Mibabe wa siasa wajipanga kisiri kuhusu 2022

Na BENSON MATHEKA

MIKUTANO ya siri kati ya viongozi wakuu wa kisiasa imeshika kasi huku mabadiliko makubwa yakitarajiwa kuhusiana na uchaguzi wa 2022.

Inakisiwa kuwa lengo la mikutano hiyo ni kusuka miungano mipya ya kisiasa, ambayo wadadisi wanasema itaamua mwelekeo wa siasa za Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, jambo ambalo limewatia tumbojoto washirika wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto.

Mkutano wao wa hivi punde umeripotiwa kufanyika mjini Mombasa. Walipotangaza muafaka wao Machi 29, viongozi hao walikiri kwamba walikuwa wakikutana kwa siri hadi walipokubaliana kufanya kazi pamoja.

Baada ya kukutana Mombasa, Rais Kenyatta alikutana na Rais Mstaafu Daniel Moi na mwanawe Seneta Gedion Moi, nyumbani kwa Mzee Moi, Kabarak.

Rais alisema alipitia kumjulia hali Mzee Moi ambaye ni mlezi wake kisiasa, akielekea katika mazishi ya mke wa jirani yake, Luteni Jenerali Jackson Kasaon.

Hata hivyo, kukosekana kwa Naibu wake William Ruto, hasimu wa kisiasa wa familia ya Moi, ambaye pia alihudhuria mazishi hayo, kulizua maswali kuhusu dhamira ya mkutano huo.

Ikizingatiwa kuwa ziara ya Rais huchukua muda na rasilmali kupanga, wadadisi wanasema haukuwa mkutano wa kupitia tu.

Haikuwa mara ya kwanza Rais Kenyatta kutembelea Mzee Moi akiwa na mwanawe Gedion, ambaye ilisemekana alimzuia Bw Ruto kumuona baba yake alipomtembelea mapema mwaka huu.

Juhudi za Bw Ruto kumtembelea Mzee Moi zilijiri siku chache baada ya Bw Odinga kumtembelea rais huyo wa pili wa Kenya akiandamana na Gedion.

Hii ilifuatiwa na mkutano wa Seneta Moi na wafanyabiashara mabwenyenye kutoka ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta ya eneo la Mlima Kenya.

Duru zilisema kuwa mkutano huo ulilenga kupanga mikakati ya kumjenga Gideon kabla ya 2022 ili aweze kutekeleza wajibu mkubwa.

Wafanyabiashara hao wana ushawishi mkubwa wa kisiasa eneo hilo na Kenya kwa jumla na wadadisi wanasema mkutano wao na Seneta Moi hauwezi kupuuzwa.

Baada ya mkutano huo, mbunge wa Tiaty, William Kamket alinukuliwa akisema kuwa marafiki wote wa Moi ambao wanajali nchi hii wanakutana kote nchini.

Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat naye alinukuliwa akisema kuwa watu wengi wako tayari kushirikiana na cha Kanu. “Watu wengi wako tayari kuungana nasi kwenye safari hii na tunakutana nao kubadilishana maoni, Tegea tu na hivi karibuni utaona mabadiliko makubwa,” alisema Bw salat.

Kwa upande wake, Bw Odinga amekuwa akikutana na vinara wenzake wawili katika NASA, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi kwenye juhudi za kufufua muungano huo.

Tayari, Bw Musyoka, ambaye pia amekutana na Seneta Moi ameongoza chama chake kutangaza kitaunga mkono serikali ya Rais Kenyatta.

Duru zingine zinaeleza kuwa Bw Musyoka, Bw Mudavadi na kinara mwenzao katika NASA Moses Wetangula nao wamekuwa wakikutana bila Raila kupanga mikakati yao ya kisiasa.

Naye Bw Mudavadi na Bw Wetangula wamekuwa wakikutana kuandaa mikakati ya kuunganisha vyao vya ANC na Ford Kenya.

Japo Bw Ruto amekuwa akiendeleza siasa zake za 2022 chini kwa chini, wadadisi wanasema amekuwa akipanga mikakati yake kwa kutuma wandani wake wa kisiasa kukutana na wanasiasa maarufu kote nchini kwa sababu hataki kuonekana kuhujumu serikali ya Jubilee kwa wakati huu.

Baadhi ya wanasiasa tayari wametangaza kuwa watamuunga mkono kwenye uchaguzi wa 2022.

Warembo wa Uganda wapiga magoti kumshukuru hakimu baada ya kuachiliwa

Na RICHARD MUNGUTI

WASICHANA 20 raia wa Uganda Jumatano waliizuzua mahakama ya Milimani, Nairobi kwa kupinga magoti na kumshukuru hakimu mkuu Bw Francis Andayi kwa kuwaachilia huru wakitumia lugha ya Kiganda. “Weballessebo, asante mkubwa,” walisema.

“Bila shaka hawa hawezi kuwa Wakenya. Wasichana wetu hapa nchini hawawezi kufanya haya,” akasema Bw Andayi na kusababisha waliokuwa mahakamani kucheka.

Wasichana hao wote walipiga magoti na kuinamisha vichwa vyao na kuinua mikono wakisema wakitoa shukrani kwa mahakama waliposikia wako huru.

Akiwaachilia wasichana hao Bw Andayi alisema  “kwa moyo wa ushirikiano wa mataifa ya Afrika Mashariki ninawaachilia na kuwapeana kwa ubalozi wa Uganda nchini warudishwe kwao.”

Ubalozi wa Uganda ulimwandikia hakimu ukimsihi awaachilie ndipo uchunguzi ufanywe kubaini mshukiwa aliyekuwa anataka kuwalangua wasichana hao kuwauza nchini Oman kama wajakazi.

Bw Andayi alisema kuwa wasichana hao walikutwa wameghushi visa ya Kenya katika pasipoti zao.

Wasichana hao walibanduliwa kwenye ndege waliyokuwa wameabiri ya shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) iliyokuwa inaenda nchini Oman.

Wakili wao David Ayuo alisema wasichana hao walikuwa wanalanguliwa na kundi la majangili wanaodai watawatafutia kazi mataifa ya ng’ambo.

“Naomba hii mahakama iwahurumie wasichana hawa wenye umri mdogo kati ya miaka 16-22 waliodanganywa kuna kazi inayowasubiri ng’ambo,” alisema Bw Ayuo.

Alisema walisukumwa na umaskini kutoka nyumbani kwao lakini wakaishia mikononi mwa mikora.

Kesi ya Mutua kuamuliwa Agosti 6

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Juu itasikiza Agosti 6 kesi iliyowasilishwa na Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua anayepinga uamuzi wa kumtimua mamlakani.

Mahakama ya rufaa ilifutilia mbali ushindi wa Dkt Mutua na kuamuru uchaguzi mdogo ufanywe katika kaunti ya Machakos.

Majaji hao walisema Dkt Mutua hakuchaguliwa kwa njia halali na kuharamisha ushindi wake.

Punde tu baada ya uchaguzi wake kubatilishwa  Gavana Mutua aliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Juu .

Jaji Mkuu David Maraga , naibu wake Philomena Mwilu na majaji wengine watasikiza rufaa hiyo.

Ikiwa wataunga mkono uamuzi wa mahakama ya rufaa basi Dkt Mutua atakuwa Gavana wa kwanza kupoteza kiti cha ugavana baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Afueni kwa mabinti 22 wa UG walionaswa Kenya wakisafiri Dubai

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA imefuta mashtaka dhidi ya wasichana 22 raia wa Uganda waliotiwa nguvuni Kenya wakiwa na paspoti feki za usafiri.

Washtakiwa hao walikuwa wanajaribu kusafiri hadi Dubai kutafuta ajira walipotiwa nguvuni na maafisa wa idara ya uhamiaji.

Kiongozi wa mashtaka kutoka idara hiyo Bw Mutelo alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi  Bw Francis Andayi kuwa pasipoti za washtakiwa zilikuwa na Visa zilizoghushiwa.

“Mbona mmetengeneza cheti kimoja cha mashtaka,” Bw Andayi alimwuliza Bw Mutelo na kuongeza , “ Ushahidi uko wapi utakaoniwezesha kuwapata washtakiwa na hatia.”

Mahakama ilikataa mashtaka yaliyotayarishwa na maafisa hao na kuamuru washtakiwa warudishwe rumande na kuagiza kila mmoja ashtakiwe peke yake.

DPP aitisha faili ya askari jela aliyemuua mwanachuo

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameitisha faili ya Askari jela anayeshtakiwa kwa kumgonga dafrau na kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa Jumapili iliyopita akiwa mlevi.

Na wakati huo huo Mahakama ya kuamua kesi za trafik ilifutilia mbali kibali cha kumtia nguvuni Konstebo Dismas Gitenge Motongwa alipochelewa  kufika kortini.

“Naomba hii mahakama isimlaumu mshtakiwa. Nilikuwa naye tukitafuta faili ya hii kesi jina lake alipoitwa lakini hakuonekana. Mnilaumu mimi mwenyewe,” wakili Danstan Omari alimweleza  hakimu mwandamizi Bi Electa Riany.

Bw Omari aliomba korti ifutulie mbali kibali cha kumtia nguvuni mshtakiwa kwa kufika kortini akiwa amechelewa.

