Washukiwa wa mauaji wamtisha kiongozi wa mashtaka

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mwandamizi Bi Martha Mutuku alimtaka kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha atayarishe ushahidi wote katika kesi ambapo washukiwa watano wanakabiliwa na mashtaka ya wizi wa mabavu.

Miongoni mwa walionyang’anywa na kuuawa ni aliyekuwa Rubani wa Shirika la Ndege la Kenya Airways Bw Ng’ang’a.

Baada ya kumuua washukiwa hao walidaiwa walificha maiti yake kwa shimo la choo.

Bi Mutuku alimwagiza Bw Naulikha awasiliane na maafisa wawasiliane na maafisa wa polisi wanaochunguza kesi hiyo na kuwapa washukiwa nakala za mashahidi.

Hakimu alitoa agizo hilo baada ya washtakiwa kumlalamikia wamekuwa wakiteswa na polisi kwa kutopewa nakala za mashahidi.

“Naomba hii mahakama iamuru  afisa anayechunguza kesi hii, polisi na Bw Naulikha wajiandae sawasawa kwa vile kutakuwa na kivumbi kesi hii ikianza,” alisema mmoja washtakiwa Bw Daniel Kioko.

Bw Kioko alisema polisi wamekuwa wakichukulia kesi hiyo kwa mzaha ila hawajui “maisha yao (washtakiwa) yamo hatarini.”

Watano hawa wakiongozwa na Bw Daniel Kioko walimlalamikia Bi Mutuku kwamba maafisa wa polisi wanaochunguza kesi hii wanawachezea kwa kutowapa nakala za mashahidi.

Watano hao walimtaka Bw Naulikha ajiandae kwa vile siku ya kusikizwa kwa kesi “atajua kilichomtoa kanga manyoya na kile kinasababisha nyani kuishi juu ya miti.”

Kesi itasikizwa Julai 23, 2018.

Watu 8 washtakiwa kunyang’anya Muriuki Sh100,000

Mshukiwa wa nane, Hussein Suleiman ashtakiwa kwa kumnyang’anya kimabavu Timothy Muriuki pesa katika hoteli ya Boulevard. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

SHAMBULIZI la mfanyabiashara Timothy Muriuki limepelekea washukiwa wanane kushtakiwa kwa kumnyang’anya Sh100,000..

Mnamo Alhamisi  Bw Hussein Suleiman alifikishwa kortini kuhusiana na shambulizi hilo.

Alikabiliwa na shtaka la kumnyang’anya Bw Muriuki katika hoteli ya Boulevard Nairobi na kumwumiza wakati wa kitendo hicho.

Katika picha zilizopigwa kuhusu shambulizi hilo Bw Suleiman alionekana akimnyanyua mlalamishi na kumfurusha nje ya hoteli hiyo.

Bw Suleiman alishtakiwa hwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Alikanusha shtaka la kumnyang’anya kimabavu Bw Muriuki pesa na wakati wa kitendo hicho wakamuumiza.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Avedi hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

“Kuna kesi nyingine tatu zilizofikishwa kortini kuhusu shambulizi hili la Bw Muriuki. Tayari washukiwa wengine saba wameshtakiwa. Kesi hii itaunganishwa na hizo nyingine tatu,” alisema Bi Avendi.

Bi Avedi aliambia mahakama kuwa katika kesi hizo nyingine washukiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kesi hiyo itaunganishwa mnamo Mei 23, 2018.

Wakili Cliff Ombeta anayemtetea mshtakiwa aliomba korti baada ya kesi kuunganishwa upande wa mashtaka uagizwe umkabidhi nakala za mashahidi.

Bi Mutuku aliamuru Bw Suleiman aachiliwe kwa dhamana ya Sh200,000 sawa na washukiwa wale wengine walioshtakiwa awali. Aliamuru kesi dhidi ya Bw Suleiman iuanganishwe na zile nyingine.

Korti iliorodhesha kesi kusikizwa Julai 17.

ERC inavyowaumiza watumizi wa mafuta taa

Na BERNARDINE MUTANU

Huenda mamilioni ya wananchi wakaathiriwa na pendekezo la Tume ya Kusimamia Kawi (ERC) kumaliza matumizi ya mafuta taa.

ERC ilitangaza azma ya kupandisha bei ya mafuta taa zaidi kwa lengo la kuwazuia raia wengi kutumia bidhaa hiyo.

Hata hivyo, bado mamilioni ya Wakenya hutumia taa za mafuta taa, maarufu kama ‘koroboi’.

Hii ni licha ya serikali kujikakamua kuhakikisha kila boma ina umeme. Mwezi  Aprili, Mkurugenzi Mkuu wa ERC Pavel Oimeke alisema serikali ilikuwa na mpango wa kuongeza bei ya mafuta taa ili ifanane na ile ya dizeli kwa lengo la kuwazuia watu kutumia mafuta taa.

Alisema kwa kuongeza ushuru kwa mafuta taa, serikali itakuwa na uwezo wa kuokota Sh354 bilioni na kulinda biashara za kuuza nje na magari kwa kuimarisha matumizi ya mafuta bora.

ERC inalenga kukuza matumizi ya sola na gesi katika kampeni ya kuimarisha mazingira.

Bomba jipya la KPC kusafirisha lita milioni 1 kwa saa

Na BERNARDINE MUTANU

Mafuta ya kwanza yaliyoboreshwa yataanza kusafirishwa kwa kutumia bomba mpya la mafuta Julai 1.

Bomba hilo limetengenezwa kwa gharama ya Sh48 bilioni. Kampuni ya Kenya Pipeline ilisema ilimaliza kutengeneza mfumo wake na kuunganisha na umeme mnamo Machi 2018.

Bomba hilo lina uwezo wa kupitisha 2.6 milioni za mafuta kwa lisali moja kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Julai 1, lita milioni moja kwa saa moja zitasafarishwa kwa kutumia bomba hilo. Lina kipenyo cha inchi 20 na litakuwa na uwezo wa kutosheleza Kenya na majirani wake mahitaji ya mafuta mpaka 2044, alisema meneja Mkurugenzi wa KPC Joe sang.

