikuwa wamesimamishwa kazi baada ya kuhusishwa na vitendo vya ushoga.

Kupitia kwa wakili William Muthe, Wadhamini Waliosajiliwa wa Kanisa Anglikana walisema ombi la makasisi hao katika Mahakama ya Leba ya Nyeri halifai.

Makasisi hao John Gachau, James Maigua na Paul Warui, walikuwa wamewasilisha ombi hilo kutaka wadhamini hao waadhibiwe kwa kukiuka agizo lililoamrisha warudishwe kazini.

idha, kupitia kwa wakili wao, Bw Donald Onsare, walimwomba Jaji Nzioki wa Makau aagize wadhamini hao wafungwe gerezani kwa miezi sita kwa kukosa kuwalipa ridhaa ya Sh6.8 milioni.

Walisema wadhamini wa kanisa hilo wamepuuza maagizo mawili yaliyotolewa na Mahakama ya Leba mnamo Septemba 30, 2016.

“Hatua ya washtakiwa kupuuza na kutotii agizo la mahakama ni dharau kwa mahakama hii ya heshima na ni lazima tabia hiyo iadhibiwe,” akasema Bw Onsare.

Alisema kanisa halijatii maagizo hayo licha ya kuwa yaliwasilishwa, na akatoa wito hatua ichukuliwe ili kulinda hadhi na mamlaka ya mahakama.

Wakili huyo alieleza kuwa msimamo wa kanisa kutotii agizo la mahakama unaathiri makasisi hao vibaya na hivyo basi kuwazidishia matatizo ya kimawazo.

Wakijitetea, wadhamini hao walisema ombi hilo lina dosari kubwa na halina msingi kisheria.

Wakili Muthee alisema afisi ya wadhamini wa kanisa ni shirika lililosajiliwa na hivyo basi haiwezekani kulihukumu kifungo cha gerezani.

“Ombi hili halijatimiza matakwa ya Sheria za Ukiukaji wa Maagizo ya Mahakama. Jinsi lilivyonakiliwa, haliwezi kukubalika,” akasema Bw Muthee.

 

 

 

 

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Aprili 5, 2018 mbele ya Jaji Nzioki Makau katika Mahakama ya Leba ya Nyeri.

Kahawa yageuka chungu kwa wakuzaji

Na MWANGI MUIRURI na IRENE MUGO

WAKULIMA wa kahawa katika eneo la Mlima Kenya sasa wameamua kuacha kilimo hicho kinachowapa hasara na kuwafanya maskini.

Zaidi ya viwanda 10 vimefungwa katika maeneo mengi ya Mlima Kenya kutokana na kuongezeka kwa madeni, usimamizi mbaya, bei duni ya zao la kahawa na uchuuzi wa zao hilo.

Katika eneo la Mathira, chama cha akiba na mikopo cha Mathira North Coffee Farmer’s Co-operative Society kiko katika hatua za mwisho kuporomoka.

Viwanda vyake vitatu vimeshafungwa baada ya asilimia 99 ya wakulima kujiondoa wakilalamikia malipo duni.

Mambo ni mabaya zaidi katika kaunti ya Murang’a, ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wakulima wameng’oa zao hilo kutoka ekari 750.

Wanaripotiwa kutupilia mbali kilimo hicho ili kukumbatia uwekezaji katika sekta ya ujenzi wa nyumba na pia kujiingiza katika kilimo cha mimea mingine yenye faida.

Hatua hii ni hatari kubwa kwa jitihada za Kaunti hiyo kufufua kilimo cha kahawa hadi kurejelea kilele chake cha miaka ya 1980 ambapo Kaunti hiyo ilikuwa ikizalisha asilimia 80 ya mavuno ya kahawa yote hapa nchini.

Miaka hiyo, Murang’a ilikuwa ikivuna tani 200 za kahawa na pato lake lilikuwa la kupendeza kiasi kwamba mashirika ya wakulima wa kahawa yalikuwa yakikopesha serikali pesa.

Ripoti hiyo ya afisa wa ustawishaji kilimo cha kahawa katika Kaunti, Paul Mutua akitoa ukadiriaji wa sekta hiyo katika kufunga mwaka wa kifedha wa 2016 -17, alisema kuwa bei duni, ushindani wa nafasi za ujenzi na kilimo cha mboga na matunda na pia kukosekana kwa imani ya wakulima kunahatarisha kilimo cha kahawa katika eneo zima la Mlima Kenya.

Anasema kuwa hali ikiendelea katika mtindo huo ambapo katika mwaka wa 2015 ekari 350 zilikuwa zimeng’olewa miti ya kahawa, basi kabla ya
2030 kufika, kilimo hicho kitakuwa kimefifia.

Ripoti hiyo inaangazia hatari hiyo kuwa, kabla ya mwaka 2022, kutoka idadi ya sasa ya wakulima 70,000 wanaolima kahawa, watakuwa wamepunguka hadi chini ya 40,000.

Ingawa bei ya kahawa sokoni imekuywa ilkiripotiwa kupanda kwa kasi, ile bei ambayo humfikia mkulima imesemwa kuathiri sana bidiii za wakulima kuzalisha zao hili.

Ripoti hiyo inasema kuwa licha ya kilo moja ya kahawa lkatika mnada kubakia zaidi ya Sh120, katika Kaunti ya Murang’a mkulima amekuwa akifikiwa na Sh50 mwaka wa 2012 kwa kilo moja, ikapunguka hadi Sh30 mwaka wa 2013 na kisha ikapanda tena hadi Sh42 mwaka wa 2014.

Mwaka wa 2015 bei hiyo ilipanda tena hadi Sh55, ikashuka tena hadi Sh45 mwaka wa 2016 lakini kwa sasa bei ni Sh30.

 

Vitabu vilivyopewa wanafunzi na Serikali vimejaa makosa – Walimu

Na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Walimu wasema walianza kugundua makosa mengi mara walipopewa vitabu hivyo, na sasa wamelazimika kuviweka kando
  • Tatizo hilo haliko kwa vitabu vya Kiswahili pekee bali pia katika vile vya masomo ya Kiingereza, Hesabu, Fizikia, Kemia na Bayolojia
  • KICD yalikiri kwamba kuna dosari katika baadhi ya vitabu na tayari kuna mikakati iliyowekwa kusahihisha makosa
  • Itaamuliwa baadaye kama vitabu husika vitahitaji kubadilishwa au walimu watafahamishwa kuhusu marekebisho yanayofaa kufanywa

WALIMU katika shule za umma za sekondari wameacha kutumia vitabu vilivyopewa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwezi Januari wakisema vinapotosha kutokana na makosa mengi.