“ Naomba korti pia imrudishie dhamana ya mshtakiwa iliyokuwa imefutiliwa mbali na mshtakiwa kuagizwa azuliwe gerezani,” Bw Omari alimsihi hakimu.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi la kufutiliwa mbali kwa kibali cha kumtia nguvunu mshtakiwa.

“Sipingi mshtakiwa akirudishiwa dhamana na pia kibali cha kumtia nguvuni kikiondolewa,” Bi Riany alifafahamishwa.

Akitoa uamuzi Bi Riany alimrudishia mshtakiwa dhamana na kumuonya vikali dhidi ya kuchelewa kufika kortini.

Mahakama iliamuru faili ya Konstebo Motongwa ipelekwe moja kwa hadi kwa DPP aisome kisha atoe ushauri.

Bi Riany alikubalia ombi la kiongozi wa mashtaka la kuahirisha kesi dhidi ya Konstebo Motongwa hadi Agosti 2 kuwezesha DPP  kusoma faili ya kesi hiyo kisha atoe ushauri jinsi kesi itakavyoendeshwa.

Mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuendesha gari akiwa mlevi, kuendesha gari bila makini na kusababisha kifo cha  Mourine Wambui Gachagua mwenye umri wa miaka 22 na kutosimama baada ya kusababisha ajali hiyo.

Mshtakiwa alikiri shtaka la kutosimama mnamo Julai 15aliposababisha  ajali kisha akatozwa faini ya Sh10,000.

Konsteno Motongwa alikuwa anaendesha garu muundo wa Volkswagen nambari ya usajili  KCN 285B mnamo Julai 15 ajali hiyo ilipotokea.

Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa nane unusu karibu na duka la Nexgen Mall.

Mshtakiwa alikuwa anaelekea jijini Nairobi.

Pia anadaiwa alikuwa amekunywa pombe akapitisha kiwango  kinachokubalika dereva kuendesha gari.

Kesi dhidi ya mshtakiwa huyo itatajwa tena Agosti 2 ndipo DPP atoe mwelekeo.

Kesi dhidi ya waziri wa kaunti aliyeaga yatupwa

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji amefutilia mbali kesi dhidi ya mmoja wa mawaziri wa Serikali ya kaunti ya Busia aliyeaga Bw Timon Otieno.

Otieno alishtakiwa pamoja na Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong na mawaziri wengine watatu wa kaunti hiyo. Kesi dhidi ya Otieno iliondolewa n

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) Douglas Ogoti alifahamishwa Otieno aliaga Juni 17 2018.

“Nathibitisha kuwa Timon Otieno aliaga mnamo Juni 17, 2017 . Natamatisha kesi dhidi yake,” Kiongozi wa Mashtaka Alexander Muteti alimweleza hakimu , huku akimkabidhi nakala ya cheti cha kifo cha mshtakiwa.

Bw Muteti aliwasilisha cheti kipya cha mashtaka dhidi ya Mabw Ojaamong , Bw Lenard Wanda Obimbira, Allan Ekweny Omacha na Bw Bernard Krade Yaite.

Washukiwa wengine ambao hawakufika kortini Bw Samuel Ombui, Bi Edna Adhiambo Odoyo, Renish Achieng ,Sebastian Hallensleben na Madam R Enterprises Limited watatiwa nguvuni.

Washukiwa hao hawakufika kortini na Bw Muteti aliomba watiwe nguvuni.

Na wakati huo huo mahakama ilitenga Septemba 11 siku ya kuanza kusikizwa kwa kesi dhidi ya Bw Ojaamong na wenzake watatu.

Upande wa mashtaka ulisema utachukua masaa 24 kuwasilisha ushahidi dhidi ya washtakiwa.

Bw Ogoti aliamuru upande wa mashtaka uwakabidhi washtakiwa nakala zote za ushahidi.

Pia aliamuru mawakili wanaotaka kujiondoa katika kesi hiyo wafanye hivyo mapema badala ya kung’atuka kwenye kesi siku ya kusikizwa kwa kesi na kuvurunga utaratibu.

Bw Ojaamong yuko nje kwa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu.

Mahakama ilikubalia ombi la wakili Danstan Omari anayemwakilisha Ojaamong kwamba gavana huyo asiwe anaenda kupiga ripoti katika afisi za tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC eneo la Busia kwa wafuasi wengi wa kiongozi huyo wataandamana naye.

Bw Ojaamong alikanusha shtaka la kufanya njama za kuilaghai Serikali ya kaunti ya Busia Sh8milioni kwa kuruhusu utafiti ufanywe kuhusu takataka na kampuni ya Ujeruman bila mpango.

Alikana alifanya mashauri kuhusu utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Ujerumani bila ya kuwashirikisha maafisa wakuu wa kaunti hiyo.

Akiwa mjini Berlin, Ujerumani Gavana Ojaamong aliruhusu malipo ya Sh8milioni kinyume cha sheria.

Kesi itatajwa Septemba 4 upande wa mashtaka kueleza ikiwa umewakabidhi washtakiwa nakala za ushahidi zote.

Bidhaa ghushi za Sh7.5 bilioni zimenaswa, walaghai 75 wamezimwa – Ripoti

NA CECIL ODONGO

MISAKO ambayo imekuwa ikiendeshwa na serikali dhidi ya bidhaa ghushi nchini tangu Juni 2018 imenasa bidhaa zenye thamani ya Sh7.5 bilioni, serikali ilisema Jumanne.

Operesheni hiyo pia imewanasa walaghai 75 miongoni mwao maafisa 10 wa serikali ambao tayari wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Naibu Mkuu wa utumishi wa umma Wanyama Musiambo alisema kwamba thamani ya sukari ghushi ndiyo  ilikuwa  juu zaidi  kushinda bidhaa nyingine zilizonaswa.

“Kati ya Sh 7.5 bilioni, thamani ya sukari ghushi ilikuwa  Sh5.3 bilioni. Bidhaa za sigara (Sh828milioni), kilimo(Sh341milioni), vifaa vya stima(Sh300milioni), na pombe(Sh241milioni) pia zilichangia thamani hiyo,” ikasema taarifa ya Bw Musiambo.

Serikali pia imezamia mbinu kabambe ya kuhakikisha bidhaa ghushi haziingizwi nchini kwa kuimarisha ukaguzi na usalama kwenye miji ya mipaka. Mipaka iliyotajwa ni Busia, Malaba, Isbania, Shimoni, Moyale, Lunga Lunga na bandari ya Mombasa.

Hata hivyo maafisa waliojukumiwa kuhakikisha bidhaa haziingizwi nchini kiharamu watakuwa na beji maalum kama kitambulisho chao kitakachowatofautisha na wakora wanaojifanya maafisa halali kwa lengo la kuwapunja wafanyabiashara wanaotumia njia za kisheria kuingiza bidhaa nchini.

“Maafisa wanaoendesha misako hii wanatoa onyo kwa umma kujihadhari na wahalifu wanaojifanya kuwa maafisa halali ingawa lengo lao ni kulaghai wafanyabiashara. Maafisa wetu wana beji maalum na hufuata sheria bila kuwahangaisha wafanyabiashara, kuvunja maduka yao au kufunga biashara halali,” ikasisitiza taarifa hiyo.

Afisa huyo wa serikali alifichua kwamba bidhaa zote ghushi zilizonaswa zitaharabiwa huku juhudi zote zikifanywa kuhakikisha mtandao wa kuagiza na kusambaza bidhaa ghushi unaomilikiwa na wafanyabiashara wakora unaangamizwa.

Aidha aliwataka wananchi kuungana na serikali kufaulisha vita dhidi ya bidhaa ghushi kwa kuwa ni moja ya changamoto zinazotatiza kutimizwa kwa nguzo nne za utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ikiwemo nguzo muhimu ya uundaji bidhaa.

Kerr mwingi wa shukrani kwa kikosi baada ya kuibuka kocha bora Julai

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa Mabingwa mara 16 wa  KPL Gor Mahia Dylan Kerr amewashukuru wachezaji wake na benchi ya kiufundi kwa kuchangia ushindi wake wa kocha bora, mwezi Julai.

Kwenye sherehe fupi iliyoandaliwa Jumanne katika uwanja wao wa mazoezi wa Camp Toyoyo jijini Nairobi, mkufunzi huyo ambaye hakutarajia kutuzwa wakati huo aliwamiminia sifa kedekede wanadimba wake kwa kushinda mechi zote tano za mwezi huo.

Mkufunzi huyo alipigiwa kura zilizompa ushindi huo na muungano wa wanahabari wa michezo baada ya timu yake kutopoteza mechi yoyote mwezi Juni na kushinda baadhi ya mechi hizo  kwa idadi kubwa ya magoli.

Wakati wa sherehe hiyo, Kerr alituzwa kombe pamoja na hundi ya Sh75,000.

“ Lazima nishukuru benchi yangu ya kiufundi kwa usaidizi mkubwa wanaonipa. Wachezaji wangu pia wametia juhudi kubwa tena  wa kupigiwa mfano kufanikisha ushindi wa tuzo hii,” akasema Kerr.

Mwezi Juni, K’ogalo waliwaonyesha wapinzani wao kivumbi. Waliwapa Wazito FC kichapo kizito cha 4-0, wakaifunga Nzoia FC 3-1, wakaikalifisha Ulinzi Stars 2-0, wakainyeshea mvua ya magoli Posta Rangers FC 5-0 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya SoNy Sugar FC kwa ushindi wa 1-0.

