Habari Mseto

Anavyoteka hela kupitia viungo maalum vya kuku  

March 19th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU 

ZICK Onyango alipopoteza ajira miaka kadhaa iliyopita, hakujua hatma ya maisha yake ikizingatiwa kuwa ni mume anayeandamwa na majukumu ya familia. 

Onyango, 31, sawa na vijana wengine wenye bidii za mchwa hakuwa na budi ila kujituma mitaani kutafutia familia riziki.

Aliingilia uchuuzi wa bidhaa za kula, akidokeza kwamba kazi aliyoona itamfaa ni kuuza soseji na smokie.

Mapato, hata hivyo, anasema hayakuwa ya kuridhisha akifichua kwamba kwa siku angeweka kibindoni faida ya Sh150.

Faida, ni pesa za ziada kwenye biashara baada ya mwekezaji kuondoa gharama ya matumizi, ikiwemo; kurejesha stoki na kuondoa leba.

Zick Onyango, mfanyabiashara katika Kaunti ya Kisumu. PICHA|SAMMY WAWERU

“Faida ya Sh150 kipindi ambacho gharama ya maisha na uchumi inazidi kupanda kila uchao ingemudu kukithi familia mahitaji muhimu ya kimsingi?”

Ni mojawapo ya maswali yaliyotinga bongo la Onyango.

Hakuwa na budi ila kufanya vyema mahesabu yake, na ni katika harakati za kujipanga mapema 2023 alielezwa kuhusu mradi wa Chicken Basket Ltd kupiga jeki vijana Kisumu kujiendeleza kibiashara.

Ni mpango unaolenga vijana wanaochuuza bidhaa za kula hususan smokie, soseji na mayai.

“Huwapa vifaa maalum vya kuchoma, vikamatio na aproni, kisha tunawauzia kwa bei ya chini bidhaa wanazochuuza,” anasema Abisai Nandi, mwasisi wa kampuni hiyo.

Bidhaa hizo zinajumuisha viungo maalum vya kuku, mayai na smokie za kuku.

Zick Onyango akihudumuia mteja. Anamtengenezea yai, katika kituo chake cha kazi eneo la Kibos, Kisumu. PICHA|SAMMY WAWERU

Chicken Basket Ltd, ni kampuni ya ufugaji kuku na inaendeleza mpango huo maarufu kama Choma Preneurship jijini Kisumu, Siaya, Kakamega na Vihiga.

Kulingana na Onyango, kufikia Aprili 2023 alikuwa ameshawishika kwamba alihitaji kupanua mawazo hivyo basi akajiunga na mradi huo.

“Nililipa Sh2, 500, nikapewa vifaa maalum vya kazi, mayai, smokie pakiti moja na makaa ya upekee – briquettes,” anasema.

Mwaka mmoja baadaye, mjasirimali huyu anayeendeleza biashara hiyo katika mtaa wa mabanda wa Kibos, Kisumu, ana kila sababu ya kutabasamu.

Zick Onyango akiandalia mteja wake smokie. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, biashara yake inaegemea viungo maalum vya kuku, smokie na mayai, akivisafu kwa kachumbari.

Bei yake inachezea kati ya Sh30 hadi Sh200.

“Kwa siku, sikosi kuweka mfukoni faida isiyopungua Sh800,” Onyango akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano.

Huku akitumia grili iliyoboreshwa, kiwango chake cha usafi ni cha hadhi nyingine – juu, mvuto kwa wateja.

Isitoshe, tabasamu yake kwa wanunuzi na aproni safi anayovalia itakuchochea umezee mate anachouza.

Akikiri ana deni kimaombi kwa Chicken Basket Ltd kufuatia hatua alizopiga kimaisha, Choma Preneurship inahudumu na zaidi ya vijana 50.

Baadhi ya bidhaa za kuku, zikiwemo mayai, smokie za kuku na vipande maalum vya kuku ambavyo Zick Onyango huuza Kisumu. PICHA|SAMMY WAWERU