Walimu waliohojiwa na Taifa Leo, ambao tumebana majina ili kuwalinda wasiadhibiwe, walisema walianza kugundua makosa mengi mara walipopewa vitabu hivyo, na sasa wamelazimika kuviweka kando. Walisema badala yake wanatumia vingine ili wasipotoshe wanafunzi wao.

Vitabu hivyo vilivyogharimu Sh7.5 bilioni vilipeanwa kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza chini ya mpango wa Elimu Bila Malipo. Usambazaji wa vitabu hivyo ulizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Januari 5 mwaka huu na kufikia sasa vimesambazwa kwa wanafunzi wa shule za umma.

 

Masomo yalioathirika

Malalamishi mengi zaidi yametoka kwa walimu wa Kiswahili ambao wanasema mojawapo ya vitabu walivyopewa kinaonekana kilichapishwa kwa haraka na kampuni moja mashuhuri ya uchapishaji nchini.

“Ni shida tupu. Tunakitumia tu kwa vile serikali ilisema tutumie lakini kina matatizo tele,” akasema mwalimu wa shule moja ya upili ya kitaifa.

Makosa yaliyopatikana katika baadhi ya vitabu vya Kiswahili ni kama vile mifano potovu ya vivumishi, nomino, vitenzi na utumizi wa vipengele ambavyo havitambuliki katika lugha. Pia walimu wanasema mpangilio wa mada pia unakanganya.

Maoni sawa na hayo yalitolewa na walimu kutoka pembe tofauti nchini ambao walisema tatizo hilo haliko kwa vitabu vya Kiswahili pekee mbali pia katika vile vya masomo ya Kiingereza, Hesabu, Fizikia, Kemia na Biolojia.

 

Kuchanganyika

Suala lingine ambalo walimu wamezua ni kuwa baadhi ya mada zimechanganyika ambapo zinazopasa kufunzwa katika vidato cha pili hadi nne vimo katika vitabu vya kidato cha kwanza.

“Matatizo mengine yaliyopo yanahusu ufinyu wa mada. Hakuna maelezo ya kina. Wachapishaji waliharakisha bila kupitia ile kazi waliyokuwa wakichapisha. Hii inaathiri wanafunzi kwa sababu wanasoma mambo ambayo hayawafai ama yanawapotosha,” akasema.

Afisa anayesimamia utafiti katika Taasisi ya Kenya ya Uundaji wa Mtaala (KICD), Bw Cyril Oyuga, alikiri kwamba taasisi hiyo imefahamu kuna dosari katika baadhi ya vitabu na tayari kuna mikakati iliyowekwa kusahihisha makosa.

Hata hivyo, alisema vitabu hivyo vilikuwa bora zaidi miongoni mwa vile vilivyotathminiwa wakati wa utoaji zabuni na makosa yaliyopatikana ni machache yasiyoweza kuathiri elimu ya wanafunzi.

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika shule ya Moi Girls, Eldoret wakionyesha vitabu walivyopewa chini ya mpango wa Serikali mapema mwaka huu. Walimu wamelalamika kuwa baadhi ya vitabu hivyo vina makosa yanayopotosha wanafunzi. Picha/Jared Nyataya

Marekebisho

“Kuna makundi ambayo tayari yameundwa kufanya utathmini kuhusu makosa hayo na wanafanya marekebisho. Hilo litatatuliwa,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kulingana naye, itaamuliwa baadaye kama vitabu husika vitahitaji kubadilishwa au walimu watafahamishwa kuhusu marekebisho yanayofaa kufanywa.

“Tunakiri kwa sasa kuna makosa machache. Kama kuna chochote cha ziada watakachoona walimu tunaomba wawasiliane nasi kisha tutazidi kuboresha vitabu hivyo,” akasema.

Mpango wa kusambaza vitabu milioni 33 shuleni ulinuiwa kufanikisha lengo la Serikali ya Jubilee ya kutoa elimu bora bila malipo kwa kila mtoto, hasa kwa watoto wanaotoka katika jamii zisizojiweza kimapato.

Huenda Mugabe akaitwa bungeni kueleza zilikoenda pesa za Almasi

Na AFP

HARARE, ZIMBABWE

Ikiwa tutalazimika kumwagiza Bw Mugabe kufika mbele yetu, lazima atufafanulie kuhusu zilikoenda fedha hizo. Lazima atwambie kuhusu hatua ya serikali kuzifukuza kampuni za kibinafsi za uchimbaji madini, ilhali zilikuwa zikiiletea nchi faida kubwa ya kifedha – Temba Mliswa

HUENDA aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, akafika Bungeni kuelezea alikopeleka zaidi ya Sh1.5 trilioni anazodaiwa kupora kupitia biashara ya Almasi.

Hilo linatokana na ripoti maalum iliyoandaliwa na kamati moja ambayo inachunguza kashfa ya biashara ya uchimbaji wa madini hayo, wakati Bw Mugabe akiwa uongozini.

Mbunge Temba Mliswa ambaye anaiongoza kamati hiyo, anadai kwamba Bw Mugabe alikuwa mhusika mkuu katika biashara hiyo haramu. Bw Mliswa alikuwa mwanachama wa chama tawala cha Zanu-PF, ila akakigura.

Biashara hiyo ilikuwa ikiendelea katika migodi ya Chiadzwa, mashariki ya taifa hilo.

Mnamo 2016, Bw Mugabe aliliambia shirika la habari nchini humo kwamba nchi hiyo ilipata chini ya Sh200 bilioni kutokana na mauzo ya almasi. Hata hiyo, wachunguzi wanadai kwamba Bw Mugabe alinufaika kwa hadi Sh1.5 trilioni, kwani ndiye pekee aliyeidhibiti.

Mkewe, Grace, pia aliwahi kuhusishwa na biashara hiyo kupitia kwa kampuni moja ya kisiri.

