Maraga arukwa katika uteuzi wa Jaji Nyachae

Bw Charles Nyachae aliyeteuliwa jaji kuwakilisha Kenya katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ). Picha/ Maktaba

Na WALTER MENYA

Kwa ufupi:

  • Idara ya Mahakama ilikuwa imempendekeza Jaji Hannah Okwengu katika cheo hicho
  • Taifa Jumapili imepata barua kati ya Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki na idara hiyo, ambapo Jaji Mkuu David Maraga alimpendelea Bi Okwengu
  • Bw Nyachae alimfanyia kampeni Rais Kenyatta na Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kisii, kwenye chaguzi za Agosti 8 na Oktoba 26

SERIKALI Kuu ilipindua pendekezo la Jaji Mkuu Jaji Maraga, kuhusu jaji aliyefaa kuwakilisha Kenya katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), imefichuka.

Imebainika Idara ya Mahakama ilikuwa imempendekeza Jaji Hannah Okwengu katika cheo hicho, lakini badala yake jina la Bw Charles Nyachae, aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta ndilo likatumwa.

Hata hivyo, serikali ilipuuzilia mbali pendekezo la idara hiyo na badala yake kumteua Bw Nyachae.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Tume ya Utekelezaji Katiba (CIC) aliapishwa rasmi mnamo Ijumaa, jijini Kampala, Uganda ambapo alichukua nafasi ya Jaji Isaac Lenaola.

Kipindi cha kuhudumu cha Bw Lenaola kitaisha mnamo Julai 1.

Aidha, Taifa Jumapili imepata barua kati ya Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki na idara hiyo, ambapo Jaji Mkuu David Maraga alimpendelea Bi Okwengu.

“Jaji David Maraga, aliye pia Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Kenya amependekeza Jaji Okwengu kuwa kuhudumu katika mahakama ya EACJ,” akasema Bi Anne Amandi, ambaye ni Msajili wa Idara ya Mahakama, iliyoandikwa mnamo Februari 14.

Barua ya Bi Amadi ilikuwa majibu ya barua ya Wizara hiyo mnamo Desemba 22, 2017 ikiiomba Idara ya Mahakama kumpendekeza mtu atakayeteuliwa kuhudumu katika mahakama hiyo. Barua ya wizara ilitiwa saini na Dkt Alice Yalla, kwa niaba ya Katibu wa Wizara.

 

Amsaidia Rais kwa kampeni

Bw Nyachae alimfanyia kampeni Rais Kenyatta na Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kisii, kwenye chaguzi za Agosti 8 na Oktoba 26.
Mbali na hayo, aliwania useneta katika kaunti hiyo kwa tiketi ya JP.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili nchini (LSK) anayeondoka, Bw Isaac Okero, alisema: “Mwafaka wa Muungano wa Afrika Mashariki (EAC) ni mojawapo ya sheria zetu.

Unasema kwamba kuna utaratibu unaopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa majaji katika EACJ. Kulingana na taratibu zilizopo, mtu huyo anapaswa kupendekezwa kwa rais na Tume ya Huduma za Mahakama, hilo likimaanisha kuwa lazima mchakato wa uteuzi uwe wenye uwazi.”

Naye mwenyekiti wa zamani wa LSK, Bw Eric Mutua, anasema kuwa, hatua hiyo ni ishara ya wazi kwamba Idara ya Mahakama imenyang’anywa mamlaka yake.

Mdahalo ikiwa Raila atagusa kombe la Dunia watawala mitandao

Na ELVIS ONDIEKI na VALENTINE OBARA

MJADALA umeibuka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kama Kinara wa NASA, Bw Raila Odinga, ataruhusiwa kugusa Kombe la Dunia wakati litakapotua nchini kesho.

Wakati kombe hilo lilipoletwa nchini mwaka wa 2013, Bw Odinga, ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu, alikatazwa kuligusa kwa sababu ni marais wa taifa pekee ambao huruhusiwa kufanya hivyo. Wakati huo, rais alikuwa ni Bw Mwai Kibaki.

Hata hivyo, mwaka huu Bw Odinga alijiapisha kuwa ‘rais wa wananchi’ ilhali Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi kwenye uchaguzi wa urais uliofanywa mwaka uliopita.

“Ni rais mmoja pekee anayeruhusiwa kuligusa. Itakuwa ni Uhuru au Baba Raila?” akasema mtumizi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, aliyejitambua kama Elijah.

Kombe hilo litatua Kenya kwa mara ya tatu kesho, baada ya kuletwa mwaka wa 2010 na 2013 kabla mchuano wa kuushindania kufanywa Urusi kuanzia Juni 14 hadi Julai 15.

Kombe hilo la kilo sita lililotengenezwa kwa dhahabu na lenye urefu wa sentimita 36 litaletwa nchini kwa udhamini wa kampuni ya Coca Cola.

Wiper: Kalonzo sasa hataapishwa

Na KITAVI MUTUA

VIONGOZI wa chama cha Wiper wameondolea mbali uwezekano wa kinara mwenza wa NASA Kalonzo Musyoka kuapishwa kuwa Naibu wa Rais wa Wananchi.

Wakiongozwa na seneta wa zamani Johnstone Muthama na aliyekuwa waziri Titus Mbathi, viongozi hao walimshauri Bw Musyoka kwamba kuapishwa kwake hakutakuwa na faida yoyote kwake, kisiasa.

Badala yake wamemtaka kuelekeza nguvu na rasilimali kuimarisha chama cha Wiper ili kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

“Mbona uapishwe ilhali hautapewa mamlaka yoyote ambayo yataleta faida kwa wafuasi wako baada ya halfa hiyo,” Mbw Mbathi akamwambia Bw Musyoka mbele yake katika mkutano wa viongozi wa Ukambani katika mkahawa wa Stoni Athi Resort, kaunti ya Machakos.

Alilalamika kuwa Bw Musyoka ametusiwa hadharani na wafuasi wa ODM kwa kutohudhuria halfa ya kuapishwa kwa Raila Odinga ihali hakuna faida yoyote iliyotokana na shughuli hiyo.

Kauli sawa hiyo ilitolewa na Bw Muthama, akisema yeye pia aliamua kutohudhuria hafla hiyo ilhali alikuwa mwanachama wa kamati andalizi ya shughuli hiyo.
Alisema yeye pia alikwepa hafla hiyo ili kulinda masilahi ya chama cha Wiper.

 

BI TAIFA FEBRUARI 22, 2018

MERCY Njoki, 21, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Uraibu wake ni kusakata densi, kusikiliza muziki na kuendesha baiskeli. Picha/ Anthony Omuya

Gor kumenyana na mahasidi wa Tunisia Klabu Bingwa Afrika

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 16 wa Kenya, Gor Mahia, watafufua uhasama wao dhidi ya mabingwa mara 27 wa Tunisia, Esperance de Tunis hapo Machi 6, 2018 kwenye raundi ya kwanza (32-bora) ya Klabu Bingwa Afrika.

Gor walibandua nje Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kulazimisha sare ya 1-1 ugenini. Vijana wa kocha Dylan Kerr walishinda mechi ya mkondo wa kwanza 2-0 zaidi ya wiki moja iliyopita.