“Tunatumia teknolojia mpya ili kurahisisha uchukuzi wa mafuta na bidhaa zingine zinazotokana na petroli.

KPC pia imesakini pambu nne mpya maeneo ya Changamwe, Maungu, Mtito Andei na Sultan Hamud na pampu zingine za kuimarisha operesheni katika eneo la Kipevu.

Ni faida tu kwa benki ya Equity

Na BERNARDINE MUTANU

BENKI ya Equity imetangaza ongezeko la asilimia 22 ya faida baada ya kutozwa ushuru.

Kampuni hiyo ilipata faida ya Sh5.9 bilioni kutoka 4.9 bilioni mwaka uliotangulia.

Mwaka 2017, kampuni hiyo ilipata ongezeko la faida la asilimia 14 baada ya kutozwa ushuru wakati benki zingine zilikuwa zikitangaza hasara.

Faida hiyo ilitokana na ongezeko la wateja wapya 1 milioni na hivi sasa ina wateja 12.2 milioni ambapo pesa zilizowekwa na wateja wake ziliongezeka kwa asilimia tisa hadi Sh382.4 bilioni kutoka 349.3 bilioni, ilisema benki hiyo jana katika taarifa.

Kwa sasa Equity ina wateja 12.2 milioni.

Serikali yajiondoa kwa biashara ya hoteli

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeanza mikakati ya kuuza hisa zake katika hoteli kubwa za kifahari nchini.

Hoteli hizo ni InterContinental, Hilton na Mountain Lodge. Tume ya kubinafsisha inatafuta wataalamu kufanyia hoteli hizo uchunguzi na hoteli zingine ndogo kwa lengo la kuziuzia wawekezaji wa kibinafsi.

Tume hiyo hata hivyo haikuelezea pesa inazotarajia kupata kutoka kwa mauzo ya hoteli hizo.

Wachunguzi hao wanatarajiwa kubainisha hali ya kifedha ya hoteli hizo na kutayarisha kandarasi ikiwemo ni pamoja na mikataba ya kuhawalisha hisa hizo.

Mauzo ya hoteli hizo yalitangazwa mara ya kwanza 2011 kama sehemu ya kuimarisha mapato ya serikali.

Serikali ina hisa 40.57 katika Mahoteli ya Intercontinental yanayomiliki Hoteli ya Hilton.

Inalenga kutoa asilimia 33.83 ya hisa zake kwa Kenya Hotel Properties Limited ambayo inasimamia InterContinental na asilimi 39.11 inazomiliki katika Hoteli ya Mountain Lodge, chini ya usimamizi wa TPS Serena.

Je, maji haya yatapunguza gharama ya umeme?

Na BERNARDINE MUTANU

Bei ya umeme inatarajiwa kushuka zaidi katika muda wa miezi kadhaa ijayo kutokana na ongezeko la kiwango cha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme nchini.

Tangu 2015, kiasi cha sasa cha maji katika mabwawa hayo ndicho cha juu zaidi. Waziri wa Kawi Charles Keter Jumanne alisema viwanda vya kuzalisha umeme katika Mto Tana vina maji mengi zaidi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini.

Hii ni kumaanisha kuwa gharama ya matumizi ya umeme itapungua kwa watu binafsi na kampuni.

Kwa sasa, kiwango cha umeme unaotolewa kwa kuzalishwa na maji ni asilimia 40. Alisema hayo saa chache baada ya serikali kutangaza mpango wa kuondoa baadhi ya ada katika matumizi ya umeme nchini.

“Tuko sawa hadi Desemba,” alisema Keter na kukanusha hofu kwamba huenda gharama ya kununua stima ikaongezeka.

Lakini hadi Wakenya wajionee ukweli wa maneno yake katika muda wa miezi ijayo kwani awali kumekuwa na ahadi za kupunguza gharama ya umeme huku ikizidi kupanda.

KEBS kuharibu bidhaa za thamani ya Sh250 milioni kwa kukosa ubora

Na BERNARDINE MUTANU

BIDHAA za thamani ya Sh250 milioni humu nchini zitaharibiwa baada ya kukataa kufikisha upeo wa ubora.

Bidhaa hizo zilizo katika kontena 163 zilikuwa ni pamoja na tairi, spaghetti, mchele. Zilitengwa baada ya Shirika la kutathmini ubora wa bidhaa (KEBS) kusema hazikufikia ubora unaohitajika.

Kulingana na shirika hilo, mchele ulikuwa umeharibika baada ya kufikisha siku ya mwisho ya uuzaji. Spaghetti kwa upande wake hazikuwa zimefikia ubora unaohitajika na KEBS, baada ya uchunguzi wa mahabara.

Tairi zilizuiliwa kwa sababu Kenya huwa haikubali tairi kukuu hazikubaliwi nchini,” alisema meneja Mkurugenzi wa KEBS Charles Ongwae.

Wafanyibiashara wamekuwa na wakati mgumu forodhani kuirai KEBS kukubalia bidhaa zao humu ikiwa hawajapitia utaratibu uliowekwa na shirika hilo.

Bidhaa zote zinazoingia humu nchini zinakaguliwa eneo zinakotoka kwanza na kuwekewa kiwango cha ushuru na shirika hilo.

Hatua hiyo ni kwa lengo la kuzuia ukwepaji wa ushuru.

Kiwanda kipya cha Coca-cola kupunguza ukosefu wa ajira

Na BERNARDINE MUTANU

KAMPUNI ya Coca-Cola imefungua kiwanda cha kutengeneza vinywaji kwa gharama ya Sh7 bilioni katika tawi lake lililoko Embakasi, Nairobi.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza chupa 28,000 za soda kwa saa moja. Kutokana na hilo, kiwanda hicho kiliunda nafasi 24 za kazi katika tawi hilo.

Tofauti kati ya kiwanda hicho na kiwanda cha kawaida ni kwamba sharubati hupakiwa kwa chupa ikiwa moto sana, alieleza meneja mkurugenzi wa Coca Cola Afrika-Kenya (CCBA) Daryl Wilson.

