Habari za Kitaifa

Afrika ni simba, atanguruma nikiinga AU, asema Raila

Na BENSON MATHEKA August 27th, 2024 1 min read

BARA la Afrika, ni simba anayetishia mabara na mataifa mengine yaliyoendelea ulimwenguni kutokana na uwezo wake mkubwa wa raslimali na nguvukazi, mgombeaji wa Kenya wa kiti cha uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika Raila Odinga amesema.

Chini ya uongozi wake iwapo atachaguliwa kuongoza AUC, Afrika itatumia uwezo wake kujistawisha na sio kufaidi nchi na mabara mengine pekee.

Akihutubu katika Ikulu ya Nairobi, Jumanne, Agosti 27, 2024 wakati wa kuzinduliwa kwake rasmi kuwania wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa Barani Afrika, Bw Raila alisema Afrika ina uwezo mkubwa ambao umekuwa ukimezewa mate na kutumiwa na mataifa mengine kujiendeleza huku ikibaki nyuma kimaendeleo.

Alitaja madini mengi ya bara hili ambayo hayatumiwi kustawisha wakazi kikamilifu.

“Ninawapa notisi, simba Afrika ananguruma na anakuja kuchukua nafasi yenu kimaendeleo,” alisema.

Alisema Bara la Afrika linapaswa kufidiwa kutokana na hasara ya mabadiliko ya tabianchi (Climate change) kwa kuwa inatoa kiwango cha chini cha gesi ya Kaboni inayochangia hali hiyo, huku akitangaza kuwa ataimarisha uunganishaji wa miundomsingi kote barani, miongoni mwa masuala mengine.

“Nitaongozwa na malengo ya viongozi wa kwanza wa Afrika huru ambao waliongoza vita vya ukombozi,” akasema.

Bw Odinga alisema ruwaza yake inaazimia Afrika yenye uthabiti wa kisiasa.