Esperance walijikatia tiketi ya kumenyana na Gor baada ya kulipua Concorde ya Mauritania kwa jumla ya mabao 6-1. Walitoka sare 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kuwika 5-0 Jumatano.

Gor na Esperance wamewahi kukutana katika mashindano haya ya kifahari mara nne katika Klabu Bingwa.

Gor waliibuka mabingwa wa Afrika mwaka 1987 kwa mabao ya ugenini baada ya kukaba Esperance 2-2 nchini Tunisia na kupata sare ya 1-1 nchini Kenya katika fainali.

Mwaka 2014, Gor walipepetwa 3-2 nchini Kenya kabla ya kunyeshewa mabao 5-0 katika mechi ya marudiano nchini Tunisia. Mechi hizi mbili zilikuwa za raundi ya kwanza.

Droo ya mechi za raundi ya 16-bora za Klabu Bingwa (2018):

Saint George (Ethiopia) vs. KCCA (Uganda)

Wydad Athletic Club (Morocco) vs. Williamsville AC (Ivory Coast)

Aduana (Ghana) vs. ES Setif (Algeria)

Al Ahly (Misri) vs. Mounana (Gabon)

MFM (Nigeria) vs. MC Alger (Algeria)

Horoya (Guinea) vs. Generation Foot (Senegal)

Young Africans (Tanzania) vs. Township Rollers (Botswana)

Gor Mahia (Kenya) vs. Esperance (Tunisia)

Etoile du Sahel (Tunisia) vs. Plateau United (Nigeria)

AS Togo (Togo) vs. El Hilal (Sudan)

Zesco (Zambia) vs. ASEC Mimosas (Ivory Coast)

TP Mazembe (DR Congo) vs. UD Songo (Msumbiji)

Difaa Hassan (Morocco) vs. AS Vita (DR Congo)

Primeiro de Agosto (Angola) vs. Bidvest (Afrika Kusini)

Rayon Sports (Rwanda) vs. Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

Armed Forces (Gambia)/Zanaco (Zambia) vs. Mbabane Swallows (Swaziland)

Chipukizi wa raga kupigania ubingwa wa Afrika Julai

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za raga za wachezaji saba kila upande za chipukizi za Kenya zitawania ubingwa wa Afrika katika mashindano ya African Youth Games mnamo Julai 18-28, 2018.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Raga la Afrika (Rugby Africa), Kenya ni miongoni mwa mataifa 22 yaliyojiandikisha kushiriki makala haya ya tatu.

“Nashukuru kamati za kitaifa za Olimpiki za Afrika (ANOCA) kwa usaidizi wao wa katika usajili wa timu zitakazoshiriki mashindano ya chipukizi mwezi Julai. Ni kwa sababu yao tumeweza kupata ithibati kutoka kwa mataifa 22,” amesema Rais wa Rugby Africa, Abdelaziz Bougja. Mashindano haya yatahusisha wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18.

Kenya ilizoa jumla ya medali 25 (saba za dhahabu, 11 za fedha na saba za shaba) katika makala ya mwaka 2014. Kutoka idadi hiyo ya medali, Kenya ilijishindia fedha katika raga ya wachezaji saba kila upande ya wavulana. Kenya ilizabwa 60-0 na Afrika Kusini katika fainali jijini Gaborone nchini Botswana.

Orodha ya mataifa yatakayoshiriki:

Timu za wavulana

Kenya, Algeria, Benin, Burkina Faso, Burundi, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ivory Coast, Madagascar, Mauritius, Morocco, Namibia, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tunisia, Zambia na Zimbabwe.

Timu za wasichana

Kenya, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Madagascar, Morocco na Tunisia.

Kipsang’ alenga tena kuvunja rekodi ya dunia kwenye Tokyo Marathon

Mshindi wa NewYork City Marathon mwaka 2014, Wilson Kipsang’ akisherehekea. Picha/ Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kukosa rekodi ya dunia ya saa 2:02:57 kwa dakika moja na sekunde moja mwaka 2017, Wilson Kipsang’ ataivizia rekodi hiyo tena kwenye Tokyo Marathon hapo Februari 26, 2018.

Mkimbiaji huyu Mkenya, ambaye atafikisha umri wa miaka 36 mwezi ujao Machi 15, aliwahi kushikilia rekodi ya dunia ya mbio hizi za kilomita 42 mwaka 2013 aliposhinda Berlin Marathon nchini Ujerumani kwa saa 2:03:23.

Rekodi yake ilivunjwa na Mkenya mwenzake Dennis Kimetto katika Berlin Marathon mwaka 2014.

Hakuna mtu amefanikiwa kuvunja rekodi ya Kimetto. Hata hivyo, tangu mwaka 2016, rekodi ya Kimetto imekuwa hatarini. Karibu ifutwe katika Berlin Marathon mwaka 2016 Muethiopia Kenenisa Bekele na Kipsang’ walipomaliza umbali huo kwa saa 2:03:03 na 2:03:13, mtawalia.

Pia bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge alikosa rekodi hiyo pembamba katika mbio za London Marathon mwaka 2016 aliponyakua taji kwa saa 2:03:05. Kipchoge alitwaa ubingwa wa Berlin Marathon kwa saa 2:03:32.

 

Wapinzani wakuu

Baadhi ya wapinzani wakuu wa Kipsang’ katika makala haya ya 12 ni mabingwa wa Tokyo Marathon mwaka 2014 Dickson Chumba (Kenya) na mwaka 2016 Feyisa Lilesa (Ethiopia).

Wakenya wengine wanaoshiriki makala haya ni Vincent Kipruto, Amos Kipruto, Gideon Kipketer na Bernard Kipyego. Mahasimu wa jadi wa Kenya, Ethiopia, pia wanawakilishwa na wakimbiaji Tesfaye Abera na Tsegaye Mekonnen.

Bingwa wa Tokyo Marathon mwaka 2016, Helah Kiprop ataongoza kampeni ya kinadada kutoka Kenya. Atashirikiana na Purity Rionoripo, ambaye alishinda Paris Marathon nchini Ufaransa mwaka 2017.

Tishio kubwa ni kutoka kwa Waethiopia Shure Demise, Ruti Aga, bingwa wa mwaka 2015 Birhane Dibaba, na Meseret Defar, ambaye atashiriki marathon kwa mara ya kwanza kabisa.  Kiprop ameonya wapinzani wake watarajie vita vikali vya kuwania taji.

KAPI yataka teknolojia itumike kuzima biashara ya dawa feki

Mhudumu wa duka la dawa akitia tembe za dawa kwa chupa. KAPI imeonya kuwa huenda baadhi ya dawa zinazosafirishwa nchini zikawa feki. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

Chama cha Wauzaji Dawa nhini (KAPI) kimeitaka Bodi ya Dawa na Sumu nchini (KPPB) kuanza kutumia teknolojia ya dijitali kukomesha biashara ya dawa ghushi nchini.

Katika taarifa, KAPI ilisema bodi hiyo inahitaji kufuata meli za shehena zenye kubeba dawa ili kutambulisha bidhaa ghushi na kuzizuaia kuingia nchini Kenya.

“Bidhaa ambazo hazijaidhinishwa katika soko la humu nchini ni hatari zaidi kwa sababu huenda zilihifadhiwa vibaya ndani ya meli,” alisema mwenyekiti wa KAPI Bi Anastasia Nyalita katika taarifa hiyo.

