Msigawanyike, Kalonzo ataachiwa urais na Uhuru Kenyatta – Mbunge

Na Gastone Valusi

MBUNGE wa Kathiani Robert Mbui ameiomba jamii ya Akamba kuwapuuzilia mbali viongozi ambao wanatumiwa na wanasiasa kutoka nje kusambaratisha juhudi za kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwania urais mnamo 2022.

Bw Mbui alisema jamii hiyo inapaswa kujihadhari dhidi ya wale wanaolenga kuyumbisha juhudi za Bw Musyoka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Alisema baadhi ya wabunge ambao si wanachama wa chama hicho wanatumika kuigawanya jamii hiyo.

Alisema viongozi wa sehemu hiyo wamegawanyika kwa muda mrefu.

Alitoa kauli hiyo Jumatatu katika eneo la Kathiani, kwenye mkutano na wazee.

 

Mtoto aliyenusurika mafuriko kimiujiza afadhiliwa masomo

Na CHARLES LWANGA

MWANAFUNZI wa Darasa la Tatu aliyepotea kwenye mto Tana baada ya boti la kuwaokoa waathiriwa wa mafuriko kuzama na kupatikana baada ya siku nane bila kuvamiwa na mamba na viboko sasa amebahatika kupata ufadhili wa kimasomo.

Naibu mkurugenzi wa Shirika la Msalaba Mwekundu (KRSC) Dkt Asha Mohamed na Bi Najat Ibrahim wa KRCS tawi la Malindi, walijitolea kumfadhili mtoto huyo, Khadija Mohamed hadi chuo Kikuu wakati wa sherehe za kuchangisha pesa kuwasaidia zaidi ya watu 86,000 waliyoathirika na mafuriko katika Kaunti za Kilifi na Tana River.

Kati ya watu watatu waliopotea kwa siku kadhaa baada ya boti hilo kuzama, Khadija ndiye pekee aliyepatikana hai baada ya kukwamilia gongo lililokuwa linaelea majini hadi alipopata usaidizi.

Babake, Bw Bakero Dube hangeweza kudhibiti machozi yake aliposimulia mamia ya wafadhili waliohudhila hafla kisa hicho cha Aprili 27 ambacho kilimwacha bintiye wa miaka 12 marehemu na mwingine kutoweka hadi leo.

Bw Dube aliyeambatana na mwanawe Khadija alisema Khadija ambaye ni mwanafunzi katika shule ya Galili huko Garsen alipatikana kilomita saba kutoka eneo walikozama.

“Niko hapa kusema asante kwa shirika hili la Msalaba Mwekundu kwa yale wamenitendea na nikupitia msaada wao tunaendelea kupata nafuu baada ya msiba huo,” alisema.

Wapiga mbizi wa Msalaba mwekundu walimpata Khadija akiwa mnyonge huku amekwamilia gongo kwenye kichaka kilichojaa maji kutokana na mafuriko.

“Boti letu lilizama baada ya kugongana na boti lingine lililokuwa linaokoa waathiriwa. Tayati nimemzika binti yangu mwingine wa miaka 12 aliyeokolewa na KRCS ambao walikuwa wamepoteza matumaini kabla ya kumpata Khadija, mwingine hajawahi kupatikana hadi wa leo,” alisema.

Masharti makali yatolewa kulinda wanafunzi tamashani

Na IRENE MUGO

MABASI yanayosafirisha wanafunzi kuhudhuria mashindano ya kitaifa ya muziki yanayoendelea katika Kaunti ya Nyeri yatazuiliwa yakipatikana barabarani baada ya saa kumi na mbili jioni.

Kulingana na Mwenyekiti wa mashindano hayo, Bw Peter Wanjohi, walimu wa shule husika watahitajika kuwatunza wanafunzi wao ipasavyo.

“Shule zote zimepewa arafa inayotoa mwongozo kuhusu masharti haya. Sheria za trafiki zitatekelezwa na maafisa wa usalama watahakikisha sheria imefuatwa kikamilifu,” akasema.

Alitangaza hayo baada ya wanafunzi kumi kufariki kwenye ajali ya barabarani usiku wa kuamkia Jumapili.

Wachuuzi pia wamezuiliwa kuuza bidhaa zao katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi ambako mashindano hayo yanafanyika ili kuhakikisha wanafunzi hawapewi vyakula vitakavyodhuru afya zao.

Hatua hii pia imenuia kuzuia ulanguzi wa dawa za kulevya na pombe katika eneo hilo.

“Ili kuhakikishia wanafunzi wetu usalama, hatutaki kuona wachuuzi wakiingiza bidhaa zao hapa ndani,” akasema Bw Wanjohi. Maafisa wa afya ya umma katika kaunti wanatarajiwa kuchunguza maandalizi ya vyakula vyote vitakavyopikwa kwa ajili yawanafunzi hao 120,000.

Wakati huo huo, maafisa wa matibabu wamekita kambi katika chuo hicho endapo kutakuwa na matukio yoyote ya dharura yanayowahitaji.

Hii ni mara ya kwanza mashindano hayo kufanywa Nyeri na katika eneo la kati kwa jumla.

Katika tamasha hiyo kutakuwa pia na maonyesho kutoka kwa wanafunzi wa nchi za Rwanda na Sudan Kusini.

Maonyesho ya kwanza yalifanywa na wanafunzi wa chekechea na walemavu.

Kamishna wa eneo la kati, Bw Wilson Njenga, alihakikishia wanaohudhuria tamasha hiyo watadumishiwa usalama kwa wiki zote mbili.

Fedha za umma zilizofujwa zirejeshwe upesi – Sapit

Na GERALD BWISA

SERIKALI imeombwa kushinikiza kurejeshwa kwa pesa zilizoibwa katika ufisadi huku juhudi zikiimarishwa kupambana na ufujaji wa pesa za umma.

Akizungumza na wanahabari Kitale Jumapili, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana la Kenya, Jackson ole Sapit, alimwambia Rais Uhuru Kenyatta asilegeze kamba katika juhudi hizo.

Alisema inafaa mapambano dhidi ya ufisadi yaendelee hadi wakati pesa zote za umma na rasilimali zilizopotea zirudishwe na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi.

“Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na Idara ya Mashtaka ya Umma zimepiga hatua kubwa kwa kufikisha mahakamani wale wanaojihusisha katika ufisadi lakini haifai yaishie hapo. Kama kuna pesa zozote zilizopotea katika ufisadi inafaa zirejeshwe,” akasema.

Bw Sapit alisema kuna taasisi kama vile hospitali za umma ambazo zina uhaba wa mahitaji muhimu ilhali watu binafsi wanafuja pesa za umma.

“Tuna uhaba wa dawa hospitalini, pesa zinazofujwa zinafaa zirejeshwe ili zitumiwe kununua dawa hospitalini na pia kutumiwa kwa ujenzi wa miundomsingi kwa manufaa ya wananchi,” akasema.

Alitoa wito pia kwa bunge la taifa, hasa kamati inayochunguza sakata ya sukari kuhakikisha ripoti zinazotolewa zimezingatia ukweli uliopo.

Aliwataka wabunge wajiepushe kushawishiwa ili wafiche uweli bali waseme yote waliyobainisha kwenye uchunguzi wao.

Askofu huyo mkuu aliomba pia viongozi nchini wawe na malengo yatakayodumisha utulivu nchini hata wakati watakapoondoka mamlakani.

Alisema viongozi watakutana kufanya mashauriano kuhusu jinsi ya kuzuia changamoto zinazoweza kuweka vikwazo kwa utekelezaji wa malengo muhimu kwa taifa. Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri wa Wanyamapori na Misitu, Dkt Noah Wekesa, aliunga mkono juhudi za rais kupambana na ufisadi.

Dkt Wekesa alisema ufisadi umeathiri maendeleo ya nchi. Alitoa wito kwa viongozi wa makanisa kuongoza Wakristo ili watekeleze majukumu yao ya kuchangia katika kupambana na ufisadi na kuhakikisha kuna mafanikio katika juhudi hizo.