Ni kiwanda cha pili cha aina hiyo Afrika Mashariki, baada ya kiwanda kingine kama hicho kuzinduliwa Uganda.

Baadhi ya bidhaa zitakazotengenezewa katika kiwando hicho ni sharubati ya matunda, chai iliyotiwa barafu na vinywaji vingine vya spoti.

Kampuni hiyo inapata maembe kutoka Murang’a.

Wakenya sasa wachangamkia mashangingi

Na BERNARDINE MUTANU

Idadi ya magari ya kifahari yanayonunuliwa imeongezeka kwa asilimia tano katika robo ya mwanzo ya 2018.

Mauzo ya mashangingi hayo yameongezeka katika maduka ya DT Dobie na RMA Kenya ambayo ni 65 ikilinganishwa na 62 mwaka 2017.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa takwimu kutoka Chama cha Wauzaji Magari (KMI).

Hata hivyo, mauzo ya magari hayo bado yamo chini yakilinganishwa na magari ya kawaida (mapya) ambayo mauzo yake yaliongezeka kwa asilimia 13.6 kutoka 2,755 hadi magari 3,130.

Mauzo ya magari aina ya Porsce pia yaliongezeka ikiwemo ni pamoja na Porsche Cayenne hadi 22 kutoka matano.

Hii ni kutokana na kampeni kubwa ya mauzo iliyofanywa na Porsche, alisema afisa wa kampuni hiyo.

UTALII: Mkiendelea kuiga wenzenu mtatimua watalii

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni na mashirika ya kitalii yametakiwa kufanya mambo kwa njia tofauti kwa lengo la kuvutia watalii zaidi.

Wataalamu wamesema kuwa baadhi ya changamoto zinazoshuhudiwa na mashirika hayo yanatokana na kuiga yanachofanya mashirika mengine.

Kulingana na Tume ya Kitalii Ulimwenguni, mwaka 2017 idadi ya watalii ulimwenguni ilikuwa ni 1.2 bilioni ambapo 62 milioni walizuru Afrika.

Kulingana na takwimu kutoka shirika hilo, nafasi 8.3 milioni za kazi ziliundwa wakati wa kipindi hicho katika sekta ya utalii barani Afrika.

Katika mkutano uliofanywa Afrika Kusini, Durban, wataalamu wakiongozwa na Waziri wa Utalii Afrika Kusini Derek Hanekom waliwataka washikadau kutafuta njia za kukabiliana na changamoto na kuunda mazingira shwari ya kitalii.

Airtel yalemewa na biashara Afrika, yapanga kung’atuka

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya mawasiliano ya simu Bharti Airtel inadaiwa kulenga kuondoka katika Soko la Afrika.

Kampuni hiyo ndiyo mzazi wa Airtel Kenya na katika hatua zake za hivi punde, inalenga kuuza robo ya hisa zake Afrika katika azimio hilo kulingana na ripoti ya vyombo vya habari nchini India.

Ripoti iliyochapishwa katika magazeti India inaonyesha kuwa kampuni hiyo inalenga kupata Sh150 bilioni kwa kuuza sehemu ya hisa zake kwa lengo la kuokoa deni la Sh460 bilioni katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Shughuli ya mauzo hayo inatarajiwa kuzinduliwa Afrika Kusini au Uingereza kulingana na habari hizo.

Mwishoni mwa mwaka jana, Bharti Airtel ilisema ilikuwa tayari kuuza asilimia 20 ya hisa zake ndani ya Airtel Kenya kwa wawekezaji wake humu nchini kabla ya kuondoka nchini kabisa.

Kampuni hiyo inalenga kukomesha biashara zake Kenya, Rwanda na Tanzania na kwa sasa inatafuta mkataba wa kuuza hisa zake kwa kampuni za humu nchini, kununuliwa au kuungana na kampuni zingine.

Buda amwachia mke uwanja agawe uroda anavyotaka, bila bughudha

Na TOBBIE WEKESA

NETIMA, BUNGOMA

Kalameni mmoja kutoka hapa alitoroka boma lake akidai alikuwa akiwindwa na polo aliyeshuku kuwa mpango wa kando wa mke wake. 

Kulingana na mdokezi, polo alifunganya virago na kutorokea jijini huku akiwaacha wenyeji vinywa wazi.

Inadaiwa kalameni alimlaumu mkewe kwa masaibu yaliyomzonga.

“Mke wangu si mtu mzuri. Heri niondoke nimpe nafasi aendelee na raha yake. Sitaki kuuliwa hapa,” kalameni aliwaambia majirani.

Kipusa alijaribu kumzuia polo asiondoke lakini alilemewa nguvu na polo.

“Kazi yako ni mipango ya kando tu. Juzi umenitusi kuwa mimi sikutoshelezi ndio maana unakimbizana na vijana barobaro,” kalameni alimkaripia mkewe.

Kipusa alipinga madai ya polo huku akidai kuwa yalikuwa uongo mtupu.

“Wewe acha uongo wako. Huyo unayesema si mpenzi wangu bali ni jamaa yangu,” kipusa alijitetea.

Penyenye zinasema polo alikuwa akizozana na mkewe kuhusiana na tabia yake ya kuchovya nje.

Penyenye zilizotufikia zinasema polo alikuwa akipata jumbe za kumtishia maisha akiendelea kumgombeza mkewe.

“Juzi huyo jamaa alinisimamisha njiani na akanipa onyo kali. Aliniambia uhusiano wenu ulianza mkiwa shule ya msingi na nikiwa kizingiti nitanyoroshwa,” kalameni alimfokea mkewe.

Majirani walibaki kutazama sinema ya bure jamaa akifichua masaibu yake.

“Jana usiku nimesikia jamaa akitembea hapa nje. Najua ni mimi wanatafuta. Heri nikuachie boma uendelee na tabia zako nao,” polo alimueleza mkewe.

Baada ya kumaliza kupakia mizigo yake, polo aliitisha bodaboda na kuondoka akiapa kutorudi.

