Habari za Kitaifa

Bunge kukata rufaa kuhusu uamuzi wa CDF

Na NDUBI MOTURI September 21st, 2024 1 min read

BUNGE la Kitaifa limetangaza kuwa litakata rufaa kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ambao uliharamisha Hazina ya Ustawi wa Maenebunge Nchini (NG-CDF).

Hii inaonekana kama njama ya wabunge kuhakikisha kuwa mabilioni ya pesa ambazo wamekuwa wakitengewa katika hazina hiyo haziwatoki.

Muda mfupi baada ya uamuzi huo wa korti, Bunge la Kitaifa lilifafanua kuwa kitengo chake cha kisheria kilikuwa kimeupokea na sasa kinapanga kukata rufaa.

“Bunge la Kitaifa litawasilisha rufaa kupinga uamuzi wa kuharamisha CDF. Pia litaomba mahakama itoe amri kuwa uamuzi huo usitekelezwe hadi rufaa isikizwe na kuamuliwa,” ikasema taarifa ya bunge.

Kifungu cha CDF kiliharamishwa kwa sababu majaji walisema hakizingatii Katiba na Bunge la Seneti halikushauriwa wakati wa kuwekwa kwake.

Majaji Kanyi Kimondo, Mugure Thande na Roselyn Aburili pia walitoa uamuzi kuwa CDF haifai kuwepo kuanzia Juni 30, 2026.

“Kifungu kinachohalalisha uwepo wa CDF ambacho kilifanyiwa marekebisho mnamo 2022 na 2023 si cha kikatiba. CDF na miradi yake yote haifai kuwepo kufikia Juni 30,” akasema Jaji Kimondo.

Wakiondoa CDF, majaji waliwashutumu wabunge kwa kuingilia majukumu ya serikali za kaunti na ile ya kitaifa.

Walisema eneobunge si kitu cha kutoa huduma na kuwatengea wabunge mabilioni ya pesa ni kufuja pesa za walipa ushuru.

Uamuzi huo unafuatia kesi ambayo iliwasilishwa na mwanaharakati Dkt Wanjiru Gikonyo na Cornelius Oduor ambao walisema kuwa CDF ilikiuka Sheria za Usimamizi wa Fedha za Umma na Mgao wa Mapato.