Kulingana naye, bidhaa hizo bandia hubandikwa majina kwa lugha zingine ambazo ni vigumu kwa Wakenya kuelewa, kama vile Kituruki, Kiarabu na Kijerumani.

Chama hicho kilipongeza KPPB kwa kuchukua hatua kabambe kumaliza wauzaji wa dawa bandia nchini.

Mawakili maarufu wateuliwa kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani

Wakili maarufu Bw Otiende Amollo. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

MAWAKILI maarufu Otiende Amollo na Judy Thongori, ni miongoni mwa wapatanishi 180 waliosajiliwa na mahakama katika juhudi za kupunguza mrundiko wa kesi za kibiashara na kifamilia nchini.

Bw Omollo ambaye ni mbunge wa Rarieda, alisimamia ofisi ya kupokea malalamishi ya umma ilipoanzishwa chini ya katiba mpya, naye Bi Thongori ni mtetezi shupavu wa haki za wanawake.

Wapatanishi hao huteuliwa baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na kamati ya mahakama ya upatanishi inayosimamiwa na Jaji Alnashir Visram wa Mahakama ya Rufaa.

Kwenye taarifa, kamati hiyo ilisema kufikia Januari 18 mwaka huu, ilikuwa imefaulu kuwasajili wapatanishi 180 kote nchini.

“Wapatanishi huchaguliwa kutoka wanaotuma maombi na kutimiza masharti yaliyowekwa na kamati. Mfumo wa kuwasajili huwa wa wazi na unaendelea,” ilisema taarifa ya kamati.

Kulingana na taarifa hiyo, kuna wapatanishi 99 wa kesi za kibiashara na 81 wa kushughulikia kesi za kifamilia. Baadhi ya mawakili ambao wamesajiliwa ni Maria Goreti Nyariki na Kyalo Mbobu.

Alipozindua mfumo huo mwaka jana, Jaji Mkuu David Maraga aliwakosoa mawakili kwa kutoukumbatia kikamilifu.

 

Kuathiri mapato

Alisema mawakili wanahisi kwamba mfumo huo ambao umefaulu kutatua kesi katika mahakama ya kusikiliza mizozo ya kibiashara na kifamilia utaathiri mapato yao.

“Mawakili ni kizingiti katika mfumo huu muhimu. Wanahisi kwamba mapato yao yatapungua iwapo mfumo huu utafaulu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba una manufaa makubwa kwao kwani unapunguza muda na gharama ya kesi, kusaidia katika utafutaji wa haki na kujenga jamii yenye amani,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza kwamba katika upatanishi, pande zote huwa washindi.

Tangu mfumo huo uanze kutumiwa, kesi katika mahakama ya kutatua mizozo ya kibiashara zimepungua kwa asilimia 50. Muda wa kusikiliza kesi pia ulipungua kwa siku 50.

Kupitia mfumo huo, mahakama imetatua kesi 25 na kuokoa zaidi ya Sh500 milioni kufikia mwaka jana.

Jaji Visram alisema wapatanishi huidhinishwa baada ya kukaguliwa na kuhojiwa vikali na kuna zaidi ya 400 waliotuma maombi na yanashughulikiwa.

Shughuli mahakamani zasitishwa kupisha uchaguzi wa mawakili

Mawakili wakipiga foleni kumchagua rais wao Februari 22, 2018 katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

SHUGHULI katika mahakama za Nairobi zilisimamishwa Alhamisi na uchaguzi wa mawakili uliofanyika kote nchini.

Katika mahakama ya Milimani Nairobi kesi nyingi ziliahirishwa kwa vile mawakili walikongamana katika maegesho ya Mahakama ya Juu na Mahakama Kuu kuwachagua viongozi wao.

Nyadhifa zilizowaniWa ni kadhaa lakini ule wa urais wa chama cha mawakili nchini LSK ulizua utata mkali kwa vile wakili Nelson Havi aliwasilisha kesi akiomba jina lake lichapishwe katika makaratasi ya kura.

Vibanda vya kupigia kura viliwekwa katika maegesho ya Mahakama ya Juu na Mahakama Kuu.

Milolongo mirefu ya mawakili ilishuhudiwa katika mahakama hizi mbili.

“Leo ni kama tuko na sikukuu. Hatuendi kortini kuwatetea wateja wetu. Tunatekeleza majukumu yetu kuwachagua viongozi,” Wakili Bernard Koyyoko aliambia Taifa Leo katika Mahakama ya Milimani.

Kesi nyingi katika korti za mahakimu na majaji ziliahirishwa kuwezesha mawakili kushiriki katika zoezi lao.

Wadhifa wa urais unawaniwa na mawakilI Aggrey Mwamu na Allan Gichuhi.

 

Mawakili 9,009

Mawakili wapatao 9,009 walishiriki katika zoezi hilo la kuwachagua wawakilishi wao katika kamati mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya kusikiza mawakili wasio na nidhamu.

Mabw Mwamu na Gichuhi wanang’ang’ania kuona atakayemrithi rais wa sasa Isaac Okero.

Katika kesi ambayo Bw Havi aliwasilisha alikuwa akiomba mahakama ishurutishe LSK kuweka jina lake katika makaratasi ya kura. LSK ilipinga kesi hiyo ikisema hajahitimu.

Jaji John Mativo alisikiza kesi hiyo na kuitupilia mbali akisema hajatimiza miaka 15 inayotakiwa kwa mmoja kufaulu kuwania urais wa LSK.

Akitupilia mbali kesi ya Bw Havi, Jaji Mativo alisema LSK hakikukosea kilipokataa kuchapisha jina la Bw Havi kwenye makaratasi ya kura.

Serikali ya Kenya ilihadaa mahakama – Miguna Miguna

Bw Miguna Miguna alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado Februari 6, 2018. Picha/ KANYIRI WAHITO
Bw Miguna Miguna alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado Februari 6, 2018. Picha/ KANYIRI WAHITO

Na BENSON MATHEKA

WAKILI Miguna Miguna, sasa anadai kwamba serikali ya Kenya ilidanganya mahakama kuhusu paspoti yake iliyotwaliwa kabla ya kufurushwa Kenya.

Bw Miguna alisema serikali kupitia idara ya uhamiaji, haikutii agizo la mahakama la kuwasilisha paspoti hiyo kortini mbali ilichofanya ni kuwasilisha paspoti feki.

Mnamo Jumatano, mkurugenzi wa uhamiaji, Bw Gordon Kihalangwa, kupitia kampuni ya mawakili ya Ngatia and Associates, aliwasilisha paspoti ya Kenya ya Bw Miguna alivyoagizwa na Jaji Luka Kimaru wiki tatu zilizopita ikiwa imeharibiwa.

Bw Kihalangwa alisema ni kawaida ya paspoti kuharibiwa watu wanazozimiliki wakitimuliwa nchini na kwamba kufurushwa kwa wakili huyo kulikuwa halali.

Hata hivyo, Bw Miguna alisema Bw Kihalangwa alikaidi agizo la Jaji Kimaru la kuwasilisha paspoti yake halali katika muda wa siku saba baada ya agizo kutolewa.

