FATAKI: Ukiachwa kubali yaishe, hii tabia ya kitoto ya kumpapura mwenzio mitandaoni ni ushenzi!

Na PAULINE ONGAJI

Siku kadha zilizopita tulitofautiana na kaka mmoja mtandaoni kufuatia hatua yake ya kuchapisha ujumbe kumtusi binti fulani.

Inasemekana kuwa kaka huyu alikuwa amemtema binti huyo ambaye alikuwa mpenzi wake wa zamani. “Mwanamume akikuacha nenda zako. Badala ya kumfuatafuata ishi maisha yako uache kuwa kama nzi wanavyofuata kinyesi,” aliandika chini ya picha ya msichana huyo.

Hayo hayakuishia hapo tu kwani baadaye dume hili lilichapisha picha yake wakibusiana na binti mwingine huku akidai kuwa alikuwa mpenzi wake mpya pengine kumfanya mshikaji wake wa zamani ahisi wivu.

Bila kuzingatia nini kilichosababisha uhasama baina ya wapenzi hawa wa zamani, suala dhahiri ni kuwa bwana huyu alionyesha tabia ya kipumbavu na kitoto.

Lakini ukichunguza zaidi utapata si yeye tu, wapo wengine. Ni mara ngapi umeshuhudia watu wakielekeza hasira zao mtandaoni baada ya uhusiano wao kuvunjika?

 

Picha

Au hata kuchapisha picha za wapenzi wao wa sasa ili kumtonesha kidonda wa zamani? Kuchapisha picha za wapenzi wao wapya kwenye kurasa zao za Facebook, kwenye WhatsApp miongoni mwa mambo mengine?

Kadhalika kunao wanaochapisha nukuu za matusi mtandaoni ili kuwaudhi wapenzi wao wa zamani.

Pengine unafanya hivi ili kumuudhi mwenzako mbali na maoni yako kupendwa na watu kadha, lakini mwishowe unapaswa kujiuliza ungehisi vipi ikiwa mwenzako angeutangazia umlimwengu wote kuwa amekutema?

Hiyo ni tabia ya kitoto na inasinya hata zaidi hasa ikiwa ni mwanamume aliyeota ndevu anayefanya hivi. Kwani unadhani penzi lako ni oksijeni? Wadhani bila wewe maisha yatamkatikia mwenzako?

 

Kiburi

Watu wanapaswa kukomesha hiki kiburi kinachowadanganya kuwa wana umuhimu sana maishani mwa watu wengine kiasi cha kuwa wakiondoka, basi dunia itafika mwisho.

Kabla ya hata kuingiwa na fikra za aina hii unapaswa kujiuliza mlikutana na mhusika akiwa na umri gani? Kabla ya kuja maishani mwake hakuwa na uwezo wa kupumua?

Je, wewe ni chakula au maji ya mhusika kiasi cha kwamba ukimtema, basi atakufa njaa au kwa kiu? Je, ni wewe pekee uliye stadi katika masuala ya mahaba?

Kwa kifupi acha kuonyesha upumbavu wako mtandaoni. Ukitema au kutemwa na mwenzio, nenda zako kwa amani. Penzi lako sio muhimu sana maishani mwa mwenzio kiasi cha kwamba ukiamuacha basi hakuna mwingine ambaye ataona uzuri wake.

Pindi utakapoelewa, basi pengine tabia za kitoto zitakuondoka.

TAHARIRI: Heko Spika Muturi kukataa ombi tata

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi. Picha/ Maktaba

NA MHARIRI

SPIKA wa Bunge la Taifa, Bw Justin Muturi, Jumanne alitumia busara kwa kukataa ombi la wakili Adrian Kamotho Njenga la kutaka wabunge wamuondoe Jaji Mkuu David Maraga na makamishna wengine sita wa Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).

Bw Muturi alisema Bw Njenga angewasilisha ombi lake mbele ya JSC ambayo ni tume ya kikatiba iliyotwikwa jukumu la kupokea malalamishi yote kuhusu maafisa wa Mahakama akiwemo Jaji Mkuu David Maraga na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Ulikuwa uamuzi wa busara na wa hekima ambao ulizima tetesi kwamba hatua ya Bw Njenga ilikuwa njama ya Jubilee ya kuadhibu Mahakama kwa kutotoa maamuzi yanayopendelea serikali.

Uamuzi wa Bw Muturi umezuia bunge kutumiwa vibaya na watu wanaotaka kugonganisha mihimili mitatu ya serikali; Bunge, Mahakama na Serikali Kuu.

Tunasema hivyo kwa sababu akiwa wakili, Bw Njenga anaelewa jukumu la JSC na japo alilenga makamishna wa tume hiyo, kuna utaratibu aliopuuza makusudi kwa msukumo wa kujitanua kwamba aliangusha majaji iwapo ombi lake lingekubaliwa na kufaulu.

Kumekuwa na tabia ya watu kadhaa ya kutaka kutumia asasi za serikali kulipiza kisasi dhidi ya wanaohisi kuwa wapinzani au kikwazo kwao.

Hii ni tabia inayopaswa kukomeshwa kwa kila hali na Bw Muturi alifaulu kwa hilo alipozima ombi la Bw Njenga.

Kuna haja ya kila asasi ya serikali kuwa makini katika kila hatua inayochukua na kufahamu kwamba inaweza kufanya makosa yanayoweza kuathiri nchi kwa miaka mingi.

Kwa kutowasilisha ombi hilo kwa kamati husika ya bunge, Bw Muturi alionyesha kwamba anaweza kulinda uhuru wa bunge kwa kutoruhusu miswada na mijadala inayoenda kinyume na katiba.

Aidha, alionyesha kwamba japo wabunge wengi ni wa Jubilee, bunge linaweza kukataa kutumiwa kutia muhuri maazimio ya serikali kwa kupitisha miswada inayoenda kinyume cha katiba.

Bw Muturi alisaidia kuiondolea serikali tuhuma ambazo baadhi ya wananchi walikuwa wameanza kuzitoa, kwamba hatua hiyo ni ile ahadi ya kuifunza adabu idara ya Mahakama.

Huu ndio mwelekeo ambao tunatarajia kutoka kwa viongozi na maafisa wa serikali ambao waliapa kulinda, kutetea na kuheshimu katiba yetu.

 

 

Miili ya maafisa wawili kutoka Bomet yapatikana Homa Bay

Na BARACK ODUOR

MIILI ya watu wawili wanaoaminika kuwa wafanyakazi wa serikali ya Kaunti ya Bomet, ilipatikana imetupwa katika Kaunti ya Homa Bay Jumatatu jioni.

Polisi wanachunguza vifo hivyo baada ya kupata miili hiyo katika kijiji cha Kanga Omuga, kaunti ndogo ya Rachuonyo Kusini, ikiwa na majeraha mbalimbali.

Miili hiyo ilipatikana imetupwa kichakani katika barabara iliyo kwenye mpaka wa kaunti za Homa Bay na Kisii.

Kulingana na chifu wa eneo hilo, Bw Joshua Otieno Oluso, wakazi waliona gari aina ya probox likitupa miili hiyo kisha likaondoka kwa kasi kuelekea mahali pasipojulikana.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Homa Bay, Bw Maris Tim, alisema wawili hao walitambuliwa kama Bw Bernard Kimutai Kirui na Bw Rotich Kipkorir Dominic.

Kamanda huyo wa polisi alisema wanaume hao walikuwa wamepeleka pesa kwa benki kugharamia kesi inayoendelea mahakamani katika kaunti. Alisema risiti za benki na pesa zilipatikana kando ya miili hiyo.

 

Wakenya kuhesabiwa idadi Agosti 2019

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) Bw Zachary Mwangi. Picha/ Maktaba

Na LUCY KILALO

SHIRIKA la Kitaifa la Takwimu (KNBS) linapanga kuendesha shughuli ya kitaifa ya kuhesabu watu Agosti mwaka 2019.

Mkurugenzi Mkuu wa KNBS, Bw Zachary Mwangi alisema shughuli hiyo itagharimu Sh18.5 bilioni, ambapo itahusisha wafanyakazi 170,000.

Bw Mwangi aliiambia kamati ya Bunge la Kitaifa ya Kufuatilia Utekelezaji wa Masuala ya Kikatiba, kwamba shughuli yenyewe itafanywa Agosti 24 na 25 mwaka ujao, ingawaje mwigo wake utafanywa tarehe hizo mwaka huu.

Japo watu watahesabiwa 2019, Wakenya watasuburi kwa karibu mwaka moja kupata matokeo kamili.

“Matokeo ya mapema yatatolewa katika muda wa mwezi moja, ripoti ya kimsingi baada ya miezi mitatu, na ripoti yenye taarifa kamili na tathmini kutolewa baada ya miezi 12,” alieleza Bw Mwangi.