“Sitaki kupigwa na hao watu wako. Ukitaka kuwaleta hapa, basi una uhuru sasa,” polo alimueleza mkewe huku akienda.

…WAZO BONZO…

Pendekezo rais ahudumu kwa miaka 4 na seneta miaka 7

Na LUCY KILALO

CHAGUZI za nyadhifa sita zinazofanywa nchini kwa wakati mmoja zinastahili kufanywa nyakati tofauti ili kupunguza joto la kisiasa kila baada ya miaka mitano, pamoja na kutoa nafasi kwa wanaoshindwa kuwania nafasi nyingine.

Mapendekezo hayo ya kubadilisha vipengee kadha vya Katiba, kulingana na mwasilishaji wake, yatahakikisha pia Wakenya wanawapiga msasa vilivyo wanaotaka uongozi.

Bw Ezekiel Njeru Namu aliambia Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Haki na Masuala ya Sheria kuwa kufanyika kwa chaguzi za urais, useneta, ugavana, ubunge na udiwani kwa wakati mmoja ndiyo chanzo cha vurumai zinazoshuhudiwa nchini kila baada ya miaka mitano.

Bw Njeru sasa anapendekeza mabadiliko, akimtaka rais na diwani kuhudumu kwa kipindi cha miaka minne na uchaguzi wao kufanyika pamoja. Naye gavana ahudumu kwa miaka mitano, mbunge kwa miaka sita na seneta kwa miaka saba. Hata hivyo, anataka nafasi ya Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ifutiliwe mbali.

“Nahisi tunastahili kubadilisha jinsi tiunavyofanya uchaguzi, kwani huwa tunaelekeza nguvu zote upande mmoja. Pia tutapunguza gharama ya uchaguzi,” alisema.

“Huwa tunakosa kuwahoji vilivyo wanaogombea kila mmoja binafsi. Wakenya hawajui tofauti ya viongozi hao kwani utapata watu zaidi ya 100 kila mmoja akiwania na akiwa na manifesto yake, na ndiyo sababu mwishowe tunapata viongozi ambao hatukutaka, kwa kuwa hatuna nafasi ya kuwapiga msasa vilivyo.”

Bw Njeru pia anasema kuwa uamuzi wake wa uchaguzi wa urais na diwani kufanyika wakati mmoja, ni kuhakikisha kuwa mwaniaji wa urais analazimika kufika mashinani, jambo ambalo kulingana naye halijakuwa likifanyika.

Pia anatetea jinsi alivyopanga vipindi vya kuhudumu, akisema kuwa vinapatia muda ikiwa ni maseneta, kukagua vilivyo utendaji kazi wa viongozi katika kaunti.

Aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, William Cheptumo kuwa nafasi kama ya Seneta ni muhimu na kwamba wanahudumia eneo kubwa, ambalo ni kaunti, na wanastahili kulipwa zaidi na sio kiwango sawa na wabunge.

Anataka pia suala la elimu lisizingatiwe kwa wanaowania nafasi hizo, pamoja na kuhimiza utumizi wa lugha ya mama katika bunge za kaunti.

Wakati huo huo, kamati hiyo pia ilisikiliza sababu za Bw Mohamed Mohamed Sheikh, ambaye anataka umri wa rais, usizidi miaka 70. Alisema kuwa majaji wanastaafu wakiwa na umri wa miaka 70, na watumishi wa umma miaka 60, hivyo rais na naibu wake wanastahili kuwa watumishi wa umma, na lazima umri huo wa kustaafu udhibitiwe.

Kamati hiyo itaangalia mapendekezo hayo na kuwapa wawasilishaji majibu katika kipindi cha siku 60 kuhusu uamuzi wao.

 

 

MZAHA WA SONKO: Miguna akataa uteuzi

Na WAANDISHI WETU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko, alionekana kuwachezea shere wakazi wa Nairobi na taifa kwa jumla alipotangaza Jumatano usiku kuwa amemteua wakili mbishi Dkt Miguna Miguna kuwa naibu wake.

Hii ni kwa sababu alipotoa tangazo hilo, Gavana Sonko alifahamu uwezekano finyu wa Dkt Miguna kuwa naibu wake na hivyo tangazo hilo lilijitokeza tu kama mzaha ama lililokuwa na nia ya kuafikia malengo fulani ya kisiasa.

Kwa kufahamu tangazo lilikuwa la kuchezewa, Dkt Miguna alipuzilia mbali uteuzi huo akiutaja kama mbinu ya kumkanganya katika juhudi zake za kupigania kurudishiwa paspoti yake na vita vyake dhidi ya utawala anaosisitiza ni wa kidikteta.

Bw Sonko alifahamu kuwa hata kama Dkt Miguna angekubali uteuzi wa kuwa naibu wake jijini Nairobi, angekuwa ameanza safari isiyoelekea kokote. Kiti hicho kiliachwa wazi na Polycarp Igathe alipojiuzulu Februari.

Tatizo la kwanza ambalo Dkt Miguna angekumbana nalo ni kuwa kwa sasa Serikali inasisitiza hana uraia wa Kenya, ambao sharti awe nao ili kuhudumu katika wadhifa wa Naibu Gavana. Juhudi zake awali kutambuliwa kama raia zimegonga mwamba.

Bw Miguna, ambaye pia ana uraia wa Canada, alifukuzwa nchini Februari na alipojaribu kurejea mwezi uliofuata alikatazwa kuingia na badala yake akarudishwa Canada. Alikuwa amesema atakuja Kenya Jumatano lakini hakufanya hivyo kutokana na suala la paspoti yake.

Idara ya uhamiaji imesisitiza sharti Dkt Miguna afuate kanuni ili apate uraia wa Kenya ambao inasema aliukana alipochukua wa Canada kulingana na Katiba ya awali.

 

Uraia kwanza

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi alisema sharti wakili huyo angepata uraia wa Kenya kabla ya madiwani wa Nairobi kumpiga msasa kama inavyotakikana kisheria.

