Habari Mseto

Bei ya mafuta taa yazidi kupanda

October 15th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

WANANCHI wa kipato cha chini wanaotegemea mafuta taa kwa matumizi mbalimbali nyumbani watazidi kuathirika na bei ya bidhaa hiyo mwezi huu.

Hii ni baada ya bei ya mafuta taa kuongezwa kwa Sh 0.43 na Tume ya Kudhibiti Kawi nchini (ERC).

Bei mpya za mafuta zilizotangazwa jana pia zinaonyesha bei ya mafuta ya Diesel itapanda kwa Sh1.60.

Hii ina maana kwamba isipokuwa wateja wa mafuta ya petroli ambao walipunguziwa angalau Shilingi moja, wanaotumia mafuta ya taa na wale wa dizeli wataendelea kuhangaika kwa mwezi mmoja ujao.

Mkurugenzi Mkuu wa ERC, Bw Pavel Oimeke, alisema bei hizo zimebadilishwa kwa kuzingatia jinsi bei ya mafuta ilivyo katika soko la kimataifa, ambapo bei ya mafuta taa na Diesel zilipanda huku ile ye petroli ya Super ikiteremka.

Mjini Mombasa, petroli ya Super itauzwa Sh113.10 kwa lita moja, Diesel Sh107.10 na mafuta taa Sh106.21. Bei ya bidhaa hizi Nairobi itakuwa Sh1.73, Sh109.72 na Sh108.84 mtawalia.

Serikali imekuwa ikilenga kupandisha bei ya mafuta taa kama njia ya kuzuia wafanyabiashara walaghai kuichanganya kwa aina nyingine za mafuta wakitaka kujiongezea faida kiharamu.

Mpango huu pia hunuiwa kuhimiza wananchi kuacha kutumia mafuta hayo nyumbani kwani utafiti huonyesha moshi ambao hutoka kwa mafuta taa husababisha maradhi ya afya kwa binadamu hasa magonjwa yanayoathiri uwezo wa kupumua vyema.