“Tuliheshimu kila mpinzani tuliyekutana naye mwezi Juni lakini udhabiti na umoja wetu ulitusaidia pakubwa ikizingatiwa kwamba msongamano wa mechi za kuwajibikia katika ratiba ulitulazimu kusakata mechi kila baada ya siku tatu,” akahitimisha Kerr.

Gor Mahia Julai 22 waliendeleza rekodi yao ushindi kwa kuwaangusha watani wao wa jadi AFC Leopards kwa mabao 2-1 kwenye debi ya ‘Mashemeji’ na kufungua mwanya wa alama 12 uongozini mwa KPL (alama 52).

Mpinzani wake aliyeibuka wa pili  katika tuzo hiyo alikuwa kocha wa Sofapaka John Baraza.

Wakurugenzi 10 kortini kwa kufyonza mamilioni ya KPC

Na RICHARD MUNGUTI

WAKURUGENZI  kumi  kutoka kampuni mbalimbali walishtakiwa Jumatatu kwa kupokea kwa njia za ufisadi Sh15milioni kutoka kwa  kampuni ya usambazaji nguvu za umeme nchini (KPLC).

Mashtaka dhidi yao yalisema kuwa makampuni yao yalikuwa yameorodheshwa kinyume cha sheria kuhusika na usafirishaji bidhaa na utoaji wa huduma kwa KPLC.

Baadhi ya wakurugenzi hawakufika kortini kama na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) iliomba mahakama itoe kibali cha kuwatia nguvuni.

Kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi wa mahakama ya Milimani Nairobi kuwa washukiwa hao wamezima simu na imekuwa vigumu Polisi kuwafikia.

Bw Mugambi aliombwa atoe kibali cha kuwatia nguvuni.

Mawakili waliofika kortini kuwatetea washtakiwa walipinga ombi hilo la DPP wakisema wakurugenzi ambao hawakufika kortini walihojiwa na mkurugenzi wa idara ya jinai (DCI).

“Wakurugenzi 12 ambao hawakufika kortini walishirikiana na maafisa wa uchunguzi wa jinai waliowahoji. Hakuna haja ya kutoa kibali cha kuwatia nguvuni bila ushahidi walikataa kufika kortini,”  Bw  Mugambi alifahamishwa.

Hakimu alitupilia mbali ombi la DPP akisema “ hakuna ushahidi walikuwa wamepewa samanzi wafike kortini kujibu mashtaka na wakakataa.”

Baadhi ya wakurugenzi waliofika kortini ni pamoja na Bw Hillary Njaramba ambaye kampuni yake ya Touchline Electrical Limited ilishtakiwa kupokea Sh8,333,933 kutoka kwa KPLC.

Kampuini hiyo ilikuwa imeorodheshwa kwa njia isiyo halali kuwa itakuwa inatoa huduma za uchukuzi na huduma nyinginezo kupitia zabuni nambari KP1/9AA-02/OT/58/PJT/16-17.

Kampuni hiyo ilidai ilitoa huduma hizo kwa KPLC kati ta Aprili 12 2017 na Juni 12 2018.

Bw Njaramba ameshtakiwa pamoja na Mkurugenzi mwingine wa kampuni hiyo Bi Esther Nyambura.

Wengine walioshtakiwa ni wakurugenzi wa kampuni ya Millous Enterprises Co.Ltd Bi Catherine Wamarwa Mwangi, Catherine Wanjiku Njuguna , Christine Nyawara na Edwin Macharia Ngamini. Walikana walipokea kinyume cha sheria Sh1,413,492 kutoka kwa KPLC ilhali kampuni yao ilikuwa imeorodheshwa kwa njia isiyo halali kutoa huduma za uchukuzi na nyinginezo.

Kampuni hiyo ilipokea pesa hizo kayi ya Aprili 12 2017 na Juni 12 2018.

Washtakiwa wengine Bi Susan Wanjiru Kamau kupitia kwa kampuni yake Pestus Investments Liimited alikana alipokea Sh112,483 kutoka kwa KPLC kwa njia ya ulaghai.

Wengine waliofikishwa kizimbani Bi Catherine Wambui Mwangi, Jacquilline Wanjiru Mbaria kupitia kwa kampuni yao Kazimix Enterprises Limited wakidaiwa kupokwa Sh1,413, 492.

Kampuni ya Jake Building & Construction Limited ilishtakiwa pamoja na wakurugenzi wake Jason Morara Kerei , Jeremiah Onduko Otero, Jane Wanjiku King’ori na James Ogechi kwa kupokea Sh623,060.

Kampuni ya Gachema na wakurugennzi wake  ilishtakiwa kupkea Sh623,060. Wakurugenzi hao ni Bw Stephen Njoroge Maina, Alice Wanjiku Chege na Raphael Matheri Wanjiku.

Kampuni ya Mint Ventures Limited ilidaiwa ilipokea Sh1,702,208 .Wakurugenzi wake Petty Wanjiku Kigwe na Francis Thuku Chege walifikishwa kortini.

Kampuni nyingine ni Appenco Holdings Limited ambayo ilishtakiwa pamoja na wakurugenzi wake Mabw Samuel Gichini Njogu na Chatles Muthui Mathenge kuppkea Sh231,107.

Washtakiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh400,000 pesa tasilimu.

Washukiwa 12 ambao hawakufika kortini waliagizwa wafike kortini Julai 26.

Awali hakimu alikuwa amekataa kuendelea na kesi ikiwa washtakiwa watakuwa wamejifunika nyuso kwa leso.

Mzee aliyehonga jaji azirai ghafla mahakamani

Na RICHARD MUNGUTI

MAMBO yalimwendea mrama MZEE mwenye umri wa miaka 67  anayeshtakiwa kujaribu kumhonga Jaji Roselyn Aburilili  wa Mahakama kuu Milimani Nairobi.

Kwa ghafla Mzee Joseph Wainaina alianza kutokwa na jasho na kuishiwa na nguvu.

Alijaribu kusimama lakini akashindwa hata ikabidi hakimu mwandamizi Lawrence Mugambi kumtaka mshtakiwa akae kwanza apate afueni.

Dau la Mzee Wainaina lilipigwa na mawimbi ya hofu na woga aliposikia jina lake limetajwa karani wa Jaji Aburili , Bi Adeline Shitawa Murunga aliposomewa mashtaka.

Mzee huyo alikabiliwa na shtaka la kumpa mlungula Bi Murunga ndipo amshawishi Jaji Aburili ampendelee akitoa uamuzi katika kesi aliyokuwa ameshtaki.

Mzee  Wainaina kutoka kaunti ya Murang’a alishtakiwa kwa kumpa Bi Murunga, aliyekuwa karani wa Jaji Aburili Sh50,000 ndipo atweze haki katika kesi aliyokuwa anasikiza jaji huyo.

Shtaka lilisema alitoa hongo hiyo mnamo Januari 6, 2017 katika mahakama ya Milimani.

Mzee Joseph Wainaina akiwa mahakamani Julai 20, 2018. Picha/ Richard Munguti

Kabla ya jina lake kuitwa asimame kizimbani , Mzee Wainaina aliinama na kumwita wakili wake Bw Mbiyu Kama huku amejishika kichwa akisaga meno.

Mshtakiwa alimnong’onezea Bw Kamau jambo masikioni ndipo wakili huyo akaomba mahakama isimsomee mshtakiwa shtaka kwa vile anaugua.

“Naomba kesi dhidi ya Mzee Joseph Ngigi Wainaina ihairishwe kwa muda wa dakika kumi apate nafuu. Amenieleza hajisikii vizuri. Hata unaona anatokwa na jasho na anatetemeka,” wakili Mbiyu Kamau alimsihi hakimu mwanadamizi Bw Lawrence Mugambi.

Bw Mugambi aliahirishwa kesi hiyo na kuamuru mshtakiwa atolewe kizimbani apelekwe kwenye veranda akapate hewa safi.

Mzee Wainaina alitolewa nje na afisa wa pol;isi huku akitembea mwendo wa kinyonga.

Nje kwenye kiti kinachokaliwa na mashahidi wakisubiri kuingia mahakamani, Mzee Wainain alilia huku amejishika kichwa.

Alitoa pakiti ya tembe kwenye mfuko wa korti na kumeza huku akitokwa na jasho.

Alikaa kwa muda wa dakuika ishirini kisha akarudi ndani ya korti na kusomewa mashtaka mawili dhidi.

Shida ya kuugua kwa ghafla kwa , Mzee Wainaina ilianza aliposikia karani wa Jaji Aburili , Bi Adeline Shitawa Murunga akisomewa kuwa alipokea Sh50,000 kutoka kwake (mzee wainaina) amshawishi jaji atoe uuamuzi unaompendelea katika kesi nambari JR451/408/2016.

Mzee Wainaina na Bi Murunga walishtakiwa kila mmoja peke yake.

Karani huyo alishtakiwa kuwa mnamo Januari 6, 2017 katika mahakama kuu ya Milimani alipokea hongo ya Sh50,000 kutoka kwa Mzee Wainaina akidai atamshawishi Jaji Aburili atoa uamuzi unaompendeleza Mzee huyo.

Kila mmoja alikanusha mashtaka mawili na kuomba waachiliwe kwa dhamana.