“Kwa sasa Dkt Miguna ni raia wa Canada. Ni sharti asuluhishe utata wa uraia wake na serikali,” alisema Bi Elachi.

Na iwapo Bw Miguna angeondolewa kizingiti cha uraia, angekabiliwa na kibarua kigumu cha kuwashawishi Bunge la Nairobi kuidhinisha uteuzi wake hasa ikizingatiwa Jubilee ina wingi wa wajumbe.

Alhamisi, Spika Elachi na Seneta Johnston Sakaja walipuzilia mbali uwezekano wa wakili huyo kuidhinishwa na bunge la kaunti. “Miguna hatakuwa Naibu Gavana wa Nairobi. Nawahakikishia hilo,” alisema Bw Sakaja.

Tatizo lingine ambalo angekumbana nalo ni kuwa yeye si mwanachama wa Jubilee. Kiongozi wa wengi katika Kaunti ya Nairobi, Bw Abdi Guyo alisema jana kuwa wazo la Dkt Miguna kuwa Naibu Gavana ni ndoto tu.

 

Wanasiasa wa misimamo mikali

Suala lingine ni kuwa hata kama miujiza ingetendeka na ateuliwe, ingekuwa vigumu kwake kufanya kazi na Bw Sonko ikizingatiwa tofauti kali za misimamo baina yao.

Wawili hao wamekuwa wakirushiana cheche kali za maneno na kutofautiana vikali kuhusu uongozi wa Nairobi.

Mnamo Mei 2016, Bw Sonko alisema licha ya Dkt Miguna kumshambulia kila mara, atakapochaguliwa kuwa gavana atampa wadhifa katika serikali yake. Bw Miguna alijibu: “Ndugu yangu Sonko siwezi kuhudumu chini au pamoja na jambazi. Unaelewa?”

Wakati wa mdahalo wa wawaniaji wa ugavana Nairobi, Dkt Miguna aliwakabili vikali Bw Sonko na mtangulizi wake Dkt Evans Kidero kwa kile alichosema ni kushirikiana na wakora kufuja fedha za kaunti.

Kwa upande wake, Bw Sonko alimjibu Dkt Miguna kwa kumtaja kama ‘mtu mwenye akili punguani.’

Kenya sasa nambari 111 duniani viwango vya soka

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars ndiyo timu pekee kutoka eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) iliyoimarika kwenye viwango bora vya soka duniani, Alhamisi.

Viwango hivi vipya vimetangazwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), huku Kenya ikipaa kutoka nafasi ya 113 hadi nambari 111.

Stars imenufaika pakubwa na Zimbabwe na Madagascar kuteremka nafasi tatu kila mmoja hadi nambari 113 na 114, mtawalia.

Katika eneo la Cecafa, Uganda imesalia katika nafasi ya 74 duniani. Kenya ni ya pili (imeimarika kutoka 113 hadi 111) nazo Rwanda, Sudan na Tanzania zimesalia katika nafasi za 123, 126 na 137 duniani, mtawalia.

Ethiopia na Burundi zimeshuka nafasi moja kila mmoja hadi nambari 146 duniani. Sudan Kusini imeteremka nafasi mbili hadi nambari 157 duniani nayo Djibouti imekwamilia nafasi ya 198. Eritrea na Somalia zinavuta mkia katika nafasi ya 207 duniani.

Tunisia ndiyo nambari moja Afrika. Inashikilia nafasi ya 14 duniani. Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Morocco, Misri na Nigeria zinafuatana katika nafasi za 28, 38, 42, 46 na 47 duniani, mtawalia.

Cameroon na Ghana zimeruka juu nafasi moja hadi nambari 50 duniani nayo Burkina Faso iko chini nafasi moja hadi nambari 54 duniani. Cape Verde imesalia katika nafasi ya 58 duniani nayo Algeria inafunga 10-bora Afrika na katika nafasi ya 64 duniani. Algeria imetupwa chini nafasi mbili.

Hakuna mabadiliko katika nafasi 47 za kwanza duniani, huku Ujerumani, Brazil, Ubelgiji, Ureno, Argentina, Uswizi, Ufaransa, Uhispania, Chile na Poland zikiwa ndani ya mduara wa 10-bora, mtawalia.

Chelsea yaadhibiwa kwa kukosa nidhamu uwanjani

Na GEOFFREY ANENE

CHELSEA imepigwa faini ya Sh2, 716,057 na Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA) kwa utovu wa nidhamu.

Wachezaji na makocha walifanya kosa la kuzingira refa na kumfokea wakati wa mapumziko wa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Huddersfield iliyomalizika 1-1 Mei 9, 2018.

‘The Blues’ walikasirishwa na uamuzi wa refa Lee Mason kuwapa kona, lakini kabla ya Willian kuipiga, akapuliza kipenga cha kukamilisha dakika hizo 45 za kwanza. Afisa huyu aliamua kwamba kipindi cha kwanza kilikuwa kimetamatika.

Nahodha Cesar Azpilicueta, kiungo Cesc Fabregas na beki Antonio Rudiger waliongoza katika kumchemkia Mason. Kocha msaidizi Carlo Cudini aliondoa Rudiger karibu na refa huyo kwa kumvuta. Cudini pia aliongelesha Mason.

“Chelsea imepigwa faini ya Sh2, 716,057 baada ya kukubali kosa la kushindwa kuhakikisha wachezaji na maafisa wake wanaonyesha mfano mwema,” taarifa kutoka FA ilisema.

Chelsea ilikashifu Huddersfield kwa kupoteza muda wakati wa mechi hiyo, matokeo yaliyozima matumaini yake ya kuingia Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao. Kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Newcastle katika siku ya mwisho ya Ligi Kuu ya Uingereza hapo Mei 13 kilihakikisha Chelsea inakamilisha katika nafasi ya tano.

Chelsea ya kocha Antonio Conte inaweza kumaliza msimu na taji ikiwa itafaulu kulemea Manchester United ya kocha Jose Mourinho katika fainali ya Kombe la FA hapo Mei 19 uwanjani Wembley.