Maswali kadha yaliibuka katika kikao cha jana, ambapo mbunge wa Kajiado Mashariki, Bi Peris Tobiko alitaka kujua ikiwa utaratibu huo utawajumuisha waliozaliwa na jinsia zote mbili, kuwa na maelezo ya kuaminika hasa baada ya utata ulioibuka kuhusiana na matokeo ya hesabu ya watu ya 2009 na iwapo teknolojia wanayonuia kutumia itakuwa ya kutegemewa.

Matokeo ya hesabu ya watu ya 2009 yalionyesha kulikuwa na takriban watu 38.6 milioni nchini.
Hesabu ya mwaka ujao itatumiwa katika ugawaji wa raslimali.

 

Uchomaji makaa wapigwa marufuku Narok

Na GEORGE SAYAGIE

SERIKALI ya kaunti ya Narok, imepiga marufuku uchomaji wa makaa kwa muda usiojulikana kufuatia ukataji miti katika misitu ambao umesababisha Kenya kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kaunti za Kitui na Machakos pia zimepiga marufuku uchomaji wa makaa.

Hatua hii inajiri siku mbili baada ya Naibu Rais William Ruto kusimamisha ukataji miti katika misitu yote nchini kwa miezi mitatu ijayo.
Gavana Samuel Tunai aliagiza uchomaji wa makaa kusitishwa mara moja.

Aidha, alipiga marufuku usafirishaji wa makaa katika kaunti hiyo na kuagiza maafisa wa usalama kuhakikisha marufuku hiyo imetekelezwa.

Akiandamana na kamishna mpya wa kaunti hiyo Bw George Natembea na kamanda wa polisi Thomas Ngeiywa, Bw Tunai aliwataka polisi kusaka wanaofanya biashara ya makaa.

Alitangaza marufuku hiyo baada ya kukutana na makamanda wa polisi, wakuu wa wilaya, maafisa wa misitu, maafisa wa shirika la kulinda wanyama pori na maafisa wa ujasusi pamoja wale wa upelelezi wa jinai katika hoteli ya Lexington mnamo Jumapili.

Kwenye taarifa kwa wanahabari, Bw Tunai aliagiza ukataji miti katika misitu ya Mau, Nyakweri eneo la Transmara, Enoosupukia ulioko Narok Mashariki na Loita ulioko Narok Kusini isitishwe mara moja akisema ni haramu.

 

Kufurushwa

“Kutakuwa na msako mkali kuhakikisha wakataji miti katika maeneo haya wamefurushwa na watakaokiuka sheria watakabiliwa vikali,” alisema Bw Tunai.

Aliwaagiza wakazi kuripoti vitendo vya ukataji miti na uchomaji makaa kwa polisi. Alipiga marufuku usafirishaji wa makaa mchana na usiku kwa magari au njia yoyote ile.

Kaunti hiyo inaongoza kwa utoaji wa makaa ikifuatwa na Kajiado.

Watetezi wa mazingira wamekuwa wakionya kwamba misitu asili kama Mau, Nywakweri, Loita, Aitong na Naimina-Enkiyo, ambayo ni chanzo cha mito mingi inaangamia kufuatia shughuli za binadamu. Ukataji miti katika misitu hiyo umesababisha kiwango cha maji katika mito inayoanzia misitu hiyo kupungua.

Kulingana na takwimu za shirika la kulinda misitu nchini kaunti ya Narok ina ekari 139, 298 za misitu ikiwa ni asilimia 16.6 ya misitu yote nchini. Ekari 52,239 zinasimamiwa na KFS na 87,050 zinasimamiwa na serikali ya kaunti hiyo.

Kaunti ya Narok inatoa tani 25 milioni za makaa kila mwaka na uchomaji makaa hayo unasemekana kuwa chanzo cha kuharibiwa kwa msitu wa Mau.

 

Wasiwasi wanawake wengi kujihusisha na ugaidi

Mkewe Sheikh Aboud Rogo aliyeuawa, Hania Sagar, akiwa katika mahakama ya Shanzu, Mombasa Februari 16, 2018. Sagar alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na hakimu Diana Mochache kuhusiana na ugaidi. Picha/ Maktaba

Na MOHAMED AHMED

TARKIBAN wanawake 13 ni ama wanatumikia kifungo, wamewahi kuzuiliwa katika gereza la Shimo La Tewa au wameachiliwa baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na ugaidi.

Ufichuzi huu unakuja huku maafisa husika wakieleza wasiwasi kuhusiana na ongezeko la wanawake kujiunga na makundi hayo ya kigaidi.

Katika uchunguzi wa Taifa Leo tumekusanya idadi hiyo ya wanawake ambao wamewahi kukamatwa baada ya kuhusika na ugaidi.

Mnamo Septemba 11 mwaka 2016 kituo cha polisi cha Central jijini Mombasa kilivamiwa na magaidi.

Magaidi hao walikuwa ni wanawake walioweza kuwaua maafisa wa usalama. Kuhusika kwa wanawake hao katika shambulizi hilo kulipelekea kufichuka baina ya idara za usalama kuwa wanawake wamekuwa katika msitari wa mbele katika makundi ya kigaidi.

Wanawake hao wanaojiunga na makundi hayo ikiwemo Al shabaab wanasemekana kuhusika na kufanya kazi kama vile upishi na kuwa majasusi wa makundi hayo.

Miongoni mwa wa wanawake ambao wanatumikia vifungo kufuatia kuhusika kwao na ugaidi ni pamoja na mke wa imamu aliyeuawa Aboud Rogo, Bi Hania Sagar na Bi Mwanasiti Masha ambaye ni mke wa aliyekuwa mwanajeshi.

Bi Sagar anahudumu kifungo cha miaka 10 huku Bi Masha akihudumu kifungo cha miaka saba katika gereza hilo la Shimo la Tewa.

Wanawake wengine watano ambao wamewahi kushtakiwa kwa mashtaka yanayohusiana na ugaidi ni Ummulkheir Sadri Abdalla, Khadija Abubakar Abdulkadir, Maryam Said Aboud, Halima Adan na Feruz Abubakar Hamid.

Watano hao wapo nje baada ya kuachiliwa kwa dhamana na kesi zao zinaendelea na zitasikizwa mwezi Machi.

Ummulkheir Sadri Abdalla, Khadija Abubakar Abdulkadir, Maryam Said Aboud na Halima Adan walishtakiwa mnamo mwaka 2015 baada ya kukamatwa kwa madai kuwa wanaenda kujiunga na kundi la Al Shabaab.

Bi Hamid alikamatwa eneo la Bondeni Mombasa baada ya kupatikana na vilipuzi. Katika mahojiano Bi Khadija ambaye ni mmoja ya wanawake hao alisema kuwa kesi yao imekuwa ikienda polepole hata hivyo alisema kuwa yupo na matumaini ya kuachiliwa huru.

 

Mswada wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka kuliko Rais wapendekezwa

Na LUCY KILALO

Kwa ufupi:

 • Mswada unapendekeza Waziri Mkuu ambaye atakuwa mkuu wa serikali, atakayewateua na kuwafuta mawaziri, makatibu, mwanasheria mkuu na mabalozi
 • Seneta Mutula Kilonzo amepinga mswada huo akielezea kuwa iwapo kuna nia yoyote ya kubadilisha Katiba, lazima vipengee vyote viangaziwe 
 • Rais lazima awe na umri usiopungua miaka 50
 • Mswada unawataka mawaziri kuteuliwa miongoni mwa wabunge
 • Waziri mkuu ataweza kuondoka ama kujiuzulu iwapo kutakuwa na kura ya kutokuwa na imani naye
 • Unataka kuwepo na afisi ya kiongozi wa upinzani. Waziri Mkuu atakuwa na mamlaka ya kumteua Mkuu wa Mashtaka ya Umma

WADHIFA wa Waziri Mkuu utarudi katika utawala wa Kenya iwapo Kielelezo cha Mswada mpya uliodhaminiwa na Mbunge wa Tiaty, Kassait Kamket (KANU) utapitishwa.

Mswada huo unapendekeza Waziri Mkuu ambaye atakuwa mkuu wa serikali na mwenye mamlaka ya kuwateua na kuwafuta mawaziri, makatibu, mwanasheria mkuu na hata mabalozi.

Wadhifa wa Rais utasalia lakini hatakuwa na mamlaka. Pia hatachaguliwa na wananchi bali na Bunge.

Kiongozi wa NASA Raila Odinga alishikilia nafasi ya Waziri Mkuu baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008 uliokumbwa na ghasia. Nafasi hiyo iliundwa wakati huo kujaribu kutuliza joto la kisiasa kwa kuunda serikali ya muungano. Manaibu wake wakati huo walikuwa Musalia Mudavadi na Uhuru Kenyatta (rais wa sasa).

Mswada huo wa Bw Kamket unapendekeza kuwepo kwa manaibu wawili wa Waziri Mkuu.

Katika harakati za uchaguzi wa 2017, na hata baada ya utata kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais, suala la kuwepo kwa nafasi ya waziri mkuu pamoja na nafasi ya kiongozi wa upinzani limekuwa likichipuka, baadhi ya wanaopendekeza wakisema kuwa ni mojawapo ya suluhisho la kutatua mivutano ya kisiasa nchini.