Aidha, Mliswa alisema kuwa licha ya umri wake mkubwa, Bw Mugabe atahojiwa kuhusu hatua kuu ya serikali kuzifurusha kampuni zilizokuwa zikichimba madini hayo kutoka migodi hiyo mnamo 2006. Baada ya kuondolewa kwa kampuni hizo, ambazo nyingi zilikuwa za kibinafsi, serikali ilianza kusimamia uchimbaji wake.

 

Ufafanuzi

“Ikiwa tutalazimika kumwagiza Bw Mugabe kufika mbele yetu, lazima atufafanulie kuhusu zilikoenda fedha hizo. Lazima atwambie kuhusu hatua ya serikali kuzifukuza kampuni za kibinafsi za uchimbaji madini, ilhali zilikuwa zikiiletea nchi faida kubwa ya kifedha,” akasema Bw Mliswa, kwenye mahojiano na mtandao wa ‘New Zimbabwe.’

“Hatukuona manufaa yoyote ya biashara hiyo, licha ya nchi kupata mabiloni ya fedha,” akasema. Mugabe alishinikizwa kuondoka uongozini mnamo Novemba 2017 na jeshi.

Licha ya hayo, ingali kubainika ikiwa kiongozi huyo mkongwe atafika mbele ya kamati hiyo.

Hiyo itakuwa kashfa ya kwanza kumkabili yeye binafsi, baada ya kashfa za hapo awali kuwakabili mawaziri wake.

Miongoni mwa wale waliofunguliwa mashtaka ya kashfa za rushwa ni mawaziri wa zamani Samuel Undenge (Kawi) na Walter Nzembi, aliyehudumu kama waziri wa Mashauri ya Kigeni.

Wanawe Bw Mugabe; Bellarmine Chatunga na Robert Junior pia ni miongoni mwa watu ambao wanalengwa na serikali ya Rais Emmanuel Mnangagwa, kwa madai ya kuipora nchi hiyo mabilioni ya fedha kupitia kandarasi ghushi walizopata kwa mlango wa nyuma.

Alipochukua mamlaka mapema mwezi Desemba mwaka uliopita, Bw Mnangagwa aliapa kufanya kila awezalo “kulainisha utawala” wan chi hiuo, kwa kuhakikisha kuwa wale wote walioipora wamekabiliwa kisheria.

 

Waititu amshtaki Ngilu kwa dai la kueneza chuki

Na RICHARD MUNGUTI 

Kwa ufupi:

  • Bw Waititu anaomba mahakama kuu imzuie Bi Ngilu kueneza chuki na kusababisha hali ya taharuki
  • Wakazi wa Kiambu walikuwa wanaomba hatua uchukuliwe dhidi ya Bi Ngilu
  • Bi Ngilu alisema marufuku hiyo ya makaa na usombaji changarawe itadumu

GAVANA wa Kiambu Bw Ferdinard Waititu jana alimshtaki Gavana Charity Kaluki Ngilu kwa matamshi ya uchochezi kuhusu biashara ya makaa.

Katika kesi hiyo dhidi ya Bi Ngilu, Bw Waititu alisema kumekuwa na uhasama mkali baina ya wakazi wa kaunti hizi mbili

Bw Waititu anaomba mahakama kuu imzuie Bi Ngilu kueneza chuki na kusababisha hali ya taharuki kati ya wakazi wa kaunti ya Kitui na wafanyabiashara wa makaa.

Gavana huyu amesema uhusiano kati ya kaunti za Kiambu na Kitui umedorora.

“Naomba hii mahakama imzuie Bi Ngilu kutoa matamshi ambayo yanaweza kuibua hisia za chuki na uchochezi baina ya wakazi wa kaunti hizi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishirikiana na kufanya biashara mbalimbali,” alisema Bw Waititu katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu jana.

Gavana huyu wa Kiambu amesema mnano Feburuari 2018 Bi Ngilu alitoa matamshi kwamba uchomaji makaa umepigwa marufu.

Bw Waititu alisema kuwa tangu matamshi hayo yatolewe kumekuwa na kisa ambapo lori la kusafirisha bidhaa liliteketezwa katika kaunti ya Kitui.

Kutokana na visa hivyo vya uteketezaji magari ya kusafirisha makaa, wakazi wa Kiambu waliandamana na kusababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Nairobi- Busia.

Wakati wa kisa hicho magurudumu ya magari ya watu yalitolewa pumzi na kuzua hali ya taharuki. Kwa muda wa jumla ya saa nane, hali ilikuwa si hali kwenye barabara hiyo.

Wakazi wa Kiambu walikuwa wanaomba hatua uchukuliwe dhidi ya Bi Ngilu.

Kufuatia matamshi hayo Bi Ngilu aliagizwa afike mbele ya tume ya kitaifa ya utangamano na uuwiano kuandikisha taarifa kuhusu matamshi hayo.

 

Marufuku haitajadiliwa

Ijumaa baada ya ushindi wa Bi Ngilu wa Agosti 8 2017 kuthibitishwa na Mahakama kuu ya Milimani Nairobi, akiwahutubia wafuasi wake na wakazi wa Kitui waliofika kufuata uamuzi , gavana huyu alisema , “marufuku ya uchomaji makaa hayatajadiliwa tena. Hakuna kuchoma makaa na hakuna kupitisha makaa katika kaunti ya Kitui.”

Bi Ngilu alisema marufuku hiyo ya makaa na usombaji changarawe itadumu.

“Kaunti ya Kitui imegeuzwa kuwa jangwa. Miti asili yote imekatwa na kuchomwa makaa na wafanyabiashara kutoka kaunti nyingine. Marufuku haya yatadumu,” alisema Bi Ngilu huku akishangiliwa.

Bw Waititu anaomba mahakama iratibishe kesi aliyomshtakiwa Bi Ngilu kuwa ya dharura.

Bingwa wa Olimpiki Ruth Jebet adaiwa kutumia pufya

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Ruth Jebet, ambaye alibadili uraia na kuwa Mbahraini mnamo Februari mwaka 2013, anakabiliwa na tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli kupata ufanisi mashindanoni.

Bingwa huyu wa Olimpiki mwaka 2016 wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji anashikilia rekodi ya dunia ya mbio hizi ya dakika 8:52.78 aliyoweka katika Riadha za Diamond League nchini Ufaransa mnamo Agosti 27 mwaka 2016.

