Aliyefanyiwa upasuaji vibaya akijifungua Gatundu afariki

Na LAWRENCE ONGARO

MWANAMKE aliyefanyiwa upasuaji vibaya alipokuwa akijifungua katika hospitali ya Gatundu Level 4 wiki mbili zilizopita, alifariki wikendi.

Mama huyo wa miaka 30 alikuwa ameenda katika hospitali hiyo alipopatwa na uchungu wa uzazi na akazaa mtoto wa kiume kupitia upasuaji.

Kulingana na nduguye, Bw Mwangi Kanyingi, siku tatu baada ya kurejea nyumbani, alihisi maumivu makali tumboni na akarejeshwa katika hopsitali hiyo, lakini madaktari wakapendekeza apelekwe Thika Level 5 kwa matibabu zaidi.

“Sisi kama familia tulimpeleka tena hadi Thika ili afanyiwe uchunguzi zaidi. Baadaye alilazwa huko kwa mara nyingine, huku madaktari wakipendekeza afanyiwe  upasuaji mara nyingine ili kubaini tatizo. Baada ya upasuaji huo wa pili, alivuja damu nyingi na kuaga dunia,” alisema Bw Kanyingi.

Waziri wa Afya  katika Kaunti ya Kiambu, Dkt Joseph Murega alisema wanachunguza chanzo cha marehemu kuvuja damu nyingi.

“Tayari tumewasilisha chembe chembe za damu yake katika mahabara  ya serikali jijini Nairobi ili ifanyiwe uchunguzi zaidi kubainisha sukweli wa mambo,” alisema Dkt Murega.

 

Mvua zaidi yaja, Idara ya Utabiri yasema

Na WAANDISHI WETU

MVUA inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo tofauti ya nchi wiki hii, huku mafuriko yakizidi kusababisha uharibifu.

Kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, msimu wa mvua utaendelea mwezi huu na maeneo kama vile Magharibi, Kati, Rift Valley na Pwani ndiyo yataathirika zaidi, mbali na sehemu kadhaa za Mashariki na sehemu chache Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kufuatia hali hii, Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) tawi la Mandera, kimeomba wakuu wa shule za eneo hilo na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuruhusu walimu wachelewe kurudi shuleni kwa muhula wa pili kutokana na jinsi barabara zilivyoharibiwa na mvua.

Katibu Mkuu wa chama hicho Mandera, Bw Kulow Mohamed, alisema walimu wengi wamekwama katika maeneo mbalimbali ya Kaskazini Mashariki kwa sababu ya mafuriko.

Alisema barabara zimeharibika na hazipitiki katika Kaunti za Marsabit, Garissa, Wajir na Mandera.

“Walimu wakuu na TSC wataanza kuwaadhibu walimu hawa bila kujali matatizo yanayowakumba katika msimu huu wa mvua ambao husababisha shida za usafiri,” akasema.

Katika eneo la mashariki, Serikali Kuu imeanza kusambaza chakula cha msaada kwa wakazi wa nyanda za juu za mashariki mwa Kenya, ikiwemo Kaunti za Isiolo na Marsabit, ambao nyumba zao ziliharibiwa na mafuriko.

Mratibu wa serikali katika eneo la Mashariki, Bw Wycliffe Ogallo, alisema walifanya ukaguzi kutoka angani wakatambua maeneo yaliyoathirika zaidi ni Iloret na Loiyangalani, katika kaunti hizo mbili.

Akizungumza akiwa mjini Embu, alisema mpango wa kutoa misaada utaenezwa hadi maeneo mengine yaliyoathirika.

“Tutatumia helikopta kusambaza vyakula katika maeneo hayo ili kuhakikisha hakuna atakayelala njaa,” akasema, na kuomba wanaoishi katika maeneo ambapo hukumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi wahamie maeneo salama.

Hasara iliwakumba wakazi wa eneo la Mariashoni, Elburgon wakati ng’ombe watatu na kondoo watano waliposombwa na mafuriko.

Mimea na miti pia iliharibiwa huku mvua ikizidi kunyesha katika maeneo mengi ya kaunti ndogo za Elburgon na Molo.

 

Uharibifu

Bw Samwel Kipchumba alisema mahindi yake katika ekari tatu ya shamba yaliharibiwa huku wakazi wakishangaa kwani hawajawahi kushuhudia mvua kubwa namna hiyo kwa miaka mingi.

Mvua hiyo iliyonyesha usiku wa Alhamisi pia ilitatiza usafiri katika barabara ya Elburgon kuelekea Nakuru katibu na soko la Kamwaura eneo la Njoro, baada ya bwawa la Tarakwet kuvunja kingo zake.

Usafiri kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen pia unaendelea kutatizwa na mvua kubwa ambayo imepelekea sehemu kadha za barabara hiyo kuharibika. Mnamo Jumapili, madereva na wasafiri waliokuwa kwenye msafara wa kwanza wa mabasi ya usafiri wa umma walilazimika kukaa eneo la Milihoi kwa zaidi ya saa moja baada ya daraja kwenye eneo hilo la barabara kusombwa na maji ya mafuriko.

Aidha msafara wa pili wa mabasi hayo ya usafiri wa umma haungeweza kuvuka eneo hilo, hivyo kulazimisha abiria zaidi ya 200 waliokuwa tayari wamekata tiketi kuelekea Malindi na Mombasa kukatiza safari zao.

Wasafiri wengine waliokuwa kwenye magari madogo ya kibinafsi na pikipiki wakielekea Mpeketoni na Mombasa pia walikatiza safari zao na kurudi Hindi, Mokowe na Lamu baada ya kushindwa kuvuka eneo hilo la Milihoi.

Ripoti ya VALENTINE OBARA, CHARLES WANYORO, MANASE OTSIALO, JOHN NJOROGE na KALUME KAZUNGU

Niko tayari kuungana na UhuRaila kuunganisha Wakenya – Kalonzo

Na FRANCIS MUREITHI

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema yuko tayari kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta katika juhudi za kuunganisha Wakenya na kuzika siasa za mgawanyiko.

Bw Musyoka alipongeza hatua ya Rais Kenyatta kuanza mikakati ya kuunganisha Wakenya kwa ushirikiano na kinara wa NASA Raila Odinga mnamo Machi 9, mwaka huu.

Bw Musyoka pia alimpongeza rais kwa kuomba msamaha kwa kutoa matamshi ya kugawanya Wakenya wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2017.

Makamu huyo wa rais wa zamani, alisema hayo alipokuwa akihutubia wanahabari katika hoteli moja eneo la Elementaita, Nakuru wakati wa kufunga kongamano la siku mbili la viongozi wa Wiper.

“Ningependa kumpongeza Rais Kenyatta kwa kujitokeza wazi na kuomba Wakenya msamaha. Ni viongozi wachache mno wanaoweza kunyenyekea na kuomba wananchi msamaha. Nimempa hongera kwa hilo. Huu ni wakati wa kusamehe na kuhubiri amani,” akasema Bw Musyoka.

 

Kukutana na Mzee Moi

Bw Musyoka alisema anapanga kukutana na Rais Mstaafu Daniel arap Moi hivi karibuni.

“Ninapanga pia kumtembelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki na mama yake rais, Mama Ngina Kenyatta,” akasema Bw Musyoka.

Bw Musyoka alimkejeli Naibu wa Rais William Ruto ambaye juhudi zake za kukutana na Mzee Moi ziligonga mwamba wiki iliyopita.

“Walioshindwa kumwona Rais Mstaafu Moi wajaribu tena,” akasema Bw Musyoka huku akisababisha kicheko.

Alisema mwafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unastahili kuleta maendeleo na wala si kusuluhisha mizozo ya kisiasa tu.

Alisisitiza kuwa muungano wa NASA bado ni thabiti huku akisema kuwa atashinikiza NASA isajiliwe kama chama cha kisiasa. Alisema Bw Odinga hajajiunga na chama cha Jubilee na bado yuko katika Upinzani.

Alisema kabla ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kusalimiana, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kushinikiza viongozi hao wawili wakutane ili kuzungumza.

“Nilikuwa katika mstari wa mbele kuwataka Rais Kenyatta na Bw Odinga wakutane na kusitisha siasa za mgawanyiko. Inaonekana Bw Odinga alisikia wito wangu na akakubali kukutana na Rais Kenyatta japo hakunifahamisha,” akasema Bw Musyoka.

“Chama cha Wiper kiko tayari kuanzisha mchakato wa kuunganisha nchi na kuhubiri amani,” aliongeza.

Bw Musyoka pia alisema anaunga mkono Katiba kufanyiwa mabadiliko.

“Niliitwa tikitimaji kwa sababu nilisema kuwa Katiba ilifaa kuangaliwa kwa makini. Sasa Wakenya wameona umuhimu wa niliyosema.

Chama cha Wiper kinaunga mkono mabadiliko ya Katiba na tunafaa kujadili suala hili kwa makini,” alisema Musyoka.

Waathiriwa wa mafuriko Afrika Mashariki wakodolea macho njaa

Na CHRIS OYIER

Kwa muhtasari:

  • Nchi za Afrika Mashariki zimekumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha eneo hilo
  • Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya takriban wati 120 nchini Kenya, watu 116 nchini Rwanda, 14 nchini Tanzania na watu 3 nchini Uganda
  • Mafuriko hayo yaliyoshuhudiwa yamewaacha maelfu ya raia bila makazi  na chakula
  • Huenda tukio hilo likasababisha njaa katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo

TOFAUTI na ukame ulioshuhudiwa mwanzoni mwa mwaka wa 2017 katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, mwaka wa 2018 umekuwa tofauti kwani mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha yasababisha mauti, kuharibu nyumba na mali huku kilimo kikipata pigo. 

Hali hiyo imeshuhudiwa katika nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya ambapo kulingana na shirika la Msalaba Mwekundu, takriban watu 120 wamefariki na maelfu wengine kuachwa bila makao katika kaunti 32 zilizoathirika zaidi na mafuriko.

“Familia 48, 177 zimeachwa bila makao, hali ambayo inawaacha jumla ya watu 260,200 bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji,” Katibu Mkuu wa shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya Abbas Gullet alisema.

Nchini Tanzania, hali ni mbaya kwani watu 14 wameripotiwa kufariki huku Uganda ikiandikisha vifo vya watu 3.

Kulingana na jarida la Uganda la New Vision, wanajeshi wa AMISOM nchini Somalia waliwaokoa takriban watu 10,000 kutoka eneo la Beledwenye, kusini mwa nchi hiyo ambayo nyumba, mifugo na mimea ilisombwa na maji.