Kigali Peace Marathon yavutia watimkaji 8,000

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI 8,000 watashiriki makala ya 14 ya Mbio za Amani za Kigali Marathon mnamo Mei 20, 2018.

Gazeti la New Times nchini Rwanda limesema Alhamisi kwamba mwenyeji Felicien Muhitira ameapa kumaliza utawala wa Kenya katika kitengo cha wanaume cha mbio za kilomita 21.

“Wakati wangu wa kutwaa taji ni mwaka huu. Sijawahi kuhisi niko tayari kabisa kwa mashindano haya kama mwaka huu. Nataka kupanda kwenye jukwaa hilo, nitazame bendera ya taifa langu ikipepea kabisa na wimbo wa taifa langu ukiimbwa.

Najua ni kibarua kigumu, hasa kutoka kwa Wakenya, lakini nimekuwa nikishindana nao nchini Italia na ninaamini naweza kuwalemea,” Muhitira alinukuliwa na gazeti hilo akisema.

Mwaka 2017, Bartile Kiptoo aliongoza Mkenya mwenzake Ezekiel Kimeli kunyakua nafasi mbili za kwanza katika mbio za kilomita 21 za wanaume, huku Mrwanda John Hakizimana akifunga tatu-bora.

Naye Salome Nyirarukundo alishindia Rwanda taji lake la kwanza kabisa katika mbio za kilomita 21 cha Kigali Peace Marathon katika kitengo cha wanawake. Alifuatwa na Mkenya Sheilla Chesang na Mrwanda Claudette Mukasakindi.

Mashabiki wa Gor wakejeli washambuliaji kwa kufuma mabao hewa

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia wamelia sana kuhusu ubutu wa washambuliaji wao mbele ya lango baada ya klabu hiyo kukabwa 0-0 na USM Alger katika mechi ya pili ya Kundi D ya Kombe la Mashirikisho, Jumatano.

Baada ya mechi hiyo iliyochezewa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, mashabiki walilaumu sana washambuliaji na hata kupendekezea kocha Dylan Kerr wazo la kuimarisha kikosi kwa kusajili washambuliaji. Lawama kubwa ilielekezwa kwa raia wa Ivory Coast Ephrem Guikan.

Shabiki Kassusy Judy Jeff alisema, “Safu ya mbele Bwana Kerr…”

Naye Apong Kor, “Guikan anahitaji kuchukulia kazi yake kwa uzito. Atafanya Gor ijute sana (kupoteza nafasi nyingi)! “Nilimtazama na kulalamika wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Hull City (Mei 13). Anafaa kutemwa mapema.”

Davvy Robberto Starboy, “Guikan ni butu kabisa.” Benard Awright, “Huyu mchezaji anaitwa Guikan siwezi kumtazama tena akivalia jezi ya Gor. Hafai kuvaa jezi hiyo, hawezi kutumia nafasi nyingi anazopata, tukiendelea kuandikisha sare, tutajipata tukivuta mkia kwenye kundi letu.”

Naye Tarzan Johnso alisema, “Gor ilicheza mechi safi…shida yetu kubwa ni safu ya mbele…(washambuliaji wetu) hawawezi kukamilisha hata nafasi rahisi…mambo yalikuwa hivi dhidi ya Esperance (Tunisia), Rayon Sport (Rwanda), Hull City (Uingereza) na sasa USM Alger…tunahitaji (kununua) mshambuliaji…(Jacques) Tuyisenge, Guikan na (Meddie) Kagere hawana utulivu…tusipobadilika, hatutaenda mbali.

Soka ni mchezo wa kutumia nafasi zako vyema. Hata hivyo, natofautiana na wengi wanaolaumu Guikan. Nadhani alicheza vyema. Tuyisenge ndiye alipoteza nafasi nyingi na alikuwa butu.”

Marefa pia hakuponea hasira ya mashabiki. Kevin Gama Pintoh alisema,” Hii ndiyo sababu marefa wengine wanatiwa adabu… Hata hivyo, naomba mmpeleke Guikan katika klabu nyingine kwa mkopo kwa sababu bado anakosa ujuzi wa kupita mabeki. Tafadhali (Gor) tafuteni mvamizi kutoka Misri kwa sababu wana kasi na nguvu kukabili mabeki na kusababisha bao la kujifunga ama penalti.”

Gor imesalia katika nafasi ya pili kwenye kundi lake kwa alama mbili. Kabla ya sare tasa dhidi ya Alger, Gor ilikuwa imekabwa 1-1 dhidi ya Rayon nchini Rwanda.

Alger inaongoza kwa alama nne. Ilipepeta Young Africans ya Tanzania 4-0 nchini Algeria katika mechi ya kwanza. Rayon ina alama mbili nayo Yanga inavuta mkia kwa alama moja. Mechi ijayo ya Gor ni dhidi ya Young Africans hapo Julai 18 nchini Kenya.

Huenda City Hall ikaadhibiwa vikali na Kenya Power

Na BERNARDINE MUTANU

HUENDA serikali ya kaunti ya Nairobi ikakatiwa umeme na kampuni ya Kenya Power kutokana na bili kubwa.

Mahakama Jumatano iliipa Kenya Power ruhusa ya kuitisha Sh732 milioni inazodai Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Ikiwa serikali hiyo haitalipa pesa hizo, Kenya Power ilipewa ruhusu ya kukatia serikali hiyo umeme.

Kulingana na Jaji John Mativo, serikali ya Kaunti ya Nairobi ilipoingia mamlakani ilikubali kutwaa madeni yote ya Baraza la Jiji la Nairobi.

Serikali ya Evans Kidero ilienda mahakamani kupiga kutozwa bili hiyo kwa kusema iliachwa na NCC.

Sonko apinga kesi ya Sh1.7 bilioni

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA  Mike Mbuvi Sonko Jumatano aliomba mahakama kuu itupilie mbali kesi aliyoshtakiwa  na mwakilishi wa wadi ya Makongeni (MCA) Bw Peter Imwatok anayepinga bima ya afya ya Sh1.7 bilioni.

