Pasta amfurusha mke kwa kutisha kusambaratisha kanisa

Na CORNELIUS MUTISYA

NZAIKONI, MACHAKOS

PASTA wa kanisa moja eneo hili alimfurusha mkewe akidai alikuwa amechoshwa na tabia yake ya udaku. Jamaa alisema tabia ya mkewe nusura isambaratishe kanisa lake na hangemvumilia.

Kulingana na mdokezi, pasta alifungua kanisa hapa na likavutia watu wengi. Waumini walikuwa wakifurika kanisani kupata chakula halisi cha roho.

Inasemekana kwamba mkewe alipewa jukumu la kuwapa ushauri nasaha wanawake kanisani.

Hata hivyo, wanawake hao hawakuwa na imani na uongozi wake wakidai alikuwa mwenye kiburi na mjeuri kupindukia.

Yasemekana alikuwa akiwasengenya akina mama hao kokote alikoenda.

Hata akiwa saluni, ama akinunua mboga sokoni, alikuwa akieneza porojo kuhusu vile wanawake wa kanisa la mumewe walikuwa wachoyo, washamba na waliokosa hadhi ya kuitwa wanawake kwa sababu ya kutojua kujipodoa.

Kulingana na mdokezi, wanawake hao walipochoshwa na udaku mke wa pasta, walianza kususia ibada.

Hata hivyo, mmoja wao aliwashauri wamjulishe pasta wao kabla ya kuchukua hatua yoyote.

“Akina mama hao walimwendea Mtumishi wa Mungu ofisini na wakamueleza malalamishi yao. Pasta aliwaomba radhi na akawaahidi kuchukua hatua muafaka,’’ akasema mpambe wetu.

Duru zaarifu kuwa, pasta alifululiza hadi nyumbani na kumuamuru mkewe kufunganya virago vyake na kutokomea kwa kumharibia sifa.

“Siwezi nikakubali kanisa langu lisambaratike kwa sababu ya sususu na umbea wako. Nenda zako. Wewe ni bure kabisa!’’ pasta alimfokea mkewe.

Twaarifiwa kwamba, mke wa pasta alifunganya virago vyake na kutokomea kusikojulikana. Aliacha nyuma watoto wawili ambao wanaendelea kutunzwa na baba yao huku kanisa likizidi kushamiri.

…WAZO BONZO…

 

 

Iran yateketeza bendera ya Amerika bungeni

AFP na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Iran walitekeza bendera ya Amerika huku wakiimba “Kifo kwa Amerika” Jumatano ndani ya bunge la taifa hilo.

Walikuwa wakipinga uamuzi wa Rais wa Amerika Donald Trump wa kuondoa taifa lake kutaka mkataba wa kinyuklia unaoshirikisha mataifa kadha.

Picha zilizopeperushwa katika vyombo kadha vya habari nchini Irani zilionyesha mbunge mmoja akipeperusha kijibendera kabla ya kukiteketeza ndani ya ukumbi wa bunge.

Mojtaba Zolnour ambaye ni mbunge wa chama cha Conservative naye mbunge huyo na kuteketeza nakala ya mkataba huo wa kinuklia.

Wabunge wengine waliungana nao wakiimba, “Kifo cha Amerika”, kauli ambayo imeshika kasi miongoni mwa wabunge wa Conservative.

“Mjihadhari msiteketeze bunge,” Spika Ali Larijani alisema.

Maafisa wakuu nchini Iran wamelaani uamuzi wa Trump kuiondoa Amerika katika mkataba huo uliotiwa saini mwaka wa 2015.

Kutiwa saini kwa mkataba huo kulipelekea kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran kwa makubaliano kwamba isitishe shughuli za utengenezaji zana za kinyuklia.

Wakati huo huo, mataifa ya bara Uropa yenye uwezo kiuchumi Jumatano yalijitahidi kuokoa mkataba huo baada ya Trump kuondoa Amerika kutoka kwayo na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.

Hatua hiyo ya Trump ilishutumiwa na mataifa kadha ya ulimwengu, kwani huenda ikapelekea ongezeko la fujo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Trump aliukosoa mktaba huo wa 2015 kwenye hotuba aliyotoa Jumanne akiwa katika Ikulu ya White House.

Mbinu ilizotumia Safaricom kuzoa faida ya Sh55 bilioni licha ya wimbi la #Resist

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom ilipata faida ya Sh55.29 bilioni, baada ya kutozwa ushuru, katika mwaka wa kifedha uliokamilika Machi 31, 2018, kutoka Sh48.44 bilioni ilizoandikisha mwaka 2017.

Hii ni sawa na ongezeko la faida kwa kima cha asilimia 14.1.

Mapato yake ya jumla pia yaliimarika kutoka 212.9 bilioni mwaka 2017 hadi Sh233.7 bilioni mwaka huu, ongezeko linalowakilisha asilimia 9.8.

“Faida yetu iliendelea kuimarika 2017 licha ya changamoto za kiuchumi, ukame na kupanda kwa joto la kisiasa kufuatia kupindi kirefu cha uchaguzi,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji Bob Collymore Jumatano.

“Faida hii ya kima cha asilimia 14.1 inaashiria kuwa Safaricom ilimarisha usamamizi wa rasilimali zake huku ikidumisha huduma kwa wateja wake,” akaongeza afisa huyo Jumatano asubuhi alipohutubia wawekezaji wa kampuni hiyo kupitia teknolojia ya video ya mtandaoni.

Bw Collymore ambaye amekuwa katika likizo kupata nafasi ya kupokea matibabu alitangaza kuwa atarejea kazini hivi karibuni kwani afya yake imeimarika.

“Nasubiri idhini ya madaktari kabla ya kurejea nchini Kenya kuendelea na majukumu yangu,” akasema afisa huyo ambaye aliondoka nchini Oktoba mwaka 2017 kwenda Afrika Kusini kwa matibabu.

Safaricom pia iliungama kuwa hatua ya muungano wa upinzani (NASA) kuchochea wafuasi wake kususia huduma na bidhaa za kampuni hiyo Septemba mwaka 2017 iliathiri mapato yake “japo sio kwa kiwango kikubwa zaidi”.

“Siasa chafu za baada ya uchaguzi mkuu uliopita haswa zilitatiza soko letu la huduma za kupiga simu kati ya mwezi Septemba hadi Desemba 2017,” Bw Collymore akawaambia wawekezaji hao katika makao makuu ya kampuni hiyo, jumba la Safaricom, Westlands, Nairobi.

Sehemu kubwa ya faida ya Safaricom ilitokana na huduma za kupokea na kutuma pesa kupitia simu, maarufu M-PESA, ambayo iliiwezesha kupata jumla ya Sh62.9 bilioni kutoka Sh36.4 bilioni katika kipindi kama hicho 2017.

“Hii ina maana kuwa mapato huduma za M-PESA yaliimarika kwa kima cha asilimia 14.2 katika mwaka wa kifedha uliokamilika Machi 31 mwaka huu.

Huduma hii inachangia asilimia 28 ya mapato ya Safaricom,” Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha Sateesh Kamash akasema alipowasilisha takwimu za matoke0 ya faida. Kufikia sasa wateja wa M-PESA wamefikia watu 2.1 milioni.

Bw Kamash alitangaza kuwa Safaricom itatumia kati ya Sh35 bilioni na Sh38 bilioni katika mwaka wa kifedha wa hadi Machi 31, 2019 kwa ajili ya kupanua mitambo yake ya kutoa huduma.

“Katika mwaka wa kifedha hadi 2019 tunatarajia kuimarisha mitandao yetu ya mawasiliano, huduma za data na mipango mingine ya kuiwezesha kampuni kuimarisha huduma zake na faida,” akasema.

Bw Kamath alisema bodi ya wakurugenzi wa Safaricom imeidhinisha mgao (dividends) wa Sh44.1 bilioni kwa wenyehisa wake.

Hela hizi zitalipwa kwa kiwango Sh1.10 kwa kila hisa.

Mashine hizi zinatupotezea hamu ya uroda, wakulima wa chai walia

Na PETER MBURU

VIONGOZI wa wafanyakazi wa kuchuna majani chai wameunga mkono baadhi ya serikali za kaunti ambazo zimo mbioni kuunda sheria kupinga matumizi ya mashine za kuchuna majani chai, ama kuzitoza ushuru wa juu.

Wasema mashine hizo zimeleta hasara kuu ya kiuchumi na kiafya kwa wafanyakazi na kwamba, sasa wanaume wanaozitumia wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya chumbani na kuwakolesha wapenzi wao tendo la ndoa.

Waliunga mkono serikali za kaunti Nandi na Kericho ambazo zinasemekana kuandaa miswada itakayohitaji mashine hizo kulipiwa ushuru na kuharamishwa kabisa.

Wakihutubia wanahabari mjini Nakuru jana, viongozi hao walisema kumeripotiwa visa vya wanaume wanaotumia mashine hizo kupoteza makali yao chumbani, mbali na kukumbwa na matatizo ya mgongo na kichwa.

“Wafanyakazi wanahitajika kubeba mashine kwa saa nyingi na hivyo wanaishia kuathirika na msukosuko wake kiafya.

Visa vya shida za mgongo, kichwa na hamu ya mapenzi kwa watumizi kwenda chini na hivyo kushindwa kutosheleza wapenzi wao vimeripotiwa,” akasema katibu mkuu mshirikishi wa wafanyakazi wa mashamba makubwa na kilimo nchini (KPAWU) Henry Omasire.

Kulingana na viongozi hao, kaunti ya Nandi inaandaa mswada utakaotoza ushuru mashine hizo, ilhali Gavana wa Kericho Paul Chepkwony naye yuko mbioni kulitaka bunge la kaunti yake kutunga sheria kuharamisha utumiaji wa mashine hizo.

Walisema hatua za kaunti hizo zitawaokoa wafanyakazi wengi masikini ambao wameathirika tangu mashine hizo ziagizwe nchini.

Walidai wafanyakazi 10,000 wamepoteza kazi tangu 2006, mbali na madhara ya kiafya.

Hii, waliongeza, ni kando na kuhatarisha usalama wa miji iliyoko karibu na mashamba ya majani chai.