“Rais ana ajenda nne anazolenga kufanikisha. Kwa mtazamo wangu akiendelea kupambana na ufisadi kwa moyo wake wote, hilo pekee litapewa umuhimu kuliko ajenda hizo nne kwa kuwa ufisadi umeelekeza nchi yetu pabaya,” akasema.

Vioski vya muguka vyaanza kubomolewa Mombasa

Na MOHAMED AHMED

SIKU moja baada ya wawakilishi wa wadi ya Mombasa kuanzisha mikakati ya kupiga marufuku uuzaji wa muguka askari wa kaunti Jumatatu walianza kubomoa vibanda vinavyouza mmea huo.

Zaidi ya askari 20 walivivamia vibanda hivyo na kuvibomoa eneo la Tononoka ambapo soko kubwa la Muguka hupatikana.

Kamati ya Afya ya bunge la Mombasa ilisema kuwa Muguka umeathiri pakubwa ndoa nyingi na kuchangia kuvunjika kwa baadhi ya ndoa hizo.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Fatma Kushe alisema kuwa idadi kubwa ya vijana wanaotumia mmea huo inatishia kizazi kijacho.

Jumatatu, mkurugenzi wa askari wa kaunti Mohammed Amir alisema kuwa ubomozi huo ulifanyika baada ya agizo kutoka katika kitengo cha afya kufuatia ongezeko la visa vya vijana wadogo kuingia katika uraibu huo.

Ubomoaji huo pia unakuja wiki moja baada ya wawakilishi wa wodi ya Mombasa kupendekeza agizo la kupiga marufuku ya Muguka katika kaunti hiyo.

Askari wa kaunti ya Mombasa wang’oa paa la kioski cha muguka eneo la Tononoka Agosti 6, 2018. Picha/ NMG

Hata hivyo kufikia sasa bado serikali ya kaunti haijapitisha agizo hilo la kuzia kuuzwa na utumizi wa Muguka. Mombasa ni kaunti ya tatu sasa ambayo imeingia katika kampeni ya kupiga marufuku mmea huo huku serikali ya Kwale ikiwa tayari imepitisha agizo la kuzuai kuuzwa na kutumiwa kwa Muguka.

Vijana wengi kutoka kwale hununua bidhaa hiyo eneo la Likoni ambapo ni karibu na kaunti hiyo. Kaunti ya Kilifi pia inaendesha mipango ya kuzuia utumizi wa Muguka huku baadhi ya viongozi wakilia ongezeko la matumizi yake miongoni mwa vijana wa shule.

Aidha, jana wafanyabiashara jijini Mombasa walilalamika kuvunjiwa vibanda vyao na kuwashutumu askari hao kutekeleza ubomoaji huo.

“Hakuna agizo lolote ambalo limepitishwa, mbona watuvunjie vibanda vyetu? Sisi kila siku tunalipa ada ya kufanya biashara kwa askari hao wa kaunti leo hii wanatukatizia riziki yetu bila sababu yoyote. Wanataka twende wapi? Ama wanafurahia kukiwa na uhalifu?” akalalama Bw Gabriel Kithaka, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara eneo hilo la Tononoka.

Mfanyabiashara mwengine Bi Miriam Wangeci, alipinga madai kuwa mmea huo unachangia katika kuvunja ndoa.

“Hayo ni madai tu kama mtu hawezi shughuli basi ni Mungu amemuumba hivyo na sio Muguka.Kuna watu wanatumia dawa za kulevya ambazo wanajua ni mbaya kwa afya lakini bado wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” akasema.

Mudavadi adai Raila aliwaficha kuhusu muafaka

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, ameibua shaka kuhusu kama Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga alikuwa mwaminifu kwa vinara wenzake wa NASA kabla aungane na serikali.

Kulingana na Bw Mudavadi, uamuzi wa Bw Odinga kushirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta uliashiria kuwa wawili hao walikuwa wakishauriana kwa muda mrefu bila vinara wengine wa NASA kujua.

“Hakuna jinsi angechukua hatua aina hii ghafla. Ni wazi mipango hiyo ilikuwa ikiendelezwa kwa muda mrefu ilhali mimi kibinafsi sikufahamu,” akasema kwenye mahojiano Jumapili usiku katika Runinga ya NTV.

Kwenye mahojiano tofauti, Bw Odinga amewahi kuthibitisha kuwa hatua yake kushirikiana na Rais Kenyatta ilikuwa siri yao wawili ingawa haifahamiki walikuwa wakishauriana kwa muda gani.

Waziri huyo mkuu wa zamani pia amekuwa akikosolewa na wenzake wanaodai alienda kula kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’ katika uwanja wa Uhuru Park walipokuwa wakimsubiri kwingine.

Bw Mudavadi alimwonya Bw Odinga na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu ushirikiano wao na serikali akasema hatafuata mkondo huo bali chama chake kitatekeleza majukumu ya upande wa upinzani nchini.

Kulingana na makamu huyo wa rais wa zamani, hakuna ubaya kwa viongozi wa pande tofauti za kisiasa kushirikiana lakini kuna hatari kubwa wakati ushirikiano huo unapotishia kuangamiza upinzani.

“Hatufai kuonekana kwamba sote sasa tunafululiza kujiunga na serikali. Jubilee inakumbwa na matatizo mengi serikalini na hatustahili kuwa washirika wake katika makosa inayofanya,” akasema.

Wiki iliyopita, Bw Musyoka alitangaza kuwa wanachama wa Wiper walikubaliana kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, na wabunge wake wakaagizwa kuunga mkono ajenda za serikali wakiwa bungeni.

Hata hivyo, Bw Mudavadi alisema uamuzi wake haumaanishi amekosana na Bw Odinga kwani wote wana haki ya kuchukua misimamo tofauti kisiasa.

Alisema muafaka ulikuwa muhimu kutuliza taharuki nchini lakini haamini una uwezo wake kuleta mabadiliko ikizingatiwa kuwa Bw Odinga aliwahi kuchukua hatua sawa na hiyo wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 alipoungana na aliyekuwa rais Mwai Kibaki.

“Muafaka wa 2007/2008 ulitokana na wizi wa kura. Wakati huu pia ulitokana na uchaguzi tatanishi. Ni wazi katika ile miaka mitano changamoto iliyokuwepo haikutatuliwa. Sasa mwaka mmoja umekamilika na hatuoni kama kuna juhudi za kusuluhisha mizozo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,” akaeleza.

Kuhusu uchaguzi ujao wa 2022, Bw Mudavadi alisema si lazima aungwe mkono na Bw Odinga wala kinara mwingine yeyote wa NASA ili ashinde urais bali atajitahidi kushawishi wananchi kuhusu uwezo wake wa kuongoza taifa.

Kumekuwa na fununu kwamba vinara wa muungano huo walikubaliana kumuunga mkono Bw Odinga kwa msingi kuwa atamuunga mkono mmoja wao 2022, ingawa ODM husisitiza kitakuwa na mgombeaji wake wa urais.

Wabunge walalamikia kuachwa kwa mabwanyenye ndani ya Mau walalahoi wakifurushwa

Na Anita Chepkoech

WABUNGE wawili wa Jubilee wamelaumu serikali kwa kufurusha maskini kutoka Msitu wa Mau na kuwaacha mabwanyenye.

Mbunge wa Konoin Brighton Yegon na mwenzake Maalum Gideon Keter walisema mabwanyenye 25 walio na ushawishi serikalini wametengewa jumla ya hekta 500 ndani ya Msitu wa Mau na hawajaathiriwa na operesheni inayoendelea ya kuwafurusha wakaazi.

Wanasiasa hao walidai kuwa miongoni mwa mabwanyenye hao ambao wanaendelea kuendesha shughuli zao ni Seneta, aliyekuwa msaidizi wa rais na mbunge; ambao hawakuwataja.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika eneo la Mogogosiek, Konoin wakati wa uzinduzi wa tovuti ya eneobunge itakayotumika kuweka rekodi ya miradi inayoendeshwa na Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF).

“Operesheni ya kuhamisha watu kutoka Msitu wa Mau inaonekana kuwa na njama fiche ya kisiasa. Wamiliki wa mashamba makubwa ndani ya msitu hawajaguswa ilhali wamiliki wa mashamba madogo ambao ni maskini wanafurushwa,” akasema Bw Yegon.