Nchini Rwanda watu 116 waliripotiwa kufariki kutokana na mafuriko huku mamia ya watu wengine wakiachwa bila makao.

Waathiriwa wa mafuriko wanaishi kwa hofu ya kutegemea msaada baada ya mimea yao kusombwa na maji katika nchi hizo.

Ijumaa, Mei 4, shirika la Msalaba Mwekundu liliwaomba Wakenya kuisaidia kuchangisha Sh500 milioni ili kushughulikia mahitaji ya waathiriwa wa mafuriko ambao wanahitaji vyakula, malazi, dawa na vifaa vya kutumia.

Hata hivyo, shirika hilo lilikiri kuwa kukabiliana na athari za mafuriko kutachukua muda, ikizingatiwa kuwa linategemea msaada kuwapa waathiriwa hao chakula.

Mwezi Machi, serikali ya kaunti ya Nairobi ilitenga KSh 194 milioni kurekebisha miundo msingi ili kuzuia mafuriko katika sehemu kadhaa za jiji.

Serikali kuu nchini Kenya haijatangaza itakavyowasaidia waathiriwa na mafuriko ambao wako kwenye hatari ya kukosa chakula kutokana na mimea yao kusombwa na maji na ikizingatiwa hawawezi kurejea katika mashamba yao yaliyofurika kwa sasa kuendeleza kilimo.

Nimeishiwa na ladha ya ugavana, asema Kidero

Na BARACK ODUOR

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi, Evans Kidero, amekanusha madai kwamba anapanga kugombea kiti cha ugavana kaunti ya Homa Bay akisema ananuia kugombea kiti kikubwa.

Kauli yake inajiri baada ya kudaiwa kwamba anapanga kugombea kiti hicho ushindi wa Gavana Cyprian Awiti ulipobatilishwa na Mahakama Kuu. Gavana Awiti alikata rufaa akitaka uamuzi wa Mahakama Kuu ufutiliwe mbali.

Akiongea kwenye harambee ya kusaidia shule ya sekondari ya Wikoteng’ iliyo Asumbi, Homa Bay mnamo Jumamosi, Bw Kidero alisema anapanga kugombea kiti kikubwa ambacho hakutaja. Kabla ya uchaguzi mkuu uliopita, Bw Kidero alikuwa ametangaza kuwa atagombea urais 2022.

“Wale ambao wamekuwa wakisema kwamba ninataka kumuondoa Gavana Awiti iwapo kutakuwa na uchaguzi mdogo wanafaa kukoma kwa sababu sio ukweli. Nitagombea kiti kikubwa,” alisema Bw Kidero.

Alitumia fursa hiyo kumshambulia mrithi wake katika kaunti ya Nairobi – Mike Sonko, akisema ni wazi kuwa hawezi kubadilisha jiji la Nairobi. “Tutarejesha Nairobi sifa zake za awali kwa sababu wale walio uongozini wameshindwa,” alisema.

Aliwaomba wakazi wa Homa Bay kuunga miradi ya maendeleo ya Gavana Awiti akisema miaka mitano ya kwanza ilikuwa ya kuweka msingi. Hata hivyo, alimtaka Bw Awiti kuwafuta kazi maafisa wa kaunti wazembe.

Aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi katika serikali ya Kidero George Wainaina alisema Gavana Sonko ameshindwa na kazi. Wabunge Ayub Savula (Lugari), Lilian Gogo (Rangwe) na Elisha Odhiambo (Gem) walimuunga Dkt Kidero kwamba Sonko ameshindwa kuwahudumia wakazi wa Nairobi.

 

JAMVI: Wito wa Atwoli watikisa msingi wa chama cha Jubilee

Na BENSON MATHEKA

WITO wa kutaka mabadiliko ya katiba ili Rais Uhuru Kenyatta aendelee kuhudumu serikalini baada ya kumaliza kipindi chake cha pili 2022, ni pigo kwa ustawi wa demokrasia nchini na linaweza kusambaratisha chama cha Jubilee.

Na ingawa baadhi ya washirika wa rais wanapinga pendekezo lililotolewa na katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Cotu Francis Atwoli, kwamba katiba ibadilishwe kubuni wadhifa wa waziri mkuu kumwezesha Rais Kenyatta kuendelea kushiriki siasa baada ya 2022, wadadisi wanasema hatua kama hiyo itavunja chama cha Jubilee.

“Pendekezo la Atwoli sio hewa tupu. Katika siasa mambo hubadilika haraka sana. Usisahau washirika wa rais, hasa kutoka ngome yake wanahisi hawana mtu wa kumrithi na wangetaka aendelee kuwa serikalini kwa sababu wanahisi anawakilisha maslahi yao. Siasa za Kenya ni telezi sana,” asema Bw Alloys Mwangi, mdadisi wa masuala ya siasa.

Kulingana naye, mjadala kuhusu kubadilisha katiba kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu baada ya 2022 umekuwepo kwa muda, japo chini kwa chinichini.

“Nahisi kuna mikakati ambayo imekuwa ikiendelea chini kwa chini katika mrengo mmoja wa Jubilee. Hofu ya wakereketwa wa mabadiliko hayo ni azma ya Naibu Rais William Ruto ya kugombea urais 2022.

Rais mwenyewe pia aliahidi kustaafu baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na kumuunga Bw Ruto. Hata hivyo, inaonekana kuna shinikizo mpya zilizojiri na muafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga,” alisema Bw Mwangi.

 

Uhuru awe Waziri Mkuu 2022

Akiongea kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni katika bustani ya Uhuru Park Jumanne, Bw Atwoli alipendekeza katiba ifanyiwe mageuzi ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu utakaoshikiliwa na Rais Kenyatta baada ya 2022.

Kulingana na Bw Atwoli, Rais Kenyatta atakuwa bado na nguvu atakapomaliza kipindi chake cha pili 2022 na anafaa kuendelea kushiriki siasa.

“Tubadilisheni katiba hii na kutumia rasimu ya Bomas ili kuhusisha watu wote kwa sababu sio kila mtu anaweza kuwa rais. Kufanya hivi kutamshirikisha Rais Kenyatta ambaye angali bado chipukizi. Tusipofanya hivyo, tutampeleka wapi?” alihoji Bw Atwoli.

“Nawaambia kwamba hata mtu mwingine akiongoza Kenya, ni lazima atashirikiana na watu wa Mlima Kenya na huo ndio ukweli wa mambo,” alisema Bw Atwoli.

Kulingana na rasimu ya katiba ya Bomas, Kenya ingekuwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye angechaguliwa na bunge na kuwa na na mamlaka makuu.

Wadadisi wanasema pendekezo hilo ni njama ya kuzima azima ya Naibu Rais William Ruto ambaye  amepinga mabadiliko yoyote ya katiba yanayolenga kubuni nyadhifa mpya serikalini. Wanasema si ajabu mabadiliko hayo yalikuwa miongoni mwa masuala ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga walikubaliana katika muafaka wao.

Mchanganuzi Barack Muluka anahisi suala la kuhakikisha Rais Kenyatta ataendelea kuhudumu kama waziri mkuu lilijadiliwa kwenye mikutano iliyotangulia muafaka wake na Bw Odinga.

 

Raila na Uhuru wana maoni sawa

“Odinga anaamini kwamba atakuwa rais pengine akiwa na naibu kutoka  Rift Valley na mwingine kutoka Pwani. Kenyatta anaweza kuwa waziri mkuu akiwa na manaibu wawili kutoka Magharibi na Mashariki. Hawa wawili wana maoni sawa,” Bw Muluka alisema.

Kwenye makala yaliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini kabla ya tamko la Bw Atwoli, Bw Muluka  alisema viongozi hao wawili watawaagiza wabunge na madiwani wa vyama vyao kuunga mabadiliko ya katiba wakisingizia wanalenga kuunganisha nchi.

“Kuna wale watakaopinga mabadiliko hayo na kwa hivyo kutazuka makabiliano ya kisiasa na kikatiba nchini Kenya,” alitabiri Bw Muluka.

Kulingana na kiongozi wa wengi katika seneti Bw Kipchumba Murkomen, ambaye ni mshirika wa Bw Ruto, katiba haiwezi kubadilishwa ili kubuni nyadhifa kwa sababu ya watu binafsi.

“Rais ameshughulikiwa ipasavyo katika katiba na hahitaji kutengewa wadhifa,” alisema Bw Murkomen na kuungwa mkono na mwenzake katika bunge la taifa, Aden Duale ambaye pia ni mwandani wa Bw Ruto.

“Rais Kenyatta ametangaza wazi kwamba, atafurahi kustaafu siasa baada ya kumaliza kipindi chake cha pili,” alisema Duale.

Wadadisi wanasema njama zozote za kumzuia Bw Ruto kugombea urais 2022 zinaweza kuvunja chama cha Jubilee.

“Bw Ruto atahisi kuwa amesalitiwa baada ya kumuunga Rais Kenyatta tangu 2013. Amekuwa akilenga urais 2022 na yeye na washirika wake hawatachukulia hatua yoyote ya kuzima ndoto yake kwa urahisi,” asema Bw Doris Chebet wakili na mdadisi wa siasa.

Anasema pendekezo la kumtaka Rais Kenyatta kuendelea kuhudumu ni njama za watu binafsi wanaomzunguka na ambao wanataka kuendelea kufurahia mamlaka.

 

Kuongezwa kwa muhula

“Usishangae kusikia baadhi yao wakipendekeza muda wa kipindi cha rais kuhudumu uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba,” alisema Bi Chebet.

Bw Atwoli alisema kwa sababu Rais Kenyatta atakuwa na umri wa miaka 60 atakapomaliza kipindi chake cha pili, ngome yake ya kisiasa haitakubali astaafu.

Wanaopinga pendekezo hilo wanamhimiza Rais Kenyatta kuiga viongozi wanaoheshimiwa kote ulimwenguni kwa kukataa kukwamilia mamlakani.

Bw Mwangi anasema Bw Atwoli hakuwa wa kwanza kutoa pendekezo kama hilo.

“Nakumbuka mapema mwaka huu, David Murathe, ambaye ni afisa mkuu wa chama cha Jubilee (naibu mwenyekiti) alinukuliwa akisema kuna watu wanaotaka Uhuru astaafu akitimiza miaka 60 ilhali Raila anataka kuwa rais akiwa na miaka 75.

Hii inaonyesha huenda kuna njama pana zinazopikwa kuhakikisha Uhuru anasalia serikalini baada ya 2022” alisema Bw Mwangi na kuongeza kuwa washirika wa Bw Ruto wanaweza kuondoka Jubilee iwapo hilo litatendeka.