 

Ajuta kumbaka mpenziwe wa zamani

Na BENSON MATHEKA

MWANAMUME aliyekabiliwa na shtaka la kumbaka mpenzi wake wa zamani, alipatikana na hatia ya kumshambulia mwanadada huyo na kutozwa faini ya Sh30,000.

Paul Angweny atafungwa jela mwaka mmoja iwapo hatalipa faini hiyo aliyotozwa na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Barbara Ojoo. Mahakama haikumpata na hatia ya kumbaka mwanamke huyo ilivyodaiwa lakini ikampata na hatia ya kumjeruhi kimaksudi.

Angweny aliambia mahakama kwamba, mwanamke huyo alikuwa mpenzi wake wa zamani lakini akakanusha kwamba alifanya mapenzi naye bila hiari yake akimtisha kwa kisu.

Ilidaiwa kwamba alitenda kosa hilo Januari 31, 2013 mtaani Kabiria eneo la Dagoreti jijini Nairobi.

Kwenye ushahidi wake, mwanamke huyo alieleza mahakama kwamba, mshtakiwa alimvizia kwa njia na kumpiga kabla ya kumsukuma hadi nyumbani kwake ambapo alimbaka. Alidai kwamba mshtakiwa alimtisha kwa kisu ambacho pia alitumia kumtisha jirani aliyeenda kumuokoa.

“Alimweleza jirani huyo kwamba nilikuwa mpenzi wake na hakufaa kuingilia. Jirani huyo aliondoka alipogundua kwamba alikuwa na kisu,” alisema mwanamke huyo.

Angweny alikanusha madai hayo akisema alisingiziwa makosa alipotofautiana na mwanamke huyo.

Akimhukumu kwa kosa la kupiga na kujeruhi, hakimu alisema kulingana na ushahidi uliotolewa kortini, ilikuwa wazi kwamba mshtakiwa alikuwa amepanga kumdhuru mlalamishi.

Wabunge walia kuhangaishwa mitandaoni

Na JOSEPH WANGUI

WABUNGE watatu wa Nyeri wamelalamika kuhusu jinsi wanavyoshambuliwa kwenye mitandao ya kijamii na watu wanaopinga uongozi wao.

Wabunge hao ambao ni Rigathi Gachagua wa Mathira, Mwangi Gichuhi (Tetu) na Gichuki Mugambi (Othaya) wameonya wanablogu dhidi ya kueneza uvumi kuwahusu na kusema wanaofanya hivyo watakuwa hatarini kuadhibiwa vikali wakati sheria mpya kuhusu uhalifu wa kimitandaoni itakapoidhinishwa.

“Watumizi wengi wa intaneti wamo hatarini kufungwa jela kwa sababu ya yale mambo wanayoandika mitandaoni. Mimi binafsi nitawatumia mswada huo mpya kwa usalama wao wenyewe. Wabunge wanahitaji kupewa nafasi ya kufanya kazi na kutekeleza ahadi zao,” akasema Bw Gachagua.

Alisema amechoshwa na shinikizo analoekewa na watumizi wa intaneti akiongeza kuwa baadhi ya wanaomshambulia wanamezea mate nyadhifa za kisiasa.

“Kama unadhani unaweza kuhudumu vyema kuliko wale waliochaguliwa, subiri hadi 2022 uwanie wadhifa kisha utekeleze miradi unayotaka. Lakini kwa sasa wape wale waliochaguliwa mamlakani nafasi ya kufanya kazi,” akasema akiwa mjini Nyeri.

Mwenzake wa Tetu, Bw Gichuhi, aliwaomba watumizi wa mitandao ya kijamii wasome na kuelewa sheria zilizopendekezwa.

Alionya kuwa kuna adhabu kali dhidi ya wale watakaopatikana na hatia ya kutumia vibaya uhuru wa intaneti.

“Sheria zilizopendekezwa zinatoa adhabu kali na wanablogu wengi watanaswa kama hawatajihadhari. Inafaa watupe muda wa kutimiza ahadi zetu ingawa tunapokea vyema ukosoaji unaotolewa kwa ustaarabu,” akasema Bw Gichuhi.

Kwa upande wake, Bw Mugambi aliomba wabunge wapuuze mashambulio yanayoelekezwa kwao kwenye intaneti na badala yake wachape kazi.

“Watumizi wa intaneti bado wako katika hali ya kisiasa na inafaa tupewe nafasi kufanya kazi. Msijibu matusi yanayoelekezwa kwenu katika mitandao ya kijamii,” akaambia wenzake.

Sheria iliyopendekezwa inalenga kuadhibu watu wanaotumia vibaya mitandao wakiwemo wanaotesa wenzao, wanaoingilia akaunti za wengine bila ruhusa, wasambazaji wa habari feki na wanaosambaza picha za uchi au picha za watoto walio uchi.

Matukio haya sana sana hushuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApp humu nchini.

Mswada huo ulichapishwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Serikali kukata rufaa ya uamuzi kuhusu Pasta Ng’ang’a

Na AGEWA MAGUT

KUTOKANA na kuachiliwa huru kwa Mchungaji James Maina Ng’ang’a aliyeshtakiwa kwa ya mauaji barabarani, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i Jumanne alisema atakata rufaa huku Wakenya wakizidi kulalamika.

Katika barua, Dkt Matiang’i aliagiza Mwendeshaji wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji kukata rufaa ya kesi hiyo ambapo Bw Ng’ang’a alishutumiwa kwa kuendesha gari vibaya na kusababisha kifo.

Kulingana naye, kuna ushahidi wa kutosha wa kuendesha kesi hiyo.

“Niwaomba kukata rufaa na kuwatafutia haki waathiriwa na wananchi wa Kenya,” alisema Dkt Matiang’i kwenye barua.

Wakenya walikasirishwa na hatua ya mahakama kumwachilia huru Mhubiri Ng’ang’a baada ya kushtakiwa kwa kuua mwanamke kwa kuendesha gari vibaya miaka mitatu iliyopita.

Watumiaji wa mtandao wa Twitter walielezea kutoridhishwa na mahakama na kuonekana kukata tamaa baada ya mchungaji huyo kuwekwa huru na mahakama moja ya Limuru mnamo Jumatatu.

Wakenya wengi walioneka kumkashifu Jaji Mkuu David Maraga, ambao wanaamini kuwa amepuuza kinachoendelea katika Idara ya Mahakama.

“Ni kumaanisha kuwa haki katika mahakama zetu ni kwa matajiri pekee? Watu maskini wanaweza kupata haki kweli katika mahakama zetu zilizooza,” aliuliza Victor Achochi.

“Baba mkwe wa mwendazake aliuliza: “Kuachiliwa huru kwa washtakiwa ni kumaanisha watoto wangu walitayarisha ajali iliyosababisha mauti ya mkwe wangu?” Hilo ni swali la haki, familia lazima itakata rufaa uamuzi huo wa mahakama,” alisema Joe Muhahami.

Wengine walisema kuwa uendeshaji wa mashtaka ndio ulikuwa na shida lakini haikuwa hakimu aliyetoa hukumu hiyo.

Wengine waliwashutumu maafisa wa polisi, ambao baadhi yao hushirikiana na washtakiwa na kuchukua hongo kwa lengo la “kupoteza” ushahidi.

Katika kisa hiki, baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo iliyotokea Julai 2015, walisema walimuona mhubiri huyo akiendesha gari hilo.

Hata hivyo, katika taarifa ya polisi, sehemu hiyo ya ushahidi haikurekodiwa. Hivyo, Hakimu Godfrey Oduor alitoa hukumu iliyompendelea mchungaji huyo kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

Mwangi Francis aliandika, “Soma stakabadhi ya mashtaka, ni rahisi kusema kwamba imegeuzwa. NTV ilionyesha picha za leseni iliyokamilika muda wake ya Mchungaji Ng’ang’a. Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama ilithibitisha kuwa alikuwa amelewa. Hadithi sasa imekuwa tofauti…”

Maskwel@Omogirango aliandika, “Majaji huwa hawafanyi uchunguzi, kabla ya kupiga kelele #JusticeForMercyNjeri, ninawaalika kukabiliana na waendeshaji mashtaka kwanza, ndio mtajua mahali na wakati kesi hiyo iliisha.”

Wengine walieleza aina ya maisha wanayoishi baadhi ya wachungaji kutokana na zaka na sadaka kutoka kwa wafuasi wao.

Paul Njogu alisema: “Utamaduni wa Kiafrika uliheshimu maisha ya binadamu, hakuna aliyeepuka haki.”

Polisi wanatumiwa kututishia – Wahadhiri

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Muungano wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini (UASU) na Chama cha wafanyakazi wa vyuo hivyo (KUSU) wameshtumu serikali kwa kutumia polisi kuwashambulia na kuwanyanyasa wahadhiri wanaoshiriki mgomo.

Katibu Mkuu wa UASU Dkt Constantine Wasonga alisema kwamba dhuluma hizo katu hazitawalazimisha kusitisha mgomo huo na kuitaka serikali na manaibu chansela wa vyuo kutumia njia zinazokubalika ili kufikia makubaliano yatakayowarejesha madarasani

Baadhi ya vyuo vikuu alivyovitaja kwamba usimamizi wao umechukuliwa na Polisi ni Masinde Muliro, Maasai Mara, Pwani na Kenyatta.

“Tunalaani kwa kinywa kipana kuendelea kutumiwa kwa wakora na maafisa wa polisi katika vyuo vyetu ili kuwalazimisha wahadhiri kurejea darasani. Mgomo unaendelea wapende wasipende hadi watutatulie maslahi yetu,” akasema Dkt Wasonga.

Katibu huyo pia aliulaumu uongozi wa vyuo vyenyewe wakiwemo manaibu chansela kwa kutumia swala la mgomo kuzua uhasama mkubwa kati ya wahadhiri na wanafunzi. Katika siku za hivi karibuni wanafunzi wa baadhi ya vyuo wamekuwa wakiandamana na kupinga mgomo huo huku wakiwakabili wahadhiri wanaogoma.