Mbunge wa Tiaty, William Kassait Kamket. Picha/ Maktaba

Hata hivyo, Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo amepinga mswada huo akielezea kuwa iwapo kuna nia yoyote ya kubadilisha Katiba, lazima vipengee vyote viangaziwe na sio vya nyadhifa za uongozi pekee.

“Ikiwa wanataka hilo, basi kila kitu kwa Katiba kibadilishwe. Kwa sasa naona ni hali ya kujitafutia umaarufu tu wa kisiasa,” alisema katika mahojiano na Taifa Leo.

Bw Kamket anapendekeza katika mswada kuwa Rais achaguliwe na wabunge, asiwe na mamlaka isipokuwa kuwa ishara ya umoja wa kitaifa, na hafai kushikilia nafasi yoyote ya kuchaguliwa ama katika chama cha kisiasa.

“Rais atachaguliwa katika kikao cha pamoja cha Bunge ambacho kitaandaliwa Alhamisi ya kwanza ya kila mwaka wa saba ama kulingana na hali nyingine zilizopo kikatiba,” mswada huo wa Marekebisho ya Katiba 2017 unaeleza.

 

Umri wa rais

Rais huyo lazima pia awe na umri usiopungua miaka 50.

Kwa sasa, mbunge huyo atatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bajeti na Makadirio kutetea mapendekezo yake, hasa jinsi itakavyoathiri matumizi ya fedha za umma.

Baada ya kuwasilishwa bungeni, mswada huo utaelekezwa kwa kamati husika, kabla ya umma kushirikishwa kutoa mapendekezo yake katika muda wa siku 90. Mswada huo unawataka mawaziri kuteuliwa miongoni mwa wabunge.

Waziri mkuu kulingana na mswada huo ataweza kuondoka ama kujiuzulu iwapo kutakuwa na kura ya kutokuwa na imani naye ama serikali yake, hatua ambayo italihitaji bunge kufanya uchaguzi upya.

 

Kiongozi wa upinzani

Mswada huo unataka kuwepo na afisi ya kiongozi wa upinzani. Pia unapendekeza uchaguzi wa madiwani na magavana kuwa Jumanne ya pili ya Desemba kila mwaka wa tano.

Waziri Mkuu vile vile atakuwa na mamlaka ya kumteua Mkuu wa Mashtaka ya Umma baada ya kuidhinishwa na bunge.

Mbali na hivyo, pia unapendekeza mabadiliko katika uteuzi wa maseneta, na kutaka kuwa idadi iongezeke kutoka 47 wanaochaguliwa hadi 94. Kulingana naye, maseneta hao 94, mmoja wa kike na kiume, watawakilisha kila kaunti, na kuchaguliwa na Bunge la Kaunti.

Pia kutakuwa na wengine sita watakaoteuliwa kuwakilisha vijana na wenye ulemavu.

 

Ashangaza kushangilia kukamatwa kwa mumewe

Na DENNIS SINYO 

KIMAMA, MLIMA ELGON

WAKAZI wa sehemu hii walishangaa kumuona mama mmoja akishangilia baada ya kupata habari kwamba mumewe alikuwa amekamatwa na polisi wa utawala.

Mama huyo aliabiri pikipiki hadi kituo cha polisi kudhibitisha kwamba mumewe alikuwa amewekwa kwenye seli kwa kupatikana na kwa mama-pima akinywa pombe haramu.

Wengi walitarajia kwamba mama huyo alitaka mumewe kuachiliwa huru lakini wakashtuka kusikia akisema maafisa walikuwa wamefanya jambo zuri sana.

“Huyu mtu alikuwa amenishinda nyumbani na kama mko naye hapa, najua leo nitalala kwa amani bila kusumbuliwa. Najua atabadilisha tabia zake mbaya,” mama huyo alisema.

Yasemekana mumewe alikuwa akipata hela nyingi kazini lakini alikuwa akizitumia vibaya kwa ulevi na anasa jambo ambalo hakufurahia. Licha ya kumsihi kuacha pombe, jamaa alijifanya kiziwi.

Visa vya jamaa kupoteza pesa na wakati mwingine kuibiwa na wenzake kwa mama pima vilimkera mama huyo na akafurahi alipotiwa mbaroni.

Alidai hiyo ilikuwa nafasi bora ya jamaa kupata funzo ili abadilike. “Mama huyo alidai mumewe alikuwa amemea pembe na kuwadharau watu wote waliojaribu kumshawishi kuacha ulevi,” alisema mdokezi.

Aliwataka polisi kumwadhibu abadilike kabla ya kumwachilia.

Kulingana na mdokezi, mama alirejea nyumbani na kumuacha mumewe kwenye seli akisema hiyo ilikuwa nafasi ya pekee ya jamaa kuacha starehe na ulevi.

Wanakijiji waliokuwa hapo walibaki vinywa wazi wakishangaa mama alipowataka polisi kumnyorosha sawasawa badala ya kuwaomba wamuachilie mumewe.

Baadhi walidai akili ya mama haikuwa sawa kwa kuchochea polisi waendelee kumzuilia baba ya watoto wake na kurudi nyumbani.

 

Uhuru ategwa na wanyakuzi wa ardhi

Na MWANGI MUIRURI

Kwa ufupi:

 • Wakuu serikalini wanahakikisha wanamiliki vipande vya ardhi katika shamba la ekari 40,000 viungani mwa jiji la Nairobi
 • Njama ya kuingilia shughuli hiyo inashirikisha watu 2,500 walionunua hisa katika kampuni hiyo kwa njia za ulaghai kisha wakajitwalia ardhi
 • Sababu kuu ya matatizo ya uhalalishaji wa umiliki ulioagizwa na Rais Kenyatta ni kuwa walionunua hisa kwa ulaghai wanahudumu katika ngazi za juu serikalini
 • Wenyehisa halali wanafaa kuwa 13,500 lakini orodha inaonyesha kuwa kuna jumla ya 15,500

RAIS Uhuru Kenyatta amewekewa mtego na wakuu serikalini na wafanyabiashara wakubwa ambao wanafanya kila juhudi kuhakikisha wamepata hatimiliki za ploti walizopata kwa njia za ulaghai katika shamba la Embakasi Ranching.

Njama ya wakuu hao, walioko serikalini na waliostaafu na wanaoshirikisha maafisa wa juu serikalini, utawala, usalama na wafanyabiashara ni kuhakikisha majina yao yako katika orodha inayotayarishwa na Wizara ya Ardhi ya wenyehisa watakaopewa hatimiliki.

Duru zinasema wanafanya kila juhudi kuhakikisha wana usemi katika shughuli ya kuhalalisha umiliki wa vipande vya ardhi katika shamba hilo la ekari 40,000 viungani mwa jiji la Nairobi.

Kulingana na Katibu wa Wizara ya Ardhi, Dkt Nicholas Muraguri, Rais Kenyatta aliitaka wizara kuhakikisha wenyehisa wamegawiwa ploti zao na kupewa hatimiliki haraka iwezekanavyo. Hii ni kufuatia vilio ambavyo vimekuwa vikimfikia kutoka kwa wenyehisa.

Uchunguzi umebaini kuwa njama ya kuingilia shughuli hiyo inashirikisha baadhi ya watu kati ya 2,500 walionunua hisa katika kampuni hiyo kwa njia za ulaghai kisha wakajitwalia ardhi katika mashamba ya kampuni hiyo. Wenyehisa wengine 13,000 ndio waanzilishi wa kampuni hiyo lakini hawana usemi.

 

Walagai waingiwa na wasiwasi

Hatua ya Rais Kenyatta kutaka wenyehisa halali wapewe mashamba yao imewatia wasiwasi waliopata hisa kwa njia za mkato kutokana na hofu kuwa huenda wakapoteza ardhi waliyonyakua iwapo agizo hilo litatekelezwa kikamilifu, kwa uwazi na haki. Wengi wao tayari wamejenga kwenye ploti hizo.

Rais Kenyatta alikuwa amepangiwa kutoa hatimiliki kwa wenyehisa mnamo Februari 1 mwaka huu lakini hilo halikufanyika. Hii ni baada ya kufahamika wenyehisa halali walikuwa wamepanga kuandamana siku hiyo kwa kile walihofia ni wamiliki wasio halali kunufaika.

Dkt Muraguri anasema anafahamu kuhusu njama za kuvuruga shughuli ya kuhalalisha umiliki. “Tunashughulikia hilo kwa umakinifu zaidi na tumefungua ofisi ya kupokea malalamishi ya wenyehisa. Pia, tumetwaa orodha ya wenyehisa kutoka kwa kampuni hiyo ya Embakasi Ranching ili kubaini wenye hisa halali.