Takribani watu 10,000 wamefurushwa kutoka Msitu wa Mau katika juhudi za kutaka kuokoa ekari 46,000 ambazo ni chanzo cha maji.

Bw Keter alisema kuwa kubatilishwa kwa baadhi ya hatimiliki za mashamba ni ishara kwamba serikali iliwahadaa hivyo maskini hawapaswi kuadhibiwa kutokana na uozo katika wizara ya Ardhi.

Atwoli akana kutoroka na mke wa watu

VICTOR OTIENO na PETER MBURU

KATIBU Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli amejitokeza kujibu uvumi uliotokea hivi majuzi kuwa alimnyanganya mwanamume mwingine mkewe, akisema kamwe hawezi kufanya hivyo.

Akizungumza mjini Kisumu jana, Bw Atwoli alipinga madai kuwa alitoroka na mke wa wenyewe (anayedaiwa kuwa msomaji wa habari za runinga), akisema alishauriwa na babake kutojihusisha na wake za watu.

Bw Atwoli alisema kabla ya kuoa mke mwingine, ni hulka yake kufika kwa wazazi na kutaka kujua ikiwa ameolewa ama yuko huru.

“Kuna mtu hivi majuzi alijaribu kuniharibia jina kuwa nilitoroka na mkewe, ni mwanaume mpumbavu wa aina gani, babangu alinishauri kuwa niwapo uhai nisicheze na wake za watu na hivyo siwezi kufanya hivyo,” akasema Bw Atwoli.

Katibu huyo alisema hata wake wengi aliooa hadi sasa, amekuwa akifuata taratibu zinazofaa kuhakikisha si wake wa wenyewe.

“Jamaa huyu hana akili timamu. Hata wake kadhaa nilio nao nimekuwa nikihakikisha kutoka kwa wazazi wao ikiwa wana wenyewe au la kabla sijawasilisha posa,” akasema Bw Atwoli.

Alisema kuwa babake alimshauri akitaka kuishi maisha marefu asiwahi kucheza na wake za watu.

Hii ilikuwa baada ya tetesi kuibuka kutoka kwa mwanasiasa kutoka eneo la Magharibi kuwa kiongozi huyo wa wafanyakazi alimnyanganya mke na kumtishia kumchukulia hatua kali.

 

Kimombo kilimpiga chenga mfanyakazi wetu, Chandarana yajitetea

Na BRIAN OKINDA

WAMILIKI wa maduka ya Chandarana Foodplus yanayokabiliwa na madai ya kueneza chuki na ubaguzi wa rangi wanadai mfanyikazi aliyeandika baruapepe ya kubagua Wakenya, Rima Patel, hajulikani aliko.

Duka hilo pia limelaumu idara inayodhibiti mawasiliano na taarifa zinazotolewa kwa umma kwa kashfa hiyo.

Meneja Msimamizi wa Duka hilo Hanif Rajan aliyekuwa akihojiwa na Tume ya Utangamano (NCIC), alishikilia kuwa mfanyakazi huyo aliajiriwa hivi majuzi na hakuwa na ufahamu wa kutosha wa lugha ya Kiingereza.

“Kufikia sasa hatujui alipoenda kwani alitoweka mara tu baada ya kuandika baruapepe iliyoshutumiwa kote nchini. Hajafika kazini tangu Julai 27 aliposikia kwamba tulilenga kumwadhibu,” akasema Bw Rajan.

Meneja huyo alisema Bi Patel alitoka India na alikuwa amepewa kandarasi ya kufanyia kazi duka hilo kwa kipindi cha miezi mitatu na mkataba ulifikia kikomo Agosti 6.

“Tumetoa taarifa kumhusu kwa maafisa wa uchunguzi ili waweze kubaini alipo,” akasema.

Mkurugenzi wa Idara ya Malalamishi na Masuala ya Sheria wa NCIC, Kyalo Mwengi, alisema tume hiyo imeanzisha uchunguzi ili kubaini kiini cha baruapepe ya ubaguzi wa rangi ambayo iliwakera Wakenya.

“Huku tukiendelea kumsaka mfanyakazi huyo, tunafanya uchunguzi pia kubaini ikiwa ni sera ya duka hilo kuwatunuku wateja kwa misingi ya rangi yao,” akasema Bw Mwengi.

Matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo ndiyo yataamua ikiwa mfanyakazi huyo alikiuka sheria au alikuwa mfichuzi aliyeweka wazi uozo wa duka hilo.

Dereva wa lori lililoua wanafunzi 10 akana mashtaka

BONIFACE MWANIKI na KITAVI MUTUA

DEREVA wa lori lililosababisha ajali iliyoua wanafunzi 10 wa Shule ya msingi ya Mt. Gabriel mjini Mwingi, Jumatatu alifunguliwa mashtaka tisa ya kusababisha kifo kwa uendeshaji mbaya wa gari.

Abdalla Hassan ndiye aliyekuwa akiendesha lori lilipogongana na gari la shule ya upili ya Nguutani, waliokuwa wametoka ziara ya kimasomo mjini Mombasa.

Hassan alikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu wa Mwingi, Kibet Sambu, na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini sawa na kiasi kama hicho.

Kesi hiyo itasikizwa Agosti 20, 2018.

Kwingineko, wanafunzi watatu na mlezi wao jana walikuwa wakitibiwa katika hospitali ya Mwingi Level Five.

Msimamisi wa Matibabu katika hospitali hiyo, Dkt Evans Mumo, alisema hali za wanafunzi hao zimeimarika, ingawa bado wanahitaji kufuatiliwa kiafya kwa karibu.

Wawili kati yao walipelekwa katika chumba cha upasuaji ili kurekebisha miguu yao iliyovunjika, huku wa tatu akipangiwa kufanyiwa upasuaji maalumu. Atafanywa upasuaji huo na madaktari wa Cuba ambao walitumwa kuhudumu katika Kaunti ya Kitui.

“Wanafunzi hao hawamo hatarini, ingawa bado wamelazwa katika wadi zetu. Wamefanyiwa matibabu maalum ili kurekebisha hali zao, hasa miguu yao iliyovunjika,” akasema Dkt Mumo.

Hospitali hiyo pia inajitayarisha kufanya upasuaji kwa miili ya wanafunzi wanane ambao walifariki papo hapo kwenye ajali hiyo. Mwili wa mwanafunzi aliyefariki katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na mwili wake kurudishwa Mwingi pia utafanyiwa upasuaji.

Waziri wa Afya katika kaunti hiyo Dkt Richard Muthoka alisema upasuaji huo utasaidia katika utambuzi wa miili hiyo kabla ya kukabidhiwa kwa wazazi.

Waziri alisema kaunti hiyo iliwaondolea gharama zote, zikiwemo ada za mochari na upasuaji. Serikali pia itawasaidia katika mipango ya mazishi.

Mkuu wa Dayosisi ya Katoliki ya Kituo Kaasisi Joseph Mwongela alisema kanisa hilo litafanya misa ya wafu kesho kwa wanafunzi 10 ambao walifariki katika ajali hiyo.

“Tumeanza mipango ya mazishi, ambapo kanisa, shule na wadau wengine watakusanyika shuleni kwa maombi maalum baada ya hospitali kumaliza upasuaji na utambuzi wa miili kumalizika,” akasema kasisi huyo.

Mshauri wa Raila, Silas Jakakimba asakwa Zimbabwe kwa ‘kuchochea ghasia’

VALENTINE OBARA na BARACK ODUOR

POLISI wa Zimbabwe wanamtafuta msaidizi wa Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, kwa madai kuwa alichochea ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa urais nchini humo wiki iliyopita.

Mashirika ya habari Zimbabwe yalimnukuu Msemaji Mkuu wa polisi, Bi Charity Charamba, akisema wanataka kumhoji Bw Silas Jakakimba kuhusiana na ghasia hizo zilizotokea wakati upande wa upinzani ulipinga matokeo ya uchaguzi.

Katika uchaguzi huo, Rais Emmerson Mnangagwa wa chama cha ZANU-PF alitangazwa mshindi dhidi ya Bw Nelson Chamisa wa chama pinzani cha Movement for Democratic Change (MDC).