Gazeti la Guardian nchini Uingereza linasema ripoti kadhaa zinadai kwamba Jebet, 21, amepatikana na kosa la kutumia dawa za aina ya EPO alizotumia bingwa wa marathon kwenye Olimpiki za mwaka 2016, Mkenya Jemimah Sumgong, ambaye sasa anatumikia marufuku ya miaka mine.

“Ingawa habari hizi hazijathibitishwa, duru kadhaa zimedai Jebet amefeli vipimo vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli za aina ya EPO,” gazeti hilo liliripoti Machi 4, 2018.

Ikithibitishwa ni mhalifu wa dawa hizo haramu, atakuwa mzawa wa Kenya aliye na jina kubwa kuwahi kufeli vipimo hivyo.

Mzawa wa Kenya ambaye amewahi kupatikana na hatia ya kutumia uhalifu wa dawa za kusisimua misuli kupata ufanisi ni Abraham Kiprotich.

Mfaransa huyu alipigwa marufuku mwaka 2013 miaka miwili baada ya kupatikana alitumia dawa za kusisimua misuli za EPO kushinda mbio za Istanbul Marathon nchini Uturuki mwaka huo. Alipokonywa taji hilo.

Kiprotich aliruhusiwa kurejea mashindanoni baada ya kukamilisha marufuku yake. Alinyakua taji la Lagos Marathon nchini Nigeria mwezi Februari mwaka 2018 na kujishindia zawadi ya Sh5,065,500.

NYOTA YAKO: MACHI 5, 2018

Na Sheikh Khabib

KONDOO
Machi 21 – Aprili 20: Epuka ubishi wowote leo ili moyo wake uridhike. Utakubana na mambo mengi ya kukukuudhi, hata hivyo unakumbushwa kwamba leo sio siku ya mzaha kamwe. Jitulize na ulale mapema na usifungue mlango wa nyumba yako usiku.

 

NG’OMBE
Aprili 21 – Mei 20: Usiende uwanjani wakati huu kwani naona mambo yasiyokuridhisha huko. Shughulikia sana mambo ya biashara na familia.Utafurahia jasho lako la muda mrefu wakati huu. Ongeza juhudi maradufu.

 

MAPACHA
Mei 21 – Juni 21: Chunga marafiki wasikupotoshe. Naona wakikujia uwasaidie lakini nia yao ni kuchunguza mienendo yako. Usibadilishe msimamo wako uwafurahishe. Songa mbele na mipango yako.

 

KAA
Juni 22 – Julai 22: Naona umepuuza ushauri fulani unaohusu maisha yako na matokeo yamekuwa mambo kukwendea kombo. Jirudie ufanye linalotakikana ujiepushe na hali hii. Ukifanya hivi mambo yatanyooka yenyewe.

 

SIMBA
Julai 23 – Agosti 22: Usifanye mambo usiku uepuke hatari inayokujia.Usifanye mambo kwa ujanja. Kumbuka wema hulipwa kwa wema na upandacho ndicho uvunacho. Ukifuata ushauri huu utanufaika maishani.

 

MASHUKE
Agosti 23 – Septemba 23: Watu wamekuzoea sana kwa sababu umekuwa ukitoa siri zako kwa kila mtu. Ingawa hutaki kusikia hivi, unajiweka hatarini. Dhibiti maneno ya kinywa chako.Ukifanya hivi utapata amani na watu watakuheshimu, chaguo ni lako.

 

MIZANI
Septemba 24 – Oktoba 23: Utapokea habari za kusikitisha hivi karibuni. Ajabu ni kwamba zitakuwa mwanzo wa mambo mema. Usishangae kamwe na mambo ya dunia. Baada ya matukio haya maisha yatakwendea unavyotaka watu wakose kuamini.

 

NGE
Oktoba 24 – Novemba 22: Usitarajie mtu wa karibu nawe akusaidie, tafuta msaada kwa watu msio na uhusiano wa kifamilia kamwe. Hata hivyo usiwachukie wanaokutenga ukiwa na shida kwa sababu sio kupenda kwao, utawahitaji kesho.

 

MSHALE
Novemba 23 – Desemba 21: Unatumia nguvu nyingi katika kazi isiyo na mapato kwa sababu umeisomea. Marafiki zako wanavuna pesa nyingi wakifanya kazi ambazo sio taaluma zao. Itakubidi ubadilishe kauli ikiwa unataka kufaulu maishani.

 

MBUZI
Desemba 22 – Januari 20: Wacha kumfikiria asiyekufikira. Wazuri hawajazaliwa. Toka ukakutane na anayekufaa maishani. Usimdharau, anayekutaka mbali kuwa mwangalifu kabla ya kuanzisha uhusiano mpya wa kimapenzi kwa sasa.

 

NDOO
Januari 21 – Februari 19:
Umejiamini kupita kiasi na hii imekunyima mambo mengi mazuri. Namwona mwalimu wako wa zamani akikujia kukushauri. Hivi ni kuonyesha kwamba kujiamini kwako kumevuka mipaka. Kumbuka mganga hajigangi.

 

SAMAKI
Februari 20 – Machi 20: Una mali nyingi isiyo yako kwa sababu umeikopa. Hautapata amani hadi ulipie mali hiyo yote. Kwa sasa naona unashtukashtuka kwa sababu hujui waliokukopesha watachukua hatua gani. Heri ni kwamba nyota yako inakulinda dhidi ya wadeni wako.

Utulivu warejea Burkina Faso baada ya shambulio la kigaidi

Ouagadougou, Burkina Faso

SHUGHULI za kibiashara zilirejea katika soko kuu la jiji kuu la Burkina Faso, Ouagadougou Jumamosi siku moja baada ya magaidi wa Kiislamu kushambulia Ubalozi wa Ufaransa na makao makuu ya kijeshi ambapo watu wanane waliuawa na wengine 80 wakajeruhiwa.

Kundi linaloshirikiana na mtandao wa Al Qaeda la The Group to Support Islam and Muslims (GSIM) lilikiri lilitekeleza shambulio hilo ambalo waziri mkuu alilitaja kama la watu waoga.

GSIM ilisema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi mauaji ya baadhi ya viongozi wake na jeshi la Ufaransa wiki mbili zilizopita Kaskazini mwa Mali. Uchunguzi unaendelea kuhusu shambulio hilo.

Watu walirejea katika barabara za jiji hilo. Wanajeshi waliwaua magaidi wanane na watu kadhaa walikamatwa. Harufu ya moshi ilitanda katika jiji hilo Jumamosi.