“Washtakiwa hawakutii agizo la Jaji Kimaru. Agizo la Mahakama linaeleza wazi kwamba washtakiwa ni lazima wawasilishe paspoti kwa msajili wa Mahakama Kuu katika muda wa siku saba,” alisema Bw Miguna.

Aliendelea: “Hii inamaanisha kuwa kurudishwa kwa paspoti halali, inayotumika ilivyokuwa walipoitwaa kwa nguvu na kinyume cha sheria kutoka kwangu.”

Kulingana na Bw Miguna, washtakiwa hawakuagizwa kuwasilisha mahakamani paspoti tofauti na walichompokonya.

 

Kukaidi agizo

“Kile ambacho serikali hii haramu imefanya ni kuwasilisha paspoti iliyoharibiwa kwa kukaidi agizo la korti,” alisema.

Alisema Bw Kihalangwa alidanganya mahakama kwamba aliasi uraia wake Kenya 1986 ikidai mwaka huo alikuwa katika chuo cha Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) kilichoko Gilgil.

“Kihalangwa sasa anadai kwamba nilipoteza uraia wangu 1986. Kutoka Februari hadi Agosti nilikuwa chuo cha NYS, Gilgil. Kutoka Septemba hadi Desemba 1986 nilikuwa mwanafunzi @uonbi, chuo kikuu cha Nairobi) Kenya,” alisema.

Alisema kuanzia Machi 2 , ataanza ziara ulimwenguni itakayong’oa nanga  Washington, Amerika katika kampeni aliyoitaja kama “vita vikuu vya ukombozi.”

Gor yafuzu kwa raundi ya pili CAF

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Gor Mahia imefuzu kwa raundi ya pili ya kufuzu kwa mchuano wa ubingwa wa bara Afrika, CAF.

 Mabingwa hao wa ligi ya KPL walifuzu kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kuagana sare ya 1-1 na Klabu ya Leones Vegetarianos ya Equitoria Guinea. Mkondo wa kwanza ulishuhudia Gor wakiwabamiza mabao 2-0 uwanjani Machakos.

Kwenye mchuano huo  wenyeji walichukua uongozi  katika dakika sitini na walihitaji kuongeza bao moja tu ili mchuano huo uamuliwe kwa penalty lakini hilo halikutimia.

K’ogalo walizidisha mashambulizi na kupata bao dakika za majeruhi baada ya kona uliochanjwa vizuri na Francis Kahata kujazwa wavuni na mchezaji wa Klabu hiyo.

Matokeo hayo sasa yanaiweka Gor katika ulazima wa kukutana na mabingwa wa ligi nchini Tunisia,Esperance. Mechi ya mkondo wa kwanza utachezwa hapa nchini.

Esperance waliwafunga Gor jumla ya mabao 8-2 kwenye  mikondo yote miwili mwaka wa 2014 walipokutana kwenye kipute hicho.

Gor kuvaana na Kariobangi huku Ingwe ikikabiliana na Ulinzi

NA CECIL ODONGO

 Ligi kuu ya KPL inarejelewa wikendi hii klabu za Gor Mahia  na AFC leopards zikishuka dimbani baada ya kushiriki mechi  za CAF, huku mashabiki wakiisubiri kwa hamu kuu.

Japo ligi hiyo inaingia kwenye raundi ya nne, Gor watakuwa wanacheza mechi yao ya tatu huku AFC leopards wakicheza mchuano wao wa pili.

Gor walifuzu kushiriki hatua ya pili ya kipute cha kuwania ubingwa wa Afrika baada ya kuwatandika Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-1.

 AFC kwa upande wao waliondolewa kwenye kombe la Mashirikisho barani Afrika na Klabu ya Fosa Juniours kutoka kisiwa cha Madagascar kutokana na sheria ya CAF ya bao la ugenini.

Wana Ingwe walifungana 1-1 na timu hiyo uwanjani Bukhungu kisha wakatoka sare tasa kwenye mechi ya marudio.

Kwenye michuano ya ligi K’ogalo watakipiga dhidi ya kikosi cha Kariobangi Sharks uwanjani Machakos nao AFC wavaane na mabingwa wa zamani Ulinzi Stars uwanja wa manispaa waThika.

Kwenye msimamao wa ligi Gor wapo kwenye nafasi ya pili baada ya kushinda mechi zao mbili. Waliwachabanga Zoo Kericho 4-2 na Nakumatt FC 4-0.

Leopards wamecheza mechi moja tu dhidi ya Rangers walikotoka sare ya 1-1.

Mechi za KPL hata  hivyo zitaanza kugaragazwa Ijumaa hii kwa pambano kati ya vijana wa Francis Kimanzi Mathare united na Sofapaka yake Kocha Sam Ssimbwa.

Mathare United walikitia kibindsoni taji la KPL mara ya mwisho mwaka wa 2008 nao Ulinzi wakibeba ubingwa mwaka wa 2010.

Red Cross yaomba msaada wa Sh1 bilioni kukabili njaa nchini

Na BERNARDINE MUTANU

Mabadiliko ya hali ya anga yameonekana nchini kwa muda ambapo kila mwaka wananchi wameonekana kuhitaji chakula.

Hivi sasa, wananchi kufikia milioni 3.4 wanahitaji msaada wa chakula katika kaunti kame nchini. Kati yake, wananchi 1.4 milioni wanahitaji msaada huo kwa dharura.

Shirika la Msalaba Mwekundu Februari 22, 2018 limezindua ombi jipya la ufadhili kutoka kwa wananchi.

Ili kuweza kukabiliana na hali hiyo katika Kaunti za Garissa, Wajir, Isiolo, Tana River, Kajiado na Kilifi, shirika hilo linahitaji ufadhili wa Sh1 bilioni.

Kaunti zingine ambazo zinafuatiliwa kwa karibu ni Mandera, Marsabit, Kitui na Taita Taveta.

Habari zaidi kufuata…

BI TAIFA FEBRUARI 21, 2018

ROSE Williams, 22, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Anaenzi kutazama filamu, kusafiri maeneo mapya na kuogelea. Picha/ Anthony Omuya

Kenya kupokea mkopo mwingine wa Eurobond wa Sh200 bilioni

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI imetangaza kuwa imefanikiwa kupata mkopo mpya wa Sh203 bilioni wa Eurobond.

Waziri wa Fedha Henry Rotich alisema fedha hizo zitatumiwa katika miradi ya ujenzi wa miundomsingi na kulipa madeni mengineyo.

“Tutaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundomsingi na miradi mingineyo ya maendeleo,” akasema Waziri Rotich kupitia taarifa yake kwa wanahabari.

Rais Uhuru Kenyatta alisema mafanikio ya mkopo huo ni ishara kuwa wawekezaji wa kimataifa wana imani na uchumi wa Kenya.

Mkopo wa Eurobond mnamo 2016, uliibua mjadala mkali kuhusiana na matumizi yake huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akidai kuwa fedha hizo ziliibwa na baadhi ya maafisa wakuu serikalini.

Mnamo Mei 2016, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Keriako Tobiko alisema kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuonyesha kuwa fedha hizo ziliporwa.

Afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko kufikia sasa imeshindwa kutegua kitendawili kuhusiana na fedha hizo.