“Wananchi wanaojua aliko wanaombwa kuwasiliana na idara ya upelelezi wa jinai au kuripoti kwa kituo chochote cha polisi kilicho karibu nao,” akasema Bi Charamba.

Bw Jakakimba ni mmoja wa wandani wa kisiasa wa Bw Odinga na amekuwa akiandamana naye kwa ziara mbalimbali zikiwemo za mataifa ya kigeni mbali na kuwa kati ya wanaompangia kigogo huyo wa kisiasa mikakati yake.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Jakakimba alithibitisha aliwahi kuhudhuria mkutano wa hadhara wa MDC wakati wa kampeni lakini hakuwa mpangaji mikakati wa chama hicho wala wa Bw Chamisa.

Katika mkutano huo wa hadhara uliokuwa wa mwisho jijini Harare, Bw Chamisa alimtambulisha kama mwakilishi wa Bw Odinga ambaye chama chake cha ODM kimekuwa mshirika wa karibu wa MDC kwa miaka mingi.

Akizungumza kutoka bomani kwake katika kijiji cha Kakimba, Kisiwa cha Mfangano, Kaunti ya Homa Bay, alisema alikuwa Harare kwa siku tatu akaondoka Jumanne iliyopita na kurejea Nairobi kabla ghasia zianze kushuhudiwa Zimbabwe.

“Nilipotoka Harare hali ilikuwa tulivu na shughuli zilikuwa zikiendelea kama kawaida,” akasema.

Chama cha MDC kilipinga matokeo ya uchaguzi wa urais na kudai kulikuwa na ulaghai.

Kabla tume ya uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo, wagombeaji hao wawili walikuwa kila mmoja akitangaza kuongoza kwa idadi ya kura na hali hii ilisababisha taharuki nchini humo.

Ilibidi wanajeshi na polisi kutumiwa kutawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakiandamana na watu kadha wakauawa kwenye makabiliano hayo.

TUNARUDI TENA CHAMA KIMOJA? Demokrasia hatarini

Na BENSON MATHEKA

Kenya inarejea taratibu katika utawala wa chama kimoja kufuatia matukio ya hivi majuzi ya wanasiasa kujiunga na Serikali.

Dalili zaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka minne ijayo, kuna hatari ya kurudisha nyuma maendeleo ya demokrasia ya vyama vingi ambayo Wakenya wamekuwa wakifurahia kwa miaka 26 iliyopita.

Tangu Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga asalimiane na Rais Uhuru Kenyatta, wanasiasa wa upinzani wamefuata nyayo na kukubali kuunga serikali ya Jubilee.

Siku mbili kabla ya muafaka wa Rais Kenyatta na Raila, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye ni mwandani wa Rais, alibashiri kuwa Kenya itakuwa chini ya utawala wa chama kimoja kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Kufikia Desemba 2018, Kenya itakuwa demokrasia ya chama kimoja,” aliandika Bw Kuria kwenye ukurasa wake wa Facebook bila kufafanua.

Hali hiyo inaendelea kujitokeza na kufikia wakati huo, vyama vikubwa vya kisiasa vitakuwa kwa jina tu bila uwezo wa kukosoa serikali kama ilivyo katika nchi za Rwanda na Uganda.

Japo viongozi wa vyama hivyo wanasisitiza wangali katika upinzani na wanachounga ni vita dhidi ya ufisadi na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo pekee, dalili ni wazi kuwa wanaelekea serikalini.

Raila mwenyewe amekoma kukosoa serikali na amenukuliwa akisema ni kwa sababu anawasiliana moja kwa moja na Rais Kenyatta. Wabunge wa chama chake cha ODM wamechukua misimamo ndani ya chama cha Jubilee, baadhi wakimuunga Rais Kenyatta na wengine wakimuunga Naibu Rais William Ruto.

Chama cha Wiper ambacho pamoja na ODM, Ford Kenya na Amani National Congress vinaunda muungano wa upinzani wa NASA, pia kimetangaza kushirikiana na serikali na kuna fununu kwamba huenda kiongozi wake Kalonzo Musyoka akapatiwa wadhifa mkubwa serikalini.

Baada ya Wiper kutangaza kuwa kitashirikiana na serikali, kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani, hatua ambayo wadadisi wanasema ni kejeli.

“Wetangula amekaribia serikali kama vinara wenzake katika NASA. Tofauti yake na Bw Odinga na Bw Musyoka ni kuwa, anaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto katika chama cha Jubilee,” alisema mbunge mmoja kutoka Rift Valley ambaye hakutaka kutajwa jina.

Siku tatu baada ya Wiper kutangaza kuwa kitashirikiana na serikali, Bw Musyoka alimwalika Bw Wetangula katika kilichotajwa kama juhudi za kumshawishi kufuata nyayo za vinara wenzake.

Duru zinasema kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi huenda akapatiwa wadhifa mkubwa serikalini hatua ambayo huenda ikamvuta Wetangula upande wake iwapo juhudi za kuunganisha vyama vyao zitafaulu.

Bw Mudavadi amekubali kuunga vita dhidi ya ufisadi na Ajenda Nne za Maendeleo za Serikali ya Jubilee na iwapo atapatiwa wadhifa serikali hataweza kukosoa serikali.

Kulingana na Profesa David Monda wa City University, New York kurejea kwa utawala wa chama kimoja kwa hali yoyote ni hatari.

“Ni suluhu mbadala na hatari kwa tofauti za kisiasa Kenya,” asema.

Wachumba wamwagiwa kinyesi kwa kula uroda nje ya ndoa

Na MASHIRIKA

LANGSA, INDONESIA

WAPENZI wawili walimwagiwa kinyesi kwa kudaiwa kushiriki ngono nje ya ndoa zao katika eneo la Langsa, Indonesia.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha umati wa watu ukiwavuruta mwanamume na mwanamke wanaoonekana kuwa wenye miaka ya thelathini na kuwapeleka kando ya shimo la maji taka.

Walikalishwa hapo kisha umati ukaleta ndoo ambazo zilitumiwa kuchota maji hayo yenye uchafu wa kila aina ikiwemo kinyesi, na kuwamwagia vichwani na mwilini.

Nchini humo wakazi wengi hufuata sheria za Kiislamu na hivyo basi ni haramu kwa watu kutenda ngono nje ya ndoa.

Ripoti za habari zilisema mwanamume huyo ni mkubwa wa idara ya kiserikali na mwanamke husika ni mwajiriwa wake.

Ilidaiwa mwanamume huyo alikuwa akienda nyumbani kwa mwanamke mara kwa mara, na wakazi waliwachunguza mienendo yao kwa muda kabla kuwanasa.

Ilisemekana wawili hao walijitetea na kusema walioana kwa njia ya kidini lakini umati ukaendelea kuwaadhibu.

Walichukuliwa na polisi baadaye ambao walinukuliwa kusema watafanya uchunguzi zaidi na ikiwa itabainishwa kwamba cheti chao cha ndoa ni feki, huenda wakaadhibiwa kisheria kwa kuchapwa mijeledi hadharani.

-Imekusanywa na Valentine Obara

Alilamba vya pembeni, sasa hana ‘transfoma’ baada ya mke kuikata kwa makasi

Na MASHIRIKA

FENGCHENG, UCHINA

MWANAMUME anauguza majeraha mabaya baada ya mke wake kumkata uume wake.

Inasemekana mwanamke huyo alishuku mume wake ana mpenzi wa kando ndiposa akachukua makasi na kumkata uume.

Kulingana na mashirika ya habari Uchina, mwanamume huyo alikuwa akipiga mswaki wakati mke wake alipomshambulia ghafla. Walikuwa wamebishana awali lakini hakujua mke wake alikuwa bado ana hasira.

Duru katika hospitali ambako mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Li alillazwa zilisema alifikishwa huko akivuja damu jingi.

Mashirika ya habari yalimnukuu akisema kuwa mke wake alikuwa akimshuku sana.

Ilidaiwa alisema mke wake alimpiga marufuku kuzungumza na rafiki yeyote wa kike wala hata kutabasamu na mwanamke kwa mbali.

Ingawa wamekuwa wakibishana mara kwa mara, hakutarajia kuna siku ingefika ambapo mke wake angemkata uume wake.