Shimo kubwa kwenye uwanja wa makao hayo na alama kwenye ukuta zilidhihisha jinsi magaidi waliovalia sare walilipua bomu kwenye gari wakilenga chumba ambacho maafisa wakuu wa jeshi walipaswa kukutana lakini wakaamua kukutana eneo tofauti kulingana na maelezo ya waziri wa usalama Clemement Sawangongo.

Chumba hicho kiliharibiwa kabisa na vipande vya magari kutapakaa kote ndani ya makao makuu ya jeshi. Sawadogo alisema kuwa iwapo mkutano usingefanyika katika chumba tofauti, jeshi lisingesalia na wakubwa. Mwanajeshi mstaafu Amado Belem aliambia shirika la habari la Associated Press kwamba hakufurahishwa na shambulio hilo.

“Inashtusha kuona jeshi likishambuliwa rahisi hivi”, alisema.

 

Mara ya tatu

Hii ilikuwa mara ya tatu ya magaidi wa Kiislamu kushambulia jiji hilo tangu Januari 2016 na kufanya jeshi kulaumiwa. Kufikia Jumamosi hakuna kundi lililojitokeza kudai lilitekeleza shambulio hilo.

Watu walijazana karibu na makao makuu ya jeshi na Ubalozi wa Ufaranza kutazama uharibifu huo. Mabaki ya gari lililochomeka yalikuwa nje ya Ubalozi huo uliojaa mashimo ya risasi ukutani.

Ubalozi huo ulishambuliwa saa nne na robo Ijumaa huku watu waliokuwa ofisi jirani za kituo cha runinga cha serikali wakisema washambuliaji walifika wakibebwa na lori mdogo wakiimba Allahu Akbar na kuanza kufyatua risasi.

Hakuna aliyejeruhiwa katika Ubalozi huo lakini mlinzi mmoja na washambuliaji wanne waliuawa, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema kwenye ujumbe uliopeperushwa kupitia runinga.

Wakazi walisema wanahofia usalama wao kufuatia shambulio hilo. “Hali ni mbaya sana. Unaona, tulidhani ni vitoa machozi vilivyokuwa vikilipuliwa kutoka ubalozi wa Ufaranza lakini ilikuwa ni risasi halisi zilizoua watu.

Watu walikimbia hadi ofisi ya waziri mkuu. Ilikuwa hivi siku nzima ,” alisema Sylvain Some, anayefanya kazi kwenye kibanda karibu na Ubalozi huo. GSM limekuwa likitekeleza mashambulio mali.

SHANGAZI AKUJIBU: Mume wangu bado anafuatafuata mke wa zamani

Kwako shangazi. Nimeolewa na mwanamume ambaye alikuwa amezaa na mwanamke mwingine kabla hajanioa. Sasa nimegundua bado anamfuata mwanamke huyo. Tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Iwapo unayosema ni kweli, inaonekana wawili hao wamefufua uhusiano wao ama hata hawakuachana licha ya mwanamume huyo kukuoa. Ni muhimu ujue msimamo wa mume wako kuhusu suala hilo ndipo uchukue hatua unayohisi inafaa.

 

Aliyenipa mimba kahepa, nasumbuka

Vipi shangazi? Kuna mwanamume aliyenipa mimba kisha akanihepa na kuoa mwanamke mwingine. Sasa wazazi wananilaumu na wananifukuza nyumbani sijui nitaenda wapi. Kuna wengi wanaotamani kunioa. Nishauri.
Kupitia SMS

Ni kweli ulikosea, sio tu wazazi wako, bali wewe mwenyewe, kwa kuzaa kabla hujaolewa ingawa pia si vyema kwao kukufukuza nyumbani. Kama kuna wanaume wanaotaka kukuoa, chagua mmoja wao akuoe kwani baba ya mtoto wako tayari ana mke na hutarajii kuwa atakurudia.

 

Nashindwa kuacha tajiri huyu aliyeoa
Nina umri wa miaka 20 na nina uhusiano na mwanaume wa miaka 33 ambaye ameoa na wana watoto wawili. Nimejaribu kuachana naye lakini nimeshindwa kwa kuwa nampenda sana. Ameniwekea biashara na anataka kunioa mke wa pili lakini naogopa. Nishauri.
Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, ni dhahiri kuwa umekwama kwa mwanamume huyo na itakuwa vigumu kujitoa. Sasa huna budi ila kuendelea kuwa mpango wake wa kando ama ukubali kuolewa mke wa pili. Utaamua mwenyewe.

 

Nataka kutengana na mume mbanifu
Nimekuwa na mpenzi kwa miaka sita sasa lakini nahisi hanifai. Sababu ni kuwa tangu tujuane hajawahi kuninunulia chochote bila kumuitisha, hata pesa za matumizi ni lazima nimuombe. Nimejaribu kumrekebisha lakini nimeshindwa. Nishauri.
Kupitia SMS

Inawezekana kuwa mwanaume huyo hajui jinsi ya kujenga na kutunza uhusiano ama ni mkono gamu tu. Uhusiano ni chaguo la mtu binafsi kwa hivyo kama unahisi huyo siye mtu ambaye ungependa kuishi naye unaweza kujiondoa katika uhusiano huo.

 

Mchumba hataki nimlipie mahari
Hujambo shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamke fulani ambaye ana mtoto kwa miaka mitano sasa. Niko tayari kupeleka mahari kwa wazazi wake lakini amekataa. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Hizo ni dalili kwamba mwanamke huyo hajaamua kwamba wewe ndiye utakuwa mume wake. Anajua vyema kuwa kupeleka mahari ni kuhalalisha ndoa na ndiyo maana amekataa. Kama unamtaka mke inaonekana haitawezekana.

 

Jamaa ninayempenda ni mkali kama chui
Hujambo shangazi. Nimepandana na kijana fulani lakini tatizo ni kuwa ni mkali sana hata namuogopa. Sasa sijui itakuwaje akinioa. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Kama tayari anakuonyesha ukali hata unamuogopa ilhali nyinyi bado ni wapenzi, nahisi kutakuwa na shida utakapokuwa mke wake. Itabidi uchukue hatua inayofaa kabla hamjaenda mbali.