“Hatuna jingine ila tu kuvunja kampuni hii ili mtindo wa utapeli ambao umekuwa ukiendelezwa ukomeshwe. Ni mpango ambao tutaufanikisha kwa umakinifu na wenyehisa halali watapata haki yao, na wale ambao waliingia katika mradi huu kwa njia ya magendo watapoteza,” akasema Dkt Muraguri.

Kwa mujibu wa msemaji wa wenyehisa wa mradi huo, Joseph Njenga, sababu kuu ya matatizo ya uhalalishaji wa umiliki ulioagizwa na Rais Kenyatta ni kuwa wale ambao walinunua hisa kwa ulaghai wanahudumu katika ngazi za juu serikalini.

 

‘Wezi wamo serikalini’

“Walioiba mashamba yetu wamo serikalini na wana ushawishi mkubwa. Wanafanya kila mbinu kuhakikisha wao ndio watakaonufaika na mpango wa kuhalalisha umiliki wa ardhi. Wanamweka Rais kwenye mtego wa kuidhinisha ulaghai wa mashamba,” alisema Bw Njenga.

Mradi wa Embakasi ulianzishwa 1978 kwa lengo la kilimo cha matunda na mboga na ufugaji ng’ombe. Lakini mnamo 1990 uligeuzwa kuwa kampuni ya uuzaji mashamba kupitia hisa.

“Wakurugenzi walianza kuuza ploti kwa matajiri huku nyingine zikinyakuliwa na wakuu serikalini. Wenyehisa halali wanafaa kuwa 13,500 lakini orodha inaonyesha kuwa kuna jumla ya 15,500,” asema Bw Njenga.

Anasema kuwa hisa iliyompa mnunuzi uhalali wa kumiliki robo ya ekari ya ardhi katika mradi huo ilikuwa ikiuzwa kwa Sh4,000 na kufikia 1990 ikaamuliwa kuwa kila mwenyehisa angepewa ploti moja ya ziada.

“Hapo ndipo ukora ulipoanza kuingizwa na wakurugenzi, ambapo wenyehisa wasio na ufahamu, wale waliokuwa wameaga na pia wale ambao hawakuwa wakifuatilia kwa makini shughuli za kampuni walipokonywa ploti zao na zikauzwa,” asema Njenga.

 

Kubadilishwa kwa ploti

Anasema kuwa hali iliendelea kuwa mbaya zaidi ambapo maeneo ya umma katika mradi huo yalianza kuuzwa huku wanyehisa halali wakibadilishiwa ploti zao zilizokuwa katika meneo ya bei za juu na kusukumwa ndani kwa maeneo ya bei za chini.

Katika hatua inayoonekana kama njia ya kuchelewesha shughuli hiyo, wakurugenzi wa kampuni hiyo wametaka kila mwenyehisa kulipa Sh25,000 za hatimiliki.

Lakini Dkt Muraguri amekashifu wakurugenzi hao na kuwataka wakome kudai pesa hizo akisema kuwa serikali itagharamia utoaji wa hati hizo na pia huduma za usoroveya.

Hata hivyo, wakurugenzi hao wakiongozwa na Mwenyekiti, Thuita Mwangi bado hawajapunguza kiwango hicho, wakisema kuwa kampuni hiyo ni ya kibinafsi.
Kulingana na Bw Thuita, wakurugenzi hao wanatathmini agizo la Dkt Muraguri.

Mmoja wa wenyehisa Bi Mary Wambui, ambaye ni mjane wa aliyekuwa Mbunge wa Starehe Bw Muhuri Muchiri alieleza Taifa Leo kuwa amepokonywa ploti tano. Anasema wenyehisa wana wasiwasi kwani kuna hatari ya wanyakuzi kutumia hila kupata hatimiliki huku wenyehisa halali wakikosa.

 

SHANGAZI: Nilimfumania ndani ya gari akigawa asali. Nitafanya nini?

Na SHANGAZI SIZARINA

Pokea salamu zangu shangazi. Ninaumwa sana moyoni baada ya mwanamke mpenzi wangu kusaliti penzi letu. Juzi mimi naye tuliandamana na mwanaume rafiki yangu katika maskani fulani ya starehe. Tuliburudika kwa vinywaji na wakati fulani wawili hao wakatoka kila mmoja akisema anaenda msalani. Walipokawia nilitoka kuwatafuta na nikawafumania ndani ya gari la rafiki yangu. Baadaye mpenzi wangu aliniomba msamaha akidai alikuwa amelewa na hakujua alichokuwa akifanya. Ninampenda sana na sijui nitafanya nini.
Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa kikulacho ki nguoni mwako. Sasa umejua kuwa mwanamume huyo unayemuita rafiki yako si rafiki hasa bali ni mbwa mwitu ndani ya ngozi ya kondoo. Sidhani unaweza kumwamini tena kwa hivyo itabidi uvunje urafiki huo. Huenda mpenzi wako pia alikuhadaa eti alikuwa mlevi, lakini unaweza kumpa nafasi nyingine kisha uendelee kuchunguza kwa makini mienendo yake.

 

Nilipata mchumba akiwa na wake wa zamani

Vipi shangazi. Nimechumbia mwanamke fulani na tunaendelea kupanga harusi. Hata hivyo nilishangaa sana juzi nilipomtembelea nyumbani kwake kama kawaida na nikampta na mwanaume aliyekuwa mpenzi wake. Sijamuuliza walikuwa wakizungumzia nini lakini nina wasiwasi. Nishauri.
Kupitia SMS

Bila shaka ni lazima uwe na wasiwasi hasa ukizingatia kwamba wawili hao walikuwa wapenzi. Isitoshe, mwanaume huyo amemtembelea wakati ambao mnaendelea na mipango yenu ya harusi. Badala ya kunyamaza na kuumia kwa hofu, ni muhimu umuulize mpenzi wako ili ujue kiini hasa cha mpenzi wake wa zamani kumtembelea.

 

Ananikataza kulima shamba

Vipi shangazi? Kuna mwanamke ambaye tumekuwa na uhusiano kwa mwaka mmoja sasa na nampenda sana. Tatizo ni kuwa nikitaka penzi lake yeye hunipa vijisababu vya kila aina. Amenishinda, tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Kila kitendo kina sababu. Labda mwananke huyo hakupendi ama anahisi kwamba unamharakisha sana. Kumbuka mmejuana kwa mwaka mmoja pekee na huenda anahitaji muda zaidi ili akujue vizuri. Kuwa na subira kwani mvumilivu hula mbivu.

 

Aliaga nikiwa mjamzito

Habari yako shangazi. Nina umri wa miaka 21 na ninaishi maisha ya kujuta. Sababu ni kuwa nilipata mtoto nikiwa mchanga baada ya kudanganywa na mwanamume fulani. Aliaga dunia nikiwa na mimba ya mtoto huyo na kuniachia mzigo wa kumlea. Natafuta mwanamume ambaye atanioa pamoja na mtoto wangu na amkubali kama wake. Tafadhali nisaidie.
Kupitia SMS

Tunaambiwa kuwa majuto ni mjukuu, huja kinyume. Kadhalika, maji yaliyomwagika, hayawezi kuzoleka. Ninaamini ujumbe wako huu utawafikia wanamume wanaotafuta wake na labda kuna atakayevutiwa akitafute. Nakutakia kila la heri.

 

Amekosa uaminifu
Kwako shangazi. Kuna kijana fulani ambaye amekuwa akiniambia eti ananipenda lakini juzi nilishtuka nilipomfumania na msichana mwingine. Baadaye alinitumia ujumbe wa SMS akiomba nimsamehe na kusisitiza kuwa ni mimi tu anayependa. Tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Hata kama unafikiria kumsamehe, ni muhimu kwanza ujue iwapo kuna chochote kinachoendelea kati yake na msichana uliyewapata pamoja. Ni baada ya hapo ambapo utaweza kufanya uamuzi wa busara.

 

Amedai kuonja asali, nipakue?
Kuna mwanaume ambaye tumekuwa na uhusiano kwa miezi kadhaa na tumekutana mara tano tangu tujuane. Amenialika kwake na ameniambia wazi kuwa anataka asali. Je, niende ama nisiende?
Kupitia SMS

Umejua kwa hakika kwamba mwaliko wa mwanaume huyo kwake ni wa kuonja asali. Kwa sababu hiyo, ukienda atajua kwamba umempelekea asali na ukikataa hatakuelewa. Kama huko tayari kumpakulia, basi usiende. Kutana naye mahali tofauti umwelezee sababu.

 

TAHARIRI: Haki itendewe wote Turkana

Kituo cha utathmini wa mafuta cha Ngamia 1, Turkana. Picha/ Maktaba

Na MHARIRI

SUALA kuhusu ugawaji wa mapato yanayotokana na uchimbaji wa madini limekuwa likijadiliwa katika siku za majuzi. Sababu kuu ya mjadala huu mpya ni pendekezo kwenye Mswada unaopendekezwa kuhusu ugawanaji wa mapato hayo.