Madaktari walinukuliwa kusema alifanyiwa upasuaji wa dharura kuokoa maisha yake lakini hawezi kuhakikishiwa atarejelea hali yake ya kawaida ya udume atakapopata nafuu.

-Imekusanywa na Valentine Obara

Wanandoa wanyweshwa mkojo kwa kuoana kisiri

Na MASHIRIKA

MADHYA PRADESH, INDIA

MWANAMUME na mke wake walitekwa nyara wakapigwa na kulazimishwa kunywa mkojo na familia ya mke huyo ambayo ilidai aliolewa bila idhini yao.

Ripoti zinasema mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 23 alifugwa kwenye mlingoti na kutandikwa huku mke wake, 21, akivuliwa nguo na kunyolewa nywele kisha wakalazimishwa kunywa mkojo.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha kisa hicho ambacho kilithibitishwa kilitendeka katika eneo la Alirajpur, Madhya Pradesh, India.

Ilisemekana wawili hao waliishi katika kijiji kimoja ndipo wakaoana Mei mwaka huu ilhali familia ya mke ilikuwa haijaidhinisha ndoa hiyo.

Kulingana na mashirika ya habari, mwanamume huyo alijitahidi kuwaomba waruhusu waoane na hata akalipa mahari ya mbuzi wawili na pesa lakini wapi!

Iliwabidi waoane kisiri kisha wakahama kijiji hicho lakini walipoenda kutembelea jamaa zao hivi majuzi, walishikiwa bunduki na kutekwa nyara kisha wakapigwa na kuaibishwa hadharani.

Polisi walinukuliwa kusema walitekwa nyara katika nyumba ambako walikuwa wakiishi wakati huo.

Wahusika kadhaa walikamatwa kwa kuhusika katika kisa hicho.

-Imekusanywa na Valentine Obara

Kocha asifu vijana wake kuandaa gozi kama alivyowaagiza

NA CECIL ODONGO

KOCHA wa Zoo Kericho FC Sammy Okoth amewamiminia  sifa kocho kocho wachezaji wake kwa kusakata gozi kulingana na maagizo yake kwenye ushindi wa 2-1 walioutwaa dhidi ya Kariobangi Sharks katika mechi ya KPL Jumapili Agosti 5 ugani Camp Toyoyo, jijini Nairobi.

Kulingna na mnoaji huyo, kikosi chake kilitumia mbinu za kipekee kuangusha Sharks baada ya kusoma mtindo wao wa uchezaji katika mechi zao za nyuma.

“Kipindi cha kwanza kilikuwa chenye kasi sana  na walituzidi mbio. Hata hivyo tuliweza kudhibiti kasi yao katika kipindi cha pili na wanasoka wangu walitii agizo la kumiliki mpira na kupunguza kasi yao,” akasema Okoth baada ya ushindi huo.

Kocha huyo katika sifa zake hakumsaza mastraika wake ambao walizidisha mashambulizi ya kuvizia langoni mwa wapinzani  huku ushindi huo ukizidi  kuwasongesha mbali  na eneo la hatari la kushushwa daraja.

Hata hivyo mkufunzi huyo alisikitikia hatua ya difenda wake Earnest Kipkoech kulishwa kadi mbili za manjano kisha kutimuliwa kwa kadi nyekundu na akadai kwamba hatua hiyo huenda ikaiponza timu katika mechi zao mbili zijazo.

“Ni pigo kubwa kwetu kwa kuwa Kipkoech alikuwa akicheza katika nafasi ya Nicholas Kipkurui ambaye pia anatumikia marufuku ya mechi mbili. Alikuwa ameimarika sana lakini tuna wingu la matumaini kwamba atakawajibikia nafasi hiyo atang’aa jinsi wawili hao walivyofanya,” akaongeza Okoth.

Baada ya ushindi huo, Zoo Kericho sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 29 baada ya kujibwaga uwanjani mara 25.

Zoo Kericho watakuwa wenyeji wa Nzoia Sugar katika mechi yao ya Agosti 11 itakayogaragazwa Kericho Green Stadium, Kaunti ya Kericho.

Binti gaidi mwenye umri mdogo zaidi duniani atupwa jela maisha

Na MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

LONDON, Uingereza

GAIDI wa kike mwenye umri mdogo zaidi duniani, ambaye ni mwanachama wa kundi moja la kigaidi nchini Uingereza Ijumaa alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kupanga mashambilio London, mnamo 2017.

Polisi walisema kuwa Safaa Boular, 18,  alishirikiana na mamake pamoja na dadake kutekeleza uhalifu huo baada ya juhudi zake za kujiunga na kundi la kigaidi la Islamic State (IS) nchini Syria kutibuliwa.

“Wanawake hao watatu walijawa na chuki na itikadi mbaya na walikuwa wanapanga kutelekeza shambulio la kigaidi,” Naibu Kamishna wa polisi Dean Haydon, ambaye pia ni mshirikishi wa kikosi cha kupambana na ugaidi, alisema.

“Kama wangefauli, wangewaua watu wengi na wengine wengi wakijeruhiwa,” akaongeza kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Maafisa wa upelelezi walinakili mawasiliano ya simu kati ya watatu hao ambapo ilibainika kuwa wapanga kuandaa “karamu” baada ya kufanikisha mipango yao.

Wapelelezi hao waliwafuata  huku wakizunguka katika barabara za London mnamo Aprili 2017, katika kile maafisa wa polisi wanaamini ilikuwa ni ziara yao ya kutambua vituo ambavyo wangeshambulia.

Siku iliyofuata walienda kwa duka moja la Supermarket katika eneo la Wandsworth, kusini magharibi mwa London ambapo walinunua paketi yenye visu vya jikoni.

Miezi miwili baadaye, dadake Boular, Rizlaine Boular, 22, alifungwa maisha pamoja na kifungo kisichoweza kukatiwa rufaa cha miaka 16 katika jela Old Bailey.

Mamake, Dina Dich, 44, alipewa kifungu cha miaka 11 na miezi tisa gerezani, adhabu ambayo hangeweza kukata rufaa dhidi yake. Hii ni kando na kifungo cha maisha.

Lucy Wangui agunduliwa kuwa mtumizi sugu wa pufya

Na GEOFFREY ANENE

ZIMWI la wanariadha kutumia njia ya mkato kutafuta ufanisi mashindanoni linazidi kuandama Kenya baada ya Lucy Wangui Kabuu kuwa mkimbiaji wa hivi punde kufeli vipimo vya dawa zilizoharamishwa.

Bingwa huyu Jumuiya ya Madola wa mbio za mita 10,000 mwaka 2006 amepatikana na kosa la matumizi ya pufya katika mbio za Milano Marathon alizoshinda nchini Italia mwezi Aprili mwaka 2018. Alipimwa wakati wa mbio hizo na matokeo tayari yamefikishwa kwake.

Mzawa huyu wa mwaka 1984 hakuwa amepata ushindi mkubwa kama huo wa Milano Marathon katika mbio za kilomita 42 katika historia yake. Alinyakua taji la Milano miezi miwili baada ya kupona jeraha. Aliwahi kushinda mbio za kilomita 21 za Delhi Half Marathon nchini India mwaka 2011, Ras Al Khaimah Half Marathon nchini Milki za Kiarabu (2013) na Great North Run nchini Uingereza (2011).

Kenya, ambayo ilishuhudia karibu visa 50 kati ya mwaka 2012 na 2016, iliingia kwenye orodha ya mataifa yanayotenda uovu huu sana ya Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli (WADA) mnamo Mei 12 mwaka 2016. Bado inakabiliwa na tishio la kupigwa marufuku kushiriki mashindano kimataifa kama Urusi.

Kisa cha Kabuu kinawasili wiki chache baada ya wakimbiaji wengine watajika kutoka Kenya, Asbel Kiprop (mita 1,500) na Boniface Mweresa (mita 400) kupatikana watumiaji wa dawa hizo haramu. Kutokana na uhalifu huu, Kiprop, Mweresa na Kabuu wanakabiliwa na marufuku ya miaka minne kutoka kwa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

Barcelona, PSG na Juventus kivumbini kumsajili Pogba

Na MASHIRIKA

Tetesi zinadai kwamba kiungo mbunifu Paul Pogba anang’ang’aniwa na klabu za Barcelona, Paris Saint-Germain (PSG) na timu yake ya zamani Juventus.