Wakili Harrison Kinyanjui alimweleza Jaji Hedwiq Ong’udi kuwa kesi aliyoshtaki  Bw Imwatok ilifaa isikizwe na kuamuliwa na  kamati ya kusimamia zabuni.

Bw Kinyanjui aliomba mahakama itupe kesi hiyo iliyoshtakiwa na Bw Imwatok akisema “ hajawasilisha ushahidi wowote kuthibitisha utoaji zabuni  ya huduma za afya kwa wafanyakazi wa kaunti ya Nairobi ulifanywa kwa njia isiyofaa.”

Pia Bw Kinyanjui alieleza Jaji Ong’undi kwamba MCA huyo wa wadi ya Makongeni alistahili kuwasilisha malalamishi yake kwa kamati inayohusika na masuala ya utoaji zabuni kwa kaunti.

MCA huyo analaumu  usimamizi wa Bw Sonko kwa kutumia vibaya pesa za umma ikiwa atalipa ada ya Sh1.7 bilioni.

Kesi hiyo itasikizwa mnamo Juni 7, 2018.

Kesi ya jaji aliyetupa kesi iliyomkabili Pattni kusikizwa upya na Mahakama ya Juu

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Juu Jumatano iliahirisha kusikizwa kwa kesi ya Jaji Joseph Mbalu Mutava aliyefutwa kazi kwa kutupilia mbali kesi dhidi ya bwanyenye Kamlesh Pattni ya wizi wa Sh5.8 bilioni kutoka kwa Serikali miaka 26 iliyopita.

Wakiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga majaji wa Mahakama ya Juu waliamuru kesi hiyo isikizwe Julai 18, 2018.

Jaji Mutava aliwasilisha kesi kupinga kutimuliwa kazini na jopo iliyoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Kesi hiyo iliahirishwa baada ya korti kufahamishwa na wakili Kyalo Mbobu kwamba wakili Philip Nyachoti anayemwakilisha Jaji Mutava anawakilisha Magavana katika kesi za uchaguzi.

Bw Nyachoti alikuwa anaendeleza kesi hizo katika Mahakama  ya Rufaa, Eldoret.

Wakili huyo anasema jopo la majaji iliyoongozwa na Jaji Maraga kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu ilikosea kumpendekezea Rais Kenyatta amfute kazi Jaji Mutava.

Ugali ghali wabisha

Na BERNARDINE MUTANU

HUENDA gharama ya unga wa ugali ikaongezeka ikiwa mswada uliowasilishwa Bungeni utapitishwa na kuidhinishwa na rais.

Mswada huo ulifikishwa Bungeni miezi kadhaa iliyopita. Mswada huo wa Marekebisho ya Ushuru 2018 unalenga kubadilisha hadhi ya mahindi, ngano na mhogo, ambazo hazitozwi ushuru.

Kulingana na watengenezaji wa unga, kiwango cha ushuru kikibadilishwa kitapandisha bei ya unga, gharama itakayolimbikiziwa wateja wa unga.

“Hii ni kumaanisha kuwa watengenezaji wa unga hawawezi kujilipa ushuru unaotozwa bidhaa (VAT) kwa malighafi wanayotumia kutengeneza unga, kumaanisha kuwa gharama hiyo itapitishwa kwa wateja,” kilisema chama cha watengenezaji unga.

Bili hiyo inalenga mapato yanayotokana na unga wa mahindi, mkate na unga wa mhogo.

Yaibuka Igathe anafaa zaidi kwa sekta ya benki

Na BERNARDINE MUTANU

Aliyekuwa Naibu Gavana Nairobi, Bw Polycarp Igathe amerejea kwa sekta ya benki kwa kishindo.

Hii ni baada ya kuteuliwa na Benki ya Equity kama Afisa Mkuu wa Biashara (CCO), baada ya kuona kwamba anafaa zaidi kwa nafasi hiyo na wala si siasa.

Bw Igathe alijiuzulu kama naibu wa gavana mapema mwakani baada ya kutofautiana na Gavana Mike Sonko.

Benki hiyo inatarajiwa kumtangaza kama msimamizi wa wajibu huo wakati wa mkutano wa wawekezaji Alhamisi.

Alipojiuzulu, Bw Igathe alisema alikuwa amekosa kupata uaminifu wa mkubwa wake (Gavana Sonko), hivyo hakuweza kufanya kazi vizuri.

Mkakati mpya wa kupunguza ada ya umeme

Na BERNARDINE MUTANU

Ni habari njema kwa Wakenya baada ya serikali kuondoa baadhi ya ada inazotoza umeme.

Hatua hiyo ni kumaanisha gharama ya matumizi ya umeme itapungua kwa kiwango fulani. Kwa sasa, asilimia 77 ya malipo ya stima huenda kwa ushuru.

Ada hizo ni asilimia 24.8 isiyobadilika, asilimia 27.7 ya uzalishaji wa umeme ambapo asilimia 13.6 ni ushuru wa matumizi ya umeme(VAT), sarafu ya kigeni ni asilimia nane na asilimia tatu ni mfumko wa bei ambapo Mamlaka ya Kusimamia Rasilimali ya Maji (WARMA) hupokea asilimia o.1.

Zinazobakia ndio umeme ulionunuliwa na mteja, alisema mkurugenzi wa ERC Pavel Oimeke hivi majuzi.

Lakini Rais Uhuru Kenyatta aliagiza baadhi ya ada hizo kuondolewa. Kutokana na hilo, Waziri wa Fedha na mwenzake wa Kawi Charles Keter watakutana kujadiliana agizo hilo.

Ada zinazolengwa ni ile ya WARMA na ERC. Lakini ada hizo ni asilimia 0.001 ya bili yote ya stima.

Ada nyingine inayotarajiwa kuondolewa ni ile ya stima maeneo ya mashambani ambayo ni asilimia tano ya kiwango cha umeme kilichonunuliwa.

Wakenya sasa watalipa Sh10 chini kwa kila 50 kWh kutoka Sh24.03. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Wakenya kulalamikia kiwango cha juu cha gharama ya umeme.