Kulingana na mapendekezo ya mswada huo, Serikali za kaunti zinapaswa kupata asilimia 15 huku jamii za maeneo kunakochimbwa madini zikipata asilimia tano. Sehemu nyingine ya asilimia 80 inafaa kwenda kwa Serikali.

Mapendekezo hayo ni kinyume na mswada wa 2016, ambao haukutiwa sahihi, uliopendekeza asilimia 20 kwa serikali husika ya kaunti na asilimia 10 kwa jamii.

Wale wanaopinga mswada mpya wanaonelea kuwa kaunti na jamii husika wameonewa kwa kupunguziwa mgao wao. Wale wanaoshikilia maoni haya wana kila sababu ya kuchukua msimamo huo.

Hii ni kwa sababu jamii yoyote ile inafaa kupata manufaa kutokana na raslimali inayopatikana mahala wanapoishi.

Jamii ambayo zaidi inahusika katika suala hilo ni ya kaunti ya Turkana, ambako kumegunduliwa kiasi kikubwa cha mafuta.

Ugunduzi huu ulipotangazwa ulileta matumaini makubwa kwa wakazi wa Turkana, kuwa hatimaye wamejaaliwa raslimali ambayo itakuwa chombo cha kuwatoa kwenye matatizo na umaskini, ambao wamekuwa nao kwa miongo na miongo.

Sehemu kubwa ya Turkana ni kame, jambo ambalo limefanya wakazi wake kutegemea zaidi ufugaji. Hata hivyo, ufugaji huo mara kwa mare umekuwa unatatizwa na ukame. Hivyo kupatikana kwa mafuta katika kaunti yao kulitarajiwa kusaidia kubadilisha hali ya maisha ya wakazi.

Ingawa raslimali zote ni za kitaifa, ni makosa kwa Serikali Kuu kujitengea sehemu kubwa ya mapato na kupunguza inayofaa kufika mashinani ili kunufaisha jamii inayoishi sehemu husika. Usawa unafaa kuwepo ili wakazi hao nao wafurahie matunda ya raslimali zao.

Kile Serikali ingefanya ni kushikilia pendekezo la awali la asilimia 20 kwa kaunti na 10 kwa jamii husika. Hatua ya kupunguza mapato yanayofika mashinani inatoa picha mbaya, kwani inaonekana kama serikali haijali maslahi ya jamii zinazoishi maeneo yenye madini.

Tunaomba Serikali kutathimini upya pendekezo lake na kuhakikisha kuwa haki inatendewa wakazi wa Turkana na maeneo mengine yenye raslimali za madini.

Kanisa alimozikwa Yesu lafungwa

Na AFP

JERUSALEM, ISRAELI

VIONGOZI wa kidini nchini Israeli Jumatatu walifunga kanisa moja la kihistoria, ambako Yesu anaaminika kuzikwa, kulalamikia sheria mpya ya kuyatoza kodi makanisa.

Viongozi hao walisema walichukua hatua hiyo, kama juhudi za kuishinikiza serikali kuitathmini upya sheria hiyo.

Aidha, walisema kuwa kanisa hilo litabaki limefungwa hadi pale watakapotoa tangazo la kufunguliwa kwake tena.

Kanisa hilo huwa muhimu sana, kwani huwa linatumika na waumini wa makanisa ya Orthodox kutoka Ugiriki, Kanisa la Kiarmenia na Wakatoliki kuendeshea ibada zao.

Kanisa hilo linachukuliwa kuwa eneo takatifu zaidi katika dini ya Kikristo, kwani limejengwa katika eneo ambalo Yesu anaaminika kusulubiwa.

Malalamishi makuu ya viongozi ya kidini ni kwamba kodi hiyo ni sawa na kuingilia utakatifu wa makanisa.

Mbali na hayo, wanashikilia kwamba hilo litatoa nafasi kwa ufisadi kuanza katika shughuli za usimamizi wa masuala ya kanisa. “Lazima sheria hiyo itathminiwe upya ili kuhakikisha kuwa utakatifu wa kanisa umedumishwa,” akasema kiongozi mmoja.

Israeli ni baadhi ya nchi ambazo haziingilii masuala ya dini hata kidogo, ila sheria hiyo imezua hisia mbalimbali katika ulimwengu wa kidini.

 

Nigeria yaanza kusaka wasichana 110 waliotekwa na Boko Haram

Na AFP

ABUJA, Nigeria

SERIKALI ya Nigeria imeanza harakati za kuwatafuta wasichana 110 wa shule moja, wanaoaminika kutekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram wiki iliyopita.

Serikali ilisema imetuma wanajeshi zaidi na ndege ili kuimarisha operesheni hiyo.

Wasichana hao walitoweka muda mfupi baada ya wanamgambo hao kuvamia shule yao Jumatatu iliyopita katika mji wa Dapchi, jimbo la Yobe.

Rais Muhammadu Buhari alitaja kisa hicho kama “janga la kitaifa” huku akiomba msamaha kwa familia za wasichana hao. Tukio hilo linajiri baada ya jingine lililofanyika mnamo 2014, ambapo wasichana 276 walitekwa nyara na kundi hilo.

Familia za wasichana hao zimekumbwa na ghadhabu, baada ya ripoti kuibuka kwamba serikali ilikuwa imewaondoa wanajeshi wake katika maeneo muhimu ya Dapchi, mwezi uliopita. Mji huo uko umbali wa kilomita 275 kutoka eneo la Chibok, ambako shambulio la 2014 lilifanyika.

Wanamgambo hao wanadaiwa kuvamia Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi ya Serikali, ambayo huwa na wasichana pekee.

Wakazi walio karibu walisema kuwa vikosi vya kijeshi vilijibu shambulio hilo mara moja kwa kutumia ndege za kivita.

Awali, mamlaka zilikanusha kwamba wasichana hao walikuwa wametekwa nyara, zikishikilia kuwa walikuwa wamejificha ili kutoonekana na washambuliaji hao.

Kundi la Boko Haram limekuwa likipigania kubuniwa kwa taifa huru katika ukanda wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hadi sasa, wasichana waliotekwa nyara awali wangali kufahamika waliko.

Serikali baadaye ilitoa taarifa ikithibitisha kutekwa nyara kwa wanafunzi hao.

 

Uvamizi shuleni

“Serikali ya Nigeria ingependa kuthibitisha kwamba wanafunzi 110 kutoka Tasisi ya Kiufundi ya Serikali, mjini Dapchi hawajulikani waliko baada ya wanamgambo wa Boko Haram kuvamia shule yao,” ilisema taarifa kutoka Wizara ya Habari na Mawasiliano.

Kisa hicho kimeibua maswali kuhusu hali ya utayarifu wa jeshi hilo kuwakabili wanamgambo hao. Aidha, hili linajiri baada jeshi hilo kudai kwamba lilikuwa tayari kuwazima wanamgambo hao.

Kauli ya Rais Buhari pia imekosolewa vikali na baadhi ya wanaharakati, huku wakiamini kwamba serikali imeshindwa kabisa kulikabili kundi hilo.

Alipochaguliwa kama rais mnamo 2015, Bw Buhari, ambaye alikuwa mtawala wa kijeshi aliahidi kukabiliana na kundi hilo. Hii ni baada ya mtangulizi wake, Goodluck Jonathan kulaumiwa vikali kwa kushindwa kulikabili.

Mwalimu mmoja katika taasisi hiyo, Amsani Alilawan, alisema kwamba kulikuwa na wanajeshi katika eneo hilo hadi mwezi uliopita, ila wakaondolewa.

“Waliwaondoa wanajeshi hao wote na kuwahamisha katika maeneo mengine,” akasema.

 

Raia wa Urusi aliyejitapa hatumii pufya afeli vipimo kwenye Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

MWANAMICHEZO Nadezhda Sergeeva aliyejigamba hatumii dawa za kusisimua misuli amefeli vipimo vya matumizi ya dawa hizo haramu.

Kwa mujibu wa tovuti ya Huff Post, raia huyo wa Urusi, ambaye anashiriki fani ya bobsled alionekana kwenye video katika mtandao wa Instagram mnamo Februari 15 akivalia tishati iliyokuwa na maandishi “I Don’t Do Doping (Mimi situmii dawa za kusisimua misuli).”

Siku tatu baadaye, Sergeeva alipatikana na kosa la kutumia dawa zilizopigwa marufuku kwenye Olimpiki za msimu wa baridi mjini Pyeongchang nchini Korea Kusini.

Alikataa kwamba alitumia dawa zilizomfanya afeli vipimo hivyo. Mnamo Februari 18, Sergeeva, ambaye alimaliza katika nafasi ya 12 katika kitengo cha bobsleigh cha wachezaji wawili wanawake, alipatikana ametumia dawa ya kutibu ugonjwa wa angina iliyokuwa na dawa za kumfanya awe bora kuliko wapinzani wenzake.