Kulingana na  Bi Chebet, mswada wa mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket unaopendekeza katiba ibadilishwe Rais ahudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba na kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka makuu, haufai kupuuzwa.

“Marais wengi wametumia mabadiliko ya katiba ili waendelee kuhudumu, hasa wakiwa na idadi kubwa ya wabunge. Jubilee ina wengi katika bunge na seneti na hata wanaomuunga Ruto wakikosa kuunga mabadiliko, wale wa ODM wanaweza kuyaunga kufuatia muafaka wa Uhuru na Odinga,” alisema.

Atwangwa na mkewe kama mburukenge kwa kutomnunulia nyama

Na BENSON MATHEKA

GITHUNGURI, KIAMBU

WAKAZI wa hapa, waliachwa vinywawazi baada ya jombi kupokonywa mboga na kutandikwa na mkewe kama mburukenge akimlaumu kwa kutomnunulia nyama.

Mwanadada huyo huwa anauza bidhaa sokoni kuchuma riziki.

Yasemekana kidosho huyo hakuweza kwenda kufanya kazi yake sokoni kwa sababu ya mvua mkubwa na mumewe akachukua jukumu la kununulia familia yake ilichohitaji.

Siku ya kisanga, jamaa alienda kazini ilivyokuwa desturi yake.

“Aliomba ruhusa kazini na kuondoka mapema kuliko kawaida na akiwa njiani kurudi nyumbani, aliamua kupitia katika kituo cha biashara ili ajirudishie mkono kwa kuchapa kazo nzito siku nzima,” alisema mdokezi,

Inasemekana kuwa jamaa alijitosa kilabuni na kuagiza vikombe kadhaa vya ‘Keg’ ndipo akalewa chakari.

Kulingana na mdokezi, hata baada ya kulewa, jamaa hakusahau jukumu lake la kununulia familia chakula. Alielekea dukani akanunua unga na mboga.

Inasemekana alipofika nyumbani badala ya mkewe kumpokea, alianza kumrushia cheche za matusi.

“Kitu gani mbaya na wewe? Kwa hivyo badala ya kutununulia vitu nzuri kama nyama unanunua mboga.

Kwani unafikiri sisi ni sungura wa kutafuna matawi kila siku? Mwanamume gani usiye na akili wewe. Nitakuonyesha jinsi wanaume kama wewe hufunzwa na kupata akili,” alichemka mama huyo.

Inasemekana kuwa mama watoto alimpokonya mumewe mboga na kurushia kondoo wake kabla ya kumtwanga mangumi na mateke. “Jamaa alipiga nduru zilizowavutia majirani,” alisema mdokezi.

Iliwabidi majirani hao kungilia kati na kumuokoa jamaa huku wakimlaumu mama kwa kumdharau mumewe.

Haikujulikana uhusiano wake na mkewe ulivyoendelea baada ya kisa hicho.

…WAZO BONZO…

KINAYA: ‘Baba’ asisubiri hisani ya Uhuru aambiwe akalie kigoda cha ikulu!

Na DOUGLAS MUTUA

‘BABA’ ametongozwa akatongozeka, lakini atakula huu na hasara juu! Aliyemtongoza pia atakula huu. Lakini hii haitakuwa mara ya kwanza kwa ‘Baba’ kujaribisha ujanja wa kisiasa na kuambulia patupu.

Inashangaza hajajifunza chochote tangu anoe alipoingiza tingatinga tumboni mwa jogoo akitarajia Mzee Kirungu apaliwe na moshi wa tingatinga, akohoe kishenzi na kumwambia ‘chukua kigoda cha ikulu ukalie!’

Ni heri ‘Baba’. Anayemtongoza sasa hajui kwamba hajui. Wanasiasa hujiambia wanapendwa sana, hakuna mwingine kama wao, ila siku ya siku ikifika huaibishwa.

Ikiwa ‘Ithe wa Jaba’ anajidanganya kwamba angali maarufu katika uliokuwa mkoa wa Kati, basi anaota mchana hali yu macho. Huko kulitokwa mwaka jana.

Sasa hawezi hata kuwashawishi wenyeji wamchague mtu yeyote mwenyekiti wa josho la ng’ombe kwao kijijini Ichaweri.

Watu walinidhani kichaa miaka kadha iliyopita nilipoandika kwamba iwapo Baba Jimmy angeamua kumrithisha ‘Baba’ urais mnamo 2013 angekuwa peke yake.

Hata Mama Jimmy na nyumba yake yote hawangekubali kumpa kura ‘Baba’. Kisa na maana? Hawamtambui, kwao huyo ni mtu wa kelele nyingi asiyeaminika.

Hiyo ndiyo ‘injili’ ambayo watu wengi wa pale mlimani wamejua tangu enzi za mababu zetu, mengineyo hawatambui.

Hivyo basi kwa mtu kudhani anaweza kubadilisha hali hiyo ni kujidanganya, yaani kung’ata mnofu mkubwa hali hajajaaliwa meno makubwa na makali kuutafuna.

Wakati huo niliandika kuhusu ugumu wa Agwambo kuungwa mkono huko kwani wakati fulani tulipokuwa na serikali ya muungano Baba Jimmy alionekana kumpenda sana.

Baba Jimmy alipodhani mtu bora zaidi kumrithi alikuwa MaDVD, wadau wa siasa za mlimani walijitokeza na kusema”‘ng’o! ni ‘Kamwana’ pekee, Mzee upende usipende…”

Baba Jimmy hakufanya chochote kwa maana yeye mwenyewe alikuwa mlezi wa ufalme tu, wenye mamlaka katika ufalme huo ni wengine na ndio huamua.

Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo ningali naangua kicheko, nusura mbavu ziniteguke, kwa wapayukaji kudai kura ya maamuzi ili tuunde wadhifa wa waziri mkuu.

Wakenya si wapumbavu; kila wakati ukitaja ‘waziri mkuu’ wanajua ni ‘Baba’ anayetafuta kuingia ikulu kupitia mlango wa nyuma.

Najua ni hoja ambayo inaweza kuungwa mkono zaidi na wafuasi wa ‘Baba’, hasa kina yakhe ambao hufuata upepo kama bendera.

Lakini inaweza kutumika na kina mwana wa mlimani kumwaibisha mwenzao anayestaafu; mkataba wake nao ulikamilika mwaka jana alipochaguliwa tena.

Kuanzia sasa, maamuzi ya hatima ya siasa za mlima Kenya si yake kabisa. Yeye sasa ni wa kuketi na kuambiwa, yaani kuwasikiliza wadau wakuu, asipopenda akajinyonge!

Watu wa mlimani wameapa hata kwa dawa hawawezi kukubali tuwe na wadhifa wa waziri mkuu, sikwambii wameungana na wenzao wa Bonde la Ufa katika msimamo huo.

Akitaka kustaafu vibaya, ‘Ithe wa Jaba’ ajaribu kuandaa kura ya maamuzi kuhusu wadhifa wa waziri mkuu. Atashindwa vibaya, aiache nchi katika kilele cha uhasama na taharuki.

Wabunge wakiungana kuwaundia watu nyadhifa zisizo kwenye Katiba, waikwepe kura ya maamuzi, watakataliwa kwa fujo mashinani ifikapo 2022. Hii Kenya si ya mama ya mtu!

 

mutua_muema@yahoo.com

MAKALA MAALUM: Madereva wa kike sasa kivutio kipya katika teksi jijini, wanaume pabaya!

Na MASHIRIKA

WANAWAKE wameteka biashara ya teksi jijini Nairobi na idadi yao inazidi kuongezeka.  Inakisiwa kuwa jijini Nairobi pekee kuna teksi 12,000 ambazo kwa jumla huzoa mapato ya Sh20 milioni kwa siku.

Madereva wa kike wanasemekana kuwa asilimia tatu pekee lakini wadau wanasema idadi yao inaongezeka kwa haraka.

Sababu kuu ya ongezeko hilo ni visa vya dhuluma na mashambulizi vinavyoripotiwa hususan na wateja wanawake dhidi ya madereva wa kiume.

Vile vile, kumekuwa na ongezeko la kampuni zinazotoa huduma za teksi na ambazo zimechangia kuimarisha mazingira ya kazi, na hivyo kuwavutia madereva wanawake.

Kampuni hizi zinatumia teknolojia ya kisasa kuunda programu za simu (Apps) zinazounganisha madereva na wateja wao, katika mfumo wa e-taxi.

Moja ya kampuni hizo Little Cabs ambayo programu yake inakupa fursa ya kuchagua dereva wa kiume ama kike, imeshuhudia ongezeko mara 13 katika idadi ya madereva wake wa kike kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.

“Tulikuwa na madereva 27 wa kike wa Little Cab tulipoanzisha huduma zetu 2016, sasa wamefika 381. Tunalenga kuwa na madereva 1,000 wa kike kufikia mwisho wa mwaka huu,” alisema Jefferson Aluda, meneja wa mipango wa Little Cabs.

“Watu wengi hudhani kazi ya udereva wa teksi ni ya wanaume pekee lakini mtazamo huo unabadilika. Wateja wetu wanawasifia madereva wa kike; kwamba ni waangalifu sana na hudumisha weledi kazini. Tunatarajia wanawake zaidi kuungana nasi tutakapofanya uteuzi.”

Huku idadi ya kampuni za teksi zinazotumia teknolojia ikizidi kuongezeka, ili kuziba mwanya wa mfumo mbovu wa uchukuzi wa umma jijini Nairobi, idadi ya wanawake wanaosaka ajira za madereva inapanda.

Wanawake hao wanasema kuwa wanavutiwa na ratiba rahisi ya kazi, fursa ya kuchagua mteja wa kubeba na hakikisho la malipo.

“Kuwa dereva wa teksi si jambo ambalo ningeliwazia awali, lakini baada ya kujiunga na kampuni ya teksi inayotumia App kutoa huduma, nimebaini kwamba ni kazi nzuri kwa wanawake,” asema Lydia Muchiri, 29.

“Ni mwafaka, rahisi na salama – bora zaidi kuliko kuketi nyumbani kusubiri misaada,” aliongeza.

Hata hivyo, wanawake bado wanakabiliana na changamoto mbalimbali ili kustawi kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini.

Wanachangia asilimia 33 pekee ya wafanyakazi 2.5 milioni walio na ajira za ofisini huku wakimiliki asilimia 1 pekee ya ardhi za kilimo, kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS).

 

Kuimarisha maisha

Kuchipuka kwa apu za teksi kumechangia pakubwa kuwapa wanawake fursa ya kupata ajira na hivyo kuimarika kiuchumi.