KILIO CHA HAKI: Sababu za ubakaji kukithiri katika mitaa ya mabanda

Na BENSON MATHEKA
IDADI ya kesi za unajisi wa watoto inaendelea kuongezeka katika Mahakama ya Kibera hasa kutoka mitaa ya mabanda jijini Nairobi. 

Takwimu katika mahakama hiyo zinaonyesha hali ya kusikitisha huku kesi zaidi ya 10 zikifunguliwa kila wiki. Katika mwezi mmoja uliopita, kesi zaidi ya 40 zilisajiliwa katika mahakama hiyo na washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Ingawa sio wote wanaopata dhamana, kuachiliwa kwa washukiwa kunawatia hofu waendeshaji wa mashtaka kwamba huenda wakawatisha waathiriwa na mashahidi.

Waendeshaji wa mashtaka wanasema japo ni haki ya mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana, hofu kwamba wanaweza kuwatisha mashahidi haiwezi kuepukika.

Baadhi ya kesi za ubakaji huondolewa na washukiwa kuachiliwa huru baada ya mashahidi kukosa kufika kortini na juhudi za polisi kuwasaka kukosa kufua dafu.

Miongoni mwa kesi za ubakaji  zilizosajiliwa majuzi ni ya Keith Mbugua na Edwin Aluda kutoka kituo cha polisi cha Muthangari kinachohudumia mtaa wa Kawangware miongoni mwa mingine, Kelvin Orenge, Alfred Simbiri, Godffrey Osiemo na Romano Mbaya kutoka kituo  cha polisi cha Kabete na ya Salim Makhanu na Julius Mwangi kutoka kituo cha polisi cha Langata.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa walidaiwa kuwanajisi watoto baadhi yao wenye umri wa miaka mitatu. Rekodi hizo zinaonyesha kwamba washukiwa waliachiliwa kwa dhamana ya kati ya Sh200,000 na Sh300,000.

Hali ni mbaya hivi kwamba Jaji Mkuu David Maraga  anawataka wazee kuingilia kati na kuwashauri vijana kuepuka kujihusisha na visa hivi. Akizungumza alipozuru mahakama zilizoko Magharibi mwa Kenya mapema mwaka huu, Jaji Maraga alitaja kesi hizi kama janga linalofaa kukabiliwa na kila mmoja.

Rekodi katika mahakama hiyo zinaonyesha kwamba visa vingi hutokea mitaa ya mabanda ya Kawangware, Riruta, Kangemi, Kabete na Kibera ambayo inaishi watu wengi wa mapato ya chini.

Viongozi wa mashirika ya kijamii na ya kutetea watoto wanasema maisha ya wasichana katika mitaa ya mabanda yamo hatarini.

“Maisha ya wasichana yamo hatarini kwa sababu ya tisho la wanajisi. Tunashughulikia visa vya unajisi kila wakati na vinazidi kuongezeka,” alisema mtoaji ushauri nasaha kwa watoto Jane Atieno wa shirika la Just a Kid Foundation.

Alisema mbali na visa vinavyoripotiwa, wanahofia kwamba  kuna visa vingi ambavyo haviripotiwi kwa sababu ya mila na vitisho kutoka kwa washukiwa.

Takwimu za polisi zinaonyesha wanaohusika na ukatili dhidi ya wasichana na wanawake ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 18 na 36 japo kuna watu wa umri mkubwa wanaoshtakiwa.

Wizara ya Elimu yaishangaa NLC kununua ardhi bila hatimiliki

Na BERNARDINE MUTANU

WIZARA ya Elimu imeshutumu Tume ya Ardhi nchini (NLC) kwa kutumia Sh1.5 bilioni kununua ardhi ya shule mbili za umma, bila hati za umiliki.

Tume hiyo inasemekana kununua vipande hivyo katika eneo la Ruaraka, Nairobi.

Katibu Mkuu wa Elimu Dkt Belio Kipsang wakati wa mahojiano mbele ya kamati ya seneti alisema licha ya kuandikia barua tume hiyo kupata hatimiliki ya ardhi kutoka Kampuni ya Afrison Import and Export Limited, tume hiyo ilikiuka ombi hilo.

Maseneta hao walikuwa wakihoji Dkt Kipsang kuhusiana na utwaaji wa lazima wa ekari 13.534 ambamo shule ya upili ya Ruaraka na Shule ya Msingi ya Drive zimejengwa kwa jumla ya Sh3.2 bilioni.

Wizara hiyo kupitia kwa NLC ililipa Sh1.5 bilioni kwa shamba la Whispering Farms Limited. Shule hizo mbili zilijengwa miaka 34 na 32 iliyopita kwa shamba la kibinafsi.

Kenya yakataa mkataba wa Uchina kulinda biashara zake

Na BERNARDINE MUTANU

Kenya imekataa kutia sahihi mkataba wa kibiashara ambao serikali ya China imekuwa ikisukuma mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuidhinisha tangu 2016.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi na Biashara Bw Chris Kiptoo.

Jumatatu Mei 14, Bw Kiptoo alisema uamuzi huo ulitokana na haja ya kuzilinda kampuni za Kenya.

Hii ni kutokana na kuwa Kenya ikikubali mkataba huo huenda ukaathiri kampuni za humu nchini ambazo ni changa, kwa sababu ya bidhaa za China za bei ya chini.

Huenda hatua ya Kenya ikazua mgogoro wa kidiplomasia kati yake na China. Kwa sasa, biashara kati ya EAC na China inapendelea zaidi taifa hilo.

Kwa sasa miongoni mwa bidhaa zinazonunuliwa nje ya nchi, asilimia 25 hutoka China.

Hivyo, kuidhinishwa kwa Eneo la Biashara Huru (FTA) ni kumaanisha kuwa bidhaa kutoka China zitaongezeka nchini zaidi, na kulemaza bidhaa zilizotengenezewa humu nchini.

Hata hivyo, bidhaa ambazo Kenya huuza nchini China ni za chini zaidi (asilimia mbili) ya bidhaa zote zinazouzwa kutoka Kenya nje ya nchi.