Siku tano kabla ya kufeli vipimo hivyo, Sergeeva hakuwa amepatikana na kosa hilo. Alisema hakutumia dawa hizo. Rais wa mchezo huo nchini Urusi, Alexander Zubkov alisema mwanamichezo huyo hakuambiwa atumie dawa zozote kwa matibabu.

Mtoto aliyepotea apatikana amefariki ndani ya gari la askofu

NA MOHAMED AHMED

POLISI jijini Mombasa wanachunguza kifo cha mtoto wa shule ya chekechea aliyepatikana amefariki ndani ya gari la askofu wa kanisa la Ushindi Baptist eneo la Likoni, Mombasa.

Mwili wa Emmanuel Wasike mwenye umri wa miaka sita ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Amart Academy ulipatikana Jumatatu asubuhi ukiwa katika viti vya nyuma vya gari hilo lilokuwa limeegeshwa katika uwanja wa kanisa.

Gari hilo aina ya Toyota Allion linamilikiwa na askofu wa kanisa hilo, kulingana na polisi.

Dereva wa kanisa ambaye alikuwa ameenda kubadilisha betri ya gari hilo aliupata mwili wa kijana huyo ukiwa ndani ya gari hilo, kulingana na mshiriki wa kanisa hilo.

Mtoto huyo alikuwa ameripotiwa kupotea mnamo Jumapili na mamake. Akizungumza na Taifa Leo, babake kijana huyo Richar Wasike alisema kuwa mtoto wake hakurudi pale walipokuwa baada ya ibada.

“Kawaida huwa kuna makundi ya ibada yakiwemo yale ya watoto na huwa anaenda kuungana na watoto wenzake na baada kuja kutuunga sisi. Lakini siku hiyo baada ya ibada hatukumona,” akasema Bw Wasike.

Alisema kuwa aliweza kuondoka kanisani hapo akijua kuwa Emmanuel alikuwa na wenzake.

 

Kumtafuta

“Mamake alianza kumtafuta kanisani na baadaje kuja nyumbani akijua kuwa nimeenda naye na alipofika nyumbani ndipo alipojua kuwa sikuwa nimetoka na watoto. Tulienda kanisani kumtafuta na baada tukaripoti polisi,” akasema Bw Wasike.

Jumatatu asubuhi wazazi hao walipigiwa simu kutoka kanisani na kujuzwa kuwa kijana wao amepatikana ndani ya gari akiwa amekufa.

Kulingana na polisi gari hilo lilikuwa halijafungwa. Polisi waliokwenda katika eneo alipopatikana mtoto huyo walisema kuwa mtoto huyo anaonekana kufariki baada ya kukosa hewa wakati alipojifungia ndani ya gari hilo.

Afisa mkuu wa upelelezi enoe la Likoni Henry Ndombi alisema kuwa wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo cha mtoto huyo they have launched investigations into the incident.

Alisema kuwa tayari wameanza kuwahoji washiriki wa kanisa hilo ambao walikuwepo kanisani siku mtoto huyo alipopotea.

“Mtoto huyo hajaonekana na majeraha yoyote mwilini lakini uchunguzi wetu wa kina utatupa taarifa zaidi,” akasema Bw Ndombi.

Alisema mwili huo umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya mkoa wa Pwani na unasubiri upasuaji.

Kalameni afukuzwa kanisani kwa kulemewa kutoa sadaka na fungu la kumi

Na LEAH MAKENA

MUTHAMBI, CHOGORIA

POLO wa hapa alijipata pabaya pale jina lake lilipoondolewa kwenye sajili ya washirika wa kanisa kwa madai kwamba alizembea kutoa sadaka.

Penyenye zasema kuwa pasta alianza kulalamika kuwa washiriki hawakuwa wakitoa sadaka wakidai hali ya maisha ilikuwa imewalemea.

Yasemekana pasta aliagiza uchunguzi ili kubaini waliokuwa wamechukua muda mrefu bila kutoa sadaka na fungu la kumi.

“Hili kanisa haliwezi kusonga mbele bila pesa. Kila siku mnapata kikombe cha chai baada ya ibada pamoja na huduma zingine za bure. Mnataka tuendeshe ibada vipi iwapo nyinyi sio waaminifu kwa kutoa sadaka?” pasta aliteta.

Baada ya kufanya kazi yao, wachunguzi walimkabidhi mchungaji orodha ya washiriki waliokuwa wamezembea kutoa fungu la kumi kwa muda wa miezi kumi mtawalia.

Kulingana na mdokezi, baada ya kukagua orodha, pasta alimkabidhi jamaa barua ya kumpiga marufuku kuwa mshiriki wa kanisa kwa kutotoa chochote kwa mwaka mmoja.

Minong’ono yasema kuwa baadhi ya washiriki walikashifu hatua ya pasta ila wakashindwa kumkosoa hadharani kwa kuogopa kutengwa.

Apigwa na butwaa demu kutafuna nyama kilo moja

Na TOBBIE WEKESA

UGENYA, SIAYA

KALAMENI mmoja alipigwa na butwaa baada ya mrembo kutafuna kilo moja ya nyama peke yake.

Kulingana na mdokezi, ilikuwa ni siku yake ya kwanza kukutana na mrembo ana kwa ana. Wawili hao walikutana Facebook, wakajuana na kisha wakaanza harakati za kuchumbiana.

Inadaiwa polo alimuomba mrembo wakutane katika hoteli ili waweze kujuana zaidi. Mrembo alikubali ombi la polo la kukutana. Polo alianza kuwaza ni kitu gani angemnunulia ili afurahie.

Duru zinaarifu kwamba mrembo alipowasili, polo aliagiza kilo moja ya nyama choma, kuku robo na chupa kadhaa za soda. Penyenye zinasema baada ya weita kuandaa meza, mrembo aliivamia nyama kwa fujo. Polo aliamua kula kuku choma kwa vile hakuwa mraibu wa nyama choma.

Muda si muda, sahani ilibakia tupu. Polo alibaki kumtazama tu huku akitamani kucheka. “Kwani ulikuwa na njaa gani! Tangu uinamishe kichwa hutaki kutazama juu,” polo alimuuliza mrembo kwa mshangao. Mrembo alienda moja kwa moja hadi kwa soda na kuanza kuteremsha kana kwamba hakusikia maneno ya polo.

Polo aliendelea kula kuku wake bila haraka. Baada ya muda mfupi, mrembo alimaliza kunywa soda. “Nikuongezee nyama nyingine?” polo alimuuliza mrembo kwa utani.

Mrembo alimuangalia polo na kumshukuru. “Nashukuru sana kwa kuninunulia nyama. Mimi napenda sana kula nyama choma. Hata kesho tukikutana, ninunulie tu choma. Sitaki kitu kingine,” mrembo alimueleza polo.

Tukio hili lilimshangaza polo zaidi. “Unamaanisha umekula nyama kilo moja peke yako na kuimaliza? Na bado ukaongezea soda. Kwani tumbo lako ni pana aje?” polo alishangaa.

Inadaiwa mazungumzo aliyotaka polo na mrembo hayakufanyika tena.

“Najua umeshiba. Tutazungumza tutakapokutana tena,” polo aliamka akalipa chakula na kuondoka.

Mchakato wa kumng’oa Jaji Maraga waanza

Na BENSON MATHEKA
WAKILI mmoja wa Nairobi, amewasilisha ombi bungeni akitaka Jaji Mkuu David Maraga na makamishna saba wa Tume ya Huduma kwa Mahakama (JSC) waondolewe.

Katika ombi hilo, wakili Adrian Njenga anataka bunge kuwaondoa makamishna hao kwa kile anachotaja kuwa na tabia isiyofaa. Bw Njenga amewataja Bw Maraga, naibu wake Philomena Mwilu, Jaji Mohammed Warsame, Jaji Aggrey Muchelule, wakili Tom Ojienda, Bi Emily Ominde na Bi Mercy Deche katika ombi lake kwa bunge.

Wakili huyo anawalaumu makamishna hao wanaowakilisha vitengo tofauti vya mahakama na chama cha mawakili (LSK) kwa kukiuka Katiba.

“Wameshindwa kulinda na kufanikisha uhuru na uwajibikaji katika Mahakama na uwazi katika utoaji wa haki,” anaeleza katika ombi lake.

JSC ina makamishna kumi na wawili. Mbali na anaotaka waondolewe, wengine ni walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta ambao walihojiwa na bunge wiki jana.

Wao ni Profesa Olive Mugenda, Bw Patrick Gichohi na Bw Felix Koskei. Mwanasheria Mkuu pia huwa kamishna wa tume hiyo inayoajiri majaji, mahakimu na maafisa wengine wa mahakama. Msajili wa Mahakama Anne Amadi ni katibu wa tume hiyo.

Bw Njenga analaumu makamishna aliotaja kwa kuwalinda, kuwatetea na kuwaondolea lawama majaji anaodai wanahusika na tabia isiyofaa. “Wamepuuza, bila kuzingatia Katiba, malalamishi yanayowasilishwa katika JSC,” wakili huyo anasema kuhusu makamishna hao.