“Serikali sasa imeamua kutugonganisha na wanafunzi ambao ni watoto wetu wakifikiria hilo litatutia uoga. Tunawaomba wanafunzi wasiende vyuoni kwa sababu wakora na polisi watawadhuru,” akasema

Aidha, katika onyo kali kwa serikali, kiongozi huyo alisema endapo mwanachama yeyote wa vyama hivyo viwili atajeruhiwa au kufariki kutokana na vitendo vya kihalifu vya polisi basi serikali iwe tayari kupokea lawama kubwa.

Kwa upande wake Dkt Charles Mukhwaya ambaye ni katibu mkuu wa chama cha KUSU alishangaa haja ya wao kuendelea kushirikishwa kwenye mikutano mingi na jopo lililoundwa na waziri wa elimu Amina Mohamed ilhali hawajawasilishiwa pendekezo mbadala la matakwa yao.

“Tunashinda katika vikao na jopo hilo ilhali wanachama wake hawajawahi kutupa pendekezo lao lakini wanatarajia mgomo usitishwe. Dhuluma wanazotenda dhidi ya wahadhiri ndizo zinazidi kutonesha vidonda vyetu,” akasema Dkt Mukhwaya

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika mkutano na wanahabari katika makao makuu chama katika Jumba la Unafric mjini Nairobi.

 

Polisi waonya huenda Al-Shaabab watekeleze uvamizi Ramadhan

Na BERNARDINE MUTANU

POLISI wamewatahadharisha Wakenya kuhusu uwezekano wa magaidi wa Al-Shabaab kutekeleza mashambulio wakati wa mwezi mtakatifu wa Ramadhan.

Katika taarifa Jumanne, Polisi walisema makundi ya kigaidi, likiwemo al-Shabaab, yalikuwa yametoa onyo kuhusu mashambulizi kuanzia Mei 15.

“Tunapoelekea mwezi mtakatifu wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza Mei 15, 2018, makundi ya kigaidi yametoa tahadhari na kuwarai wanachama wake kuzidisha mashambulizi wakati huo,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa NPS, Bw Charles Owino katika taarifa.

Makundi mengine yaliyo na mipango hiyo ni ISIS na al-Qaeda, “Ingawa uwezo wa al-Shabaab umelemazwa, tuna habari za kuaminika zinazoashiria kwamba kundi hilo linapanga kutekeleza mashambulizi nchini,” alisema.

Al-Shabaab mara kwa mara waibuka kutekeleza mashambulizi nchini wakati wa Ramadhan hasa katika maeneo ya Pwani na Kaskazini Mashariki na sehemu za miji nchini.

Hivyo, NPS iliwaomba wananchi kuwa makini hasa katika maeneo yaliyo na watu wengi vikiwemo vituo vya mabasi, mahoteli, makanisa, na shule.

Idara hiyo iliwahakikishia wananchi kwamba vikosi vya usalama viko makini, “Tunakagua kwa umakini shughuli zote zinazoendelea katika mpaka wa Kenya na Somalia ili kusambaratisha mashambulizi yoyote dhidi ya Kenya,” alisema Bw Owino.

Wakati huo huo, alisikitikia wananchi walioshambuliwa Mandera katika mgodi wa Shimbir Fatuma. Wakati wa kisa hicho, wananchi wanne walipoteza maisha yao, “Tunaomboleza na familia za waliotuacha na tunaendelea kuwasaka waliotekeleza shambulizi hilo,” aliongeza.

Kulingana na taarifa hiyo, vikosi vya usalama tayari vimewakamata baadhi ya washukiwa wanaosaidia katika uchunguzi wa shambulizi hilo.

Alisema visa vya mashambulizi ya kigaidi nchini vimepungua pakubwa.

Mbunge alala ndani kwa kushambulia mfanyabiashara

Na WYCLIFFE MUIA

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki, Simon Mbugua, alilala seli Jumanne pamoja na watu wengine watatu wanaoshukiwa kuhusika katika uvamizi wa aliyekuwa mwenyekiti wa wafanyabiashara jijini Nairobi, Timothy Muriuki.

Jumanne, maafisa wa ujasusi walimuwinda Bw Mbugua na kumkamata katika hoteli ya Sagret jijini Nairobi na baada ya kumhoji saa kadhaa wakamuweka ndani na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Mbunge huyo alikamatwa pamoja na washukiwa wengine Anthony Otieno Aboo almaarufu Jamal, Solomon Benjamin Onyango almaarufu Solo na mshukiwa mwingine aliyekuwa nao katika hoteli ya Sagret.

Mkuu wa Ujasusi katika Kaunti ya Nairobi Ireri Kamwende aliongoza kikosi cha maafisa kadhaa kumkamata mbunge huyo.

“Tutamhoji zaidi ili aweze kutusaidia kujua ukweli kuhusu uvamizi huo wa mfanyabiashara,” alisema Bw Kamwende.

“Tulifanikiwa kuwakamata Jamal na Solo lakini wenzao watatu bado wako mafichoni. Tuna uhakika tutawakamata pia,” alisema Kamwende.

Washukiwa hao wengine ni Brian Owino almaarufu Orange, Michael Mbanya na Suleiman Hussein almaarufu Rescue.

Wananume hao watano walinaswa wakimvamia vikali Bw Muriuki kabla ya kumtimua katika hoteli moja jijini Nairobi alipokuwa akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu hali ya uongozi wa jiji la Nairobi.

Sura mpya ya ‘Baba’ baada ya salamu

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga amechukua sura mpya tangu Machi 9, 2018 alipoamkuana na Rais Uhuru Kenyatta. Alibadilika ghafla na sasa si tena kigogo wa upinzani aliyefahamika Afrika na duniani kote kwa ukakamavu wa kisiasa.

Tofauti na awali alipokuwa mkosoaji mkuu wa serikali, Bw Odinga ameacha kulaumu serikali, amepunguza mikutano yake na wanahabari na kueleza kauli zake katika mitandao ya kijamii.

Pia amejitenga na wanasiasa wa upinzani na washirika wake waliokuwa na misimamo mikali kama yeye. Badala yake, ratiba yake imekuwa ya kuwapokoea mabalozi, makundi ya wazee na wakosoaji wake wa zamani kama vile Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Kabla ya kuamkuana na Rais Kenyatta, Bw Odinga alikuwa mstari wa mbele kukashifu Serikali kwa kukopa sana kutoka nchi za kigeni kwa kile alichokuwa akionya kuwa hatua hatari kwa uchumi. Lakini majuzi Serikali ilipokopa mabilioni ya pesa za Eurobond, Bw Odinga hakusema chochote.

Amekuwa msiri hivi kwamba kufikia sasa, hakuna anayefahamu aliyokubaliana na Rais Kenyatta isipokuwa taarifa ya pamoja waliyotoa kwa Wakenya hapo Machi 9 walipotangaza mwafaka.

Jumanne, Bw Odinga aliambia mkutano wa Baraza Kuu la ODM kwamba hivi karibuni yeye na Rais Kenyatta wataandaa misururu ya mikutano kote nchini kuelezea yaliyomo kwenye mkataba wao wa maelewano (MOU).

Kiongozi huyo pia amekuwa kimya kuhusu masuala mengine ambayo hapo awali angekuwa amezungumzia.

Haya ni kama vile juhudi za Serikali kukabiliana na mafuriko ambayo yamekumba maeneo mengi ya nchi ambapo hatua za kusaidia waathiriwa zimeonekana kutotosha.

Hajasema chochote kuhusu ukosefu wa usalama eneo la Kapendo katika mpaka wa Turkana na Baringo ambapo watu watano waliuawa majuzi.

Pia hajazungumzia mauaji ya wanajeshi 8 wa KDF katika eneo la Dhobly nchini Somalia mnamo Jumatatu, licha ya msimamo wake wa awali kuwa wanajeshi hao waondolewe Somalia.

Kabla ya Machi 9, Bw Odinga pia alikuwa mwepesi wa kuitisha vikao vya wanahabari mara kwa mara katika ofisi yake ya Capitol Hill Square ambapo alikuwa akikosoa serikali.

Baada ya kusalimiana na Rais Uhuru Kenyatta vikao vyake na wanahabari vimepungua na mtindo wake siku hizi ni kutuma taarifa moja moja kwa vyombo vya habari kupitia kwa msemaji wake Dennis Onyango.

Jumanne, Raila aliambia wajumbe wa ODM kwamba analenga kuona Kenya mpya katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

 

 

 

Sukari ya Sh5 bilioni kusalia bandarini

Jaji Mkuu David Maraga, naibu wake Philomena Mwilu, Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala na Isaac Lenaola wakati wa kesi. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MAMLAKA ya ushuru nchini KRA Jumanne iliamriwa isiondoe sukari ya Sh5 bilioni katika bandari ya Mombasa.

Mahakama ya Juu iliagiza sukari hiyo iliyoingingizwa nchini Novemba 2017 isalie bandarini Mombasa hadi rufaa iliyowasilishwa na kampuni iliyoingiza sukari hiyo kutoka Brazil isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Mkuu David Maraga, naibu wake Philomena Mwilu, Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala na Isaac Lenaola walisema ni muhimu kuzuia KRA kutwaa sukari hiyo kabla ya ukweli  kubainika.

Lakini kampuni ya Darasa Investments Limited ilisema ilikuwa imelipa ushuru wa zaidi ya Sh422 milioni na kwamba, KRA ilipasa kuiruhusu iuze sukari hiyo.

Darasa iliingiza Sukari hiyo humu  nchini mnamo Novemba 2017.

Kampuni hiyo inaomba mahakama iamuru Serikali iilipe Sh5bilioni ikiwa ni hasara ambayo imepata kwa kuendelea kuzuilia sukari hiyo.

Isitoshe, Darasa inaomba uamuzi wa Majaji Alnashir Visram, Wanjiru Karanja na Martha Koome ufutiliwe mbali na iruhusiwe kuondoa sukari yake kutoka bandari ya Mombasa iuze.

“Baada ya kusikiliza ushahidi wa Darasa kupitia kwa wakili Mansur Issa, hii mahakama inakubali kuwa kuna masuala mazito ya kisheria yanayopasa kuamuliwa kabla ya sukari hiyo kuachiliwa kutoka bandarini,” walisema majaji hao wa Mahakama ya Juu.

