Habari za Kitaifa

AUC: Ni kufa kupona kwa Raila Odinga

Na JUSTUS OCHIENG August 29th, 2024 2 min read

SERIKALI ya Kenya inafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga anashinda kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Hii kwa kuwa ikiwa Bw Odinga atashindwa, itachukua eneo la Afrika Mashariki miaka 30 kupata wadhifa huo kwa kuwa ni wa mzunguko.

Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei, anasema ni lazima Kenya ihakikishe Bw Odinga atashinda kiti hicho katika uchaguzi utakaofanyika Februari 5 mwaka ujao.

“Ni lazima tumfanye mwenyekiti (wa AUC) kwa kuwa tukishindwa, itachukua Kenya miaka 30 kwa sababu wadhifa huu ni wa mzunguko,” Dkt Sing’oei alisema.

Alisema kwamba mnamo Machi 2024, Baraza Kuu la Muungano wa Afrika liliidhinisha mapendekezo ya kamati ya wawakilishi wa kudumu ikiwemo wadhifa huo ushikiliwe kwa mzunguko kutoka eneo moja hadi nyingine na hii ilifanya ukanda wa Afrika Mashariki kutoa mgombezi kwa wadhifa wa mwenyekiti wa AUC huku Afrika Kaskazini ikitoa wagombeaji wa wadhifa wa naibu mwenyekiti.

Hivyo basi, Dkt Sing’oei alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) haitaweza kuachia mgombeaji kutoka Kenya siku zijazo iwapo Bw Odinga atashindwa katika uchaguzi wa Februari 2025.

“Hata kama itakuwa nafasi nyingine ya Afrika Mashariki, Kenya italazimika kuachia nchi nyingine ya Afrika Mashariki kutoa mwaniaji,” alisema.

Rais William Ruto anatarajiwa kumpigia debe Bw Odinga pembezoni mwa kongamano la Tisa la Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC), litakalofanyika Beijing kati ya Septemba 4 na 6, 2024.

Mnamo Jumanne, Agosti 27, 2024, Dkt Ruto alimzindua Bw Odinga kama mgombeaji wa wadhifa wa AUC wa Kenya katika hafla iliyohudhuriwa na marais watatu wa nchi wanachama wa EAC Salva Kiir (Sudan Kusini), Samia Suluhu (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda), Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca, na watu wengine mashuhuri wakiwemo marais wastaafu Olusegun Obasanjo (Nigeria) na Jakaya Kikwete (Tanzania).

Mwezi ujao, Septemba 2024, Bw Odinga anatarajiwa kuzindua kampeni zake katika makao makuu ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Kenya inapanga kutumia mabalozi wake na wanadiplomasia wakuu katika kampeni zake barani.

Mnamo Jumanne, Agosti 27, serikali ilitafuta uungwaji mkono wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilipozindua rasmi ugombeaji wa Bw Odinga katika Ikulu ya Nairobi.

Rais Ruto alisema ni muhimu kuchukua hatua madhubuti za pamoja kwa manufaa ya raia wa mataifa ya kanda na Bara zima la Afrika.

Eneo letu la Afrika Mashariki, ambalo ni nyumbani kwa zaidi ya watu milioni 500, kwa hakika linachukulia wakati huu kuwa zamu yake ya kutoa uongozi kwa misingi ya kanuni ya mzunguko baina ya kanda.