Habari za Kitaifa

Amoth akaribia kuteuliwa rasmi kama Mkurugenzi Mkuu wa Afya


KAMATI ya pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Afya,  imempendekeza Dkt Patrick Amoth,  kwa wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini.

“Baada kumhoji Alhamisi wiki jana kubaini ufaafu wake, tumeridhishwa na ufaafu wake kwa wadhifa huo. Tumeandaa ripoti ya pamoja inayopendekeza kwamba Bunge la Kitaifa na Seneti zimwidhinishe Dkt Patrick Amoth kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Afya,” Mbunge mmoja ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya ameambia Taifa Leo Dijitali.

“Ripoti hiyo itajadiliwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti wakati wowote kuanzia leo (Jumatano Julai 31, 2024) na ninaamini itapitishwa,” akaeleza Mbunge huyo ambaye aliomba tulibane jina lake kwa sababu kanuni za bunge hazimruhusu kuongea kwa niaba ya kamati hiyo.

Dkt Amoth amehudumu kama kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini kwa zaidi ya miaka minne, tangu 2019, baada ya kumrithi Dkt John Masasabi.

Aliyekuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha,  alimpendekeza Dkt Amoth kwa wadhifa huo mnamo Juni 23, 2024.

Hii ni baada ya mtaalamu huyo kuibuka bora zaidi miongoni mwa watu waliotuma maombi kujaza nafasi hiyo.

Tume hiyo iliwahoji watu 11 kwa wadhifa huo akiwemo Dkt Amoth.

Mnamo Februari 20, 2024 Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) iliweka tangazo la kualika maombi kutoka kwa wanaohitimu kwa wadhifa huo.

“Niliwasilisha jina la Dkt Patrick Amoth bungeni baada ya kuibuka kuwa bora zaidi miongoni mwa waliohojiwa kwa wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini,” Bi Nakhumicha akasema kwenye taarifa Juni 23, 2024.

Kabla ya kuteuliwa kwake kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa Afya, Dkt Amoth alihudumu kama mshauri wa kiufundi katika Wizara ya Afya.

Aliangaziwa zaidi katika vyombo vya habari katika mwaka wa 2020 baada ya mlipuko wa ugonjwa hatari wa Covid-19 akiandamana na aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutoa habari muhimu kuhusu janga hilo.

Kulingana na Sheria ya Afya ya 2007, baada ya kuidhinishwa na mabunge yote mawili,  Dkt Amoth atateuliwa rasmi na Waziri wa Afya.

Uteuzi huo utacheleweshwa hadi Waziri Mteule wa Afya Dkt Debra Mlongo Barasa, atakapopigwa msasa na bunge, kuidhinishwa na kuapishwa rasmi.