Wakala wa Mfaransa huyu wa Manchester United anatarajiwa kuwasili uwanjani Old Trafford juma hili kwa mazungumzo muhimu kuhusu hali yake.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinasema Mino Raiola ataeleza United kwamba anaweza kufanikisha mpango wa uhamisho hadi Barcelona wa Sh13 bilioni.

Juventus na PSG pia zimehusishwa na nyota huyu aliyetua United kwa Sh11.6 bilioni kutoka Juventus mwaka 2016.

Maisha ya baadaye ya Pogba, 25, uwanjani Old Trafford yamekuwa ya wasiwasi kutokana na uhusiano wake na kocha mkuu Jose Mourinho kuzorota. Pogba anasalia na miaka mitatu kwenye kandarasi yake na United.

Raiola pia anawakilisha kiungo Mwitaliano Marco Verratti, ambaye wakati mmoja United ilivutiwa naye sana.

Huku kipindi kirefu cha uhamisho kikiratibiwa kufungwa Agosti 9, huenda watu wakashuhudia Pogba akielekea Barca katika mpango wa kubadilishana wachezaji utakaohusisha raia wa Colombia Yerry Mina kuhamia Old Trafford kutoka Camp Nou. United inamezea mate Mina, ambaye bei yake ni Sh4.5 bilioni.

Chelsea sasa yataka usogora wa Ramsey

Na AFP

CHELSEA iko tayari kuipiku Liverpool katika juhudi za kupata huduma za mchezaji wa Arsenal, Aaron Ramsey kabla ya soko kufungwa Agosti 9 kwa kutoa Sh4.5 bilioni.


Kiungo huyu kutoka Wales yuko katika mwaka wa mwisho kwenye kandarasi yake na Arsenal iko tayari kupata fedha za kujiimarisha kwa kumuuza.


Gumzo linadai kwamba kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri amekubali hawezi kupata sahihi ya mchezaji wa Aston Villa, Jack Grealish, ambaye ataelekea Tottenham, ikifanikiwa kumshawishi, ili ashiriki Klabu Bingwa Ulaya.


Sarri, ambaye hakuweza kunyakua wachezaji kadhaa aliotaka kutoka Italia, atamgeukia Ramsey, ambaye hajaongeza kandarasi yake ugani Emirates.

Nusra afutwe kazi kwa kuonja mlo wa mdosi

Na DENNIS SINYO

POLO mwenye tabia ya kuonjaonja chakula cha bosi wake, alijipata pabaya baada ya kupatikana peupe akiteremsha mchuzi wa nyama uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya mwajiri wake.

Jamaa huyo ambaye si mpishi, alikuwa na mazoea ya kuingia jikoni saa saba mchana kila siku.

Inasemekana alikuwa akitumia nafasi hiyo kuwachenga wapishi ili kupata nafasi ya kuonja mapochopocho wanayopikia mkubwa wa kampuni iliyokuwa imemwajiri.

Licha ya kupewa onyo mara kadhaa, jamaa hakukoma kabisa kuingia jikoni. Tabia hiyo iliwakera wapishi ambao waliamua kumripoti kwa msimamizi wao ili achukuliwe hatua kali kwani alikuwa amevuka mipaka.

Inasemekana kwamba jamaa huyo aliwekewa mtego bila kujua.

“Mdosi alikuwa amewaambia wapishi wamfahamishe punde tu baada ya jamaa kuingia jikoni. Jamaa alipokuwa akionja chakula ilivyokuwa kawaida yake, mdosi alidunda jikoni na kumfumania peupe,” alisema mdokezi.

Kalameni hakuamini macho yake alipomuona mdosi akimtazama kwa jicho la hasira.

“Kumbe ni ukweli unaonja chakula changu? Unajua kuwa kosa hilo linaweza kukufanya upoteze kazi yako?’’ alifoka mdosi.

Swali hilo lilimfanya jamaa kuishiwa na nguvu na kubakia mdomo wazi. Alilazimishwa kutafuna chakula chote wafanyikazi wengine wakimtazama kwa mshangao.

“Jamaa alishindwa kula chakula hicho na badala yake akapiga magoti kuomba msamaha kwa kosa hilo.

Mdosi wake alisema alikuwa amechoshwa na tabia ya jamaa akisema ilikuwa kinyume na kanuni za kampuni. “Tabia hii haikubaliwi katika kampuni yetu na sitaki kuona tena tukio hilo,” alichemka mdosi.

Jamaa aliinuka na kuondoka jikoni asiamini kwamba ulafi wake nusura umfanye amwage unga. Aliapa kutoingia jikoni tena huku wapishi wakipewa onyo la kutoruhusu yeyote kuingia humo kwa mara nyingine.

WASONGA: TSC, walimu waelewane kukomesha mgomo shuleni

Na CHARLES WASONGA

SHULE zilifungwa wiki iliyopita baada ya kukamilika kwa muhula wa pili ulioshuhudia visa vingi vya utovu wa nidhamu, hasa katika shule za upili.

Shule kadhaa zilifungwa, kwa muda, baada ya wanafunzi kuteketeza mabweni yao, kama hatua ya kutuliza hali. Hii ina maana mkondo wa masomo katika shule uliathirika kiasi kwamba baadhi ya walimu hawakuweza kukamilisha silabasi inavyopasa.

Kwa hivyo, muhula wa tatu utakapoanza mapema Septemba, walimu watakuwa mbioni kuwaanda watahiniwa kwa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) na kidato cha nne (KCSE) itakayoanza mwishoni mwa Oktoba.

Hii ndio maana ni muhimu kwa serikali, Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) na vyama vya kutetea masilahi ya walimu (Knut na Kuppet) kuzungumza na kuelewana kwa lengo la kukomesha mgomo ambao umeitishwa mapema mwezi ujao.

Walimu, kupitia vyama hivyo, wametangaza kuwa watagoma kuanzia Septemba mosi ikiwa TSC haitatimiza matakwa kadhaa waliyowasilisha, kama vile, kusitishwa kwa uhamisho wa walimu na utathmini wa utendakazi wao.

Vile vile, walimu wanataka wenzao waliopanda ngazi kimasomo wapandishwe vyeo, pendekezo ambalo TSC imepinga.

Mapema mwaka huu vigogo wa kisiasa nchini, Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, walionyesha mfano mzuri wa kumaliza tofauti kati yao kwa kuketi katika meza ya mazungumzo, hatua iliyomaliza joto la kisiasa nchini.

Wawili hao waliweka kando tofauti zao za kisiasa kwa manufaa ya Wakenya milioni 45 ambao waliathirika pakubwa kufuatia ghasia zilizoshuhudiwa maeneo kadha nchini.

Sasa taifa linavuna matunda ya muafaka kati ya Uhuru na Odinga kwani sekta mbalimbali za kiuchumi, mathalan utalii, zimeanza kuimaika huku vita dhidi ya ufisadi vikiendeshwa kwa kasi.

Kwa mantiki hiyo hiyo, TSC inafaa kuzungumza na vingozi wa Knut na Kuppet ili kuzuia mgomo wa walimu ambao huenda ukatatiza masomo na mitihani ya KCPE na KSCE.

Endapo walimu watatekeleza tishio lao bila shaka watakaoathirika moja kwa moja ni watahiniwa kwani maandalizi yao yatavurugika. Matokeo ya hali hii ni kwamba wanafunzi wataandikisha matokeo duni hali ambayo, bila shaka, itaathiri mustakabali wao.

Aidha, huenda ratiba ya mitihani hiyo ikabadilishwa, hatua ambayo itaigharimu serikali na wazazi fedha zaidi.

Kwa hivyo, Wizara ya Leba inapasa kuingilia kati vuta nikuvute hii katika ya TSC na walimu kwa lengo la kuzima mgomo.

Waziri Ukur Yattani anafaa kuitisha mkutano wa pamoja ya viongozi wa Knut na Kuppet na maafisa wa TSC ili kutatua tofauti kati yao kwa manufaa ya wanafunzi.