Katika miaka mitatu iliyopita, takriban Apps 10 zimezinduliwa kukidhi mahitaji ya tabaka la watu wanaotumia simu za kisasa kusaka huduma mbadala za uchukuzi za bei nafuu na salama.

Madereva wa teksi hulipwa takriban Sh30 kwa kila dakika huku kampuni ikiwatoza ada ya hadi asilimia 25. Licha ya hayo, wanawake wamepongeza kampuni ambazo zimewapa fursa ya kuhudumu kama madereva wa teksi kama vile Uber, Taxify, Little Cabs na Pewin.

Ukiondoa ada ya kampuni, mafuta na kukodisha gari, madereva wanaohudumu kwa saa 12 kila siku hupokea takriban Sh60,000 kila mwezi, duru katika sekta zasema.

Faridah Khamis, mzazi wa pekee wa watoto watano, aliamua kuwa dereva wa e-taxi Februari mwaka 2017 baada ya kuhimizwa na dereva mmoja wa kiume.

“Ingawa malipo yako chini na lazima nifanye kazi saa 12 kwa siku – watoto wangu wakiwa shuleni na usiku wakiwa wamelala – ni afadhali kuliko kazi za ofisi za siku hizi,” alisema mama huyo mwenye umri wa miaka 36 kando ya gari lake aina ya Mazda Axela.

 

Usalama

“Vile vile, ni salama kwa wanawake. Mimi ndiye huamua wakati wa kufanya kazi, ni wapi nitakapoenda na wateja nitakaobeba. Ningekuwa dereva wa teksi za kawaida ingenilazimu kuwa barabarani wakati wote ili kusaka wateja. Kupitia apu ya simu mimi huwapata wateja kwa urahisi nikiwa nyumbani kwangu.”

Madereva hao wa kike huchagua wateja ambao maelezo yao ni mazuri, na hukubali tu kubeba wateja wanaoenda maeneo yaliyo na watu wengi.

Kampuni zao pia huwafuatilia kupitia GPS na apu zao ziko na pahali pa kubonyeza wakihisi wamejipata katika hatari.

Maafisa wa Uber, kampuni nyingine inayotumia teknolojia kutoa huduma za teksi, wanasema programu hizo za simu za kisasa ni fursa nzuri ya kiuchumi kwa wanawake hususan katika mataifa yanayoendelea kama Kenya.

“Apps kama za Uber zinasaidia kuondoa vizingiti vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika ukuzaji uchumi,” msemaji wa Uber kanda ya Afrika Mashariki, Bi Janet Kemboi, alisema.

“Vizingiti hivi ni pamoja na ubaguzi wa kijamii, hatari za usalama, kutengwa kifedha na kidijitali na ugumu wa kupata magari pamoja na mali nyingine.”

Licha ya mazingira kuimarika na sekta kushuhudia ongezeko la madereva wa kike, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za ubaguzi na dhuluma.

Kama vile ugumu wa kukodisha magari kwa sababu ya dhana potovu kwamba wanawake si madereva wazuri na usumbufu wa wateja wanaume walevi.

 

Usumbufu

Kwa sababu nambari zao za simu zinapatikana kwa urahisi kwenye apu za teksi, wanawake madereva husumbuliwa na simu za “kuwajulia hali’ kutoka kwa wateja ambao wanataka uhusiano wa kimapenzi.

Vile vile, wanakabiliwa na dhana kwamba wao ni makahaba kwa sababu ya kuvalia maridadi, kufanya kazi usiku na kufanya kazi ya “wanaume”.

Hata hivyo, wanawake hao wanasema changamoto hizo si za kila siku na kwamba kufanya kazi kama dereva wa teksi kumewafanya baadhi kuota maono ya kumiliki magari yao binafsi ya teksi – ya wateja wanawake zinazoendeshwa na madereva wanawake.

“Kuna hitaji la madereva wa teksi wa kike. Wateja hupongeza mienendo na weledi wetu. Baadhi yao hutuambia kwamba magari yetu ni salama na safi zaidi kuliko ya madereva wanaume,” akasema Muchiri.

“Tunajivunia kazi yetu. Sisi si duni kuliko wale wanaofanya kazi za ofisi. Magari yetu ndiyo ofisi zetu na tunaamini kwamba tunapoingia ndani ya gari lazima tuwe weledi.”

(Makala yametayarishwa kwa hisani ya Thomson Reuters Foundation).

Madaktari watoa sindano 7 kutoka tumbo la mtoto

TITUS OMINDE na DENNIS LUBANGA

MADAKTARI katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret wamefanikiwa kutoa sindano saba kutoka tumboni mwa mtoto wa miaka mitatu.

Mtoto huyo alilazwa hospitalini humo kutoka katika kaunti ya Pokot Magharibi siku tatu zilizopita.

Upasuaji huo wa saa moja na dakika 45 uliongozwa na Prof Robert Tenge ambaye anasimamia kitengo cha upasuaji watoto hospitalini humo.

Kwa mujibu wa Prof Tenge, sindano sita zilikuwa zimekwama katika maini huku sindano nyingine ikiwa imekwama katika utumbo.

Profesa Tenge alisema historia ya afya ya Dorcas Chepchumba ilionyesha kuwa amekuwa akiishi na sindano hizo za kushona nguo tumboni mwake kwa mwaka mmoja uliopita.

Sindano hizo ziligunduliwa alipolazwa katika hospitali ya kaunti ya West Pokot mjini Kapenguria mapema wiki jana akilalamikia maumivu ya tumbo.

Uchunguzi wa x-ray hospitalini humo ulibaini mtoto huyo alikuwa na sindano tumboni mwake kabla ya kuelekezwa katika hospitali ya MTRH kwa upasuaji.

“Tulipokea mtoto huyo na kumfanyia uchunguzi ambapo tulibaini kuwa alikuwa na sindano tumboni mwake, kabla ya kuanzisha mikakati ya kutoa sindano hizo tumboni humo,” alisema Profesa Tenge.

 

Mzozo Knut wachacha huku Sossion akitupwa nje

Na BERNARDINE MUTANU

MZOZO katika Chama cha kitaifa cha Walimu (KNUT) uliendelea kutokota zaidi jana baada ya wanachama wa Kamati Kuu Simamizi (NEC) kutwaa afisi ya Katibu Mkuu Wilson Sossion na kumpa Hesbon Otieno.

Maafisa wa NEC Jumamosi walisema wanapanga kumuapisha Bw Otieno, kwa kuwa hawamtambui Bw Sossion.

Walitangaza hayo licha ya Bw Sossion kusisitiza kuwa ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho baada ya kuenda mahakamani kuzuia kuondolewa kwake afisini.
Kamati hiyo jana ilitangaza kuwa tayari kuna mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hicho.

Wakati wa mkutano na wanahabari jana katika afisi kuu za KNUT, Nairobi, wanachama wa NEC waliofika katika mkutano huo walisema tayari msajili wa uhusiano wa leba amethibitisha kupokea notisi ya mageuzi katika uongozi wa chama hicho.

“Kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa katibu mkuu ndugu Sossion ni kuambatana na sheria. Tulituma ombi la mageuzi katika uongozi wa KNUT kuambatana na sheria ya uhusiano wa leba,” alisema Bw John Gitari Munyi, ambaye ni mdhamini katika bodi ya KNUT.

Alisema waliwasilisha ombi hilo Aprili 30 na kutoka wakati wa kuwasilishwa kwake kuendelea, Hesbon Otieno Agolla ndiye Kaimu Katibu Mkuu mpya wa KNUT.

Mnamo Alhamisi, msajili wa vyama vya leba Bw E. N Gicheha alithibitisha kusajili notisi ya mabadiliko yaliyoombwa bodi ya KNUT kumwondoa Bw Sossion kama katibu mkuu.

“Msajili ameeleza bayana kwamba kuna mabadiliko katika usimamizi wa KNUT. Kama wadhamini, tunajua kuna agizo la mahakama lakini agizo hilo lilitolewa baada ya msajili kuthibitisha mabadiliko ndani ya chama,” alisema Bw Gitari.

Wanachama hao hata hivyo walisisitiza kuwa hawakumwondoa Bw Sossion kwa sababu alikuwa amechaguliwa mbunge lakini kwa sababu ya kutowajibika kazini, udanganyifu na kuzembea kazini kuambatana na Kifungu cha 9 kipengee cha C7 cha katiba ya KNUT.

Walipuuzilia mbali tangazo la Bw Sossion kwamba ataitisha Kikao Maalum cha Wajumbe mwakani kwa kusisitiza kuwa ni NEC ndiyo yenye uwezo wa kufanya hivyo.

Viongozi hao kutoka maeneo mbali mbali nchini waliimba nyimbo za kumkashifu mbunge huyo maalum, na kumtaka kulenga siasa na kuachana na masuala ya walimu.

 

Kaunti za Meru na Embu zapigania miraa

DAVID MUCHUI na CHARLES WANYORO

SERIKALI za Kaunti za Embu na Meru zinazozania Sh2.2 bilioni zilizotolewa kuwafaa wakulima wa miraa katika kaunti hizo.

Huku gavana wa Embu Martin Wambora akisema serikali yake iko tayari kuzungumza na serikali ya Meru kuhusiana na jinsi ya kugawanya pesa hizo, serikali ya Meru imesema kuwa hakuna mazungumzo yoyote ya aina hiyo.

Wambora Jumatano alisema wajumbe kutoka Embu walikuwa katika Kaunti ya Meru kuzungumzia jinsi ya kugawanya pesa hizo na jinsi zitakavyotumiwa.

Alizungumzia Sh1 bilioni, lakini jumla ya Sh2.2 bilioni zilitolewa katika mwaka wa 2016/2017 ambapo Sh1 bilioni zinashikiliwa na Hazina ya Fedha ili kungoja Wizara ya Kilimo kuunda kamati kutekeleza ripoti ya jopo kuhusu miraa iliyotolewa mwaka 2017.

Wambora alisema Embu ililenga kutumia mgao wake kununua miche ya mimea tofauti kwa lengo la kukuza aina tofauti za mazao ili kuepuka kutegemea miraa.

Biashara ya miraa imehusishwa na kiwango kikubwa cha vijana wanaoacha shule eneo hilo.

Alisema uongozi wake ulikuwa umetoa miche 5,000 ya makadamia kwa wakulima katika maeneo wanakopanda miraa.

Hata hivyo, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na chama cha wauzaji miraa cha Nyambene (Nyamita) alipuzilia mbali madai hayo kwa kusema pesa hizo zitatumika kufufua masoko ya miraa.

Bw Kiraitu alisema pesa hizo zitatumika kuambatana na mapendekezo ya jopo kuhusiana na miraa.