“Mzee Maina amekuwa akifika katika afisi  za tume ya kupambana na ufisadi nchini, Hata leo (jana) alijisalamisha kwa mahakama. Alikuwa nje kwa dhamana ya Polisi ya Sh20,000,” alisema Bw Kamau.

Bw Mugambi aliamuru kila mmoja alipe dhamana ya Sh80,000 pesa tasilimu ama dhamana ya Sh200,000.

Kesi itatajwa tena Agosti 2, 2018 korti ielezwe ikiwa washtakiwa walipewa nakala za mashahidi.

Akiri alipokea mamilioni kununulia wanakijiji shamba

Na RICHARD MUNGUTI

KINARA wa shirika la kuboresha makao ya wakazi wa vijijini Bi Jane Weru Jumatatu alikiri kuwa alipokea pesa kutoka kwa wakazi 2,200 wa kitongoji cha Mukuru eneo la Embakasi kaunti ya Nairobi kuwanunulia shamba la ekari 23 kwa bei ya Sh81 milioni.

Bi Weru aliyekuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo ameshtakiwa na wakazi hao wa mtaa wa mabanda wa Mukuru alimweleza Jaji Elijah Ombaga.

Mkurugenzi huyo mkuu wa Muungano wa Wanavijiji Akiba Mashinani Trust alimweleza Jaji Ombaga kuwa wakazi hao walimwendea na kumsihi awasaidie kununua shamba hilo la ekari 23 lillokuwa linamilikiwa na kampuni ya Whitemills.

Kinara huyo alisema kuwa kampuni hiyo ilikubali kuuzia wanakijiji hawa shamba hilo kwa bei ya Sh104milioni lakini tukasikizana ipunguze kwa vile hati ya umiliki ilikuwa na kampuni nyingine kwa jina Dhrupa.

Kampuni hii ya Dhrupa ilikuwa imepewa mkopo kununua shamba hilo na benki hiyo ya EcoBank na ikashindwa kuulipa.

“Tulikubaliana na Dhrupa kwamba tutailipia mkopo ndipo hati miliki ya shamba hili liandikishwe kwa jina la Mukuru Makao Bora. Nilikubaliana na Benki hiyo ipatie wanakijiji hao mkopo wa Sh50 milioni ambapo Sh26 milioni italipia mkopo na Sh24 milioni zitawekwa kwa akaunti ya wanakijiji hawa,” alisema Bi Weru.

Alisema wanakijiji walikusanya pesa zikatosha kununua pesa hizo.

“Walalamishi walikusanya pesa na kunipa nikaweka katika akaunti kisha nikalipa mwenye shamba,” alisema Bi Weru.

Wakanakijji hawa waliofika kortini kusikiza kesi dhidi ya Bi Weru wanaomba mahakama kuu imshurutishe Bi Weru awape hatimiliki ya shamba hilo ndipo walistawishe na kujijenga nyumba zao.

Pia wanaomba mahakama kuu imshurutishe Bi Weru awape hesabu ya pesa zilizokatika akaunti yao.

Wanakijiji hawa wanaserma Bi Weru amekawia sana kuwapa hati miliki ya shamba la ilhali walikamilisha kuilipia kitambo zaidi ya miaka 10 iliyoputa.

Akitoa ushahidi  Bi Weru alisema wakati wanakijiji hao walimwuliza awasaidie hawakuwa na pesa za kutosha na walikopeshwa pesa na mashirika mengine ndipo walipe pesa kwa wizara ya ardhi ndipo hatimiliki hiyo ilipiwe pesa za stempu.

Mahakama ilijulishwa pia mkopo huo ulikuwa unapata riba. “Ilibidi niombe benki ya EcoBank iwakopeshe wanakijiji Sh3.5 milioni za kulipa Wizara ya Ardhi.”

Aliongeza kusema kuwa mikopo hiyo ya benki ilikuwa inapata riba.

Mshtakiwa huyo (Weru) aliomba mahakama akubaliwe kuwasilisha ripoti ya mkaguzi wa hesabu kuhusu mkopo huo na wapesa zile alizopokea kutoka kwa wanakijiji hao.

“Naomba mahakama iahirishe kesi ninywe maji. Nahisi kiu. Nimesimama kwa muda mrefu,” Bi Weru alirai.

Jaji Ombaga aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 7 2019 akisema , “Daftari ya kuorodhesha za kusikizwa mwaka huu haina nafasi.”

Wakili kizimbani kwa kuvunja vikombe na sufuria

Wakili Mohammed Salaani (kulia) akiwa kizimbani pamoja na Bw Osman Godana Jillo na Abdulaziz Hassan Abdullahi waliposhtakiwa kwa kuharibu vyombo. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI alishtakiwa kuvunja vikombe na kuharibu sufuria na chakula na kusababishia mkahawa ulioko katika jengo la Jamia, Nairobi hasara ya Sh400,000.

Wakili Mohammed Salaani alishtakiwa pamoja na Bw Osman Godana Jillo na Abdulaziz Hassan Abdullahi mbele ya hakimu  mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

Walikanusha shtaka dhidi yao baada Bw Andayi kukataa ombi la wakili Salaani la kusitisha akisomea shtaka. Bw Salaani aliwakilishwa na Bw Muendo Uvyu.

Bw Uvyu alimsihi hakimu asitishe kesi dhidi ya Bw Salaani asuluhishe mambo kadhaa na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DDP).

“Naomba kesi dhidi ya Bw Salaani iahirishwe kwa muda wa wiki moja asuluhishe mambo kadha na afisi ya DPP,” Bw Uvyu aliomba.

Aliendelea kusema , “ Mshtakiwa huyu ni wakili na hakuhusika na kisa hiki. Naomba kesi dhidi yake iahirishwe hadi asuluhishe mambo kadha na afsi ya DPP.”

Hakimu alimwuliza Bw Uvyu , “Je, si ni afisi ya DPP iliyoidhinisha kesi dhidi ya washtakiwa hawa watatu iwasilishwe kortini?”

“Ndio,” akajibu Bw Uvyu.

“Na je, ni suluhu gani nyingine mshtakiwa anatafuta kama afisi ya DPP ndiyo iliamuru ashikwe na kufunguliwa mashtaka,” Bw Andayi alimhoji wakili.

Hakimu alikataa ombi la mshtakiwa huyo na kuamuru kesi iendelee na kuamuru wasome shtaka dhidi yao.

Walikabiliwa na shtaka la kuharibu mali katika Mkahawa ulioko kwenye Jamia Shopping Mall unaomilikiwa na Bi Aisha Wacuka Wahome mnamo Julai 13 2018.

Shtaka lilisema kuwa watatu hao walivunja , masahani , vikombe, bilauri, masufuria na chakula. Thamani ya mali iliyoahiribiwa ni Sh400,000.

Washtakiwa waliachiliwa kwa dhamana kesi dhidi yao kuorodheshwa kusikizwa Agosti 21, 2018.

“Hata wakishtakiwa bado tutawasilisha mamalamish yetu kwa DPP Bw Noordin Haji,” alisema Bw Uvyu.

Polo ajuta kutomasa mama pima kazini

NA TOBBIE WEKESA

Mukuru, Nairobi

Kizaazaa kilizuka eneo hili baada ya makalameni kumkabili polo walipomkuta akitaka kumbusu mama pima.

Inasemekana makalameni hao walikasirika sana walipogundua kwamba jamaa ndiye aliyefanya wasihudumiwe upesi kwa kumpapasa mama pima.

Kulingana na mdokezi, makalameni hao walifika kwa mama pima asubuhi na mapema ili kupata dozi. Kilichowashangaza ni jinsi mama pima alivyojikokota kuwahudumia. “Kwani leo huyu mama hataki hela zetu?” kalameni mmoja alisikika akisema.

Makalameni waliamua kumpa mama pima muda kidogo. “Ama ameshakuwa tajiri? Acha tumpe muda pengine anajitayarisha kuamka,” makalameni walisema.

Duru zinasema baada ya kungoja kwa muda mrefu, makalameni waliamua kuchungulia ndani ya nyumba ya mama huyo ili kubaini kilichokuwa kikiendelea.

Penyenye zinasema walimuona polo kwenye kochi bila wasiwasi wowote. Kando yake mama pima alikuwa ameinamisha kichwa chake kwenye bega la jamaa.

“Angalia huyu jamaa. Tunaendelea kupigwa na baridi tukingoja pombe kumbe yuko hapa kumzubaisha mama yetu,” kalameni mmoja alisikika akisema.

Makalameni walianza kumfokea jamaa. “Bosi, hatuwezi kuumia kwa sababu yako. Toka hapa haraka,” makalameni walichemka.

Kutokana na aibu, mama pima aliwahimiza makalameni watulie ili awape kinywaji. “Kazi yake tunaijua. Yeye na wanawake hawaachani. Atoke haraka ama tumpe adabu,” mapolo walifoka.

Habari zilizotufikia zinasema makalameni walianza kutafuta viboko tayari kumuadhibu jamaa. “Kama anataka mtu wa kupapasa aje jioni. Hawezi kutupotezea wakati hapa. Hata sisi tuna shughuli nyingine za kufanya,” makalameni waliteta.

Inadaiwa jamaa alipoona mapolo wakiingia kila mmoja akiwa na kiboko, aliamua kuchana mbuga kuhepa aibu.