 

Natamani mpenzi ila naogopa wanaume
Vipi Shangazi? Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20. Natamani sana kuwa na mpenzi lakini huwa naogopa kuzungumza na wanaume. Nimejaribu kuondoa uoga huo nimeshindwa. Nishauri.
Kupitia SMS

Hiyo ni hali inayotokana na maumbile na watu wameumbwa kwa namna tofauti. Hata hivyo, maumbile hubadilika jinsi mtu anavyokuwa. Jaribu uwezavyo kutangamana na wanaume na hatimaye woga wa kuzungumza nao utakutoka.

 

Nina hamu kubwa ya kuwa na mume
Shangazi shikamoo. mimi ni msichana mwenye umri wa miaka na 23 sina mpenzi. Natamani sana kuwa na kwangu. Nishauri.
Kupitia SMS

Mapenzi hayanunuliwi dukani kama nguo mwanangu. Ni lazima kwanza mwanamume akuone, akupende, nawe pia umpende ndipo muwe wapenzi. Utaratibu huo unaweza kuchukua muda mrefu na itabidi uwe na subira. Isitoshe, wewe bado ni mchanga na huna haja ya kuwa na wasiwasi.

 

Wanasiasa wa South Rift sasa wamtetea Koros

Na VALENTINE OBARA

MATATIZO yanayokumba Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) yamechukua mkondo wa kikabila baada ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la South Rift kujitokeza kumtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo, Bi Lily Koros.

Wakiongozwa na Gavana wa Kericho, Prof Paul Chepkwony, viongozi hao jana walikosoa hatua ya Waziri wa Afya, Bi Sicily Kariuki, kumpa Bi Koros likizo ya lazima baada ya mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa kimakosa hospitalini humo wiki iliyopita.

“Baada ya kushauriana tumebaini kama viongozi wa Kaunti ya Kericho kwamba kuna juhudi zinazoendelezwa na watu fulani iwe wako serikalini, katika siasa au makundi ya watu binafsi wanaolenga kuondoa watu wa jamii moja mamlakani na kuweka watu ambao wanawapendelea,” akasema kwenye kikao cha wanahabari Nairobi.

Bi Koros aliagizwa kuenda likizo ya lazima pamoja na naibu wake, Dkt Bernard Githae, Ijumaa ili kutoa nafasi uchunguzi ufanywe kuhusu kisa hicho cha Jumatatu iliyopita.

Visa vingine vilivyofanya hospitali hiyo igonge vichwa vya habari mwaka huu ni wizi wa mtoto na madai ya ubakaji wa kina mama waliojifungua.

Prof Chepkwony alisema madai ya ubakaji yalibainika kuwa ya uongo huku wizi wa mtoto ukitatuliwa na mshukiwa kufikishwa mahakamani na hivyo basi akahisi kuna nia fiche kuhusu uamuzi wa kumwadhibu Bi Koros.

“Haieleweki jinsi anahusishwa na masuala ya upasuaji. Kuna wataalamu waliofunzwa wenye ufahamu kuhusu mambo haya na ambao wanafaa kuwajibika moja kwa moja,” akasema Chepkwony.

Mnamo Jumamosi, wabunge kutoka Kaunti ya Kericho wakiongozwa na Seneta Aron Cheruiyot, walidai kuna njama ya kumsimamisha kazi Bi Koros kwa sababu ana misimamo mikali ya kuzuia ufujaji wa pesa za umma katika hospitali hiyo.

Kulingana naye, KNH ni miongoni mwa taasisi za serikali ambazo zinatarajiwa kutengewa kiasi kikubwa cha pesa ili kufanikisha malengo ya serikali ya Jubilee kuhusu utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.

Hata hivyo, hatua ya viongozi wa kisiasa kujitokeza kutetea watu wa makabila yao wanaojikuta katika hali kama hii hata kabla uchunguzi kukamilika si jambo geni humu nchini.

Wavulana na wasichana wa Iterio wembe mkali maigizoni

Na ANTHONY NJAGI

SHULE za Iterio Girls na Iterio Boys zilisisimua katika mashindano ya Kaunti ya Kisii ya Uigizaji kwa shule za sekondari yaliyoandaliwa katika Chuo cha Walimu cha Nyabururu.

Wavulana wa Iterio Boys waliibuka simba katika michezo ya kuigiza wakifuatwa na Nyakoiba nao Mobamba wakamaliza katika nafasi ya tatu.

Verah Orare wa Shule ya Upili ya Masongo akariri shairi ‘Red rage” akiongozwa na Dkt George Aroba katika mashindano ya Maigizo Kisii Machi 1, 2018. Picha/ Anthony Njagi.

Iterio Boys walisisimua hadhira kwa mchezo wao uliofahamika kama “Pandemonium” ambao uliwasilisha ujumbe kuhusu ubinafsi unavyotatiza juhudi za kuleta umoja wa kitaifa.

Mwandishi wa mchezo huo, Franklin Nyambane alielezea matumaini yake kuwa mchezo huo utafika hadi mashindano ya kitaifa yatakayoandaliwa Nairobi.

Shule ya Upili ya Kerongorori yacheza densi ya kitamaduni katika mashindano ya maigizo kaunti ya Kisii Machi 1, 2018. Picha/ Anthony Njagi.

Nao wanadada wa Iterio waliibuka washindi katika kitengo cha Densi ya Kisasa na kufuatwa na Masongo Secondary huku Nyatieko wakimaliza katika nafasi ya tatu.

Katika ukariri wa shairi la mtu mmoja, Nyamonaria walichukua nafasi ya kwanza wakifuatwa na Cardinal Otunga na Masongo mtawalia.

Kuhusu shairi la makundi, Kisii School waliwika wakifuatwa na Mobamba Secondary huku Kioge Girls wakimaliza wa tatu.

Celestine Nyakania na Naomi Osoro wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Nduru wasimulia hadithi katika mashindano ya maigizo yaliyofanyika kaunti ya Kisii Machi 1, 2018. Picha/ Anthony njagi.

Katika Densi ya Kitamaduni, Sengera Girls walipepea mbele ya Babaracho na Ogorera.

Shule ya Mobamba Secondary nayo ilinyakua ushindi katika hadithi ikifuatwa na Gesabakwa katika nafasi ya pili huku Kisii School ikimaliza katika nafasi ya tatu.

Bogeka Secondary nao waliibuka washindi katika sarakasi wakifuatwa na Mobamba katika nafasi ya pili mbele ya Magena Girls.