“Kwa sasa, Mbunge wa Igembe Kasakazini Maore Maoka ndiye anayefaa kufuatilia suala hilo kwa serikali ya kitaifa kuhusu wakati zitakapotolewa pesa hizo,” alisema.

ODM kupigania fidia kwa jamii zote zilizopoteza jamaa

Na BARACK ODUOR

KINARA wa upinzani Raila Odinga amewaomba wabunge wa ODM kumsaidia kupitia bungeni kuhakikisha familia zilizopoteza jamaa wao zimefidiwa na serikali.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na mwenzake kutoka Suba kaskazini Bi Millie Odhiambo wamedokeza kuwa Bw Odinga anataka uungwaji mkono kutoka bungeni kuhakikisha sekali imetoa malipo ya fidia kwa waliouawa.

Viongozi hao walisema wanaendelea kuandaa orodha ya idadi kamili ya familia zilizoathiriwa ili kuwasilisha kwa serikali kupitia afisi ya Bw Odinga.

“Tunajua watu wengi wanauliza kuhusu hatima ya waliofariki wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi wa Rais Kenyatta. Sisi tukiwa wabunge kutoka Nyanza tunasukuma suala hili la kufidiwa kwa wahasiriwa,” alisema Bw Amollo.

Wakizungumza wakati wa mazishi ya Mzee Isaac Ooro, baba yake mshauri wa kisiasa wa Bw Odinga, Silas Jakakimba katika kijiji cha Kakimba kisiwani Mfang’ano Jumamosi, wabunge hawa wa walisema watashinikiza hadi wahusika wafaidi kutokana na ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge hawa walisema kuwa lazima haki ipatikane kwa walioathiriwa wakati wa makabiliano hayo kati ya waandamanaji na Polisi.

“Salamu na ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta haujatufanya tusahau maafa yaliyotokea Wakenya wasio na hatia walipouawa na dhuluma nyingine kutekelezwa,” alisema Bw Amollo.

Mbunge huyo pia alisema kuwa maafa na dhuluma za hapo awali lazima zijadiliwe ndipo suluhisho lipatikane.

Bw Amollo alisema kwamba wabunge kutoka eneo hilo wanashirikiana kuhakikisha wafuasi wa NASA waliothiriwa wamepata haki.

“Tuko tayari kuwasilisha majina ya wahasiriwa kwa Serikali na pia mahakamani kuhakikisha haki imetendeka na dhuluma zilizotokana na uchaguzi mkuu zimetatuliwa,” alisema Bw Amollo.

Mipango yangu yote ya kando ni Wakikuyu – Sonko

Na CAROLYNE AGOSA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko alizua kicheko baada ya kusisitiza kuwa hana kinyongo na jamii ya Wakikuyu na kufichua kuwa hata ‘mipango wake wote wa kando’ wanatoka jamii hiyo.

Kwenye kanda ya video iliyosambazwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Gavana Sonko alitaja nyadhifa mbalimbali za juu katika serikali yake ambazo ameteua Wakikuyu.

“Watu walisema Sonko hapendi Wakikuyu. Mimi ningependa kusema napenda Wakikuyu. Nimeteua madiwani Wakikuyu zaidi ya 10. Naibu gavana (wa Nairobi) anayekuja ni mwanamke Mkikuyu. Katibu wangu wa kaunti ni Mkikuyu. Baraza langu lina mawaziri wanne Wakikuyu.

Mkuu wa watumishi wangu ni Mkikuyu. Niko na maafisa wakuu sita wa idara ambao pia ni Wakikuyu,” alisema Bw Sonko.

Gavana huyu wa Nairobi, ambaye anatoka jamii ya Wakamba, aliibua kicheko katika umati alipoeleza uhusiano wake wa kifamilia na Wakikuyu.

“Wake wangu wa kwanza ni Wakikuyu. Watoto wangu ni Wakikuyu. Wakwe zangu ni Wakikuyu. Mipango yangu ya kando wote ni Wakikuyu!”

Kanda hiyo inakujia wiki chache baada ya Gavana Sonko kukemea kundi la wanasiasa na viongozi fulani aliodai wanajizatiti kumfanya aonekane ni kizingiti kwa maslahi ya jamii ya Wakikuyu – ambao wanadhibiti biashara nyingi jijini Nairobi.

Bw Sonko alipuuza madai kuwa analenga jamii hiyo katika msururu wa hatua za kuwafuta kazi wafanyakazi wa baraza la jiji, akisema nia yake ni kuwang’oa wafisadi na mabwanyenye ambao wameliteka jiji.

“Niko na watu kutoka jamii ya Kikuyu walio na vyeo vya juu katika serikali yangu. Mtu asieneze uvumi wa uongo kwamba nimewatenga (Wakikuyu),” akasema katika hafla moja City Hall mwezi jana.

Miguna aapa kurejea nchini hapo Mei 16

Na WYCLIFFE MUIA

WAKILI Dkt Miguna Miguna anakusudia kurejea nchini mwezi huu japo haijabainika iwapo serikali ya Kenya imemrudishia pasipoti yake ili kufanikisha usafiri wake kutoka Canada.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Dkt Miguna alisisitiza kuwa yeye ni Mkenya na kuwa tayari mahakama ya imetoa maagizo wazi kwa serikali kumrejesha nyumbani.

“Nitarudi Kenya Mei 16, 2018. Mimi ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa. Mahakama Kuu imewaagiza Dkt Fred Matiangi, Kihalangwa, Joseph Boinnet na George Kinoti mara 13 wanipe pasipoti ya Kenya na pia waweke mipango kamili ya kunirejesha nchini Kenya bila masharti,”aliandika Dkt Miguna katika Twitter yake.

Mwezi uliopita, Jaji Chacha Mwita wa Mahakama Kuu, Nairobi alitoa maagizo kwa serikali kumrejesha Dkt Miguna nchini ili kutoa ushahidi moja kwa moja mnamo Mei 18.

Wakili Miguna amekuwa akimkabili kinara wa ODM Raila Odinga kwa kushindwa kutumia muafaka aliyotia saini na Rais Uhuru Kenyatta kumrudisha humu nchini ili kudhihirishia Wakenya kuwa analenga kuleta umoja.

Wakili huyo alimtaka Bw Odinga kuelezea Wakenya kwa nini muafaka wake na Rais Kenyatta haujamwezesha kurejea nchini kutoka Canada licha ya kuwaahidi kuwa atahakikisha amerejea.

“Kama nilituhumiwa kwa kukuapisha, kwa nini haukukamatwa na kufurushwa kutoka Kenya kama mimi…? Iwapo muafaka wako na Uhuru unalenga kuunganisha nchi, kwa nini sijarudishwa Kenya? Elezea Wakenya wazi wazi,” Miguna alimwambia Bw Odinga kupitia Twitter.

Inasubiriwa kuonekana iwapo serikali itatii amri ya mahakama na kukubali Miguna kurejea nchini kufikia Mei 18 ili kutoa ushuhuda wake kuhusiana na uraia wake tata.

Magavana 10 sasa walenga urais na useneta 2022

Na JUSTUS WANGA

MAGAVANA 10 wanaohudumu kwa kipindi cha pili na cha mwisho tayari wameanza kuweka mikakati kuhusu maisha yao ya kisiasa baada ya 2022.

Huku wachache kama Hassan Joho, 45, (Mombasa) na Alfred Mutua, 47, (Machakos) wakielekeza macho yao katika kiti cha urais, sehemu kubwa ya waliosalia wanawazia kujitosa katika kinyang’anyiro cha Useneta ama ‘Nyumba ya Wazee’ – kama ambavyo imerejelewa na wabunge kadha wa kitaifa katika vuta nikuvute zao za kuonyesha ubabe baina yao na maseneta.

Magavana wamelazimika kuanza kujipanga kutokana na Kifungu 180 (7a) cha Katiba kinachowazuia kuwania tena kiti hicho baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili mtawalia.

Sharti hilo halizingatii umri wala umaarufu wa gavana.

Ni hali halisi ambayo imewapiga kumbo magavana hao ambao wamelazimika kuanza kujitayarisha kwa maisha ya baadaye ya kisiasa miezi kadha baada ya kutetea viti vyao na miaka minne kabla utawala wao kukoma.

Ukweli mwingine mchungu kwa wale wanaomezea mate kiti cha urais ni kwamba, ingawa mfumo wa ugatuzi unaruhusu ‘marais wadogo’ 47 ni mmoja pekee anaweza kuwa kiongozi wa taifa, jambo ambalo limefanya kinyang’anyiro cha urais kuwa na ushindani mkali.

Gavana mchanga kabisa ni Alex Tolgos, 38, wa Elgeyo Marakwet na duru zinasema anawazia kuingia Seneti.

Wandani wake wanasema kuna uwezekano wa ‘kubadilishana’ viti na Kiongozi wa Wengi Seneti Kipchumba Murkomen, ingawa seneta huyo amewadokezea marafiki wa karibu nia yake ya kuendelea kushikilia wadhifa muhimu katika serikali ya Naibu Rais William Ruto iwapo atafanikiwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya wakuu hao wa kaunti wanalenga nyadhifa za ubalozi na uwaziri katika serikali ijayo.

Mahojiano na wengi wao yamedhihirisha jinsi hawana haja ya kung’ang’ania viti vya ubunge kutokana na hadhi ya kiti cha ugavana pamoja na fedha nyingi ambazo magavana husimamia.

Gavana Joho asema ananuia kuwania urais kwa tiketi ya chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

“Nitafika kila pembe ya nchi kuomba kura za urais,” aliambia Taifa Jumapili.

Dkt Mutua ametangaza wazi kwamba safari yake ya kwenda Ikulu imeshaanza, kauli ambayo imeibua uhasama kati yake na makamu wa rais wa zamani na kigogo wa siasa za Ukambani, Bw Kalonzo Musyoka, ambaye pia anamezea mate kiti cha urais.

“Kwa neema ya Mungu nitakuwa rais wa tano wa Kenya,” akasema Dkt Mutua.

Gavana wa Muranga Mwangi Wa Iria, 47, ni miongoni mwa vigogo wa Mt Kenya walio na matumaini ya kunyakua uongozi wa taifa.

 

Rais Kenyatta namba wani Afrika kwa miundomsingi

Na BERNARDINE MUTANU

RAIS Uhuru Kenyatta ametangazwa mshindi wa mwaka huu Afrika katika tuzo za uchukuzi na mifumo ya barabara.

Katika hafla iliyofanywa jijini Dakar, Senegal Jumamosi, shirika la Africa Road Builders lilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa tuzo ya Babacar Ndiaye 2018, kwa kuanzisha miradi katika mfumo wa uchukuzi wa reli, barabara pamoja na uchukuzi wa ndege.