Ashtakiwa kulangua wasichana wa kigeni

Na Richard Munguti

MMILIKI wa kilabu kimoja maarufu jijini Nairobi alishtakiwa Jumatatu kwa ulanguzi wa wasichana tisa kutoka nchi za Nepal na Pakistan kufanya kazi za kuwafurahisha wateja wake kinyume cha sheria.

Mabw Shaikh Furoan Hussain na Abdul Waheed Khan walikanusha mashtaka manne dhidi yao ya ulanguzi wa binadamu na kukandamiza haki za wasichana hao kwa kuchukua pasipoti zao na kuzificha kinyume cha sheria.

Mabw Hussain , mwenye kilabu cha Balle Balle kilichoko mtaani Parklands walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi.

Walikanusha mashtaka ya ulanguzi wa bindadamu kisha wakili Cliff Ombeta akaomba waachiliwe kwa dhamana.

Wawili hao walishtakiwa kuwa kati ya Feburuari 19 na Julai 9 mwaka huu wakishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani waliwaingiza raia mmoja wa Pakistan na raia wanane wa Nepal humu nchini kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka lilisema kuwa wasichana hao waliokamatwa wakicheza densi katika kilabu hicho kujipatia riziki.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kuwa wawili hao walitwaa pasipoti za wasichana hao tisa kwa lengo la kuficha idara ya uhamiaji uraia wa wasichana hao.

Washtakiwa hao walikabiliwa na shtaka jingine la kuwasaidia wasichana hao kuingia humu nchini kinyume cha sheria za idara ya uhamiaji.

Shtaka lingine la kuwaficha wasichana hao kinyume cha sheria katika mtaa wa Parklands Nairobi.

“Upande wa mashtaka unapinga washtakiwa hawa wakiachiliwa kwa dhamana ndipo kiini chao kuwaingiza wasichana hawa hapa nchini kijulikane,” akasema Bw Naulikha.

Alisema adhabu ya makossa waliyofanya washtakiwa ni kali na wakiachiliwa kwa dhamana washtakiwa watatoroka.

Aliomba mahakama iwazuilie washtakiwa gerezani hadi kesi inayowakabili isikizwe na kuamuliwa.

Bw Ombeta alisema dhamana ni haki ya kila mshtakiwa na kumsihi asiwaachilie washtakiwa kwa dhamana.

“ Washtakiwa ni raia wa Kenya. Mahala pao pa kuishi na kufanyakazi panajulikana,” alisema Bw Ombeta.

Alieleza mahakama mshtakiwa anaweza kunyimwa dhamana ikiwa ushahidi umewasilishwa kuthibitisha atavuruga utekelezaji wa haki.

“Naomba hii mahakama iwaachilie kwa dhamana kwa vile ni haki yao ya kikatiba,” alirai Bw Ombeta.

Bw Andayi aliamuru washtakiwa wazuiliwe gerezani akisubiri kutoa uamuzi wa ombi lao ya dhamana.

Katika mahakama hiyo hiyo, wakili alishtakiwa kuvunja vikombe na kuharibu sufuria na chakula na kusababishia mkahawa ulioko katika jengo la Jamia hasara ya Sh400,000.

Mohammed Salaani alishtakiwa pamoja na Bw Osman Godana Jillo na Abdulaziz Hassan Abdullahi.

Walikanusha shtaka dhidi yao baada ya Bw Andayi kukataa ombi la wakili Salaani la kusitisha akisomea shtaka.

Bw Salaani aliwakilishwa na Bw Muendo Uvyu ambaye alimsihi hakimu asitishe kesi dhidi ya Bw Salaani asuluhishe mambo kadhaa na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DDP).

Kalonzo aonya Uhuru kuhusu wandani wake

Na VALENTINE OBARA

JUHUDI za Rais Uhuru Kenyatta kupambana na ufisadi ziko hatarini kuhujumiwa na wandani wake, Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameonya.

Akizungumza alipokutana na Wakenya wanaoishi Uingereza, Bw Musyoka alisema kwamba anaunga mkono juhudi hizo za rais lakini akamtahadharisha kuhusu wandani wake ambao wamejitolea mhanga kuzivuruga.

“Rais Uhuru Kenyatta ana nia njema katika jitihada zake za kuangamiza ufisadi nchini Kenya lakini kuna watu wenye mamlaka makubwa ambao ni vizingiti na wanaweza kuhatarisha sana lengo lake,” akasema.

Kwa miezi kadhaa sasa, maafisa wa mashirika mbalimbali ya serikali wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kushtakiwa kwa madai ya kuhusika katika ufisadi.

Mashirika hayo yanayojumuisha Kenya Power na shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) yamedaiwa kukumbwa na ufujaji wa mamilioni ya pesa za umma.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hasa kutoka maeneo ya Rift Valley, wamekuwa wakilalamika wakidai kwamba juhudi hizo zinalenga kuhujumu azimio la Naibu Rais William Ruto kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanywa 2022.

“Natumai rais atasimama kidete na kulenga ruwaza yake ya kuangamiza ufisadi nchini. Kenya iko katika njiapanda na inahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu kukabiliana na ufisadi uliokithiri na kupunguza madeni makubwa ya taifa,” akasema Bw Musyoka.

Akizungumza Jumapili alipokuwa katika Kaunti ya Kilifi, Bw Ruto alitaka wanasiasa wote washirikiane kutatua changamoto zinazokumba wananchi bila kuingiza siasa katika juhudi zinazoendelezwa.

Alitaka viongozi wajiepushe na uchochezi wa kisiasa kwani unaathiri maendeleo ya wananchi, na kuwakumbusha kuwa kipindi cha uchaguzi kilikamilika mwaka uliopita.

“Ninawaomba viongozi wenzangu wote waliochaguliwa, nafasi tuliyonayo si ya kuchochea uhasama bali kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazotukumba. Ni lazima tutafute suluhisho kwa njia yenye heshima,” akasema naibu rais.

Akiwa Uingereza, Bw Musyoka alizindua tawi la Chama cha Wiper katika jiji la Birmingham.

Alirejelea kauli kuwa anaunga mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kwani unalenga kuleta umoja wa Wakenya na maendeleo nchini.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kwamba chama chake kinaendeleza mikakati ya kutafuta ushirikiano na vyama mbalimbali kwa maandalizi ya uchaguzi wa 2022.

Katika ziara hiyo, aliandamana na Kaimu Mwenyekiti wa Wiper, Bw Patrick Kiilu, Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Makueni, Bi Rose Mumo Museo na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Kennedy Musyoka.

Walimu waonywa dhidi ya kuuza sodo za serikali

VIONGOZI kutoka Kaunti ya Turkana, wameonya walimu wa shule za msingi na upili dhidi ya kuuza sodo zinazotolewa na serikali bila malipo kwa wasichana wa darasa la sita hadi kitato cha nne.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Turkana, Bi Joyce Emanikor, Mbunge wa Turkana ya Kati, John Lodepe, na Kamishna wa Kaunti, Seif Matata, walisems sodo hizo zilitolewa na serikali kuu kusaidia wasichana hasa wanaotoka katika familia masikini.

Kulingana nao, hatua hiyo ya serikali ilinuiwa kulinda hadhi ya wasichana na kuwawezesha kuendeleza masomo yao bila matatizo.

Bi Emanikor alisema ni sharti walimu wote wahakikishe kuwa sodo zinapofikishwa shuleni mwao, zote zinapeanwa kwa wasichana waliolengwa kwa kiwango kitakachowasaidia kwa muhula mzima.

“Tunataka kila kaunti ndogo na kila wadi ipate sodo za kutosha kwa wasichana wanaolengwa na hakuna sodo zinazofaa kuekwa katika afisi yoyote ya elimu wala stoo ya shule,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Lodepe alisema kila msichana anafaa kupewa pakiti nne ambazo zitawasaidia kwa muhula mzima jinsi ilivyonuiwa.

Alisema wasichana wengi wamekuwa wakikosa kwenda shuleni na wengine kuacha shule kwa sababu ya aibu wanazopitia wanapokuwa kwa hedhi.

Bw Matata alitoa wito kwa machifu, manaibu wao na manaibu wa kamishna wa kaunti kuhakikisha hakuna sodo yenye chapa ya serikali itauzwa madukani.

“Tutachukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayepatikana akiuza sodo hizo. Ninaomba pia wazazi wa wasichana wawe huru kutoa habari kuhusu mwalimu yeyote atakayeuza sodo hizo ili hatua zichukuliwe dhidi yao haraka,” akasema.

Nitamwonyesha Ruto kivumbi 2022 – Joho

Na WINNIE ATIENO

Gavana wa Mombasa Hassan Joho amepuzilia mbali ziara nyingi za Naibu Rais katika eneo la Pwani kutafuta kuungwa mkono, katika azma yake ya kuwania urais 2022, akisema yeye bado ndiye jogoo wa mwambao.

Naibu huyo wa kiongozi wa ODM alisema Bw Ruto anapoteza muda wake Pwani na akaapa kumwonyesha kivumbi 2022 kwa kufanya kazi na wapinzani wa Naibu Rais kuhakikisha ameambulia patupu.

Katika siku za majuzi Bw Ruto amenyemelea Pwani mara tisa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, na juhudi zake zimezaa matunda kwani amevua wabunge 15, ambao wamemwambia watamfanyia kampeni eneo la Pwani 2022.