Wahusika katika suala hili waige mfano wa Rais Kenyatta na Odinga ili kuleta utulivu katika sekta ya elimu.

cwasonga@ke.nationmedia.com

OBARA: Twahitaji muujiza wa pili ili mwafaka ufanikiwe

Na VALENTINE OBARA

Baada ya kusubiri kwa miezi mitano, hatimaye mojawapo ya malengo makuu ya muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga imeanza kutekelezwa.

Kamati maalum iliyobuniwa na wawili hao tayari imetoa wito kwa wananchi kuwasilisha maoni yao kuhusu jinsi ya kupambana na ufisadi.

Ingawa hii ni hatua bora katika kuendeleza mbele malengo ya muafaka huo, kuna wasiwasi kwamba kamati hii huenda ikaishia tu kuwa kama zingine nyingi ambazo zimewahi kuwepo katika miaka iliyopita.

Kenya imekuwa maarufu kwa uundaji wa kamati na majopokazi chungu nzima kila mara tunapokumbwa na changamoto mbalimbali lakini kinachosikitisha ni kuwa, ripoti zinazotolea huwa hazitekelezwi.

Hii ni licha ya kuwa kamati hizo hutumia rasilimali za umma kuendeleza shughuli zao ikiwemo kutumia fedha zinazotoka katika kapu linalofadhiliwa na mlipaushuru.

Hakika, masuala mengi ambayo Bw Odinga na Rais Kenyatta walitaja kuwa changamoto wanazolenga kutatua yamewahi kuchunguzwa.

Mfano ni suala kuhusu utendaji wa haki sawa kwa kila mwananchi bila kujali kabila, tabaka wala misimamo ya kisiasa.

Hili ni jambo ambalo lilichunguzwa kwa kina mno na Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ambayo ilitumia muda na rasilimali tele za umma kuzunguka nchini kote kushauriana na wananchi.

Tume hiyo ilikusanya malalamishi na maoni ya Wakenya hasa kutoka jamii zilizokuwa zimekandamizwa kihaki katika tawala zilizopita.

Utoaji wa ripoti ya tume hiyo ulikumbwa na utata kwa kuwa ilitoa mapendekezo yaliyoshutumu watu mashuhuri nchini kwa kudhulumu haki za raia wa kawaida.

Hatimaye ripoti ilipotolewa, kulikuwa na minong’ono kwamba haikuwa ripoti halisi bali ilifanyiwa ukarabati. Hata hivyo, ripoti hiyo iliyotolewa haijatekelezwa kufikia sasa.

Masuala mengine mengi ambayo yamewahi kuchunguzwa na kamati tofauti ni kuhusu mauaji ya kikatili ya raia na pia ya viongozi mashuhuri, mbali na suala sugu la unyakuzi wa ardhi.

Kwa mtazamo wangu, kamati iliyobuniwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga haingepoteza muda mwingi ila kurejelea ripoti hizo zote na kupendekeza kinachofaa kutekelezwa kutoka kwazo.

Kuna hatari ya kamati hii kutumia muda na rasilimali tele kisha mwishowe ije na mapendekezo yale yale ambayo yamewahi kuwasilishwa kwetu.

Wakifanya hivyo, natumai malaika aliyetenda muujiza wa kuwapatanisha viongozi hao wawili kisiasa atakuwa bado anatembeatembea humu nchini ili atende muujiza mwingine wa kufanya ripoti itakayotolewa itekelezwe kikamilifu.

Bila hilo, tujiandae tu kurudi uchaguzini 2022 tukiwa tungali tumebeba mzigo huu mzito wa matatizo ya ufisadi, ukiukaji wa haki za kibinadamu, dhuluma za kikabila miongoni mwa mengine.

Tuna nafasi bora ya kupata mabadiliko ambayo yatasaidia kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida lakini hilo litawezekana tu kama viongozi wetu watajitolea kuweka kando maslahi yao ya kibinafsi kwa muda.

TAHARIRI: Tusikubali madereva watumalizie watoto

NA MHARIRI

WANASEMA ajali haina kinga wala kafara, lakini kuna ajali ambazo zinaweza kuzuiwa kama tungekuwa makini na kuzingatia sheria.

Wakati aliyekuwa waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiangí alipoagiza mabasi ya shule yawe na rangi ya manjano, hekima iliyokuwepo ni kwamba wananchi wangeweza kutambua kwa urahisi magari hayo.

Wananchi wangejua kuwa mabasi yanabeba wanafunzi, na kwa hivyo wangelikuwa jicho la serikali kuhakikisha madereva hawakiuki kanuni za uchukuzi. Miongoni mwa kanuni hizo ni kupiga marufuku safari za usiku za magari ya kubeba wanafunzi.

Inasahangaza kwamba basi lililowabeba wanafunzi 50 wa wa Shule ya Msingi ya St Gabriel’s Mwingi lilihusika kwenye ajali mwendo was aa sita za usiku. Ikizingatiwa kuwa basi hilo lilitoka Mombasa asubuhi, ina maana kuwa dereva alikiuka kanuni na kuendelea na safari hata baada ya muda unaoruhusiwa.

Isitoshe, dereva wa trela lililokwaruza basi hilo ubavuni na kuliangusha kwenye mto Kanginga, alijawa na ubinafsi na kuamua kulipita basi kwenye daraja.

Kanuni za udereva ziko wazi – kwamba yeyote anayeendesha gari, pikipiki au hata baiskeli, haruhusiwi kumpita mwenzake wanayeelekea upande mmoja iwapo; kuna ukungu na mtu hawezi kuona vyema, kuna kona, kwenye daraja, penye mteremko au mlima na kadhalika.

Kwa kulipita basi kwenye daraja jembamba, inaonyesha dereva wa trela alikuwa na nia ya kukiuka kanuni zote za udereva kwa kuwa alikuwa maeneo ya mashambani.

Kutoroka baada ya ajali hiyo, kunatia hasira kwamba mtu anaweza kugonga gari lenye watoto bila ya kujali maisha ya watoto hao.

Ajali ya jana ambayo tukienda mitamboni ilikuwa imeua watoto 11, inatupatia tahadhari Wakenya tuwe macho na kuwazuia madereva wasiojali kuwaua watoto wetu.

Likizo hii ndio wakati ambapo shule mbalimbali hufanya ziara za masomo katika kila pembe ya nchi. Je, ina maana kuwa watoto wetu wataendelea kufa barabarani eti kwa sababu kuna madereva wasiozingatia sheria? Je, madereva hao wataachwa tu waue wanavyotaka kwa kuwa hakuna mwenye akili timamu anayeweza kuwazuia?

Basi hilo la wanafunzi lilivuka vizuizi vingi barabarani kabla ya ajali hiyo. Hivi polisi wa trafiki wanafahamu kwamba kuna sheria inayokataza mabasi ya shule kusafiri usiku?

Walichukua hatua gani? Pole za wanasiasa na maonyo yao ni muhimu, lakini yafaa tuwe na mfumo unaojisimamia, usiosubiri ajali itokee ndipo kufanywe msako.

KURUNZI YA PWANI: Kampeni ya kuangamiza unywaji wa pombe haramu yaanza

Na HAMISI NGOWA

VIONGOZI wa kidini pamoja na mashirika ya kijamii kwa ushirikiano na maafisa wa utawala katika eneobunge la Likoni Kaunti ya Mombasa sasa wameanzisha mbinu mpya za kukabiliana na unywaji pombe haramu na utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana katika eneo hilo.

Mbinu hizo mpya ambazo wakazi wana imani kwamba zitasaidia kuangamiza ulevi wa pombe pamoja na utumizi wa bangi miongoni mwa vijana wa eneo hilo ni operesheni za ghafla za kuwanasa wauzaji na wagema wa pombe hizo.

Mwishoni mwa wiki, viongozi hao walizindua rasmi operesheni hiyo iliyopewa jina ‘maliza pombe haramu na bangi mitaani’ ambapo watu watatu walimakatwa pamoja na zaidi ya lita 200 za Chang’aa.

Viongozi hao aidha waliharibu kwa kuviteketeza kwa moto baadhi ya vifaa vilivyonaswa wakati wa operesheni hiyo ambavyo vinadaiwa kutumika katika shughuli za biashara hiyo.