Rais wa Habari, Miundo Msingi na Fedha Barani Afrika Adama Wade alitaja reli ya kisasa (SGR) kati ya Nairobi na Mombasa kuwa mradi muhimu sana ambao ulikuwa na manufaa makubwa kwa wananchi.

“Mradi wa SGR umepunguza nauli kati ya Nairobi na Mombasa kwa nusu na pia muda unaotumiwa kusafiri kati ya miji hii umepungua sana,” alisema.

Mradi huo ulilenga uchukuzi wa abiria milioni moja kwa mwaka. Pia serikali ililenga kupunguza msongamano katika barabara kuu za humu nchini.

Kwa kumpongeza Rais Kenyatta, kamati ya uteuzi wa washindi ilitangaza kuwa tuzo hiyo itatolewa Mei 23, mjini Busan, Korea Kusini, wakati wa mkutano mkuu wa kila mwaka wa Benki ya African Development.

 

Wandani wa Raila wamshauri ajitose debeni 2022

ELISHA OTIENO na RUSHDIE OUDIA

WANDANI wa kisiasa wa Kinara wa upinzani Raila Odinga jana wasisitiza kwamba waziri huyo mkuu wa zamani hatastaafu kutoka jukwaa la kisiasa hivi karibuni bali atakuwa debeni katika uchaguzi wa 2022.

Wakiongozwa na Kiongozi wa wachache kwenye bunge la seneti James Orengo, viongozi hao walisema liwe liwalo lazima Bw Odinga awe debeni mwaka huo.

Wakizungumza katika kijiji cha Piny Oyie, eneobunge la Suna Magharibi katika kaunti ya Migori wakati wa hafla ya makaribisho ya nyumbani ya Mwakilishi wa kike wa kaunti Bi Pamela Odhiambo ambayo ilihudhuriwa na Bw Odinga mwenyewe, walisema kwamba kigogo huyo wa siasa za upinzani yuko tayari kuonana kiume na wawaniaji wengine.

Naibu Rais William Ruto anaongoza orodha ya wawaniaji wengine wanaokimezea mate kiti cha urais.

Jumamosi, Bw Orengo alianzisha mjadala huo wa uchaguzi wa 2022 ingawa katika mazishi ya mwanasiasa Kenneth Matiba Rais Kenyatta na Bw Odinga waliwaonya wanasiasa dhidi ya kuanzisha kampeni za mapema na badala yake wahudumie Wakenya.

Aliposimama kuzungumza, Bw Odinga hakugusia suala hilo na badala yake akatetea maridhiano kati yake na Rais akisema siasa wakati mwingine huhitaji ubunifu na tajriba.

“Mimi ni mwanasiasa mwenye ujuzi anayeipenda nchi hii. Hatungeendelea kusambaratisha nchi ndiposa tuliamua kushirikiana,” akasema Bw Odinga.

Aliwataka wanaouliza kwa nini aliamua kushirikiana na hasimu wake wa kisiasa kubadilisha mtazamo na kujiuliza ni matunda yapi yalitokana na maafikiano hayo.

Aidha Bw Odinga aliwaonya waliofuja fedha za wananchi na kuendelea kuzitoa kama michango katika hafla ya Harambee kwamba watajipata pabaya hivi karibuni.

Viongozi wengine walioandamana na Bw Odinga walionyesha utiifu wao kwake na kumtaka asibabaike katika juhudi zake za kutetea wananchi.

Wanasiasa wanataka kuniua, alia Atwoli

VICTOR OTIENO na JUSTUS OCHIENG

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli amedai kuwa maisha yake yako hatarini. Akiwahutubia wanahabari katika Chuo cha Leba cha Tom Mboya, Kisumu Bw Atwoli alidai kuwa amepokea habari kuwa kuna wanasiasa fulani ambao wamewakodi wahuni ili wamuue katika muda wa wiki moja ijayo.

Bw Atwoli alisema vitisho hivyo vinatokana na matamshi yake kuhusiana na masuala yenye “faida” kwa taifa hili.

“Hivi ni vitisho vya watu wachache ambao wamekodisha majambazi kuniua kwa muda wa wiki moja ijayo. Tayari nimepiga ripoti kwa serikali na nimehakikishiwa kuwa nitalindwa,” akasema Bw Atwoli.

Alipotakiwa kutaja kituo cha polisi ambako amepiga ripoti kuhusu vitisho hivyo, Bw Atwoli alisema: “Nimewaarifu maafisa husika. Vitengo vyote vya usalama vina habari kuhusu mipango hiyo.”

Lakini Msemaji wa Polisi Charles Owino alisema hana habari ikiwa Bw Atwoli amepiga ripoti kwamba maisha yake yako hatarini.

“Sina habari kuhusu ripoti zozote kuhusu vitisho dhidi ya maisha ya Bw Atwoli. Nitawasiliana naye ili anipe ufafanuzi,” akasema Bw Owino, kwa simu.

Atwoli alisema atachukulia suala hilo kwa uzito haswa ikizingatiwa awali vitisho dhidi ya maisha ya viongozi vimepuuzwa ila baadaye wakauawa.

Wakati wa sherehe za Leba Dei Jumanne wiki iliyopita, Bw Atwoli alipendekeza kuwa Katiba ifanyiwe marekebisho ili kubuniwa wadhifa fulani kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atastaafu 2022, akisema “Uhuru bado ni kijana sana na akiachwa hivyo atasumbua.”

“Ikiwa hatutarekebisha Katiba, mnadhani Uhuru ataenda wapi na yeye bado ana umri mdogo. Sharti tuirekebishe hiyo Katiba ili tupate nafasi ya kumpa ili asiwasumbue wale ambao watachukua usukani,” akasema katika bustani ya Uhuru, Nairobi.

Gideon Moi akaangwa mazishini kwa ‘kukataza’ Ruto kusalimia babake

Na FLORAH KOECH

MAGAVANA, maseneta na wabunge Jumamosi walimkabili vikali Seneta wa Baringo Gideon Moi kwa ‘kuhujumu’ azma ya Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Licha ya Bw Ruto na Seneta Moi kusalimiana punde baada ya kuwasili katika mazishi ya mbunge wa Baringo Kusini Grace Kipchoim, eneo la Mochongoi, wandani wa Naibu Rais walimshambulia seneta huyo wakimtaka azime ndoto yake ya kutafuta urais 2022 na kukubali wanasiasa wamtembelee babake, Rais mstaafu Daniel Moi.

Naibu Rais aliwasili kabla ya Seneta Moi na kundi kubwa la wanasiasa kutoka chama cha Jubilee ambao walionekana kuwa tayari kumkabili seneta huyo kwa kumzuia Bw Ruto kukutana na mzee Moi mnamo Ijumaa.

“Wewe ni feki kwa sababu ulimruhusu mtu kutoka nje (ya Rift Valley), Raila Odinga, ambaye alipinga Jubilee katika uchaguzi uliopita kumsalimia babako lakini ukamfungia nje nduguyo,” Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alianza kumrushia Gedion kombora la kwanza. Baadhi ya wanasiasa hao walimuonya Seneta Moi akome kufanya siasa na afya ya babake.

“Wakenya tayari wameamua ni Ruto, iwapo rais mstaafu atasalimiana na watu au la,” alisema mbunge wa Keiyo Kusini, Daniel Rono.

Mbunge wa Marakwet Mashariki Kangogo Bowen aliwaomba wakazi wa Bonde la Ufa kuheshimu viongozi wote wawili.

“Wacheni fahali waendelee kupigana, ikiwa mmoja ataonyesha dalili za kukosa uwezo wa kuzalisha ifikiapo 2022 anafaa kuhasiwa,” alisema Bowen.

Naye mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa alisema Rais Uhuru Kenyatta anaheshimu Katiba, wananchi na naibu wake na kuongeza kuwa Bw Ruto atapeperusha bendera ya Jubilee 2022.

“Usisikilize propaganda iliyoanzishwa na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli,” alisema Bw Ichungwa.

Bw Atwoli alipendekeza kubadilishwa kwa sheria ili kumpa Rais Kenyatta muda zaidi wa kutawala.

Kauli ya Bw Ichungwa iliungwa mkono na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aliyesema wakati wa siasa za urithi uliisha kitambo nchini.

Mwakilishi wa Kike wa Samburu Maison Leshomo alimtaka seneta huyo kuwaruhusu viongozi wengine kukutana na rais mstaafu Moi.

“Mzee Moi alikuwa rais wetu kwa miaka 24. Sio mali ya mtu yeyote, kama viongozi tunahitaji maarifa katika uongozi,” alisema mbunge huyo wa KANU.

Kauli yake ilisisitizwa na Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, Mbunge wa Taveta Naomi Shaaban na waziri msaidizi Rachel Shebesh.

Gavana wa Baringo Stanley Kiptis vilevile alimuonya Seneta Moi dhidi ya kugawanya kura za Rift Valley.

 

‘Msitaje babangu’

Seneta Moi aliyeonekana kukerwa na shutuma dhidi ya familia yake, aliwasihi viongozi wakome kutaja babake katika cheche zao.

“Nawasihi mkome kuhusisha babangu katika suala hili. Sina kinyongo na yeyote anayetaka kujikabili lakini naomba mmutoe babangu katika huu mjadala,”alisema Seneta huyo.

“Kila mtu hapa ni Gideon, Gideon, Gideon…Wakenya wanajua nani wangetaka awaongoze.”

Bw Ruto kwa upande mwingine alihepa suala hilo na badala yake akamsifu marehemu kwa uchapakazi wake hadi wakati wa kifo chake mnamo Aprili 20 kutokana na saratani ya tumbo.

Mnamo Aprili 14, Bw Odinga alimtembelea Mzee Moi nyumbani kwake Kabarak na kupokelewa vyema ambapo Gideon alikuwa miongoni mwa waliomkaribisha.

Mkutano huo ulionekana kama kuidhinishwa kwa muafaka kati ya Raila na Rais Kenyatta na kiongozi huyo wa zamani.

Akemea pasta kanisani kumchochea aachane na mumewe amtafutie bwanyenye

Na CORNELIUS MUTISYA

KAVIANI, MACHAKOS

MAMA wa hapa alimkemea pasta wake mbele ya waumini akimshutumu kwa kumchochea amteme mumewe ili amtafutie mume mwingine tajiri.

Kulingana na mdokezi, mama huyo alikuwa muumini katika kanisa la pasta huyo. Ajabu ni kwamba, pasta hakuwa ameoa licha ya kutimu umri wa kuwa na mke.

Tetesi zilitanda mtaani kuwa mama alikuwa mpango wa kando wa Mtumishi huyo wa Mungu.