Hata hivyo wadadisi wa siasa za Pwani wanasema ni mapema mno kuamua mustakabali wa wakazi wa eneo hilo.

Pia wanadokeza kuwa huenda wabunge hao wasimfae Bw Ruto kwenye uchaguzi wa 2022 ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya wabunge eneo hilo huwa hawachaguliwi kwa awamu mbili.

Kwenye uchaguzi wa 2017 wabunge wengi walikojitambulisha na Serikali walipigwa kumbo na wakazi.

Eneo hilo limekuwa likimuunga mkono kwa dhati kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Bw Joho anapania kutegemea ngome zake kwenye azma yake ya kuwania urais.

Licha ya kampeni za kisiasa zilizoanzishwa mapema Pwani, matatizo mengi ya wenyeji hayajashughulikiwa kwani wangali wanakabiliwa na uhaba wa mashamba, umaskini mkubwa, miundo msingi duni miongoni mwa matatizo mengine chungu tele.

Akiongea jana alipofungua wadi ya kina mama wanaopata changamoto baada ya kujifungua katika Hospitali Kuu ya Pwani, Bw Joho alisema azma yake ya kuwania uongozi wa kitaifa haitasimamishwa na yeyote.

Alisema wale wanaopinga ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga ni viongozi wanaoendeleza siasa za chuki.

“Lazima tushirikiane ili tuwe na amani. Kama si ufisadi Kenya ingekuwa mbali sana, kwani fedha hizo zingetumiwa kuboresha maisha ya Wakenya,” akasema.

Mbunge wa Likoni, Mishi Mboko alimuunga mkono akimpa moyo Bw Joho: “Usibabaishwe Bw Joho tuko nyuma yako na tutakusimamia. Wabunge wanaomfuata Bw Ruto wanafanya hivyo ili kumdhalilisha Bw Joho ilhali ni mpwani mwenzenu. Mujue urais unatoka kwa Mungu wala si binadamu.”

Aliwafokea wanasiasa ambao wanazunguka kila pembe ya nchi wakichapa siasa za 2022 akiwataja kama wasio na ajenda ya kuwafaa wananchi.

“Hawa ni watu waliopoteza mwelekeo. Mwingine anadhania ni tajiri sana kila asemacho Wakenya waamini au wafuate. Lakini Wakenya ni wajanja sana na wanaelewa,” akaeleza Bi Mboko.

Kenya yalima Namibia kutinga nusu fainali magongo

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya Kenya ya wavulana imetinga nusu-fainali ya mashindano ya chipukizi ya magongo ya Afrika jijini Algiers nchini Algeria, Julai 23, 2018.

Kenya ilijikatia tiketi baada ya kushangaza Namibia kwa mabao 3-1. Haikuwa imeshinda mechi katika awamu ya makundi ilipolizwa 2-1 na Nigeria na kupokea kichapo sawa na hicho kutoka kwa Zambia katika Kundi B.

Wakenya watapambana na mshindi kati ya Zambia na Algeria katika nusu-fainali nayo Nigeria ina kibarua kigumu dhidi ya Afrika Kusini.

Namibia ilikamilisha Kundi A katika nafasi ya pili kwa alama sita ilizopata kwa kunyuka Zimbabwe 5-2 na Algeria 4-1. Ilikuwa imechabangwa 4-0 na Afrika Kusini katika mechi ya ufunguzi Julai 19.

Nigeria ilipepeta Zimbabwe 1-0 katika robo-fainali ya kwanza Jumatatu. Mechi nyingine ya robo-fainali itakutanisha Zambia na Algeria. Afrika Kusini ilinyuka Zimbabwe 6-0, Namibia 5-0 na Algeria 9-0 katika mechi za makundi. Kenya haishiriki magongo ya wasichana ambayo yamevutia Afrika Kusini, Ghana, Zimbabwe, Namibia, Nigeria na Algeria.

Mashindano ya magongo yatakamilika Julai 26. Algeria inaandaa makala ya tatu ya mashindano ya chipukizi yanayojumuisha fani 31. Yalianza Julai 18. Yatakamilika Julai 28. Riadha, ambayo Kenya inasubiri sana, itaanza Machi 24.

Crested Cranes wapata dawa yao Cecafa

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Tanzania wameandikisha ushindi wao wa kwanza katika Soka ya Wanawake ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kupepeta Uganda 4-1 jijini Kigali, Rwanda, Jumatatu.

Kilimanjaro Queens, ambayo ililimwa 1-0 na Rwanda mnamo Julai 19 na kukabwa 1-1 dhidi ya Kenya katika mechi ya pili Julai 21, ilifufua kampeni ya kutetea taji kupitia mabao ya nahodha Asha Rashid, Donasia Daniel na Asha Hamza Shaban. Daniel alimegea Rashid pasi safi iliyozalisha bao dakika ya 17.

Rashid ‘alirudisha mkono’ kwa kumega pasi murwa iliyokamilishwa na Daniel dakika ya 23. Rashid alipachika bao la tatu dakika ya 45 kabla tu ya mapumziko baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Fatuma Issa.

Tanzania, ambayo ilicharaza Kenya 2-1 katika fainali ya makala yaliyopita nchini Uganda, ilipata bao la nne kupitia kwa Shaban dakika ya 52. Alipokea pasi nzuri kutoka kwa Stumai Abdalla.

Crested Cranes, ambayo ilishangaza Kenya 1-0 katika mechi ya ufunguzi na kulima Ethiopia 2-1 katika mechi ya pili, ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 90.

Cranes inaongoza mashindano haya ya mataifa matano kwa alama sita. Itarukwa na Rwanda ikiwa wenyeji hawa watalemea Ethiopia baadaye Jumatatu. Harambee Starlets ya Kenya haina mechi hadi Julai 25 itakapomenyana na Ethiopia. Starlets ina alama moja. Tukienda mitamboni, Ethiopia haikuwa na alama.

Makumbi aonyeshwa mlango na Western Stima

NA CECIL ODONGO

KLABU ya Western Stima ambayo inashiriki ligi ya Supa Jumanne imemwachisha kazi  kocha wake raia wa Uganda Richard Makumbi.

Stima, imekuwa ikisajili matokeo yasiyoridhisha na mnamo Jumapili Julai 22,2018 walibanduliwa nje ya mashindano ya kombe la ngao ya SportPesa na Mabingwa wa KPL mwaka wa 2009, Sofapaka baada ya kulazwa mabao 4-0.

“Kutokana na matokeo mabaya katika mkondo wa pili wa ligi, usimamizi wa klabu umeafikia uamuzi wa kumpiga kalamu Richard Makumbi,” ikasema taarifa kutoka Western Stima FC.

Hili likuwa pigo kubwa kwa wanaumeme hao waliotarajia ushindi na ambao ungewavumisha hadi robo –fainali na kuimarisha uwezo wao wa  kutwaa kombe hilo.

Baada ya kuongoza jedwali la NSL katika mkondo wa kwanza wa ligi, timu hiyo sasa imeshuka hadi nafasi ya pili, alama mbili nyuma ya viongozi Ushuru FC.

Cha kushangaza ni kwamba kikosi cha stima kimeporomoka na kupoteza uongozi hata baada ya kufungua mwanya wa alama 12 kati yao na nambari kabla ya mechi tano za mwisho wa mkondo wa kwanza.

Kufuatia kutimuliwa kwa Makumbi, uongozi wa Western Stima umempokeza usukani kwa muda aliyekuwa naibu kocha wa Kisumu All Stars Paul Ogai.

Makumbi alijiunga na Western Stima Septemba, 2017 kujaza nafasi ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Henry Omino ambaye pia alionyeshwa mlango kutokana na sababu iyo hiyo ya kusajili matokeo mabaya.

Alitarajiwa kunasua Stima kutoka kwa hatari ya kuteremshwa ngazi ila hakufaulu. Hata hivyo amejizolea sifa kedekede kwa kuleta umoja na udhabiti timuni.

Kasisi motoni kwa kupora wanawake Sh1.3 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA aliyejitambulisha kwa kikundi cha kina mama kuwa Kasisi wa kanisa la Kianglikana na kupokea zaidi ya Sh1.3milioni Jumatatu alishtakiwa kwa kuwadanganya angeliwasaidia kununua ardhi katika eneo la Kitengela kaunti ya Kajiado miaka sita iliyopita.

Bw Gordon Apora Anyumba aliyefikishwa mbele ya hakimu mkuu Mahakama ya Milimani Nairobi Bw  Francis Andayi alikanusha shtaka la kuwatapeli kina mama hao Sh1,350,000.

Shtaka lilisema kuwa kikundi hicho cha kina mama kinajulikana kwa jina Lima Women Group.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha , alisema Bw Anyumba alijitambulisha kwa kikundi hicho cha kina mama kuwa Kasisi wa Kanisa la Anglican Church of Kenya (ACK) anayehudumu katika kanisa la St Stephens tawi la Jogoo Road Nairobi.

Bw Naulikha alisema mshtakiwa alikuwa anakutana na wanachama 13 wa kikundi hicho cha kina mama katika kanisa hilo la ACK tawi la Jogoo akidai ardhi aliyokuwa anawasaidia kina mama hao kununua inamilikiwa na kanisa hilo la ACK.