Ombi hili linaonekana kama juhudi za serikali za kuingilia uhuru wa mahakama ambayo inadai inatatiza shughuli zake.

Itakumbukwa kuwa Mahakama ya Juu ilipobatilisha ushindi wa Uhuru Kenyatta, Rais aliahidi kuchukulia mahakama hatua akishinda uchaguzi wa marudio na kuwataja majaji kuwa wakora.

JSC ni muhimu katika kuleta mabadiliko katika mahakama kwa sababu inaajiri majaji, kupokea na kushughulikia malalamishi kuhusu maafisa wa mahakama.

Tume hiyo ina nguvu za kutoa mapendekezo kwa Rais kuunda jopo la uchunguzi ikipata kwamba kuna sababu za kumuadhibu jaji.Hata hivyo, kumuondoa Jaji Mkuu kitakuwa kibarua kikuu kwa sababu itabidi sheria ya JSC ibadilishwe au wafutwe kazi.

Mwaka jana, mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu aliwasilisha ombi kwa JSC akitaka Bw Maraga na naibu wake Mwilu waondolewe ofisini.

Kalonzo sasa ni wakili wa Gavana Ngilu

Na CECIL ODONGO

Kwa ufupi:

 • Bw Kalonzo na mawakili wengine walipinga hatua ya NCIC kumsomea gavana huyo wa chama cha NARC madai tofauti
 • Alisema mteja wake anaandamwa na wanasiasa wakuu wanaopinga juhudi zake za kulinda mazingira kaunti ya Kitui
 • Kiongozi huyo alimtaka Bi Ngilu asimame imara kuhusiana na utekelezaji wa marufuku dhidi ya usafirishaji makaa na uzoaji wa mchanga 
 • Gavana wa Kiambu Bw Ferdinard Waititu pia aliingilia suala hilo na kutaka Bi Ngilu akabiliwe kisheria

KINARA wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka Jumatatu alijikumbusha taaluma yake ya uwakili, alipoandamana na gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu katika afisi za Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) akiwa wakili wake mkuu.

Makamu huyo wa rais wa zamani alijitokeza mbele ya tume hiyo inayoongozwa na Bw Francis Ole Kaparo, akiwa wakili mkuu wa Bi Ngilu.

Bi Ngilu alikuwa ameitwa kuhusiana na madai ya kuchochea uchomaji wa lori la kampuni ya usafiri ya Juja Transporters.

Hata hivyo, Bw Kalonzo na mawakili wengine walipinga hatua ya NCIC kumsomea gavana huyo wa chama cha NARC madai tofauti.

Bi Ngilu akiwa ameandamana na kundi la akina mama waliomsifu kwa nyimbo, alijulishwa kuwa alitoa matamshi ya uchochezi.

Mawakili wake walipinga hatua hiyo mpya, na kusema kuwa tume hiyo ilikuwa na njama fiche. Kwa hivyo walimshauri Bi Ngilu kuitikia wala kuzungumza chochote hadi NCIC itoe maagizo mapya.

 

Vita vya kisiasa

Akiwahutubia wanahabari, Bw Kalonzo alisema mteja wake anaandamwa na wanasiasa wakuu wanaopinga juhudi zake za kulinda mazingira kaunti ya Kitui.

“NCIC wametupotezea wakati kwa sababu hata hawajawasilisha madai tuliyoyatarajia. Vita dhidi ya Gavana Ngilu ni vya kisiasa na wanaotaka ukame uwe janga la kitaifa,” akasema Bw Kalonzo.

Japo Bi Ngilu hakuzungumza na wanahabari, Bw Kalonzo alimtaka asimame imara kuhusiana na utekelezaji wa marufuku dhidi ya usafirishaji makaa na uzoaji wa mchanga kwenye kaunti yake.

Mawakili wengine waliofika kumtetea Bi Ngilu ni Bw Martin Oloo, Bw Daniel Maanzo, Davison Makau na Bi Rachel Osendo.

Wabunge wengine wa chama cha Wiper na mwaniaji wa ugavana kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti waliandamana na Gavana Ngilu katika makao makuu ya tume hiyo.

Kiongozi wa chama cha Wiper Bw Kalonzo Musyoka anong’onezeana na Gavana wa Kitui Bi Charity Ngilu katika hafla ya awali. Picha/ Maktaba

Kuchoma lori

Bi Ngilu alikuwa anakabiliwa na madai ya kuchochea kundi la vijana kuchoma lori la mfanyibiashara mmoja kutoka kaunti Kiambu, lililokuwa likisafirisha makaa.

Wiki iliyopita, mwanasiasa huyo ambaye amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali za uwaziri serikalini, alifika katika makao makuu ya idara ya upelekezi wa Jinai (DCI ) na kuandikisha taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Kuchomwa kwa lori hilo kulizua maandamano mjini Limuru, waandamanaji wakimlaumu gavana huyo kwa kuendeleza ukabila.

Gavana wa Kiambu Bw Ferdinard Waititu pia aliingilia suala hilo na kutaka Bi Ngilu akabiliwe kisheria.

Awali, Bw Waititu aliongoza wanasiasa wengine wa eneo la Kati kutaka hatua za haraka zichukuliwe, ili kumdhibiti Bi Ngilu.

 

BI TAIFA FEBRUARI 27, 2018

MAUREEN Wairi, 23, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Uraibu wake ni kutazama filamu, kusafiri na kusoma vitabu. Picha/ Anthony Omuya

Usain Bolt aahidi kufichua klabu ya soka aliyojiunga nayo

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi za dunia za mbio za mita 100 na mita 200, Usain Bolt amesema amepata klabu ya kusakatia soka yake ya malipo.

Mjamaica huyu mwenye umri wa miaka 31 aliyestaafu kutoka riadha mwaka 2017, ametangaza Jumatatu kwamba atafichua klabu hiyo Februari 27, 2018 (saa tano asubuhi saa ya Afrika Mashariki).

Tovuti ya Vanguard nchini Nigeria imemnukuu akisema, “Nimejiunga na klabu moja ya soka. Fahamu jina ya klabu hiyo Jumanne (8am GMT).”

Kwa mujibu wa tovuti hiyo, shabiki huyu sugu wa Manchester United aliratibiwa kufanyiwa majaribio na klabu ya Borussia Dortmund nchini Ujerumani mwezi ujao wa Machi.

Alifanya mazoezi na mabingwa wa zamani wa Afrika, Mamelodi Sundowns, kutoka Afrika Kusini mwezi Januari mwaka 2018.

“Mojawapo ya ndoto yangu kubwa ni kujiunga na Manchester United. Hata hivyo, Dortmund ikiridhika na mimi, nitajiunga nayo na kujitahidi vilivyo mazoezini.

Nimeongea na (kocha wa zamani wa United) Alex Ferguson na kumueleza anahitaji kuishawishi kwa maneno matamu. Aliniambia nikiwa fiti na tayari, atajaribu kadri ya uwezo wake kutimiza ndoto yangu,” amesema.

Nakumatt yamumunywa kama pipi na Nkana ya Zambia

Na GEOFFREY ANENE

NAKUMATT FC imelimwa 4-0 na miamba wa Zambia, Nkana, katika mechi ya kirafiki uwanjani Camp Toyoyo, Nairobi, Jumatatu.

Klabu hii inayoshikilia nafasi ya tisa kwenye Ligi Kuu ya Kenya, ilifungwa mabao mawili katika kila kipindi.

Walter Bwalya aliweka Nkana bao 1-0 juu dakika ya 37 kabla ya mabingwa mara 12 wa Zambia kuenda mapumzikoni 2-0 mbele Idris Mbombo alipoongeza bao la pili dakika ya 42. Jacob Ngulube alimega pasi zilizofungwa na Bwalya na Mbombo.

Festus Mbewe aliimarisha uongozi hadi 3-0 dakika ya 61 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Freddy Tshimenga kabla ya Humphrey Maseneko kufunga ukurasa wa mabao dakika ya 71. Maseneko alimegewa pasi murwa na Tshimenga.

Nkana inajiandaa kumenyana na Chabab Riadhi Belouizdad ya Algeria katika mechi ya raundi ya kwanza ya mashindano ya Afrika ya Confederations Cup ugenini hapo Machi 6.

Ilikaba mabingwa wa Kenya, Gor Mahia, 1-1 katika mechi ya kirafiki uwanjani Camp Toyoyo mnamo Februari 24, 2018.

Katika mchuano huo, Mrwanda Jacques Tuyisenge alifungia Gor dakika ya 20 kabla ya Nkana kusawazisha kupitia Mbewe dakika ya 64.

Nkana imeratibiwa kuondoka Kenya hapo Februari 27 kuelekea jijini Lusaka kabla ya kupaa hadi jijini Algiers nchini Algeria.