Madeni ya vipodozi yamaliza ndoa yake

Na TOBBIE WEKESA

SHANZU, MOMBASA

Kioja kilizuka eneo hili baada ya polo kumtimua mkewe alipogundua kwamba alikuwa na madeni mengi ya vipodozi.

Kulingana na mdokezi, wawili hao walikuwa wamemaliza miezi miwili katika ndoa.

Walipokuwa wakichumbiana, polo alikuwa akishangazwa na vipodozi na mavazi ya bei ghali aliyokuwa akivalia mrembo.

Polo alianza kushuku mwanadada alikuwa na sponsa wa nguvu sana. Yasemekana mambo yalimuendea kombo kipusa baada ya wenye madeni kuanza kumdai.

Penyenye zinasema demu alikuwa amewakopa pesa karibu marafiki wake wote alizokuwa akitumia kununua vipodozi na mavazi.

Baadhi ya waliomdai walienda hadi kwa mumewe kumdai. Inadaiwa kipusa alikuwa amewaelekeza baadhi yao kwake huku akifikiri polo angemlipia madeni hayo.

Kulingana mdokezi, kipusa aliamua kumueleza polo kuhusu yaliyokuwa yakiendelea.

Baada ya kusikia kiwango cha hela alichokuwa akidaiwa, polo alimuamrisha ashike njia na kurudi kwao.

“Kazi yako ilikuwa ni kukopa pesa kutoka kwa kila mtu! Hauna aibu kuniambia. Nijiuze ndio nipate hizo pesa!” polo alimshtumu kipusa.

Polo aliamua kumtimua kipusa huku akiwaeleza waliomdai wajipange. “Mimi sikuoa madeni. Mtajipanga na yeye. Na tena simtaki kwangu. Huyu ataniletea hasara,” polo alidai.

Kipusa alimuomba polo msamaha lakini wapi. “Nimesema rudi kwenu. Wewe utanipora. Hata pengine umeshaenda benki na kuchukua mkopo kwa jina langu. Kwenda kabisa,” polo alimtimua kipusa.

Wenye madeni walikuwa pale wakitazama akitimuliwa na mumewe.

Mapambano ya kurithi Tsvangirai yaanza kutikisa chama cha MDC

Mwili wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Bw Morgan Tsvangirai watolewa kwa ndege tayari kwa mazishi yaliyofanyika Februari 21, 2018. Picha/ Mashirika

Na AFP

KIFO cha kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai, kimeibua mvutano kuhusua anayefaa kumrithi katika Chama cha Movement for Democratic Change (MDC) alichokiongoza, hali ambayo inatishia kugawanya chama hicho.

Mzozo huo wa mamlaka ulishuhudiwa hata kabla ya Tsvangirai kuzikwa Jumanne, wakati naibu rais wa chama hicho, Bw Thokozani Khupe, alipozomwa wakati wa mazishi, kwa mujibu wa afisa wa chama, Bw Douglas Mwonzora.

Zimbabwe imepanga kufanya uchaguzi mkuu mwezi Julai na Rais Emmerson Mnangagwa, anayeongoza chama tawala cha ZANU-PF aliahidi uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika kwa heshima ya marehemu.

Maelfu ya watu walikusanyika kumpa buriani kigogo huyo wa kisiasa ambaye ni mmoja wa viongozi wa upinzani waliothaminiwa zaidi barani Afrika.

“Tunasherehekea maisha ya shujaa,” alisema kaimu rais wa MDC, Bw Nelson Chamisa.

Tsvangirai ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa utawala wa kiimla wa aliyekuwa rais Robert Mugabe, alifariki Jumatano iliyopita akiwa na umri wa miaka 65 katika hospitali moja ya Afrika Kusini ambako alikuwa anatibiwa saratani ya utumbo.

Mwili wake ulisafirishwa hadi mazishini kwa helikopta ya kijeshi, ukiwa umeandamana na mamake, Bi Mbuya Tsvangirai.

Maelfu ya waombolezaji walivumilia mvua na kukusanyika katika boma lake lililo Buhera, kilomita 220 kusini mwa mji mkuu wa Harare. Naibu Rais wa Zimbabwe, Oppah Muchinguri, pia alihudhuria pamoja na mabalozi wa Amerika na Ulaya.

 

Kilio

Watu wengi walivaa tisheti nyekundu zenye picha ya Tsvangirai huku wakipuliza firimbi huku wengine wakilia.

Ingawa azimio la Tsvangirai kumng’atua Mugabe mamlakani kupitia kwa uchaguzi lilizimwa katika chaguzi kadhaa, alifanikiwa kushuhudia Mugabe akijiuzulu Novemba mwaka uliopita baada ya kutawala kiimla kwa miaka 37.

Mugabe na mke wake, Grace, walituma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu.

Tsvangirai alimshinda Mugabe katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa urais mwaka wa 2008 lakini kulingana na tume ya uchaguzi, hakufikisha idadi ya kura kumwezesha kutangazwa Rais.

Alikataa kushiriki marudio ya uchaguzi baada ya ghasia kutokea ambapo wafuasi wake wasiopungua 200 waliuawa.

Kiongozi wa zamani wa upinzani, Bw Arthur Mutambara, ambaye alikuwa naibu wa Tsvangirai katika serikali ya mseto, alisema Tsvangirai ndiye alikuwa rais halisi wa Zimbabwe.

“Alikamatwa akapigwa. Wanachama wa ZANU-PF pia wako hapa, wao ndio walimuua Morgan Tsvangirai,” akasema.

TAHARIRI: Ahadi ya kumaliza ufisadi itekelezwe

Katibu mpya katika Wizara ya Ugatuzi Bw Nelson Marwa. Picha/ Maktaba

AKIHOJIWA kutwaa nafasi ya Katibu katika Wizara ya Ugatuzi, Bw Nelson Marwa, ameahidi kukabiliana vikali na makundi ya wafisadi na kukomesha utumizi mbaya wa fedha za umma katika serikali za kaunti.

Akipigwa msasa na kamati ya bunge Jumatano, Bw Marwa alijitokeza kuwa mtu mwenye uadilifu na anayejali zaidi maslahi ya Wakenya.

Ingawaje amefanya kazi kwa miaka mingi serikalini, aliwashangaza wanakamati hiyo ya bunge kwa kutangaza kuwa na utajiri wa Sh25 milioni pekee, huku akisema amezingatia zaidi kusaidia jamii kama kudhamini masomo ya wanafunzi, katika maeneo mengi ambayo amehudumu kwa ngazi za utawala.

Hata hivyo, alikiri kuwa kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa pesa za umma hasa katika kipindi cha kwanza cha ugatuzi nchini, hali ambayo alisema lazima idhibitiwe.

Katika taarifa za mkaguzi mkuu wa matumizi ya fedha ambazo zimekuwa zikichunguzwa na Seneti, ni wazi kuwa baadhi ya serikali hizo za ugatuzi hazijaweza kufafanya vilivyo kuhusu pesa zilizoelekezwa kuboresha maeneo hayo ya mashinani. Idadi kubwa ya wasambazaji bidhaa na huduma pia wanalalama kukosa kulipwa na kaunti hizi.