Mahakama Ilifahamishwa kuwa mshtakiwa aliopkea pesa hizo kutoka kwa kundi hilo la kina mama waliokuwa wanataka kuekeza katika mradi wa ujenzi wa nyumba kati ya Agosti 24 na Novemba 14 2012.

Mshtakiwa alikanusha shtaka hilo na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Bw Naulikha hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bw Andayi alimwagiza mshtakiwa awasilishe dhamana ya pesa tasilimu Sh300,000 na kutengeza kesi hiyo isikizwe  Agosti 21 mwaka huu.

Mahakama pia iliamuru mshtakiwa akabidhiwe nakala za ushahidi ulionakaliwa na polisi.

TUZO YA NOBEL: Sheria ambazo Raila anafaa kufuata kushinda tuzo

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA wamechangamkia hoja iliyowasilishwa na raia wa Uingereza Ali Abdi akitaka kiongozi wa upinzani Raila Amolo Odinga ateuliwe kuwa mshindi wa tuzo ya kifahari ya amani ya Nobel. Hata hivyo, licha ya kuwa wazo nzuri, inaonekana Mkenya huyu hakufuata taratibu.

Kwa mujibu wa tovuti ya www.nobelprize.org, jina la mpendekezaji pamoja na jina la mtu ama shirika linalopendekezwa kuwania tuzo hii yanafaa kuwa siri hadi miaka 50 ikamilike.

Shughuli ya uteuzi ya wawaniaji huanza mwezi Septemba. Huo ndio wakati Kamati ya Nobel ya nchi ya Norway inajiandaa kupokea maombi.

Maombi haya huwasilishwa na wabunge, serikali, na mahakama za kimataifa za sheria; machansela wa Vyuo Vikuu, maprofesa wa sayansi ya jamii, historia, falsafa, sheria na theolojia, viongozi mambalimbali wa taasisi za utafiti za amani na taasisi za masuala ya kigeni; washindi wa zamani wa tuzo ya Nobel; wanachama wa bodi ya mashirika ambayo yamepokea tuzo hii; wanachama wa zamani na wa sasa wa Kamati ya Nobel ya Norway; na washauri wa zamani wa wa taasisi ya Nobel ya Norway.

Februari ni mwezi wa mwisho wa kuwasilisha maombi hayo. Ili kutiwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya Nobel mwaka unaozungumziwa, kwa mfano mwaka 2018, uteuzi huwa unatumwa kwa Kamati ya Nobel nchini Norway jijini Oslo kabla ya Februari 1 mwaka huo.

Maombi yanayopokelewa baada ya Januari 31 saa sita usiku yanatiwa katika orodha ya kujadiliwa mwaka unaofuata. Katika miaka ya hivi karibuni, Kamati hii imepokea karibu maombi 200 kuwania vitengo tofauti vya tuzo ya Nobel.

Tovuti ya tuzo hii inasema kuna wagombeaji 330 mwaka 2018, watu 216 binafsi na mashirika 114. Idadi ya barua zinazopigia debe wawaniaji/mashirika wakati mwingine huwa juu kwa sababu mara nyingi zinakuwa zinaunga mkono wagombea ambao si tofauti.

Orodha fupi kisha huundwa kati ya Februari na Machi baada ya kamati kutathmini kazi ya mwaniaji. Kati ya Machi na Agosti, mshauri anapitia teuzi hizo.

Washindi wa tuzo ya Nobel huchaguliwa mwezi wa Oktoba. Kamati ya Nobel inafanya kazi hiyo kwa kupiga kura, mshindi akiwa mwaniaji aliyepata kura nyingi. Uamuzi huo wa kura na hauwezi kubadilishwa hata kwa kukata rufaa. Majina ya washindi wa tuzo hii ya amani ya Nobel kisha yanatangazwa.

Hafla ya kutuza washindi wa tuzo ya Nobel hufanywa Desemba 10 jijini Oslo. Washindi hupewa tuzo hiyo ambayo huandamana na medali ya Nobel na Diploma na cheti kinachothibitisha zawadi ya fedha iliyotolewa.

Kwa mfano, mshindi wa mwaka 2017 Shirika la kumaliza sila za nyuklia (International Campaign to Abolish Nuclear Weapons – ICAN) lilipokea Krona 9, 000, 000 (Sh102, 382,827 za Kenya). Marehemu Maathai alizawadiwa Krona 8, 218, 994 za Uswidi, ambazo zikibadilishwa kwa pesa za Kenya ni Sh93, 495,974.

Mshindi wa tuzo ya mwaka 2018 atatangazwa Oktoba 5 jijini Oslo nchini Norway. Atapokea zawadi Desemba. Tuzo hii imepeanwa kutoka mwaka 1901 isipokuwa miaka 1914-1916, 1918, 1923, 1924, 1928, 1932, 1939-1943, 1948, 1955-1956, 1966-1967 na 1972. Tangu tuzo hii ianzishwe mwaka 1901, washindi 131 wameipokea (watu 104 binafsi na mashirika 27).

Ni Mkenya mmoja pekee amewahi kushinda tuzo hii. Mwendazake Wangari Maathai aliibuka mshindi mwaka 2004. Mchango wake mkubwa katika maendeleo, demokrasia na amani yalimfanya kutawazwa mshindi.

Kutokana na taratibu iliyoelezewa na tovuti ya tuzo hii, inaonekana ombi la Abdi kutaka kiongozi Odinga ajumuishwe katika orodha ya wawaniaji wa mwaka 2018 liliwasili kuchelewa.

Abdi amemmiminia Bw Odinga sifa tele katika juhudi za kutafuta amani nchini Sudan Kusini pamoja na kutatua uhasama mkubwa uliokuwa ukitokota nchini Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2017 kupitia mkataba wa amani na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018, miongoni mwa masuala mengine mengi yakiwemo kupigania demokrasia barani Afrika.

Kufikia Julai 23 asubuhi, tovuti kadhaa nchini Kenya ziliripoti kwamba Wakenya 1, 870 walikuwa ametia sahihi ombi la Abdi kupigia debe Odinga kuwania tuzo hiyo.

Magunia ya bangi yanaswa Nakuru

NA PETER MBURU

Polisi mjini Nakuru Jumanne walinasa gari lililokuwa likisafirisha bangi kuelekea upande wa Nairobi, ikihofiwa kutoka taifa jirani.

Gari hilo aina ya Fielder (KBZ 676Z) lilikamatwa eneo la Mbaruk, kilomita chache baada ya kupita mji wa Nakuru likiwa limejaa magunia na misokoto ya bangi.

Maafisa wa usalama waonyesha mbinu ambazo walanguzi huweka bangi wakati wa usafirishaji. Picha/ Peter Mburu

Kulingana na naibu wa kamishna wa kaunti eneo la Nakuru Mjini Mashariki Herman Shambi, bangi hiyo ina dhamana ya Sh1.3milioni na ilipitia sehemu za magharibi mwa nchi.

Bw Shambi aliwaonya wale wanaotumia barabara hiyo kusafirisha bidhaa haramu kwa watakamatwa na polisi wa kaunti hiyo ambao wako macho kila wakati.

Maafisa wastaajabu kuona maelfu ya misokoto ya bangi iliyonaswa Nakuru. Picha/ Peter Mburu

“Watafute njia mbadala kwa kuwa hapa lazima tutawakamata, hivi ni vita ambavyo tutapambana navyo kwa kuwa askari wetu wako imara na wamejipanga vizuri,” akasema Bw Shambi.

Afisa huyo aidha aliwatahadharisha wazazi kuwa makini kuchunguza mienendo ya watoto wao haswa wakati huu ambapo likizo ya shule inaelekea, akisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa walengwa wa soko la mihadarati.

Magunia ya bangi yaliyonaswa mjini Nakuru. Picha/ Peter Mburu

“Hii bangi inauziwa wakenya na imeharibu watoto wengi sana, wazazi tuangalie maadili na mienendo ya watoto wetu. Huenda baadhi ya visa vya utovu wa nidhabu tunavyosikia kutoka shule nyingi vinatokana na mambo haya,” akasema Bw Shambi.

Bidhaa hizo zilipelekwa katika makao makuu ya idara ya ujasusi Nakuru, huku polisi wakisisitiza kuwa uchunguzi mkali tayari umeanzwa kuwakamata waliokuwa kwenye gari hilo kwani walitoroka kwa miguu.

Polisi waliongeza kuwa watachunguza na kumkamata mmiliki wa gari hilo, ili asaidie katika uchunguzi.

Sukari sasa ni salama, Munya aambia Wakenya

Na CECIL ODONGO

WAKENYA hawafai kuhofia kuhusu uwepo wa sukari ghushi sokoni baada ya ripoti ya uchunguzi uliofanywa na maabara ya serikali na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS) kutaja kwamba kiasi kikubwa cha sukari iliyonaswa kilikuwa ghushi na kitaharibiwa.

Kulingana na matokeo ya uchunguzi huo, kati ya magunia 1,266,668 ya sukari yaliyoshukiwa kuwa ghushi, magunia 837,224 yalipatikana kuwa hayafai kwa watumiaji bidhaa huku magunia 157,392 yakipatikana kuwa hayana kasoro.

Katika kaunti 28 ambazo sampuli 82 za sukari hiyo zilipimwa, sampuli 31 (38%) zilipatikana na kasoro huku sampuli nyingine 51(62%) zikipatikana kuwa sawa kwa matumizi ya binadamu.