Siku moja, pasta alimualika katika ofisi yake ili ampatie ushauri wa kiroho kufuatia maono aliyodai yalimjia usiku akiwa usingizini.

“Alimweleza kwamba alifunuliwa kuwa ndoa yake haikuwa shwari na akamwambia roho alimfunulia aondoke katika ndoa hiyo yenye laana mara moja. Alimwambia angemtafutia mume mwingine tajiri,” alieleza mdokezi.

Hata hivyo, mama huyo alitilia maanani ushauri wa pasta na akaenda nyumbani, alifunganya virago vyake na akakodi chumba sokoni hapa akisubiri pasta amtafutie mume mzuri na tajiri.

“Miezi sita ilipita bila pasta kumtafutia mume na akaanza kukata tamaa. Alianza kujuta kwa kuhadaiwa aondoke katika ndoa yake,” alisema mpambe wetu.

Inasemekana siku ya kioja mama alifika kanisani akiwa na hamaki kuu na akaanza kumfokea pasta peupe.

“Kumbuka ulinidanganya niondoke katika ndoa yangu ukidai ulitumwa na roho mtakatifu. Miezi sita imepita na hujanitafutia mume ulivyodai ulifunuliwa,” alifoka mama huyo huku waumini wakibaki vinywa wazi.

Penyenye zaarifu pasta alipata fedheha na akamwambia mama azidi kusubiri miujiza.

Hata hivyo, waumini walishangaa jinsi pasta alivyoweza kuvunja ndoa akidai angemtafutia mwanamke huyo mume mwingine ilhali yeye mwenyewe hakuwa na mke.

…WAZO BONZO…

BAJETI: Ujenzi wa reli, elimu zapewa kipaumbele

Na CAROLYNE AGOSA

UJENZI wa barabara na reli mpya ya SGR, uimarishaji elimu na uhifadhi mazingira zimepewa kipaumbele katika bajeti ya serikali ya mwaka 2019.

Katika Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 utakaoanza Julai 1, sekta ya usalama na hususan idara za polisi na jeshi pia zitanufaika na ufadhili mkubwa.

Wasiojiweza katika jamii, vijana na wanawake pia wamepewa mgao mkubwa kwenye makadirio hayo yanayoonyesha jinsi serikali inapanga kutumia fedha katika miezi 12 ijayo. Bajeti hiyo ya Sh Sh2.53 trilioni iliwasilishwa Alhamisi katika Bunge la Kitaifa na Kiongozi wa Wengi, Bw Aden Duale.

Inalenga hususan kufadhili ajenda nne kuu za Rais Uhuru Kenyatta kwa kitita cha Sh460 bilioni.

Ajenda hizo ni: chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi, huduma bora za afya kwa kila Mkenya, kujenga takriban nyumba 500,000 za bei nafuu ifikapo 2022, na kuimarisha uzalishaji bidhaa nchini.

Serikali imetenga Sh6.76 bilioni kwa miradi mbalimbali ya kunyunyiza maji mashamba kwa lengo la kuzalisha magunia milioni 2.76 ya mahindi, viazi na mchele. Vilevile, hifadhi ya kitaifa ya chakula cha dharura itapokea Sh1.42 bilioni huku mpango wa kuimarisha uzalishaji nafaka ukipokea Sh1.89 bilioni.

Wakulima nchini watapata afueni baada ya mbolea iliyopunguzwa bei kutengewa Sh4.3 bilioni. Vilevile, serikali imetenga Sh300 milioni kukabiliana na mdudu sugu wa viwavijeshi. Kupunguza hasara zinazotokea baada ya wakulima kuvuna mazao yao serikali imetenga Sh300 milioni kwa bima ya mimea.

Sekta ya elimu imetengewa Sh194.9 bilioni. Serikali ya Jubilee imeazimia kutimiza ahadi ya kutoa elimu ya shule za upili bila malipo kwa kutenga Sh59.4 bilioni kufadhili mpango huo. Elimu ya msingi bila malipo imetengewa Sh13.4 bilioni.

Serikali pia inanuia kutimiza ahadi ya kuondoa ada ya mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa shule za umma ; imetenga Sh4 bilioni kugharamia ada hizo.

Serikali itatumia Sh6 bilioni kuajiri walimu wapya. Vilevile, Sh2.3 bilioni zitatumika kwa lishe ya wanafunzi.

Vyuo vikuu ndivyo vitanufaika zaidi katika bajeti ya mwaka ujao ya elimu baada ya kutengewa Sh90.5 bilioni.

 

HELB yapungua

Hata hivyo, ufadhili kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) umepungua hadi Sh9.6 bilioni kutoka Sh10.1 ilizopewa mwaka wa sasa wa fedha 2017/2018.

Upunguzaji huo umetokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu vya umma– kutoka wanafunzi 564,507 mwaka jana hadi 520,893 mwaka huu.

Taasisi za mafunzo ya kiufundi zitapokea Sh9.7 bilioni katika juhudi za kuimarisha ujuzi wa kiufundi nchini.

Serikali imezingatia athari za mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini kwani imetenga Sh60.4 bilioni za kukabiliana na mafuriko, kuhifadhi maji na kulinda mazingira.

Ujenzi wa mabomba ya maji na maji taka utapata sehemu kubwa ya fedha hizo – Sh31.2 bilioni, huku miradi ya kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji ikitengewa Sh10.8 bilioni.

Masikini, wakongwe, walemavu, mayatima, wanawake na vijana watanufaika na hazina mbalimbali ambazo zimetengewa jumla ya Sh53.9 bilioni. Hata hivyo, kuna hatari ya fedha za wakongwe kukauka kabla mwaka wa fedha kukamilika.

Serikali imewatengea Sh5.1 bilioni pekee licha ya hazina hiyo kuhitaji Sh15.6 bilioni kuwafaa wakongwe hao 523,129 waliokuwa wamesajiliwa kufikia Machi.

 

Afya

Katika sekta ya afya serikali ya Jubilee imetenga Sh44.6 bilioni zitakazofadhili masuala mbalimbali ikiwemo Mpango wa Kukodisha Vifaa vya Matibabu (MES) kwa hospitali kuu za kaunti; na mpango wa huduma za afya bila malipo kwa akina mama na watoto ambao awali uligharamia tu huduma za kujifungua.

Sehemu kubwa ya fedha hizo pia itapewa hospitali kuu za rufaa nchini: Kenyatta (Sh9.4 bilioni) na Moi mjini Eldoret (Sh6.2 bilioni). Taasisi za mafunzo na utafiti wa matibabu zitapokea jumla ya Sh5.3 bilioni huku wahudumu wa afya wanagenzi wakitengewa Sh2.9 bilioni.

Mradi wa kusambaza umeme nchini, kuweka taa barabarani, kuimarisha usambazaji umeme katika maeneo bunge, kupunguza ada ya kuwekewa umeme nyumbani, kukuza kawi inayotokana na mvuke, ugunduzi na usambazaji wa mafuta na gesi ni baadhi ya miradi iliyotengewa Sh45.3 bilioni katika sekta ya kawi.

Wizara ya Fedha imetenga Sh45.3 bilioni kwa ajenda ya Rais Kenyatta ya kujenga nyumba 500,000 za bei nafuu kufikia 2022, kuimarisha mitaa ya mabanda, kujenga nyumba za polisi na askari wa magereza, kuimarisha utoaji huduma katika jiji la Nairobi na viunga vyake, na ustawi wa miji nchini.

 

Mke ataka talaka kwa kunyimwa ‘mlo wa usiku’ na mumewe

Na BRIAN OCHARO

MWANAMKE mmoja amewasilisha kesi mahakamani kutaka apewe talaka ili kumaliza ndoa yake ya miaka 22 kwa madai kuwa mumewe amemnyima tendo la ndoa.

Lizzie Mapenzi Harrison anataka ndoa kati yake na mumewe John Musunza Muthengi kusambaratishwa kwa kusema ndoa hiyo haiwezi kuokolewa kutokana na uzinzi wa mumewe unaochangia amnyime ‘mlo wa usiku’.

Kupitia kwa wakili wake Michael Oloo, mwanamke huyo alisema mumewe ametelekeza familia yake na kuondoka nyumbani. Alisema pia kuwa mwanamume huyo alikuwa akimpiga sana mara kwa mara, hatua ambayo humlazimu kuondoka nyumbani kwenda kwa jirani.

“Mlalamishi anasema kuwa kwa sababu ya udanganyifu katika ndoa, dhuluma na kutelekezwa, na utengano wa mara kwa mara, hawezi kuendelea kukaa katika ndoa hiyo. Anaamini kuwa ndoa hiyo haiwezi kuokolewa,” alisema katika stakabadhi alizowasilisha mahakamani.

Walifanya harusi eneo la Jomvu Kuu, Mombasa mwaka 1996 na wana watoto wawili ambao ni watu wazima.

Bi Mapenzi alisema ndoa yao ilianza kutatizika mwaka wa 2007 alipogundua kuwa mumewe alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, ambaye pamoja walikuwa na mtoto.

Kutoka wakati huo, amekuwa mkali kwake, alieleza. Kutokana na uhusiano wa mapenzi nje ya ndoa na mtoto mwingine nje ya ndoa, alieleza kuwa ulileta matatizo katika ndoa yao. Mama huyo alielezea hofu yake kuhusiana na mali yao, ambayo iko kwa jina la mumewe.

“Mwaka wa 2013, mume wangu alininyima tendo la ndoa kwa kuhamia chumba tofauti. Kutokana na hilo, nilihisi kutokuwa na thamani yoyote,” alisema.

Kutoka wakati huo mpaka leo, wamekuwa wakiishi vyumba tofauti kwa sababu mumewe amekuwa na uadui mkubwa na kushiriki mapenzi nje ya ndoa.

Mwanamke huyo alisema juhudi za kuokoa ndoa yake kwa kukutana mara nyingi na wazazi zimekataa kuzaa matunda kwa sababu mwanamume huyo amekataa kuacha uzinzi.

Zaidi, alikataa kugawanya mali yao zaidi ya kukataa kuwatunza wanawe ikiwe ni pamoja na kuwalipia karo ya shule.

Alieleza mahakama kuwa maisha kwake yamekuwa magumu sana tangu mumewe alipoanza uhusiano mwingine.

Serikali yawazia kuzuia matumizi ya mafuta taa

Na PETER MBURU

MAMILIONI ya Wakenya ambao hutegemea mafuta ya taa kwa kupika na kupata mwangaza huenda wakalazimika kutumia mbinu nyingine baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi nchini (ERC) kupendekeza kuondoa bidhaa hiyo sokoni.