Majaji Visram, Karanja na Koome wa Mahakama ya Rufaa waliamuru KRA ifanye hesabu ijue kiwango cha kodi ambacho Darasa ilitakiwa ilipe.

KRA ilitakiwa ifuate sheria iliyochapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali ya Mei 12, 2017 na kufanyiwa marekebisho mnamo Oktoba 4, 2017.

Kampuni hiyo ilikuwa inaomba KRA ishurutishwe kuilipa fidia ya $8milioni (832,000,000) kwa sababu ya kukataa kuiruhusu iondoe sukari hiyo kutoka bandarini.

Pia, Darasa ilikuwa imeomba korti iamuru KRA ilipe ada zote za kuhifadhiwa kwa sukari hiyo tangu iingizwe humu nchini na meli ijulikanayo  kama NV Iron Lady,

Pia, iliomba korti iamuru ikubaliwe kuondoa  sukari hiyo bandarini pasi na kulipia ushuru wa forodha.

Majaji Visram, Karanja na Koome walisema kulikuwa na stakabadhi mara mbili kuhusu kuingizwa kwa sukari hiyo ya tani 40,000 kutoka nchini Brazil zilizokuwa zinakanganya.

Kalameni amtoroka slay queen akihofia hasara zaidi

Na DENNIS SINYO

LESSOS, ELDORET

POLO mmoja mtaani hapa alimhepa kipusa alipoitisha pombe badala ya soda wakiwa katika eneo moja la burudani.

Yasemekana ilikuwa mara ya kwanza wawili hao kukutana ana kwa ana kujivinjari baada ya kufahamiana kwenye mtandao.

Kulingana na mdokezi, jamaa na kidosho huyo waliingia kwenye hoteli moja ya kifahari na kisha wakaitisha menu.

Licha ya jamaa kuitisha chupa ya juisi, mwanadada huyo alimwambia weita amletee chupa ya mvinyo kali.

Jamaa huyo ambaye ameokoka, alishangaa sana na kudhania kwamba huenda demu alikuwa akifanya mzaha tu.

Huku wakipiga gumzo, jamaa huyo aliletewa sharubati na kipusa akaletewa chupa ya mvinyo alioagiza.

Kulinga na mdokezi, jamaa alisema mvinyo alioagiza demu ni wa bei ghali na hutumiwa na mabwenyenye.

Binti alifungua chupa na kuanza kumimina mvinyo kwa ustaarabu huku jamaa akimtazama.

Inasemekana hamu ya jamaa kunywa sharubati iliisha. Baada ya dakika chache, mwanadada alilewa na kuropokwa huku akimpapasa jamaa kwenye mikono na mabega.

Jamaa alishindwa kuendelea na mazungumzo, akaacha kinywaji chake na kwenda kukilipia.

Baada ya kulipa bili yake, aliondoka upesi, akapanda pikipiki na kwenda zake kukutana na marafiki.

Alipowasimulia kilichompata, walimwambia alifanya vyema kujitoa kwenye meno ya simba.

Kalameni mmoja alidai alijipata katika hali sawa alipokutana nakipusa mara ya kwanza baada ya kurushiana misitari mtandaoni.

“Huyo ni slay queen. Umefanya vizuri kuhepa. Vipusa kama hao wanaweza kukufanya ulale seli za polisi. Hawa warembo weupeweupe wana majaribu mengi,’’ kalameni alisema.

Polo huyo aliapa kwamba hatasaka warembo kwenye mitandao ya kijamii tena kufuatia kioja hicho.

…WAZO BONZO…

Ford Kenya na ANC wakosa kuafikiana

Na SHABAN MAKOKHA

MGAWANYIKO umezuka kati ya viongozi wa chama cha Ford Kenya na ANC kuhusu mtindo wa kuwachagua viongozi wao wakuu iwapo vyama hivyo vitaunganishwa viwe chama kimoja.

Vyama hivyo tayari vimeanzisha mchakato wa kuunganishwa kwa lengo la kuwaleta pamoja jamii ya waluhya wakilenga uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Naibu Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Boni Khalwale aliashiria kwamba Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ndiye atateuliwa kiongozi wa chama kitakachobuniwa kwa kuwa ni mkubwa kiitifaki kuliko Bw Moses Wetangula.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Ford Kenya Dkt Eseli Simiyu alikataa wazo hilo.

“Hatujashauriana vilivyo kuhusu swala hili la kuunganisha vyama vyetu. Fikira zisizofaa zinazohujumu mpango huo hazifai kwa wakati huu,” akasema Dkt Simiyu.

Katibu huyo wa Ford Kenya aliungwa mkono ma mwenzake wa ANC Godfrey Osotsi ambaye pia alikataa pendekezo la Bw Mudavadi kupewa uongozi wa chama.

Wawili hao walisema usimamizi unaoshughulikia maswala ya muungano wao haujajadili swala la nani atakiongoza chama na kuongeza kwamba ni mapema sana kuangazia swala hilo.

“Bado tuko katika hatua ya mwanzo katika kuunganisha vyama vyetu. Lakini hatujajadili kuhusu wale watakaoshikilia nyadhifa mbalimbali chamani,” akasema Dkt Simiyu.

Kwa upande wake Bw Osotsi alipuuzilia mbali hatua ya kuunganisha vyama hivyo akisema ni ajenda inayosukumwa na watu wachache wenye nia ya kufaidika kibinafsi na kisiasa.

Aliongeza kwamba muungano unaopendekezwa unakosa ajenda ya kudumu na wanachama wengi wa vyama husika hawajashauriwa wala kuhusishwa akisisitiza umoja wa jamii ya Waluhya unatumiwa tu kama kisingizio na viongozi wakuu.

Akihutubu katika mazishi kijijini Eshikhoni kaunti ndogo ya Navakholo, Dkt Khalwale alisisitiza kwamba jamii ya Mulembe imejipanga vizuri kuliko miaka ya nyuma ili kutoa mwaniaji mmoja wa kutwaa kiti cha urais mwaka wa 2022.

Dkt Khalwale alimlaumu Katibu Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyikazi(COTU) Francis Atwoli kutokana na kauli aliyotoa wakati wa sikukuu ya Leba kwamba katiba inafaa kurekebishwa ili kumpa Rais Uhuru Kenyatta nafasi mpya ya uongozi baada ya kustaafu mwaka wa 2022.

“Hakuna haraka ya kufanya mabadiliko ya kikatiba ili kuwanufaisha watu wachache kwa kuwapa nyadhifa za uongozi. Rais Kenyatta anafaa kukataa pendekezo hili,” akaseama Dkt Khalwale.

Kulingana naye mabadiliko kwa katiba yatamwezesha Rais Kenyatta kupata wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka amubwa na naibu wake akiwa Seneta wa Baringo Gideon Moi huku Raila Odinga akiutwaa wadhifa wa urais.

 

 

 

 

Wanaosaka ajira ughaibuni watahadharishwa dhidi ya ugaidi

Na WINNIE OTIENO

WAKENYA wanaotafuta kazi ng’ambo wametahadharishwa kuwa makini na kampuni zinazotumia nafasi hiyo kusajili watu kujiunga na makundi ya kigaidi.

Waziri wa Leba, Bw Ukur Yatani, aliwahatadharisha Wakenya kuwa makini na kampuni hizo akisema wizara yake imeidhinisha na kusajili kampuni 65 pekee za kibinafsi ambazo zimepewa idhini ya kuwaajiri Wakenya kufanya kazi ughaibuni.

Aidha alisema serikali imeanza kuchunguza kampuni zinazoshukiwa kuhusika na ulanguzi wa binadamu humu nchini.

Kwa muda sasa kampuni za kusajili Wakenya kufanya kazi ughaibuni zimelaumiwa kwa ulanguzi wa binadamu hususan kujiunga na kundi la kigaidi la ISIS nchini Syria.

Wiki iliyopita, jeshi la humu nchini liliwaokoa vijana 13 waliosajiliwa kujiunga na kundi la kigaidi la Al-Shabaab Somalia.

Akiongea Jumamosi alipokutana na baadhi ya wamiliki wa kampuni hizo eneo la Pwani, Bw Yatani aliwahakikishia Wakenya kuwa wizara yake itakabiliana na kampuni ghushi zinazoshukiwa kuwasajili wananchi kwenye makundi ya kigaidi.

“Kuna kanuni mpya za kuajiri Wakenya kwenda kufanya kazi ughaibuni. Ni sikitiko kuwa kampuni nyingi zinafuata kanuni lakini za huku Pwani hazifuati,” akasema waziri huyo katika Hoteli ya Sarova Whitesands.

Aliongeza: “Yale yanayotendeka si hadithi tunazozisoma au kuona kwenye runinga. Imefanyika  nchini mwetu. Kuna ulanguzi wa watu katika maeneo yasiyojulikana na ni lazima tuwe makini. Tunasihi kampuni za kusajili Wakenya kutupasha habari kuhusu kampuni ghushi ama zinazoshukiwa.”

Alilaumu kampuni ghushi kwa masaibu ambayo Wakenya wngi wanapitia wanapoenda kufanya kazi Uarabuni.

“Tusidanganyane kwani Wakenya wanateseka sana huko Uarabuni. Lakini ni sharti tuhakikishe hawateseki wanaposafiri nchi hizo. Maisha ya Wakenya ni muhimu sana lazima walindwe,” akasema.

 

 

 

Prof Ghai ataka fedha zilizotumika na Jubilee Ikulu ziwekwe wazi

Na BENSON MATHEKA

SHIRIKA moja lisilo la kiserikali, limeandikia barua Msimamizi wa Ikulu Bw Kinuthia Mbugua, likitaka aeleze kiwango cha pesa zilizotumiwa kuandaa mikutano ya chama cha Jubilee katika Ikulu ya Nairobi na ikulu ndogo nchini mwaka 2017.

Katiba Institute, linataka kujua gharama ya mikutano yote ambayo chama cha Jubilee kiliandaa katika ikulu wakati wa kampeni, aliyeitisha mikutano hiyo na aliyesimamia gharama.