Kwa hivyo, iwapo Bw Marwa atapata kuidhinishwa, ni matarajio ya wengi kuwa akiwa pamoja na Waziri Eugene Wamalwa wataweza kukabiliana na ufisadi na kuhakikisha kuwa Wakenya wanafurahia matunda ya ugatuzi, ambayo dhamira yake kuu, ilikuwa kusongeza huduma karibu nao na kuboresha maisha mashinani.

Tayari kuna suala kama la kaunti ya Nyeri kupendekeza kujenga lango kuu na makao yake makuu litakalogharimu Sh20 milioni, mbali na pendekezo la kujenga nyumba ya gavana itakayogharimu Sh200 milioni.

Baadhi ya masuala haya ndiyo Wakenya wanatarajia yafuatiliwe ili kuhakikisha kuwa pesa za mlipaji kodi zinalindwa na kutumika ipaswavyo.

Vile vile, Bw Marwa alitaja jana suala la mali kuwazungukia wachache tu humu nchini. Ni kweli kuwa ni wachache wanaopata biashara za mabilioni humu nchini, na Wakenya wengi wanatarajia kuwepo kwa usawa ili kuhakikisha kuwa kila pembe ya nchi inafaidika na kujiimarisha kwa njia moja ama nyingine.

Mawaziri wapya walioapishwa pia wameahidi kukabiliana na donda sugu la ufisadi, na kwa sasa Wakenya wanatazama kuhakikisha kuwa wanatimiza ahadi zao kwao.

 

Wajakazi waandamana wakitaka watambuliwe kama sekta rasmi

Na LUCY KILALO

WAFANYAKAZI wa Nyumbani Jumatano waliandamana wakitaka kutambuliwa kama sekta rasmi humu nchini na kuthaminiwa.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Nyumbani, Hoteli, Taasisi za Elimu na Hospitali (KUDHEIHA), Bw Albert Njeru, walisema kuwa wajakazi wa nyumbani hawaheshimiwi, na baadhi ya watu wanawalipa kwa kuwatupia nguo kuu kuu.

“Wakati umefika tutambuliwe, tulipwe mshahara kama mfanyakazi yeyote mwingine, wakati umefika tupewe likizo ya siku 21 kama wafanyakazi wengine, tutambuliwe kama wafanyakazi, tupate bima ya matibabu (NHIF), Malipo ya Uzeeni (NSSF), tunataka kulindwa na sheria ya Kenya na pia kimataifa.

Mfanyakazi wa nyumbani lazima awe kama wale wengine wako kwa ofisi,” alisema Bw Njeru.

Wafanyakazi wa nyumbani waandamana nje ya majengo ya Bunge la Kitaifa jijini Nairobi Februari 21, 2018 wakitaka watambuliwe kama wafanyakazi wa ofisini. Picha/ Lucy Kilalo

Wafanyakazi hao katika Barua yao kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Jumatano walisema kuwa wanataka kuona Mkataba wa Shirika la Leba la Kimataifa (ILO) Nambari 189 kuhusiana na kazi yenye heshima kwa wafanyakazi wa nyumbani ikiratibiwa humu nchini.

Mbunge wa Emuhaya, Omboko Milemba, ambaye ni katibu wa chama cha Kuppet, na mbunge Maalum Godfrey Osotsi, walipokea barua hiyo kwa wafanyakazi hao waliokuwa wameandamana nje ya majengo ya bunge.

Bw Milemba alisema kuwa watahakikisha bunge linapitisha mkataba huo akitaja wafanyakazi hao muhimu kwa jamii.

 

Geti ya Sh20 milioni ni kosa la uchapishaji, gavana sasa ajitetea

Nyeri county government headquaters in Nyeri town on February 20, 2018. The county has proposed to spend Sh20 million to contruct a new gate. BY GRACE GITAU

Na GRACE GITAU

GAVANA wa Nyeri, Bw Mutahi Kahiga, amejitetea kuwa pendekezo la kujenga lango kuu la makao makuu ya kaunti yake kwa Sh20 milioni, lilikuwa ni kasoro ya uchapishaji.

Alisema hayo huku wakazi wakilalamika pakubwa kufuatia ufichuzi huo Jumatano.

Hata hivyo, alitetea mpango wa kujenga nyumba rasmi ya gavana kwa Sh200 milioni na kusema itatumiwa pia kwa ujenzi wa nyumba ya naibu gavana.

“Ujenzi wa geti ulikamilishwa na hakuna ukarabati wowote utakaofanywa kwake. Kile kilichokuwa kwenye ripoti ya maandalizi ya bajeti kilikuwa ni kasoro ya uchapishaji,” akasema.

Geti iliyopo kwa sasa ilijengwa miaka miwili iliyopita na utawala wa aliyekuwa gavana, Bw Nderitu Gachagua.

Huku akialika wananchi kutoa maoni yao kuhusu mipango ya matumizi ya fedha Ijumaa, gavana huyo aliahidi kuhakikisha kuwa fedha za umma zitatumiwa inavyofaa.

Bw Amos Muchiri, ambaye ni mkazi wa Nyeri mjini alisema Sh20 milioni ni pesa nyingi ambazo zinaweza kusaidia kuweka lami kwa kilomita mbili ya barabara au hata kukamilisha ujenzi wa soko la Nyeri.

“Sidhani kaunti hii inahitaji ukarabati wa geti kwani ile iliyopo haina tatizo lolote. Ingawa hilo lilikuwa ni pendekezo tu na kutakuwa na uchanganuzi wa kina kabla bajeti ipitishwe, ni pendekezo lisilo na umuhimu wowote,” akasema.

Mbali na kuibua hasira katika kaunti, pendekezo la kujenga geti kwa Sh20 milioni liliibua msisimko pia kwenye mitandao ya kijamii.

 

Ilani yatolewa kwa Wakenya walioko Sudan Kusini

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Bi Monica Juma. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI Jumatano  ilitoa ilani ya usafiri kwa Wakenya wanaoishi Sudan Kusini, hali inayoweza kusababisha mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Ilani hiyo iliyotolewa kupitia kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Biashara za Kimataifa, ililenga zaidi Wakenya wanaoishi katika maeneo ya Upper Nile nchini humo, hasa majimbo ya Bieh, Latjoor, Akobo, Jonglei, Liech Kaskazini na sehemu za majimbo ya Maiwut, Nile Mashariki, Boma na Yei River.

Hatua hii si ya kawaida ikizingatiwa kuwa Kenya na Sudan Kusini ni nchi jirani zilizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na pia Kenya ni miongoni mwa nchi zilizo katika mstari wa mbele kujaribu kupatanisha pande hasimu zinazozozana nchini humo.

Ilani hiyo ilitolewa siku moja baada ya marubani wawili waliokuwa wametekwa nyara na wanamgambo Sudan Kusini kurejea nchini baada ya kuzuiliwa kwa siku 42.

Marubani Frank Njoroge na Kennedy Shamalla, waliachiliwa huru baada ya wanamgambo wa chama pinzani cha Sudan People’s Liberation Army-In Opposition (SPLA-IO) kulipwa ridhaa ya Sh11 milioni. Kulingana na wanamgambo hao, ajali ya ndege iliyofanyika mpakani ilisababisha kifo cha mwanamke mmoja na ng’ombe 11.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Bi Monica Juma, alipowalaki marubani hao alisema: “Serikali ya Kenya inakashifu hatua ya kikatili ya SPLM-IO kwa tukio ambalo lilikuwa ni ajali kwani sote tunajua ajali haina kinga.”