Naibu Kamishna wa eneo hilo Bw Erick wa Mlevu ambaye aliongoza opereresheni hiyo,alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao huku akiwaonya maafisa wa polisi dhidi ya kuwaalichia kwa njia zisizoeleweka.

Bw Wamlevu alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote wa serikali katika eneo hilo atakayepatikana akijihusisha kwa njia yoyote ile ya kujaribu kuwahifadhi wauzaji pombe haramu, bangi pamoja na dawa za kulevya.

“Nataka kuwaambia kwamba mkiona afisa yoyote wa serikali akichukuwa bahasha kwa hawa watu wanaoangamiza vijana wenu kwa kuwauzia vileo, tafadhalini tumieni simu zenu kuwapiga picha na mniletee ili niwe na ushahidi wa kutosha wa kuwaadhibu,’’ akasema.

Walemavu aidha aliwashukuru viongozi hao kwa kujitolea na kuahidi kwamba serikali itaendelea kushirikiana nao katika vita hivyo kwa lengo la kuwanusuru vijana.

Alidokeza kwamba operesheni hiyo itakuwa ikifanyika kila wiki hadi maskani zote zinazotumiwa kwa shughuli hiyo haramu zitakapoangamizwa.

Naye mwenyekiti wa Baraza la walimu wa kiislamu eneo hilo Ustadhi Suleiman Kilembi alisema japo opereresheni hiyo ilianza dhidi ya wauzaji wa pombe haramu,pia itawaandama na wale wanaouza bangi na dawa za kulevya. Aliihimiza jamii kuunga mkono juhudi za viongozi hao ili kuhakikisha wanaojihusisha na biashara hiyo wanakamatwa na kukumbana na mkono wa sheria.

“Sisi kama viongozi wa kidini tumesema imetosha na kwamba sasa hatutakaa kimya tukiangalia watu wachache wakiangamiza vizazi vyetu.Tutawasaka popote walipo hadi tuwaondoe,’’ akasisitiza.

Lakini kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika la Coast People Struggle For Human Rights, Bw Hamisi Mifale aliitaka serikali kutowapa msamaha wala dhamana watu wanaotuhumiwa kwa ulanguzi wa mihadarati.

Alisema hukumu kali zinafaa kuwekwa kwa wanaopatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya ikiwemo kifungo cha maisha gerezani ili kuwa mfano kwa wengine.

Alisema miaka mitatu iliyopita,wakazi wa eneo hilo walianzisha vita vikali dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya lakini juhudi hizo zikalemazwa na hatua ya kupewa msamaha kwa baadhi ya washukiwa wakuu wa ulanguzi wa dawa za kulevya eneo hilo.

“Changamoto kubwa ilioko ni sheria na hukumu ndogo inayopewa walanguzi wa dawa za kulevya, nadhani kuna haja kwa wabunge kuipiga msasa ili wanaopatikana na hatia ya ulanguzi wa mihadarati wawe wanapewa hukumu kali zaidi,’’ akasema.

Pombe imezuia vijana kuzaa – Gavana Kahiga

Na Stephen Munyiri

GAVANA wa Nyeri, Bw Mutahi Kahiga, amedai upungufu wa watoto wanaojiunga na shule za chekechea umetokana na ulevi wa vijana katika kaunti hiyo.

Bw Kahiga alisema mwaka huu serikali yake iliajiri walimu zaidi ya 700 wa chekechea lakini kuna wasiwasi kwamba idadi ya watoto inapungua.

Akihutubia wananchi katika kituo cha basi cha Karatina baada ya kukagua ukarabati wa barabara, alidai wanaume wengi wamekosa nguvu za uzazi kwa sababu ya unywaji pombe kupindukia.

“Tumejenga shule tukaajiri walimu wa chekechea lakini inasikitisha kuwa hatuna watoto wa kutosha kwa sababu ya unywaji pombe kupindukia.

Hii inahuzunisha. Acheni kunywa pombe kupita kiasi na mzae watoto zaidi,” akasema na kuibua kicheko kutoka kwa umati uliokuwepo.

Bw Kahiga alitoa mfano wa mji wa Karatina ambapo kuna mabaa yanayofunguliwa hata saa mbili asubuhi akaonya kuwa serikali yake itafutilia mbali leseni zao.

Miezi miwili iliyopita, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alipozuru Karatina alionya maafisa wa utawala wa serikali eneo hilo ambao hufumbia macho biashara za pombe haramu na kuwaambia watafutwa kazi.

Mbunge apinga wazo la kuondoa shule za mabweni

Na MAGATI OBEBO

MBUNGE wa Bomachoge Chache, Bw Alfa Miruka, amepinga pendekezo la kufutilia mbali shule za mabweni nchini.

Badala yake, mbunge huyo ametoa wito kuwe na mashauriano yatakayolenga kukabiliana na migomo ya mara kwa mara na uharibifu wa mali unaosababishwa na watoto wa shule za upili.

Bw Miruka alisema shule za bweni hutoa mandhari bora kwa wanafunzi kuendeleza masomo yao ikilinganishwa na shule za kutwa.

“Uchomaji wa mabweni shuleni haifai kuwa sababu ya kutosha kuanzisha mdahalo kuhusu kugeuza shule za mabweni kuwa za kutwa. Badala yake inafaa tuhimize wazazi kuhusu umuhimu wa kuwafanya watoto wao wawe wenye adabu njema kabla wajiunge na shule hizi,” akasema Bw Miruka.

Alhamisi iliyopita, Waziri wa Elimu Amina Mohamed, alisema pendekezo hilo litaamuliwa na wadau katika sekta ya elimu.

Waziri huyo alisema Kenya ni miongoni mwa mataifa machache katika ukanda huu ambayo bado hutumia shule za mabweni.

Jopokazi lililoundwa kuchunguza matukio ya migomo shuleni lilipendekeza kuwa baadhi ya shule za mabweni zigeuzwe kuwa za kutwa ili kukabiliana na utovu wa nidhamu katika shule hizo.

Bw Miruka alikuwa akizungumza katika Shule ya Upili ya St Edwards Nyabioto, eneo la Sengera katika eneobunge lake wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika masomo yao.

Alikabidhi basi la shule lililogharimu Sh6.9M kutoka kwa Hazina ya Serikali Kuu ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NGCDF) kwa shule hiyo.

Shule ya walemavu yang’aa tamashani

Na LAWRENCE ONGARO

SHULE ya msingi ya walemavu ya JOY Town, mjini Thika, iliibuka ya pili katika mashindano ya muziki yaliyoshirikisha shule 16 za msingi kutoka eneo la Kati.

Mkurugenzi wa kampuni ya Nut Company Ltd, Bi Anne Mwaura, alisema walemavu wanastahili kupewa nafasi ya kwanza katika mambo yao ya kila siku.

Aliiomba serikali kujitokeza wazi na kuzingatia maslahi ya walemavu hasa wakati wa kutunga mitihani.

“Walemavu wanastahili kupewa muda zaidi wa kufanya mitihani yao kwani hali yao ya maumbile husababisha changa moto tele,” alisema Bi Mwaura, na kuongeza wengi wao huchukua muda mrefu kuelewa mambo.

Alitoa changa moto kwa walimu kuwa mstari wa mbele kuwapa motisha wanafunzi walemavu ili wapige hatua katika masomo yao.

Mwalimu mkuu wa shule ya Joy Town, Bi Mary Wangui Mukami, aliwahimiza wazazi kuwapeleka wana wao walemavu shuleni badala ya kuwaficha kwenye nyumba.

“Ni jambo la kusikitisha kupata ya kwamba wazazi wengi bado huwafungia wana wao manyumbani huku wakiogopa kuchekelewa na jamii. Hii tabia inastahili kukoma mara moja,” alisema Bi Mukami.

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi wakati wa fainali ya mashindano ya miziki ya shule za msingi mkoa wa kati, uliofanyika katika shule ya Joy Town mjini Thika.

Shule hiyo iliibuka ya pili kati ya shile 16 zilizoshiki kwa kutunga wimbo uliotajwa kama ‘Ngarisha’.