 

Shirika lafichua miradi inayopendekezwa na wakazi hupuuzwa

Na OSCAR KAKAI

RIPOTI ya shirika lisilo la serikali katika kaunti ya Pokot Magharibi inaonyesha kuwa vyama vya kisiasa katika serikali iliyopita vilikuwa vikibadilisha miradi ambayo ilikuwa imependekezwa na kupewa kipaumbele na wakazi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wawakilishi wa wadi katika bunge la kaunti hiyo walikuwa wakibadilisha miradi kulingana mirengo yao ya kisiasa ili kujinufaisha.

Akiongea katika mkutano wa mwaka wa Speaking Pokot Accountability Network, katibu wa shirika hilo Bw Francis Soprin, alisema kuwa serikali  iliyopita ilikuwa ikishirikisha wakazi kupendekeza miradi za kupewa kipaumbele  na baada ya wao kutoa mapendekezo miradi hiyo ilikuwa ikibadilishwa.

“Watu wachache walikuwa wakishirikishwa kuchagua miradi ambayo inawafaa lakini baada ya mchakato huo  wawakilishi wa kaunti walikuwa wakibadilisha ili iwiane  na matakwa yao ya kisiasa.

Bw Soprin alisema kuwa hali hii imewapa changamoto kushinikiza serikali ya kaunti ya sasa kuunda  mswada wa kushirikisha umma ili kuhakikisha mapendekezo ya miradi  yanatekelezwa.

“Mswada huo utasaidia wakazi kuhusishwa kikamilifu kupendekeza miradi ambayo wanaipa kipaumbele ili itekelezwe,” alisema.

 

Mafunzo

Katibu huyo alisema kuwa wametoa mafunzo kwa mtu mmoja katika kila wadi kwenye  wadi zote ishirini za kaunti hiyo ili kuwa wachunguzi wa  kijamii wanaopiga msasa na kuchunguza miradi ambayo inatekelezwa na serikali za kaunti na kitaifa.

“Wakenya wanalipa ushuru ili kufadhili miradi hiyo. Tunataka kuwa na watu mashinani ambao wanafuatilia na kuchunguza ikiwa matakwa yao yanatimizwa,” akasema.

Alidai kuwa shirika lake limepokea vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi, wakati wa kufuatilia miradi baada ya kupata ripoti kutoka kwa wachunguzi wa kijamii.

Bw Soprin alipongeza serikali ya sasa ya kaunti hiyo kwa kutoa  ufadhili wa wanafunzi  kwa usawa.

Bi Salome Chepkemei  afisa wa shirika hilo alizitaka serikali za kaunti na kitaifa kuhakikisha kuwa asilimia 30  ya zabuni zinapeanwa na akina mama na vijana kulingana na katiba.

“Serikali hizi mbaili zinafaa kuhakikisha kuwa kuna uwazi wakati wakutekeleza miradi zao.

 

MAKALA MAALUM: Reli ya Nanyuki-Nairobi kufufua uchumi wa eneo la Mlima Kenya

NA JOSEPH WANGUI

“Reli hiyo itapunguza unyanyasaji wa wakulima wadogo na kufanya mazao yao ya shambani kufika sokoni kwa haraka. Viwanda ambavyo vilifungwa kama kiwanda cha kahawa cha Kenya Planters Coffee Union (KPCU) vitapata nafasi ya kurejelea biashara. Miji kama ya Sagana na Karatina itakuwa mikubwa kupanuka kiuchumi,”
asema mkulima wa mchele na mfanyabiashara kutoka kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi wa Kanga’ra.

MPANGO ya magavana wanane wa eneo la Mlima Kenya kufufua reli ya kutoka Nanyuki hadi Nairobi umeibua matumaini mengi miongoni mwa wakazi, ikiwa ni pamoja na ukuaji wa kiuchumi na uboreshaji wa biashara.

Jumuiya ya wanabiashara na viwanda imesifia mpango huo na kueleza kwamba hatua hiyo itaunda nafasi za ajira na kufungua nafasi za biashara hadi katika nchi jirani ya Ethiopia.

Kiongozi wa jumuiya ya wanabiashara wa kaunti ya Laikipia, Bw Francis Gitonga, alisema mradi huu utabadilisha mji wa Nanyuki na kuufanya ‘bandari ya nchi kavu’.

Hata hivyo, ameomba magavana hao kuimarisha reli hiyo na kuifanya ya kisasa (Standard Gauge) wala si tu kuifufua kwa kuirekebisha.
Anasema wanabiashara pamoja na wakulima ndio wamelengwa kunufaika na mradi huo zaidi.

“Pia reli hiyo itaokoa fedha za serikali kwa ajili ya kutengeneza barabara na kuvutia wawekezaji kuelekea maeneo mengine ya ndani ya nchi si tu Nairobi pekee. Muda na gharama ya usafiri ni sababu za kuzingatia katika biashara yoyote”, anasema Bw Gitonga.

Amewaomba magavana kuboresha reli hiyo kwa kusaka ujuzi kutoka nchi zilizoendelea kama Uchina, Marekani na Uingereza.

“Sekta za utalii na ujenzi zitafaidika pakubwa kutokana na mradi huo ukikamilika. Serikali ya taifa inapaswa pia kuunga mkono wazo la magavana hao na pia kuzipa serikali za kaunti fedha zaidi,” anasema Bw Gitonga.

Serikali za kaunti ya Nairobi, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Laikipia, Nyandarua na Isiolo mwaka jana zilikubaliana kutenga Sh25 bilioni ili kufufua njia hiyo ya reli yenye urefu wa kilomita 240 kutoka Nairobi hadi Nanyuki. Kisha baadaye wanapania kuiendeleza hadi Isiolo.

Kaunti hizo zilianza kwa kuchanga Sh100 milioni kila mmoja na kuelekeza fedha hizo kwenye mradi huo.

Waziri wa Biashara na Uwekezaji katika Kaunti ya Nyeri Bi Diana Kendi asema mipango bado inaendelea huku akithibitisha kwamba serikali hizo zishaanza kuchanga hela husika.

Mkulima wa mchele na mfanyabiashara kutoka kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi wa Kanga’ra amefurahia wazo hilo la magavana na kusema kuzinduliwa kwa usafiri wa reli kutaleta manufaa kwa jamii ya Mlima Kenya.