Eneo la Upper Nile nchini Sudan Kusini huwa na utajiri mkubwa wa mafuta. Limekumbwa na vita kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa upinzani kwa muda mrefu.

Katika ilani yake, serikali ya Kenya ilitaka wananchi wake wanaoishi Sudan Kusini au wanaopanga kwenda nchini humo waondoke katika maeneo yenye vita hasa sehemu ambapo kumekuwa na vita kwa miezi sita iliyopita.

Mbali na hayo, Wakenya wote wanaoishi nchini humo walitakiwa kujisajili katika ubalozi wa Kenya ulio Juba au kupitia barua pepe kwa anwani kembaju@gmail.com.

Wizara hiyo pia ilitoa wito kwa wananchi wake wawe wakipiga ripoti mara moja kuhusu hali za dharura zinazowakumba kupitia barua pepe kwa diaspora@mfa.go.ke au nambari ya simu +25420494992.

 

Mau Mau wadai walificha hazina ya siri kuu Mlima Kenya, wataka kukutana na Rais Kenyatta

Kutoka kushoto: Jenerali Kiambati, mwanawe Solomon Kiambati na Brigedia Kiboko. Picha/ Maktaba

Na WAIKWA MAINA

WAPIGANIAJI uhuru wa Mau Mau wanataka kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kujadili jinsi ya kuchimbua hazina wanayodai iliwekwa mafichoni katika Mlima Kenya.

Wakongwe hao wanadai hazina hiyo ni siri ya viongozi wakuu wa Mau Mau akiwemo rais wa kwanza wa Kenya, hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Walisema Mzee Kenyatta aliunga mkono azimio kwamba hazina hiyo inaweza tu kufichuliwa katika sherehe maalum ya utakaso, lakini kwa bahati mbaya aliaga dunia kabla sherehe kutekelezwa.

“Tulikuwa na agano kwamba kutafanywa sherehe ya utakaso baada ya kupata uhuru, lakini kabla ya kuondoka msituni kujiunga na familia zetu. Kiapo kiliandikwa na kufichwa katika madhabahu ya siri Mlima Kenya.

Tulihisi utakaso ulikuwa muhimu kusafisha damu iliyomwagwa wakati wa vita hivyo vya ukombozi,” akasema kiongozi wa wapiganiaji hao Brigedia John Kiboko.

 

Sherehe ya utakaso

Brigedia Kiboko anadai kuwa misukosuko inayokumba taifa inatokana na maagano ambayo hayajatimizwa, na iwapo sherehe ya utakaso haitafanywa laana hiyo itaandama taifa na vizazi vijavyo.

Anahofia hazina hiyo haitawahi kupatikana iwapo wapiganiaji walio hai hawatapewa fursa ya kuifichua.

Bi Wambui Gichakuri, ambaye alikuwa kapteni wa Mau Mau na pia msaidizi wa Jenerali Mathenge Mirugi wakati wa vita hivyo, alisema tambiko za Kikuyu zilizostahili kuandaliwa kabla yao kuungana na familia hazikufanywa.

Kila mmoja alifululizwa hadi ofisi za wilaya yake na kisha kupelekwa nyumbani.

“Tunataka kujadiliana na Rais Kenyatta kuhusu hazina hiyo, kama kiongozi wa taifa na kwa sababu babake alijua kuwepo kwake. Babake aliacha maagizo kuhusu hazina,” akasema.

Kijana aliyetoroka Al Shabaab asimulia maisha yalivyokuwa akiwa gaidi

Na MOHAMED AHMED

Kwa Muhtasari:

  • Kijana huyo amekuwa akiishi maisha ya kisiri ili maafisa wa usalama ama wafuasi wa Al Shabaab wasimtambue
  • “Nilimtembelea binamu yangu Lamu na kuishi kwake kwa miezi mitatu. Baadaye alinijulisha kwa vijana wengine watatu kisha akatupa Sh10,000 kila mmoja”
  • “Tulifika kwenye kambi iliyokuwa na vijana wapatao 200. Hapo ndipo nilipong’amua kuwa nilikuwa ndani ya kambi ya Al Shabaab nchini Somalia”
  • Mafunzo yalihusisha jinsi ya kutumia silaha tofauti kama bunduki, gurunedi miongoni mwa nyingine. Pia tulibebeshwa magunia mazito yaliyojaa mchanga
  • “Singeweza kuvumilia tena. Mwezi moja baada ya kugombana na kamanda, nilipanga na Mkenya mwingine jinsi tungehepa”

VIJANA wanaorudi nchini baada ya kuhepa Al Shabaab nchini Somalia wanajutia kwa kujiunga na kundi hilo la kigaidi.

Majuto yao yanatokana na kuwa hawawezi kuishi maisha ya kawaida kwa hofu ya kuwindwa na polisi ama kuuawa na wafuasi sugu wa kundi hilo ambalo limetatiza usalama hasa kaunti za Lamu, Wajir na Mandera.

Taifa Leo ilikutana na mmoja wa vijana hao, ambaye ni kijana wa miaka 29 katika kaunti ya Kwale aliyerudi nchini 2015.

Kijana huyo amekuwa akiishi maisha ya kisiri ili maafisa wa usalama ama wafuasi wa Al Shabaab wasimtambue. Tulipomtembelea nyumbani kwao, mwanzo alikataa kuzungumza nasi kwa kuhofia kuwa tulikwa makachero. Lakini alikubali tulipomhakikishia kuwa sisi ni wanahabari:

“Safari yangu ya kujiunga na Al Shabaab ilianza 2014. Binamu yangu alinialika Lamu kwa ahadi kuwa ningepata kazi nzuri. Alifahamu kuwa nilikuwa nafanya vibarua hapa na pale licha ya kuhitimu katika Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS). Aliniambia ningeajiriwa kazi yenye malipo mazuri.

Nilimtembelea binamu yangu Lamu na kuishi kwake kwa miezi mitatu. Baadaye alinijulisha kwa vijana wengine watatu kisha akatupa Sh10,000 kila mmoja. Alitwambia tuingie gari la kibinafsi tupelekwe mahala ambapo tungeanza kufanya kazi aliyokuwa ameahidi ambapo tungelipwa Sh40,000 kwa mwezi.

 

Mafunzo ya miaka miwili

Tulifika kwenye kambi iliyokuwa na vijana wapatao 200. Hapo ndipo nilipong’amua kuwa nilikuwa ndani ya kambi ya Al Shabaab nchini Somalia. Humo kambini tulianza kupokea mafunzo ya kijeshi ambayo yalikuwa yachukue miaka miwili. Baadaye tungetumwa uwanja wa vita kupigana.

Mafunzo yalikuwa makali sana. Tulikuwa tukiamka saa kumi alfajiri ambapo tulishiriki mafunzo na mazoezi hadi saa kumi na moja jioni.

Mafunzo yalihusisha jinsi ya kutumia silaha tofauti kama bunduki, gurunedi miongoni mwa nyingine. Pia tulibebeshwa magunia mazito yaliyojaa mchanga. Ilikuwa ni lazima ushiriki mafunzo upende usipende.