Hata hivyo, kinaya kikubwa  ni kwamba sukari hiyo haikuwa na madini ya zaibaki na shaba jinsi ilivyodaiwa na wengi  ila iliharibika baada ya kuhifadhiwa vibaya katika maghala ya kuhifadhi bidhaa.

Katika kikao na wanahabari ofisini mwake wakati wa kutoa  matokeo hayo, Waziri wa Viwanda Peter Munya aliliagiza shirika linalopigana na bidhaa ghushi nchini liharibu sukari hiyo mara moja  katika shughuli ya wazi  kwa umma na wanahabari.

“Kutokana na matokeo haya, KEBS kwa ushirikiano na taasisi husika zitaharibu kulingana na sheria sukari yote iliyofeli vipimo vya uchunguzi  na walioiagiza watalazimika kugharamia uharibifu huo la sivyo tutaisafirisha katika nchi ilikotolewa,” akasema Bw Munya.

Bw Munya pia alisisitiza kwamba bidhaa zinazoingizwa hapa nchini zitakagukuliwa na ziwekewe alama spesheli ya KEBS ya kuzitambuai kabla hazijaidhinishwa kuuzwa sokoni kama njia ya kuhakikisha ubora wao.

“Tutashiriki ukaguzi wa kipekee kwa mashehena mbalimbali haswa ya bidhaa za vyakula. Pia tutaingia sokoni ili kuondoa  bidhaa ambazo hazijatimiza ubora unahitajika na shirika la KEBS,” akaongeza Bw Munya.

Uchunguzi huo pia ulifichua kwamba,  Kati ya tani 7,750 za sukari zilizonaswa tani 3,555  hazikuwa ghushi na zimerejeshewa wafanyabiashara waagizaji huku KEBS ikiendelea kufanyia uchunguzi tani 4200 zilizosalia.

Waziri huyo pia alithibitisha kwamba serikali imefanyia uchunguzi sampuli 40 ya shehena za mafuta yaliyonaswa  kwa kushukiwa kuingizwa  nchini kimagendo.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionyesha kwamba ni shehena 25 ndizo zilifeli vipimo vya KEBS huku 15 zikipatikana kuwa sawa.

Kizimbani kwa kuiba TV watazame Kombe la Dunia

Na RICHARD MUNGUTi

WASHUKIWA wawili waliompora mwenye duka la elektroniko televisheni kutazama mechi za Kombe la Dunia  walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka. 

Mabw Alfred Oyugi Orwaru na Franc Omondi Amolo walikanusha shtaka la kupokea mali kwa njia ya udanganyifu.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Francis Andayi alijaribu awezalo kujua sababu ya washtakiwa kutolipa mwenye duka lakini “walinyamaza kabisa.”

“Nataka mnieleze sababu hamkulipa mwenye duka televisheni aliyowapatia yenye thamani ya Sh65,000,” hakimu aliwahoji.

Akamwulia Oyugi , “Wewe nieleze ulimlipa mwene duka pesa gapi?”

Alijibu, “Nilienda  kwa Bw Robinson Murage nikamlipa pesa kisha nikapewa runinga.”

Lakini licha ya kuwashauri kuwa atawaachilia kwa vile pesa wanazodaiwa ni ndogo “hawakutoboa siri ya kukataa kulipia televisheni hiyo.”

“Sitaki kuharibu wakati na kesi ya Sh65,000. Muda uliopo ni wakuamua kesi za milioni mia tano na mabilioni ya umma yaliyoibwa. Mngeliomba msamaha ningeliwaachilia kisha niwaambie mkitaka kuendelea na wizi endeleeni tutakuja kuokota maiti zenu kama mmepigwa na raia,” Bw Andayi.

Washtakiwa waliomba wapewe muda wasuluhishe deni hilo na Bw Murage.

Kesi hiyo itatajwa Julai 23, 2018 kwa vile Bw Murage hakuwa na mtu wa kumwacha kwenye duka afike kortini kurekodi makubaliano.

Wanakijiji waua mamba 300 kulipiza kisasi

Na MASHIRIKA

JAKARTA, INDONESIA

WANAKIJIJI waliua mamba karibu 300 kulipiza kisasi kwa mwenzao aliyeangamizwa na mmoja wa wanyama hao.

Kulingana na mashirika ya habari, mwanamume alikuwa ameuawa na mamba katika shamba la kuwafuga katika Wilaya ya Sorong, mkoa wa West Papua.

Maafisa wa serikali walinukuliwa kusema mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 48 alikuwa akivuna nyasi za kulisha mifugo wakati aliposhambuliwa na kuangamizwa.

Hili halikufurahisha wanakijiji ambao waliamua kulipiza kisasi, wakachukua visu, nyundo na marungu na kuua mamba 292 baada ya kumzika mwenzao.

Picha zilizosambazwa mitandaoni zilionyesha wanakijiji wakiwa wamesimama kando ya mamia ya mizoga ya mamba.

Maafisa wa serikali walisema shamba hilo lilikuwa likifuga mamba tangu mwaka wa 2013 na leseni ilitolewa kwa msingi kuwa ufugaji huo hautatatiza jamii.

Hata hivyo, hatua ya wanakijiji pia ilikashifiwa kwani ilisemekana wangetafuta njia mbadala ya kupooza hasira zao.

-Imekusanywa na Valentine Obara

Watoto 5 wabambwa kwa kubaka msichana kwa zamu

Na MASHIRIKA

DEHRADUN, INDIA

WATOTO watano wa kiume walikamatwa na polisi kwa kumbaka msichana mwenye umri wa miaka minane baada ya kutazama filamu za ngono.

Ripoti zinasema wavulana hao wenye umri wa kati ya miaka tisa na 14, walikuwa wametazama filamu hizo kwenye simu ya rununu.

Polisi walinukuliwa kusema kuwa walimhadaa msichana huyo kwenda nyumbani kwa rafiki yao katika eneo la Sahaspur lililo Dehradun, kisha wakamvamia na kumbaka mmoja baada ya mwingine.

Mkuu wa polisi wa Sahaspur, Naresh Rathore, alinukuliwa na vyombo vya habari kusema wavulana hao walifahamu msichana huyo huwa yuko peke yake nyumbani wakati walipomtendea ukatili huo unaoaminika walipanga siki kadhaa awali.

Ilisemekana walimwona mwathiriwa akicheza peke yake nje wakati walipomhadaa aandamane nao.

Wavulana hao waliwekwa kizuizini na kfufunguliwa mashtaka, kisha baadaye wakapelekwa katika kituo cha kurekebisha tabia huku mwathiriwa akitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

-Imekusanywa na Valentine Obara

Kuira bingwa wa Shibetsu Half Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Paul Kuira aliibuka mshindi wa mbio za Shibetsu Half Marathon nchini Japan baada ya kuzikamilisha kwa rekodi mpya ya saa 1:03:10 Julai 22, 2018.

Kuira alilazimika kufanya kazi ya ziada katika hatua za mwisho kwenye mbio hizi za kilomita 21 zilizofanyika wakati wa joto kali na kuwanyima Wajapani Tomohiro Tanigawa na Tsubasa Hayakawa ushindi. Tanigawa alikamilisha katika nafasi ya pili kwa saa 1:03:15 naye bingwa mtetezi Hayakawa akafunga tatu-bora kwa saa 1:03:18.

Mkenya James Ndirangu alishikilia rekodi ya Shibetsu Half Marathon ya saa 1:03:22 aliyoweka akishinda taji la mwaka 2016 kabla ya Kuira kuifuta.

Kuira ni mwanamume wa tano kutoka Kenya kuwahi kushinda mbio hizi baada ya Solomon Kariuki (1996), Kipng’eno Kibet (2008), Kiragu Njuguna (2009) na Ndirangu (2016).

Wakenya Esther Wanjiru, Ruth Wanjiru na Winfrida Kebaso wamewahi kunyakua mataji ya Shibetsu Half Marathon. Esther alitawazwa bingwa mwaka 1996 na 1999, Ruth akashinda mwaka 2006 naye Kebaso akaibuka mshindi mwaka 2015. Kotomi Tsubokura alihakikisha taji la mwaka huu linasalia nchini Japan alipokata utepe kwa saa 1:15:42.

Matokeo (Julai 22, 2018):

Wanaume (Kilomita 21)

 1. Paul Kuira (Kenya) saa 1:03:10
 2. Tsubasa Hayakawa (Japan) 1:03:15
 3. Tomohiro Tanigawa (Japan) 1:03:18
 4. Ryo Matsumoto (Japan) 1:03:44
 5. Kenta Iinuma (Japan) 1:04:21

Wanawake (Kilomita 21)

 1. Kotomi Tsubokura (Japan) 1:15:42
 2. Ayaka Inoue (Japan) 1:16:15
 3. Kikuyo Tsuzaki (Japan) 1:16:22
 4. Madoka Nakano (Japan) 1:16:28
 5. Hiroko Miyauchi (Japan) 1:16:38

Wanawake (Kilomita 10)

 1. Natsuki Omori (Japan) dakika 34:08
 2. Mai Ito (Japan) 34:16
 3. Junna Suzuki (Japan) 34:17
 4. Ikumi Fukura (Japan) 34:21

5. Kanako Takemoto (Japan) 34:28