Habari Mseto

Basari: Mbunge ataka fedha zaidi za NG-CDF kuwafaa wanafunzi

June 4th, 2024 1 min read

NA LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuongeza zaidi fedha za mgao za maendeleo za NG-CDF eneobunge la Ruiru kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alisema eneo lake la uwakilishi limepanuka na kuwa na idadi kubwa ya wakazi.

Ruiru inakadiriwa kuwa na takriban watu 1 milioni.

Alisema katika maeneo ya Gikumari na Mwihoko, kumekuwa na idadi kubwa ya wakazi ambapo yeye kama mbunge wa eneo hilo amejenga madarasa kadha ya shule za msingi.

“Nikipata mgao zaidi wa NG-CDF nitaweza kuongeza madarasa zaidi katika maeneo tofauti,” alieleza mbunge huyo.

Alisema bado kunahitajika madarasa mengine kama 12 katika shule za upili ili kuwapa nafasi wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza.

Alisema Ruiru ni eneo kubwa na barabara ya Thika Superhighway imechochea maendeleo mengi na ukuaji wa idadi ya watu.

“Jambo linalonipa furaha ni kwamba Ruiru ni eneo linalojumuisha makabila tofauti. Hii inanipa motisha ya kusambaza fedha za maendeleo za NG- CDF bila ubaguzi wowote,” akasema.

Hivi majuzi Waziri wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo alizuru Ruiru ili kuzindua kituo cha ICT kitakachowasaidia vijana wengi kujiendeleza.

Bw King’ara alisema kuna vituo vinane vitakavyowekwa mitambo ya ICT ili vijana wengi waweze kunufaika na taaluma hiyo.

Mbunge huyo aliyasema hayo mnamo Jumatatu alipofanya kikao na wakazi wa Ruiru huku akiwarai wahimize wana wao kujiunga na kozi za ICT, akiwaaminisha kwamba ndizo zitawapa ajira ya haraka.

“Singetaka kuona vijana waliokamilisha elimu ya Kidato cha Nne wakizubaa mitaani bila kujihusisha na jambo muhimu la kuwafaa maishani,” akasema.