“Dhamira ya barua hii ni kuomba habari kuhusu gharama iliyotokana na mikutano ya chama cha Jubilee katika Ikulu na Ikulu ndogo kati ya Septemba 2, 2017 na Oktoba 2, 2017,” inasema barua iliyotiwa sahihi na mwenyekiti wa shirika hilo Prof Yash Pal Ghai.

Shirika hilo linataka Bw Mbugua kueleza ikiwa Ikulu ni ukumbi wa kukodishwa kuandaa mikutano na ada inayotozwa.

“Je, Ikulu inaweza kukodishwa kuandaa mikutano ya vyama vya kisiasa au hafla zinazoegemea upande mmoja, na ikiwa inakodishwa, ada ni gani?” aliuliza Prof Ghai.

Anataka Bw Mbugua au afisa anayehusika, kueleza aliyelipa gharama ya kukodisha ikulu, vinywaji na mlo katika kila mkutano.

“Unaweza kutukabidhi nakala za risiti, hati za kutoa huduma zilizotolewa kwa kila mkutano,” anaomba kwenye barua aliyoandika Mei 4 mwaka huu.

Profesa Ghai anataka maafisa wa ikulu kueleza iwapo gharama ililipwa na wahusika wengine kikiwemo chama cha Jubilee, pesa walizolipa na risiti za kuthibitisha kwamba walilipa pesa hizo.

“Ikiwa serikali ililipa gharama ya kuandaa mikutano hiyo, ni maafisa gani walioidhinisha malipo hayo. Ikiwa serikali ililipa gharama ya kuandaa mikutano hiyo ilitumia pesa ngapi,” mtaalamu huyo wa katiba anataka kujua.

Aidha, anataka maafisa hao waeleze iwapo pesa za kuandaa mikutano hiyo zilikuwa zimetengwa kwenye bajeti na jina la kila afisa aliyeidhinisha pesa hizo kutumika.

Profesa Ghai anaambatisha orodha ya mikutano 12 ambayo wajumbe wa chama cha Jubilee wakiwemo wabunge walitembelea ikulu kukutana na rais kabla ya marudio ya kura ya urais ya Oktoba 26 mwaka jana.

“Iliripotiwa katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na tovuti rasmi ya ofisi ya rais kwamba Rais aliandaa mikutano kadhaa katika ikulu na ikulu ndogo kuhusu masuala ya chama cha Jubilee na kwa kampeni zake pamoja na mikutano ya kundi la wabunge la chama cha Jubilee,” anasema Prof Ghai.

Kulingana naye, Rais alipokea wajumbe wa chama cha Jubilee kutoka maeneo kadhaa kote nchini katika ikulu walioahidi kumuunga mkono.

Anasema anatoa ombi hilo chini ya sheria ya haki ya raia kupata habari kutoka kwa serikali, na haki ya serikali kuchapisha habari kwa manufaa ya wananchi na iwapo haitampa habari hizo ataishtaki mahakamani.

Nia ya Raila yasalia kuwa siri kuu

Na VALENTINE OBARA

PENDEKEZO la Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kuhusu marekebisho ya Katiba limezidi kuacha viongozi na wananchi wa pande zote za kisiasa wakijikuna vichwa kuhusu anachotaka kuafikia.

Sisitizo lake kuwa hana njama ya kujipangia mikakati ya 2022 kupitia muafaka huo halijazuia wanasiasa kuhisi ana nia fiche, huku wengine wakijaribu kutegua kitendawili chake.

Hali hii imezidishwa na jinsi wawili hao hawajatangaza lolote kuu kuhusu muafaka wao kufikia sasa, isipokuwa kuchagua kikundi cha watu 14 ambao pia majukumu yao hayajafafanuliwa wazi kwa umma.

“Inahitajika kuwe na ufafanuzi ili kuondoa usiri mkubwa ulio katika shughuli hii. Kwa sasa kuna hali ya kuchanganyikiwa kwani tayari kuna asasi za umma zinazofaa kushughulikia masuala yaliyotajwa kwenye muafaka wao,” alisema Katibu Mkuu wa Chama cha Amani National Congress, Bw Barrack Muluka.

Bw Odinga amependekeza kuwe na wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake, na kuwe na ngazi tatu za uongozi.

Mahasimu wake wanahofia kwa kupendekeza hivyo anatafuta mwanya wa kuingia serikalini kwa mlango wa nyuma na kufanya iwe vigumu kwa Naibu wa Rais William Ruto kuungwa mkono eneo la Kati mwaka wa 2022 na endapo Bw Ruto atashinda uchaguzini, asiwe rais mwenye mamlaka makubwa.

Mbunge wa Ndaragua, Bw Jeremiah Kioni, alisema ingawa Katiba inahitaji kurekebishwa, mbinu inayotumiwa ni ya kutiliwa shaka kwani inaonekana lengo ni kumvuruga Bw Ruto kisiasa.

“Jamii yetu iliahidi kumuunga mkono Bw Ruto. Huwezi kutufanya tuonekane tunamtoroka wakati huu. Tunahitaji marekebisho ya Katiba lakini mdahalo huu wote ulianzishwa kwa njia isiyofaa,” akasema Jumatatu.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na wanasiasa wengine wa eneo la Kati ambao hawamwamini Bw Odinga.

Seneta wa Narok, Bw Ledama ole Kina ambaye ni mwanachama wa ODM, alikiri kuna hofu inayohitaji kutulizwa kabla watu wazungumzie marekebisho ya Katiba.

“Kwa kweli watu wana hofu. Hata mimi ningeogopa kama ningekuwa naibu wa rais kisha mtu aseme anataka kubadilisha katiba wakati nimekaribia kuingia mamlakani,” akasema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Third Way Alliance, Dkt Ekuru Aukot, alipendekeza katiba irekebishwe ili watu ambao wamewahi kuwa rais, naibu au makamu wa rais, waziri mkuu au naibu wasiruhusiwe kuwania urais.

Kulingana naye, hatua hii itafanya marekebisho yasilenge kutimiza maazimio ya wanasiasa ya kibinafsi, na itatoa nafasi kwa viongozi wapya kuongoza nchi.

HISTORIA: Kenya kutuma setlaiti ya kwanza kwenye sayari

Na VALENTINE OBARA

KENYA inatazamia kuweka historia Ijumaa hii wakati setilaiti ya kwanza kuwahi kutengenezwa nchini itakapotumwa katika sayari.

Chombo hicho cha kuzunguka sayari kilitengenezwa na wanafunzi na watafiti wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa ushirikiano na shirika la teknolojia za sayari la Japan Space Agency (JAXA).

Naibu Chansela wa UoN, Prof Peter Mbithi (pichani), alisema mafanikio hayo ni dhihirisho la hatua kubwa zilizopigwa nchini kuhusu utafiti wa kiteknolojia ambao unaweza kuchangia katika maendeleo yatakayokuza uchumi wa kitaifa.

Setilaiti hiyo yenye ukubwa wa sentimita kumi kimchemraba itarushwa sayarini kutoka kwa kituo kilicho Japan, lakini Wakenya kadhaa watapewa nafasi kushuhudia matukio hayo katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo yatapeperushwa moja kwa moja.

“Kutakuwa na tukio Japan, katika sayari na hapa UoN. Kile kitakachofanyika Japan kitashuhudiwa na baadhi ya Wakenya ambao watakuwa huko.

Hapa tutakuwa na hafla katika ukumbi ambapo matukio yatapeperushwa moja kwa moja. Tunasubiri siku hiyo kwa hamu,” akaambia wanahabari Jumatatu.

Wale ambao wangependa kuhudhuria hafla hiyo katika ukumbi wa Chandaria ulio UoN bewa la jijini Nairobi watahitajika kutuma maombi kwenye tovuti ya chuo hicho na watafahamishwa kama wamebahatika kupata nafasi.

Prof Mbithi aliongeza kuwa setilaiti hiyo itatumiwa kukusanya deta kuhusu masuala mbalimbali muhimu kama vile mabadiliko ya hali ya anga, uhifadhi wa wanyamapori, utabiri wa hali ya hewa miongoni mwa mengine.

Alitoa wito kwa wadau wengine waungane nao ili kuimarisha zaidi utafiti kuhusu masuala ya sayari pamoja na kutia nguvu chombo hicho ili kifanikiwe kutimiza malengo yake.

Mkuu wa taasisi ya mafunzo ya uhandisi katika chuo hicho, Prof Jackson Mbuthia, alisema setilaiti hiyo yenye uzani wa kilo 14 itasafirishwa hadi kwenye sayari mwendo wa saa saba mchana Ijumaa.

“Huu ni mwanzo wa safari ambayo itawezesha Kenya kushiriki kwenye sayansi ya sayari. Ni mara yetu ya kwanza kupiga hatua hii lakini tunaamini ni muhimu katika ustawishaji wa sayansi nchini,” akasema.

Kulingana naye, sayansi ya sayari imechangia pakubwa kwa maendeleo ya mataifa makuu kiuchumi na hivyo basi Kenya itapata nafasi bora ya kunufaika kwa jinsi hiyo hiyo.

Mbali na JAXA, mradi huo pia ulishirikisha mchango kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Sayari (UNOOSA).

Mvua yazuia mashahidi wa kesi ya Konza City kufika kortini

Wakurugenzi wa kampuni ya mashamba ya Malili, kaunti ya Makueni wakiwa kizimbani Jumatatu. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MASHAHIDI wanne waliokuwa wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya wizi wa Sh553 milioni za mauzo ya ekari 5000 za shamba la Malili, kaunti ya Makueni ambapo kutajengwa jiji la Konza Techno dhidi ya wakurugenzi wanne wa kampuni ya Malili Ranch Limited (MRL) hawakufika kortini Jumatatu kwa sababu ya mvua iliyonyesha.

Kiongozi wa mashtaka Bi Lilian Obuor alimweleza hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi kwamba polisi waliwakuwa wamewapelekea samanzi mashahidi saba kufika kortini kutoa ushahidi wa Mabw David Ndolo Ngilai, James Kituku Munguti,Leonard Kyania Kitua na Julius Mbau Nzyuko.

“Ni mashahidi watatu tu waliofaulu kufika kortini kutoa ushahidi, wanne walikumbwa na matatizo ya usafiri kwa sababu ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha kaunti ya Makueni,” Bi Obuor alisema kortini.