Bw Kang’ara asema kuwa reli hiyo itapunguza unyanyasaji wa wakulima wadogo na kufanya mazao yao ya shambani kufika sokoni kwa haraka.

 

Viwanda kufufuka

“Viwanda ambavyo vilifungwa kama kiwanda cha kahawa cha Kenya Planters Coffee Union (KPCU) vitapata nafasi ya kurejelea biashara. Miji kama ya Sagana na Karatina itakuwa mikubwa kupanuka kiuchumi,” anasema Bw Kang’ara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maji ya Tana Athi

Anaongeza kuwa sekta za kilimo kama chai, kahawa, macadamia na kilimo cha mboga huenda zikanufaika kwa njia kubwa kwa kuwa mazao ya kilimo kwa sasa husafirishwa kwa kutumia malori.

“Usafirishaji bidhaa kwa reli utatufaa sana. Tutakuwa na watu wanaofanya kazi Nairobi na kuishi vijijini kwa sababu gharama na muda wa kusafiri utapungua,”anasema Bw Kang’ara.

Simon Wachira akivuna kahawa katika shamba lake eneo la Kiamwathi, kaunti ya Nyeri Agosti 28, 2017. Picha/Maktaba

Anatazamia zaidi kwamba kutakuwa na nafasi za ajira katika maeneo ya stesheni za abiria za reli na kuwa vijana watapata kazi za upakiaji wa bidhaa za kusafirishwa.

Hata hivyo, mkulima wa chai na mfugaji wa ng’ombe wa maziwa eneo la Othaya Kaunti ya Nyeri anakosoa serikali hizo za Kaunti.

Bw Easu Kioni anasema mradi huo haustahili kupewa kipaumbele katika mipango ya Magavana.

Alisema mradi huo una athari ndogo za kiuchumi na kwa maisha ya wakazi wa eneo hilo la Mlima Kenya.

Anasema Magavana hao wanane wanapaswa kulainisha utendakazi wao na kuipa kipaumbele miradi ya barabara za vijijini katika wilaya zao.

Pia anawahimiza kushawishi serikali kuu kuharakisha ujenzi wa barabara kuu ya Thika-Nanyuki-Isiolo au kufadhili ujenzi huo kwa kutumia zile Sh25 bilioni wanazopangia kuchanga.

 

Taarifa muhimu

“Wakazi na umma hawakuhusishwa kabla ya magavana kutangaza mradi huo. Wananchi wanatakiwa kuwa na taarifa kuhusu ni bidhaa gani itakuwa ikibebwa kutoka eneo hili kwa kutumia njia ya reli ambayo haiwezi kubebwa kwa kutumia barabara zilizopo,” anasema Bwana Kioni.

Bw Kioni ambaye pia alikuwa mshauri wa usalama wa Rais mstaafu Mwai Kibaki, alisisitiza kuwa mradi huo hauna umuhimu kwa sasa.

Anasema kwamba kutumika kwa reli ya Nanyuki ambayo ilijengwa na serikali ya ukoloni mwaka wa 1913 kulipunguka hatua kwa hatua tangu miaka ya 1990 baada ya wakazi kukubali usafiri wa barabara.

Anasema kulikuwa na malalamishi kwamba kusafiri kwa gari la moshi kulichukua muda mrefu. Baadaye sehemu kadhaa za reli hiyo zilianza kuharibiwa na kuporwa.

Magavana wanapanga kuzindua reli ya Nanyuki na kuiunganisha na ukanda wa Lamu Port-South Sudan-Ethiopia Transport (LAPSSET).

Bw Kioni anashauri Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui na Francis Kimemia wa Nyandarua kwamba badala ya kushughulika na reli hiyo ya Nanyuki, washawishi ujenzi wa barabara ya kilomita 52 inayounganisha kaunti hizo tatu kupitia hifadhi ya Wanyamapori ya Aberdare.

“Barabara ya Aberdare itakuwa na ufanisi mkubwa wa kiuchumi kwa wakazi wa kaunti hizo tatu kuliko reli. Pia itapunguza muda na umbali wa kusafiri kutoka Nyeri hadi Kinangop na Nakuru”, anasema Mr Bw Kioni.

Seneta wa zamani wa kaunti ya Nyeri Bw Mutahi Kagwe, kwa upande wake, anakumbatia wazo la magavana hao lakini anatilia shaka uwezo wa serikali za kaunti kupata fedha za kujenga reli.

 

Hazina uwezo

“Serikali za kaunti kivyao hazina uwezo wa kukopa hela nje ya nchi na haziwezi kujenga reli. Njia ya reli ya Nairobi-Isiolo si gharama kidogo kama inavyodhaniwa. Kaunti husika ziko sehemu ambayo ina milima na ukweli ni kwamba wakazi wanataka reli ya kusafiri kwa haraka wala si ile ya zamani,” anasema Bwana Kagwe.

“Hebu tuwe wakweli, reli ya kisasa ya kiwango cha Mombasa-Nairobi inayojulikana kama SGR ilitumia Sh325 bilioni. Je, unadhani serikali ndogo zina uwezo huo?”auliza Bw Kagwe.

Anahimiza kuwa serikali za kaunti husika zihimize serikali kuu izindue reli ya Nanyuki lakini wasielekeze fedha wanazopata kwa mradi huo.

“Njia ya reli ya Nairobi-Isiolo itakuwa ya manufaa sana ikiwa itafanywa ya kisasa. Ukarabati tu ni jambo la muda mfupi na kupoteza muda na raslimali.Inapaswa kuwa mradi mpya,” anasema Bw Kagwe.

Aliongeza kwamba serikali hizo za kaunti hazistahili kuachilia huduma nyingine na kuelekeza fedha katika mradi huo.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Tetu Mwangi Gichuhi anasema Wabunge wa eneo la Mlima Kenya walikubaliana kuanzisha kundi la kushughulikia mambo ya kiuchumi ya jamii ya Mlima Kenya na kufanya kazi pamoja na magavana.

Wabunge hao walifanya uamuzi huo baada ya mkutano katika hoteli moja mjini Thika.

“Tulikubaliana kwamba tunapaswa kudai haki yetu kama eneo la kati la taifa. Tunafuatilia miradi mingine kama ujenzi wa mabwawa, barabara pamoja na umoja wetu kama jamii,”  alisema Bw Gichuhi.