ERC inasema kuwa utumiaji wa mafuta ya taa nchini umezidi na kuzidisha madhara yake kwa watu na mazingira, na hivyo inataka kupandisha bei yake kufikia ile ya mafuta ya dizeli kama mbinu ya kuwafanya Wakenya kutoyanunua.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Pavel Oimeke Jumamosi alieleza Taifa Leo kuwa kutokana na bei ya chini ya mafuta taa, wauzaji watundu wamekuwa wakichanganya bidhaa hiyo na mafuta ya dizeli na kuwauzia watumizi wa magari, jambo linaloharibu injini za magari.

Bw Oimeke, ambaye alikuwa akizungumza katika kongamano la kujadili masuala ya kawi na watumizi, alisema utundu huo umeharibia Kenya biashara ya diseli na mataifa ya nje kama Uganda, Rwanda, Burundi na sehemu za Tanzania ambayo sasa yamechoshwa na kuuziwa mafuta machafu.

“Mamlaka imekuwa ikishauriana na wizara ya fedha na ya kawi kwa nia ya kushinda changamoto ya kuchafuliwa kwa mafuta. Kwa sasa Kenya inatumia lita milioni 33 za mafuta taa japo inafaa kuwa chini ya lita milioni 5 kwa mwezi,” akasema Bw Oimeke.

Alisema, hata hivyo kuwa lita milioni 27 huishia kutumiwa na magari kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuchanganya na mafuta ya diseli na hivyo kuharibu magari kwa wingi.

Bw Oimeke alitaja bei ya chini ya mafuta taa kuwa sababu ya utumizi huo mkubwa, na hivyo akasema ERC imeamua kuongeza bei ya mafuta taa ili kutoa suluhu.

“Tunataka serikali kuongeza ushuru kwa mafuta taa badala ya bidhaa nyingine za petroli, ili kuokoa Sh34 billioni za ushuru tunaopata kutoka mataifa ya nje, kuokoa misitu na afya ya Wakenya,” akasema Bw Oimeke.

Hata hivyo, Wakenya watapewa mbinu mbadala kama mpango wa gesi za bei rahisi pamoja na taa zinazotumia nguvu za jua zilizopunguzwa bei na serikali.

Katibu Mkuu wa muungano wa watumizi wa bidhaa (Cofek) nchini Stephen Mutoro alisema kuwa japo wazo la ERC litasaidia kutetea mazingira na afya ya wakenya, ni vyema hatua zichukuliwe kwa mpangilio ili kuzuia kuwaumiza watumizi wa bidhaa hiyo.

“Tunakubaliana na mdhibiti wa kawi lakini hatua hizo sharti zichukuliwe kwa mpangilio,” akasema Bw Mutoro.

Raila atangaza mwisho wa ‘Resist’

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa upinzani, Raila Odinga, Jumanne alitumia sherehe za Leba Dei za mwaka huu, kusitisha marufuku ya wafuasi wake ya kutotumia bidhaa za kampuni ambazo muungano wa NASA ulidai zilisaidia serikali ya Jubilee kuvuruga uchaguzi mkuu 2017.

Alisema marufuku hiyo ilichangia kudorora kwa uchumi na kwa sababu amekubali kushirikiana na serikali, hakuna haja ya kuendelea kususia bidhaa za kampuni hizo.

“Tuliwaambia mkome kutumia bidhaa za Safaricom, Brookside, Bidco na Haco miongoni mwa kampuni nyingine kwa sababu zilikuwa zikisaidia serikali ya Jubilee.

Sasa kwa sababu Rais Kenyatta alinitafuta na mimi nikamtafuta na tukakutana na kuzungumza, ninawaambia endeleeni kutumia bidhaa za kampuni hizo,” alisema Bw Odinga.

Ilikuwa mara yake ya kwanza kurudi Uhuru Park tangu kuapishwa kwake kama rais wa wananchi Januari 30 mwaka huu.

Alisisitiza kuwa muungano wa NASA ungali imara licha ya tofauti kuzuka baada ya kujiapisha na kusalimiana na Rais Kenyatta. “NASA iko na ingali imara. Mnaniona hapa na Musalia Mudavadi. Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula pia wametuma salamu zao,” alisema.

Kwenye sherehe za jana viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri walitumia fursa hiyo kuitaka serikali kusitisha mabadiliko ya sheria za Leba.

Wakihutubu katika bustani ya Uhuru Park ambako sherehe hizo ziliandaliwa, viongozi hao walisisitiza kuwa mabadiliko hayo yananuiwa kunyima wafanyakazi haki zao za kikatiba na hawatayakubali.

“Wafanyakazi wamekataa mabadiliko yoyote ya kisheria ambayo yanalenga kuwanyima haki zao za kikatiba. Tunasema kwamba hatutakubali,” alisema Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (Cotu) Bw Francis Atwoli. Aliwataka wabunge kukataa mabadiliko hayo yakiwasilishwa mbele yao.

Katibu Mkuu wa chama cha walimu Wilson Sossion alisema wafanyakazi hawatakubali wawakilishi wao kuondolewa katika bodi za NSSF na NHIF.

 

Gathimba kuwania mamilioni Matembezi ya Dunia Uchina

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Riadha Duniani (IAAF) limetangaza zawadi nono kwa wanariadha watakaoshindana kwenye Matembezi ya Dunia ya Kilomita 20 mjini Taicang, Uchina, Mei 5-6, 2018.

Kenya inawakilishwa na mshindi wa medali ya shaba ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, Samuel Gathimba.

Tuzo za binafsi ni Sh3,013,725 kwa mwanamedali wa dhahabu, Sh1,506,862 (fedha) na Sh1,004,575 (shaba). Nambari nne hadi sita watatia mfukoni Sh703,202, Sh502,287 na Sh301,372, mtawalia.

Tuzo za timu ni Sh1,506,862 (mabingwa) nao nambari mbili hadi sita watatunikiwa Sh1,205,490, Sh904,117, Sh753,431, Sh602,745 na Sh301,372. Mtembeaji atakayevunja rekodi ya duniani, atapata bonasi ya Sh502,2875.

Mjapani Yusuke Suzuki anashikilia rekodi ya dunia ya wanaume ya saa 1:16:36 aliyoweka katika Riadha za Bara Asia mwaka 2015 nchini Japan. Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya matembezi ya kilomita 20 kwa wanawake ni Mchina Liu Hong. Anajivunia kukamilisha umbali huo kwa saa 1:24:38 mwaka 2015 nchini Uhispania.

Watembeaji 386 kutoka mataifa 49 watashiriki makala ya mwaka 2018.

Ni mara ya kwanza Kenya inashiriki matembezi haya tangu Patrick Mokomba, Mutisya Kilonzo, William Sawe na Isaac Kiplimo wamalize makala ya mwaka 1989 katika nafasi za 74, 78, 96 na 98 mtawalia kutoka orodha ya washiriki 130 mjini Catalunya nchini Uhispania.

Gathimba, 41, alishindia Kenya medali ya matembezi ya Jumuiya ya Madola alipokamilisha nyuma ya Dane Bird-Smith (Australia) na Muingereza Tom Bosworth kwa saa 1:19:51 mjini Gold Coast mnamo Aprili 8.

Muda wake ulikuwa sekunde 49 nje ya rekodi ya Afrika inayoshikiliwa na Mtunisia Hatem Ghoula tangu mwaka 1997.

Kibarua kwa Obiri mita 3,000 Diamond League

Mkimbiaji Sandrafelis Chebet baada ya kukamilisha mbio za nyika katika uwanja wa Posta kwenye barabara ya Ngong Road, Nairobi. Picha/ Geoffrey Anene

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa mbio za mita 5,000, Hellen Obiri atakuwa na kibarua kigumu kuanza Riadha za Diamond League za mwaka 2018 vyema baada ya kitengo atakachoshiriki nchini Qatar hapo Mei 4 cha mbio za mita 3000 kuvutia majina makubwa.

Bingwa huyu wa dunia wa mbio za mita 3000 za Riadha za Ukumbini mwaka 2012, ambaye pia anajivunia mataji ya dunia na Jumuiya ya Madola, atakabiliana na bingwa wa dunia wa Mbio za Nyika Agnes Tirop na bingwa wa dunia wa mbio za mita 3000 kwa wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 18 mwaka 2013 Lilian Kasait.

Wakenya wengine katika kitengo hiki ni mshindi wa nishani ya fedha ya mbio za mita 2000 kuruka viunzi na maji mwaka 2015 Sandrafelis Chebet, bingwa wa Afrika wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji Norah Jeruto, bingwa wa dunia wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji mwaka 2015 Hyvin Kiyeng’, bingwa wa Mbio za Nyika za Afrika mwaka 2011 Caroline Kipkirui na Mary Kuria, ambaye alifika fainali ya mbio za mita 1500 kwenye Jumuiya ya Madola mjini Gold Coast wiki tatu zilizopita.

Kutazama Elijah Manangoi na nduguye wakimenyana? Utasubiri zaidi

Na GEOFFREY ANENE

WAPENZI wa riadha watalazimika kusubiri zaidi kuona ndugu na mabingwa wa duani Elijah Manangoi na George Manangoi wakitoana jasho katika mbio moja.

Hii ni baada ya Wakenya hawa wa dunia kuingia vitengo tofauti vya mbio katika duru ya kwanza ya Riadha za Diamond League itakayoandaliwa jijini Doha nchini Qatar mnamo Mei 4, 2018.

George atawania taji la mbio za mita 1500 naye Elijah ameamua kutimka katika mbio za mita 800.

George, ambaye ni bingwa wa dunia kwa wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 18, atakabiliana na Wakenya wenzake Bethwell Birgen, Collins Cheboi, Vincent Kibet, Jackson Kivuva, Andrew Rotich, Charles Simotwo na Justus Soget pamoja wakiambiaji kutoka Morocco, Canada, Australia, Qatar na Ethiopia.

Bingwa wa Riadha za Dunia za Watu wazima na Jumuiya ya Madola wa mbio za mita 1500 Elijah Manangoi, atashindania taji la mbio za mita 800 dhidi ya Wakenya wenzake Ferguson Rotich, Emmanuel Korir na bingwa wa dunia kwa wakiambiaji wasiozidi umri wa miaka 20 Kipyegon Bett na raia wa Burundi, Antoine Gakeme, ambaye ni mshindi wa medali ya fedha ya mbio hizi za mizunguko miwili katika Riadha za Ukumbini.

Wakali Bram Som (Uholanzi) na Adam Kszczot (Poland) wako katika orodha ya wakimbiaji 11 watakaowania ubingwa wa kitengo hiki.