Kiongozi huyo wa mashtaka  aliambia mahakama mashahidi 60 wameandikisha  taarifa kwa polisi wakieleza jinsi wakurugenzi wa MRL waliiuzia Serikali ekari 5,000 kupitia kwa Wizara ya Habari na Mawasiliano bila idhini ya wenye hisa.

Serikali ililipa MRL Sh1,000,000,000 kupitia kwa wakili Eric Mutua.

Bi Obuor alimweleza hakimu  kuwa atafanya mashauri na maafisa wa polisi waliochunguza kesi hiyo waafikiano idadi ya mashahidi watakaoitwa kwa vile wote wanazugumzia suala moja.

Akitoa ushahidi mwanahisa wa MRL Bw Joseph Kavoo alisema alifahamishwa na mwanahisa mwenzake kuwa shamba alililogawiwa la ekari 7.8 liliuziwa Serikali na “wanahitajika kufika katika afisi ya Bw Mutua achukue hundi ya Sh1.1 milioni.”

Bw Kavoo alisema alifululiza hadi afisini mwa Bw Mutua na kupokea hundi ya Sh1.1milioni.

“Je, malalamishi yako ni nini dhidi ya wakurugenzi hawa wanne?” Bi Obuor alimwuliza Bw Kavoo.

“Shida yangu ni kwamba  wakurugenzi wa MRL hawakuwaita wenye hisa wapitishe hoja ya kuuzwa kwa ekari 5,000,” alijibu Bw Kavoo na kuongeza , “Wanahisa wengine walikuwa wanalipwa Sh1.4 milioni na zaidi lakini mimi nilipewa Sh1.1 milioni. Mwenye kupokea pesa kutoka kwa Serikali anatakiwa anilipe kiasi nilichostahili kulipwa.”

“Je, ulipokea pesa kutoka kwa washtakiwa hawa?” “Hapana.”

Wakurugenzi hao wamekanusha mashtaka ya wizi na kukaidi maadili ya afisi yao kwa kuruhusu kuuzwa kwa ekari 5,000  za shamba la MRL bila idhini ya wanahisa.

Kesi itaendelea Mei 15, 2018.

Mabadiliko ya sheria ya SRC yaibua hofu

Na IBRAHIM ORUKO

HOFU imekumba Tume ya Mishahara (SRC) baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia sahihi mabadiliko ya pamoja ya sheria inayompa mamlaka ya kuteua mwenyekiti wa tume hiyo.

Rais Kenyatta aliidhinisha mabadiliko hayo Ijumaa na yanaathiri sheria ya SRC, Sheria ya Pensheni na sheria ya kudhibiti dawa na sumu.

Kufuatia mabadiliko katika sheria ya SRC, makamishna wa tume hiyo hawatakuwa wakihudumu kwa muda na rais atakuwa na mamlaka ya kumteua mwenyekiti.

Hata hivyo, kuna wasiwasi katika SRC kuhusu uhalali wa hatua hiyo na gharama ya utekelezaji wa mabadiliko hayo.

Wafanyakazi wa tume wanahofia kuwa uamuzi wa kuwafanya makamishna wafanyakazi wa kudumu unaweza kupingwa mahakamani kwa msingi kuwa idadi yao inazidi iliyowekwa kikatiba.

Wasiwasi wa wafanyakazi hao ni kuwa tume itahitaji ofisi kubwa kutosheleza makamishna wa kudumu na wafanyakazi zaidi kuajiriwa katika ofisi zao.

SRC ina makamishna 11 wanaowakilisha taasisi tofauti.

Wanawakilisha Tume ya Huduma ya Bunge, Tume ya Mahakama, Seneti, Baraza la Usalama, Muungano wa Vyama wa Wafanyakazi (Cotu), Shirikisho la Waajiri Kenya (FKE) na shirika la wataalamu.

Wengine ni Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu na waziri wa utumishi wa umma.

Makamishna hao huwa wanahudumu kwa kipindi kimoja cha miaka sita na hawawezi kuteuliwa tena. Kwa sasa, shughuli ya kuteua makamishna wapya inaendelea baada ya kipindi cha iliyoongozwa na Sarah Serem kumalizika mwaka 2017.

Ingawa sheria ya SRC inataja taasisi zinazofaa kutoa makamishna, katiba inasema kila tume huru inapaswa kuwa na makamishna wasiozidi tisa.

“Tuna wasiwasi na uwezo wa tume kwa sababu kufuatia sheria iliyotiwa sahihi na rais sasa itatubidi tuhame ofisi zetu za sasa,” alisema afisa mmoja wa cheo cha juu wa tume hiyo ambaye aliomba tusimtaje jina kwa sababu haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya tume.

Alisema itabidi tume ipate ofisi kubwa na kuajiri wafanyakazi zaidi kwa sababu kila kamishna atahitaji kuwa na karani, msaidizi wa kibinafsi na dereva.

Kiranja wa walio wachache katika bunge Junet Mohammed anaunga makamishna wa muda kwa sababu jukumu lao ni la kutoa ushauri.

“Kazi yao kuu ni kushauri serikali kuhusu mishahara na masharti ya kazi ya watumishi wa umma. Baada ya kufanya hivyo, watakuwa wakifanya kazi gani? aliuliza.

 

Pwani yaapa kujisuka upya kuingia serikalini 2022

Na KAZUNGU SAMUEL

VIONGOZI wa Pwani wanapanga kuungana na kuwa katika serikali mwaka wa 2022 na wakapendekeza kuwa Gavana wa Kilifi, Amason Kingi aongoze kampeni hiyo.

Wengi wakiwa wanasiasa, walisema Jumamosi wakati wa mazishi ya waliyekuwa mbunge wa Ganze, marehemu Joseph Kingi kwamba wameanza harakati za kutimiza azimio la umoja wa Pwani.

Gavana Kingi aliwataka wanasiasa wakongwe na viongozi wa kidini kuhakikisha azimio la umoja wao linafanikiwa.

“Ikiwa mimi niko tayari, mwingine pia awe tayari na mwingine vile vile. Tukifanya hivyo kama wakazi wote wa Pwani, basi lengo letu la kuwa katika serikali tukiwa kitu kimoja litafaulu,” akasema Gavana Kingi.

Mazishi hayo yalifanyika katika kijiji cha Mitsemerini, Bamba na kuhudhuriwa na miongoni mwa wengine, mkuu wa majeshi Jenerali Samson Mwathethe.

Viongozi hao ambao walikuwa ni wabunge wa sasa na wa zamani, walisema maeneo mengine ya Kenya yanaheshimiwa kwa kuwa viongozi wote wanaongea kwa sauti moja.

Mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana alisema kuna haja ya kuwa na msimamo kati ya wakazi wa Pwani na viongozi wao ili kutoyumbishwa katika siasa.

“Mara hii tunataka kuwa katika nyumba yetu. Hii tabia ya kushika nyumba za wengine haitatusaidia.

Tunashukuru kwamba baada ya Bw Raila Odinga na RaisUhuru Kenyatta kushikana mikono, kile ambacho  tumeona sasa ni utulivu wa nchi. Lazima tufurahie hatua hii ambayo viongozi wetu walichukua,” akasema Bw Katana.

Wanasiasa wengine walikuwa Teddy Mwambire (Ganze), Ken Chonga (Kilifi Kusini), Asha Jumwa (Malindi), Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na Mwakilishi wa akina mama wa Kaunti Bi Mbeyu Mwanyanje.

Waliowahi kuwa wabunge ni pamoja na Gunga Mwinga, Abdalla Ngozi, Francis Baya, Morris Dzoro, Katana Ngala na Gonzi Rai.

Bw Mwambire alisema kuwa umoja wa viongozi wa Pwani umetatizwa mara nyingi na chuki pamoja na masengenyo na wivu miongoni mwa viongozi wenyewe.

 

Kuimarisha umoja

“Tunataka sasa kuhakikisha kwamba tunatimiza lengo kamili la umoja wetu. Lakini tatizo linakuja wakati ambapo chuki huanza kuwaingia viongozi na kuanza kupigana vita, kuchongeana na kubezana. Wakati tukiacha hili, basi tutafanikisha azimio letu la umoja,” akasema.

Naye Bi Jumwa alisema kuwa tayari eneo hilo liko na umoja lakini kinachosumbua ni kuwa bado hakujapatikana kiongozi ambaye ataweza kuwaleta pamoja kama Wapwani.

“Gavana Kingi yuko hapa lakini tatizo letu ni kuwa kila kiongozi ambaye anajitokeza kutaka kutupeleka mbele anapingwa. Hili ni tatizo kubwa kwetu na ni lazima tubadilike,” akasema Bi Jumwa.

Bw Owen alisema gavana anatosha kuchukua usukani kama kiongozi wa Pwani na kuwapeleka katika serikali mwaka wa 2022.

Aliyekuwa mbunge wa Kaloleni Bw Gunga pia alisema eneo la Pwani linatatizika kwa sababu halina viongozi ambao wanaweza kusukuma sera za eneo hilo kitaifa.

“Lazima tupate kiongozi ambaye atatushika mkono kama Pwani na kutuweka pamoja katika mizani ya maendeleo,” akasema.

 

Mwili wa mwanamke aliyetoweka wapatwa umezikwa shambani

Na PETER NJERU

MWILI wa mwanamke aliyepotea kwa karibu wiki moja ulipatikana Jumapili ukiwa umezikwa kwenye shamba la mahindi katika eneo la Magutuni kaunti ya Tharaka-Nithi. 

Mwili huo uliokuwa umeanza kuoza uligunduliwa na mmiliki wa shamba hilo, ambaye alipiga ripoti kwenye kituo cha polisi cha Ntumu na maafisa wa polisi wakauchukua na kupeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Chuka.

Afisa mkuu wa polisi wilayani Chuka/Igambang’ombe Bw Barasa Sayia aliiambia Taifa Leo kuwa polisi wameanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo.

“Polisi walichukua mwili na kupeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti na wakaanzisha uchunguzi mara moja,” alisema Bw Sayia.

Tukio hilo la mauaji liliwaghadhabisha  wakazi ambao waliomba polisi kufanya uchunguzi wa kina na kumkamata muuaji.