Ochieng’ hapitiki katika safu ya ulinzi, Mkenya asifiwa Uswidi

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA David ‘Cheche’ Ochieng’ na Eric Johana Omondi walichezea klabu ya Brommapojkarna na kuisaidia kubwaga Dalkurd 2-0 kwenye mashindano ya Svenska Cupen nchini Uswidi mnamo Februari 25, 2018.

Ochieng’ alicheza dakika zote 90 naye Omondi aliingia kama mchezaji wa akiba mahali pa Marko Nikolic dakika ya 75.

Tovuti ya Brommapojkarna imemsifu Ochieng’. “Pandikizi la mtu Ochieng’ alikuwa hakipitiki katika safu ya ulinzi. Aliwazima wachezaji wa Dalkurd moja baada ya mwingine walipojaribu kumpita wakifanya mashambulizi,” tovuti hiyo imesema.

Wachezaji Marko Nikolic na Martin Rauschenberg walifungia Brommapojkarna mabao ya ushindi dakika za 31 na 51, mtawalia.

Mashabiki 600 walihudhuria mchuano huo katika uwanja wa Grimsta jijini Stockholm. Brommapojkarna, ambayo ilizaba Gefle 2-0 katika raundi ya kwanza, itakutana na miamba Malmo FF katika raundi ijayo mnamo Machi 4, 2018.

Omondi alijiunga na Brommapojkarna kutoka klabu ya Vasalunds IF hapo Januari 1, 2018 kwa kandarasi ya miaka minne.

Naye Ochieng’ alisajiliwa na Brommapojkarna mnamo Januari 12, 2018 kwa kandarasi itakayomweka klabu hiyo hadi Desemba 31, 2020. Alitokea New York Cosmos nchini Marekani alikokuwa amecheza miaka miwili.  Brommapojkarna itashiriki Ligi Kuu mwaka 2018 baada ya kupandishwa daraja. 

Chepkoech awabwaga wapinzani kwenye IAAF World Indoor Tour

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Beatrice Chepkoech alitia kibindoni Sh2, 340,595 katika siku ya mwisho ya Riadha za IAAF World Indoor Tour zilizokamilika mjini Glasgow, Scotland, Februari 25, 2018.

Chepkoech alifahamu vyema kuwa ushindi utamweka juu ya jedwali la mbio za mita 1,500.

Akiwa na ufahamu huo, mkimbiaji huyu, ambaye ni gwiji wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, hakufanya masihara. Alifuata mwekaji kasi unyounyo katika mizunguko ya kwanza kabla ya kumpita na kufungua mwanya mkubwa kati yake na mpinzani wake wa karibu Muethiopia Axumawit Embaye.

Chepkoech alikamilisha mbio wa kwanza kwa dakika 4:02.21 na kujinyakua tuzo ya mshindi ya Sh305, 295 na kuongezwa Sh2, 035,300 kwa kushinda msimu.

Alimaliza msimu mbele ya Muethiopia Genzebe Dibaba (alama 20), Mjerumani Konstanze Klosterhalfen (14), Mmoroko Rababe Arafi (13) na Mkenya Winny Chebet (13).

Mbali na kupata ufanisi huo, Chepkoech pia anamiliki rekodi mpya ya Kenya ya mbio za ukumbini za mita 1,500 ya dakika 4:02.21 baada ya kufuta rekodi ya 4:02:23 aliyoweka mwaka 2017.

Mkenya Justus Soget alijishindia Sh305, 100 kwa kunyakua taji la Glasgow la mbio za mita 3,000 kwa dakika 7:39.09. Soget alimaliza msimu nyuma ya Waethiopia Yomif Kejelcha (alama 22) na Hagos Gebrehiwet (17), Mhispania Adel Mechaal (11) na Mkenya Edward Cheserek (10).

Mjini Glasgow, Soget alifuatwa kwa karibu na Muamerika Paul Chelimo (7:39.10), Kejelcha (7:39.36) na Mkenya Davis Kiplangat (7:40.12).

Wakenya Bethwell Birgen na Vincent Kibet walinyakua nafasi mbili za kwanza katika mbio za mita 1,500 mjini Glasgow kwa dakika 3:37.76 na 3:37.88 naye raia wa Australia, Ryan Gregson akafunga tatu-bora (3:38.00).

Mashindano ya IAAF World Indoor Tour yalianza Februari 3 mjini Karlsruhe mjini Ujerumani na kuzuru miji ya Dusseldorf nchini Ujerumani (Februari 6), Madrid nchini Uhispania (Februari 8), Boston nchini Marekani (Februari 10), Torun nchini Poland (Februari 15) kabla ya kufikia kilele mjini Glasgow (Februari 25).

BI TAIFA FEBRUARI 26, 2018

LISA Kainae, 20, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Anapenda kusakata densi, kutazama filamu na kuogelea. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA FEBRUARI 25, 2018

LISA Cherop, 21, ni mwanamitindo jijini Nairobi. Anaenzi kuogelea, kuendesha baiskeli na kupiga gitaa. Picha/ Anthony Omuya

BI TAIFA FEBRUARI 24, 2018

Linda Jerop, 22, ni mwanamitindo mjini Eldoret. Uraibu wake ni kusafiri, kuimba ma kusikiliza muziki. Picha/ Anthony Omuya

Serikali igharamie safari ya Miguna Miguna kurudi nchini, mahakama yaamuru

Na RICHARD MUNGUTI

Kwa ufupi:

 • Jaji Mwita aikashifu serikali kwa kukandamiza haki za wananchi na za Dkt Miguna kwa madai “usalama wa nchi uko hatarini bila kutoa ushahidi”
 • Agizo la kuharamisha vuguvugu la National Resistant Movement (NRM) pia lilifutwa
 • Miguna naweza kutumia paspoti ya Canada kurudi nchini iwapo idara ya uhamiaji itachelewa kumpa pasi ya KenyaK
 • Kurudi nchini kwa Dkt Miguna kufadhiliwe na serikali iliyomtangaza kwa pupa kuwa mhamiaji haramu 

KATIKA uamuzi wa kihistoria Mahakama kuu Jumatatu iliamuru mwanaharakati Dkt Miguna Miguna arudi nchini akitumia pasi ya kusafiria ya nchi ya Canada.

Jaji Enock Chacha Mwita aliikosoa serikali kwa kukaidi haki za Dkt Miguna ilipomtangaza kuwa “mhamiaji haramu ilhali ni mzaliwa wa Kenya.”

Jaji Mwita aliikashifu serikali kwa kukandamiza haki za wananchi na za Dkt Miguna kwa madai “usalama wa nchi uko hatarini bila kutoa ushahidi.”

Na wakati huo huo, agizo la kuharamisha vuguvugu la National Resistant Movement (NRM) na Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i lilitupiliwa mbali.
Sasa NRM inaweza kuendelea na shughuli zake.

Kabla ya kufurushwa kutoka nchini Dkt Miguna alikuwa “amejitangaza Jenerali wa NRM.”

Jaji wa Mahakama Kuu, Enock Chacha Mwita. Amefutilia mbali kufurushwa kwa Dkt Miguna, ameamuru serikali ifadhili safari yake ya kurudi nchini. Picha/ Maktaba

Arudishwe na serikali

Jaji Mwita aliamuru kurudi nchini kwa Dkt Miguna kufadhiliwe na serikali iliyomtangaza kwa pupa kuwa “mhamiaji haramu ilhali ni mzaliwa wa eneo la Nyando katika Kaunti ya Kisumu na aliwania kiti cha Ugavana Nairobi na kushindwa na Bw Mike Sonko Mbuvi.”

Aidha, alilitaka shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu nchini (KNHRC) lihakikishe Dkt Miguna hasumbuliwi akiwarudi nchini.

Jaji huyo aliharamisha maamuzi yote ya Dkt Matiang’i na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa ya kumtangaza Dkt Miguna kuwa mhamiaji haramu.

Pia alifutilia mbali uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji wa kutotambua cheti cha usafiri cha Dkt Miguna alichopata akiwa nchini Canada.

 

Atumie paspoti ya Canada

“Mlalamishi anaweza kutumia paspoti ya Canada kurudi nchini iwapo idara ya uhamiaji itachelewa kumpa pasi ya Kenya.”

Aliongeza kusema kuwa asasi zote za serikali zinapasa kuimarisha utekelezaji wa Katiba. Kila mmoja nchini Kenya anatakiwa kuhakikisha kwamba Katiba iliyo sheria kuu nchini imefuatwa na haki za wananchi hazikandamizwi.

Mahakama iliwashutumu maafisa wakuu Serikalini waliokiuka Katiba na sheria na kumfurusha Dkt Miguna Miguna kutoka nchini “akisubiriwa mahakamani na Jaji Luka Kimaru.”

Jaji Mwita alisema Dkt Miguna amewasilisha kesi iliyo na mashiko makuu kisheria na kwamba haki zake zilikandamizwa.

“Ushahidi katika kesi unahitaji kutolewa na mlalamishi mwenyewe kisha ahojiwe na wakili wa Serikali Bw Emmanuel Mbittah,” alisema Jaji Mwita.