Siku moja kamanda aliniagiza ninyanyue gunia la kilo 50 la mchanga lakini nikateta. Alichomoa kisu kwa nia ya kunidunga. Nilishika kisu hicho kikanijeruhi mkono wa kushoto. Hivyo ndivyo nilivyopata jereha hili mkononi ambalo hunikumbusha masaibu niliyopitia mikononi mwa Al Shaabab.”

Majonzi yalivyokumba kijiji cha Malili, Witu kaunti ya Lamu Agosti 2017 baada ya wanakijiji kuuawa na magaidi wa Al Shabaab. Polisi wamehusisha baadhi ya vijana waliojiengua kwa kundi hilo na mashambulio yaliyofanyika Kwale. Picha/ Maktaba

Alivyohepa

“Singeweza kuvumilia tena. Mwezi mmoja baada ya kugombana na kamanda, nilipanga na Mkenya mwingine jinsi tungehepa. Ilikuwa Agosti, 2015 ambapo tulitoroka usiku na kuanza kutembea tukiwa na imani tungefika Kenya.

Tulifahamu kuwa hatua hiyo ilikuwa hatari kwani tungeweza kuuawa na wenzetu wa Al Shabaab ama maafisa wa usalama. Lakini tuliamua heri tufe tukitafuta uhuru wetu badala ya maisha ndani ya Al Shabaab.

Baada ya kutembea kwa siku mbili msituni tulipatana na mzee ambaye alitusaidia kufika Mandera. Kisha tuliingia lori lililotupeleka Garissa. Mjini Garissa tulipanda basi lililotupeleka Mombasa kisha mimi nikaja hapa nyumbani naye mwenzangu akaenda kwao Kilifi.

Watu hapa kijijini hawashuku hata kidogo kuwa nilikuwa nimejiunga na Al Shabaab. Niliingizwa katika kundi hilo bila kufahamu. Tangu niliporudi nimekuwa nikiishi maisha ya utulivu na familia yangu. Kinyume na wengine wanaorudi, mimi sitaki kujiingiza katika uhalifu.”

 

Miguna Miguna: Raila ndiye aliniambia Jubilee ilimpa Magaya Sh30 milioni

Na BENSON MATHEKA

WAKILI mbishi Miguna Miguna sasa amedai kwamba kinara wa NASA, Raila Odinga, alimweleza binafsi kwamba Afisa Mkuu wa muungano huo Norman Magaya, alipokea Sh30 milioni kutoka kwa chama cha Jubilee. 

Akihojiwa na kituo cha runinga cha TRT World jijini Toronto, Canada mnamo Jumanne usiku, Bw Miguna alikanusha madai kwamba anampiga vita Bw Odinga na viongozi wengine wa NASA.

“Ni kweli Bw Magaya alipokea Sh30 milioni kutoka kwa Jubilee ndipo aondoe kesi ya kupinga ushindi wa gavana wa Nairobi. Raila Odinga mwenyewe alinifahamisha hayo,” alidai Bw Miguna.

Wiki iliyopita, Bw Miguna alimlaumu Bw Magaya na mwanamikakati wa NASA, David Ndii, akisema wanatumiwa na Jubilee kuvuruga NASA. Alidai kwamba Bw Ndii alipinga kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa “rais wa wananchi”.

Siku iliyofuata Bw Odinga aliwatetea maafisa hao akisema wanatekeleza wajibu muhimu katika NASA na kuwataka wafuasi wa muungano huo kumpuuza Bw Miguna.

Lakini wakili huyo aliambia kipindi cha Newsmakers cha runinga ya TRT World kwamba kwa kumpuuza, Raila anahatarisha hatima yake ya kisiasa.

 

‘Huwezi kunipuuza’

“Huwezi ukampuuza Bw Miguna. Hata Raila Odinga hawezi. Vijana walio Nairobi hawatakusikiliza, vijana wa Kenya hawatakusikiliza, kwa sasa wanamwamini sana Miguna Miguna,” alisema.

Alisema serikali ya Jubilee ilimfukuza nchini kwa sababu inafahamu ushawishi wake wa kuongoza raia kudai haki.

“Jubilee wanajua kwamba sisemi jambo nisiloweza kutimiza. Nilisema nitamuapisha Bw Odinga na nikafanya hivyo mbele ya mamilioni ya watu.

Nilipowataka Wakenya kuchoma picha za Rais Kenyatta, nilikamatwa na kuzuiliwa kwa wiki moja kinyume cha sheria kabla ya kutimuliwa pia kinyume cha sheria,” alisema.

Alisisitiza kuwa atarejea Kenya mwezi ujao kuendeleza kampeni ya vuguvugu lililoharamishwa la NRM.

“Ninatarajia kurudi Kenya mwezi ujao baada ya kuzuru miji ya hapa Canada, Amerika, Uropa, Uarabuni na Afrika,” alisema Bw Miguna.

 

 

Afikishwa kortini bila viatu kwa kuiba mtoto

Bi Edinah Kerubo Mabuka alipofikishwa kortini kwa makossa ya kumwiba mtoto wa wiki tatu. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE anayeshukiwa kumwiba mtoto wa wiki tatu Jumatano alifikishwa kortini jijini Nairobi bila viatu.

Hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot aliamuru Edinah Kerubo Makuba azuiliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani kuwasaidia polisi kuwafichua wanachama wa genge linalowaiba watoto.

Afisa anayechunguza kesi hiyo aliambia korti mahojiano aliyofanya yamedhihirisha kuwa mshukiwa huyu ni mshirika wa kundi la kuwaiba watoto linaloendesha biashara jijini Nairobi na maeneo mengine.

Koplo Emmanuel Kiptoo alisema mshukiwa huyo yuko na taarifa ambazo zitasaidia polisi kuwafikia  washukiwa zaidi.

Bw Cheruiyot aliamuru Kerubo azuiliwe kwa siku tano.

Kerubo alikiri huyo ndiye alikuwa mtoto wake wa kwanza kumwiba na alikuwa anatazamia kumrudishia mama yake.

Atarudishwa kortini Jumatatu kushtakiwa.

Mtanzania anaswa JKIA akiwa na dhahabu ya Sh100 milioni

Na BERNARDINE MUTANU

SHIRIKA la Kukusanya Ushuru nchini (KRA) Jumatano limenasa dhahabu ya thamani ya Sh100 milioni katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), jijini Nairobi.

Dhahabu hiyo ilisemekana kubebwa na raia mmoja wa Tanzania na ilipatikana na maafisa wa forodhani kwa ushirikiano na maafisa wa usalama katika uwanja huo.

Dhahabu hiyo ya gramu 32,255.50 ilipatikana pamoja na hati ya malipo ya Sh100 milioni.

Mshukiwa huyo alikamatwa baada ya maafisa wa polisi kudokezewa na umma kulingana na taarifa ya KRA Jumatano.

Kulingana na shirika hilo, kusafirishwa kwa dhahabu hiyo kulikuwa kinyume cha sheria ya kusimamia forodha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dhahabu hiyo imezuiliwa na KRA, huku uchunguzi zaidi kuhusiana na suala hilo ukianzishwa.