Bw John Kithinji, momoja wa wakakijiji aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtu anayejulikana na wenyeji kama, Bw Mutembei alikuwa mtuhumiwa wao mkuu.

“Mwanamke huyu amekuwa akihishi katika chumba kimoja na Bw Mutembei na kwa wiki moja iliyopita, wawili hao hawajaonekana,” alisema Bw Kithinji.

Bi Mary Gatwiri, mwanakijiji mwingine alisema usiku wa Jumatatu ya wiki jana, walisikia kelele iliyokuwa ikitoka  kwenye chumba ambacho marehemu aliishi na mtu huyo na asubuhi iliyofuata, wawili hao hawakuonekana.

Wakazi hao walilalama kuwa watu wengi wameuawa katika eneo hilo kwa kipindi cha miezi michache iliyopita na wakaomba polisi kuongeza usalama.

Aidha, wakaazi walisema kuongezeka kwa matumizi ya pombe haramu kwenye eneo hilo ni swala ambalo limechangia pakubwa kuongezeka kwa uharifu.

“Eneo hili linauzwa haina zote za pombe haramu na madawa wa kulevya sanasana bhangi,” alisema Bw Julius Mugendi, mwenyeji mwingine.

 

Jombi ageuzwa gumzo mtaani kwa kuoa ajuza

Na JOHN MUSYOKI

KIVANDINI, MATUU

KULIWA na kioja hapa mzee mmoja alipozomea mwanawe kwa kuoa mwanamke aliyemzidi umri.

Inasemekana jamaa alikuwa kapera kwa muda mrefu lakini alipoamua kuoa, alishangaza watu  kwa kuoa mwanamke mzee kumliko hadi akawa ngumzo kijijini.

“Jamaa alioa mwanamke mzee sana hadi watu wakawa wanamsema jambo ambalo halikumfurahisha baba yake.

Siku ya kioja, baba ya jamaa alipogundua kuwa watu walikuwa wakimkejeli mwanawe kwa kuoa mwanamke mzee, alienda kwa mwananawe na kuanza kumkemea.

“Nimepata habari kuwa eti mwanamke uliyemuoa majuzi ni mzee kukuliko.

Kwa nini ulioa mwanamke mzee na kuna mabinti wa umri mdogo na wabichi wa kuchumbia?

Una akili timamu ama ulirushiwa ndumba na mwanamke huyo? Watu kijijini wanakusema kila kuchao kuwa haukufanya vizuri kuoa mwanamke huyu mzee,” baba ya polo alilalamika.

Alimtaka kumtimua mwanamke huyo na kutafuta mwingine wa kuoa ikiwa alitaka baraka zake za kuanzisha familia.

Hata hivyo, jamaa alikanusha madai ya babake ya kumtaka amfukuze mkewe kwa sababu alikuwa  mzee kumliko.

“Wacha wanaosema waseme. Watasema mchana lakini usiku watalala. Kinachowawasha ni kipi? Hata kama nilioa mwanamke mzee kuniliko, shida yao ni gani?

Ndio nilioa mwanamke mzee lakini hawana nafasi ya kukatiza mapenzi yetu kwa kusema au wewe kuja kunizomea kama mtoto.

Hata kama mke wangu ni mzee nilimchagua kwa sababu nilimpenda. Hakuna  aliye na haki ya kuingilia ndoa yangu na sitakubali upuzi huo,” kalameni alisema.

Ilibidi buda kuuma kona kalameni aliposhikilia msimamo wake na kukataa kumfukuza mkewe.

Alimweleza mzee kutokanyaga kwake kujadili mkewe. Hata hivyo haikujulikana iwapo ndoa yao ilidumu baada ya mzee kukosa kuwapa baraka.

…WAZO BONZO…

Ligi ya Super 8 yashika kasi

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Shauri Moyo Blue Stars walitoka nyuma na kusajili ushindi wa kipekee wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao Zamalek FC katika mtanange wa ligi ya Super 8 uliovutia idadi kubwa ya mashabiki uwanjani Ziwani Jumapili.

Mshambulizi Papalai Morio aliifunga penalti safi dakika za majeruhi na kuwapa ushindi Shauri Moyo wanaoshikilia nafasi ya pili hii ikiwa ushindi wao watano mfululizo katika mechi saba walizosakata.

Timu hiyo sasa imezoa alama 16 wakiwa na upungufu wa alama nne ili kufikia viongozi Makadara Junior League SA.

Klabu hiyo kutoka mtaa wa Kamukunji walichukua uongozi wa mechi dakika ya tano kupitia mshambulizi Erick Kyalo mechi ikianza kabla ya wageni kusawazisha  kupitia ikabu ya Godfrey Gladson dakika tatu baadaye.

Kocha wa Blue Stars Ken Odera aliwapongeza wachezaji wake kwa kupigana hadi mwisho kupata ushindi huo.

“Nawapongeza vijana wangu kwa kudhihirisha soka ya juu na kupigana kufa kupona hadi mechi ikakamilika. Tunalenga kufanya vivyo hivyo katika mechi zijazo,” akasema Kocha Odera.

Kufuatia kichapo hicho Zamalek waliokuwa wakitafuta ushindi wao wa pili msimu huu wanashikilia nafasi ya 15 kwa alama tano na kocha wao Julius Katenge anaamini bado wana nafasi ya kuimarika.

“Tulipigana kiume na kusawazisha bao walilotufunga lakini matokeo yakawa vinginevyo. Tunalenga kujiimarisha kwenye mechi zijazo ili kuboresha matokeo yetu,” akasema baada ya mechi.

Viongozi wa ligi Makadara Junior League SA ndiyo walivuna pakubwa wikendi iliyopita baada ya kuandikisha ushindi wa kuridhisha wa mabao 5-0 dhidi ya Leads United uwanjani Camp Toyoyo.

Mshambulizi Tyrone Yara scored aling’aa kwa kufunga mabao matatu huku Zidane Ochieng’ na nahodha Billy Mutsami wakifunga bao moja kila moja kudumisha mwanya wa alama nne uongozini.

Katika matokeo mengine timu ya Makongeni Sports Association (MASA) Jumamosi ilipitia fedheha baada ya kucharazwa mabao 2-0 na Jericho All-Stars ugani Camp Toyoyo.

Vijana wa Chuo Kikuu cha TUK walipoteza 4-2 dhidi ya RYSA na kuzidi kusalia mkiani mwa jedwali.

Na kwenye uwanja wa Posta mjini Ngong NYSA waliwalambisha sakafu Melta Kabiria kwa mabao 3-2.

Ni udhalimu kuongeza bei ya mafuta taa, Wakenya walia

NA PETER MBURU

WAKENYA wengi hawajafurahishwa na wazo la Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) nchini kutaka bei ya mafuta taa ipandishwe, na wanalichukulia kuwa hatua itakayowaadhibu Wakenya masikini, Taifa Leo imebaini.

Wakenya wanaitaka serikali kutochukua hatua hiyo kwani wanahisi itawaathiri vibaya watu wa mapato madogo, ambao ni sehemu kubwa ya taifa.

Wale waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuwa endapo itachukuliwa, hatua hiyo itaishia kuwaumiza watu wasio na kazi, wenye mapato madogo, wazee katika jamii na masikini ambao kwa jumla wanaunda sehemu kubwa ya wakenya.

Walisema ni vikundi hivyo vinavyotumia mafuta taa kwa wingi kama mbinu ya kupata mwangaza nyumbani na pia kwa kupikia kwa stovu.

“Kupandisha bei ya mafuta taa kutaishia kuniathiri vibaya pamoja na maelfu ya Wakenya wenzangu ambao hatuna pesa kwani yanatusaidia katika shughuli za nyumbani. Ninayatumia kwa upishi kila siku,” akasema Joseph Mwaura, mfanyakazi wa vibarua mjini Nakuru.

Wengi wa waliohojiwa walisema mbeleni walitegemea makaa kwa upishi lakini wakahamia kutumia mafuta taa baada ya serikali kupiga marufuku ukataji miti kwa ajili ya kuchoma makaa.

Watu wengine walitilia shaka uwezo wa serikali kuleta bidhaa mbadala za kutosha kwa niaba ya mafuta taa na kwa bei itakayowiana na ya mafutaa kwa sasa.

“Watu wengi hupenda kutumia mafuta taa kwani bei yake ni rahisi na hivyo familia hutumia kama Sh30 pekee kwa siku au hata chini kupata mwangaza na kupika. Tunashangaa kama mbinu mbadala inazoahidi serikali zitakuwa rahisi hivyo ama zitakuja kuchukua pesa zaidi,” akasema Bi Angela Jeruto, mkazi wa Rongai.

Wakenya wengi, haswa maeneo ya mashambani ambapo umeme haujapenyeza na maeneo ambayo kupotea kwa nguvu za umeme ni hali ya kila siku bado wanatumia mafuta taa kwa wingi.

Wiki iliyopita, tume ya ERC ilirai serikali kupandisha bei ya mafuta taa kufikia ile ya dizeli, kama mbinu ya kuwakomesha Wakenya kununua bidhaa hiyo.

Kulingana na ERC, wazo hilo lilikuja baada ya kubaini kuwa matumizi ya mafuta taa nchini yamezidi kufikia kiwango cha lita milioni 33 kwa mwezi, ilhali inafaa kuwa chini ya lita milioni tano kwa kipindi hicho.

Mamlaka hiyo ilikosoa matumizi hayo ikisema zaidi ya asilimia 80 ya kiwango cha mafuta yanayotumiwa nchini kiliishia kwa magari, kutokana na hulka mbaya ya wanabiashara watundu kuchanganya bidhaa hiyo na mafuta ya dizeli na kuwauzia watumizi wa magari bila kujua.

“Zaidi ya lita milioni 27 zinaishia kutumiwa na magari jambo ambalo limeharibu magari mengi. Jambo hili aidha limeharibia Kenya soko la nje la mafuta ya dizeli na hivyo kuishia kupoteza ushuru wa Sh34bilioni,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa ERC Pavel Oimeke wiki iliyopita.

Kulingana na tume hiyo, kampuni kadhaa zitapewa kandarasi kusambaza bidhaa mbadala kwa bei iliyopunguzwa na serikali kama njia ya kupunguza ukali wa mabadiliko yanayotarajiwa.

Kitambi atajwa kocha bora wa mwezi KPL

Na JOHN ASHIHUNDU

Kocha wa AFC Leopards anayeondoka, Dennis Kitambi ametawazwa Kocha Bora wa Mwezi Aprili KPL.

Katika uteuzi huo uliofanywa na waandishi wa habari za michezo, Kitambi, alijinyakuliwa Sh75,000, bali na kombe kutoka kwa wadhamini wa tuzo hiyo, Fidelity Insurance.

Raia huyo wa Tanzania aliibuka mshindi baada ya kuwaongoza vijana wake kupata ushindi mara nne mwezi Machi, muda mfupi baada ya kuchuua usukani kutoka kwa Robert Matano.

“Nimeifurahia zawadi hii ambayo nimeipata wakati nikijipanga kuondoka. Nawashukuru wachezaji pamoja na wenzange tuliokuwa nao katika idara ya ukufuzni muda wote nimekuwa hapa nchini Kenya. Ufanisi wangu umetokana na msaada wa kila mtu aliyeniunga mkono.

“Naondoka japo kwa roho ngumu, lakini muda wangu wa kuondoka umefika kuambatana na mkataba wangu na Ingwe. Namtakia kocha anayechukua nafasi yangu ufanisi katika majukumu yake,” Kitambi alisema.

Kitambi ametwaa tuzo hiyo baada ya awali mshambuliaji Ezekiel Odera pia wa Ingwe kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Machi.

Kitambi ataondoka nchini kesho kuelekea Bangladesh ambako atajiunga na basi wake wa zamani, Stewart Hall anayeandaa klabu ya Saif Sporting Club.

Ingwe wanashikilia nafasi ya tano jedwalini wakiwa na pointi 21 kutokana na mechi 14 wakati huu wakijiandaa kucheza na Nakumatt juma lijalo.

Kipa Oluoch aikosesha Gor ushindi ugenini Rwanda

Na JOHN ASHIHUNDU

Mashabiki wa Gor Mahia kwa mara nyingine wamefedheheshwa na uchezaji wa kipa Boniface Oluoch ambaye kosa lake liliisaidia Rayon Sports kufunga bao la kusawazisha katika sare yao ya 1-1, ugenini mjini Kigali.

Gor Mahia walitangulia kufunga bao katika mechi hiyo iliyochezewa Nyamirambo Stadium, Jumapili usiku.

Wakati huo huo, haijajulikana itakapochezewa mechi ya pili ya Mei 16 kati ya mabingwa hao wa ligi kuu nchini na klabu ya USM Alger ya Algeria, wakati huu maafisa wao wanasubiri kufahamishwa iwapo uwanja wa MISC Kasarani utakuwa umekamilika.

Akizungmza na waandishi jana, Naibu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ronald Ngala alisema jana kwamba huenda mechi hiyo ikaamishiwa Kenyatta Stadium mjini Machakos ikiwa uwanja wa Kasarani utakuwa haijakamilika.

“Tunangojea kufahamishwa kuhusu uwanja wa Kasarani ili tuwasiliane na CAF. Uwanja wa Machakos utabakia kuwa mbadala kwa sasa,” alisema.

USM Alger wanaongoza Kundi D baada ya kuitandika Young Africans ya Tanzania kwa 3-0 mwishoni mwa wiki, ambapo mechi yao dhidi ya K’Ogalo Jumatano ijayo ni muhimu kwa timu zote.

Sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Rayon Sport imewaacha Gor Mahia katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo ambapo lazima waandishe ushindi katika mechi ijayo ili kufufua matumaini ya kusonga mbele ili kufuzu kwa hatua ya 16 bora.

Dhidi ya Rayon Sports, kipa wao chaguo la kwanza Boniface Oluoch amelaumiwa kutokana na bao walilofungwa dakika ya 24 kufuatia fri kiki ya Erick Rutanda in the 24thminute.

Oluoch, amewahi kufungwa mabao kama hayo katika mechi muhimu, hali ambayo imezua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo.

Bao hilo lilivuruga matumaini ya Gor Mahia ambao walitangulia kufunga mapema kupitia kwa Meddie Kagere.

Kagere ambaye alionyeshwa kadi ya njano kwa mara ya pili ataikosa mechi hiyo.

Kwingineko, beki wa Harambee Stars David Owino Jumamosi alifunga bao lake la kwanza katika mashindano ya bara  akiwajibikia timu yake ya Zesco United katika kipute cha kuwania klabu bingwa barani Afrika.

Zesco United ilikuwa ikichuana na Mbabane Swallows kutoka Swaziland kipute kilichoishia sare ya 1-1 ugani Levi Mwanawasa eneo la Ndola nchini Zambia.

Beki huyo wa zamani wa Gor Mahia alitia wavuni bao hilo muhimu katika dakika ya 65 huku wapinzani wao wakibahatika kuona lango zikiwa zimesalia dakika kumi mechi ikamilike.

Katika matokeo mengine vigogo wa soka barani Al Ahly kutoka Misri na Esperance kutoka Tunisia walitoshana nguvu kwa sare tasa katika mechi ya kwanza ya kundi A iliyogaragazwa juzi.

Minnows Township Rollers ya Uswazi walionyesha Kampala City kutoka nchi jirani ya Uganda vimulimuli kwa kuwapokeza kichapo chembamba cha 1-0 na kuchukua uongozi wa mapema wa kundi A.

Kundi B ilishuhudia TP Mazembe kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakichukua uongozi baada ya kuwabamiza wapinzani wao Entente Setif kutoka Algeria mabao 4-1.

Timu nyingine katika kundi hilo Moulodia Alger kutoka Algeria na Difaa el Jadida ya Morocco ziliagana sare ya 1-1.

Katika matokeo mengine ya makundi, WAC Casablanca ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo waliagana sare ya 1-1 na Mamelodi Sundowns kisha Togo Port wakakalifishwa 2-1 na Klabu ya Horoya kutoka Guinea.

Michuano ya mwaka huu inatarajiwa kunoga zaidi kwa sababu timu ambazo zinashiriki zimeonyesha nia ya kuwa wagombezi halisi na zinatarajia kumaliza ubabe wa miaka mingi wa klabu za Esperance, Al Ahly, TP Mazembe na WAC Casablanca.

OBARA: Serikali isibadili sembe bila ruhusa ya raia wake

Na VALENTINE OBARA

WIKI iliyopita nilipigwa na butwaa nilopofahamishwa kwamba serikali imenuia kuunda sera ambayo itawalazimu wasagaji mahindi kuchanganya unga huo na ule wa nafaka nyinginezo kama vile mtama, wimbi na mihogo.

Pendekezo hilo lililotangazwa na Katibu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia masuala ya mimea na sera, Bw Richard Lesiyampe, linalenga kupunguza jinsi wananchi hula kiwango kikubwa cha mahindi kila mwaka kuliko kile tunachozalisha.

Hakuna ubaya kuchanganya unga wa nafaka hizi kwani hiyo hufanywa na wanaotaka kwa hiari, lakini tatizo lililopo ni kwamba sera hiyo ilivyopendekezwa itaingilia biashara za watu binafsi isivyofaa.

Ulimwenguni kote jukumu la serikali huwa ni kubuni sera ambazo, mbali na kulenga kuboresha maisha ya wananchi wake, hutoa mazingira bora kwa wawekezaji kuendesha biashara zao bila kutatizwa isivyostahili.

Humu nchini inafahamika wazi kwamba unga wa mahindi ni bidhaa muhimu jikoni ndiposa kunapokuwa na uhaba wake, huwa taifa linaingia hofu kwani wengi huhisi kuna janga kuu la ukosefu wa chakula.

Hali huwa hivi hata kama kuna vyakula vingine sokoni kama vile mchele na viazi ambavyo virutubishi vyao vinaweza kuchukua mahala pa mahindi.

Hakika, wawekezaji katika biashara ya kilimo cha mahindi kwenye mashamba makubwa, uagizaji mahindi kutoka mataifa ya nje na utengenezaji wa unga wa mahindi wanafahamu fika jinsi Wakenya wanavyoenzi ugali wa mahindi na hivyo basi faida iliyo katika biashara hii.

Faida ni lengo kuu la biashara yoyote ile, na ni kutokana na faida hii ambapo serikali hupata ushuru wa kutosha kuendeleza majukumu mengine ya kujenga nchi.

Kwa hivyo sera yoyote inayopendekezwa na kupitishwa haifai kudhuru uwezo wa mfanyabiashara kupata faida zake.

Hatari iliyopo kuhusu pendekezo la Bw Lesiyampe ni kwamba linaweza likasababisha hasara kwa waekezaji na athari zake hazitapendeza.

Ingekuwa vyema kama tungeelezwa pendekezo hili lina msingi wake kwa utafiti upi ambao ulipata kuwa Wakenya watajitolea kununua unga wa ugali wenye mchanganyiko wa nafaka.

Kwa mtazamo wangu, hili ni suala ambalo kwanza litahitaji mchango wa wananchi kwani masuala ya unga si ya kufanyiwa mzaha katika nchi hii.

Ni bora serikali iweke mawazo yake na rasilimali kwa juhudi ambazo zinaendelezwa kuongeza kiwango cha mahindi kinachozalishwa kama vile kilimo cha unyunyizaji maji mashambani badala ya kuleta mapendekezo ambayo hayana msingi.

Ilivyo kwa sasa, takwimu zinaonyesha kuwa Kenya huzalisha karibu magunia milioni 40 ya mahindi na kutumia magunia milioni 30 kila mwaka, lakini kuna lengo la kupunguza matumizi hadi milioni 20 ili kusiwe na hatari endapo kutakuwa na mahitaji ya dharura.

Kile ambacho serikali pengine inaweza kufanya kama ina lazima kupunguza matumizi, ni kuweka ushuru kwa unga wa mahindi matupu, na kuondoa ushuru kwa bidhaa nyingine zinazoweza kuchukua mahala pa unga wa mahindi ikiwemo unga huo wa mchanganyiko ambao unaweza kuleta hasara kwa biashara.